Utafiti wa Lugha ya Kiswahili

By , in MAENDELEO YA KISWAHILI on . Tagged width:

Katika mojawapo ya makala zangu, nimewahi       kueleza kuwa mojawapo ya njia za kukiimarisha Kiswahili ili kiwe kweli ni tunu ya taifa ni lazima serikali itoe fedha za kutosha za kufanya utafiti lengo likiwa ni kuimarisha msamiati na istilahi za Kiswahili na hatimaye kuchapisha kamusi za istilahi za taaluma mbalimbali. Tunaweza kufanya hivyo kwa kutumia hazina iliyopo katika lugha zetua za asili zikiwamo lugha za Kibantu na pia zile ambazo siyo za Kibantu. Eneo jingine la utafiti ni katika lahaja za Kiswahili kama Kimvita, Kiamu, Kimtang’ata, Kipemba, Kitumbatu, nk.

Nilitoa mifano ya maneno ambayo yamesanifiwa na Bakita katika kipindi cha nyuma ambapo maneno ya asili kama ya lugha za makabila yetu yamsanifiwa na kuingizwa katika lugha ya Kiswahili. Orodha ya msamiati na istilahi imetayarishwa na kusanifishwa na kuchapishwa na Bakita katika vijitabu vilivyojullikana kama ‘Istilahi za Kiswahili’. Waandishi wa makala na vitabu wanatumia vijitabu hivi kujipatia tafsiri mbalimbali za kitaaluma kwa Kiswahili.

Utayarishaji wa orodha ya maneno ya kitaaluma yaliyosanifiwa ni sehemu tu ya utafiti katika lugha ya Kiswahili. Yako maeneo mengine ya utafiti wa Kiswahili kama vile maandishi ya zamani yaliyoandikwa na mabigwa wa Kiswahili ambayo yako katika nyaraka za zamani. Baadhi ya nyaraka hizi ambazo zimefichika bado hazijachapishwa. Tunao mfano wa mwandishi nguli wa Kiswahili kama Sheikh Shaaban Robert aliyeandika vitabu vingi vya fasihi ya Kiswahili. Vitabu hivi vimetumika kama vitabu vya kiada katika shule na vyuo tangu wakati wa uhuru na hadi sasa. Pia imefahamika kwamba nyaraka nyingi ambazo bado hazijachapishwa zinaweza kutayarishiwa  vitabu baada ya kuhaririwa. Ziko nyimbo na majigambo mengi kutoka katika lugha za asili na pia lahaja za Kiswahili kama Kipemba, Kitumbatu, Kimtang’ata, Kimvita, Kiamu, n.k. ambazo ni hazina kubwa ya lugha ya Kiswahili.

Eneo jingine la kufanyia utafiti ni katika ufundishaji wa Kiswahili katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu. Ufundishaji unaambatana na upatikanaji wa vitabu. Hata hivyo, uandishi wa sasa  wa vitabu ni wa kulipua kwani hauzingatii fasihi na sarufi ya Kiswahili. Wako waandishi wanaorubuniwa na wachapishaji ili waandike vitabu na kuvisambaza shuleni kama vitabu vya kiada. Vitabu hivi havihakikiwi na taasisi husika hivyo vinakuwa chini ya viwango kitaaluma. Utayarishaji wake hauzingatii misingi ya sarufi na fasihi  wala  mitalaa iliyotayarishwa ili kulingana na kiwango cha taaluma ya wanafunzi. Inatakiwa kuwe na umakini mkubwa unaotakiwa katika matumizi ya lugha   iliyo sanifu na yenye mada sahihi  tofauti na ilivyo  sasa ambapo  yako makosa mengi katika vitabu hivi. Hali hii inaonyesha kuwa waandishi na wachapishaji wanalipua katika kazi zao na kujipatia fedha nyingi ambazo si halali.

Mbali na umakini katika utayarishaji wa vitabu, eneo jingine ni uteuzi na utayarishaji wa wanachuo kuwa walimu weledi wa kufundisha shule za msingi na sekondari. Walimu wanapaswa kuwa hodari katika masomo yao hasa katika lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo wanaochaguliwa kujiunga na vyuo wanatakiwa wawe wamefaulu daraja la kwanza, la pili au la tatu. Iwe ni mwiko kumchagua mwanafunzi aliyefeli somo la Kiswahili au aliyefaulu daraja la nne. Inaonekana kuwa tumeanzisha daraja la nne kama danganya toto. Wanaopata  daraja la nne wamefeli na hawawezi kuchaguliwa kuendelea na mafunzo ya aina yoyote.                                                                                                                                                                                                                                                                                                                             Nakumbuka  katika kipindi ukoloni cha miaka ya 1950 -1960, Daraja la Nne halikuwapo bali kulikuwa na ‘General Certificate of Education (GCE)’ na waliopata daraja hilo walisomea ualimu Daraja B ijapokuwa walikuwa wamemaliza darasa la XII.

Eneo jingine la kukiimarisha Kiswahili ni kuwa na wataalamu wa lugha mikoani. Katika kipindi cha miaka ya 1974 – 1990 walikuwapo maofisa lugha kwa kila mkoa na wilaya. Kazi yao ilikuwa ni kuhamasisha ukuzaji na kuratibu matumizi ya Kiswahili mikoani na wilayani katika shule na ofisi za serikali na mashirika ya umma. Maofisa lugha wa mikoa walikuwa ni wale waliosomea somo la Kiswahili katika Kidato cha Sita. Serikali Kuu iliwaajiri na kuwaandaa kwa kuwapa mafunzo mafupi ya mbinu za utafiti na uendelezaji wa Kiswahili. Baadaye kada hii ya wataalamu wa lugha ilifutwa. Ingekuwa jambo bora kama tungekuwa na kada hii tena ambayo itaandaliwa vizuri zaidi na kupewa utaaluma na vifaa vya utafiti. Baada ya kuchaguliwa, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) wangepewa jukumu kuwa la kuwanoa vilivyo. Kwa kufanya hivyo, tanzani kweli itakuwa ni chimbuko la lugha hii na mahali pa kujifunza Kiswahili.

Chanzo >>>>>

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!