USANIFU WA MAANDISHI

By , in Kidato V-VI on .

Maana:

Usanifu ni ufundi au ustadi wa kufanya jambo kwa kutumia lugha. Ni kwa vipi msanii anaifuma lugha katika kujadili jambo fulani.

Usanifu wa maandishi ni utaalamu wa kuchunguza maandishi na kupata mbinu muhimu zilizosaidia kukamilisha habari fulani. AU

Ni kitendo cha kuchunguza mbinu mbalimbali za kifani au za kisanaa ambazo zimemuwezesha msanii (mwandishi) kufanikiwa au kutofanikiwa katika kuandaa kazi yake.

VIPENGELE MUHIMU  VYA KUZINGATIA KATIKA  USANIFU WA MAANDISHI

 1. Aina ya matini (kazi iliyoandaliwa)

Katika kuangalia aina ya matini tunayoishughulikia, matini huweza kugawanywa katika makundi ya msingi matatu, ambayo ni mkondo/muundo wa;

 1. Riwaya

Tunaweza kamua aina ya matini kuwa ni ya muundo wa huu ikiwa kuna uwepo wa monolojia/masimulizi yaani kazi hiyo imetawaliwa na matumizi ya nafsi ya tatu umoja na wingi, na haina muundo wa tamthiliya wala ushairi.

 1. Tamthiliya

Itakuwa ni ya muundo wa tamthiliya  ikiwa ina majibizano ya pande mbili yaani dayalojia. Ni muundo unaotawaliwa na matumizi ya nafsi ya kwanza, umoja na wingi na haina muundo wa riwaya wala ushairi.

iii.  Ushairi

Aina ya matini itakuwa ni ya muundo wa ushairi endapo kuna uwepo wa beti, yaani habari imewekwa katika vifungu vya mistari kadhaa kadhaa na haina muundo wa riwaya au tamthiliya.

Matini zinazoweza kushughulikiwa zaweza kuwa:-

–   Kama ni kifungu cha habari (nathali) yaani masimulizi.

–   Yaweza kuwa mazungumzo (majadiliano)

–  Kama ni ushairi utakuwa kwenye beti.

Kumbuka: kama itatokea mwandishi ametumia muundo wa riwaya na ushairi kwa pamoja tutaangalia ni mtindo upi umeutawala mwingine. Kwa mf. Msanii aliyetumia muundo wa riwaya anaweza kuingizia beti za shairi katika kazi yake hiyo kama mbinu tu ya kuipamba, hivyo kazi hiyo itakuwa ni ya muundo wa riwaya. (hakuna muundo/aina ya matini iitwayo changamano)

 1. Kwa ufupi, eleza matini inahusu nini

Katika kipengele hiki huwa tunaangalia matini tuliyopewa imehusu jambo gani au imezungumzia kitu gani? Mfano matini yaweza kuelezea magonjwa hasa UKIMWI, malaria, kifua kikuu, maisha ya kijana masikini, mapenzi kati ya msichana na mvulana, vita kati ya nchi moja na nyingine n.k

 1. Muundo uliotumika katika matini

Ni mpangilio/mtiririko/mfuatano wa matukio katika kazi ya fasihi, yaani mwanzo, mwendelezo kilele/upeo na mwisho ambao hugusa mambo yote katika tamthilia (maonesho) na riwaya (sura). Hivyo kama matini ni ya muundo wa riwaya au tamthiliya, muundo waweza kuwa wa moja kwa moja, rejeshi au muundo rukia.

Kama ni ushairi tunaangalia idadi ya mistari katika ubeti wa shairi na kupata miundo tofauti tofauti kama tamolitha (1), tathnia(2), tathlitha(3), tarbia(4), takhmisa(5), au sabilia (6 +……..)

KUMBUKA: Endapo umekuta shairi lina mchanganyiko wa idadi ya mistari katika beti zake yaani mfano ubeti wa kwanza una mistari mitatu, wa pili una mistari minne, wa tatu una mistari sita, wa nne una mistari miwili…….. Hutajadili muundo katika shairi hilo. (Muundo wa namna hiyo haujadiliwi katika usanifu wa maandishi)

 1. Mtindo

(TUKI, 1981) Ni namna/jinsi ya kufanya kitu kwa kufuata utaratibu fulani. AU

Ni namna/jinsi msanii anavyoiumba kazi yake na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha tofauti toka msanii mmoja hadi mwingine. (upekee wa mwandishi)

Katika tamthiliya na riwaya msanii anaweza kutumia mitindo mbalimbali ili kuipamba kazi yake na kuipa mvuto wa upekee. Mitindo hiyo yaweza kuwa;

 • Matumizi ya monolojia na dayalojia.
 • Matumizi ya nafsi, yaani nafsi ya kwanza, ya pili au ya tatu.
 • Matumizi ya igizo ndani ya igizo.
 • Matumizi ya taarifa ya habari katika redio.
 • Matumizi ya maandishi katika mabango.
 • Matumizi ya kukopa msamiati toka lugha nyingine.
 • Matumizi ya picha na taswira.
 • Matumizi ya nyimbo.
 • Matumizi ya barua.
 • Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi.
 • Matumizi ya lugha matusi n.k

Katika ushairi tunaangalia uzingatiaji na kutokuzingatia kanuni za utunzi wa mashairi hasa urari wa vina na mizani na muundo wa tarbia. Hivyo kuna miundo ya aina mbili katika ushairi ambayo ni mtindo wa kisasa/kimapingiti/kimapinduzi na mtindo wa kimapokeo/kijadi.

 1. Wahusika na jinsi walivyotumika

Ni viumbe hai au visivyo hai vinavyobuniwa na msanii ili kuwakilisha matendo, tabia fulani za watu katika kazi ya fasihi.

Wahusika huweza kuwa watu, wanyama, milima, mimea, wadudu, n.k

Wahusika wote huwa na wasifu wa nje na wa ndani ambao humpambanua mhusika na kumtofautisha na muhusika mwingine. Wahusika nao wamegawanywa katika aina kadhaa.

AINA ZA WAHUSIKA

Kuna aina tatu za wahusika ambazo ni

 • wahusika wakuu

Ni wahusika ambao hubeba wazo kuu la kazi ya fasihi na kujitokeza mara kwa mara kuanzia mwanzo hadi mwisho wa kazi ya fasihi(riwaya na tamthiliya) yaani huitawala kazi ya fasihi. Hubeba kiini cha dhamira kuu na maana ya hadithi yote.

 • wahusika wasaidizi

Ni wahusika ambao hujitokeza hapa na pale katika kazi ya fasihi ili kukamilisha maudhui ya kazi hiyo. Hawa husaidia kujenga dhamira fulani fulani katika kazi ya fasihi. Huwa ndio vipaza sauti wa kazi ya fasihi.

 • wahusika wajenzi

Ni wahusika ambao hutokea mara moja na kupotea katika kazi ya fasihi ili kukamilisha maudhui fulani, kuwajenga na kuwakamilisha wahusika wakuu na wasaidizi.

– Chunguza namna kila muhusika alivyojitokeza katika matini unayoijadili ili kupata maelezo ya kueleza jinsi alivyotumika katika matini.

 1. Matumizi ya lugha

Katika kipengele hiki tunaangalia lugha iliyotumika katika matini ni rahisi/nyepesi au ngumu, wepesi na ugumu wa lugha iliyotumika huwa ni katika kueleweka kwa hadhira na si vinginevyo yaani kiuhalisia hakuna lugha ngumu. Ila kimsingi katika kipengele hiki huwa tunashughulikia vipengele vya msingi vitatu ambavyo ni tamathali za semi, semi na mbinu nyingine za kisanaa. (REJEA NADHARIA YA FANI KATIKA KIPENGELE CHA MATUMIZI YA LUGHA kuangalia vitu hivyo namna vinavyojitokeza)

 1. Mandhari

Ni sehemu/mahali/mazingira ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutendeka/hufanyika/hutokea. Mwandishi anaweza kuyagawa mandhari katika makundi mawili yaani;

–  Mandhari halisi

Ni mandhari ambayo inapatikana katika mazingira ya kawaida mfano katika nchi yoyote, mkoa au eneo lolote ambalo linajulikana kwa kina na watu.

–  Mandhari ya kubuni

Ni mandhari ambayo mwandishi anayachora yakiwa hayafanani na eneo lolote katika hali halisi.

 1. Tathmini ya ujumbe

Kwa vipi mwandishi amezitumia vyema stadi hizo kisanaa kuwasilishia ujumbe wake? Ni ujumbe upi ulioupata kutoka katika matini hiyo? Na kiasi gani amefanikiwa au hakufanikiwa?

Facebook Comments
Donate
Recommended articles