UHAKIKI: RIWAYA YA USIKU UTAKAPOKWISHA

By , in Kidato V-VI on . Tagged width:
 
UHAKIKI: RIWAYA YA USIKU UTAKAPOKWISHA
MWANDISHI: MBUNDA MSOKILE
MWAKA-1990
WACHAPISHAJI-DUP
UTANGULIZI
Riwaya ya Usiku Utakapokwisha imejadili kwa
kina masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika  jamii ya
Tanzania baada ya miaka ishirini na mitatu ya Azimio la Arusha.Mwandishi
ameyaangalia baadhi ya kwa jicho pevu matatizo yanayoikumbaTanzania katika
juhudi zake za kujenga jamii mpya ya kijamaa. Riwaya hii imekitwa kwa wahusika
watatu: Chioko, Gonza na Nelli.
     Nelli ni mchumba wake Chioko na
wanaishi kwa Gonza ambaye ana chumba kimoja tu,Gonza  anaishi kwa
kutegemea kuuza karanga na kufanya shughuli nyingine ambazo Chioko hazifahamu.
Katika msako unaofanyika mjini ili kutafuta wazururaji, Nelli anakamatwa na
kupelekwa kijii cha mapinduzi. Chioko hafanikiwi katika juhudi zake za kutafuta
kazi: Gonza anamshauri Chioko waende Zambia amabako watapata kazi. Chioko
anatilia mashaka mpango huo; lakini anapopata barua kwa Nelli kumweleza
kwamba,anakuja kumtembelea na hali yeye hana pesa anashawishika na mpango huo.
     Mwandishi Kupitia wahusika hawa
watatu anaichambua jamii ya Tanzania na hali nzima ya mfumo wa kiuchumi na
kijamii, na kuonesha uozo uliomo katika jamii hii ambayo inatarajia kujenga
mfumo wa Ujamaa. Suala la rushwa, na utumiaji mbaya wa madaraka kwa viongozi,
matabaka, dhiki za Walalahoi/makabwela na masuala mengine mengi yanayohusiana
na hali halisi ya kiuchumi,kisiasa na kijamii Mwandishi ameyapa nafasi
kubwa na kuyajadili kwa kina  katika riwaya hii.
MAUDHUI
DHAMIRA KUU;UMASKINI AU HALI NGUMU YA MAISHA
Hali ngumu ya maisha au umaskini  kwa makabwela
umemshughulisha sana Mwandishi katika riwaya hii ya Usiku UtakapokwishaKatika
riwaya hii, mwandishi anaonesha kuwa umasikini umewatawala sana watu wa tabaka
la chini kiasi kwamba, hata mahitaji muhimu hukosa na kusababisha vifo vyao,
kama asemavyo msanii (uk.7);
“Kifo kilichotokea kati ya mama na watoto wake wawili uko
Buguruni kinasikitisha. Ukweli ni kwamba haya ni madhara ya ufukara na
umasikini, watu hawa hawakua na kazi kwa muda mrefu na maisha yao yamekuwa
yakitegemea mno chakula kilichotokana na kuuzwa kwa vifaa na vyombo vyao vya
nyumbani. Lakini vifaa na vyombo hivyo vimeuzwa hadi vikaisha. Mwishoni wakafa
kutokana na kukosa chakula”.
Ugonjwa wa ufukara ulikuwa umewasonga sana watu wa tabaka la
chini. Kila wakijaribu kuutibu kwa kufanya kazi walishindwa (uk.11). Matatizo
ya maisha yaliwakumba wengi.Walijitahidi kupambana na shida usiku kucha, mchana
kutwa lakini mafanikio yao yakazidi kuwa duni. Mtatizo haya hayakuwakumba watu
wa tabaka la chini tu, yaliwakumba hata vijana wa shule.Katika uk. 16 mwandishi
anasema;
“Kwa watoto wa shule, hasa wasichana walipita mitaani huku
wakiwa wamebeba vyeti vya maisha yao. Kwa upande wao, mtu aliyempa chai ni
‘mpendwa’. Aliyetoa pilau ni mfadhili na yule aliyetoa lifti wakati wa jua kali
lililokausha midomo yao na kuwatoa jasho alikuwamungu mtu”.
Kutokana na umasikini vijana wengine walipoona hawana fedha,
walivuta bangi ili kutoa woga. Kisha wakawa wanauza bangi kwa siri,
walifanikiwa na walioshindwa walijiingiza kwenye vitendo vya wizi (uk.17).
Mwandishi ameonyesha namna makazi ya makabwela yanavyokatisha
tamaa. Waliishi sehemu duni ambazo hazina miundo mbinu kama Manzese. Manzese ni
sehemu muhimu ya mji wa Dar-es-salaam na ina mambo mengi. Huko ndiko wanakoishi
makabwela na makapera wa jiji hili, sehemu ambayo ni chafu na
haitamaniki.Katika uk.1 mwandishi anasema;
 “Sehemu ya jiji ambayo inafukuta harufu ya uozo wa aina
aina; sehemu ambayo ina mashimo na makaro yanayobwabwaja maji machafu ya mji,
sehemu ambayo ina mabanda mbavu za mbwa yenye kushika tama kwa unyonge! Manzese
inahuzunisha!”.
Mwandishi ameonyesha namna makabwela/maskini wanavyoishi maisha
ya taabu sana, nyumba zao si salama, chakula chao cha taabu daima wanaishi na
wadudu kama vile nzi, mbu, panya, kama rafiki zao. Maisha ya mtu masikini
hayakudhaminiwa ndio maana hata wakipeleka malalamiko yao serikalini
hawashughulikiwi (uk.7).
 Hali ngumu ya maisha au Umaskini imesababisha makabwela
kutegemea majaa ya takataka kupata chakula chao.Hawa waliokota vile vyakula
vilivyotupwa na wenye pesa ili kuokoa maisha yao ya kila siku. Katika uk.25
mwandishi anasema;
 “Wengine walikua wamejaa kwenye jaa moja la takataka,
karibu na barabara wakiokota punje ndogo ndogo za mchele zilizokuwa zimetupwa
huko.Pengine ilibidi wapepete makapi ya mchele zilizokuwa zimetupwa
huko.Pengine ilibidi wapepete makapi ya mchele kwa saa nyingi huku jua kali
likiwachoma.Hakika lilikuwa tatizo”.
Hali ya umasikini ina madhara yake kwa jamii.Kutokana na
umasikini makabwela wanapoteza utu wao. Mfano mtu yuko tayari kufungwa kwa
niaba ya mwenye pesa ya kununulia chakula kama asemavyomsanii (uk. 40);
“Mtu mmoja, mheshimiwa, mwenye pesa alikuwa amepatikana katika
kosa, akahukumiwa kifungo. Lakini yeye liamua kulinda hadhi yake kwa kumtafuta
mtu wa hali ya chini akafungwe ili alipwe pesa”.
Maisha ya masikini yalitegmea kuzunguka mitaani na kuuza
karanga, na njugu huku wakifukuzwa na mgambo kila sehemu. Maisha yao niya
kukimbizana na mgambo kila sehemu; masikini akipata matako hulia mbwata. Kwa
ujumla, msanii anaonesha kuwa watu masikini kula kwao ni kwa taabu, kulala kwa
kwa taabu, kunywa kwao kwa taabu, kila kitu ni taabu kwao, hawana nafuu yoyote.
    Mwandishi anaonyesha
kuwa  kwenye hoteli za makabwela vyakula vinavyouzwa navyo ni vya
hali ya chini sana ukilinganisha na mahoteli makubwa wanaokula viongozi na watu
wengine wenye pesa.Katika uk.37 mwandishi anasema;
“Akapita mbele ya jingo moja, akaona kibao kimeandikwa bei
mbalimbali za vyakula. Maandishi yake yalikuwa yakisomeka wazi.
NKom Ba hoTeLI
       BEI: MAkonGolo……………………………………..Shs 25.00
      BatA La
kUchoMA………………………………………….Shs 20.00
      PUA ya
nguruwe……………………………………………Shs 15.00
      MBavu
YamBuZI…………………………………………..Shs 20.00
      SuPu Ya kicHwa CHA
kuku…………………….………..Shs  3.00
     UtumBo wa
KUKU…………………………………………Shs  4.00
     KichWA chA
KuKu…………………………………………Shs  6.00
    UGAli…………………………………………………………Shs  5.00

fIrIGIsi la BAtA ……………………………………………Shs 10.00
                                                Fika
JioNEE mWENYEWE: nDunGu:
                                        ChAKula
Ni   uZIMA: NKomBa end GampaNi 
  Sehemu
hii ilikuwa maarufu kwa watu wa tabaka la chini, lakini wa hali ya juu haikuwa
sehemu maarufu kwao, kwani hoteli yenyewe haikuwa ya hadhi yao. Pua ya nguruwe,
supu ya kichwa cha kuku, utumbo wa kuku, na filigisi za bata ni vyakula vya
makabwela.
      Katika kuondokana na tatizo
hili la umasikini. Gonza anasema lazima itafutiwe sababu ili tuweze kuondokana
na umasikini. Gonza anasema (uk.8);
“Panapowezekana pawezekane! Panaposhindikana pashindikane;na
sababu itafutwe na kutolewa hadharani”.
Mwandishi anaona kuwa ili tuondoe umasikini, lazima tutafute
kwanza chanzo cha umasikini huo.Chanzo kikipatikana, hata hatua zakuchukua
dhidi ya umasikini itakuwa rahisi kupatikana.Mwandishi anapendekeza kuwa,
kufanya kazi kwa bidii ni njia mojawapo ya kuondoa umasikini.(uk. 11);
 Mwandishi anaonesha
kuwa kufanya kazi kwa bidii kutaondoa ugonjwa huu wa ufukara kwa makabwela.
Bila kufanya kazi kwa bidii;itakuwa ndoto kuondokana na huu umaskini.
 Mwandishi anaona kuwa kurudi shamba si suluhisho la
umasikini kwani hata huko shamba kuna matatizo yake kama ilivyo mjini.
Mwandishi anasisitiza kuwa sio makabwela tu walazimishwe kwenda shamba
mabadiliko ya nchi lazima yawe ya watu wote na sio makabwela tu (uk. 19).
Mwandishi anaonesha kuwa lazima huduma zote muhimu zipelekwe huko kijijini ili
ziwavutie watu kwenda huko (uk. 19).
  Mwandishi anaona kuwa ili kuondokana na umasikini ni
muhimu kuanzisha miradi mjini. Lakini kwanza lazima tuwe na nia, kama
hatutakuwa na nia miradi hiyo itakufa. Miradi anayopendekeza mwandishi ni kama
vile maduka ya ushirika. Kwa upande wa Gonza na Nyundo wanaona njia pekee ya
kuondokana na umasikini ni kupambana na wenye pesa kwa nguvu na kugawana kile
wanachomiliki: Gonza na Nyundo wanaona wenye vyeo ndio wamesababisha umasikini,
kwahiyo tunapotaka kuondoa umasikini lazima tupambane nao (uk. 74);
“Leo jioni kuna kazi………leo usiku tutakwenda nyumbani kwa yule
meneja wa kampuni ya mabomba…… Tanzania frendi; hatuwezi kulala njaa wakati
watu wengine wanachezea mifwedha…… wanasaza mifedha……”
Mapambano ya Gonza dhidi ya wenye navyo yanaangamiza maisha yake
kabla usiku haujaisha. Mwandishi anatuonesha kuwa mapambano dhidi ya umaskini
si lelemama bali yanahitaji umoja na mshikamano wa makabwela, kwani umoja ni
nguvu na utengano ni udhaifu (uk. 39).
Mwandishi wa  riwaya hii  ameonesha matatizo
mbalimbali yanayoikumba Tanzania ya leo kama vile  umaskini,uongozi
mbaya na rushwa,matabaka,wizi na ujambazi,umalaya na matatizo mengine mengi na
hizo ndizo dhamira ndogo ndogo.
     1. SUALA LA UONGOZI NA RUSHWA
Azimio la Arusha lilianzishwa mwaka 1967  hapa
Tanzania  lilikusudia kujenga mfumo wa Ujamaa.Katika Azimio hilo
suala la uongozi bora lilijadiliwa kwa kina hasa misingi yake.Mwandishi
anaonyesha kuwa licha ya kulipa kipaumbele suala la kujenga ujamaa lakini bado
kuna viongozi ambao wanakiuka misingi ya kujenga jamii yenye haki na
usawa.Mwandishi  ameonesha kuwa viongozi wetu wako mstari wa mbele kupokea
rushwa ili watoe huduma .Katika uk 13 mwandishi anasema;
          “Natafuta
kazi”
     “Kazi?”
     “Ndiyo kazi”
     “Je una chochote?”
     “Kama nini?”
    “Ma-dalla kadhaa!”
    “Ya kazi gani?”
    “Ili tumlainisha meneja. Unajua meneja
ni mzee wa nyumbani, lakini habari hii ya
dalla   anaipenda        sana.
Hii ni silaha kubwa tukitaka kufanikiwa mambo ya siku hizi magumu”
   Akameza mate na kuendelea kusema
    “Isitoshe, kila mtu tutakamopita kabla
ya kufika kwa mzee itabidi kutoa dalla kadhaa.
Iko      kazi”
Pia Suala hilo linajitokeza tena katika uk.21 pale Gonza
anapomtaka Chioko amshawishi mpenzi wake Nelli ahonge mwili wake ili apate
kazi, mwandishi anasema;
  “Mwambie shemeji ahonge bwana.Kama hana pesa kama
sisi anaweza kutumia njia nyingine. Kama ujuavyo yeye ni msichana bwana. Anao
uwezo mkubwa sana wa kuwaweka sawa maofisa wa aina yoyote ile. Usiwaone
wasichana wengine wamevalia wakipita mitaan ukadhani ni hivihivi tuu”
Watu walioshika nafasi za uongozi kwenye taasisi mblimbali
wanaajiri watu baada ya kupata hongo au rushwa na Iwapo mwombaji kazi ni
mwanamke basi wanatarajia kulala nae kwanza kabla ya kumpatia kazi. Lakini
wakati mwingine msichana anayehusika anakuwa kama mcheza kamari kwani anaweza
kutoa penzi na kazi hapati kama anavyosema mwandishi (uk. 21);
     Kuna vijana ambao pengine
wanahonga lakini kazi yenyewe wasipate, na kuna wasichana ambao pamoja na
kuyakubali matakwa ya wakubwa, lakini hawafanikiwi katika matumaini yao ya
kupata kazi; wakubwa waliowaahidi kuwapa kazi wanawapa mimba na kuwatelekeza.
Hivyo basi, mwandishi anaona kuwa wanasichana hawanabudi kuepuka rushwa kwani
katika hali kama hii  msichana anaweza kuwa Malaya.
  Mwandishi anaitaka jamii  kuwainga
viongozi wanaotumia vibaya madaraka waliokabidhiwa. Badala ya kuwaajiri watu
kufuatana na kanuni zinazofahamika katika masuala ya ajira, wao wanafuata
kanuni zao wenyewe ambazo zinawaletea maslahi binafsi.Mwandishi anaonyesha kuwa
Matokeo ya msichana kutafuta kazi yanakuwa kupata mimba (uk. 42-43). Msichana
wa namna hii, ambaye anapata mtoto na hana uwezo wa kumhudumia,kuna uwezekano
mkubwa wa, kama hakufikiria kutoa mimba kabla ya kujifungua au kumtupa mtoto
baada ya kuzaa.
      Suala la uongozi mbaya, wizi
na njia mbaya ambao watu wenye nyadhifa wanazitumia ili kupata pesa za kutumia
kwa ajili ya starehe zao ni kinyume na misingi ya Azimio la Arusha. Gonza
anasema kwamba, watu wengi ambao wana fedha nyingi wamepata fedha hizo
kutokana  na njia ya dhuluma au za wizi. (uk 43);
“Wewe sikiliza, Chioko uawaona wale wenye mifedha hapa mjini”?
Wengi wao wamedhulumu walishikwa? Hawakushikwa. Walioshikwa n bahati mbaya na
hawana raha”
.
Katika hali kama hii maskini au walalahoi au makabwela
hawafurahii matunda ya uhuru yaani kana kwamba uhuru umetekwa nyara na watu
wachache ambao wananufaika kutokana na uhuru huo.
 Wakulima na wafanyakazi sio wanaonufaika na jasho lao,
bali vibepari uchwara ambavyo vimepata bahati ya kujipachika katika sehemu za
uongozi. Wao ni wanyonyaji wa jasho la wakulima na wafanyakazi. Wakati wakulima
na wafanyakazi wanatoa jasho lao kufanya kazi, viongozi hao ndio wanaolifaidi
jasho hilo. Matokeo yake ni kuwa, matunda ambayo mkulima na mfanyakazi
wanayahangaikia usiku na mchana hawayaoni. Hawaoni jinsi ambavyo serikali
inajitahidi kuondoa matatizo yao yanayowakabili. Wameshindwa kujikimu walau kwa
mahitaji yao ya lazima.
       2. UJENZI WA VIJIJI VYA UJAMAA
(Operesheni sogeza)
Miaka ya 1974 Tanzania ilifanya ikifanya jitihada ya kujenga
vijiji.Kumekuwa na juhudi mbalimbali za kujenga vijiji  .Katika
kujenga  vijiji vya ujamaa hapa Tanzania  njia mbili
zilitumika ambazo ni:
·
Kuwaweka  pamoja
watu ambao nyumba zao zilikua mbalimbali
·
Kuwasaka watu
wasio  na kazi mjini na kuwapeleka vijijini.
        Dar-es-salaam,kama
miji mingine ya Tanzania umewahi kukumbwa na msako wa watu wasio na
kazi  ambao wamekamatwa na kupelekwa kijiji cha mapinduzi.Riwaya
ya Usiku Utakapokwisha inalishughulikia tatizo hili.Watu
wasiokua na kazi wanakamatwa na kupelekwa kwenye kijiji cha ujamaa cha
mapinduzi, miongoni mwa wanaokamatwa ni wauza karanga,maji ya barafu,korosho
kama asemavyo msanii(uk. 48);
“Walishikwa wa aina aina.Wauza kashata,Njugu na
karanga,walikuweko wauza pombemwenye mabaa,walikuweko walevi pia,walikuweko
wale waliofikiriwa pia kuwa ni wezi walikuwepo.Tulipofika huko tulikua watu
wengi, huko tulikuta pia wachawi waliokuwa wamekamatwa na kupelekwa huko kama
adhabu. Tulikutana wengi……………………”
Watu hawa wote walishukiwa kwamba,wao ndio wezi ambao usiku
wanabomoa majumba. Iwapo ni hivyo, basi kitu ambacho kinafanyika ni kama
kuusafisha mji, watu ambao hawatakiwi kuwepo mjini na kuwapeleka vijijini.
  Je,ndiyo kusema kwamba vijiji ndio vimekuwa ngao ya
kuhimili mishale inayorushwa?Je, pengine kusingeweza kupatikana na uwezekano
mwingine wa kuwashirikisha watu hawa katika shughuli za kijamii wakiwa hukohuko
mijini badala ya kuwasukumizia vijijini ambako hawakai bali wanatafuta mbinu za
kutoroka na kurejea tena mjini?  Aidha, kuwapeleka watu kama wezi na
wanyang’anyi vijijini kunatoa picha ya kwamba vijijini ni mahali pa kuishi watu
wa aina iyo. Hivyo basi, kitendo hiki kinaweza kufisha juhudi zote za kujarbu
kuviimarisha vijiji na kuvifanya mahali pazuri pa kuishi.
   Katika maongezi yake, Nelli anakisifu mno
kijiji cha Helela.Anatoa picha ya kwamba hapo ni mahali ambapo hakuna matatizo
(uk. 49);
“Kijiji hiki kina wakazi wapata  elfu saba. Kina
umeme, kina maji, kina chakula kingi na cha kutosha kuwalisha majirani wa
vijiji vikubwa visivyopungua kumi. Helela imesonga mbele, kijiji cha Helela
kina mashamba mengi ya mahindi na ngano, mashamba ya maharage, ndizi na
smatunda mengineyo. Naikumbuka Helela, naipenda Helela. Helela imesonga mbele”.
Picha anayoitoa Nelli kuhusu Helela ni ishara ya maendeleo ya
kuridhisha kwa vijiji vya ujamaa vilivyoanzishwa na serikali, na vijiji lazima
viige maendeleo ya kijiji cha Helela.
Baada ya kukamatwa Nelli na kupelekwa kijiji cha mapinduzi,
kulitokea matatizo mbalimbali. Kwanza kulitokea fujo, mkusanyiko wa waovu
mbalimbali hauwezi kujenga jambo la maana. Kutokana na kuwepo kwa wachawi,
wezi, wahuni ikatokea vita vya kugombea wasichana (uk. 48).
Baada ya zile vurugu za kijiji cha mapinduzi, watu wengi sana
walifanikiwa kutoroka na kurudi tena mjini. Kurudi kwao mjini kunaonesha
kwamba, katika mfumo kuna jambo Fulani ambalo linakosekana. Je, jambo hilo ni
lipi? Nelli (uk.50) anasemaUtaratibu wake si mzuri”.
    Katika mfumo wetu wa kijamii kuna tofauti kubwa kati ya mfumo wa
mji na kijiji, mfumo wa kiuchumi na kijamii umeipendelea zaidi niji kuliko
vijiji. Katika masualaya mawasaliano na huduma nyingine za kijamii hakuna
uwiano kati ya miji na vijiji. Vitu hivi vimeshughulikiwa mjini lakini vijiji
vimeachwa nyuma. Huu upendeleo wa miji dhidi ya vijiji ndio unaowafanya watu
wakapendelea zaidi kuishi mijini kuliko vijijini. Na ndio maana watu waliosakwa
na kupelekwa kijiji cha Mapinduzi wanaamua kutoroka kutoka huko na kurudi mjini
ambako kuna starehe ambazo huko vijijini hazipatikani.
     Kwa upande wa Gonza, yeye hana
sababu ya kwenda kijiji cha mapinduzi. Gonza amezaliwa mjini, amekulia mjini na
ataendelea kuishi mjini kama alivyosema(uk. 50);
“Mimi binafsi sipendelei “Alijibu Gonza haraka haraka”.
“Kwa nini?
“Nimezaliwa mjini, nimekulia mjini; na sasa makazi yangu ni
mjini; shamba nimfuate nani na nikafanye nini?”
Kwa upande wa Nelli, amejifunza maisha ya kijijini na baada ya
kurudi mjini anatamani kurudi tena kijijinimradi tuu ahakikishwe usalama wake,
anasema (uk. 51);
“Niko tayari kurudi tena huko nikihakikishiwa usalama wangu”.
Gonza anashangaa kusikia tamko la Nelli la kutaka kurudi
kijijini. Kwa ujumla, msanii anaonesha kuwa kuwasaka watu na kuwapeleka
vijijini si suluhisho la msingi. La muhimu ni kutafuta suluhisho la matatizo
hayo mjini hukohuko.
      3. SUALA LA MAPENZI
Ni hali ya kupenda na kuvutiwa sana inayojengeka baina ya mtu
mzima mmoja na mwingine.Mwandihi ameainisha aina mbili ambazo;
·
Mapenzi ya kweli na
mapenzi ya uongo (pesa).
·
Mapenzi ya kweli
Kwa upande mwandisi ameainisha kama ifuatvyo;
Mosi,mapenzi ya kweli kati ya Chioko na Nelli; hawa walipendana hasa katika shida na
raha,katika uk.2-3  Chioko anasema;
“Barua hiyo ilikuwa imetoka kwa mpenzi wake Nelli. Nelli alikuwa
tumaini la maisha yake ……Nelli……Nelli alikuwa waridi la moyo wake.Nelli alikuwa
kioo cha maisha yake…..Nelli alijazwa katka kilakona ya maisha yake”.
Pia katika uk.6 Chioko anaendelea kusisitiza kuwa ;
“Nelli ndiye ua langu…Nelli ndiye waridi la moyo wangu mchanga
……….Nelli wangu “
Maneno ya Chioko dhidi ya Nelli ni ishara tosha kuwa ,hawa watu
walipendana kwa dhati na mapenzi yao hakuna wa kuyatenganisha labda kifo tu.
Pili,mapenzi ya kweli kati ya Chioko na Gonza, Chioko na Gonza walikuwa marafiki hasa na
wasiri wakubwa. Walikuwa wamesoma wote huko Iringa,ingawa kiini chao kilikuwa
tofauti.Wazazi wao walikuwa wakifanya kazi huko Iringa. Na huko ndiko
walikokutana vijana hawa wakashibana.Walielewana sana.Walikuwa wameelewana hata
wakawa wanazungumza kwa kutumia viungo vya miili yao na sasa walikuwa
wamekutana tena hapa jijini na waliishi pamoja kwa kusaidiana hadi kifo cha
Gonza.
Kwa upande wa mapenzi ya uongo ambayo msingi wake ni pesa mwandishi anaonyesha kuwa Wanawake wengi
waliwapenda wanaume tofauti kwa sababu ya pesa. Wanafunzi nao walikua kwenye
mkumbo huohuo,wa kupenda wanaume kwa sababu ya pesa,kama asemavyo msanii (uk
17);
“Utanipa nini nawe katika kipindi hiki cha
dhiki”?  Alidharau msichana mmoja alipokuwa ametupiwa kombora la
penzi na kivulana kitanashati kilichokua kinasoma hapa jijini”.
Mwandishi wa riwaya hii  anaonesha kuwa mapenzi ya
pesa kwa kiasi kikubwa yanatokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili watu wa
tabaka la chini. Nakutokana na hali hiyo ndiyo maana linajitokeza tatizo la
umalaya jijini.
     4.  TATIZO LA USAFIRI
Mwandishi anaonesha kuwa katika jiji la Dar-es-salaam kuna
tatizo kubwa la usafiri kwa watu wa tabaka la chini.Usafiri pekee unaotumiwa na
watu wa tabaka la chini ni UDA ambapo mtu unakaa kituoni kwa muda mrefu
Kutokana na uchache wa mabasi ya UDA.Katika uk. 27 mwandishi anasema;
“Walifika kituoni, hapa walikuta umma wa watu, utadhani kulikuwa
na sherehe ya kumtoa mwali na ambaye leo hii amefunga ndoa”
 Mwandishi anaoneshak kuwa Licha ya watu kukaa sana vituoni
kusubiri usafiri pia kuna tatizo la msongamano wa watu kwenye vyombo hivyo vya
usafiri. Watu wanasukumana, kila mmoja akigombea nafasi.Hasara za kusukumana
huko ni kuibiana na kupata vilema ambavyo havikutegemewa (uk. 29).
 Mwandishi naonesha kuwa kwenye vyombo hivyo vya usafiri,
kuna matusi ya kila aina.Mtoto anamtukana mtu mkubwa, konda anamtukana
abiria,abiria wanamtukana konda na dereva, matokeo yake ni matusi mtindo mmoja.
Kutukana matusi kwenye vyombo vya usafiri ni kinyume na utaratibu wa jamii,
kwani kwenye vyombo hivyo kuna watoto.Hivyo matusi hayo yanawakomaza watoto
kabla ya umri wao (uk. 29-34).
 Kutokana na tatizo hili la usafiri kwa watu wa tabaka la
chini; wengi wao wanachelewa makazini na kwenye shughuli nyingine za kujenga
taifa. Mwandishi ameongelea tatizo hilo miaka ya 1990, na bado tatizo hili
linaendelea, leo hii watu wanapitia madirishani kutokana na tatizo la usafiri.
      5. UTOAJI  MIMBA NA
UTUPAJI WA WATOTO
Suala la utoaji mimba linaonekana kuota mizizi katika jamii ya
sasa.Mwandishi amejadili suala hili kwa mapana.Kwa kuangalia suala hili kwa
mapana zaidi inaonekana kwamba, ukiacha wanafunzi wa vyuo vikuu, wanafunzi
wengine wote wanafukuzwa shule wanapopata mimba. Tatizo hili pia linapelekea
utoaji mimba au utupaji wa watoto (uk. 56).
Mwandishi wa riwaya hii anaonesha kuwa suala la utoaji mimba na
utupaji wa watoto ni tatizo sugu, na hili kwa kiasi kikubwa linasababishwa na
umasikini .Katika uk. 42-43 mwandishi anasema;
“…… Mara ngapi watu huimba jijini juu y wasichana wanaoitwa
Malaya ‘ na wale wanaotupa watoto mapipani……… wanawalaumu…… eti Malaya! Ati
wahuni! 
Ni kweli wanauza
miili; sawa lakini tumekaa na kufikiri kwa nini? Nani
anapenda  mwili wake? Ni mwanake gani angependa kumridhisha kila
mwanaume? Hakuna!Nani anapenda kutupa watoto? Hakuna lakini
kuna  maana  gani kutunza mtoto wakati huna chakula cha
 kumlisha?
Uhai wa mtoto huyu ni nini kama si chakula? Kwa msichana anayetafuta fedha
akipata mimba ni suala la bahati mbaya yeye anataka chakula …… matokeo ya mtoto
hayakutarajiwa wala hayaheshimu”
Suala hili linafungamana na suala zima la mfumo wa kiuchumi na
kijamii. Wasichana wanatoa mimba au kutupa watoto kwasababu hawawezi kuwakimu
kimaisha. Mkabala wa jamii dhidi yao ni wa kikatili. Kupata kwao mimba
kunaangaliwa kama mtu ambaye amefanya dhambi isiyosameheka.Kuogopa hali ngumu
ya jamii kunawasukuma wasichana hawa ama kutoa mimba au kutupa watoto.
Katika kutatua tatizo hili mwandishi anapendekeza kwamba, lazima
tuchunguze kwanza mfumo wa uchumi na kijamii. Mfumo mzima wa kiuchumi na
kijamii hauna budi kuchunguzwa. Na katika mambo hayo ndimo ambamo jawabu la
tatizo hili linaweza kupatikana.
     6.  NAFASI YA MWANAMKE  
  Katika riwaya hii mwanamke amechorwa katika nafasi
mbalimbali.
 Kwanza mwanamke amechorwa kama chombo cha starehe
kwa wanaume
.Viongozi na mameneja wengi wanawatumia wanawake kukidhi
haja zao za kimwili pindi wanawake hao wanapokwenda kutafuta kazi ili apate
kazi lazima amstareheshe kwanza mwajiri wake (uk. 23).
       Pili,mwanamke
amechorwa kama kitega uchumi
 na ndiyo maana Gonza alimshawishi
rafiki yake Chioko amshawishi mchumba wake Nelli akahonge penzi apate kazi ili
wapate hela ya kwaajili kukidhi mahitaji yao muhimu ya nyumbani.
      Tatu, mwanamke
amechorwa kama kiumbe duni asiye na maamuzi yoyote
 katika jamii
zaidi ya kumtegemea mwanaume, katika uk 56 mwandishi anasema;
“Mwanamke …kwani mwanamke nani? Kila cha maana hubebwa na
mwanaume.Haki zote anazo mwanaume. Ndio mwamuzi na hakimu nyumbani.Kazi ya
mwanamke? Kuzaa, kupika na kumtumikia mume. Mwanamke!”
   Nne,
mwanamke amechorwa kama mshauri mzuri wa mwanaume,
mwandishi
anaonesha kuwa 
Nelli kama mshauri mzuri.Kwanza aliwashauri
Gonza na Chioko kurudi kijijini na pia aliwashauri kuanzisha miradi na shughuli
mbalimbali za kibiashara zinazoweza kuwafanya waishi na ndugu na wote
wanaowahusu hapa mjini (uk. 51).
kwa ujumla Mwandishi anawalakini juu ya nafasi ya mwanamke
katika jamii.Mwandishi anaona mwanamke hana mchango wowote katika jamii zaidi
ya kumtegemea mwanaume tu.Mwanamke pia ananafasi yake katika kuleta maendeleo
ya jamii  kama alivyo mwanaume.
          UJUMBE
·
Ili tuweze
kujenga jamii mpya lazima tupige vita uongozi mbaya na rushwa.
·
Mfumo wa elimu
unaotolewa haumjengi mwanafunzi kujitegemea, bali kutafuta kazi za ofisini.
·
Umoja na mshikamano
kwa watu wa tabaka la chini ni njia mojawapo ya kupambana na umasikini.
·
Kufanya kazi kwa bidii
ni njia mojawapo ya kuondokana na umasikini.
·
Kutoa mimba au kutupa
watoto chanzo kikubwa sni hali ngumu ya maisha kwa wale wanaohusika.
·
Tatizo la usafiri
litatatuliwa iwapo tu serikali itajenga miundo mbinu zaidi ili kuwezesha
kununuliwa kwa magari mengi.
MIGOGORO
·
Kuna mgogoro kati ya
wenye navyo (matajiri) na wasio navyo (masikini).
·
Mgogoro kati ya tabaka
tawala na tabaka tawaliwa.
·
Mgogoro kati ya mgambo
na walalahoi (masikini).
 MSIMAMO
Msimamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi kwani ameonesha matatizo
mbalimbali yaliyoko katika jamii na baadhi ya suluhisho la hayo matatizo.
FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa umasikini utaisha iwapo masikini
watafanya kazi kwa bidii na kuanzisha miradi mbalimbali ya biashara ambayo
itawaingizia kipato cha kuweza kujikimu. Vilevile anaona kuwa mfumo wa kiuchumi
na kijamii lazima ubadilishwe.
           FANI
MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo wa rejea katika riwaya yake.
Ameigawanya riwaya yake katika sura tisa na matukio kutoka sura moja kwenda
sura nyingine ni changamano.
Mtindo
Msanii ametumia mtindo wa masimulizi  na Nafasi zote
tatu amezitumia. Vilevile ametumia mbinu mbalimbali za kifasihi simulizi.
Kwanza kuna matumizi ya nyimbo,mfano katika ukurasa wa  23;
KILINDWACHO
Ajabu ya kilindwacho,
kwa upeo wa kulinda,
kilindwacho hutokea.
Na kwa mwizi kikanenda
Jizi likatoa macho
na kikanena kilindwa,
mwizi ni’ be hima hima,
ili nende nikalindwe.
 Pili mwandishi ametumia hadithi ndani ya hadithi.
Hii inapatikana katika kurasa za 19, 24 na 42.
    Tatu,matumizi ya  barua,Barua
mojawapo ni ile anayoandakiwa Gonza na Chuchu kutoka Zambia inayomtaka Gonza
aende Zambia, huko kuna maisha mazuri.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha rahisi iliyojaa misemo,
methali, tamathali za semi, mbinu nyingine za kisanaa na taswira mbalimbali.
       Misemo/ Nahau
·        Mtu
anayelala mbavu za mbwa – (uk.1).
·        Mtu
anayelala na mgonjwa ndiye anayejua miugulio yake (uk. 7).
·        Hatukupata
kiamsha kinywa (uk.10).
·        Jitu
hili  la miraba mitano (uk. 29).
·        Hawamziki
mama yao akafika chini (uk. 39).
        Methali  
·        Ukishindwa
kupata kwale mawindoni rudi na bundi (uk. 43).
·        Nguo
ya kuazima haisetiri matako (uk. 36).
·        Jino
la pembe si dawa ya pengo (uk. 36).
·        Alipo
kilema usikunje kidole (uk. 3).
·        Usipochomwa
mwiba hujui kiatu (uk.5).
   TAMATHALI ZA SEMI
       Tashibiha
·
Hata majengo
yaliyokuwa yamesimama kama askari jela wa kikoloni yalikuwa shwari (uk.4).
·
Lakini iliyobeta kdogo
mithili ya mdomo wa bata (uk. 5).
·
Yalikuwa katika siri
ya moyo wake mithili ya kaburi lifichayo maiti (uk. 5).
·
Jogoo kama mfalme wa
nyumba alifunza vifaranga kunya tunduni (uk. 33).
          Tashihisi
·
Alichukuliwa na
usingizi haraka haraka, guu moja kalipinda na kuligandisha ukutani bila yeye
mwenyewe kujijua (uk. 1).
        Sitiari 
·
Sehemu ambayo ina
mabanda mbavu za mbwa yenye kushika tama kwa wanyonge (uk. 1).
·
Nelli alikuwa waridi
la moyo wake; Nelli alikuwa kioo cha maisha yake (uk. 3).
·
Nelli ndiye waridi la
moyo wangu mchanga (uk. 6).
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
      Tanakali sauti (Onomatopea)
·
“Myaau!
myaau!myaau!Sauti kali ya paka ilisikika juu ya paa (uk. 1).
·
Haa! Haa!
Mwanaume mzima unaogopa (uk. 9).
·
Baada ya muda
kidogo nasikia sauti kali pyaaaaa.
     Takriri
·
Kila kitu kilikuwa
kimya! Kimya kushoto, kimya kulia …… Hata mbele kulikuwa kimya (uk.3).
·
Alikuwa na kiu, Kiu
kubwa! ….. Alijua miugulio ya kiu (uk. 7).
·
Nimeporwa  a-a-a,
nimeporwa jamani? Watu hawakujali (uk. 29).
     TASWIRA  
Katika riwaya hii mwandishi ametumia taswira mbalimbali kama
ifuatavo;
Kwanza ametumia taswira zionekanazo za wadudu/wanyama kama vile
nzi
kunguni,
mende, viroboto, panya, paka
, n.k kuashiria makazi duni ya watu wa hali
ya chini huko Manzese.
      Pili, sehemu nyingine katika
riwaya hii giza 
limetumika
kuashiria matumaini finyu ya makabwela kuweza kupata
nafuu katika maisha yao ya kila siku.
WAHUSIKA 
Mwandishi ametumia wahusika watatu ambao ndio washiriki katika
riwaya hii. Wahusika hao ni Chioko, Gonza na Nelli: kuna wahusika wengine kama
vile Chuchu, Nyundo, Matiko, Kazimoto, Priscilla, Titos, n.k.
     1.  CHIOKO
      – Amemaliza darasa la saba na anatafuta
kazi ya ofisini. Yeye ni kiwakilishi cha vijana ambao baada ya  kumaliza masomo
yao wanakimbilia mjini ambako wana mategemeo ya kupata kazi ya kuajiriwa.
        -Chioko anakaa kwa rafiki yake Gonza, Manzese.
        -Alikuwa rafiki yake Gonza na msiri wake na
kabila lake ni Mngoni.
       -Chioko hakubahatika kwenda sekondari kutokana
na kifo cha babake aliyetakiwa ampe vifaa vya           shule.
         – Alikuwa mpenzi wake Nelli na alikuwa
tegemezi kwa kila kitu.
     2.  GONZA
      – Huyu ni rafiki yake Chioko na kabila lake
ni Mgogo na alisoma mpaka kidato cha nne.
     – Anaishi Manzese ambako anaendesha
maisha yake kwa kuuza karanga. Ni kutokana na hizo karanga ndio anaweza
kutosheleza kwa kiasi fulani maisha yake naya Chioko pamoja na Nelli.
    -Anaishi maisha ya kikabwela katika chumba
kimoja.
   – Anayaelewa maisha na mbinu za namna ya
kuyaishi. Gonza ndiye anayemfafanulia Chioko ambavyo wanawake kwa wanaume
wanavyotumia mbinu mbalimbali kupata kazi.
    – Anawakilisha mawazo na malalamiko ya
tabaka linalokandamizwa. Anaona jinsi mfumo wa uchumi unavyowapendelea baadhi
ya watu ambao wanafanikiwa kimaisha kutokana na wizi au udanganyifu, pamoja na
kutofuata maadili ambayo jamii imekubaliana.
      -Malalamiko aliyonayo ni ya kimsingi, ndiyo
yanayomsukuma kuwa mwizi.
     – Anataka kuyakimbia maisha kwa kwenda
Zambia KWANI akifika huko atapata kazi.
     3. NELLI
    – Huyu ni mpenzi wake Chioko na katika
harakati zake za kutafuta maisha anakamatwa na kupelekwa kijiji cha Mapinduzi;
ambako katika muda mfupi tu wa kuishi huko kunakuwa na athari katika maisha
yake.
     -Anataka kurudi katika kijiji cha Helela au
Mapinduzi kama watamhakikishia usalama wake.
     – Ni muhusika ambaye amechaguliwa
kuwakilisha mawazo ya kijiji. Kutokana na kuishi kwake kijiji cha Mapinduzi
amebadilika kabisa kimaendeleo, na hana analoongelea kuhusu kijiji cha Helela
isipokuwa sifa tu. Hivyo anafaa kuigwa na jamii.
MANDHARI
Mandhari ya riwaya hii ni ya jijini Dar-es-salaam,hasa sehemu za
Manzese, Kariakoo,Posta,Tandika na Buguruni.Vilevile kuna mandhari ya nyumbani,
barabarani, kwenye vyombo vya usafiri, kwenye mabaa,mitaani, n.k.  
JINA LA KITABU
Jina la kitabu Usiku Utakapokwisha linasadifu
yale yaliyomo ndani ya kitabu hiki kwa kuwa Neno Usiku linamaanisha Giza.Giza
linaloongelewa na mwandishi ni matatizo wanayokabiliana nayo watu wa tabaka la
chini kama vile; Umaskini,Hali ngumu ya maisha,Ukosefu wa ajira,Tatizo la
usafiri n.k Je lini matatizo haya yatakapokwisha? Matatizo haya yamefananishwa
na  Giza kulingana na utatuzi wa matatizo hayo.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
KUFAULU
Mwandishi amefaulu kwa kiasi kikubwa;
     -Kuonesha matatizo  mbalimbali
yanayowakabili mafukara na makabwela hapa nchini.
     -Kuonesha chanzo cha matatizo hayo.
     -Kutumia lugha rahisi inayoeleweka na
amewachora vizuri wahusika kuwakilisha hali halisi ya jamii.
KUTOFAULU
Suluhisho la matatizo ya makabwela halijapatikana mpaka mwisho
wa riwaya, tunachoona ni wahusika kuandika kwenye mikokoteni yao “Iko siku”
(uk.36). Hili ni suluhisho la kukatisha tamaa, hiyo siku ni lini na kwa nini
isiwe sasa. Kwa hapa mwandishi hajatuonesha wazi suluhisho la matatizo
aliyoyajadili.