UHAKIKI NA UCHAMBUZI WA RIWAYA YA NAKURUTO

By , in Riwaya on . Tagged width:

UHAKIKI NA UCHAMBUZI WA RIWAYA YA NAKURUTO

UTANGULIZI

JINA LA KITABU       :  NAKURUTO

JINA LA MWANDISHI: CLARA MOMANYI

MWAKA                       : 2009

HISTORIA YA MWANDISHI

Clara Momanyi ni mwandishi kutoka nchini Kenya. Historia fupi ya maisha yake ni kwamba, Clara monanyi alikuwa mwanafunzi kutoka chuo kikuu cha Kenyatta nchini Kenya, ambapo alipata shahada ya kwanza chuoni hapo katika kitengo cha elimu yaani Bachelor of Arts with Education (BAED), shahada ya pili aliipata katika fani ya uzamili (M.A) ya Kiswahili kutoka chuo hichohicho cha Kenyatta, hakuishia hapo pia Clara Momanyi alihitimu shahada ya uzamivu (PHD) katika masomo ya fasihi ya Kiswahili kutoka katika chuo kikuu cha Kenyatta nchini Kenya.

Clara Momanyi alishawahi kuwa mhadhiri na Profesa wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Kenyatta nchini Kenya, alikuwa pia mhadhiri mwandamiza katika shule ya sayansi ya jamii ya idara ya Kiswahili na lugha nyingine za kiafrika nchini Kenya. Clara momanyi alikuwa pia mwenekiti wa idara ya maendeleo ya mtaala wa Kiswahili katika chuo cha Kenyatta kilichopo chini Kenya. Kwa hivi sasa Clara Momanyi ni Profesa katika chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Kenya yaani THE CATHOLIC UNIVERSITY OF KENYA.

Clara Momanyi ni mwandishi na mhadhiri mwenye tajiriba pana katika uandishi na ufundishaji wake. Hii inadhihirishwa na kazi mbalimbali alizoweza kuzitoa ambazo ni zaidi ya ishirini (20) miongoni mwazo ni riwaya ya Nakuruto aliyoiandika 2009, fasihi ya Kiswahili aliyoshirikiana na waandishi kina Njongu aliyoitoa mwaka 2006, Siku ya Wajinga Wote 2005, Pendo katika shairi kutoka Lonhorn Publishers.

USULI WA RIWAYA YA NAKURUTO.

Riwaya ya Nakuruto ni riwaya iliyoandikwa na Clara Momanyi mwaka 2009. Riwaya hii ni ya kifantasia yaani ni riwaya ambayo inaeleza matukio ya ajabu ajabu mfano kupaa angani kwa Nakuruto, kuwa kijana mara kuwa mzee, kutua chini kutoka angani, kutokea katika mazingira ambayo hakuwepo ghafla au kupotea katika mazingira aliyokuwepo ghafla, na pia kufahamu mazingira na watu kwa nguvu ya kimiujiza.

 Riwaya hii pia imenuia kueleza na kufafanua kwa mawanda mapana suala zima la uharibifu wa mazingira pamoja na jinsi ya kutunza mazingira hayo kwa kutumia mhusika Nakuruto mwandishi Clara amefanikiwa kufikisha dhamira hii kwa jamii kwani ameweza kuelimisha baadhi ya jamii juu ya utunzaji wa mazingira hata mara baada ya kuyaharibu mfano, jamii ya walatimbi walielekezwa mbinu kadha wa kadha ili kurudisha uhai wa kijijji chao mara baada ya kuharibiwa na kutimuliwa kwa bwana Brook.

Kimtazamo mwandishi Clara Momanyi anaona kuwa ndani ya jamii yoyote, ili maendeleo yapatikane lazima kuwe na ushirikiano baina ya wanajamii na kila mmoja afanye juhudi za ziada  kuboresha hali iliyopo kwa kujitoa muhanga kama kijiji cha walatimbi walivyofanya kuboresha hali ya maisha yao na baadaye kumuondoa bwana Brook.

NADHARIA ZILIZOTUMIKA KATIKA RIWAYA HII

Maana ya nadharia, nadharia ni istilani ya kiujumla inayomaanisha miongozo inayomwelekea msomaji wa kazi ya fasihi kuifahamu kazi ya fasihi katika vipengele vyote (Njogu na Wafura 2007).

Nadharia zilizotumika katika kazi hii ni pamoja na;

Nadharia ya saikochanganuzi; nadharia hii hujulikana pia kama udodosi nafsi au unafsia. Katika riwaya hii imejitokeza pale ambapo mwandishi amemchora muhusika Nakuruto na kufikisha ujumbe wake katika hali ya kuota ndoto, kinachoaminika katika nadharia hii ni kwamba kupitia ndoto matendo yote yaliyotendwa kwa siri huwa yanaibuka yaani ung’amuzi bwete.

Nadhaia ya mwingiliano matini, hii ni nadharia inayoongelea uhusiano wowote unaoweza kuonekana katika matini moja au zaidi na uhusiano huo ni kuanzia kwenye nukuu, uelezaji wa jambo moja kwenda jingine na hata kuwa na lugha zinazofanana au hata kuhusiana. Katika riwaya ya Nakuruto mwandishi ametumia Ngano katika ukurasa wa18. Mwandishi hakuishia hapo aliendelea kuonesha nyimbo alizokuwa anaimba Nakuruto katika ukurasa wa 19, 43, 89, 92, 93, 98.

Nadharia ya uhalisia wa kimazingaombwe, katika nadharia hii msomaji humuona muhusika katika sura tofautitofaui mara mzee, mara msichana nk. Riwaya hii ni chuku kwani imetiwa chumvi nyngi sana pale ambapo mtu anapaa angani na kupitishwa maeneo mbalimbali kwa wakati uleule.

MAUDHUI KATIKA KITABU CHA NAKURUTO

Maudhui ni jumla ya mawazo ya mwandishi katika kazi ya fasihi ikiwa ni pamoja na dhamira kuu na dhamira ndogondogo, migogoro, falsafa ya mwandishi, msimamo, mtazamo na ujumbe.

DHAMIRA

Dhamira ni wazo au mawazo makuu yaliyojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira hugusa maeneo yote katika maisha yaani kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Dhamira kuu.

Katika kitabu cha Nakuruto dhamira kuu ni; Ujenzi wa jamii mpya. Mwandishi amejitahidi kuonesha kwa uwazi dhamira hii pale ambapo Nakuruto alipowahimiza wanajamii kutunza vyanzo vya maji hayo kwa maana maji ni uhai uk.71 na kuyatumia kwa manufaa yao ya kiuchumi.

Vilevile katika ukurasa wa 42-50 Nakuruto aliwahamasisha wanajamii kumtimua bwana Brook aliyekuwa akiwanyonya kama anavyosema katika uk. 43 “tupange tumwondoe dhalimu huyo katika ardhi yetu, asiendelee kuunyonya uhai wetu, pamoja na watoto wetu.

Pia ujenzi wa jamii mpya umeonekana pale ambapo muhusika Sheshije alipoamua kupanda ngazi bila kujali maneno ya wanawake wenzake ili kuleta mabadiliko katika jamii yake katika ukurasa 131.

Vilevile katika jamii zetu mambo hayo yapo na kuna watu wanaojitolea kwa hali na mali ili kujenga jamii mpya kwa mawazo yao na hata michango yao katika kupigania kuondolewa kwa ufisadi ili iweze kuwa na maendeleo.

Dhamira ndogondogo.

Unyonyaji na ukandamizaji; dhamira hii imeonekana pale ambapo mwandishi anamtumia bwana Brook aliyekuwa akiwanyonya wananchi baada ya kuwapokonya ardhi yao na kuitumia kwa faida yake huku walatimbi wakibaki na vijishamba vidogovidogo visivyo na rutuba, hasa wakina mama wakiwa na watoto migongoni  wakibeba magunia ya pamba na kupeleka katika kinu cha kuchambulia. Pia walatimbi walikandamizwa kwenye migodi ya madini, kusomba mchanga na kulipwa ujira mdogo sana ukilinganisha na ugumu wa kazi wanayoifanya katika ukurasa 31, 38 na 39.

Kwa ujumla wanajamii wa walatimbi walinyonywa na kukandamizwa, haya yanaonekana bayana katika ukurasa wa 42, pale Mkude anaposema “ huyo mzungu siku hizi anaitwa bwana Breki. Amewafunga walatimbi breki za nyuma na mbele sasa wamekuwa watumwa, vikaragosi na vibaraka  wake” Tunaona kwamba suala la unyonyaji na ukandamizaji sio geni katika jamii  zetu za kitanzania, viongozi wengi katika sehemu mbalimbali wamekuwa wakitumia nyadhifa zao vibaya mahali pa kazi kwa kuwanyanyasa watu walio chini yao huku wakijua kwamba watu hao hawawezi kufanya lolote na wanastahili kutendewa hivyo.

Suala la elimu; pamoja na kwamba elimu ni kitu cha  muhimu katika jamii yoyote ile ili iweze kuendelea. Lakini mwandishi Clara Momanyi amejitahidi kutuonesha jinsi uongozi uliokuwa madarakani katika jamii ya walatimbi haukuthamini elimu. Tunaona katika ukurasa wa 88 na 90 sehemu walizopita Nakuruto na Leboni waliona mikusanyiko ya wanafunzi chini ya mbuyu na wengine wakisomea ndani ya mahema kwa sababu ya majengo yao ya shule kuchukuliwa na matajiri waliodai kuwa shule hizo zilijengwa katika maeneo yao.

Mambo hayo pia katika jamii zetu yapo, wapo viongozi wengi  na watu ambao wana uwezo wa kifedha ambao hawathamini elimu na wanafumbia macho matatizo yaliyo katika kada hiyo. Kwa kutopeleka vifaa vya kujifunzia na kufundishia shuleni. Zipo shule ambazo mpaka leo hii wanafunzi bado wanakaa chini wakati wa kujfunza pia kuna shule ambazo hazina maabara za kujifunzia pamoja na kutoa motisha kwa walimu wanaofanya kazi hiyo ya kufundisha katika mazingira magumu.

Matabaka, hii ni dhamira nyingine ambayo mwandishi ametuonesha, matabaka yamejitokeza katika jamii ya maweni kijiji kilichojaa matabaka ya juu na chini, yaani tabaka la mabwanyenye  akina Brook wanamiliki nyanja muhimu zote za uzalishaji mali na tabaka la akina Mkude ambao maisha yao yalikuwa duni sana. Mwandishi amejitahidi kuigusa jamii yetu kwani matabaka yapo katika kila nyanja za  kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni kama tabaka la walionacho na tabaka la chini.

Uharibifu wa mazingira; pamoja na kwamba mazingira ni kitu muhimu ambacho kinafaa kutunzwa, lakini mwandishi Clara Momanyi ametuonesha jamii hizi hazikuthamini mazingira kwa kumtumia muhusika Ludao (uk 32) ambaye alikuwa anachimba mitaro ya kupitishia maji ya ziwa kwenda shambani mwake, pia kando ya ziwa wanawake na watoto wakifua huku uchafu ukiingia ziwani na kuharibu maji ya ziwa. Pia wanakijiji wa maweni waliharibu mazingira kwa kukata mti, kuchimba mchanga na kuchoma mkaa. (uk. 71). Mambo haya pia yanaonekana katika jamii zetu wapo watu wamekuwa wakiharibu vyanzo vya maji kutokana na shughuli mbalimbali kama kupasua mbao, uchimbaji madini kiholela, uchomaji mkaa na uvuvi haramu ambayo yamesababisha kutokea kwa ukame.

Nafasi ya mwanamke katika jamii. Mwandishi anamuonesha mwanamke katika nafasi mbalimbali kama ifuatavyo.

Mwanamke kama mkarimu, mwandishi anamtumia Nashelangai alivyomkarimu Nakuruto kwa kumkaribisha na kumpa mtoto wake ambariki pia alimpatia chakula na kumfulia kaniki yake. (uk 13, 14, 15, 16 na 17)

Mwanamke kama mwanamapinduzi na muhamasishaji; hii imeonekana kwa kumtumia Muhusika Nakuruto kuwahamasisha wanakijiji kufanya mgomo uliofanya matajiri kufunga viwanda na kurudi kwao. Pia Nakuruto aliwahamasisha walatimbi katika kumwondoa Brook. Uk 44

Mwanamke kama mtu mchoyo na katili. Mwandishi ameonesha haya kwa kumtumia muhusika Nariangai Nganda ambaye hakuthamini ugeni wa Nakuruto nyumbani kwake alimnyima mtoto wake na kumpa nyama mbichi na iliyoharibika.

Mwanamke kama mtu jasiri; mwandishi anaonesha hili kwa kumtumia mhusika Sheshije ambaye aliamua kupanda ngazi uk 131-136 bila kujali maneno yasemwayo na wanawake wenzake huu ni ujasiri. Mwandishi amekusudia kuonesha kuwa wanawake wananafasi ya kushika uongozi wa juu kama alivyofanya Sheshije.

Mwanamke kama kiumbe duni, mwandishi anaonesha jinsi walatimbi walivyo mchukulia mwanamke kama kiumbe duni pale ambapo Baludao aliposhangaa kitendo cha mwanamke katika kupanda ngazi. Uk 132 alisema lakini tangu lini mwanamke akahusishwa na ujenzi wa ngazi?. Pia kijana Mrisho alishangaa kwa mtoto wa kike kuongea mbele ya wazee. “mtoto mdogo wa kike anayeota ndoto tangu lini jamii hii ikaruhusu mtoto wa kike kuongea mbele ya wazee?. Uk. 70. Pia katika jamii mwanamke ameonekana ni kiumbe duni kwani hastahili kufanya kazi za ofisini, iliaminika kuwa mwanamke madaraka yake ni mekoni na kutunza watoto ili kukiendeleza kizazi kama anavyosema mama Bintifundi uk 33 na 34  “Tangulini tukawa na maafisa wanawake  hapa kwetu”

Hata katika jamii za kisasa watu wengi wanamchukulia mwanamke kama mtu asiye na mchango wowote katika jamii lakini tunaona kwamba mwanamke ni kiumbe  kama walivyo wanaume na anaweza kufanya kazi zote za ofisini, nyumbani, za kisiasa na hata za kiuchumi ilimradi tu akiaminiwa na kushirikishwa kama alivyoelezea mwandishi kwa kuwatumia wahusika Sheshinje na  Nakuruto.

Suala la wizi wa mali za umma. Mwandishi amejitahidi kueleza jinsi suala la wizi linavyorudisha nyuma maendeleo katika jamii. Na suala hili limejitokeza pale ambapo wanakijiji  waliopewa kandarasi ya kuleta mchanga na kokoto mahali pa ujenzi hawakufikisha badala yake waliwauzia watu binafsi  kama ilivyoelezwa na mwandishi katika ukurasa 123 na 124. Mwandishi amejitahidi kuigusa jamii yetu kwani mambo mengi ya umma yanakuwa hayana utekelezaji wa haraka kwa sababu  ya tabia hii ya wizi na watu kujinufaisha  wenyewe badala ya kunufaisha jamii mfano ujenzi wa majengo kama shule, zahanati hayakamiliki kwa wakati na wananchi wakapata huduma kwa sababu ya tabia kama hizo.

Rushwa, rushwa ni miongoni mwa mambo ambayo yanasababisha watu kukosa haki zao. Mwandishi katuonesha jinsi gani suala la rushwa lilivyotokea katika mkutano wa kuteua kamati ya kusimamia ujenzi ule. Katika uchunguzi ule kura ziliibwa na baadhi ya wagombea walionekana kuwahonga wapiga kura waziwazi ili wawachague na wakiwachagua watawaonesha mbimu za kuipata harufu ya nta. Mwandishi ameyaeleza haya katika uk. wa 125

Hata katika jamii zetu mambo haya yapo kwani wapo viongozi wengi wanaowahonga wananchi kwa vitu mbalimbali zikiwemo fedha ili wawachague katika nyadhifa fulani serikalini ili waweze kujinufaisha wenyewe badala ya jamii nzima kunufaika, jambo hili ni hatari kwani husababisha kuwa na viongozi wasio bora, wabinafsi, mafisadi na wala rushwa wasiojali haki za raia wao na wajibu wao kwenye nyadhifa walizoshika.

Migogoro.

Ni hali ya mvutano na msuguano kati ya pande mbili. Migogoro yaweza kuwa ya mtu na mtu, mtu na kikundi au mgogoro wa kinafsia, mwandishi Clara Momanyi amejitahidi kutuonesha migogoro hiyo kama ifuatavyo.

Mgogoro wa nafsia; mwandishi ameonesha chanzo cha mgogoro pale alipokuwa akibadilikabadilika umbile  na kumfanya ajishangae mara anaonekana binti na wakati mwingine anaonekana kikongwe kama anavyosema “mama yangu mie! Nimekuwa mkongwe hivi” na kujiuliza ni mimi huyu au ni nani? Huku akishangaa na kujaribu kusimama, anaendelea kusema “haiwezekani! Hii ni ndoto, kweli mimi naota, lazima nimo ndotoni uk na 9

Mgogoro kati ya wanakijiji walatimbi na Bwana Brook; chanzo cha mgogoro huu ni pale bwana Brook alipowanyonya na kuwapokonya wanakijiji ardhi na kuendeleza shamba lake la pambo huku akiwaacha wanakijiji hao katika maeneo yao madogo yasiyo na rutuba. Suluhisho la mgogoro huo, ni pale Nakuruto alipowahamasisha walatimbi kumuondoa bwana Brook na kufanikisha kuchoma kinu chake cha kuchambulia pamba.

Mgogoro kati ya mwenyekiti na wanakijiji wa kijiji cha Maweni; mgogoro huu ulianza pale ambapo mwenyekiti alipoungana na Nakuruto kuwahamasisha wanamaweni kufanya mgomo viwandani na kusababisha nguzo kuondoka kama ilivyoelezwa uk 69, 70 na 71 na baada ya wazungu kuondoka, wanamaweni maisha yao yalikuwa magumu kwa kuwa hakuweza kutumia viwanda kwa sababu hawakuwa na ujuzi huo. Hivyo walilaumu sana hali hiyo ilivyowakuta. Suluhisho la mgogoro huo ni pale Nakuruto alipowahamasisha tena wanakijiji kuchimba visima na mabwawa kwa ajili ya kuanzisha kilimo na ufugaji.

Ontolojia; ni kile kitu ambacho jamii inakiamini juu ya jambo fulani. Ontolojia katika kitabu cha Nakuruto imejitokeza katika namna mbalimbali.

Mwandishi ameonesha jamii ya Nashelangai aliamini kuwa watoto wadogo wakitemewa mate na vikongwe wanapata Baraka (uk 14). Pia jamii hiyo iliamini kuwa linapotokea baa la kutopata mvua au ukame wa muda mrefu ilibidi ifanyike kafara ya msichana mrembo kama Nakuruto anavyosema katika hadithi aliyomsimulia Nashelengai katika uk 18 na 19 .

Ujumbe

Ni funzo ambalo msomaji wa kazi ya fasihi anaupata baada ya kusoma kazi ya fasihi, ujumbe katika Riwaya ya Nakuruto ni kama ifuatavyo:

  • Mwandishi anatufundisha kuwa si jambo zuri kuwadharau wanawake kwani wanawake wanaweza kuleta maendeleo katika jamii.
  • Mwandishi anatufundisha kuwa wizi si kitu kizuri kwani hurudisha maendeleo nyuma.
  • Mwandishi anaifunza jamii juu ya kuyatunza mazingira kwani ndio uhai
  • Mwandishi anaifunza jamii kuwa rushwa na ubinafsi haviwezi kuendeleza nchi yoyote ile.

Msimamo na Mtazamo.

Ni mtazamo ambao mwandishi wa kazi ya fasihi anakuwa nao anaposhughulikia matatizo mbalimbali yanayoikumba  jamii husika.

Msimao wa mwandishi ni wa kimapinduzi kwani aneonesha matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii katika ujenzi wa jamii mpya ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira, wizi wa mali za umma na rushwa na kupendekeza njia mbalimbali za kutatua matatizo hayo na kuwaletea watu ahueni.

Falsafa.

Ni imani aliyonayo mwandishi wa kazi ya fasihi katika jamii yake. Mwandishi Clara Momanyi anaamini kuwa umoja na mshikamano ndio nguzo pekee zitakazowasaidia watu ili kupata maendeleo katika Nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

FANI KATIKA RIWAYA YA NAKURUTO.

Fani ni ule ufundi autumiao mwandishi au msanii katika kufikisha ujumbe wake kwa jamii inayohusika. Fani katika kazi ya fasihi huhusisha vipengele vya muundo, mtindo, wahusika na matumizi ya lugha.

Muundo

Ni mpangilio na mtiririko wa kazi ya riwaya katika visa na matukio. Dhana hii hubainisha namna ambavyo mwandishi anaweza kuvisuka visa na matukio katika kazi yake. Aina za muundo ni kama vile muundo wa msago yaani moja kwa moja, muundo wa kioo yaani urejeshi au muundo geuzi (pindu), na muundo wa mwingiliano wa visa yaani changamani.

Katika riwaya ya Nakuruto mwandishi Clara Momanyi amevisuka visa  na matukio katika muundo wa moja kwa moja (msago) visa na matukio anavipangilia kuanzia sura ya kwanza hadi sura ya saba. Katika kila sura matukio au visa vimesimuliwa kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mfano; sura ya 1: Nakuruto kuingia usingizini na njozi kuanza, nguvu ikimwinua na kumpitisha sehemu mbalimbali na kujikuta mzee. Sura ya 2: Nakuruto katika kijiji cha marangau na kutokea ziwa Nakuruto. Sura ya 3: Nakuruto katika kijiji cha walatumbi na ziwa ipe na kushuhudia uchafuzi wa ziwa ipe. Sura ya 4: Nakuruto katika kijiji cha maweni. Sura ya 5: Nakuruto katika kijiji cha Maweni. Sura ya 6: kuonekana katika kijiji cha Maweni. Sura ya 7: kuonekana tena katika kijiji cha Maboni.

Mtindo

Ni ule upekee wa mwandishi katika kuijenga kazi yake. Msanii huweza kutumia mbinu mbalimbali ili kutaka kazi yake iwe tofauti na ya mwingine.

Mwandishi Clara Momanyi katika riwaya ya Nakuruto ametumia mitindo mbalimbali katika uandishi.  Ametumia masimulizi ya hadithi katika uk. 18 – 20 Ametumia nyimbo katika maeneo mbalimbali mfano katika ukurasa wa 19,47, 89, 92 na 98. Hotuba pia imetumika pale ambapo Nakuruto alipokuwa akiongea na wanavijiji wa Maweni, Latimbi na maboni katika suala zima la utunzaji wa mazingira. Uk 34 – 35, 41 -45, 71 – 72. Dayalojia imejitokeza pia katika riwaya ya Nakuruto mfano ukurasa 12 – 16 kati ya Nakuruto na Nashelengai, uk. (33 – 34). Nakuruto na Nariangai uk. 33 – 34, Nakuruto na Mwanamke ziwani na Nakuruto na mzee Saluda

Motifu.

Motifu ni kipengele radidi katika kazi ya fasihi. Ni hali ya kujirudiarudia kwa tukio fulani katika sehemu mbalimbali za kazi ya fasihi. Mwandishi Clara Momanyi katika Riwaya ya Nakuruto visa na matukio yamejidhihirisha kuwa ni safari na msako. Kuanzia sura ya kwanza hadi ya saba safari katika ndoto inayompitisha Nakuruto katika maeneo mbalimbali yenye matukio ya uharibifu wa mazingira kwa sababu mbalimbali na kumfanya kutoa ushawishi wa urejeshaji wa hali ya awali ya mazingira hayo. Hii inasababisha mwisho wa safari katika ndoto inamrejesha katika maisha halisi ya kutafuta suluhisho la yaliyojitokeza kijijini.

Motifu ya msako inajitokeza pale ambapo Nakuruto anapoonekana kukerwa na hali ya uchafuzi wa mazingira na kutamani kuona tena hali nzuri ya mazingira inapatikana tena na jamii kuishi mahali pema mf. Uk 35. “pitisheni ujumbe huu kwa wanakijiji wote ili mjaribu kuweka mikakati ya kutunza ziwa hili”

Pia alionesha nia ya kusaidia kizazi kile pale aliposema “nina shauku ya kuwapiginia nyie na watoto wenu”. Uk 44 alitoa ushauri wa kuwaondoa wazungu waliokuwa na makampuni ya uchimbaji madini ikiwa ni shughuli mojawapo yenye kuchangia uharibifu wa mazingira. Ushauri wa uchimbaji visima uk 71. Geuzeni kijii hiki kuwa bustani itakayosifiwa na kila jamii ya watu. Nakuruto anachorwa kusaka maisha bora kwa jamii yake. Uk 50 unatuthibitishia na kusaka ndoto iliyopotea, ndoto ya mafanikio.

Mandhari

Ni mazingira ambapo ujenzi wa visa na wahusika huainishwa na mwandishi. Katika riwaya ya Nakuruto mwandishi Clara Momanyi amejenga mazingira ya aina mbili.

Mosi ni mazingira ya kubuni (kinjozi) na pili ni mazingira halisi. Mzazingira ya kubuni ni yale ya pangoni kupaishwa angani na nguvu isiyo ya kawaida. Mazingira halisi ni yale ya ziwa ipe, Milimani, shambani, Mto Milu, Kijiji cha maweni, walatimbi na Maboni.

MATUMIZI YA LUGHA

Lugha ni mfumo wa sauti nasibu na ishara ambao umekubaliwa na jamii ya watu ili itumike katika mawasiliano. Lugha ni muhimu sana na ya msingi katika uandishi wa kazi za fasihi ambapo hupambanua fikra na mawazo na ujumbe alionao mwandishi kwa jamii husika.

Tukirejelea riwaya ya Nakuruto mwandishi Clara Momanyi ametumia lugha ya kawaida na inayofikisha ujumbe kwa jamii ya wasomaji, vilevile ameweza kuingiza lugha nyingine za kienyeji na ile ya kigeni yaani Kiingereza mfano maneno kama vile shakiri uk. 72, watribu uk. 73, ….kifyefe uk. 40, …..umenijia yosayosa uk. 65, ….kwanini ulitumia haukuwabanduka uk. 82 na uk. 86, …raghba na mengine mengi.

Lugha ya Kiingereza katika uk.98 mwimbaji anapoghani …….if you don’t pay that bil… na majina ya mitaa na hoteli yaliyorithiwa mfano spider road uk. 86, vidid dreams restaurant uk. 98.

Tamathali za semi

Ni neno au kifungu cha maneno yanayotumika kwa maana tofauti. Kinyume na maana ya kawaida ili kujenga picha au athari maalumu. Mwandishi Clara Momanyi katika riwaya yake ya Nakuruto ametumia tamathali za semi mfano;

Tashibiha, hutumika kufananisha kitu kimoja na kingine kwa kutumia maneno; kama, mithili ya au sawa. Mfano; alijitupa huko na huko kama gunia la viazi uk 1.

                      ……. Akawa anatetemeka kama unyasi ..uk 2

                   …..amening’ia hewani kama ndege………..

                   ………… kasi hewani mithili ya tai.

Tashihisi, ni usemi unaokipa sifa ya uhai kitu kisichokuwa na sifa ya uhai. Mfano ……….. maji yanapoibusu ardhi…uk71, …… mito ilipinda kwa maringo …. Uk 7.

Sitiari ni neno litumikilo kwa maana isiyo ile ya msingi au viumbe viwili  kufananishwa kwa kutumia sifa wanayoweza kuwa nayo. Mfano; wasipochukuwa tahadhari uzao wao utafyekwa mfano wa moshi katika upepo. Moyo ulimdunda kifuani utadhani ngoma. Uk 6.

Mubalagha ni tamathali ya semi inayotia chumvi kuhusu uwezo wa viumbe, tabia zao na kuhusu sifa zao kwa madhumuni ya kusisitiza au kuchekesha. Mfano; mito ilipinda na kupindana kwa maringo ikaelekea isikojua, Mara inaulizana njia….. Uk. 7.

Kejeli, hutarajia au kukusudiwa kutoa maana kinyume na ukweli ulivyo. Mfano; …. Ama kweli wewe ni kidomo ladha tu. Uk 70. Hamna habari Yule pale ni afisa mazingira uk 33.

MBINU NYINGINE ZA KISANAA.

Mdokezo, maneno hukatizwa bila kumalizia maneno yanayotakiwa kumaliziwa.

 Mfano; samahani Bi mkubwa lakini… uk 16.

              Ah! Wako wapi akina………… akina…… ha. Uk 24.

               ……….mtaweza kumwondoa huyu………huyo…. Uk. 42.

              Lakini………… uk 65.

Tanakali sauti ni mbinu ya kuiga sauti au milio mbalimbali.

 Mfano; …….cheche che uk. 12.

             ……kubobokwa bobobo uk. 70.

                  …. Nyeupe pe pe pe uk. 24.

                   ……inanguruma trrrrr…………..uk. 25.

Nahau na Misemo.

Ni semi fupifupi zinazotoa maana iliyojificha.

            Mfano; Dunia ni rangi rangile. Uk 37.

                         Mme wa jaha si raha uk. 129.

                         Heri ya mrama kuliko kuzama. Uk 27.

                         Utajiri ni umande uk. 74.

                         Maji ni uhai uk. 71.

                         Raha na furaha huishia karaha. Uk 78.

                         Mzoea tamu huhalalisha hamu uk. 79.

                         Hasara humfikia mwenye mabezo uk 35.

Methali.

Ni usemi unaowasilisha dhana mbili wenye dhima ya kufunza maadili.

Mfano; mzoea tamu huhalalisha haramu uk 74.

             Unataka nimwage mtama kwenye kuku wengi uk. 124.

Taswira.Ni picha zinazojitokeza baada ya matumizi mbalimbali ya semi na ishara. Kuna taswira za aina kadhaa, taswira za hisi, taswira za mawazo na taswira zinazoonekana.

Mfano; ……walielea juu …. Ndani ya mbawa zake uk. 100.

                 Mtaa umegeuka kuwa bahari. Uk 24.

                  ……watoto chini ya mbuyu uk 88.

                  …..harufu ya nta uk 129.

WAHUSIKA

Ni watu ama viumbe waliokusudiwa wawakilishe tabia za watu katika kazi za fasihi.

Mhusika mkuu.

Nakuruto, ni mhusika mkuu katika riwaya ya Nakuruto,  mwanamke jasiri na mwanamapinduzi, mwelimishaji na mhamasishaji kuhusu utunzaji wa mazingira, ni mvumilivu, mwandishi kama mhusika wa ajabu, ni mshauri mzuri, anafaa kuigwa.

Wahusika Wadogowadogo.

Nashelengai, ni mwanamke mkarimu, anahuruma, mpenda maendeleo, mke wa Kikuete wa Magonji, anamaadili ya kitamaduni, ni mama wa maridhia, anafaa kuigwa.

Kikuete, mume wa Nashelengai, kiongozi wa ujenzi wa ngazi ya kuisaka nta, mtetezi wa wanawake, aliongoza mkutano wa wanakijiji, anafaa kuigwa.

Nariangai, mwanamke mwenye mtoto mmoja, si mkarimu, ni mchoyo na asiye na huruma, ana roho mbaya, hafai kuigwa.

Ba Ludao, mvuvi wa samaki katika ziwa Ipe, mharibifu wa mazingira kwa kuelekezea mitaro ya maji shambani mwake.

Bi Cheusi, Bi Natesha, Binti fundi; ni wanawake, wachafuzi wa mazingira.

Bwana Brook, bwanyenye mmiliki wa shamba la pamba katika kijiji cha walatimbi, katili asiye na huruma, mnyonyaji na myanyasaji wa wanakijiji wa walatimbi.

Jumanne, kibaraka wa Bwana Brook.

Kishushe, mmoja wa wafanyakazi wa bwana Brook aliyemkimbiza paka na kumvua mkufu wa dhahabu.

Mfumwa, mwenyekiti wa kijiji cha maweni, mfuasi wa Wellingstone, anasomeshewa watoto wake nje ya nchi, kiongozi kibaraka, hafai kuigwa.

Mzee Saluda, mzee aishie kijiji cha maweni, alimwongoza Nakuruto kwa mwenyekiti wa kijiji (maweni)

Sheshije, mwanamke jasiri, alifanikiwa kupanda ngazi kuingia kwenye mchakato wa kuisaka nta, hakujali ushauri wa wanawake wenzie ili kuisaka nta.

Mkude, mwanakijiji wa latimbi, kachoshwa na unyanyasaji wa Bw. Brook, ni mfanyakazi wa Bw. Brook, mwenye familia duni kwa sababu ya kazi isiyo na manufaa, mpenda mapinduzi, alishiriki zoezi la kumuondoa Bw. Brook.

Wahusika Wengine ni Jumbe Khamisi, Jumbe Hemedi, Maridhia, Saitore, Mzee Menga, Bw. Mac mapeni, Bw. Quick buck, Lebon

KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI KATIKA RIWAYA YA NAKURUTO

Mwandishi Clara Momanyi amefaulu kimaudhui kwani amejadili dhamira mbalimbali ambazo zimesawiri maisha ya jamii na kuweza kuielimisha jamii kutoka hali duni na kuweza kujenga jamii mpya kwa kutoa mbinu za ujenzi wa jamii mpya kama vile  kupiga vita uongozi mbaya, kupiga vita uharibifu wa mazingira, kutoa elimu katika jamii, kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati, hizo ni baadhi ya mbinu za ujenzi wa jamii mpya kwani Clara Momanyi amejadili kwa kina ili kuweza kuikomboa jamii.

Pia mwandishi Clara Momanyi amejadili mambo mbalimbali yanayotoke katika jamii zetu kama vile suala la elimu, usaliti, uongozi mbaya, mila na desturi na uharibifu wa mazingira. Mwandishi ameonesha kukerwa na mambo kama hayo na kuona ni vema kuishauri jamii na kuyakemea maovu yaliyowapata na wakati ili kuachana nayo na kujenga jamii mpya.

Hivyo mwandishi amefaulu kwani ameweza kutoa suluhisho na mwanga kwa baadhi ya mambo yanayojitokeza katika jamii na kuyakemea kwa kuishauri jamii ili kujenga jamii mpya.

Dhamira zote alizozielezea kwani mambo yote haya yanatokea katika jamii zetu hivyo mwandishi ameweza kuyaweka bayana ili kuikomboa jamii yake kwani fasihi ni zao la jamii, mambo hayo ni kama vile elimu, uongozi, uharibifu wa mazingira, kundeleza mila na desturi zilizopitwa na wakati, usaliti na umoja na ushikirikiano. Hivyo Clara Momanyi ametoa nasaha zake kwa jamii ili kuachana na mambo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo ya jamii na kutoa suluhisho kwa baadhi ya mambo yanayotokea katika jamii.

Kufaulu kwa mwandishi kifani

Mwandishi Clara Momanyi amefanikiwa katika kazi yake na kuweza kumvutia msomaji kwa ujuzi wake wa uandishi kwani ametumia fani mbalimbali katika uandishi wake kama vile ametumia muundo wa moja kwa moja (msago) kufikisha ujumbe kwa jamii aliyokusudia.

Pia ametumia mtindo ambao ameweza kujenga visa na matukio kwa kutumia masimulizi, nyimbo, utenzi, hadithi, semi ili kuwasilisha  mawazo yake na kuweza kuitofautisha kazi yake na kazi nyingine za waandishi kwa kutumia nyimbo, masimulizi, utenzi, hadithi na matumizi mbalimbali kwa kutumia mbinu mbalimbali za lugha  na mbinu nyingine za lugha kama vile Takriri, tashibiha, tashititi na nyinginezo.

Suala la wahusika, mwandishi amefanikiwa kuwachora wahusika kwa sifa na tabia tofauti tofauti (wasifu wa ndani wanje) zinazofaa kuigwa au kutoigwa na jamii katika ujenzi wa jamii mpya pia amewachora wahusika katika sehemu mbili yaani mhusika mkuu na wahusika wadogo.

Pia suala la matumizi ya lugha mwandishi Clara Momanyi amefanikiwa kwa kutumia vipengele mbalimbali kama vile tamathali za semi, tashibiha, sitiari, mdokezo, takriri, tanakari sauti, hali iliyofanya kazi yake kuwa na mvuto kwa msomaji, hivyo wasomaji kuweza kuipenda kazi yake na kuisoma kwa umakini bila kuchoka, ili kuelewa nini Clara Momanyi amekusudia Kuidali jamii.

KUTOFAULU KWA MWANDISHI KIMAUDHUI

Mwandishi Clara Momanyi, hakufaulu kwa baadhi  ya vipengele vya maudhui mwandishi Clara Momanyi ameshindwa kutumia njia ya amani kudai haki matokeo yake amehamasisha jamii kufanya mgomo kudai haki kwa wachimba madini kwani mgomo sio suluhisho la kutatua matatizo yaliyomo katika jamii, maana migomo huwa inahariibu maendeleo ya jamii na baadhi ya watu hupoteza maisha kwa kupigania hak,i hivyo mwandishi Clara Momanyi hakufaulu kwani muhusika wake mkuu (Nakuruto) hakujihusisha  kwenye migomo na hakuwa anashiriki hivyo hakufanikiwa kwa kuweza kutoa kanuni na taratibu za kudai haki ilihali yeye alikuwa anafahamu madhara yake na ndio maana hakuwa anashiriki bali alikuwa anahamasisha migomo.

Clara Momanyi pia hakufanikiwa kwani amehamasisha uharibifu wa rasilimali, kama vile uchomaji wa kinu cha usindikaji pamba kiasi kwamba uchomaji na mbinu nyingine kama hiyo ni kurudisha maendeleo nyuma, hayo yote yamefanywa na Clara Momanyi kwa anahamasisha jamii yetu kuchoma baadhi ya viwanda vyetu hivyo ameshindwa kutoa suluhisho katika suala la kudai haki kwa jamii na sio kujichukulia maamuzi na kuchoma kinu cha usindikizaji wa pamba.

Suala la mwisho Clara ametuonyesha nchi yenye neema na utajili mwingi lakini ameshindwa kuonesha utaratibu mzuri wa kupata wasomi wa kusimamia rasilimali hizo, pia ameshindwa kutoa utaratibu wa kusimamia raslilimali hizo katika jamii zetu kwani mambo haya yalikuwapo hata katika nchi yetu lakini raisi wetu alizuia  na kusema mpaka pale watakapopatikana wasomi lakini Clara momanyi kashindwa kutoa suruhisho

Kifani, mwandishi Clara Momanyi ametumia uwasilishaji wa kazi yake kwa kutuimia mtindo wa kinjozi yaani akiwa usingizini, inakuwa nivigumu kwa msomaji kuielewa kazi kwa urahisi kwani kazi yake inakuwa kindoto zaidi.

MCHANGO WA MWANDISHI KWA WASANII NA WAANDISHI WACHAGA.

Mwandishi ametoa mchango mkubwa katika jamii kwani amekemea maovu yanayofanywa na watu wachache na kukandamiza jamii nzima kama vile; uongozi mbaya, mila potofu, swala la elimu, usaliti, uhalibifu wa mazingira na kutoa suluhisho la matatizo hayo ili kujenga jamii mpya na endelevu.

Mwandishi pia amtoa mchango kwa waandishi wachanga kuisoma jamii na kubaini matatizo na mahitaji yake ili waweze kuikomboa kupitia fasihi itakavyoandikiwa. Pia watakuwa na uhakika na mandhari watakayotumia katika uandishi chipukizi kwa kufuata taratibu mbalimbali za uandishi na kufikisha ujembe kwa hadhira.

Jina la kitabu,

Jina la kitabu Nakuruto linasadifu yaliyomo ndani ya kitabu kwani fasihi hii inamwelezea Nakuruto, mwanake mhamasishaji, kereketwa wa haki za binadamu na utunzaji wa mazingira. Nakuruto alisafiri maeneo mbalimbali huku akitoa ushauri akihamasisha jamii hatimaye kuleta ukombozi wa watu na mazingira katika vijiji tofauti alivyotembelea.

Jalada la kitabu

Jalada la kitabu linasadifu yaliyomo ndani limeonesha picha ya mwanamke ambaye ndie muhusika mkuu akiwa pangoni, pia picha ya ziwa ambalo linajadiliwa ndani ya riwaya (ziwa Nakuruto)