UKIMYA NI SILAHA NA SAUTI

By , in ELIMUJAMII on .

No photo description available.

______________
Francis Daudi

Ukimya ni silaha muhimu pindi maneno tunayoyatamka yanapokosa maana. Sisi ni watumwa wa maneno yetu tuliyopata kuyasema, na ni kweli kwamba samaki anayefungua mdomo kula chambo ndiye hasa hunaswa na ndoano. Hii ndio kusema tunapaswa kufungua vinywa baada ya kuridhika kwamba maneno tutayoyatoa yatakuwa na thamani kuliko kukaa kimya. Ukimya huweza kuwa pia jibu la mengi, ndio maana unaweza jibu kwa kukaa kimya.

Lakini Ukimya pia ni sauti, hisia na mawazo katika fahamu zetu. Sauti, kuna zile tunazianika nje, nyingine zinabaki kinywani.Ukimya una kishindo, ni ukimya unaotufanya kujitambua na kuona nafsi na nafasi yetu duniani. Ndio maana watu kama Yuval Harari(Mwanahistoria wa Israel na Mwandishi wa Vitabu Sapiens na Homo Deus hutenga siku 30 za ukimya kati ya 365)

Jaribu, kwenye mazungumzo na mtu, kusikiliza yale mtu haongei. Ukimya wa sauti ni asili na siri ya mafanikio yoyote yale. Bahati mbaya, pilikapilika za usasa zinatufanya kupoteza tunu hiyo ya ukimya. Tunasujudu zaidi makelele! Kumbe hata, mawasiliano mazuri yanaanza na kujisikiliza kwanza. Tunapoteza nafasi kila siku kumsikiliza mtu muhimu ndani yako!

Siku hizi kila mtu anaongea, safiii! Lakini, matamshi bila umakini ni matapishi. Weka utashi katika upishi! Kuna maneno yanaweza semwa tu katika harakati za ukinywa. Usishangae! Kinywa cha mwanadamu ni kisima; katika utulivu wake ni kioo. Pale maongezi yanapopisha ukimya, tunaelewana maradufu. Siku hizi, kila mtu ana mdomo kuliko masikio, ndio maana hatuelewani. Hayati Karume(Rais wa Kwanza wa Zanzibar) alizoea kusema, tuna mdomo mmoja na masikio mawili ili tusikilize sana na kuongea kidogo!!

Matukio mbalimbali maishani yanatutaka kuwa wakimya zaidi kuliko kufungua mdomo. Tunahitaji tafakuru kubwa. Tusiogope wala kuchoka kuulizana maswali kuhusu thamani na kusudio letu hapa duniani. Hatukuja Duniani kuchat, kuumiza wenzetu au kuzurura.

Na dini karibu zote zinasema sala kubwa mbele ya Mungu ni ukimya wetu. Kwani hata jina la Mungu halisemwi, ni takatifu mno! Kama ni matamshi, basi yawe ni baada ya kina kirefu cha ukimya. Inafaa tu, binadamu arudi katika utashi na kutambua umuhimu huu wa ukimya. Turudi katika chanzo sio katika matokeo. Udhaifu wetu.

Usahaulifu ni matokeo ya kuongea bila kujipa nafasi kutafakari. Wanafunzi wapo busy kutafta habari za Mobeto na wengineo. Wanamkubali Liquid Konki wa Fire kuliko maarifa! Wazazi wamewahau malezi, wapo busy kuupdate status na mengineyo( Usisahau hats mjukuu wako atayakuta unayopost). Jipe ukimya, Tafakari.

Jitafiti na jitahidi ujipangie muda, kila siku, ujitafakari kuhusu hali yako na ulimwengu unaokabiliana nao. Usipoteze wakati. Wakati ni dawa na zawadi kuu unayoweza kumpatia mtu. Kheri upoteze madafu na sio wakati. Jipe talaka kufuata upepo, matukio na kuishi maisha ya wengine au kujilinganisha na wengine. Kama watu wanaokuzunguka sio watu wakujiongeza wala kukua, unapaswa kuachana nao. Marafiki na jirani zako wanatakiwa wasababishe uwe bora zaidi, uwe katika kiwango cha juu kabisa ili uweze kufanya makuu. Watanzania wengi wanazeeka mapema, sio tu kiumri bali kimaono, wameridhika na kuwa watu wa kawaida. Tafadhali jiamini na usibaki katika wimbi la kuishi chini ya kiwango.

Ukimya wa sauti ni muhimu. Kama nchi, katika safari ya kujenga utaifa tumekuwa waongeaji mno, kumekosa utamaduni wa kujisikiliza, kusikilizana na kukaa chini kupanga vipaumbele. Tumekosa kuwa na mijadala ya kitaifa sio tu kati yetu na watawala, bali hata ndani ya taasisi zetu. Hatuwezi kusonga bila kujitathimini. Kila mtu anatoa tamko, kila mtu analaumu tu.

Msingi wa demokrasia na ustawi wetu ni uhuru wa kufikiria. Tupinge utamaduni wa kukaa kimya penye kutupasa kuongea. Lakini hatutajenga nchi kwa matamko, dhihaka, Lawama na kukejeli kila kitu.

Twende tukaijenge nchi, hatuna Tanzania ingine Tofauti na Hii.

Wanapaita Tanzania, Tunapaita Nyumbani.

Francis Daudi,
Kaka Mkubwa.

Nimeandika kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya mtandao na mawazo ya watu waungwana.

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!