VYOMBO VYA HABARI VIMETEKWA NYARA NA MAGENGE YA WABORONGAJI WA KISWAHILI

By , in Sarufi na Utumizi Wa Lugha on .

Na KEN WALIBORA

Kwa Muhtasari

Katika miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya kuibuka kwa matangazo ya redio ya masafa ya FM, kuna wimbi la watu wasiokuwa na mafunzo maalum waliopewa ajira katika vyombo vya habari.

KATIKA miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya kuibuka kwa matangazo ya redio ya masafa ya FM, kuna wimbi la watu wasiokuwa na mafunzo maalum waliopewa ajira katika vyombo vya habari.

Wengi wao ni machale (comedians) wanaotumiwa kuleta ucheshi kwa hadhira, hasa redioni na runingani.

Mifano michache kutoka Kenya ni kama vile Inspekta Mwala wa Redio Citizen, Mwalimu King’ang’i wa Classic 105, Obinna aliyekuwa wa Easy FM, Teacher Wanjiku aliyekuwa wa QFM, Cleopas Awinja wa Milele FM na Makokha aliyekuwa wa KBC na kadhalika.

Mizaha ya machale hawa wasiowahi kusomea taaluma ya uanahabari wala uchale wenyewe, inaelekea kuwavutia wasikilizaji na watazamaji.

Ni mizaha iliyokitwa kwenye ukengeushi na ukiukaji wa kanuni, si za taaluma tu bali za lugha.

Kwa hiyo raghba yao kwa hadhira yao imo katika namna walivyotamka Kiswahili au hata Kiingereza kwa lafudhi yenye taksiri ya makundi fulani ya watu wa kabila au taifa fulani.

Obinna kwa mfano anaigiza lafudhi ya Kiingereza ya watu wenye asili ya Kinaijeria.

Mwala anaigiza lafudhi ya Kikamba na Makokha lafudhi ya Kiluhya.

Tunaweza kwa kweli tukatunga nadharia kuwa mbali na fujo na ngono kuwa vivutio vikubwa katika filamu, vyombo vya habari, na kazi ziitwazo fasihi pendwa, uborongaji wa lugha umekuwa bidhaa iliyopata soko zuri katika vyombo vya habari.

Kama hili lingeishia katika kuchekesha tu si vibaya kwa kweli.

Hakuna mtu asiyeona raha na kuangua kicheko kwa kusoma au kusikia kichekesho kizuri ila yamkini awe ana usununu usiokuwa na dawa.

Labda huo ndio ubinadamu wetu, tunapunguza makali ya dhoruba za maisha kwa mizaha, vicheko na vichekesho.

Linaweza kuwa jambo la kuchekesha kumsikia chale Daniel Ndambuki, aliye na nyuso mbili za kisanii yaani Churchill (NTV) na King’ang’i (Classic 105 FM) akiitaja Mombasa kama Mombasani.

Hata hivyo, tukiona kwamba baada ya muda Mombasa si Mombasa tena hata katika mawanda rasmi bali ni Mombasani kwa sababu chale mmoja mashuhuri amelitumia hilo katika uchekeshaji au uchale wake, tunahofia kwamba hatua kwa hatua vyombo vya habari vitakuwa vimechangia katika ukiukaji na upotoshaji mkubwa.

Kiini cha yote haya kwanza ni waajiri na wamiliki wa vyombo vya habari kufuata andasa zao tu ambazo zinadhibitiwa na tamaa ya tija ya kibiashara na liwe liwalo.

Hilo ndilo linalowafanya waajiri watu wasiokuwa wanataaluma wa uanahabari kuwa watangazaji. Isitoshe, watu hawa wanapoajiriwa kutumia Kiswahili katika ajira zao, lao kubwa ni kukitumia vibaya.

Tokeo ni mlipuko wa wanahabari bandia wanaotumia Kiswahili bandia. Ndio wanaotawala hewani- redioni na runingani.

Kwa kweli mara nyingine wale wanaotumia Kiswahili ipasavyo huwa ndio wachache na wanaposikika hewani huwa kama watu waliotoka sayari nyingine na kuzungumza lugha ya kigeni.

Hali halisi ya utata uliopo inaweza kufafafanuliwa na aina ya vipindi vya maigizo na filamu zinazonunuliwa ili kuonyeshwa katika runinga.

Katika uzoefu wangu, nimeshuhudia mwenyewe jinsi wasimamizi wanaohusika na mchakato wa kununua vipindi vya runinga wanavyovikataa vipindi vilivyoandaliwa kwa Kiswahili sanifu na fasaha.

Kisingizio chao ni kwamba Wakenya hawawezi kuelewa Kiswahili, wataelewa Sheng tu.

Yaani kwa maneno mengine kwa mujibu wa mantiki ya wasimamizi hao, Kiswahili ni kama lugha ya kigeni kama kwao hakijawa lugha ya kigeni tayari.

Je, ni kweli kwamba Wakenya hawawezi kuelewa Kiswahili ambacho wote wanaohitimu masomo ya sekondari huwa wamekisoma angalau kwa miaka kumi na miwili?

Je, Wakenya hawawezi kukielewa Kiswahil ambacho ni lugha yao ya taifa na mojawapo ya lugha zao rasmi mbili?

Je, kuna kinaya na kimako zaidi ya hiki? Je, unaweza kuwazia hali ambapo filamu na vipindi vya Kiingereza vitalazimika viwe katika Kiingereza kibaya kwa sababu Waingereza hawawezi kuelewa Kiingereza kizuri?

Itikadi Kiswahili Sanifu hakichekeshi

Sambamba na hilo, itikadi kwamba watu hawawezi kuchekeshwa kwa kutumia lugha sahihi ya Kiswahili imekita mizizi, nayo thamani ya kucheka ni kubwa.

Yamkini hakuna bidhaa inayouzwa zaidi siku hizi katika vyombo vya habari kama vichekesho.

Ila waandishi na waigizaji wa vichekesho vya Kiswahili sanifu au fasaha wameadimika kama maziwa ya kuku.

Na kama inabidi kuvuruga lugha ili kuchekesha, basi wamiliki na waajiri wako tayari kuwaajiri wataalamu wa kuvuruga na kusaidia wananchi wa kawaida kuvuruga lugha vilevile.

Ukweli ni kwamba tasnia ya utayarishaji wa vipindi vya runinga na sinema nchini Kenya, mathalan, ina muungano wa wakiritimba ambao huamua ni kipindi gani kitanunuliwa na kituo kipi na mwandishi wa kipindi hicho na waigizaji ni nani.

Aidha, wao ndio wanaoamua ni nani atapewa kazi ya kutafsiri hati zozote rasmi na zisizokuwa rasmi kama vile matangazo ya biashara na stakabadhi mbalimbali.

Tathmini yangu ni kwamba maadamu waandishi na waigizaji waliomo katika genge hili la wakiritimba huwa hawana umilisi, mafunzo, wala tajriba ya kutosha ya Kiswahili, hujilinda dhidi ya wale walio weledi wa Kiswahili hasa, kwa kuzuia vipindi vya Kiswahili halisi na kupendelea vile vya Sheng.

Au tuseme hivi, katika genge hili la wakiritimba wanaodhibiti tasnia ya filamu, vipindi na matangazo ya biashara hakuna watu wanaoweza kulia lugha ya Kiswahili ikifa.

Hawana uchungu nacho.

Recommended articles