UHAKIKI WA TAMTHILIYA YA HARAKATI ZA UKOMBOZI

By , in Tamthiliya on . Tagged width:

I. Utangulizi

Kusudio la tamthiliya hii ya Harakati za Ukombozi kama linavyoelezwa lilikuwa kuwafurahisha, kuwaadilisha na kuwafunza umma wa wakulima na wafanyakazi katika sherehe kubwa ya kusherehekea kutimiza mwaka mmoja baada ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Waandishi wake; yaani Amandina Lihamba, Penina Muhando na Ndyanao Balisidya walichukua jukumu la kuiandaa tamthiliya hii baada ya Profesa Penina Muhando (Mlama) kuombwa na vijana (Umoja wa Vijana Tanzania) kuandaa tamthiliya kwa ajili ya sherehe hiyo. Maandalizi ya tamthiliya hii yalijumuisha watu wengi waliotoka sehemu mbalimbali za nchi na wakiwa na nyadhifa mbalimbali kikazi. Maelezo ya awali yanadai kwamba tamfhiliya hii isingepata kuonyeshwa. Kwanini? Kulikuwana minong’ono yenye nguvu kuwa tamthiliya hii ilikuwa haikubaliki miongoni mwa watu wa ngazi za juu katika uongozi wa nchi hii. Aidha, katika hatua ya kushangaza na kuwafurahisha wengi, tamthiliya bii hatimaye ilipata nafasi ya kuonyeshwa Chuo Kikuu katika ukumbi wa Nkrumah. Onyesho hilo lilikuwa la kwanza.

Baada ya onyesho la Nkrumah, kulikuwa na onyesho jingine lililofanyika katika ukumbi wa Lumumba. Onvesho hili lilifanyika siku chache baada ya lile la Nkrumah.

Tamthiliya hii ilizua aina mbili za hisia kwa upande wa watazamaji. Hisia za aina ya kwanza zinawahusu watu wale ambao walipendezewa na kufurahishwa sana na tamthiliya hii. Hawa walikuwa watu wa kawaida na kimsingi walikuwa wengi katika jamii. Kuna kundi la pili lilihusu wale ambao hawakupendezewa na tamthiliya hii kwa sababu maudhui yanayaotolewa yalikuwa na bado yanagusa kiini cha Harakati za Ukombozi wa nchi ya Tanzania. Tamthiliya hiyo inawaumbua waliosaliti juhudi za dhati za ukombozi wa Tanzania. Kwa bahati mbaya hawa ni wachache na wako katika kundi la viongozi.

Tamthiliya ya Harakati za Ukombozi inamwingiza msomaji wake katika maisha ya safari ndefu ya nchi ya Tanzania tokea kule itokako na inakotegemea kuelekea na kuzua mawazo na fikra nyingi zinazozua maswali mengi. Safari hii inamfungulia msomaji hatua mbalimbali zilizopitiwa katika jitihada za Mtanzania kutaka kujikomboa kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi. Msomaji wa tamthiliya hii kila mara hujikuta anafikiri, analiwaza, na hata pengine kupata jazba kubwa. Tamthiliya hii ni kazi ya pekee ambayo imeisaili nchi ya Tanzania kwa kina, na kwa mbinu za kisanaa, katika vipengele vya mfumo wake kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Harakati za Ukombozi inaichambua nchi ya Tanzania na kuionyesha safari ndefu ya Watanzania tangu wakati ule wa majilio ya wageni na biashara mbaya na kongwe ya utumwa; majilio ya ukoloni wa Mwingereza, majilio na kuzaliwa kwa TANU na ASP na kuanzishwa kwa harakati za kugombea Uhuru, kuzaliwa kwa Azimio la Arusha; na hatimaye kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM). Labda katika toleo lakejipya, huenda patakuwa na maelezo kuhusu majilio ya yyama vingi! (sijui).

Tamthiliya ya Harakati za Ukombozi imejengwa kuwazungukia vijana. Chini ya Chama cha Mapinduzi vijana wana azima ya kuleta mapinduzi ambayo lengo lake ni kuleta uhuru halisi wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Lengo la mapinduzi hayo ni kuondoa na kuzika kabisa vitu kama unyonyaji; dhuluma na uonevu miongoni mwa watanzania na watu wengine kwa ujumla. Tamthiliya inaonyesha kwamba vijana wamechachamaa na kutaka kuleta mapinduzi katika jamii; wanataka kufanya hivyo kupitia Chama cha Mapinduzi.

Dhamira kuu zinazojitokeza ni pamoja na hizi:

· Suala la utumwa na ukoloni
· Kupatikana kwa uhuru
· Azimio la Arusha
· Nafasi ya Chama cha Mapinduzi
· Chimbuko la matatizo ni nini?

Tutazichambua dhamira hizo kwa makini. Baada ya uchambuzi wa dhamira, tutaangalia fani ya tamthiliya hiyo ya Harakati za Ukombozi.

II. Maudhui

Kama inavyofahamika, inaudhui ya kazi ya kisanaa ya kifasihi kama hii ya Harakati za Ukombozi yanajumuisha dhamira, msimamo, falsafa, mtazamo na ujumbe. Tutaanza na uchambuzi wa dhamira.

(a) Suala la Utumwa na Ukoloni Mkongwe

Waandishi wa tamthiliya hii wamejitahidi kuonyesha matatizo makubwa yaliyowapata wananchi wa Tanzania katika vipindi viwili vya kihistoria: wakati wa Utumwa na Ukoloni-mkongwe. Waandishi wanaeleza kwamba wakati wa utumwa watu walipata matatizo kama vile kuondolewa kutoka nchini mwao na kwenda kuuzwa sehemu nyingine. Thamani ya mtu ilidunishwa, alidhalilishwa na kuwa kama bidhaa yoyote ya kupigwa mnada kirahisi.

Wakati mateka wa utumwa walipokuwa wakisafirishwa kutoka nchini mwao na kupelekwa kuuzwa walikuwa wakipigwa viboko, kunajisiwa na wengine kuuawa njiani. Watoto walitenganishwa na mama zao, wake na waume hawakuweza kuwa pamoja. Aidha, walibebeshwa mizigo mizito. Ili kuonyesha adha na hisia za ukoloni mkongwe, mzee kipofu anaimba:

… Angalia balaa ya utumwa wa ukoloni.
Mateso makubwa sana yaliyotokea.
Watu kufanywa kama wanyama
Tuliuzwa kama nguo,
Wenye nguvu walichukuliwa ili sisi eti tubakie maskini,
Watanzania tuliteseka balaa la ukoloni.
Mateso mengi tukayapata ya mizigo mizito mno.
Tulipigwa na kuuawa na kupotea ugenini…. (uk.7)

Matokeo ya kuchukuliwa watu wenye nguvu yalikuwa kudhoofisha nguvu za wananchi. Nchi ilipokonywa watu wake wenye nguvu na matokeo yake ni kuingiliwa na njaa na udhaifu wa kiuchumi. Baada ya kuwachukua utumwa watu wenye nguvu, walioachwa nyuma pia walipata mateso kwa sababu hapakuwa na mtu wa kuwahudumia. Kulikuwa hakuna watu wenye nguvu wanaoweza kufanya kazi na hivyo kuwa katika hatari ya kukabiliwa na janga la njaa.

Katika nchi hii, utumwa ulipokomeshwa uliingia utawala mpya, utawala wa Mwingereza ambaye anadai alisaidia kukomesha utumwa. Mwingereza anaingiza sumu nyingine: unyonyaji. Mwingereza alipoingia Tanganyika aliikalia nchi na kulazimishwa kulimwa kwa mazao ya biashara kama vile pamba.

Kuna ushahidi kuwa Mwingereza aliwalipa wananchi fedha kidogo ambazo ilibidi walipie kodi. Hatima yajambo hili ni umaskini na dhiki kubwa. Wananchi walilipwa kwa kupendelewa, wengine walinyonywa.

Utawala wa Mwingereza ni kiwakilisho cha ukoloni Mkongwe wote, wakiwemo Wajerumani. Utawala wa Kijerumani unakumbukwa na kufahamika sana kwa ukatili wake. Wananchi waliteswa nchini mwao na Wajerumani. Wananchi walilazimishwa kulipa kodi, walioshindwa kulipa kodi walipigwa na kufanyishwa kazi ngumu. Matokeo yake? Watu walichukia, wakaamua kupambana katika vita vya Maji Maji. Lakini umaskini wao na kutokuwa na vifaa kuliwafanya washindwe vita.

(b) Mapambano ya Uhuru

Jambo jingine linaloelezwa linahusu juhudi ya kuikomboa nchi ya Tanganyika kutoka katikautawala mkongwe wakikoloni. Juhudi hizo zilionekana hata kabla ya kuzaliwa kwa TANU na ASP. Kimsingi, juhudi hizi hazijionyeshi bayana katika tamthiliya hii; lakini msomaji anazihisi kupitia kwa Mzee Kipofu ambaye ndiye anaonekana kuwa kiungo kikubwa kati ya wana CCM na vizazi kabla yake. Mzee huyu anadaiwa ameishi ili kushuhudia matukio yote ya kihistoria katika Tanzania. Mzee huyo anajitahidi kuonyesha jinsi nao walivyojitahidi sana katika enzi zao kuleta mapinduzi; lakini hawakufanikiwa. Kwa mujibu wa mzee huyo, jambo hili halikuweza kufanikiwa kwa sababu wakati huo kulikuwa na vita vilivyokuwa vikipiganwa na Bushiri na Mkwawa: vita vikiwemo vile vya Maji Maji. Lakini baadaye, jambo hili lilikuja kufanikiwa wakati wa TANU na ASP.

Suala la uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) halikuwa gumu. Nchi hii ilipata uhuru kwa njia za kikatiba. Ingawa Tanzania Visiwani (Zanzibar) walipata pia uhuru kwa misingi ya kikatiba, tatizo lilijitokeza kuwa uwezo wa kikatiba walikabidhiwa wachaehe na kuwanyima haki walio wengi. Madaraka alikabidhiwa Mwarabu. Kutokana na hali hiyo, Mwafrika alizidi kuwa raia wa daraja la pili katika nchi yake mwenyewe. Aliendelea kuwa chini ya himaya au miliki ya mtu mwingine. Mwafrika aliendelea kukosa sauti. Kwa sababu ya hali hii ASP iliamua kufanya Mapinduzi na kuiondoa serikali ya usultani wa Kiarabu!.

(c) Kupatikana kwa Uhuru

Tamthiliya ya Harakati za Ukombozi inaendela kuelezea hatua muhimu ya uhuru. Uhuru wa Tanzania ulipatikana kupitia vyama vya TANU na ASP. Uhuru unadhihirishwa kwa kauli za msingi wa TANU na ASP.

…Tutatumia chombo chetu
ambacho kina rubani
anayesaidiwa na wasafiri wote
kukitokomezeni,
Towekeni!
(Vigelegele na vifijo)
(Ngoma yenye wimbo ufuatao inapigwa)
Uhuru tumeupata
Tumeupata Uhuru
Tumeupata
(Ngoma inatowcka taratibu). (uk.ll)

Baada ya kupata uhuru, matumaini ya walala hoi, wavujajasho na watu wa kawaida yalikuwa ni kuona kuwa maisha yao yanakuwa mema na unyanyasaji kutoweka. Lakini hali haiwi hivyo baada ya uhuru. Watu walioshika madaraka waliamini sasa wangekuwa wameshika nafasi za wakoloni walioondolewa. Mzee anatamka kauli hii:

… Uhuru tuliupata, ndiyo, lakini haukuleta mapinduzi yoyote. Kwani hao ndugu zetu, ambao walishika madaraka baada ya kuondoka wakoloni walirithi pia zile tabia za kikoloni. Walijifanya wazungu weusi walihama kule Buguruni na kwenda kuishi Uzunguni. Basi mambo yao yakawa ya uzungu – uzungu na kuanza kutunyonya na kutunyanyasa sisi ndugu zao. Hivyo uhuru wetu ulikuwa wa bendera tu na sio wa kuleta mapinduzi. (uk. 11-12)

Nchini Tanzania uhuru haukuwa na manufaa sana kwa mtu wa kawaida. Baada ya kupatikana kwa uhuru Tanzania kuna viongozi waliotumia nafasi zao kujijenga. Matokeo ya tabia hii yalikuwa kuzidisha tofauti zilizokuwepo kati ya wenye nacho na wale wasionacho: viongozi wa Chama na Serikali.

Unyonyaji uliokuwa ukiendeshwa na wakoloni wakongwe ulipata waendeshaji wapya: walikuwa wananchi wa Tanzania. Viongozi ndio wanaofaidi matunda ya uhuru, kama sehemu hii ifuatayo inavyosema:

MADHAMBI YA UHURU:

Ninawatia usingizi wakati mimi nazidi kupaa angani. Mimi ni ncha ya mkuki, sipigwi konzi…. matunda ya uhuru ni yangu, nakula kwa niaba yenu,… ninahitaji mlete barabara ili bidhaa zifike viwandani haraka. Nisafirishe pamba nje ya nchi. Ninahitaji mkopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba zangu mbili, ili niishi kwa raha muslarehe kwa niaba yenu…. Huu ndio uhuru Ha! Ha! Ha! Ha! Ha! (uk.12).

Maelezo haya yanaonyesha kuwa viongozi wengi wanazidi kunawiri na kustarehe wakati wananchi wa kawaida wana hali mbaya. Kwa viongozi, uhuru kwao maana yake ni kustarehe bila kujali hali ya wananchi. Viongozi hawa ni wanafiki na kazi yao ni kupiga domo:

KIONGOZI 1:

… Hatuna budi kuwashukuru viongozi wetu wa Chama pamoja na juhudi zetu sote kwani umoja huu umefanya yule mwizi wa asali katika mzinga akafukuziliwa mbali. Hivyo asali yote sasa ni mali yetu. Na malunda ya uhuru wetu tumekwishaanza kuyaona. Na wengine wetu hata kuyaona tayari… tushirikiane wote katika kulinda uhuru wetu. Na wala hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kwani kila kitu sasa ni mali yetu.. (uk. 13).

Ingawa haya ndiyo maelezo ya kiongozi, lakini huyu kiongozi ni mnafiki. Kwa mfano mara baada ya mkutano, kiongozi anatoka na kwenda kwenye miradi yake na kukusanya mapato, anakusanya pesa kutokana na mayai, nyumba na kupangisha, mabasi na baa. Ndiyo maana Mzee anasema kwa kejeli:

… Huo ndio uhuru tulioulilia ili wachache wapate kujinufaisha. Mmeona wenyewe jinsi viongozi wa Chama na serikali wanavyojitajirisha kwa miradi mbalimbali… (uk.13)

Lakini kwa hakika huu si uhuru walioutaka wananchi baada ya mapambano makali. Uhuru walioutaka ni wa kuwanufaisha wote. Uhuru wa kuwanyima wengine haki sio uhuru walioutaka!.

(d) Kuzaliwa kwa Azimio la Arusha

Misingi ya kisiasa na kiuchumi mara baada ya uhuru haikuwapa nafasi wananchi wa nchi hii. Usawa uliokusudiwa ulizidi kuharibika na kujenga tofauti kubwa miongoni mwa wananchi. Tofauti hizi zilionekana zingehatarisha na kuleta madhara kwa nchi. Ilibidi itafutwe njia ya kurekebisha jambo hili, na ndiyo likazaliwa Azimio la Arusha.

Kutangazwa kwa Azimio la Arusha kulielezwa kuwa hatua muhimu ya kuiwezesha nchi kuelekea kwenye jamii ya kijamaa, jamii ambayo itajali usawa na hakutakuwa na unyonyaji.

Kimsingi, Azimio la Arusha lilipokelewa vizuri na kwa vifijo na hoihoi za kila namna. Kuna maandamano mengi yalifanyika kwa lengo la kuwashawishi watu waliunge mkono Azimio hilo.

Kutangazwa kwa Azimio kulileta faraja kwa wanyongewalioliona kama mtetezi wao. Matumaini yote yaliwekwa katika Azimio hilo.

Kutangazwa kwa Azimio kumefanya vijana walipe Azimio hilo sifa nyingi; ikiwa ni pamoja na:

KIJANA 3:

Ni la ukoo wa umma
Halikunjiki
Ni la Chuma cha pua
Lisilokunjika kwa nyundo (uk.16)

Katika kulienzi Azimio hilo, watu wamelifananisha na radi, siafu na mwamba. Kabla ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha viongozi mbalimbali wanasemekana waliusifia uhuru na kuongea kuhusu kulinda uhuru huo pamoja na matunda yake. Lakini kauli hii imekaa kama kejeli kwani ni viongozi wenyewe wanayoyafaidi matunda ya uhuru. Hata baada ya Azimio la Arusha viongozi walilisifia hadharani, kumbe walikuwa wakilisaliti kimyakimya.

KIONGOZI 2:

…. wachachewetu walijigeuza wao wakoloni weusi. Wakataka faida, tena vile vile walivyofanya wakoloni. Na kwa watu hawa sisi sote kwa pambja tumeazimia kuwazika wasionekane tena. Ndiyo maana ya kupitisha Azimio la Arusha, badala ya wachache kufaidi matunda ya walio wengi tuyafaidi wote. Hivyo ndugu wananchi mtaona kuwa Azimio la Arusha ni taa, ni kurunzi itakayomulika na kufichua dosari zote za utekelezaji… Azimio letu ni kisu, ni wembe utakaokatakata mirija hii inayotunyonya; na kuharibu ncha chafu zote za uhuru.. Azimio la Arusha ni ngao yetu, itakayotulinda sisi wa, nchi dhidi ya watu wapinga maendeleo… (uk. 17)

Hawa ndio viongozi wa Tanzania baada ya Azimio la Arusha. Ni viongozi wale wenye kutoa hotuba nzuri majukwaani, lakini katika uzuri wa hotuba zao wameficha madhambi makubwa. Maneno yao mazuri hayalingani na vitendo vyao viovu. Azimio la Arusha lilikuwa likitetewa jukwaani tu, lakini wakiondoka jukwaani, utetezi wote nao huisha. Jambo jingine linalojionyesha katika kipindi cha Azimio la Arusha ni knwa kabla ya Azimio hilo, mbinu zote za kulikwepa au za kujinufaisha zilikuwa wazi. Lakini baada ya Azimio, mbinu zimegeuka na kuwa za siri. Viongozi wengine wanatumia mbinu za kulikwepa: Angalia mazungumzo yafuatayo:

MENEJA:

… Iakmi mwenzenu Azimio hili linaniumiza kichwa (Wanacheka).

KIONGOZI 2:

Linakuumiza kichwa?

MENEJA:

Tena sana. Ingawa hapa tunakunywa, tunazungumza, lakini mimi mwenzenu nimekosa raha.

MKURUGENZI:

Kwa nini lakini?

MENEJA:

Hizi sheria zinazohusu viongozi.

KIONGOZI 2:

Zipi?

MENEJA:

Hizi za kusema sijui kiongozi asiwe na hisa kalika kampuni ya kibepari, kiongozi asiwe na mishahara miwili, au asiwe na nyumba za kupangisha na mengine.

KIONGOZI 1:

Sawa, lakini tatizo lako liko wapi?

MENEJA:

Tatizo langu ni kwenye nyumba bwana.

MKURUGENZI:

Ehee!

KIONGOZI 2:

Kwani bwana Meneja una nyumba ngapi?

MENEJA:

Nina nyumba nne.

KIONGOZI 1:

Nne tu?

MENEJA:

Nne!

KIONGOZI:

Aa! Mimi nilidhani una nyurnba nyingi sana, nne tu. Mbona muni ninazo kumi (wanacheka) na sina tatizo.

MKURUGENZI:

Kwani ndugu Meneja kuna watoto wowote?

MENEJA:

Nina watoto wanne. Huyu wa nne kazaliwa juzi tu, hata siku kumi hajafikisha.

MKURLIGENZI:

Sasa kumbe una shida gani. Wagawe hao watoto kwenye hizo nyumba.

KIONGOZI 1:

Eee! Kila mtoto nyumba moja.

Mjadala wa viongozi hao unaonyesha kuwa wao wamedhamiria kujinufaisha wenyewe na kuwatupilia mbali wananchi. Viongozi hao wanajilimbikizia mali, wanafanya magendo na kila uharabu na kadhalika.

Ni kweli, na kimsingi Azimio la Arusha limekusudiwa kuleta maendeleo kwa watu wote, wakiwemo wanyonge. Lakini ni muhimu ieleweke wazi kuwa kimsingi Azimio hilo lilianzishwa na viongozi ambao ndio wanalikiuka. Mzee kwa masikitiko yenye ukweli anasema:

MZEE: Waliketi kuliunda Azimio sasa wanaketi tena kulisaliti. Ni mahodari kulihubiri majukwaani, lakini kumbe wao wenyewe ndio wasaliti wakubwa wa Azimio…. (uk. 21)

Kauli hii inadokeza mengi ambayo hivi sasa (baada ya miaka zaidi ya 26) yamewekwa wazi. Azimio la Arusha kuna watu wanaokebehi na kukejeli, limetoweka na awamu ya Nyerere aliyepata kuwa Raisi wa Tanzania.

(e) Kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM)

Chama cha Mapinduzi kilizaliwa miaka kumi kamili baada ya kuzaliwa kwa Azimio la Arusha. CCM ni chama kilichozaliwa baada ya kuunganishwa kwa TANU na ASP; vyama vilivyokuwa vikitawala Tanzania Bara na Tanzania visiwani. Kuzaliwa kwa CCM kulipokelewa kwa matumaini makubwa na mapya. Matumaini mengi yanajitokeza katika mazungumzo ya vijana.

Lakini kwa upande mwingme, Mzee (uk. 21) ana wasiwasi kuhusu kufanikiwa kwa mapinduzi katika hali iliyopo, ambapo viongozi wenyewe ndio wasaliti wakubwa wa Azimio la Arusha; lakini vijana wana jibu lenye matumaini.

KIJANA I:

Hao ni baadhi tu ya viongozi. Wapo viongozi ambao waku katika mkondo mzuri. Wao pamoja na wazalendo wenye moyo safi wameshirikiana kwa pamoja na kuanzisha Chama cha Mapinduzi.

KIJANA II:

Tumeanzisha CCM ili kuwapiga vita wapinga mapinduzi hao wachache, wanaotumia mbinu haramu ili kunyonya, kulimbikiza mali na kuhujumu uchumi wetu.

KIJANA III:

Sisi vijana tutafanya chini juu kushirikiana na viongozi walio sawa na maamuzi ya chama kuzuia maovu yote yanayotendeka. (uk. 21)

Vijana wanakiona chama kama chekecheke lenye uwezo wa kuwatenga na kuwachuja viongozi wasiofaa. Ni chekecheke la kuwaengua wale wote ambao ni vizingiti vya mapinduzi katika nchi ya Tanzania. Vijana wanaamini na kujiona wanapata nguvu mpya chini ya CCM na wamedhamiria kupambana na wapinga mapinduzi. Swali linakuja: Je, Vijana wataweza kweli kuleta Mapinduzi?

MZEE:

Wananchi nipeni masikio. Kizazi kipya kimeazimia kutenda, wapeni uwanja! Lakini mazingira kilichomo chombo kipya ni yale yale. Visiki bado havijang’olewa na mnunuzi wa zana za kung’olea visiki ni yule yule. Kizazi kipya chaelekezwa katika mkondo nle ule. Kizazi kipya chaimba nyimbo zile zile, wapiga makofi wakiwa katika hali ileile.

KIJANA I:…..

Nguvu zetu ni za kipekee, mbinu zetu ni mpya.

Hatutasafiri kwa ngalawa tena, Tumeunda meli ambayo mwendo wake ni wa kasi.

Mbinu zetu za mashambulizi. Hazitokei sehemu moja.

Zinatoka kila pembe.

Tukilenga tumetungua.

Tupeni nafasi.

MZEE:

Nafasi unawezapewa lakini je mtaweza:

KIJANA 2:

Kuweza tutaweza kwa vile tumeazimia.

MZEE:

Hata sisi babuzenu tuliazimia lakini tulishindwa.

KIJANA 3:

Mlishindwa kwa sababu mlikuwa na kasumba ya ukoloni.

MZEE:

Je, ninyi mmekwishafuta hiyo kasumba?

KIJANA 4:

Ndiyo, tumeifutilia mbali, tumeitupilia mbali. Sasa tutaleta mapinduzi.

MZEE:

Haya vijana, ukumbi ni wenu, kazi kwenu, jaribuni!

KIJANA 1:

Siyo tujaribu, bali tutaleta mapinduzi kwa kutekeleza kwa vitendo maamuzi yote ya chama (uk. 23-24)

Mjadala huu unaonyesha wasiwasi wa Mzee anayesaili kuhusu uwezo wa vijana katika kuleta mapinduzi. Anaposema “Jaribuni” anaona kuwa si rahisi wao kuweza kushinda.

III. Suluhisho la Matatizo

Tatizo kubwa la tamthiliya ya Harakati za Ukombozi linatokana na mambo maovu ya kijamii. Mambo hayo ni pamoja na kuonewa, kuteswa, na kunyanyaswa katika nyakati mbalimbali za historia ya jamii ya Watanzania. Adha hizo za dhiki ziliikumba jamii ya Tanzania kuanzia wakati wa biashara ya watumwa, hadi uhuru na Azimio la Arusha. Suluhisho lilitumainiwa litokane na kuzaliwa kwa CCM. Vijana wanatarajiwa kupambana na kuhakikisha kuwa Azimio la Arusha linafanikiwa chini ya Chama cha Mapinduzi.

Pamoja na imani hiyo yako mashaka ya kufanikisha azima hii ya vijana. Hii inatokana na ukweli kuwa ingawa CCM imezaliwa kama chama kipya, bado viongozi ni walewale ambao kwa muda wa miaka 10 iliyopita wamekuwa wakilipiga vita Azimio la Arusha. Vijana wenyewe nao wametekwa, wameingia katika mkumbo wa kuimba nyimbo zilizokuwa zikiimbwa siku zote. Katika mazingira mabovu na magumu kama haya watawezaje kuleta mapinduzi? Watawezaje kuleta mapinduzi katika wimbi ambalo linaongozwa na watu ambao kimsingi wamekuwa wakikiuka maadili na misingi iliyowekwa? Matokeo yake ni kushindwa! Kuibadilisha hali hii ni lazima juhudi mpya ifanyike. Lakini itafanyika vipi katika mfumo mpya wa vyama vingi? Tusubiri!

IV. Vipengele vya Fani (4)

Baada ya kuangalia maudhui ya Harakati za Ukombozi sasa tuangalie fani yake. Tutaangalia vipengele kama vile wahusika, muundo na mtindo, mandhari na matumizi ya lugha.

(a) Wahusika

Wahusika wa Harakati za Ukombozi wako katika makundi. Makundi hayo m ya wazee, vijana na viongozi. Tunaweza kuwachambua kinaganaga.

(i) Mzee

Mhusika huyu ni muhimu sana na kimsingi amejengeka kiishara. Mzee huyo ni kiwakilisho cha watu wengi walioishi katika nyakati mbalimbali za kihistoria katika tamthiliya hii. Mzee anaonyeshwa kuwa anashuhudia adha nyingi: utumwa, kukomeshwa kwa biashara ya utumwa na majilio ya ukoloni mkongwe, ameshuhudia harakati mbalimbali za ukombozi: uhuru, kuzaliwa kwa Azimio la Arusha na hatimaye kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Mzee amechorwa kama kiungo muhimu cha vizazi mbalimbali vya kihistoria vilivyopata kuishi.

Kimsingi, waandishi wa Harakati za Ukombozi wanamtumia Mzee kutoa hisia na mawazo yao. Mzee ni msaili mkubwa wa jamii yake. Aidha, mzee hapingani na siasa inayotawala, lakini anasailijuu yauhalali wake katika kutekeleza majukumu yanayopangwa na kuhusudiwa.

Mzee anawasaili viongozi. Anataka kuona mapinduzi ya dhati na kweli yakifanyika. Lakini ana wasiwasi na haoni kama mapinduzi yanaweza kufanyika katika hali ambayo viongozi wenyewe ndio pingamizi kubwa katika kuleta maendeleo. Mzee anapiga hatua na kuona kuwa hakuna mabadiliko yaliyotokea hata baada ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi.

Mwishoni, inaelezwa kuwa mzee anajiunga kucheza ngoma na vijana; lakini inasemekana ni kwa shingo upande. Anacheza kimya kimya badala ya kuimba (uk. 25).

Kushiriki kwake kucheza ngoma kwa kusita kunaonyesha wasiwasi alionao kuhusu kufanikiwa kwa mapinduzi yanayofikiriwa na vijana. Kuishi kwake kwa muda mrefu kumempa uzoefu wa kutoamini matamko yanayofanywa na viongozi mbalimbali. Yawezekana vijana wamedhamiria kuleta mapinduzi ya kweli, lakini je, ni kweli nguvu zilizopo ziko tayari kuwaachia vijana kuyatekeleza mapinduzi hayo?

(ii) Viongozi Mudhambl ya Uhuru; Kiongozi 1; Kiongozi 2; Mkurugenzi, Meneja.

Hili ni kundi la viongozi wa Chama na Serikali. Kundi hili lina dhima ya kusukuma gurudumu la maendeleo katika jamii. Viongozi hawa wanajitokeza katika vipindi au nyakati mbalimbali za kihistoria wakati wa uhuru, Azimio la Arusha, na baada ya Chama cha Mapinduzi.

Viongozi hawa wanaonyeshwa kuwa wameuteka nyara uhuru baada ya uhuru huo na ndio wanaofaidi matunda ya uhuru huo. Wanatumia nafasi zao kujinufaisha. Azimio la Arusha linapoanzishwa viongozi hao wanatumia mbinu kulikwepa, wanaendeleza maslahi ya binafsi. Wanakuwa wasaliti wa Azimio la Arusha. Lakini ni viongozi hawahawa wanaoshika uongozi hata baada ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi, Kwa vile viongozi wamekuwa wakisaliti Azimio la Arusha kuna uwezekano wa kuendelea kulisaliti hata baada ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi,

(iii) Vijana

Vijana ni kizazi kipya cha Tanzania ambacho kimsingi kinaonyesha makusudio ya kutaka kuhakikisha kuwa ujenzi wa jamii mpya unafanikiwa. Vijana wanaonekana kuwa tayari kuilinda, kuitetea na hata kuijenga nchi yao. Ka sababu ya msimamo huo, wanaamua kutenda bila woga. Wanalisherehekea Azimio la Arusha kwa matumaini litaleta ushindi na kuondoa chuki, uonevu na unyonyaji. Kinapoanzishwa Chama cha Mapinduzi wanadhani watashinda. Lakini ni lazima watambue kuwa Mapinduzi yoyote yanayofanikiwa ni lazima yaongozwe na wale waliojitoa mhanga katika kuyalinda na kuyasimamia. Mazingira ambamo vijana hawa wamo hayaruhusu mabadiliko kiurahisi.

(iv) Wahusika wengine

Wako wahusika wengine wadogo wadogo ambao si muhimu sana, lakini wanasaidia kusukuma mbele tamthiliya ya Harakati za Ukombozi. Waliojadiliwa hapo juu ndio wahusika muhimu zaidi.

(b) Muundo na Mtindo

Tamthiliya hii imechanganya umbo la kigeni la tamthiliya na sanaa za maonyesho za kiafrika za kiasili. Harakati za Ukombozl inatumia masimulizi, nyimbo, ngoma, mkarara na majigambo. Tamthiliya hii pia inatumia maongezi ya kinathari na pia lugha ya kishairi katika majigambo. Mtindo huu umeifanya tamthiliya hii ionekane kuwa nzito sana jukwaani. Aidha, kinyume na ikisomwa, tamthiliya hii huonekana ina maneno mengi mno.

(c) Mandhari

Tamthiliya hii imetumia mandhari ya nchi ya Tanzania kuanzia enzi kabla ya ukoloni hadi mara baada ya kuzaliwa kwa CCM. Ni mandhari halisi ya Tanzania.

(d) Matumizi ya Lugha

Tamthiliya hii imetumia lugha nyepesi na ya kueleweka. Lakini kuna pia matumizi ya misemo, nahau, methali na tamathali za usemi. Kuna matumizi ya sitiari, kwa mfano, “Madhambi ya Uhuru” anasema: mimi ni ncha ya mkuki. Hapa imetumika sitiari. Aidha, kuna matumizi ya kejeli, kama yanavyojibaini ukurasa 12. Matumizi mengine ni pamoja na tashtiti, tashibiha na tashihisi. Matumizi ya majigambo yamesaidia pia katika ujenzi wa taswira mbalimbali za tamthiliyahii.

V. Hitimisho

Hii ni tamthiliya muhimu na ni ya kwanza ya aina yake. Inasaili, inafundisha na kuichambua jamii ya Tanzania kwa kina. Tamthiliya hii inaonyesha mapinduzi yanakuja kwa kasi na ni muhimu watu wote washirikiane ili kuleta mapinduzi.

Waandishi wana msimamo mkali. Wanaona kuna unafiki. Viongozi wamekuwa si wakweli. Si ajabu kwa hiyo kusikia tamthiliya hii haikuwafurahisha baadhi ya viongozi fulani fulani. Lakini ni mpaka lini viongozi watakataa kuhakikiwa? Wakati umefika wa viongozi kama hao kuukubali ukweli.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!