Uchawi katika Riwaya za Kiswahili

By , in Riwaya on . Tagged width:

Uchawi katika Riwaya za Kiswahili

A.J. Saffari

Utangulizi

Makala haya yanazungumzia nafasi ya uchawi katika riwaya za Kiswahili. Lakini kwa vile riwaya zote, japo ziwe za kubuni, zinakita mizizi na kupata uhai wake kutoka maisha halisi, suala linakuwa: Je, uchawi wenyewe ni kitu dhahiri au dhana tupu?

Waama nadharia na suala zima la uchawi limezungumziwa na kujadiliwa mwahala mwingi na watu wa kawaida tu mitaam, viongozi wa nchi pamoja na wanazuoni wa vipeo vya juu masomoni. Vitabu vya dini mbili kubwa duniani Kuruani2, yaani Msahafu, na Biblia3, vinazungumzia uchawi katika sehemu mbalimbali kadiri itakavyoonyeshwa baadaye. Nao Geofrey Parrinder4, Middleton5, Murray6, Michael7, Harwood8, Alastair Scobie9, Amold,10, Mary Douglas11 , kwa kutaja baadhi tu, wamejitoma katika mjadala kuhusu uchawi.

Makala baya yataanza na tafsiri ya uchawi, baadaye kujadili ushahidi mintaarafu ya uchawi, sababu zake, uchawi na utamaduni, pamoja na maendeleo.

Tafsiri ya Uchawi

Maana au tafsiri ya uchawi imezua utatanishi kama suala lenyewe la uchawi. Hivyo George Parrinder hajakosea anapodai kwamba ni masomo machache tu yamewakanganya watu kuliko uchawi.12 Kamusi, Encyclopaedia, na vitabu vya waandishi mbalimbali vimezidi kutatanisha maana ya uchawi. Vingi vinachanganya uchawi, wanga na uganga.

Kamusi ya Oxford inaanza kwa kudai kuwa mchawi (witch) ni mwanamke anayetumia madawa kwa madhumuni mabaya hasa miongoni mwa washenzi.13 Kwa upanae mwingine Kamusi ya Kiswahili Sanifu inaeleza kuwa uchawi ni ufundi wa kutumia dawa, aghalabu mitishamba na vitabu maalum vya uganga, ili kuleta madhara kwa viumbe, yaani sihiri. Baadaye kamusi hiyo inamwelezea mwanga kama mtu afanyaye mazingaombwe ya uchawi usiku, mtu achezaye ngoma ya mahepe.14

Ni dhahiri matatizo kadha yanajitokeza kutokana na maana au tafsiri zilizoelezwa hapo juu. Kwanza, ni kutoainishwa baina ya uchawi, wanga na madawa. Pili, madai kuwa mchawi ni mwanamke. Madai hayo yameungwa mkono na waandishi wengine kadhaa, bila ya ushahidi wowote. Na tatu, dai kuwa uchawi ni suala linalowahusu washenzi tu”. Maana yenyewe ya ushenzi haikuelezwa hapa, iwapo ni mtu ambaye hakustaarabika, yaani yuko nyuma kimaendeleo, au habithi wa matendo.

Katika mkanganyiko huo wa maana nastahabu ile inayodai kuwa uchawi ni ufundi, yaani utaalamu wa kutumia sio dawa tu, bali mbinu nyingine mbalimbali pamoja na vitabu maalum vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe. Bora kufafanua hapa kuwa hii ndiyo maana inayolingana na matumizi ya neno uchawi miongoni mwa watu wa Afrika. Lakini basi, kwamba taaluma au ufundi huu (uitwao uchawi) aghalabu huaminika na kutumika kuhasiri viumbe, haina maana kuwa hauwezi kutumiwa kwa manufaa.

Ushabidi Mintaarafu ya Uchawi

Leo hii watu wengi, nata wasomi, hawaelewi namna bomu la Neutron la Wamarekani linavyoweza kuua viumbe vyenye uhai na kuviacha visivyo na uhai bila ya athari yoyote. Hata hivyo kweli ni kuwa jambo kama hilo hutokea ingawa wanaojua kwa nini inakuwa hivyo ni wale wachache wenye taaluma hiyo. Wataalamu hao huishi chini ya ulinzi mkali kuliko marais wao na kuficha siri za utaalamu wao kama wafichavyo sehemu zao za siri. Basi ndivyo hivyo kwa elimu nyingi pamoja na uchawi wenyewe.

Baadhi ya waandishi, akiwemo George Parrinder, wanashikilia kuwa msingi wa uchawi ni imani tu. Ya kwamba imani hiyo ilianzia na kuzagaa Ulaya katika karae za kati. Hadi leo hii imani ya uchawi imelikumba Bara la Afrika na kusambaza hofu na vifo. Mwandishi huyo anaendelea kusema kuwa imani hiyo ya uchawi ilisababishwa na dhiki ya maisha. Kutokana na maradhi ya kuambukiza, uchafu na vifo vingi binadamu walitafuta sababu za maafa hayo. Walipozikosa au kutozijua, wakaanza kusingizia uchawi.15 Kama ambavyo itaelezwa baadaye, naafiki kuwa taaluma ya uchawi kwa maana ya kudhuru viumbe, imeshamiri zaidi katika jamii ambazo ziko nyuma kimaendeleo. Lakini wachawi sio masikini tu. Hata Mary Douglas anathibitisha kwamba matajiri wakubwa huko Uingereza na Ujerumani walitumia uchawi kuwaroga wenzao.16 La maana zaidi ni kuwa siafikiani na George Parrinder kuwa uchawi ni imani tu. Uchawi ni jambo la hakika wala sio dhanatupu.

Hapa sitathubutu kujinadi kujua kunga za uchawi kama vile ambavyo sijui namna bomu la atomiki linavyoua, japo linaua. Ila nitajitahidi kuthibitisha kuwa uchawi sio dhana wala imani tupu ya washenzi kama ambavyo George Parrinder na wenzake wanavyotaka tukubali.17

Je, ushahidi gani unadhihirisha kuwepo kwa taaluma ya uchawi?

Kwanza vitabu vya dini mbili kubwa duniani, yaani Korani na Biblia, vinazungumzia kwa ufasaha jambo hili. Aya ya 102, Surat l’Baqara18, inaeleza kuwepo kwa taaluma ya uchawi. Na katika tanbihi ya 105 ya Sura hiyohiyo Mungu anaelezea namna taaluma hiyo inavyoweza kutumiwa vizuri mikononi mwa watu ashrafu kama vile Hart na Marut, stadi wa taaluma hiyo walioishi Babylon awali hizo.19 Ikumbukwe kwamba katika siku hizo ayani Babylon ilivuma kuwa kitovu cha sayansi, hususan elimu ya nyota. Hata hivyo, hapohapo Mungu anaonya nanma ambavyo taaluma hiyo ya uchawi inavyoweza kutumiwa vibaya mikononi mwa mahabithi wenye ghera, choyo na tadi. Pamoja na yote hayo Mungu anasisitiza kuwa uwezo au taaluma hii ya uchawi ina ukomo; kwamba mchawi hawezi kutenda akafanikiwa kama Mungu hapendi. Yaani mchawi, japo awe fundi mangungu kiasi gani, hawezi akatumia uchawi kuroga au kuopoa akafanikiwa pasi Mungu kupenda. Kwa wale waumini wanaelewa fika kuwa kila kheri na shari humuelea Mungu.

Kuna hadithi moja iliyopokelewa enzi na enzi inayosimulia kwamba aliishi stadi mmoja wa taaluma ya uchawi kwa jina Maalim Kisisina. Hadithi inaeleza kuwa Maalim Kisisina alikuwa anabuni mipango ya kuzuia kudura za Mungu. Basi Mungu akamtuma malaika wake Jibrili kumfuata Maalim Kisisina na kumtaka undani wake. Jibrili alimwasilia Maalim Kisisina kwa umbo la mwanadamu. Kufika akamuomba amueleze aliko Jibrili kwa wakati ule. Basi Maalim Kisisina akapekua buku kubwa na taaluma ya uchawi na kumjibu kuwa kama Jibrili siye yeye mwenyewe Maalim Kisisina, basi Jibrili ni yule mtu aliye mbele yake, yaani Jibrili mwenyewe. Hadithi inasimulia kuwa mara hiyohiyo Jibrili akatumia wahyi ya Mungu kumpokonya Maalim Kisisina buku hilo la uchawi. Kufumba na kufumbua Jibrili alimpora Maalim Kisisina, naye kwa kutumia taaluma yake ya uchawi, akaapa kumuandama Jibrili. Kwa pamoja wakapaa juu na juu mbinguni hadi Mungu akamtumia tena wahyi Jibril kuwa achane karatasi moja la buku lile la taaluma na uchawi amtupie Maalim Kisisina. Jibrili alitii amri hiyo. Kuona kataa linaanguka kutoka mikononi mwa Jibrili, Maalim Kisisina akalidaka kataa hilo akiamini kuwa ni buku lake lote kumbe sivyo. Inadaiwa na hadithi hiyo kuwa taaluma yote ya uchawi duniani imo kwenye kataa lile moja alilotupiwa na kuachiwa Maalim Kisisina.

Hadithi ya Maalim Kisisina inasadikiwa na baadhi kuwa ya kweli. Lakini kama itazua ubishi bado kuwa ushahidi mwingine mwingi unaothibitisha taaluma ya uchawi. Tumeona maelezo ya Korani, sasa tuangalie Biblia.

Agano la Kale linaelezea miujiza baina ya Musa na wachawi wa Farao, namna ambavyo wachawi wa Farao walivyoweza kugeuza fimbo kuwa nyoka.20 Lakini hata hapa tunaelezwa kuwa Musa, kutokana na kubuli ya Mungu, aliweza kuitupa chini fimbo yake ikageuka joka kubwa lililowameza nyoka wote wa wale wachawi wa Farao.

Mnamo mwaka 1958 aliishi mpigania uhuru mmoja huko Tanga akiitwa Osale Otango kwa jina la utani. Waingereza waliamua kufanya msako mkubwa dhidi yake; na hatimaye kumkamata na kumpeleka Gereza la Maweni. Gereza hilo lilikuwa maarufu na humo ndani Osale aliwekwa kwenye chumba cha pekee akiwa ametatikwa pingu na minyororo ya mikono na miguu. Asubuhi iliyofuatia Mkuu wa Gereza, Mwingereza, alifika ofisini kwake mapema akakuta karatasi imeachwa juu ya meza yake imeandikwa: “Kwa heri, tutaonana. Osale Otango.” Upesi alikimbilia kule rumande na kukuta chumba salama lakini Osale Otango hayumo. Hakuna mtu aliyeiba funguo za rumande na wala hapakuweko sehemu iliyovunjwa katika rumande hiyo.

Tukio jingine lilitokea Mwanza mnamo miaka ya sabini. Tukio hili lilielezewa sana na magazeti yote ya Uhuru na Daily News. Mvulana mmoja alifariki ghafla, akazikwa. Siku nyingi kupita akapatikana hai, ingawa hakuwa na fahamu nzuri wala kuweza kuzungumza. Mvulana huyo alipelekwa Hospitali ya Bugando kwa uchunguzi zaidi.

Aidha kuna ikirari na maungamoya wachawi wenyewe. Kwa kawaida, na hata kwa mujibu wa sheria, ikirari 21 na maungamo22 ni ushahidi muhimu sana dhidi ya mtuhumiwa; madhali tu uwe umetolewa kwa hiari, bila vitisho wala ahadi za uongo. Waandishi wa vitabu kadhaa wanaelezea ikirari na maungamo haya ya wachawi. Geofrey Pamnder, kwa mfano, anaelezea kuwa wachawi huungama kukutana usiku kujadili masuala yao na kula nyama za watu ambao wamewaua kwa njia za uchawi.23 Wachawi hao hufanya mashindano kuonyeshana ujuzi na maajabu yao. Anazidi kuelezea kuwa wachawi wa Basuto hukiri kukutana usiku wakiwa uchi, hutumia madawa kuwafanya watu walale kisha huiba ng’ombe zao.24 Yafaa ikumbukwe hapa kuwa matendo hayo ya wizi wa ng’ombe kwa njia za uchawi yanafanyika mno Mwanza na Shinyanga. Wakati fulani yalifikia kiwango kikubwa cha kutisha, hata watu binafsi wenye mifugo yao wakaanza kuwasaka na kuwaua watu waliowadhania ni wachawi waliofanya madawa ya kuwaibia ng’ombe wao. Kesi maarufu ya Elias Kigandye25 ni ithibati ya kutosha. Itakumbukwa kuwa mauaji yaliyotokana na upelelezi wake si hiyo yalisababisha Mheshuniwa Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, ajiuzulu.

Mary Douglas naye anatoa mifano kadhaa ya maungamo ya wachawi Uingereza na Ujerumani. Anaelezea namna Malkia mmoja alivyokufa kwa miujiza huko Uingereza,26 na jinsi ambavyo watu mbalunbali, waume kwa wake, walivyokiri na kuungama mauaji katika miji mbalimbali ya Ujerumani ya Magharibi. Mmoja kati ya wachawi hao, Paul Camperle, mwenye umri wa miaka thelathini na tano, aliungama kuwa alianza uchawi tangia utoto wake alipofunzwa na nyanya yake. Tangu hapo alijinadi kuwa aliwaroga na kuwaua watoto mia moJa, na kuwalemaza au kuwafanya viwete matajiri kadhaa wajiji la Munich.27 Mkewe, Anne Camperle, naye aliungama kuua watoto mia na watu wazima kumi na tisa. Aidha alijitapa kumshakizia mke wa mtu mmoja kujichoma ndani ya jiko hadi kuiva. Mumewe naye akamfuatia. Akajitapa zaidi kuua idai kubwa ya ng’ombe wa watu.28 Mwanae Simon Camperle naye aliungama kuuwa watoto kumi na sita, watu wazima sita, pamoja na kuwalemaza wengine au kuwafanya viwete.29

Mtu mwingine Olrich Schelltibann, umri miaka themanini, alijifaragua kuua watoto arobaini, watu wazima thelathini, na kuwalemaza au kuwafanya wengine viwete.30 George Smeltes naye aliungama kuua watoto thelathini na sita, watu wazima kumi na tano, na kuwalemaza au kuwafanya wengine viwete.31 Maungamo hayo yanasemekana yalifanywa kwa hiari mbele ya Gavana wa Jiji la Munich. Baadaye wachawi hao walichomwa moto hadi kufa.32

Wachilia mbali maungamo hayo ya vitabuni, ushahidi uko katika sehemu mbalimbali hapa Tanzania wa wachawi kuungama kuwaua watu kwa kutumia uchawi. Wachawi hao, mathalan, wamewahi kuungama mbele ya Tekelo, Dar es Salaam; Kabwere, Tanga; na Mandondo, Korogwe. Tekelo, Kabwere na Mandondo ni waganga maarufu ambao waliweza kuwafichua wachawi katika sehemu hizo. Licha ya kuungama tu, baadhi ya wachawi hao walijitokeza na mafuvu ya vichwa, mifupa ya wafu na hata makoba yao ya uchawi na vyungu vya kupikia nyama za wafu. Wengine walidiriki hata kuelezea namna walivyogawana na kufaidi nyama ya mtu fulani.

Sababu za Uchawi

Kila kitu kina nia na madhumuni yake. Uchawi nao, kwa maana hii yake mbaya ya madhara, una sababu zake kuu zifuatazo. Kwanza ni sababu ya kiuchumi. Katika jitihada ya kupata, mathalani mifugo, kama ambavyo imeelezwa awali wachawi hutumia uchawi kuswaga ng’ombe wa wenzao. Au, ili kupata mavuno mengi, wachawi huhitaji huduma ya watu wengi mithili ya watumwa. Hivyo hutumia mbinu za kuwafanya watu waonekane wafu, kumbe wazima, kisha huwatumikisha kulima mashamba na kuyahudumia. Aina hii ya uchawi ni maarufu kote Afrika, na hapa Tanzania hujulikana kwa majina mbalimbali. Mathalan huko sehemu za Kusini, kama vile za Lindi, huitwa ndondocha. Sehemu za Mwanza na Shinyanga huitwa mitumba. Tanga huitwa msukure. Na kwajumla neno kizuu lina maana ya mtu ambaye anafungwa na kutumikishwa baada ya watu kumzika wakidhani amefariki.33

Alistaire Scobie anaelezea mauaji ya kutisha huko Basuto, yaani Botswana, kwa minajili ya kupata mali.34 Mtu mzima hukamatwa usiku na kukatwa viungo mbalimbali huku yu hai. Viungo hivyo kama vile macho, maini, huchanganywa na vitu vingine na kutumiwa kama dawa ya mavuno makubwa. Ayi Kweyi Annah pia anaelezea mauaji ya aina hiyo katika Nigeria.35

Mauaji kama hayo pia yako sehemu nyingi hapa Tanzania kwa nia ileile ya kutafuta mali. Kwa mfano, mara nyingi watu hukutwa wameuawa na kukatwa sehemu za siri. Baadhi ya wakazi wa Nyanda za Juu huamini kuwa sehemu hizo zinavutia utajiri wa biashara.36

Sababu nyingine mbili hukaribiana mno na hii ya kwanza, nazo ni sifa na uwezo. Kwa mfano, baadhi ya viungo vya mwanadamu vikikatwa yungali hai, kama vile maini na moyo, hutumiwa kumpa mchawi au yeyote anayekusudia uwezo, sifa na ujasiri. Vijiji vingi Afrika vina baadhi ya watu, waganga ambao hutisha na kuogopesha kutokana na sifa, uwezo na utajiri wao utokanao na uchawi.

Sababu ya mwisho ni kustarehe. Wachawi wanatumia taaluma hiyo kufanya ufidhuli wa kuchezea watu usiku, kama vile kuwapanda, kuonyeshana miujiza, kucheza uchi, kula nyama za watu waliowaua, n.k. Zaidi ya yote wachawi hutumia taaluma hiyo kuwapora watu wake zao, ikibidi hata kwa kuwaua waume zao kwanza.

Uchawi na Utamaduni

Matendo yote ya mwanadamu hutokana na mfumo wa kuzalisha mali na mahusiano ya uzalishaji mali yenyewe katika jamii inayohusika. Taaluma mbalimbali hubuniwa kwanza kwa kukidhi haja ya jamii inayohusika. Uchawi nao ni hivyohivyo.

Awali niliafikiana na hoja ya Parrinder kuwa mara nyingi uchawi hustawi kwenye umaskini kwa sababu aghalabu umaskini hutokana na zana duni za kuzalisha mali. (Sitazungumzia mahusiano ya uzalishaji mali.) Badala ya kutumia matrekta au majembe ya ng’ombe watu wa sehemu nyingi za dunia, hasa Afrika, hutumia viserema. Ukulima wa kiserema ni wa tonge domoni tu, basi. Anayetaka kupata mazao mengi hana budi apate watu wengi wamlimie. Na watu hao wataka kulipwa. Kulipa nako kunapunguza faida. Jambo moja la kufanya ni kupata watumwa. Lakini utumwa mkongwe hauko siku hizi. Na utumwa mamboleo nao unahitaji kiasi fulani cha ijara, sio bure. Hivyo la kufanya ni kuweza kupata watumwa kwa namna nyingine. Hapa ndipo taaluma ya uchawi kama vile ndondocha, mizuka, msukure, na kadhalika hutumika. Vizuu ni watumwa bora zaidi maana hawawezi kugoma’wala kujadili vitu vizuri. Kama asemavyo Dk. Emmanuel Mbogo, wao hulishwa kinyeke na kuridhika.37

Riwaya ya Mirathi ya Hatari inaelezea mkasa uliokitikisa kijiji cha Kitelevadzi na kuashiria mfarakano mkubwa.38 Kisa ni kuwa Mzee Kasembe alikuwa anagombania shamba la watu wengine wawili, yaani Kipedzile na Malipula.39 Ili kujipatia shamba hilo kulihali, Malipula, kwa kutumia radi, aliteketeza familia yote ya Mzee Kasembe isipokuwa Gusto ambaye hakuwa nyumbani.

Kadiri nyenzo za uzalishaji mali zinavyoimarika ndivyo taaluma ya uchawi kwa minajili ya kudhuru kwanza ili kujinufaisha inavyopotea.

Uchawi na Maendeleo

Baada ya mjadala wote uliotangulia suala linabakia: nini nafasi ya uchawi katika maendeleo ya Watanzania na riwaya zao za Kiswahili.

Kwa bahati mbaya, kwa mujibu wa ushahidi uliopo – kama ilivyoonyeshwa katika makala haya – taaluma ya uchawi imetumika zaidi kuibananga badala ya kuiendeleza jamii. Kutokana na taaluma ya uchawi inabidi kwanza mchawi adhuru ili ajinufaishe binafsi. Zaidi ya yote elimu hiyo yote ni kunga inayohifadhiwa kwa misingi ya ubinafsi dhidi ya maendeleo ya jamii kwa jumla.

Kwa kuwa, basi, kazi za sanaa kama vile riwaya hupata taswira yake kutokana na jamii inayohusika, riwaya za Kiswahili mintaarafu ya taaluma hii ya uchawi nazo zimeelezea uovu wa uchawi na hata kulaani kwamba inapasa utokomelee mbali.40

Riwaya Fadhili Msiri wa Naugua inaelezea uadui unaozuka baina ya nchi ya Naugua na Ramali. Katika hadithi hii kijana Kadi alitoka kwao Ramali nchi ya Wachawi, kwenda Naugua. Huko alimpenda mwali mmoja Mwanagele na kutaka kumuoa. Lakini kutokana na mila ya Naugua ilibidi kwanza amgombanie na kijana mwingine Fadhili, ili kupata ushindi wa kumuoa. Katika mashindano hayo Kadi alipigwa na kuumia. Watu wa Ramali wakaja juu na kutaka kuiangamiza Naugua kwa sihiri. Kwa bahati nzuri waganga – Mzee Jala na Bi Kizee Mkunyambi kutoka nchi ya Tiba – walizuia azma ya Waramali kumuua Fadhili, Mwanagele na kuteketeza familia nyingi za Wanaugua.

Mirathi ya Hatari42 nayo inaonyesha namna taaluma ya uchawi ilivyotumiwa kuteketeza watu kwa minajili ya ubinafsi wa mtu au watu wachache.

Lakini, kama ilivyodaiwa awali matumizi mabaya ya taaluma hayafanyi taaluma hiyo nayo kuwa mbaya. Hivyo katika Mirathi ya Hatari Mzee Kazembe aliukumbatia mkono wa mwanawe Gusto na kumuusia:

“Mwanangu, nakuachia kazi kubwa. Ni urithi mkubwa ukiutumia vyema; bali pia ni mirathi ya hatari usipojihadhari nayo.”43 Na hata baadaye wakati Gusto alipokuwa anatawazwa kuwa mchawi usiku kule pangoni, Mzee Mavenge, mmojawapo wa wachawi, alimsisitizia Gusto: “Kama nilivyokueleza yote hii ni elimu ya pekee. Ukufahamu na kuitumia vizuri unaweza kuumiliki ulimwengu. Ni siku hizi tu Wazungu wamekuja na elimu yao ya uongo na kweli wakawapotosha vijana wetu”.44 Kama hoja ni matumizi mabaya Mzee Mavenge alisema: “Hebu sikiliza jinsi wanavyouana! Hebu angalia mavyombo yao ya kivita! Nayo vile utasema yanasaidia kuinua hali ya binadamu!”45

Mijadala hiyo michache katika Mirathiya Hatari inapanua mawazo kuwa hakika taaluma ya uchawi ina sura mbili: ya wema, na ya uovu. Wengi wetu tunaiona ile sura ya uovu tu. Na kwa hivyo waandishi nao wameangukia katika upofu huo. Hili ni kosa kubwa kwa vile linapingana na kweli. Je, sio kweli kwamba kweli itashinda namna tunavyoishi!46

Sifa moja adhimu kwa mwandishi, na hasa msanii wa riwaya na tungo nyingine, ni kuheshimu kweli. Wakati mwingine hana budi kuitafiti na kujua kweli imesimamia wapi maana daima kuna watu ambao kazi yao ni kuipotosha na kuificha kweli.

Taaluma ya uchawi imejificha, dhahiri, lakini imepotoshwa ama kutokana na ukufi wa elimu au kwa kusudi. Kazi ya waandishi ni kutandua utandabui huu hasidi.

Hitimisho

Hoja inatolewa hapa kuiangalia vizuri sura ya pili ya taaluma ya uchawi ili kuutumia kwa maendeleo na hata ulinzi. Kwa mfano, wachawi wanaweza kuruka na kusafiri mbali kwa muda mfupi tena bila ya kuonekana. Wanaweza wakapenya ndani ya nyumba bila ya kuibomoa na kuwataa watu usingiri mzito kwa muda mrefu.47 Wanaweza wakafanya mengi mengine ya manufaa.

Basi nini wajibu wa waandishi wa riwaya katika suala hili la kuitumia taaluma ya uchawi kwa maendeleo?

Kwanza kabisa narejea katika hoja yangu ya awali kuwa moja ya sababu kubwa ya taaluma ya uchawi kutumika vibaya au kwa ubinafsi ni kutokana na kuwa na zana duni za uzalishaji mali, yaani umaskini. Kadiri maendeleo yatakavyoongezeka ndivyo matumizi ya madhara ya uchawi yatakavyopungua. Hata hivyo uchawi unaweza ukaendelea kutumika kwa madhara kwa muda mrefu kutokana na udhaifu wa wanadamu kutapia mali, uwezo, hata anasa tu, pamoja na wivu. Mchawi anaweza kuwa tajiri lakini akaamua kumuua tajiri mwenzake ili aondoe upinzani naye katika biashara.

Iwapo ni hivyo, nini wajibu wa waandishi wa riwaya katika kipindi hiki cha mapito? Ni vigumu kutoa jibu la mkato kwa sababu ileile niliyoigusia awali: kuwa kazi yoyote ya sanaa hupata taswira yake kutokana na jamii inayohusika. Hivyo kadiri uchawi unavyotumika zaidi kwa uovu ndivyo itakuwa muhali kwa waandishi kuuenzi kwa njia ya maendeleo.

Hata hivyo badala ya kuulaani tu uchawi utokomezwe kulihali, waandishi wanaweza kufanya mambo mawili makubwa: kwanza, kuwahamasisha wenye taaluma ya uchawi waifundishe pasi na kificho. Pili, waitumie kwa nia ya maendeleo kama anayoonyesha Ibrahim Hussein katika Kinjeketile48 ambapo wazalendo wa Tanganyika waliazimia kuitumia taaluma ya uchaw kupigana na wakoloni wa Kijerumani.

Tanhihi

1. Hivi karibuni viongozi wa ngazi za juu kabisa hapa nchini wamedai kuwa uchawi ni imani isiyo na msingi.

2. Yusuf, A.A. (1983) The Holy Quran. Translation and Commentary. Al Rajhi Co., Maryland.

3. Agano la Kale, (1980) T.M.P., Tabora.

4. G. Parrinder, Witchcraft, European and African. Faber and Faber, London.

5. J. Middleton, (1963) Witchcraft and Sorcery in East Africa. Praegar, New York.

6. A. Murray, (1963) The Witchcraft ni West Europe, Clarendon Press, Oxford.

7. G. Michael, (1967) The African Witch. London.

8. A. Harwood, (1970) Witchcraft, Sorcery and Social Categories Among the Wasafwa, Orford.

9. A. Scobie, (1965) Murderfor Magic. Cassel, London.

10. E. Arnold, Witchcraft. London, 1969.

11. M. Douglas, (1970) Witchcraft: Confessions and Accusations, Tavistock Publications, London.

12. Parrinder, (m.y.k.) uk. 10

13. A.S. Homby, (1924) Oxford Advanced Learners Dictionary of Current English. Oxford University Press, Oxford, uk. 131.

14. TUKI (1981) Kamusiya Kiswahili Sanifu. Oxford, Dar es Salaam.

15. Parrinder, (m.y.k.) uk. 9. Makabila ya nchi mbalimbali za Afrika yanatajwa kuhusiana na imani hiyo ya uchawi, nayo ni pamoja na Basuto wa Basutoland, siku hizi Botswana, Lorendu wa Afrika Kusini, Yombo na Ibo wa Nigeria, na Azande wa Sudan.

16. k.h.j., 114.

17. Douglas, (m.y.k.) uk. 35. Mfano unaotolewa hapa ni wa tajiri mmoja aliyeitwa Nutters aliyeishi Lancashire, Uingereza, mnamo 1622.

18. Parrinder, (m.y.k.) uk. 9.

19. A.A. Yusuf, (m.y.k.).

20. k.h.j. uk. 45.

21. Agano la Kale, (m.y.k.) uk. 803.

22. Tanzania (1962) Fungu la 19, Sheria ya Ushahidi, Na. 6.

23. Fungu la 27 k.h.j.

24. Pamnder, (m.y.k.), uk. 143.

25. k.h.j., uk. 145.

26. Tanzania (1981) Elias Kigadye na Wenzake, Shauri la Jinai la Rufani Na. 41,1981, Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Dar es Salaam.

27. Douglas, (m.y.k.) uk. 305.

28. k.h.j. uk. 318.

29. k.h.i. uk. 318.

30. k.h.j. uk. 319.

31. k.h.i. uk. 320.

32. k.hJ. uk. 320.

33. TUKI (m.y.k.), uk. 131. Kizuu ni mtu aliyefunikwa kwa mazingaombwe ili kutumika nyumbani kwa uchawi; kijumbe cha uchawi.

34. A. Scobie, (1965) Murder for Magic. Cassel, London, uk. 96.

35. A.K. Armah, (1984) The Healers. Heinemann, Logos.

36. Wakati mwingine watu hutumwa kutafuta sehemu hizo za siri au viungo vya mwanadamu na kuviuza kwa anayevihitaji.

37. E. Mbogo, (1986) “Ngoma ya Mwanamalundi” (Muswada), Dar es Salaam.

38. C.G.M. Mung’ong’o (1977) Mirathi ya Hatari. TPH., Dar es Salaam, uk. 2.

39. k.h.j., uk. 2.

40. k.h.j., uk. 26.

41. A. Kondo, (1975) Fadhili Msiri wa Naugua. TPH, Dar es Salaam.

42. Mung’ong’o, (m.y.k.).

43. k.h.j., uk. 16.

44. k.h.j., uk. 25.

45. k.h.j., uk. 26.

46. S. Robert, (19/65) Masomo Yenye Adili. Nelson, Nairobi.

47. Watu kadha wa kadha, pamoja na viongozi wengine wa nchi hii, wamewahi kujikuta wametolewa nje wakati wa usiku bila ya kujijua, wengine wakiwa uchi wa nyama.

48. E. Hussein, (1969) Kinjeketile. Oxford University Press, Dar es Salaam.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!