UHAKIKI WA DIWANI YA WASAKATONGE

By , in Kidato I-IV on . Tagged width:
UHAKIKI WA DIWANI YA WASAKATONGE
UTANGULIZI
Diwani ya Wasakatonge ni miongoni mwa diwani za hivi karibuni zinazotanabaisha matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii katika maisha yake ya kila siku. Matatizo hayo yanaonekana kuwa kama saratani isiyo na tiba. Hata hivyo, msanii ana matumaini kwamba, iwapo wananchi wa kawaida wataungana na kuamua kupambana, ni dhahiri kwamba matatizo hayo yatatoweka kabisa. Miongoni mwa matatizo hayo yataoneshwa kwenye kipengele cha maudhui huku yakishadidiwa na fani.
MAUDHUI: ni jumla ya mambo muhimu yanayoelezwa katika kazi ya kifasihi. Maudhui yanajengwa na vipengele vidogovidogo vifuatavyo; dhamira, ujumbe, mgogoro, mtazamo na falsafa.
DHAMIRA: ni jumla ya maana anayovumbua mwandishi aandikapo kazi yake na jumla ya maana anayoipata msomaji pindi anapoisoma kazi fulani ya kifasihi. Kifasihi kuna aina mbili za dhamira yaani dhamira kuu na dhamira ndogondogo. Dhamira kuu ni lile wazo kuu la mwandishi katika kazi, wakati dhamira ndogondogo ni zile dhamira zinazojitokeza ili kuipa nguvu dhamira kuu. Dhamira zilizojitokeza katika diwani hii ni kama ifuatavyo:
UONGOZI MBAYA: ni aina ya uongozi ambao haujali maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Ni uongozi unaotumia mabavu na unaojali maslahi binafsi, yaani haufuati misingi ya utawala wa sharia. Katika diwani hii msanii anaonesha kuwa nchi nyingi duniani hasa zile za kiafrika zinakabiliwa na tatizo la uongozi mbaya. Viongozi walio wengi ni madikteta ambao hawataki kuachia madaraka wala kuwapa watawaliwa uhuru wa kuzungumza.
Hali hii tunaopata katika shairi la “MADIKTETA” (uk.21) ambapo msanii anasema kuwa harakati za kusaka uhuru au demokrasia kwa njia ya mtu haijawahi kuzaa matunda yanayotarajiwa. Harakati hizi zimekuwa zikizalisha viongozi “Miungu watu” au marais walio madikteta, kama ilivyokuwa kwa Mabutu Seseko-huko Zaire (kwa sasa DRC), Bokosa-huko Afrika ya Kati na Idd Amini-huko Uganda. Madikteta hawa wamekuwa na kila aina ya uovu ikiwa ni pamoja na kukumbatia ukabila, udini na uvamizi kwa nchi nyingine. Haya tunayapata katika shairi la “SADDAM HUSSEIN” (uk.26:4) anasema;
4.    “Nakuafiki, Saddam, si kwa uvamizi wako,Na ujue kwamba,
                                                  Huo si uasi
                                      Kwa wakubwa mila, 
                                Saddam, yamesha tendeka sana!”
Viongozi wa aina hii huwanyima wananchi wao uhuru wa kusema ikiwa ni pamoja na ule wa kujiamulia mambo yao wenyewe kama katika shairi la “MARUFUKU” namba 45 (uk.36)
                               “Sitakiki uone,
Ingawa una macho,
      Sitaki useme,
Ingawa una mdomo,
                   Sitaki usikie,
Ingawa una masikio,
      Sitaki ufikiri,
Ingawa una akili,
                   Sababu utazinduka,
Utakomboka,
                   Uwe mtu,
Hilo sitaki,
                    Marufuku.”     
Viongzozi wabovu (madikteta) ni wapenda dhuluma na manyanyaso. Huwadhulumu na kuwanyanyasa raia wao na raia wa nchi nyingine kama inavyojidhihirisha katika mashairi ya “KOSA” (uk.3), na “FAHARI LA DUNIA” (uk.45). Katika shairi la “KOSA”, tunaona kuwa unyanyasaji wa wananchi wa kawaida hutokea pale ambapo wanapokuwa wanadai haki zao. Mshairi anasema:
3. “Kosa letu kubwa,
     Kudai haki?
    Yetu miliki?
   Mna hamaki,
       Na huku mnatukashifu!”
Katika shairi la “FAHARI LA DUNIA” (uk.45) tunaambiwa kuwa kuna kiongozi mwenye nguvu (Marekani) ambaye mchana kutwa usiku kuchwa linanyanyasa nchi nyingi bila sababu za msingi. Msanii anasema:
 5.     “Fahari la Dunia,
    Kwa kiburi, linatesa,
       Lajigamba,
      Linatamba,
                Kuwa mwamba,
               Linaoneya.”
 Viongozi wabovu siku zote ni wanyonyaji na hushirikiana na watu wengi wenye nguvu kubeba mirija ya unyonyaji na kuanza kuwanyonya raia wa kawaida. Hali hii hujitokeza sana katika nchi za Dunia ya tatu. Haya yote tunayapata katika mashairi ya “MVUJA JASHO” (uk.12-13), “MIAMBA” (uk.29-30), “MUMIANI” (uk.34) Katika shairi la “MVUJA JASHO” msanii anaonesha kuwa raia wa kawaida wanafanya kazi kubwa na ngumu sana lakini malipo yao hayalingani na jasho wanalolitoa. Katika shairi la “MIAMBA” tunaambiwa kuwa wanyonge hawana chao, jasho lao na wao wenyewe ni chakula cha wakubwa na watawala wao. Ubeti wa 4 wa shairi hili msanii anahoji juu ya suala hili kwa kutumia taswira ya wanyama:
4. “Wanyonge,
     Wamo shidani,
     Digidigi na nyani,
     Wamo makimbizoni,
     Fisi wafurahia,
                    Ni sharia za mbuga?”
Katika shairi la “MUMIANI” linaonesha waziwazi unyonyaji unaofanywa na viongozi au watu wa tabaka la juu dhidi ya tabaka la chini ambao wanaishi vijijini na mijini, waendao hospitalini na wapelekwao mahakamani. Katika ubeti wa 1 tunaambiwa kuwa:-
1.      “Mumiani,
Mijini,
Watembea kwa mato,
Kuzifanya kazi zao,
Kuzinyonya damu zetu,
Hawangoji,
   Tulale.”
Diwani hii inaendelea kuonesha kuwa viongozi wabovu ni wasaliti na wanafiki. Viongozi hawa wanakuwa wepesi kuwaomba wananchi ili kufanikisha jambo fulani. Lakini pindi jambo hilo linapofanikishwa tu viongozi hao huwaweka wananchi pembeni (huwasaliti wananchi). Miongoni mwa mashairi yanayoonesha usaliti na unafiki wa viongozi wa dini na wa kisiasa ni “SIKULIWA SIKUZAMA” (uk.22-23), “WASO DHAMBI” (uk.1), “UASI” (uk.8), “PEPO BILA KIFO” (uk.14), vilevile shairi la “NAHODHA” (uk.41) linaonesha kuwa kuna viongozi wengi wanaoshindwa kazi lakini hawataki kuachilia madaraka. Hata hivyo msanii anaonesha kuwa viongozi wa aina hii wanaweza kuondolewa madarakani iwapo tu wananchi wote wataungana na kuwapiga vita.
KUPIGA VITA UKOLONI: Ukoloni ni hali ya kuvuka mipaka ya nchi na kwenda kuitawala nchi nyingine kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Kutokana na madhara yanayosababishwa na ukoloni, msanii ameona kuwa tusiukumbatie bali tuupige vita ili tuweze kuishi maisha mazuri ambayo huja baada ya kujitawala. Katika shairi la “NURU YA MATUMAINI” (uk.9-10) tunaambiwa kwamba wananchi wa kusini mwa Afrika walipiga vita ukoloni ili kuondokana na ubaguzi, dharau, ubwana na utwana na hatimaye kuishi katika mazingira ya haki na usawa.
Kwa vile ukoloni unamadhara, kama inavyooneshwa katika shairi hilo, wananchi hawanabudi kuacha tabia ya kuukaribisha tena. Katika shairi la “HATUKUBALI” (uk.30) linatuambia kuwa;
4. “Hatukubali tena,
    Kutuletea usultani,
    Kutuletea na ukoloni,
    Kutuletea na uzayuni,
    Hatukubali katu,
    Ndani ya nchi yetu,
         Iliyo huru.”
Mbali na kupiga vita ukoloni mkongwe bali tunajukumu la kuutokomeza ukoloni mamboleo ambao kwa kiasi kikubwa unachangia kutufanya masikini. Ukoloni mamboleo hutufanya tusiwe na kauli juu ya bidhaa tunazozalisha na hatimaye Taifa letu kuishia kwenye lindi la umasikini. Inaonesha kuwa ukoloni mamboleo hutufanya tutekeleze matakwa ya mataifa makubwa kwa lengo la kuwa nufaisha wao huku sisi tukibaki taabani. Haya tunayapata katika shairi la “HATUNA KAULI” (uk.8-9)
6. Tumepewa yake mitaji,
     Tuwe wasimamiaji,
     Pia watekelezaji.”
Hali hii pia inajitokeza hata katika shairi la “WAFADHILI” (uk.38-39) ambapo tunaambiwa kuwa wafadhili hutupenda tu pale tunapokubali masharti yao na matakwa yao.
1.      “Wafadhili kufurahishwa,
Ni sera zao kupitishwa,
Rais anaamrishwa,
                        Tekeleza!”
Hali hii hutufanya tuwe watumwa wa ukoloni mamboleo baada ya kuondokana na ukoloni mkongwe. Katika shairi la “BUNDI” (uk.43) tunaambiwa kuwa uhuru wetu tulioupata hatujaufaidi hata kidogo kutokana na kupigwa nyundo ya kichwa na ukoloni mamboleo. Ukoloni huu ambao umefanikishwa na Bundi, tunaambiwa kuwa uko nasi kila kukicha. Ukoloni mamboleo ni mfumo usio na usawa hata kidogo. Ni mfumo ambao unawafanya wanyonge waendelee kuwa masikini, wasiomithilika huku matajiri wakiendelea kuwa watu wenye mali kupindukia. Haya yote tunayapata katika shairi la “KLABU” (uk.50) juu ya ukoloni mamboleo kwa kutuasa tuchapekazi, tujenge viwanda, tuboreshe kilimo na ufugaji, tuinue elimu, kukuza uchumi na tupige vita rushwa.
UMASKINI, UJINGA NA MARADHI: Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kusema kuwa, jamii yetu inakabiliwa na maadui wakuu watatu; Umasikini, Ujinga na Maradhi. Hali hii inajitokeza katika diwani hii kwani msanii anatuambia kuwa Bara la Afrika ni kama mgonjwa aliyemahututi katika shairi la “TIBA ISOTIBU” (uk.18) Hii ni kutokana na ujinga, umasikini na maradhi. Hali hii imekuwa ikisababisha njaa, vita, chuki na visasi vya kila aina na hivyo kufanya bara la Afrika lisiwe na amani kama ilivyo DRC, Sudani, Rwanda, Burundi, Tunisia nk. Mshairi anakereka sana na hali hii kwa kuhoji haya katika shairi la “AFRIKA” (uk.6-7)
1.      “Lini
Afrika utakuwa,
Bustani ya amani,
Ukabila kuuzika,
Udini kuufyeka,
Ni lini?”
Kwa ujumla Bara la Afrika limejaa watu masikini ambapo umasikini wao unatokana na mambo mengi kama vile unyonyaji unaofanywa na viongozi wao kwa kushirikiana na nchi za nje. Lakini pia umasikini hutokana na ujinga yaani elimu ndogo. Hali hii pia tunaikuta katika mashairi ya “WASAKATONGE” (uk.5), “MVUJA JASHO” (uk.12-13), “WALALAHOI” (uk.36-37)
MSUGUANO WA KITABAKA NA KIITIKADI (MATABAKA): Katika diwani hii msanii anaonesha msuguano mkali wa kitabaka uliopo katika jamii na katika nchi masikini na nchi tajiri. Matabaka haya yote ni zao la maisha ya kitajiri na kimasikini katika jamii. Tunaambiwa kuwa katika msuguano huu mkali baina ya matabaka, tabaka masikini linajaribu kujifaragua ili lipate angalau tonge la ugali wakati tabaka tajiri likijaribu kunyang’anya tonge linalopiganiwa na tabaka masikini. Haya tunayapata katika shairi la “TONGE LA UGALI” (uk.20)
4. “Wanapigana
     Wanaumizana,
     Wanauwana,
          Kwa tonge la ugali!”
Katika shairi la “WASAKATONGE” tunaambiwa kuwa wasakatonge na jua kali ni watu wa hali ya chini sana, wanaofanya kazi duni na ngumu na ndio waliowaweka madarakani viongozi wanaowanyonya na kuwanyanyasa. Wananchi hawa wana hali duni sana kutokana na kutothaminiwa na viongozi wao. Shairi la “WASAKATONGE” halinatofauti na mashairi ya “MVUJAJASHO” (uk.12) na “WALALAHOI” (uk.36-37) kwani yote yanazungumzia matatizo ya watu wa tabaka la chini yanayosababishwa na tabaka la juu. Katika shairi la “MIAMBA” (uk.29-30) na “MUMIANI” (uk.34) tunaona jinsi msongamano wa kitabaka unavyofanana na ule wa shairi la “TONGE LA UGALI.” Katika mashairi haya, wenye nguvu ndio hutawala na kuwanyonya wanyonge kama inavyojishihirisha katika shairi la “MIAMBA” ambalo limetumia taswira ya wanyama katika kuonesha matabaka hayo, kama msanii anavyosema:
1.      “Miamba,
Chui na Simba,
Mbugani wanatamba,
Vinyama vinayumba,
Chakula cha wakubwa
Ni sharia za mbuga?”
Hali ilivyo katika jamii yetu haina tofauti na ile ya mataifa tajiri na mataifa masikini, tunaendelea kuambiwa kuwa, mataifa masikini hayana chao mbele ya mataifa tajiri. Kazi ya mataifa masikini ni kutengeneza mipango ya mataifa tajiri kama inavyojionesha katika shairi la “HATUNA KAULI” (uk.8-9)
4. “Maagizo tunapewa,
      Mipango tunapangiwa,
      Na amri tunapangiwa.”
Mashairi mengine yanayoonesha hali hii ni “WAFADHILIWA” (uk.38) na “KLABU” (uk.50-51). Pamoja na masuluhisho yanayotolewa dhidi ya hali hii kama vile tabaka masikini kuungana na kupambana na hali hii, hasa kati ya nchi lakini bado msanii anawasiwasi juu ya kuondoka kwa hali hii katika jamii yetu. Hii inatokana na maswali anayojiuliza katika mashairi ya “TONGE LA UGALI” na “WASAKATONGE” ambapo msanii anaonesha hali ya kutokuwa na jibu rahisi katika kukomesha hali hiyo.
Pia msanii huyu amedokeza kuhusu mgongano au msuguano wa kiitikadi. Katika diwani hii tunaoneshwa kuwa, hatuna itikadi ya kisiasa inayoeleweka. Tupo kama hatupo na hatuelewi kama bado sisi ni wajamaa au mabepari. Hii inajidhihirisha katika shairi la “TWENDE WAPI” (uk.20-21)
3. “Twende wapi?
Mashariki “siko”!
Magharibi “siko”!
Wapi tuendako?
Tunatapatapa!”
Kutapatapa kiitikadi kunatusababishia tufanye mambo kama vipofu na matokeo yake ni kudaka kila kitu iwe kinachotoka magharibi au mashariki na hivyo kuathiri mfumo mzima wa maisha yetu ikiwemo mmomonyoko wa kimaadili.
UNAFIKI: Katika diwani hii tunaambiwa kuwa baadhi yetu hasa wanasiasa, viongozi au wananchi ni wanafiki wakubwa. Kwani kitendo cha baadhi ya watu kujiona kuwa hawana dhambi ni cha kinafiki kwa sababu, hakuna mwanadamu asiye na dhambi kama shairi la “WASODHAMBI” (uk.1) linavyosema;
2. Wavilemba!
            Wavilemba, na majoho, tasibihi,
                     Wajigamba, safi ni roho, ni kebehe,
                               Wanotenda,
                                             Unafiki.
Pia hata katika la “MAMA NTILIYE” (uk.17) nalo linadhibitisha hilo.
2. “Majungu na makaango, jinsi unavyoyapika,
      Na kibwebwe kiachiye, au utaadhirika,
      Kazi hiyo isusiye, hasara sijekufika.”
Diwani hii inaendelea kuonesha unafiki wa watu wa dini kupitia shairi la “UASI” (uk.8) Watu hawa hujidai mbele za watu ni waongofu wakati ni wachafu na wadhaifu katika matendo yao. Hawa ni watu wanaokashifu dini za wenzao kwa kudai kuwa zao ndizo safi na sahihi. Shairi linasema:
“Uasi
        Masheikh na masharifu,
Mapadri na maaskofu,
Kauli zao nadhifu,
Hujigamba waongofu,
Wengi wao ni wachafu,
Wenye vitendo dhaifu,
Dini wanazikashifu,
         Wanafiki.”
Unafiki wa baadhi ya watu unaendelea kuoneshwa kwenye shairi la “PEPO BILA KIFO” (uk.14) ambapo baadhi yatu hupenda vitu fulani fulani bila kufuata kanuni za upatikanaji wa vitu hivyo. Kitendo cha mtu kupenda pepo bila kuonja mauti ni cha kinafiki. Vilevile kitendo cha kupenda starehe za wanawake ni cha kinafiki kwani peponi si mahali pa kufanyia umalaya bali ni mahali patakatifu. Hivyo afikiriaye mambo haya ni mnafiki kwani hajui neno la Mungu linasemaje kuhusu pepo. Katika kuonesha unafiki shairi hili linasema:
5.  “Nibembee na hurulaini,
      Wanawake wazuri wa shani,
      Wawashindao wa duniani,
              Nipumbazike.” 
Unafiki mwingine unajionesha katika siasa ambapo baadhi ya viongozi hupata uongozi kwa kujipendekeza na kutoa maneno ya hapa na pale kwa wale wanawapatia hivyo vyeo. Haya tunayapata katika shairi la “WARAMBA NYAYO” (uk.46-47)
1.      ‘Wajikomba,
Ili kupata vyeo,
Na uluwa.”
USALITI: Mshairi Mohammed Seif Khatibu ameonesha suala la usaliti katika diwani hii  ya WASAKATONGE, kwani tunaambiwa kuwa, mara nyingi tunakuwa pamoja katika safari ya kutafuta kitu fulani lakini pindi kinapopatikana tu tunawatenga baadhi ya watafutaji wenzetu. Haya yanadhihirishwa wazi katika shairi la “SIKULIWA SIKUZAMA” (uk.22-23) ambapo msanii anabainisha kwa kusema kuwa;
1.      “Nilitoswa baharini,
 Ya dharuba na tufani,
       Walitaka nizame,
       Wao wanitazame,
Nife maji wakiona,
Waangue na vicheko,
        Na kushangilia,
        Ushindi wao!”
 Usaliti wa aina hii unajitokeza tena katika shairi la “ASALI LIPOTOJA” (uk.37-38), Shairi hili linaweza kufananishwa na hekaheka za kupigania uhuru ambapo baada ya kupata uhuru baadhi ya watu walioshiriki katika kuutafuta uhuru huo, walitengwa kabisa. Lakini pia matunda yaliyotegemewa baada ya uhuru hayajapatikana kwa wote bali kwa watu wachache tu wenye mirija mirefu (viongozi) kama lisemavyo shairi hili:
2.      “Mili ikatuvimba,
Ila hatukuyumba,
Tukabakia shambani,
Kutumaini kwamba,
Faida itawamba,
Heri itafika.”
3.      “Asali lipotoja,
Wengi walikuja,
Na mirefu mirija,
Kwao kawa tafrija,
Wakapata faraja,
Sisi tukatengwa.”
Katika shairi la “VINYONGA” (uk.49) tunabaini pia usaliti wa wanasiasa kwa wananchi. Shairi hili linaonesha kuwa wanasiasa wanatenda mambo kinyume na maadili na hivyo kuwasaliti wananchi waliowaweka madarakani. Viongozi hawa hawatekelezi yale wanayoahidi kwa wananchi wao badala yake wanatumia nafasi walizo nazo katika kujitajirisha wao wenyewe. Shairi linasema;
2.      “Jukwaa,
Meingiliwa,
Wanasiasa vinyonga,
Maisha ya ufahari,
Kauli zao nzuri,
Vitendo vyao hatari,
Ni kinyume na maadili,
Ni usaliti.”
Usaliti mwingine umejitokeza katika mapenzi. Mshairi anasema kuwa alikesha kwa ajili ya kumsubiri wake mahaba, ili baadaye wawe wawili. Hata hivyo mkesha wake haukuzaa matunda kwani mwenzie alimsaliti kwa kutofika katika eneo la tukio kama anavyoonesha katika shairi la “NILIKESHA” (uk.23-24)
4.      “Nilikesha,
      Na kulikucha sikukuona,
      Nathibitisha wako uungwana,
      Kosa langu kukupenda sana,
      Hustahiki heshima hiyo,
      Sisahau sikusamehe,
Nilikesha.”
Pia katika shairi la “SIKUJUA” (uk.28) linaonesha usaliti wa baadhi ya watu. Msanii anasema kuwa, aliyemfuga kwa mategemeo ya kumsaidia mambo mbalimbali amegeuka na kufanya kinyume na mategemeo au makubaliano. Msanii anadhihirisha hili kwa kusema;
4        “Kumbe nimefuga punda, mashuzi ndio heshima,
     Ni ukaidi wa inda, mateke kurusha nyuma,
     Nyama limekuwa nunda, mfugaji humuuma.”
MAPENZI/MAHABA: Miongoni mwa dhamira ambazo zimezungumziwa kwa kina katika diwani hii ni Mapenzi. Mshairi huyu anaonesha kuwa, mapenzi yana raha yake na pindi yanapokwenda mrama huleta karaha kubwa kwa mtu mmoja au wawili waliofarakana. Mshairi anasema kuwa mapenzi ni kitu muhimu sana kwake na yupo tayari kuitwa jina lolote lile kwa sababu ya kuyathamini mapenzi. Haya tunayapata kupitia shairi la “MAHABA” (uk.1-2)
4. Kama mahaba wazimu, sihitaji nitibiwe,
    Bora niwe chakaramu, nipigae watu mawe,
    Kuwa kwangu mahamumu, wewe isikusumbuwe,
    Dawa yangu siyo ngumu, mimi nipendwe na wewe.
Kwa vile mshairi huyu anaona kuwa mapenzi ndicho kitu cha thamani kubwa kwake ayakosapo au amkosapo yule ampendaye hukonda na kudhoofika mwili kama asemavyo katika shairi la “SILI NIKASHIBA” (uk.17)
2.  “Sili nikashiba, nikikukumbuka,
      Hula haba, na kushikashika,
      Ni chozi za huba, kweli nasumbuka.
Hali ya kupenda kwa dhati inajitokeza katika shairi la “NILIKESHA” (uk.23-24) ambapo mtu anaamua kukesha kwa kusubiri ahadi ya huba ingawa apendwaye huenda hayuko tayari kupenda. Shairi hili linasema;
1.      “Nilikesha,
      Si kwa ibada au shakawa,
      Sio kwa ngoma ama takuwa,
      Ila kwa hamu na nyingi hawa,
      Ikawa hakupambazuki,
      Ni mtekwa wa huba zako.”
Nilikesha.
Katika mashairi ya “USIKU WA KIZA” (uk.27-28) na “MACHOZI YA DHIKI” (uk.28) yanaendelea kuzungumzia hali hiyo ya mapenzi. Katika shairi la “USIKU WA KIZA” tunaoneshwa majonzi ya mpenzi mmoja aliyeondokewa na kipenzi chake. Kutoweka kwa mahabuba wake kunamfanya asile na kushiba kama shairi linavyosema;
2.      “Meniondokeya, wangu mahabuba,
  Nilikuzoweya, kwa yako mahaba,
  Nnajikondeya, sili nikashiba.”
Vilevile katika Shairia la “MACHOZI YA DHIKI” (uk.28) mpenda anabubujikwa machozi kwa kuadimikiwa na wake mahabuba, yaani anateseka kutokana na kuadimika kwa mpenzi wake.
Mshairi anaendelea kutetea mapenzi ya dhati katika shairi la “PEPO TAMU” (uk.35) ambapo anasema kuwa penzi tamu ni penzi lililojaa raha na lina ladha kushinda asali. Pendo tamu hufukuza uchoyo uheka.
“Pendo lenye tabasamu, za dhati si za uheka,
     Na nyoyo za ukarimu, uchoyo ni sumu yake,
     Haliishi yake hamu, hupendi imalizike.”
Kwa kuwa mpendwa anaonesha pendo la dhati, apendwaye pia anatakiwa aoneshe pendo lake kwa kutoa kauli kuhusu kupenda au kutopenda kwake kwa yule anayemtaka. Hii ni katika shairi la “ITOE KAULI YAKO” (uk.27)
1.      “Itoe yako sauti, kama, kweli wanipenda,
Niweze kujizatiti, moyo uondoke funda,
Nizidi kukudhibiti, sikuache hata nyanda.”
Shairi hilo linataka mpendwa atoe kauli yake kwani mpenda ameshatoa kauli yake ya upendo kama asemavyo katika shairi la “WEWE WAJUA” (uk.25)
1.      “Nakupenda, nawe wajua,
         Tusitupane,
       Tupendane,
       Kwa salama.”
Hali hii pia inajitokeza katika shairi la “NAKUSABILIYA” (uk.23) ambapo msanii anatoa pendo lake lote kwa yule ampendaye kama asemavyo katika ubeti wa kwanza;
1.      “Nakusabiliya, pendo lote kwako,
  Litaseleleya, litabaki kwako,
  Sitaliachiya, kwenda kwa mwenzako.”
Kama apendwaye ataonesha pendo la dhati kwa yule ampendaye basi watalindana na kulifanya pendo lao kuwa la wawili tu kama lisemavyo shairi la “NILINDE” (uk.15)
1.      Nilinde sichukuliwe, hata kwa moja shubiri,
Tubaki mimi na wewe, pendo letu linawiri,
Tuwazidishe kiwewe, wasotutakia heri.
Pia hali kama hii itasaidia kudumisha penzi lao milele na milele watabaki wawili peke yao huku wakifurahia pendo lao maridhawa. Haya tunayapata katika shairi la “TUTABAKI WAWILI” (uk.26) na “YEYE NA MIMI” (uk.39). Katika shairi la “TUTABAKI WAWILI”, tunaambiwa kuwa;
2.      Hakuna wa kulizima, pendo langu kufifiya,
Litabakia daima, na kwako kuseleleya,
Hadi siku ya kiyama, pendo litaendelea,
Shairi la “YEYE NA MIMI” linadai kuwa penzi tamu na dhati huwafanya watu wawili wapendanao wakeshe katika mapenzi bila kuchoka
4. “Yeye na mimi wawili, hatuna tunobakisha,
     Humsabilia mwili, hana anapobakisha,
    Ana mahaba ya kweli, usiku kucha hukesha.”
Katika diwani hii tunaambiwa kuwa kama unampenda mtu asiyekupenda basi usimchukui isipokuwa muagane kwa wema pale inapobidi kama inavyojionesha katika shairi la “KWA HERI” (uk.29)
3.      Ingawa menisusia kujipa kunigomeya,
      Mvua hunyesha masika, masika hukesha,
      Hakuna ukame,
                   Kwa heri.
Diwani hii inaonesha kuwa kukataliwa kimapenzi si mwisho wa dunia bali ni njia mojawapo ya kufunguliwa mlango kwa wengine hasa yule akupendaye kwa dhati. Haya yote tunayapata katika shairi la “NILICHELEWA KUPENDA” (uk.41)
1.      Katika uhai wangu, nilichelewa kupendwa,
Waliowakija kwangu, wale wa kunizuzuwa,
Mwaka huu mwaka wangu, nami nimejaaliwa.
Kwa upande wa pili msanii anakemea mapenzi ya sio ya dhati (ulaghai) kutokana na kutokuwa na faida yoyote kwa mtu na kwa jamii kwa ujumla. Mapenzi ya namna hii tunayapata katika shairi la “SI WEWE” (uk.21-22) ambapo msanii anahoji na kumsuta mtu aliyempenda kwa chati. Mapenzi haya hayana faida yoyote isipokuwa mateso makali kwa mhusika au wahusika;
4.      Umeshapwelewa baharini,
Wako werevu umekwisha,
Sasa unatweta,
U taabani,
Ni wewe ulo mlafi,
Si wewe?
Msanii anaendelea kusema mapenzi ya chati katika shairi la “WEWE JIKO LA SHAMBA” (uk.44) Hapa msanii anakemea tabia ya watu wanaofanya mapenzi kiholela kuwa waachane na tabia hiyo kwani haina faida isipokuwa karaha na kusutwa. Anaendelea kuwaambia kuwa;
        Takula wako ujuvi, na mwingi uhayawani,
Upikavyo haviivi, ni vibichi sahanini,
Vitachacha hivihivi, kuozea mikononi.
Watu wa aina hii sharti wajitakase ili wakubalike katika jamii yaani “wayapangue mafiga, jiko halitaivisha” wasipofanya hivyo, hawatapata kitu chochote cha maana kwani wapenzi (wawezeshaji) wamekuwa wengi. Shairi la “BUZI LISILOCHUNIKA” (uk.45)
        Msumeno utafute, na makali kuyaweka,
Ukwereze na uvute, na watu kukusanyika,
Na hutafika popote, buzi halitachunika.
Kwa ujumla msanii anazungumzia mapenzi ya aina mbili, mapenzi ya dhati ambayo kwake ndio ngao na mapenzi ya chati ambayo huleta karaha tupu katika maisha ya mwanadamu.