Wanawake Wakulima

By , in Shahada on . Tagged width:

Wanawake Wakulima

Msingi wa ukandamizaji wa wanawake wakulima unatokana na ardhi, kazi, mazao ya kazi na mzigo wa kazi za aina mbili: za kulisha na kutunza nyumbani pamoja na kuzalisha mazao ya kuuza, na sera ya kuhamia kwenye vijiji na tofauti za kitabaka. Jinsi tunavyozidi kuelewa vizuri dhana zinazotumiwa kujadili maswala hayo, ndiyo jinsi tunavyoweka msingi bora zaidi wa uchunguzi thabiti. Ingawa maswala yote yanahusiana, sura hii inasisitiza maswala machache maalumu.

Ardhi

Swala la umilikaji wa ardhi si swala la nani anamiliki ardhi kinadharia tu. Lazima tuangalie pia ni wanawake gani wakulima “wanaodhibiti” ardhi kiutekelezaji. Kudhibiti ardhi kiutekelezaji kuna maana ya nani anadhibiti matumizi ya ardhi na mazao yake – nani anaamua kuhusu matumizi ya ardhi na nyenzo nyingine za uchumi? Kwa mfano huko BukobanaKilimanjarowanaw’ake hawamiliki ardhi ambayo wanailima. Uchunguzi ulionyesha kwamba hali hii inajenga ukandamizaji wa wanawake (tazama vitomeo 62, 66 and 92). Uchunguzi uliofanyika katika jamii zinazorithi kiukeni unadhihirisha kwamba hata wanawake wakimiliki ardhi yao bado wanakandamizwa (tazama vitomeo 77 na 80). Wanawake hawana uhuru wa kutumia ardhi yao kama wanavyotaka; bado wanafungwa na masharti ya ndoa ya kiumeni. Wanawake hawana budi kutumia mashamba yao kulisha familia zao.

Kazi

Kwa hiyo swala la udhibiti wa ugawaji wa kazi ni swala la kimsingi linaloambatana na swala la ardhi. Uchunguzi unaonyesha kwamba wanawake wanafanya kiasi kikubwa cha kazi ya kuzalisha chakula na wanaume wanazalisha zaidi mazao ya kuuza (tazama vitomeo 70, 82, 85, 89 na 95). Zaidi ya hayo, mbinu za kisasa za kilimo zimeongeza mzigo wa kazi wa wanawake (tazama vitomeo 85, 89 na 95). Na kwa sababu watoto wengi kati ya miaka 7 na 14 wanakwenda shule badala ya kusaidia kulima au kufuga, mzigo wa kazi umeongezeka zaidi. Swala lingine muhimu ni zana za kazi zinazotumiwa na wanawake. Muro aliona kwamba wanawake wanatumia majembe mafupi ambayo yana ufanisi mdogo wa kazi kulingana na majembe marefu ya viwandani (kitomeo 80). Ngalulla aliona kwamba mbinu na mitambo ya kisasa inatumiwa katika kilimo cha pamba, wala si kwenye kilimo cha chakula (kitomeo 82). Kitu kingine kinachoongeza uzalishaji ni ujuzi. Fortmann (kitomeo 67) anaonyesha kwamba wanawake hawana nafasi sawa na wanaume katika kujifunza mbinu bora za kilimo zinazofundishwa na maofisa kilimo.

Mazao ya Kazi

Mwanamke yule ambaye ni mkuu wa kaya anadhibiti matumizi ya hela zinazotokana na mazao ya mashamba yake na mifugo yake, ingawa wake na vijana wanatoa mchango wao katika kuzalisha mali (tazama vitomeo vilivyotajwa hapo juu). Zaidi ya hapo, hata mke akizalisha mazao ya biashara katika shamba lake, kiutekelezaji ni mkuu wa kaya anayedhibiti hela zinazotokana na mazao hayo (tazama vitomeo 77, 80, 82).

Kihistoria, wanawake wanapata hela taslimu kutokana na kuuza mazao ya bustani (tazama uchunguzi uliofanyika na Ophelia Mascarenhas katika vijiji vitatu vya Mufindi) au mashamba yao ya chakula cha familia (tazama vitomeo vilivyotajwa hapo juu na 65). Kwa sababu wanazidi kuhitaji kununua chakula chao cha kila siku badala ya kutumia mazao ya mashamba yao, wanawake hawana budi kutafuta njia nyingine ya kujipatia hela: kufanya kazi ya kibarua katika mashamba ya wakulima walio tajiri zaidi (mara nyingi wakulima tajiri wanawake), kupika pombe, kuchoma makaa au kufanya shughuli nyingine za kiuchumi zisizo za kilimo, au kuhamia mjini kutafuta kazi (tazama vitomeo 65, 77, 88).

Inaonekana kwamba wanawake wanazidi kukandamizwa na ugawaji onevu wa mapato ya mazao. Vitu ambavyo vilinunuliwa zamani na wanaume vinaanza kununuliwa na wanawake. Kwa mfano, mafuta ya taa, dawa, nguo, ada za shule na kadhalika. Kwa hiyo mwanamume mkuu wa kaya ana uhuru wa kutumia hela za kaya kwa matumizi yake binafsi. Uchunguzi uliofanyika Kilimanjaro (tazama kitomeo 293) unaonyesha kwamba hali hii ni sababu moja ya kimsingi inayoleta utapiamlo. Sababu nyingine ni jinsi cbakula kinavyogawiwa nyumbani. Ingawa ni wanawake wanaozalisha kiasi kikubwa cha chakula, ni mkuu wa kaya anayekula sehemu kubwa zaidi ya chakula kilichopo. Kutokana na desturi hii, mara nyingi ni watoto wanaopata kiasi kidogo kabisa cha chakula.

Mzigo wa Kazi Mbili

Ingawa wanawake na wanaume wanatoa mchango karibu sawa wa kazi ya kilimo, wanawake ndio wanaofanya sehemu kubwa ya kazi zote za kutunza familia na kulea watoto (tazama vitomeo 77, 80, 82, 83, 84, 89 na 95). Mwanamke anatumia nusu ya siku ya kazi kupika na kuchota maji, pamoja na shughuli nyingine. Sachak anaona kwamba mpango wa kazi za wanawake wakulima hauna mantiki. Sisi pia tungeongeza kwamba, hata mpango wa shughuli zao zisizo za uchumi hauna mantild. Uchunguzi unaonyesha kwamba mzigo wa kazi ni kizuizi kikubwa cha kuongeza uzalishaji (tazama uchunguzi wa Kirirabai Na. 71 na vitomeo vingine vilivyotajwa hapo chini). Wanawake wamekataa kufanya kazi za kijiji wakisema kwamba wameshapewa mzigo mkubwa nano wa kazi (tazama vitomeo 77 na 89). Oomen-Myin (vitomeo 83 na 84) aliona kwamba mzigo mkubwa wa kazi unawazuia wanawake kushihki katika shughuli za kisiasa za kijiji. Jambo hili limeonekana katika uchunguzi mwingine na litajadiliwa katika sehemu inayohusu sera ya kuhamia kwenye vijiji.

Sera ya Kuhamia Kwenye Vijiji

Karibu makala zote zinazojadili sera hii zinaonyesha kwamba kuwepo kwake hakukusaidia ukombozi wa wanawake bali kumeimarisha ukandamizaji wa wanawake (tazama vitomeo 62, 69, 74, 77, 83, 84 na 91). Storgaard (kitomeo 91) na Oomen-Myin (83) wanaeleza kwamba hii ni kwa sababu sera ya kuhamia kwenye vijiji haikujaribu kupambana na mahusiano maonevu kati ya wanawake na wanaume. Kwa mfano, ingawa Sheria ya vijiji inasema kwamba kila mwanakijiji apewe uwanja wake, kiutekelezaji, mara nyingi ni mkuu wa kaya tu anayepewa ardhi. Zaidi ya hapo, serikali haijatambua wala haijachukua hatua ya kusimamia mgawanyo mzuri wa kazi wa kutunza na kulea watoto ili wote, wanaume kwa wanawake, watoe mchango.

Tofauti za Kitabaka

Makala chache sana zimeandikwa kuonyesha tofauti za kitabaka baina ya wanawake wakulima na jinsi tofauti hizo zinavyoathiri maswala yaliyotajwa hapojuu. Kufuatana na uchunguzi uliofanywa Bukoba, Bader anaona kwamba kwa, kiasi fulani uonevu wa wanawake unategemea tabaka – maskini anaonewa zaidi kuliko mwanamke wa tabaka la juu. Mary Kirimbai aliona kwamba mgawanyo wa kazi kufuatana na jinsi ni tofauti kwa tabaka mbalimbali. Katika kaya za wakulima maskini, wote, wanaume na wanawake wanasaidiana kuzalisha chakula cha familia. Lakini katika kaya zenye uwezo wa kuajiri vibarua, ni wanawake na vibarua tu wanaofanya kazi hiyo. Mwanaume mwajiri anafanya kazi ya kufuga pamoja na biashara au aina nyingine za uzalishaji bidhaa. Uchunguzi zaidi kuhusu maswala hayo yote, hasa kuhusu matumizi ya muda na hela katika kaya kwa kutumia mbinu za uchunguzi wa kushiriki unahitajika.

62. BADER, ZINNAT K. 1975 Women, Private Property and Production in Bukoba District (Wanawake, Mali ya Mtu Binafsi na Uzalishaji Mali Wilayani Bukoba). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tasnifu ya M.A. isiyochapishwa, uk. 229.

Makala hii inachunguza nafasi ya wanawake katika uzalishaji mali na jinsi nafasi hii inavyoathiriwa na tofauti za kitabaka. Mwanamke anapata mapato kidogo tu katika familia yake ingawa anazalisha mali kuliko mwanamume. Anadhulumiwa mapato yake huko nyumbani na sokoni. Hata hivyo, kiasi cha kuonewa kwake kinategemea tofauti za kitabaka zilizofuatana na mabadiliko wakati wa ukoloni na hasa wakati wa ukoloni wa kibepari. Mchunguzi anatpfautisha matabaka matatu: wanawake wakulima tajiri; wanawake wakulima wa kati (wenye mashamba madogo); na wanawake wakulima maskini. Halafu kila tabaka linagawanywa katika sehemu mbili; wanawake wasiojitegemea na wanawake wanaojitegemea. Katika jamii kama ya Wahaya ambayo ina mfumo wa kurithi kiukeni, wanawake kwa kawaida hawawezi kurithi ardhi. Wanaweza kurithi tu ikiwa hakuna mrithi wa kiume kwa kiasi kikubwa, uwezo wa kujitegemea unategemea uwezo wa kumiliki ardhi. Wanawake wanaojitegemea ni wale walioachana na waume zao, wajane, wale waliorithi ardhi na kukataa kuolewa, au wale walionunua mashamba kwa kutumia hela walizozipata kutokana na umalaya. Ukaguzi uliofanyika unaonyesha kwamba mwanamke mkulima tajiri ndiye mwenye hali nzuri zaidi. Anaweza kuwaajiri wafanyakazi na anaweza kijiunga na vikundi vya wanaume vya kazi. Mwenye hali mbaya kuliko wote ni mwanamke mkulima asiyejitegemea.

63. BADER, ZINNAT 1979 “Social Conditions of the Peasant Woman in Zanzibar and Pemba” (“Hali ya Kijamii ya Mwanamke Mkulima wa Zanzibar na Pemba”) Makala Na. 18, BW, uk. 5.

Makala haya yanatoa maelezo mafupi juu ya uchunguzi uliofanyika. Inachambua kwa kifupi historia ya kilimo cha mashamba makubwa na ya wale maskini wasio na ardhi. Wakulima maskini waliongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kuoa wake wengi zaidi. Wakulima matajiri wanaongeza uzalishaji kwa kunyonya wale vibarua wanaohamia kutafuta kazi. Makala yanatilia mkazo jinsi mabadiliko katika umilikaji wa ardhi yanavyowaathri wanawake. Ilionekana kwamba kinadharia baada ya mapinduzi, ardhi iligawiwa kwa familia, lakini ukweli ni kwamba ni mkuu wa familia tu ndiye aliyegawiwa ardhi. Wanawake hawakushirikishwa katika uamuzi wala utekelezaji wa ugawaji huo. Kama ilivyo penginepo Tanzania, wakulima wote, wanawake kwa wanaume, wanapendelea zaidi kulima mazao ya chakula kuliko ya biashara. Kilimo cha karafuu kimepungua kwa sababu mbalimbali, pamoja nazo ni kuchelewa kupanda miti, mabadiliko katika mfumo wa kukopa, bei ndogo wanayolipwa wakulima, na mshahara mdogo wa wafanyakazi wa kuchuma karafuu. Upo mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi kwenye kazi za kilimo, hata kwenye mashamba ya serikali na miradi ya mchele. Wanawake wanapewa kazi zenye mshahara mdogo, tena zisizofuatana na majira. Hela taslimu wanazozipata wanatumia kwa mahitaji ya familia. Makala hii ni taarifa ya awali ya uchunguzi unaofanyika kwa ajili ya Shahada ya Ph.D.

64. BRAIN, JAMES L. 1976 “Less than Second-Class: Women in Rural Settlement Schemes in Tanzania” (“Chini ya Tabaka la Chini: Wanawake katika Vijiji Vilivyoanzishwa Chini ya Sera ya Kuwahamishia Watu kwenye Vijiji”). Katika Women in Africa, Nancy J. Hafkin na Edna G. Bay (Wahariri) uk. 263 – 282 Stanford, Stanford University Press.

Makala haya yanalinganisha hali ya wanawake katika vijiji viwili vilivyoanzishwa chini ya sera ya kuwahamisha watu kwenye vijiji (Morogoro) na kijiji kimoja cha Chama cha Maendeleo ya Ruvuma. Vijiji vile vya mradi wa serikali vilianzishwa na kupata’msaada wa serikali. Huko Ruvuma wenyeji waliamua wenyewe kuishi na kufanya kazi pamoja. Katika vijiji vya serikali wanawake walikuwa na hali mbaya kuliko waliyokuwa nayo katika jamii zao za jadi. Mume alikuwa na haki zote kuhusu ardhi na alipewa fedha zote zilizotokana na shamba. Mwanamke alitarajiwa kufanya kazi kwa muda wa saa 8 shambani pamoja na kazi zote za nyumbani. Mumewe alipokufa au kumwacha, mke anajikuta ni maskini kabisa. Hah hii iliwawia ngumu kwa sababu wanawake hawa walitoka katika jamii inayorithi ujombani na walikuwa na haki zao kuhusu ardhi. Vilevile waliweza kujitegemea zaidi kiuchumi kuliko wanawake wa jamii nyingine. Hatimaye wanawake wengi walitoroka vijiji hivi na kupinga jinsi walivyonyimwa haki zao.

Lakini katika kijiji cha Chama cha Maendeleo cha Ruvuma, faida yote iligawiwa sawasawa kwa wanakijiji bila ubaguzi: vijana kwa wazee, wanawake kwa wanaume.

65. BRYCESON, D. na KIRIMBAI, M. (Wahariri) 1980 Subsistence or Beyond? Money Earning Activities of Women in Rural Tanzania (Kijungumeko au Zaidi? Shughuli za Wanawake za Kujipatia Mapato ya Fedha Vijijini Tanzania) BRALUP Research Report Na. 45, Dar es Salaam, BRALUP na UWT uk. 165.

Makala hii inatoa taarifa juu ya ukaguzi uliofanyika kuhusu shughuli za wanawake za kujipatia fedha taslimu vijijini Tanzania. Ukaguzi ulifanyika katika mikoa minne ya bara – Arusha, Kigoma, Dodoma, na Pwani, na Pemba na Unguja. Ripoti ina sehemu tatu: (1) Utangulizi (2) Ripoti ya Matokeo ya Ukaguzi kufuatana na mkoa (3) Muhtasari na hitimisho. Utangulizi unajadili umuhimu wa fedha taslimu kwa wanawake wa vijijini, sera ya UWT juu ya shughuli za wanawake za mapato ya fedha, na miradi ya uchunguzi. Sehemu inayotoa matokeo ya ukaguzi inaanza kwa kutoa picha ya hali ya kila mkoa, vijiji vinne vya mkoa, shughuli za UWT katika mkoa na hali ya miradi ya ushirika katika mkoa.

Ripoti inathibitisha kwamba kazi muhimu kabisa ya wanawake ni kuleta chakula, maji na kuni kwa ajili ya mahitaji ya kila siku ya familia zao.

Shughuli hizo peke yake zinaweza kuchukua muda mrefu, tangu alfajiri mpaka saa 4 usiku. Mzigo wa kazi unaongezeka zaidi na kazi ya kutunza watoto, hasa tukifikiria magonjwa mbalimbali ya watoto na akina mama wazazi, kuharibika kwa mimba, mtoto kuzaliwa amekufa, na vifo vya watoto wachanga. Shughuli za wanawake za kujipatia fedha ni za aioa tatu: (a) uuzaji wa mazao ya chakula (b) biashara ndogondogo. – (uuzaji wa pombe una faida kubwa kushinda shughuli nyingine) na (c) kuajiriwa kama kibarua au mfanyakazi wa kudumu. Katika mikoa yote isipokuwa Unguja na Dodoma, uuzaji wa mazao ya chakula ni njia kubwa ya kujipatia fedha. Mapato ya wastani kwa mwaka ni kati ya 300.00 mpaka 400.00 isipokuwa Amsha, ambapo mapato ya wastani kwa mwaka yalikuwa juu sana. Ushirikiano wa wanawake katika shughuli hizi za kujipatia hela ulitofautiana sana na haukuwa na uhusiano na hali ya k’uchumi-jamii katika mkoa. Katika mikoa yote karibu mapato yote ya hela yalitumiwa kununulia chakula, nguo na vitu vya nyumbani. Katika mikoa yote miradi ya kushirikiana haikufanikiwa sana na shughuli za UWT zilikuwa na matatizo mengi.

66. CHUWA, P.A.A. 1977 “The Role of Women in the Rural Economy of 12 Villages of Uru: Pre-Colonial Era to 1976 (“Nafasi ya Wanawake katika Uchumi wa Vijiji 12 vya Uru: Kabla ya Ukoloni mpaka Mwaka 1976”) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, taarifa ya mwanafunzi wa Historia, uk. 35.

Vijiji hivi 12 viko Wilayani Kilimanjaro. Makala inafafanua kwa undani jinsi wanawake wa Kichagga walivyonyonywa kabla ya ukoloni na jinsi unyonyaji huo unavyozidi siku hizi. Wanawake ndio uti wa mgongo wa uchumi wa kijungumeko na uchumi wa fedha, lakini kwa sababu hawana ardhi hawapati hadhi ya wazalishaji mali. Mambo mawili yalisababisha kuwapo kwa hali hii hafifu ya wanawake: kwanza hawakuwa na haki ya kumiliki ardhi na pili mila za mahari, ambazo zilimfanya mwanamke awe “mali ya mwanaume na familiayake”.

Ubepari pamoja na uchumi wa fedha na kazi za kuajiriwa ulipanua hali hii ya kutokuwa na usawa. Hii ni kwa sababu katika mfumo huu wanaume waliendelea kupewa hadhi ya wazalishaji mali wakuu ingawa waliwategemea wanawake kwenye uzalishaji wa mazao ya biashara na ya chakula. Hata kazi zile za kilimo ambazo zilikuwa kazi za wanaume ziligeuka kuwa kazi za wanawake. Ingawa wana na’fasi kubwa katika uzalishaji mali, wanawake bado hawana sauti katika kugawa mapato yanayotokana na kazi zao. Pia mume akifa, hawezi kurithi mali inayotokana na kazi yake. Na bado wanawake wanapewa hadhi ya chini katika jamii.

67. FORTMANN, L. 1979 “Women and Tanzania Agricultural Development” (“Wanawake na Maendeleo ya Kilimo Tanzania”) katika Papers in.the Political Economy of Tanzania, Wahariri K.S. Kim, R.B. Mabele na M.J. Schultheis. Nairobi, Heinemann, uk. 278 – 287.

Hapa Tanzania asilimia 97.8 ya wanawake wanaofanya shughuli za uchumi ni wakulima. Hata hivyo asilimia 5 tu ya wale wanaoajiriwa kufanya kazi za kilimo ni wanawake. Wanawake ndio msingi wa kilimo cha mazao ya chakula na biashara, lakini picha tunayopewa ni kwamba wao ni wakulima “wajinga, walioanzisha kitu chochote kipya na wanafuata kilimo cha jadi.” Kwa hiyo msaada wa elimu ya kilimo na kadhalika ulitolewa kwa wanaume. Ukaguzi wa matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo ulionyesha kwamba hakuna tofauti muhimu au kubwa kitakwimu kati ya kilimo cha wanaume na wanawake wenye uwezo wa kununua vifaa vya kisasa. Wake za wale wanaume walionunua vifaa vya kisasa vilevile walijua teknolojia hii kwa sababu wale wenyewe walifanya kazi nyingi za shamba, kama kupalilia, kupanda, kunyunyizia dawa na kadhalika. Hata hivyo ushirikiano wao una mipaka kwa sababu wanashindwa kujipatia nyenzo za uchumi, ardhi, na utaalam. Pia hawafaidi matunda ya jasho lao. Kwa hiyo hawakuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko au kusaidia kutoa uamuzi juu ya matumizi ya vifaa, ukubwa wa shamba na kadhalika. Vilevile kwa sababu ya mzigo wao mkubwa wa kazi za nyumbani na shambani, walisita kutumia teknolojia hii ambayo ingeongeza zaidi mzigo wao wa kazi.

68. MARIE J. GIBLIN 1980 “Women Peasants and the Transition to Socialism in Tanzania” (“Wanawake Wakulima na Maendeleo ya Kuleta Ujamaa Tanzania”), Columbia University, Makala iliyoandikwa kwa ajili ya somo la Siasa G9492y, Problems in Modem Africa, tarehe 24 Aprili, uk. 39.

Makala hii inachambua maisha ya wanawake wakulima wa Tanzania kwa kuzingatia uhakiki uliofanywa juu ya wakulima na uenezaji wa ubepari. Vilevile ina jinsi ubepari unavyotawala uzalishaji mali wa kijungumeko na kazi za nyumbani ambazo hazilipiwi. Makala inajadili uchunguzi uliofanywa huko Bukoba na Geita. Uchunguzi huu ni juu ya swala la mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi na uamuzi kuhusu matumizi ya fedha za mapato kwa kuzingatia sera ya kuwahamisha watu kwenye vijiji. Makala inadhihirisha hasara na faida ya kutumia mbinu za teknolojia katika kilimo cha mazao ya biashara, kwa mfano hasara moja ni kwamba wanawake wanaongezewa kazi na kushushiwa hadhi kwa sababu ya mbinu nyingine. Vilevile inaonekana kwamba mwelekeo wa mipango mingi inayohusu wakulima na hasa wanawake wakulima ni kutafuta uamuzi na utatuzi wa kiteknolojia tu. Mwelekeo huu unawadhuru wanawake kwa sababu unasaidia kujenga na kuendeleza mahusiano ya uzalishaji mali yaliyokuwepo siku zote. Mipango ya Tanzania ni mfano wa mipango iliyoshindwa kutambua na kuamsha ari na nguvu ya wanawake ya kujenga ujamaa.

Kuna haja ya kuchambua uhusiano kati ya uzalishaji mali na uendelezaji wa jamii au familia. Utawala wa kiumeni ndio msingi wa utawala wa jamii kwani unaendeleza hali ya kutokuwa na usawa kati ya wanawake na wanaume. Makala inakataa kabisa fikra ya kwamba wanawake wakitambua kwamba hawana usawa na wanaume, watajitenga katika harakati za kujenga ujamaa. “Wanawake wakitambua kwamba uonevu wao unaotokana na ubepari na utawala wa kiumeni, utambuzi huo utasaidia kujenga uwezo wa kupambana na haya mambo yote mawili”. Sasa mchunguzi huyu anafanya uchunguzi kwa ajili ya shahada ya Ph.D. kuhusu wanawake, wakulima na kanisa wilayani Ngara.

69. GONDWE, F. 1977 “Division of Labour in Mwenge Village and if it Does Liberate Women” (“Mgawanyo wa Kazi katika Kijiji cha Mwenge – Mgawanyo huu Unawakomboa Wanawake?”) Dar es Salaam, Idara ya Sosiolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mswada wa tasnifu ya B.A. uk. 36.

Kijiji cha Mwenge kilicho mjini Dar es Salaam ni tofauti na vijiji vingi vya ujamaa kwa vile kina mchanganyiko wa watu wa makabila mbalimbali na wenye uzoefu mbalimbali. Pia karibu wanakijiji wote waliendelea na masomo baada ya kumaliza darasa la saba. Wengine wamemaliza Chuo Kikuu. Kwa ujumla wanakijiji hawana moyo ule wa kufanya kazi pamoja. Wote, wanawake kwa wanaume, wanawaajiri vibarua kufanya kazi zao. Mara chache wanashirikiana kwa kazi fulani, lakini wanawake wanashiriki kidogo sana katika kazi hizo. Kwa mfano vibarua wanaofanya kazi katika mradi wa kutengeneza matofali ni wengi kuliko wenyeji wa kijiji. Duka la Ushirika linaendeshwa na wanaume tu. Wanaume wanatawala kamati zote isipokuwa kamati ya UWT na Kamati ya Utamaduni. Wanawake hawapo kabisa kwenye Kamati ya Mipango na Uchumi na Kamati ya Wazee.

70. KAMUZORA, C. LWECHUNGURA 1978 “Constraints to Labour Time Availability in African Small Holder Agriculture: The Case of Bukoba District in Tanzania” (“Mambo Yanayopunguza Muda wa Kazi katika Mashamba Madogo: Mfano wa Wilaya ya Bukoba Tanzania”) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ERB Semina, uk. 15.

Ukaguzi ulifanywa mwaka 1976 kuhusu ratiba ya kazi na muda uliotumiwa kwa kila kazi (ratiba ya muda wa kazi) kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa 2 usiku. Ukaguzi huo ulipata taarifa kutoka kwa kila mwenyeji katika kaya 105, mwenye kaya akiwa mwanamume. Siku mbili kwa wiki wenyeji walitoa taarifa kuhusu shughuli zao za siku iliyopita, na taarifa hii ilitolewa kwa misimu yote minne. Mchunguzi alitenga aina mbalimbali za shughuli za kiuchumi, kinyumbani, kijamii na nyinginezo. Halafu alikadiria wastani wa takwimu za ujumla kwa kila mwenyeji. Kwa wastani ilionekana kwamba asilimia 36.4 ya muda ulitumiwa kwa shughuli za kiuchumi, asilimia 14.7 kwa shughuli za nyumbani, asilimia 12.1 kwa shughuli za kijamii, na asilimia 30.1 kwa kupumzika. Makala inaeleza kwamba sababu ya kutumia asilimia ndogo kwa shughuli za kiuchumi ni idadi kubwa ya vifo na tatizo la kuugua mara kwa mara.

Uchambuzi huo una matatizo kwa sababu makala haikutenga shughuli za mwenye kaya (mzee), mke (wake) na watoto wa umri mbalimbali; msomaji hawezi kutambua nani anafanya kazi gani. Maelezo kuhusu shughuli za mwenye kaya yanathibitisha maoni yaliyotolewa pengine (kwa mfano Bryoeson na Mbilinyi 1979) kwamba mwenye kaya anatumia muda wake kuongoza na kusimamia kazi za kilimo zinazofanywa na wake zake pamoja na kazi zao za nyumbani. Kwa mfano “tangu saa 12 mpaka saa 2 asubuhi ni wakati wa kufungua kinywa: Mke anatayarisha kifungua kinywa na mume anatembelea shamba (la ndizi au kahawa) kuangalia maendeleo yake”. Isitoshe, ingawa asilimia 30 ya muda ni wa kupumzika, anayepumzika ni mwenye kaya tu. Hii ina maana ya kwamba anatumia asilimia 60 ya muda wake kwa “kula na kupumzika, kutembelea majirani, mabaa na mambo yasiyojulikana (!)” Kila mara mwandishi anaomba radhi kwa sababu mwenye kaya anatumia muda mwingi kwa mapumziko na kwa sababu mwanamume na mwanamke wanatumia muda wao kwa shughuli tofauti sana.

Dhana zinazotumiwa kutofautisha shughuli za kiuchumi, kijamii na kinyumbani zina matatizo vilevile. Kwa mfano, baadhi ya shughuli za uzalishaji chakula zimewekwa chini ya kazi za kiuchumi, nyingine zinawekwa chini ya kazi za nyumbani. Kwa mfano: mke anakwenda shambani kuchuma mkungu wa ndizi au kuchimba viazi vitamu na kuvileta nyumbani. Kazi hii imewekwa chini ya utayarishaji wa chakula kwa hiyo inaeleweka kuwa kazi ya nyumbani. Lakini kazi hii ni sehemu moja ya uzalishaji wa chakula (kuvuna, kusafirisha, na kadhalika).

71. KIRIMBAI, M.W. 1981 The Impact of Domestic Water Supply Projects on Rural Population and Their Role in Production and Reproduction in Dodoma Rural District (“Athari za Miradi ya Kuleta Maji Safi Nyumbani kwa Wanavijiji na Nafasi yao katika Uzalishaji Mali na Uendelezaji wa Jamii katika Wilaya ya Dodoma Vijijini). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tasnifu ya M.A. isiyochapishwa, Sosiolojia, uk, 170.

Kwa kiasi kikubwa ni wanawake wanaofanya kazi ya kuchota maji kila siku. Makala inaonyesha muda unaotumiwa kwa kazi ya kuchota maji na kwa kazi nyingine za nyumbani na kazi za uzalishaji mali. Ilionekana kwamba wanaume wanachota maji kupata hela. Wanawake wakulima tajiri waliweza kuwatuma vijana au wengine, k.v. wafanyakazi wao kuchota maji na kufanya kazi nyingine. Katika kaya za uzalishaji mali na uendelezaji wa jamii kutokana na jinsi umelegea kiasi. Kwa mfano, wote, waume kwa wake, walilima chakula. Lakini katika kaya za wakulima tajiri, mume alishughulikia mambo mengine ya kuongeza mali yake. Ilionekana kwamba bomba la maji halikutatua matatizo ya maji moja kwa moja. Matatizo yanayobaki ni yale ya kutengeneza bomba linapoharibika, uhifadhi wa maji, namna ya kuchota maji na mahali pa kuweka bomba.

72. KJAERBY, FINN 1978 “Introduction to History” and “Cattle and Conflict (“Utangulizi kwa Historia” na “Ng’ombe na Migogoro”) Miswada ya sura mbili za kitabu kuhusu Wabarabaig, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, BRALUP.

Makala hii inachambua maendeleo ya kihistoria ya Wabarabaig, ambao ni wafugaji wa Wilaya ya Hanang. Inachunguza mahusiano ya kinyonyaji yalioyo msingi wa mfumo wa rika. Katika mfumo huo wanawake na vijana wanafanya kazi kwa wazee (wa kiume) ili wajipatie riziki. Makala inatoa maelezo kuhusu mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi na “vijana bila mali” ambao hawana njia nyingine ya kupata ng’ombe isipokuwa kuwinda simba, kupigana na adui au kuiba. Mtazamo wa makala kuhusu mahusiano ya mali ni tofauti sana na ule wa Rigby. Hii ni miongoni mwa makala chache kuhusu jamii za ufugaji zinazochunguza na kutilia mkazo swala la wanawake katika uzalishaji mali na uendelezaji wa jamii. (Tazama vilevile Rigby, kitomeo 87).

73. LANDBERG, P.L.W. 1969 “The Economic Roles of Women in a Tanzania Coastal community” (“Nafasi ya Wanawake katika Uchumi wa Kijiji Kimoja cha Pwani Tanzania”) Proceedings of the Social Sciences Council Conference, 1968/69 Sociology Papers, Vol. 1 uk. 221 – 232.

Makala hii inatoa maelezo kuhusu aina za shughuli za kiuchumi zinazofanywa na wanawake wa kijiji cha Kigombe, Mkoa wa Tanga, na kuhusisha shughuli zao na uchumi wa kijiji kwa ujumla. Mifano inajadiliwa ili kufafanua hali halisi ilivyo. Kazi muhimu ya wanaume wa kijiji hiki ni uvuvi. Vilevile, wanawake na wanaume wanalima, hasa mazao ya chakula. Wanawake wanajishughulisha na mambo kama upishi na kuuza vyakula, kutengeneza vitu kama vikapu, mikeka na kadhalika, kuuza mazao na hata kuvua samaki ili wapate hela. Mambo muhimu yanayoathiri uwezo wa wanawake kufanya shughuli hizo ni afya, umri, kuolewa/kutoolewa, na muda wanaokuwa nao baada ya kumaliza kazi za nyumbani na za shambani. Kwa kawaida biashara hii ni ndogo na faida yake ni ndogo, lakini shughuli hizo ni muhimu sana kwa sababu ni njia ya pekee ya kupata fedha taslimu.

74. LEWIN, ROGER 1969 “Matetereka” Mbioni Juzuu 5 Na. 3, uk. 13 – 34.

Makala hii inaeleza umuhimu wa mchango wa wanawake katika kuleta ufanisi wa shughuli za uzalishaji mali kwenye kijiji cha Ujamaa cha Matetereka. “Kijiji cha Matetereka kipo kwa sababu ya wanawake… Lazima wapewe heshima kubwa sana kwa kazi wanazozifanya kwa ari. Huko Matetereka si kitu cha ajabu kuona wanawake wengi wakifanya kazi shambani kwa muda wa saa 10 mpaka 12 pamoja na kushughulikia nyumba zao na kuwatunza watoto.” Lakini kwa sababu ya kazi nyingi wanawake hawana nafasi wala nguvu ya kutosha ya kutunga mbinu mpya. “Wakati wanaume wanapojadiliana kwa nguvu katika mikutano ya ujamaa, wanawake wanalala. Wanafanya kazi kutwa nzima ya kuendeleza maisha ya ujamaa kiasi ambacho wanashindwa kukaa macho kwa uchovu.” Makala inatambua umuhimu wa kuleta mabadiliko. Lakini mabadiliko hayo yana matata na hatari. Ili mafanikio yawepo, lazima mabadiliko yatokane nawatu wenyewe.

Wanawake walijaribu kupunguza kazi zao. Walianzisha kikundi cha wanawake, shule ya watoto wadogo na kituo kinachopokea watoto wote. Labda mabadiliko ya kimsingi yatawezekana wakati wa kizazi kijacho, kwa sababu wale watakuwa wamepata elimu ya kijamaa. Mabadiliko hayo yatatokea ikiwa watu watatambua kwamba mazingira yanabadilika na nafasi ya wanawake iliyokuwepo zamani haifai tena kwa jamii ya leo.

75. MBILINYI, M.J. 1973 “Education, Stratification and Sexism in Tanzania: Policy Implieations” (“Elimu, Daraja za Jamii na Ubaguzi wa Jinsi katika Tanzania: Athari Zake kwa Sera”). The African Review 3 (2) uk. 327 – 340.

Makala inataja mipaka ya sera iliyopo sasa ya vijiji vya ujamaa, pamoja na matatizo yanayotokana na tofauti kati ya miji-vijiji. baada ya kuzingatia hoja hizo mbili, makala inatoa mapendekezo juu ya huduma za vijiji na kupendekeza mfumo mwingine wa elimu ambao ungewafundisha wanavijiji nje ya mfumo wa shule. Kama tungeanzisha viwanda huko kijijini na kufanya angalau kazi chache kwa pamoja, mabadiliko hayo yangeleta mfumo mwingine wa kazi kama kila mtu angepewa kazi yake maalum. Bila shaka mahusiano ya kiume yangefifia. Kijiji kingeweza kuwa na mpango wa kutoa huduma za kuwatunza wazee, kuongeza chakula, kuni au nishati, ujenzi wa nyumba, shughuli za mazishi na kadhalika. Hakika yale mahusiano ya kiumeni na “vipori” vingine vya mahusiano yaliyokuwepo kabla ya ubepari yangepitwa na wakati. Watu wa kwanza wa kuathiriwa na mabadiliko hayo ni wanawake na vijana. Makala inasisitiza hoja ya kufanya harakati dhidi ya itikadi zinazobagua wanawake katika ngazi zote za serikali hata kijijini.

76. MBILINYI, MARJORIE 1982 “Wife, Slave and Subject of the King: The Oppression of Women in the Shambala Kingdom” (“Mke, Mtumwa na Mtawaliwa wa Mfalme: Uonevu wa Wanawake katika Ufalme wa Wasambaa”) Tanzania Notes and Records 88 + 89: 1 – 13.

Makala haya yanatoa maelezo ya kinadharia kuhusu hali ya wanawake katika serikali ya kikabaila tangu mwanzo mpaka mwisho wake katika kame ya 19. Wanawake wanachambuliwa kwa kuzingatia mahusiano ya kibepari na mahusiano yaliyokuwepo kabla ya ubepari na mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi. Wakati wa ukabaila huko Usambara wanawake walikuwa hawana haki za kumiliki na walinyonywa kwa sababu ya mahasiano ya kiumeni. Wakati wa ukoloni, uchumi wa kibepari ulianza kuenea na kutawala kilimo na ubepari ulitumia msingi wa mahusiano ya kiumeni kuwaonea wanawake na watoto kwa kuwatumikisha kazi kwa faida ya mabepari tu. Swala la ufafanuzi wa aina za uzalishaji mali ni muhimu sana tukitaka kuelewa nafasi ya wanawake wa leo katika uzalishaji bidhaa wa wakulima. Makala yanajadili harakati za kiitikadi na mbinu mbalimbali za wanawake kupambana na itikadi hizo katika vipindi vyote vya historia vinavyotajwa, Makala yanapinga mtazamo wa kiantropolojia unaotumiwa na Feierman katika kazi zake (1972, 1974).

77. MBILINYI, MARJORIE 1982 “The Unity of ‘Struggles’ and ‘Research’: The Case of Peasant Women in West Bagamoyo, Tanzania” (“Umoja wa ‘Harakati’ na ‘Uchunguzi’: Mfano wa Wanawake Wakulima wa Bagamoyo Magharibi, Tanzania”) katika makala ya Maria Mies (Mhariri) Fighting on Two Fronts: Women’s Struggles and Research. The Hague, Institute of Social Studies.

Sehemu kubwa ya makala haya ni uchambuzi wa matokeo ya uchunguzi uliofanyika katika kijiji cha Diozile I. Uchunguzi huu ulikuwa juu ya muda wa kazi unaoonyesha kwamba wanawake wanafanya kazi mara mbili kuliko wanaume kwa sababu ya kazi zao za nyumbani. Ingawa wanawake wana mashamba yao, hawana uhuru wa kuchagua wafanye kazi gani na kwa muda gani. Hii ni kwa sababu wana wajibu wa kulima chakula cha familia. Uchunguzi uliofanyika juu ya ulaji unaonyesha kwamba wakulima wanaounua mahitaji yao ya lazima sokoni, na wakati wa ukame wananunua hata chakula. Makala yanachunguza ukame unavyoathiri shughuli za kiuchunu na mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi na harakati za kujihami za watu wote. Makala yanafafanua uhusiano kati ya mapambano kati ya wanawake na wanaume na harakati za kitabaka kati ya wakulima maskini na serikali na ubepari. Mfano mmoja ni mapambano yaliyozuka kuhusu kuzalisha pamba zaidi, hasa kuhusu ugawaji wa ardhi na kazi kama zilivyopangwa na serikali. Mbinu zinazotumiwa na wanawake kupambana na hali yao zinazonekana wazi katika mkutano mmoja wa Baraza la Kijiji na mkutano mmoja wa wanawake. Mwishoni mwa makala yake mchunguzi anauliza maswali yafuatayo: (1) Ni nani adui wa wanawake, ubepari na serikali au wazee wa familia? (2) Turudi kwenye uzalishaji wa kijungumeko au tupokee uenezaji wa ubepari katika uzalishaji mali na uendelezaji wa jamii za wakulima? (3) Ukandamizaji wa wanawake ni swala la ardhi au la kazi?

78. MBILINYI, SIMON MICHAEL MHELEMA 1974 Coffee Diversification, A Strategy for Development: The Case of Tanzania (Mbinu ya Kuchanganya Kilimo cha Kahawa na Kilimo cha Mazao Mengine: Mbinu ya Maendeleo: Mfano wa Tanzania) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tasnifu ya Ph.D. isiyochapishwa, uk. 354. Tasnifu hii imechapishwa baadaye na East African Literature Bureau, Nairobi.

Tasnifu hii inachunguza kwa undani mfumo wa kilimo cha kahawa kwa wakulima wadogo. Uchunguzi ulifanyika katika mikoa mitano (Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Ziwa Magharibi na Ruvuma). Mwanzoni mwa kipindi cha mwaka 1970 – 80, kahawa ilipata asilimia 20 ya thamani ya mazao yote yaliyosafirishwa nje. Pia wakulima wa kahawa walipata kiasi kikubwa cha pato lao kutokana na zao hili. Tasnifu inataja matatizo ya kutegemea zao la kusafirishwa nje, ambayo yanatokana na hali ya soko la kibepari. Inapendekeza mbinu ya kuchanganya kilimo cha kahawa na cha mazao mengine kama njia ya kutatua matatizo haya. Inapendekeza pia mbinu ya kutilia mkazo shughuli maalumu za uchumi ili kukuza soko lililoko ndani ya nchi. Tasnifu inatoa taarifa kuhusu mfumo wa umilikaji na matumizi ya ardhi na aina za kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi kwa kila mkoa. Taarifa zinasisitiza uchambuzi wa aina za kazi zinazofanywa na kila jinsi na kila rika; tatizo la kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi kwa ajili ya afya mbaya, shule, au uamuzi wa kutafuta kazi ya kuajiriwa. Kwa wastani, idadi kubwa ya vibarua wanaoajiriwa wakati kazi zinapokuwa nyingi ni wanawake, isipokuwa katika Mbeya na Ziwa Magharibi. Hata hivyo, wanaajiriwa kwa muda mfupi tu. Watoto wanaajiriwa pia wakati wa kazi nyingi.

Ilionekana kwamba mazao mapya na mbiou mpya za kilimo zilikataliwa na wakulima kama mbinu hizi hazikuoana na mgawanyo wa kazi kufuatana na jinsi.

79. MOSHA, A.C. 1975 “Training Extension Staff for Ujamaa Villages” (“Mafunzo ya Maofisa Kilimo wa Vijiji vya Ujamaa”). Makala iliyowasilishwa kwenye Workshop and Agricultural Extension in Ujamaa Villages, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Morogoro, tarehe 22 – 27 Septemba, TFNC.

Makala yanatoa hoja kwamba kupungua au kukwama kabisa kwa kilimo kunasababishwa kwa kiasi fulani na udhaifu wa huduma za elimu ya kilimo vijijini. Lakini makala hayakutaja hitilafu za elimu hii, kwa mfano ukosefu wa maofisa kilimo wa kike na tabia ya kutojali nafasi ya wanawake katika kilimo na kadhalika. Maelezo yake kuhusu mkulima wa siku hizi wa kijiji ni kaya, si mkulima wa kiume. Wala hayakuzingatia kwamba hatuwezi kutoa maelezo ya ujumla yanayojumuisha wakulima wanawake na wanaume. Hatuwezi kwa sababu zipo tofauti nyingi kati ya wanawake na wanaume wakulima, ambazo zinatokana na mahusiano ya kiumeni na mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi. Kwa mfano, makala yanasema “Mkulima ni mwanachama wa ushirika wa kijiji”, lakini ukweli ni kwamba mzee wa familia ndiye mwanachama; wake zake wanaomtegemea siyo. Vilevile wanawake hawakutajwa katika mapendekezo yaliyotolewa kuhusu idadi ya maofisa wa kilimo, sifa zao zinazotakiwa na mafunzo yao.

80. MURO, ASSENY 1979 The Study of Women’s Position in Peasant Production and Their Education and Training: A Case Study of Diozile I Village in Bagamoyo District (Uchunguzi wa Nafasi ya Wanawake katiku Uzalishaji wa Wakulima na Elimu na Mafunzo Yao: Mfano wa Kijiji cha Diozile I, Wilaya ya Bagamoyo) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tasnifu ya M.A. isiyochapishwa, uk. 179.

Muro anatumia mbinu ya uchunguzi wa kushiriki na kuangalia. Anachambua nafasi ya wanawake katika uzalishaji mali wa kijiji, hadhi yao katika kijiji na kaya, kazi za nyumbani na uwezo wa wanawake kujiunga na elimu ya watu wazima. Mwandishi alikuwa na majadiliano marefu na wanakijiji wanne wanawake, na ameweka majadiliano hayo kwenye tasnifu kutufafanulia maisha ya wanawake vijijini. Tasnifu inatoa mapendekezo maalumu ya muda mrefu na ya muda mfupi. Msingi wa mapendekezo hayo ni hali halisi ya maisha katika kijiji hiki. Hata hivyo mapendekezo yake yanafaa kwa vijiji vingine. Tasnifu ina bibliografia ya kurasa tisa inayojumuisha maandishi ya kitaifa na kimataifa juu ya swala la wanawake.

81. MUSTAFA, KEMAL, MELKIORI MATWI na JONAS REUBEN 1980 Participatory Research and Pastoralist Development: The Experience of the Jipemayo Project in Western Bagamoyo District (Uchunguzi wa Kushiriki na Kushirikisha na Maendeleo ya Wafugaji: Mfano wa Mradi wa Jipemoyo. Wilaya ya Bagamoyo Magharibi) Dar es Salaam, Wizara ya Utamaduni na Vijana, marudio, uk. 494.

Kitabu hiki kinachambua kwa undani sana swala la wafugaji. Kuna takwimu za ukaguzi uliofanyika juu ya idadi ya mifugo katika kila kaya na ripoti kamilifu katika Kiswahili za mikutano michache kati ya viongozi wa wafugaji, vijana wafugaji, wachunguzi wa Jipemoyo na maofisa wengine wa serikali na wilaya. Msingi wa uchambuzi huu ni uchunguzi wa kushiriki na kushirikisha na mtazamo wa kiyakinifu. kwa mujibu wa mtazamo huu, wafugaji wanashiriki katika uchunguzi na wachunguzi wanashiriki katika siasa. Kitabu kinaonyesha uhusiano kati ya harakati mbalimbali na uenezaji wa ubepari na dola na jinsi vitu hivi viwili vinavyoanza kutawala mifumo ya wakulima ya uzalishaji mali. Harakati hizo ni pamoja na kuandikisha kijiji chao cha Mindu Tulieni, kuingiza mambo yanayohusu ufugaji katika masomo ya shule za msingi; na kupunguza idadi ya mifugo. Kabla ya kuandika matokeo ya uchunguzi wao kwenye kitabu hiki, wachunguzi waliwasilisha matokeo kwa wafugaji wenyewe ambao waliyatumia katika mipango na taratibu zao za utendaji.

Ripoti yao juu ya Semina ya Lugoba, Semina iliyokusanya pamoja maofisa wa serikali, wakulima, wafugaji na wachunguzi, ina maelezo mengi kuhusu taratibu za kiuchumi, kisiasa na kiitikadi zinazohusu wanawake. Wanawake na wanaume wafugaji wahawasilisha wenypwe maoni yao juu ya mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi, mahusiano ya kiumeni ya uzalishaji mali na itikadi zake.

82. NGALULA, THERESIA, F.K. 1977 Women as a Productive Force in the Tanzanian Rural Society: A Case Study of Buhangwa Village in Mwanza Distnct. (Wanawake Kama Wazalishaji Mali Vijijini Tanzania: Mfano wa Kijiji cha Buhangwa Wilayani Mwanza)Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tasnifu ya M.A. isiyochapishwa.

Makala haya yanachunguza nafasi ya wanawake na wanaume katika uchumi vijijini Tanzania kwa kuchunguza kaya 90 za kijiji cha kawaida kilicho wilayani Mwanza. Yanachunguza pia uzalishaji wa kilimo na usio wa kilimo, kazi za nyumbani na shughuli za kutunza watoto. Yanaangalia vilevile unyartyasaji na ugawaji wa mapato na ushirikiano katika siasa ya kijiji. Takwimu zinaonyesha kwamba kilimo cha chakula kinafanywa hasa na wanawake. Wanaume wanatumia muda mrefu zaidi katika kilimo cha mazao ya biashara. Wanaume wana uwezo mkubwa zaidi wa kujipatia zana nzuri kama plau na trekta. Asilimia 90 ya kaya zinalima kwa jembe. Kuhusu shughuli zisizohusu kilimo, wanawake wana nafasi ndogo kuliko wanaume kwa sababu ya kazi zao za nyumbani. Kwa hiyo wanawake walijishughulisha na kufinyanga, kufuma mikeka na kutengeneza pombe. Wanaume waliweza kufanya shughuli zenye faida kubwa zaidi kama kushona nguo, kusimamia duka na kuchoma mkaa. Takwimu zinaonyesha kwamba wanaume 32 kati ya 80 walifanya shughuli zisizo za kilimo lakini wanawake 16 tu kati ya 85 walifanya shughuli zisizo za kilimo. Kazi za nyumbani na za kutunza watoto zilifanywa na wanawake tu, ingawa vijana ambao hawajaoa walitaja kwamba wanafanya kazi hizo vilevile. Wanaume tu ndio wanamiliki mashamba na mifugo. Mali imenunuliwa kutokana na mauzo ya mazao au mahari ya binti zao. Kwa kawaida vitu vilivyonunuliwa kwa kuuza mazao ni mali ya mwanamume tu; kwa mfano ng’ombe na baiskeli. Wanawke huomba hela za kununua sabuni, chumvi au za nauli na kadhalika. Wanategemea moyo wa mume kupata vitu hivi. Ushirikiano wa wanawake katika siasa ya kijiji umefungwa sana, kwa sababu ya mzigo wao mkubwa wa kazi na itikadi ya kwamba siasa ni shughuli ya wanaume. Mara nyingine wanawake walizuiwa makusudi wasijiunge na Chama. Hali kadhalika mahudhurio yao kwenye madarasa ya Elimu ya Watu Wazima yameathiriwa na kazi zao nyingi.

83. OOMEN-MYIN, MARIE ANTOINETTE 1981 Involvement of Rural Women in Village Development in Tanzania: A Case Study in Morogoro District (Kushiriki kwa Wanawake wa Vijijini katika Maendeleo ya Kijiji Nchini Tanzania: Mfano wa Wilaya ya Morogoro)Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Elimu ya Kilimo, Morogoro, Machapisho ya Uchunguzi, uk. 136.

Ripoti hii ni sehemu moja ya uchunguzi mkubwa zaidi uliofanyika juu ya matatizo ya kuanzisha miradi midogomidogo ya kijiji. Uchunguzi huu oliangalia ushirikiano wa wanawake katika uamuzi uliofanywa na kijiji, matatizo yanayozuia ushirikiano wa wanawake, na mambo ambayo yangesaidia wanawake kushiriki kikamilifu zaidi. Mchunguzi alitumia mbinu za ukaguzi na uchunguzi wa kushiriki na kuangalia. Uchunguzi ulifanyika katika vijiji 8 wilayani Morogoro kwa muda wa wiki mbili. Baadaye mchunguzi alirudi kujadiliana matokeo ya uchunguzi na wanakijiji. Matokeo ya uchunguzi yanaonyesha kwamba wanawake wanashiriki kidogo katika uamuzi wa kijiji kulingana na wanaume, ingawa walishiriki sawasawa na wanaume katika miradi ya kilimo ya kijiji. Jambo kubwa lililoathiri ushirikiano wao ni fikra za wanaume za kudharau wanawake. Hali hii inaonekana kwa sababu wakuu wa kike katika kaya walishiriki zaidi katika uamuzi kuliko wanawake walioolewa. Katika vijiji ambapo mwenyekiti alikuwa ni mwanamke (vijiji 2 kati ya 8), wanawake walishiriki zaidi.

IIionekana kwamba elimu na uanachama wa UWT haukuathiri ushirikiano wa wanawake. Zaidi ya hapo ilionekana kwamba mambo mengine yaliyoathiri ushirikiano ni mzigo wa kazi za kila siku, mimba za mara kwa mara, watoto wengi na fikra za wanawake za kutojitathmini. Sera ya kuwahamisha watu kwenye vijiji haikusaidia wanawake, bali imeleta hali mbaya zaidi kwa wanawake. Hii ni kwa sababu imeongeza mzigo wao wa kazi kwa kuwashirikisha katika miradi ya kijiji bila ya kuwashirikisha katika uamuzi juu ya miradi. Pia serikali ya kijiji inatawaliwa na wanaume na sera hii haijajaribu kutatua matatizo kama umilikaji wa ardhi unaokataza wanawake wasimiliki ardhi; na taratibu za kisiasa ambazo zinatumia sera ya kuhamia kijijini ili kuwaonea wanawake.

Jambo moja zuri katika uchunguzi huu ni kwamba unazingatia swala la itikadi, kwa mfano, fikra tofauti za wanawake walioolewa, wakuu wa kaya wa kike, na wanaume juu ya maswala kama mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi nafsi ya wanawake katika siasa ya kijiji na kadhalika. Watu walipoulizwa “je, ni matatizo gani matatu makubwa sana kwa wanawake vijijini?” Wengi wao walitaja kwanza tatizo la kuzaa watoto wengi. Wengi walitaja uzazi wa majira kama njia ya kutatua tatizo hilo. Katika majadiliano ya baadaye, wanawake walisema kwamba “wanawake wote wenye watoto wawili au watatu wangependa kupata vyombo vya kuzuia mimba kama vingekuwepo.” Lakini walisema kwamba wanaume wanakataa kwa hiyo wanawake lazima wavifiche vyombo hivi. Walisisitizi kwamba vyombo hivi havipo vijijini. Watu wa mjini wanaposema kwamba wanawake wa vijijim hawataki vyombo hivi, wanaonyesha ujinga wao na kwamba hawajui hali halisi ya wanawake wa vijijini.

84. OOMEN-MYIN, MARIE ANTOINETTE 1980 “Wanawake Wanavyoshiriki katika Shughuli za Kijiji: Utafiti Uliofanyika katika Vijiji Vinane Wilayani Morogoro” Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Elimu na Mafunzo ya Kilimo, Morogoro, AEE Working Paper 80. 18. uk. 11.

Hii ni ripoti ya uchunguzi uliofanyika katika vijiji vinane wilayani Morogoro. Uchunguzi huo ulihusu ushirikiano wa wanawake katika shughuli za uamuzi unaohusu kijiji, vikwazo na mbinu za kuviondoa (tazama vilevile kitomeo na 83 kwa ufafanuzi zaidi). Pia lengo la utafiti, mpango wake na matokeo yanaelezwa vizuri. Vilevile ripoti inaambatisha picha zilizotumiwa na mchunguzi alipojadili matokeo ya uchunguzi na wanakijiji. Ripoti hii haina jalada gumu kama tafsiri yake ya Kiingereza. Idara ya Elimu na Mafunzo ya Kilimo ingetekeleza vizuri zaidi lengo lake la kutoa taarifa ya utafiti kwa wakulima wanaohusika kama ingetayarisha ripoti ya kudumu. Pia ingesaidia kama ingetumia herufi kubwa ili wale wanaojifunza kusoma waweze kuisoma. Hata hivyo, ni mara chache Idara yoyote ya Chuo Kikuu imeamua kutoa taarifa ya utafiti kwa wale watoaji habari waliohusika. Kwa hiyo ni mfano mzuri kwa wachunguzi wengine. (Tazama vilevile kitomeo 81).

85. RALD, JORGEN na KAREN RALD 1975 Rural Organisation in Bukoba District, Tanzania (Mpangilio wa Maisha Vijijini Wilayaya Bukoba) Uppsala, Scandinavian Institute of African Affairs, uk. 122.

Uchunguzi huu unahusu jinsi watu wa Bukoba wanavyopanga maisha yao na hasa wanavyotumia muda wao. Makala inachunguza ugawaji wa kazi kwa wanafamilia, mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi na mbinu za kilimo. Inafafanua kazi zinazofanywa na muda unaotumika kwa kila kazi (bajeti ya kazi na muda), matumizi na mapato ya nyumbani. Bukoba ni eneo ambalo lina idadi kubwa ya watu na ardhi ni haba na kwa hiyo ipo haja ya kupanga vizuri endapo mtu atataka kuongeza ardhi yake. Uchunguzi uliofanyika juu ya bajeti ya kazi na muda unaonyesha kwamba zipo tofauti muhimu kati ya wakulima. Zipo tofauti pia kati ya wakulima wanawake na wakulima wanaume. Wanaume wanafanya kazi za kulima kwa asilimia 45 ya siku moja (alfajiri mpaka usiku). Wanatumia asilimia 11 kwa shughuli za jamii na asilimia 44 kwa mapumziko. Lakini wanawake wanatumia asilimia 59 ya siku moja katika kazi za kilimo, asilimia 12 kwa shughuli za jamii, na asilimia 29 kwa mapumziko. Dhana ya “mapumziko” inayotumiwa ni pana sana, yaani ni pamoja na shughuli ambazo ni kazi, hasa kwa wanawake, kwa mfano kuuguza wagonjwa, kusaidia katika matanga na mazishi na shughuli nyingine za jamii.

86. REINING, PRISCILLA 1970 “Social Factors and Food Production in an East African Peasant Society: The Haya” (“Mambo ya Kijamii Yanayoathiri Uzalishaji wa Chakula katika Jamii Moja ya Wakulima wa Afrika Mashariki: Wahaya”) katika African Food Production Systems, Mhariri, Peter F. McLoughlin, Baltimore, John Hopkins Press, uk. 41 – 89.

Kwa ujumla, msingi wa mgawanyo wa kazi ni jinsi. “Kazi zimegawanywa katika sehemu mbili. Wanaume wanalima na kudhibiti migomba na mikahawa, na wanawake wanafanya pia kazi za nyumbani na kazi ya kuwatunza watoto. Lakini mgawanyo huu unaathiriwa sana na utajiri na hadhi ya familia. Familia tajiri inaweza kuwalipa vibarua kufanya kazi nyingine kama kuchota maji, kupalilia na kuvuna. Wahaya wanafanya shughuli nyingine zisizo za kilimo. Shughuli hizo nyingi zinafanywa na wanaume tu.

87. RIGBY, PETER 1980 “Pastoralist Production and Sodalist Transformation in Tanzania” (“Uzalishaji katika Jamii za Wafugaji na Mabadiliko ya Kuleta Ujamaa Tanzania”) katika Jipemoyo 2 iliyohaririwa na A.O. Anacleti. Scandinavian Institute of African Studies.

Makala haya ya kipekee yanachambua swala la wanawake katika jamii za wafugaji za Waparakuyu, Wabarabaig na Wamasai. Kwa kawaida wataalam hawajali na hawachunguzi unyonyaji na uonevu wa wanawake katika jamii za kiumeni za wafugaji. Katika makala hii mahusiano ya ukoo na mahusiano ya rika yanahusishwa na swala la wanawake. Makala yanachunguza mila za mahari na ndoa na jinsi zinavyohusiana na udhibiti wa mali na kazi. Hoja kuu za makala ni kwamba: (1) wanaume wanamiliki njia kuu za uchumi lakini wanawake wana nafasi muhimu katika udhibiti na ubadilishaji wa mali; (2) wanawake wanadhibiti kabisa mazao muhimu ya uzalishaji yaani maziwa, siagi, ngozi. Makala inatoa maelezo juu ya mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi na mahusiano ya kijamii ya kaya.

Bryceson na Mbilinyi (1978) wanapinga msimamo wa Rigby. Wanasema kwamba wanawake hawadhibiti njia kuu za uchumi wala kazi zao. Mfumo wa mahusiano ya kiumeni unawalazimisha wanawake kufanya zile kazi za kutunza familia na kutosheleza mahitaji yao ya kila siku. Mfumo huo vilevile unaathiri ugawaji wa mapato yanayotokana na kazi za wanawake. Hawapingi hoja ya kwamba wanawake wana nafasi muhimu katika ubadilishaji wa mali. Tatizo lipo katika namna ya kuelewa nafasi hii. Ingawa wataalam wanatofautiana kuhusu kazi za Rigby, yeye ni mfano mzuri wa mtaalam anayechunguza kwa undani na anayetoa maoni ya kipekee kuhusu swala la wanawake. Ni wataalam wachache sana waliochunguza jamii za wafugaji kwa undani kama yeye (tazama vilevile, Kjaerby, kitomeo na. 72, kwa uchunguzi wenye msimamo tofauti kuhusu jamii za wafugaji na swala la wanawake).

88. SACHAK, NAJMA 1979 “Creating Employment Opportunities for Rural Women: Some Issues Affecting Attitudes and Policies” (“Kuanzisha Nafasi za Kazi kwa Wanawake wa Vijijini. Maswala Machache Yanayoathiri Sera na Maoni”). Makala iliyowasilishwa kwenye International Political Science Association Congress, Moscow, tarehe 12 – 18 Agosti, uk. 18.

Makala haya yanazingatia haja ya kufasiri upya maana ya “uajiri” hasa tunapojadili uajiri vijijini. Katika makala hii mchunguzi anafafanua kazi za kuajiriwa kama zile kazi za mkataba pamoja na za miradi inayotegemea kazi za kujitolea, kazi za kibarua na jitihada za kuepukana na njaa. Msingi wa makala hii ni uchunguzi uliofanyika katika vijiji sita vya Wilaya ya Dodoma Vijijini. Uchunguzi huu unaonyesha uhusiano uliopo kati ya uajiri wa wanawake na historia ya njaa na umaskini katika vijiji hivi. Kwa mfano, ukaguzi wa awali uliofanyika kabla ya uchunguzi huu ulionyesha kwamba asilimia 55 ya wanakijiji wa kijiji kimoja walijaribu kupata kazi ya kuajiriwa wakati wa njaa. Kwa kawaida wanawake wanatafuta kazi ya muda ya kulima mashamba ya wakulima tajiri. Wengine wanahamia mjini kutafuta kazi ya utumishi, au ya kubeba maji au kuchoma mkaa. kwa sababu ana wajibu wa kutunza familia yake, mwanamke hana budi atafute hela pengine anaposhindwa kutosheleza mahitaji yake huko shambani. Lakini kwa sababu ya wajibu huu wa kutunza familia hana uhuru wa kwenda mbali. Hawezi kuhamia mjini ingawa kazi za kuajiriwa ni chache sana huko vijijini. Mchunguzi anathibitisha umuhimu wa wanawake katika kutosheleza mahitaji ya nyumbani ya hela taslimu (wananunua nyama, nguo za watoto wao na kadhalika). Ni rahisi zaidi kwa mwanaume kupata fedha taslimu kwa sababu yeye anamiliki bidhaa muhimu ya sehemu zile, ng’ombe. Lakini hata hivyo ni wanawake wanaoleta hela taslimu nyumbanl na kutekeleza wajibu ambao kimila ni wa wanaume. Jinsi wanawake wanavyotambua uwezo wao, mahitaji yao na mahitaji ya kijiji yanaathiriwa sana na hali ya uchumi wa kijiji. Wanawake wengi wanataka zana zinazopunguza mzigo wao wa kazi, kwa mfano mashine ya kusagisha. Wanakijiji walitaja kwamba katika wale wanaohama kijijini, wengi ni wanawake walioolewa wanaotafuta kazi. Hawa huwaacha watoto wao nyumbani. Wanawake wanahama kwa sababu uchumi wao wa nyumbani hautoshi kwa mahitaji yao ya lazima kama nguo na chakula. Makala yanasisitiza kwamba jambo moja linalowafanya wanawake wahame ni mpango mbaya wa kazi na hasa matumizi mabaya ya uwezo wa wanawake wa kufanya kazi. Jambo hilo linakwamisha sana maendeleo vijijini.

89. SHPIRO, KENNETH N. 1978 “Watu, Women and Development in Tanzania” (“Maji, Wanawake na Macndeleu katika Tanzania”). Makala iliyowasilishwa kwenve Third Annual Conference ot the Internationul Water Resources Associatiun, Sao Paulo, Brazil, uk. 10).

Makala hava yanaonvesha uhusiano uliopo kitakwimu kati ya ukaribu wa maji na uzalishaji mali. Yanatoa takwimu juu ya muda unaotumiwa na wanawake kwa kazi zisizo kazi za kilimo. Ukaguzi ulifanyika katika kaya 76 za wakulima wa Wilaya ya Geita. Takwimu zinaonyesha kwamba muda unaotumiwa kwa mwaka kuchota maji una thamani ya shs. 13.00. Yaani, kama mwanamke angetumia muda ule anaotumia kuchota maji, kulima pamba, angepata faida ya shs. 13.00. Takwimu hizo zinazingatia kwamba kwa wastani kaya moja inapata shs. 500.00 kwa mwaka kutokana na pamba. Ukaguzi uliofanyika juu ya muda unaotumiwa kwa kazi zisizo za kilimo unaonyesha kwamba wanawake wanatumia muda wao mwingi kwa shughuli za nyumbani (asilimia 37). Wanaume wanatumia asilimia 8 tu ya muda wao kwa shughuli za nyumbani (hata kama matengenezo ya nyumba yanahesabiwa kuwa kazi ya nyumbani). Wanaume wanatumia muda mwingi kuliko wanawake katika shughuli za kunywa pombe, kupumzika na kuumwa. Inawezekana kwamba wanawake watapinga pembejeo nyingine kwa mfano dawa ya vidudu, kwa sababu dawa hii inahitaji maji mengi na inaongeza mzigo wao wa kazi. Zaidi ya hapo, wanaume hawataki kuleta maji wenyewe. Kwa sababu ya tatizo hilo la maji, ilibidi serikali itafute dawa nyingine inayotumia mafuta badala ya maji. Makala haya yana data yenye manufaa sana na ni mfano mzuri wa uchunguzi wa muda wa kazi.

90. STANLEY, JOYCE na ALISA LUNDEEN 1979 Audio-Cassettes Listening Forum: A Participatory Women’s Development Project (Mkutano wa Kusikiliza Kaseti: Mradi wa Maendeleo ya Wanawake Unaotumia Mbinu za Kushirikisha) Washington, D.C. uk. 108.

Mradi huu umeshirikisha wanavijiji wa vijiji viwili mkoani Arusha, Majengo na Kimundo. Wanawake wa vijiji walishiriki katika kufanya ukaguzi juu ya mahitaji ya kijiji na uwezo wa kijiji wa kutosheleza mahitaji hayo. Pia walishiriki katika kukusanya taarifa mbalimbali, kubainisha matatizo ya kijiji, kujadili kupanga na kutekeleza. Ripoti inasema kwamba mbinu hizo zimefanikiwa. Lakini mradi huu umeathiri tofauti za wanawake wa vijiji hivi viwili. Ushirikiano ulikuwa mkubwa zaidi pale palipokuwa na kiwango cha juu zaidi cha maisha na kiwango cha juu cha ushirikiano katika shughuli za vikundi vya kijiji na idadi kubwa zaidi ya miradi ya maendeleo ya kijiji. Kitabu hiki kinasifu sana mbinu rahisi na inafanikiwa. Lakini kinatoa tahadhari kwamba labda kufanikiwa kwake kunategemea mambo kama uongozi bora wa kijiji na moyo wa wanakijijii wa kupokeo na kushiriki katika mradi huu.

91. STORGAARD, BIRGIT 1976 “Women in Ujamaa Villages” (“Wanawake katika Vijiji vya Ujamaa”) Rural Africana Na. 29, uk. 135 – 155.

Makala haya yanatokana na uchunguzi uliofanyika Wilayani Bukoba. Inaelezea hadhi ya wanawake katika jamii ya jadi, ambapo wanawake walipewa hadhi ya chini. Halafu inachambua uwezo wa siasa ya ujamaa kubadilisha hadhi hii. Makala yanatoa hoja ya kwamba vijiji vya ujamaa viliendelea kutumia mfumo wajadi wa mgawanyo wa kazi, na pia viliendelea kugawa kazi kwa taasilia badala ya kuanzisha vikundi vya aina nyingine vya kazi. Kwa hiyo hali ya chini ya wanawake iliendelea kuwepo. Vijiji vya ujamaa vilitambua aina mbili za uzalishaji mali: shamba la kijiji na shamba la mtu binafsi. Mtindo huu haukusaidia wanawake. Wanawake. wangelima shamba la kijiji labda wangedhibiti angalau kidogo njia kuu za uchumi (yaani shamba) na mapato yake. Lakini ilionekana kwamba wanawake walitakiwa kulima mashamba ya waume zao. Katika kilimo cha mashamba haya wanakijiji waliendelea kushikilia mfumo wa jadi wa mgawanyo wa kazi na ugawaji wa mapato. Huduma za jamii kama bomba la maji, visima vya kijiji na vituo vya watoto wadogo havikubadilisha kimsingi hali ya wanawake katika vijiji vya ujamaa. Makala haya yana jedwali zinazoonyesha muda wa kila kazi kufuatana na elimu, mahudhurio ya mikutano ya ushirika, jinsi, na kadhalika.

92. SWANTZ, MARJA-LIISA 1977 Strain and Strength Among Peasant Women in Tanzania (Mivutano na Nguvu ya Wanawake wa Vijijini Tanzania) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, BRALUP, Research Paper Na. 48, uk. 81.

Uchunguzi ulifanyika juu ya wakulima wenye mashamba madogo wa mikoa ya Bukoba na Kilimanjaro. Madhumuni ya uchunguzi ilikuwa kuchambua hali ya mwanamke mkulima maskini katika Tanzania ya leo, kufafanua matatizp yanayozuia usawa wa wanawake, na kubainisha nguvu na uwezo wa wanawake ambao hautumiwi. Sababu ya kimsingi ya hali ya chini ya wanawake wa jamii hizo mbili ni kwamba hawana haki za kumiliki ardhi. Asilimia 97.8 ya wanawake wanaojishughulisha kiuchumi wanalima mashamba madogo ambayo hawayamiliki. Kwa hiyo wanafanya kazi lakini hawana usemi katika uamuzi juu ya kazi zao na hawadhibiti mapato ya jasho lao.

Makala inaonyesha kwamba katika mikoa yote miwili wanawake walijitahidi kujitegemea. Wanawake wasioolewa, walioachana na waume zao au wajane, waliweza kupata usawa kiasi fulani, hata kama bado walikuwa na wajibu wa kuwatunza watoto. “Kiuchumi na kijamii, hali yao ilikuwa nzuri kushinda wanawake walioolewa, na walishiriki zaidi katika shughuli za maendeleo na za kijiji. Mwenye hadhi ya juu huko nyumbani ni mwanamume, na hadhi hii inamfanya mwanamke awe mtumishi wa mwanamume”. Lakini kwa upande mwingine wanawake wa Kichagga wana nafasi nzuri ya kutumia uwezo wao wote bila kuhatarisha ndoa zao. Hii ni kwa sababu wanaume wengine wa Kichagga wanahamia mijini na wanawake wengi wanapata nafasi ya masomo.

93. TANZANIA, Wizara ya Kilimo 1977 “Demonstrations of an Interdisciplinary Approach to Planning Adaptive Agricultural Research Programmes” (“Mifano ya Mbinu ya Kutumia Elimu ya Masomo Mbalimbali katika Kuandaa Miradi ya Uchunguzi wa Kilimo”). Ripoti Na. 3 Desemba, 1977. Sehemu ya Uchunguzi, Wizara ya Kilimo na Kitivo cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na CIMMYT, Nairobi.

Ripoti hii inatumia mbinu ya uchunguzi wa kilimo inayozingatia mbinu za kuzalisha mazao na uchumi wa kilimo. Inachunguza njia za kutatua tatizo kubwa sana la ukosefu wa chakula cha kutosha katika sehemu za wilaya za Morogoro na Kilosa zinazopata mvua kidogo. Waliamua kupanda mbegu za mahindi yanayokomaa upesi. Mbegu hizi zinafaa kwa sababu ya uhaba wa mvua na upungufu wa wafanyakazi. Ripoti inaeleza “mfumo wa kilimo” pamoja na taratibu za kuuza mazao na kupanga bei. Lakini haikuangalia kabisa nafasi maalum ya wanawake katika kuzalisha, kutayarisha, kusagisha, kuhifadhi na kuuza mazao. Tangu mwanzo mpaka mwisho ripoti inasisitiza “mkulima” kama meneja wa shamba na wafanyakazi wake, yaani familia. Wanawake wanatajwa kama wale wanaoonja ladha ya aina mbalimbali za mahindi. Kosa hili la kutozingatia nafasi ya wanawake linaweza kuathiri usahihi wa matokeo ya uchunguzi huu. Zaidi ya hayo, wanapobadilisha ratiba ya kupanda na kuvuna ili wapate wafanyakazi na/au ardhi zaidi ili kuzalisha zaidi mazao ya biashara, wanasahau kwamba wanawake hawapati faida inayotokana na mazao hayu. Kwa hiyo wanawake wanaweza kusita kuongeza kilimo cha mazao ya biashara. Ripoti hii inaona kwamba wafanyakazi wote wa familia hawana matatizo. Maoni hayo si sahihi. Vilevile kwa sababu ugawaji wa mapato ni tofauti baina ya wanawake na wanaume, motisha yao ya kuzalisha zaidi ni tofauti. Kwa hiyo tamko la kwamba “wafanyakzi wote wanaweza kushiriki katika kazi zote” (uk. 17). sharti litiliwe mashaka sana.

94. TOBISSON, E. Women, Work and Nutrition in Nyamurigura Village, Mara Region, Tanzania (Wanawake, Kazi na Lishe katika Kijiji cha Nyamurigura Mkoa wa Mara, Tanzania). Ripoti iliyowasilishwa kwa TFNC 1980 uk. 127.

Makala haya yanasisitiza matatizo ya kubadilisha kilimo cha kijungumeko cha mazao mbalimbali na kuanzisha kilimo cha zao moja la biashara, na hasa athari za mabadiliko haya kwa wanawake na watoto. Makala yanaonyesha kwamba sera ya kikoloni na mbinu za serikali za kuleta maendeleo vijijini baada ya uhuru ziliendeleza ukandamizaji wa wanawake katika uzalishaji mali. Isitoshe, mbinu hizi ziliongeza kazi za wanawake. Mzigo wao mkubwa wa kazi unawazuia kushiriki katika shughuli za kisiasa na kazi za pamoja. Vilevile unaathiri upatikanaji wa chakula bora kwa familia. Ripoti ina habari nyingi kuhusu chakula na afya ya Wakuria wa kijiji cha Nyamwigura, chakula cha wanawake wenye mimba na wanaonyonyesha, mahusiano ya uzalishaji mali baina ya wanaume na wanawake kwenye kiwango cha kaya na matatizo ya wanawake kutoweza kushiriki (kwa sababu ya kukatazwa au kwa sababu ya kazi zao nyingi) katika majadiliano ya kisiasa, uamuzi na kazi za pamoja.

95. ULLA VUORELA, pamoja na msaada wa JONAS REUBEN 1981 “Women’s Role in Post-Harvest Food Conservation, Tanzania Case Study” (“Nafasi ya Wanawake katika Kuhifadhi Mavuno, Mfano wa Tanzania”). Ripoti ya Uchunguzi iliyowasilishwa UNU, Marudipa.

Uchunguzi huo ni awamu ya kwanza ya Mpango wa Hifadhi ya Mavuno unaotekelezwa kwa msaada wa Mradi wa Kufuta Njaa Duniani wa Chuo Kikuu cha Kimalaila. Uchunguzi ulitanyika katika vijiji vitatu, Msoga, Mindu Tulieni na Diozile I pamoja na kijiji cha Lunga, kilicho kando ya barabara ya Chalinzc – Mombo na kinachokuwa upesi kwa sababu ni mahali muhimu kiutawala na kiuchumi.

Wanakijiji wa Mindu Tulieni ni wafugaji na mahusiano yao ya kijamii ni ya kiumeni. Wanakijiji wa Diozile I na Msoga ni wakulima na mahusiano yao ya kijamii ni ya kiukeni. Katika kijiji cha Lunga uchunguzi ulifanyika juu ya wake wa wafanya biashara ndogondogo na wanawake wafanya biashara. Makala yanapanua sana fasiri ya chakula bora, yaani chakula bora ni mambo yote yanayohusu uzalishaji, ugawaji, utayarishaji na ulaji wa chakula. Katika uchunguzi wa chakula borajambo muhimu ni uwezo/nafasi ya mtu kujipatia chakula bora. Uchambuzi wa chakula na utamaduni wa vikundi hivi vya wafugaji na wakulima wa Lugoba ulionyesha kwamha upo uhusiano kati ya nyenzo za uzalishaji chakula na fikra za utamaduni kuhusu chakula. Vikundi vyote viwili vina mazingira yanayofanana lakini chakula chao ni tufauti kabisa.

Sehemu inayohusu Mindu Tulieni ina ufafanuzi wa undani na wa kipekee wa maswala haya katika jamii ya watugaji. Wanawake wanatatanishwa na watoto, na katika sheria za jadi wanafikiriwa kuwa sawasawa na mtoto asiyejitegemea. Mzee mmoja alisema mwanamke hahitaji mali kwa sababu “sisi tunamtunza vizuri kama tunavyotunza ng’ombe zetu”. Mwandishi anatoa hoja kwamba wanawake wanafikiriwa kuwa kitu kama bidhaa, na mara nyingi hawana thamani sawasawa na ng’ombe. Kina binti wana thamani kwa sababu ya mahari, na kwa mumewe, mwanamke ana thambani kama mzazi na mfanyakazi. Hali hii ya kutothamini wanawake kama binadamu ilidhihirishwa wakati wa kuhesabu idadi ya watu katika kaya. Hawakuhesabu wanawake wote wa kaya kama watu wazima. Ilifikiriwa kwamba watu wazima ni wanaume na wale wanawake wazee walioacha kuzaa; kwa mfano mamake mzazi yule mkuu wa kaya. Zaidi ya hapu makala inajadili uashiki na uwezo wa kuzaa, pamoja na tohara, jambo ambalu ni la lazima kwa wasichana.

Katika kijiji cha Msoga, uchunguzi ulifanyika juu ya maana ya sherehe za kutoa mwali katika jamii za kiukeni. Katika sherehe hizo kaya inatumia sembe ambayo ingetosha kulisha familia nzima kwa miezi saba. Sembe hii inatumiwa katika upishi wa pombe kwa ajili ya sherehe ya kumtoa mwali. Hali ya wanawake katika vijiji inahusishwa na harakati za wanakijiji za kujiandikisha kama kijiji. Uchunguzi uliofanyika Lunga unaonyesha kwamba wake za wafanya biashara hawana njia nyingine ya kupata mapato ya fedha isipokuwa kuwategemea waume zao. Kama ilivyo kwa wanawake wakulima, na hasa wanawake wanaopika pombe au wanaofanya biashara. hawa wake wanafungwa sana. Uchunguzi uliofanyika huko sokoni unafafanua mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi, hasa katika shughuli za biashara ndogondogu.

Marejeo Mengine

HAMDANI, SALHA 1979 “Peasantry and the Peasant Woman in Tanzania” (“Wakulima na Mwanamke Mkulima Tanzania”). Makala no. 8, BW, uk. 9.

KOKUHIRWA, H. 1975 “Towards the Social and Economics Promotion of Rural Women in Tanzania” (“Kukuza Kiuchumi na Kijamii Wanawake wa Vijijini Tanzania”) The Design of Educational Programmes for the Social and Economic Promotion of Rural Women, International Institute for Adult Literacy Methods, Tehran, Iran, uk. 239 – 254.

MAPOLU, HENRY “The social and Economic Organization of Ujamaa Villages” (“Mfumo wa Kijamii na Kiuchumi katika Vijiji vya Ujamaa”). Tasnifu ya M.A. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Na. 191 Sura inayohusika ni “The Role of Women”, uk. 161 – 168.

MBILINYI, MARJORIE 1977 Women: Producers and Reproducers in Peasant Production (Wanawake: Wazalishaji Mali na Waendelezaji wa Jamii katika Uzalishaji wa Wakulima) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Makala va ERB, 77.3, uk. 39 na bibliografia.

RALD, A. 1969 “Land Use in Buhaya Villages: A Case Study from Bukoba District, West Lake Region (“Matumizi ya Ardhi katika Vijiji vya Buhaya: Mfano kutoka Wilaya ya Bukoba, Mkoa wa Ziwa Magharibi”) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, BRALUP Research Paper Na. 5, uk. 63. 6. Wanawake Wafanyakazi

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!