UNYAMBULISHAJI

By , in Sarufi na Utumizi Wa Lugha on .

TANGULIZI.

Maana ya unyambulishaji

Massamba (2009:105), unyambulishaji ni utaratibu wa kupachika viambishi kwenye mizizi ili kuunda maneno mapya.

Unyambulishaji ni mbinu ya uundaji wa maneno,hivi kwamba viambishi mbalimbali huambikwa kwenye mzizi  husika na kuunda neno jipya.(Matinde,2012:119).

Unyambulishaji ni utaratibu katika lugha wa kupachika au kuongeza viambishi kwenye mzizi wa neno ili kuunda maneno mapya. Kwa mfano, kuunda nomino kutokana na vitenzi kwa kutumia viambishi. Maneno mapya yanayoundwa hapa huwa ya kategoria nyingine (Masebo,2012:127).

Hivyo basi tunaweza kusema kwamba unyambulishaji ni aina ya uambishaji unaosababisha neno kutoka katika kategoria moja hadi nyingine.

Unyambulishaji wa nomino

Habwe na Kalanje (2004),wanadai kuwa unyambulishaji wa nomino ni hali ya kuunda nomino kutoka kuwa kategoria nyingine za maneno huitwa unominishaji. Nomino za Kiswahili zinaweza kuundwa kutokana na vitenzi, vivumishi na hata kutokana na nomino moja hadi nyingine.

Hivyo basi, unyambulishaji wa nomino ni hali ya kuweka viambishi vinyambulishi kwenye mzizi wa neno ambao hupelekea neno hilo kuhama kutoka kategoria moja kwenda kategoria nyingine ambayo ni nomino.

Nomino.

Ni neno linalotaja kitu, kiumbe, hali, dhana au tendo kama kiti,ndege na furaha. (Massamba, 2009:68).

Unyambulishaji wa nomino hufanyika kama ifuatavyo;

Kinominishi {o} kinaweza kunominisha vitenzi vya Kiswahili katika mazingira yafuatayo;

Kwa mfano vitenzi vya kibantu vinavyoishia na kiambishi tamati {-a}

{Mzizi} + {-o}

Mfano,

Kitenzi               mzizi                         nomino

Tenda                 tend +o                     tendo

Andika               andik + o                   andiko

Jenga                  jeng + o                     jengo

Pamba                pamb + o                  pambo

Hata hivyo, kuna baadhi ya vitenzi vya kibantu ambavyo huishia na kiambishi tamati {-a} ambavyo vikiambikwa viambishi tamati {-o} haviwezi kubadilika na kuwa nomino. Kwa mfano  kitenzi ;Lowa,tembea.

Pia kiambishi cha unyambulishi {-o} huweza kunyambulisha nomino kwa kuambatana na kinyambulishi {-i} au {-li}.

kwa mfano; {mzizi} + {-i/-li-} + {-o}

Kitenzi                mzizi                                  nomino

Kaanga                kaang + i + o                    kaangio

Chuja                   chuj + i + o                       chujio

Kaa                       ka + li + o                         kalio

Mazingira mengine kiambishi kinyambulishi {o} huweza kunominisha kitenzi pale ambapo huambatana na mofimu {e}.

{mzizi} + {-e-} + {-o}

Kwa mfano; Kitenzi   mzizi                       nomino

Fyeka                fyek + e + o           fyekeo

Chekecha          chekech + e + o    chekecheo

Pia unyambulishaji wa nomino huweza kutokea kwa kuambika kiambishi {M-/Mw-} mwanzoni kabla ya shina  la kitenzi na kiambishi cha unyambulishi {-ji} baada ya mzizi wa neno. Kiambishi tamati {-ji} cha unominishaji ambacho huonesha mtu anayetenda kitendo kama kazi yake ya kila siku.

{M/Mw-}+{shina-T}+{-ji}

Mfano

kitenzishinanomino

            Baka m + baka + ji  mbakaji

            Chezam + cheza + ji  mchezaji

            Imba mw+imba+ji mwimbaji

            Omba mw +omba + jimwombaji

Nomino zenye mofolojia yenye kiambishi awali {ku}, ambacho hutumiwa kuunda nomino. Kiambishi hiki {ku} huwekwa mbele ya shina la kitenzi na hubadili kitenzi kuwa nomino.

{Ku-} + {shina-T}

Mfano,

            Kitenzi             shina                nomino

             imba               ku + imba         kuimba

Cheza              ku + cheza        kucheza

             Lia                   ku + lia             kulia

            Piga                 ku + piga        kupiga

Nomino zenye mofolojia yenye kiambishi awali {u} cha unominishaji , mzizi wa kitenzi na kiambishi tamati {vu/fu} cha unominishaji. Huonyesha mtu au watu walio katika hali fulani.

{u} + {MZIZI} + {vu/fu}

Mfano:-

Kitenzi            Mzizi                           Nomino

Tulia               u + tuli + vu                 Utulivu

Vumilia          u + vumili + vu             Uvumilivu

legea               u + lege + vu                Ulegevu

Nomino zenye mofolojia yenye kiambishi awali {ki} cha unominishaji katika umoja au {vi} katika umoja , mzizi wa kitenzi na kiambishi  tamati {o} kiambishi hiki huweza kuleta dhana ya kitu/ kifaa kinachotumika kutenda kitendo.

 {Ki/ Vi} + {MZIZI} + {o}

Mfano:-

Kitenzi             Mzizi                           Nomino

Funika             ki + funik + o              kifuniko/vifuniko

Pima                ki + pim + o                 kipimo/vipimo

Tua                  ki + tu + o                   kituo/vipimo

Kiambishi kinyambulishi {-a}

Ikiwa kitenzi huishia kwa irabu i au u irabu hizo hubadilika na mahali pake huchukuliwa na kiambishi tamati {a} hivyo husababisha kitenzi kubadili kategoria yake na kuwa nomino.

Yaani, {mzizi} + {a}

Mfano,

            Kitenzi            mzizi                nomino

            Hoji                 hoj + a             hoja

            Faidi                faid + a            faida

            Heshimu          heshim + a       heshima

Unyambulishaji katika vitenzi

Rubanza Y.I (1996), unyambulishaji wa vitenzi ni upachikaji wa mofimu fuatishi katika vitenzi.

Kitenzi ni neno ambalo huarifu tendo linalofanyika. TUKI (2012).

Mgullu (2012),anadai kuwa katika lugha ya Kiswahili vitenzi vinaweza kuundwa kutokana na vivumishi.

Kwa mfano;

 Refu           refusha

 Fupi           fupisha

 Bora            boresha

Safi              safisha

Pia mara chache sana nomino zikinyambuliwa huunda vitenzi, Masebo (2012:134).

Kwa mfano;

            Nomino           Kitenzi

Taifa                taifisha

Sulubu             sulubisha

Ratiba               ratibu

Hata hivyo kuna idadi ndogo ya vielezi vikinyambuliwa vinaweza kutumikakatika kuunda vitenzi. Kwa mfano;

            Kielezi             Kitenzi

               Haraka          harakisha, harakishwa,

HITIMISHO.

Unyambulishaji wa maneno katika lugha ni muhimu sana katika ukuaji wa lugha kwani hupelekea kuongezeka kwa misamiati katika lugha.

MAREJELEO.

Habwe na Karanja, (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Foenix Publishers.

Massebo (2012). Nadharia ya Lugha Kiswahili 1,kidato cha 5&6.Dar Es salaam: Nyambari

Matinde, S. (2012), Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo

Mgullu, (2012), Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers.

Nyangwine Publishers.

TUKI (2012). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar Es salaam: Oxford University Press.

Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.

Recommended articles