UCHAPISHAJI NA UCHAPAJI

By , in Kavazi on . Tagged width:

Uchapishaji na Uchapaji

L.M. Thonya
1. Dhana ya Uchapishaji na Uchapaji
Tofauti ya maana baina ya majina haya mawili ya Kiswahili huwatatanisha wananchi wengi ambao teknolojia ya shughuli hizi za uchapishaji (publishing) na uchapaji (printing)ni ngeni kwao. Basi, tafsiri iliyo nyepesi ni kwamba ‘uchapishaji’ ni utaratibu mzima wa kuandaa kitabu au chapisho kuanzia hatua ya muswada hadi hatua ya kulitangaza na kulisambaza chapisho hilo. ‘Uchapaji’ ni ufundi wa kupiga chapa na kutengeneza kitabu au gazeti liwe tayari kwa kuuzwa. Mathalani, mchapishaji ni kama mrasimu ambaye huchora ramani ya nyumba na kusimamia ujenzi wake; na mchapaji ni kama fundi mwashi ambaye huaka jengo la nyumba hiyo akifuatisha ramani iliyochorwa na mrasimu huyo.
2. Historia Fupi ya Uchapishaji na Uchapaji Tanzania
Teknolojia hii muhimu sana kwa maendeleo ya taifa lolote haikwenda sambamba na teknolojia za fani nyingine za elimu nchini Tanzania. Kabla ya kujitawala, Tanganyika (Tanzania) ilikuwa soko tu la kuuzia vitabu karibu vyote vilivyokuwa vikitumika nchini kutoka nchi za nje. Isipokuwa baadhi ya wamisionari walichapisha na kupiga chapa vitabu na magazeti ya kuenezea dini za madhehebu yao. Serikali ya wakati huo ilichapisha na kupiga chapa gazeti la serikali, hati na nyaraka mbalimbali za serikali; na ikaruhusu gazeti la Mamboleo lichapishwe nchini ili kuimarisha mfumo wa utawala wao. Hata hivyo, shughuli za kitaalamu za uchapishaji na uchapaji zilikuwa zikiendeshwa na wageni. Wazalendo walielekezwa tu kwa vitendo vya kikasuku kufanya kazi mbalimbali viwandani na ofisini bila ya kupatiwa mafunzo ya nadharia ya undani wa teknolojia yenyewe.
Baada ya kujitawala, na hasa baada ya serikali kutaifisha njia kuu za uchumi, kikiwemo kiwanda kikubwa cha Printpak, ndipo uchapishaji na uchapaji ukaanza kupata sura na msukumo mpya kwani uongozi wa ngazi za juu uliwekwa mikononi mwa wananchi, na wazalendo wakaanza kupatiwa mafunzo ya undani wa teknolojia ya uchapaji na uchapishaji hapa nchini na nchi za ng’ambo kuhusu fani mbalimbali.
Serikali yabidi ipongezwe kwa hatua muhimu ya msingi iliyochukua, hasa kwa kuanzisha kiwanda maarufu cha kutengeneza karatasi nchini huko Mufindi kwa ajili ya kuchapishia vitabu, daftari, magazeti na bidhaa nyingine zitokanazo na karatasi. Jiwe la msingi wa maendeleo ya uchapishaji na uchapaji limesimikwa, kinachotakiwa sasa ni kujenga na kulitumia jengo hilo kwa ufanisi zaidi.
3. Sera ya Uchapishaji na Uchapaji Tanzania
Uchapishaji na uchapaji katika Tanzania haujapatiwa sera maalumu. Mashirika yanayohusika na shughuli hizo hujiendeshea shughuli zao kadiri yanavyoamua yenyewe ilimradi tu yamejipatia leseni rasmi na serikali kwa mujibu wa sheria za nchi. Basi, kukosekana kwa sera hiyo kumesababisha matatizo mengi na malalamiko ya kweli kwa makundi yote yanayohusika na huduma hizo na kwa wananchi kwa jumla.
Mathalani, baadhi ya mashirika ya uchapishaji na uchapaji hujipangia bei kiholela kama yanawoamua yenyewe bila ya kufuata viwango vya kimataifa. Viwango vya ubora wa bidhaa zitokanazo na karatasi havizingatiwi ipasavyo. Hakuna vyombo vilivyoundwa ili kukuza na kusimamia maendeleo na msimamo wa shughuli zao kama ilivyo katika nchi nyingine; vyombo kama vile vyama vya waandishi, wachapishaji, wachapaji, wauzaji vitabu, na wauzaji wa bidhaa nyingine zitokanazo na karatasi.
Matokeo yake ni kwamba bei zisizoaminika hutumika na kuwaumiza sana wanunuzi. Vilevile kupindukia kwa kupanda bei ya karatasi kunakoendelea kila baada ya kipindi kifupi kunachangia kwa kiasi kikubwa katika kupanda kwa bei ya kutisha ya bidhaa hizo zitokanazo na karatasi. Viwango vya ubora wa bidhaa hizo navyo vimeshuka sana. Aghalabu vitabu na magazeti mengine yanayochapishwa hayasomeki vizuri kutokana na uzembe wa wapiga chapa unaosababisha uchafu wa maandishi unaokithiri. Papo hapo umezuka mtindo wa kutupiana lawama; kila kundi kulilaumu kundi jingine kwa visingizio ambavyo vimo chini ya uwezo wetu – ilimradi mambo yanazidi kuzorota. Kwa hiyo wakati umefika sasa wa kuomba serikali kuingilia kati ili kuliokoa jahazi lisizame. Dawa mojawapo muhimu ya kutibu maradhi haya ni kwa serikali kutoa ‘sera’ maalumu ya uchapishaji, uchapaji, ununuzi na uuzaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na karatasi.
4. Sheria ya Kuhifadhi Kazi za Sanaa
Tanzania Bara inayo sheria rasmi inayohusu “Haki ya Kumiliki Kazi za Sanaa” kama vile maandishi, michoro, picha, sanamu (vinyago), filamu, kanda za muziki, na kazi nyinginezo za sanaa.
Sheria hiyo ya Haki ya Kumiliki Kazi za Sanaa ilitungwa tarehe 29 Desemba, 1966, na ilianza kutumika mwaka 1967. Sheria hiyo inaitwa Tanganyika Copyright Act No. 61 of 1966. Ni sheria inayohusu Tanzania Bara tu. Hadi sasa sheria hiyo haijafanyiwa mabadiliko.
Hapo awali, kabla ya sheria hiyo kutungwa, ilikuwa ikitumika sheria ya Kiingereza ya mwaka 1911 iliyohusu “Haki ya Kumiliki Kazi za Sanaa.”
Sheria ya “Haki ya Kumiliki Kazi za Sanaa” inasimamiwa na Wizara ya Sheria. Sheria hiyo inaheshimu pia mikataba ya kisheria ya kimataifa kuhusu Haki ya Kumiliki Kazi za Sanaa.1
5. Hali Halisi ya Uchapishaji na Uchapaji Nchini
Licha ya hali ngumu iliyolikumba taifa letu, siku hizi yamezuka mashirika mengi ya uchapishaji na ya uchapaji ya uani, pia maduka ya vitabu na ya bidhaa nyingine zitokanazo na karatasi; ilimradi yamefanikiwa kujipatia leseni za serikali kuhalalisha shughuli hizo.
Baadhi ya waendeshaji wa shughuli hizo hawana utaalamu wa teknolojia inayohitajiwa; wala wengi wao hawazingatii ubora wa viwango na maadili ya kazi yanayowapasa. Wanachojali wao ni kutumia hali hii ngumu ya uchumi ili kujinufaisha na kujipatia utajiri wa harakaharaka.
Ifahamike dhahiri kwamba uchapishaji na uchapaji ni teknolojia ya hali ya juu sana kwa kiwango kilichofikiwa leo ulimwenguni. Kwa hiyo hata nchi yetu yapasa kuizingatia kwa makini mintarafu ya kuthibiti ubora wa viwango vya kimataifa na maadili katika kuendesha shughuli zetu. Tena, uchapishaji na uchapaji una fani mbalimbali na kila fani inahitaji mafunzo mahsusi ili kuwezesha kuchapisha vitabu, magazeti, na bidhaa nyingine zitokanazo na karatasi kwa kiwango cha ufanisi kinachokubalika kimataifa. Mathalani, siku hizi ni jambo la kawaida kabisa kuona maandishi yenye wino hafifu au kutosomeka kabisa; makosa ya kuendeleza maneno au matumizi yasiyo sahihi ya lugha; uchafu wa maandishi, michoro oa picha zisizoridhiaha; uhafifu wa majalada ya vitabu; mchanganyo mbaya wa rangi, n.k. Katokana na athari kama hizo, mnunuzi wa bidhaa hizo hanufaiki kullingana aa thamani ya fedha anyotoa kulipia bidhaa hizo anazonunua.
Kwa hiyo, kuna haja sasa kuanza kuyachukulia hatua masuala naya ili kuyarekebisha Hatua mojawapo iliyo muhimu ni kuweka na kuziagatia viwango vya ubora wa bidhaa hizo vinavyotakiwa; na kuwe na chombo maalumu kilichoteuliwa rasmi kusimamia utekelezaji wake. Pia kuanzishwe taasisi mahsusi za mafunzo ya taaluma ya uchapishaji, uchapaji na uuzaji wa vitabu hata kufikia ngazi ya stashahada na shahada kamili kama inavyofanyika katika nchi nyingine.
6. Soko la Wachapishaji na Wachapaji Nchini
Ni ukweli usiokanika kwamba shabaha kuu ya kuanzisha biashara yoyote ni kuwania kupata faida. Hata hivyo, sharti kuwe na viwango vya faida hiyo kulingana na asilimia inayokubalika kimataifa. Mathalani, baada ya kuhesabu gharama halisi, faida iwe baina ya asilimia 20 – 30; kamwe isipindukie asilimia 50. Jambo hili linawezekana tu iwapo, mosi, mahesabu ya kweli yatafanywa na mtaalamu wa kukadiria gharama hizo (costing expert); pili, mhasibu mzoefu atatengeneza hati ya uwiano wa mapato na matumizi ya mwaka mzima wa fedha ya shirika linalohusika (annual cashflow); na tatu, vipimo vya kazi kwa kila mfanyakazi vitawiana kwa ngazi zote na kila mmoja atawajibika ipasavyo.
Uwiano huo ukizingatiwa, basi lengo lililopangwa litafikiwa na bidhaa zitapatikana kwa kiasi cha kutosha na kwa bei nafuu. Kutokana na ukweli huu ni kwamba bei kubwa za kukithiri za siku hizi hutokana na kuongeza faida kubwa mno hata kufikia asilimia 200 na zaidi ili kufidia hasara inayotokana na uzembe, uvivu, kuajiri wafanyakazi wengi mno bila kuzingatia vipimo vya kazi zinazofanyika, na makisio yasiyo ya kitaalamu.
Jambo lingine linaloharibu soko la uchapishaji na uchapaji ni kupuuzwa kwa mashindano ya kibiashara (trade liberalisation), na kuendelezwa kwa biashara ya kuhodhi ftrade monopoly). Matokeo yake ni waandishi wa miswada ya vitabu kupigwa chenga na wachapishaji wachache walio na uwezo. Nao wachapishaji hupigwa chenga na wachapaji. Mnyororo huendelea kwa wauzaji vitabu na bidhaa nyingme zitokanazo na karatasi kupewa ahadi tupu ya “nioo kesho utapata,” kutoka kwa wachapishaji. Hivyo, shule na wananchi kwa jumla hushindwa kupata vitabu na bidhaa hizo muhimu kutoka kwenve maduka yaliyo karibn nao wanapozihitaji. Basi, mzunguko huu wa hali mbaya husababisha bidhaa hizo kuadimika, kuwa na bei za kukatisha tamaa au kukosekana kabisa. Matokeo yake ni kushuka kwa elimu shuleni na kukwama kwa juhudi za kupata maendeleo mbalimbali. Kwa hiyo, ili kudumisha soko huria na la bei nafuu, sharti kutibu maradhi yaliyodokezwa katika makala haya kabla hali hii mbaya haijapindukia upeo.
7. Uchapishaji, Uchapaji na Kiwanda cha Karatasi Nchini
Kama ilivyodokezwa katika vifungu vilivyotangulia, yapasa kuipongeza serikali kwa kuanzisha kiwanda maarufu cha karatasi nchini. Kuzinduliwa kwa kiwanda hicho kulileta matumaini makubwa kwa wananchi kwamba kingeleta ukombozi wa matatizo ya uchapishaji na kutuwezesha kupiga hatua mbele ya kujitegemea kitaifa. Wananchi walitumaini sana bidhaa zinazotokana na karatasi zingalipatikana kwa bei nafuu zaidi. Kumbe, sasa tunaona kinyume chake. Mathalani bei ya karatasi iliyoingizwa kutoka nchi za nje kwa shilingi 10 kwa kilo mwaka 1985 sasa (1987) inatengenezwa na kuuzwa hapa kwa bei inayofikia shilingi 80 kwa kilo!
Inafahamika dhahiri kwamba kupanda huko kwa bei kumetokana pia na kupungua kwa thamani ya fedha yetu kwa sababu ya kuanguka kwa uchumi wa nchi. Hata hivyo, kuna ushahidi kutokana na vyombo vya habari kwamba kukomoana kunakofanyika mathalani baina ya shirika la umeme na kiwanda hicho, huchangia katika upandaji wa bei ya karatasi. Athari za upandaji wa bei ni kwamba:

– Bei ya karatasi ikipanda, bei za uchapaji pia hupanda.
– Bei ya uchapaji ikipanda, bei za uchapishaji nazo hupanda.
– Bei za wachapishaji zikipanda, bei za wauzaji pia hupanda.
– Bei za wauzaji zikipanda, wanunuzi wa bidhaa hizo hukata tamaa.

Matokeo ya mzunguko huo wa hali mbaya ni kukwama kwa maendeleo ya uchapishaji, uchapaji, na uuzaji wa bidhaa hizo. Aidha, kupatikana kwake huwa ni kwa shida. Kwa hiyo vyombo vinavyohusika vinashauriwa kuiomba serikali kuingilia kati kurekebisha hali hiyo ili karatasi zinazotengenezwa nchini ziwe na bei nafuu kwa maendeleo ya elimu shuleni na matumizi mengine muhimu ya wananchi kwa jumla.
8. Viwanda Muhimu vya Uchapaji Nchini
Katika nchi yetu kuna viwanda vyenye uwezo mkubwa vinne ambavyo huendeshwa na mashirika ya umma. Kuna Printpak na NPC ambavyo huchapisha vitabu na magazeti; kiwanda maarufu cha Kibo Paper ambacho hutengeneza na kuchapisha makasha ya kufungia bidhaa mbalimbali, na kiwanda cha kutengenezea daftari cha TES. Viwanda hivi vikubwa vina jukumu kubwa sana la kutoa huduma kwa taifa. Kutokana na jukumu kubwa hilo huwa vina nafasi fmyu ya kuhudumia mashirika mengine ya wachapishaji au watu binafsi. Hivyo, kuna haja ya kuongeza au kuvikuza baadhi ya viwanda vingine vya uchapaji nchini ili kutosheleza mahitaji ya wachapishaji.
Kwa kweli kunahitajika nyongeza zaidi ya viwanda vikubwa kama hivyo ambavyo vitatumika maalumu kwa ajili ya uchapaji wa vitabu. Viwanda hivyo yapasa vizingatie kutoa bidhaa za viwango vya hali yajuu (guality printing). Mfano wa viwanda vya aina hiyo vinavyoweza kukuzwa ni kile cha Tanzania Litho kilichopo Arusha ambacho kwa sasa hutengeneza paketi za sigara na za sabuni. Kwa hiyo Serikali iombwe ili isaidie kutatuatatizo hili linalokabili taifa kwa sasa.
9. Bidhaa ya Karatasi na Mazao Yatokanayo na Bidhaa Hiyo
Msingi mkuu wa uchapishaji na uchapaji ni vitabu, magazeti na bidhaa nyingine muhimu zitokanazo na karatasi. Ukiondoa biashara ya bidhaa zitokanazo na karatasi hakutakuwa na uandishi wa ufanisi, wala uchapishaji au uchapaji, ama maduka ya kuuzia bidhaa nyingine za aina hiyo.
Hebu tufikirie, kama karatasi isingegunduliwa hapa duniani tungalikuwa na maendeleo haya tuliyofikia ulimwengu! Tujiulize tena maswali yafuatayo juu ya umuhimu wa bidhaa za karatasi:

(i) Kusingekuwapo karatasi elimu ingefikia kiwango hiki duniani?
(ii) Bila karatasi ofisi mbalimbali zingeendeshwaje?
(iii) Karatasi zisingekuwepo maandishi na kumbukumbu mbalimbali zingehifadhiwa vipi?
(iv) Kama hakuna karatasi mawasilino ya barua yangelifanyikaje?
(v) Pasipo karatasi za kutengenezea noti au hawala za fedha ni lundo la kiasi gani la sarafu ambalo matajiri wangebeba kila siku kwa shughuli zao?

Kutokana na mifano hiyo michache tunaweza kubainisha kwamba karatasi ni bidhaa muhimu sana – kama vile mafuta kwa kurahisisha usafiri, au dawa ambazo hutibu magonjwa na kuokoa uhai wa binadamu wengi sana.
Kwa hiyo ni kweli kabisa kwamba bidhaa zitokanazo na karatasi zina umuhimu wa pekee kwa maendeleo ya taifa letu. Msisitizo wa jambo hili ni kwamba kila mmoja wetu anawajibika kwa uwezo alio nao kufanya kila analoweza ili mazao ya bidhaa hii, kama vile vitabu, magazeti na vifaa vingine kadha wakadha vinavyotokana na karatasi, yapatikane kwa wingi wa kutosheleza mahitaji ya wananchi wote na kwa bei nafuu inavyowezekana. Badala ya bei zake kupanda kila wakati ziwe na mwelekeo wa kushuka au kubakia palepale.
Mwelekeo wa kudhibiti bei zilizo nafuu utaweza kufanikisha ustawi wa uchapishaji na uchapaji katika taifa letu na kulinufaisha kila kundi linalohusika na huduma au biashara zinazotokana na mazao ya karatasi.
10. Mapendekezo kwa Ufupi

(a) Kuwe na sera maalumu ya karatasi, uandishi, uchapishaji na uchapaji, na ununuzi na uuzaji wa bidhaa zinazotokana na karatasi nchini.

(b) Sheria ya kumiliki kazi za sanaa ifanyiwe marekebisho na kujulishwa kwa wananchi na serikali ifikirie tena uwezekano wa kuwa mwanachama wa International Copyright Convention.

(c) Mashirika ya uchapishaji, uchapaji na uuzaji vitabu yazingatie makisio halali na uwiano wa faida isiyokiuka viwango vinavyokubalika kimataifa.

(d) Kuwe na viwanda maalumu vya kuchapa vitabu kwa viwango bora (gualily printing presses).

(e) Kuwe na taasisi maalumu zinazotoa taaluma ya uandishi, uchapishaji, uchapaji na uuzaji wa vitabu hapa nchini.

(f) Kiwanda cha kutengeneza karatasi nchini kipanue shughuli zake ili kiweze kutoa aina zote za karatasi zinazotakiwa kwa huduma mbalimbali na kudhibiti bei nafuu kwa maendeleo ya taifa letu.

(g) Waandishi, wachapaji, wachapishaji na wauzaji waunde vyama vyao ili wawe na msimamo wa pamoja katika kukabili matatizo yanayozuka, na kudhibiti viwango vya ubora wa mazao yatokanayo na karatasi pamoja na kuzingatia maadili ya kuendesha biashara au huduma zao.

(h) Kuwe na Bodi.maalumu inayowashirikisha waandishi, wachapishaji, wachapaji na wauzaji chini ya uongozi wa serikali ili kutatua kwa pamoja matatizo yanapozuka na kuendeleza huduma ya hidhaa hizo zitokanazo na karatasi kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Tanbihi
1. Hata hivyo, Tanzania haijatia sahihi mkataba wowote wa kimataifa, kama vile wa Universal Copyright Convention au ule wa Berne Vnion. Kwa hiyo Tanzania si mwanachama wa The International Copyright Convention. Kutokana na kikwazo hiki, Tanzania haina idara au chombo maalumu kinachowajibika kuelimisha, kukuza na kusimamia kwa dhati “Sheria ya Kuhifadhi Kazi za Sanaa nchini.” Athari yake ni kuwa ukiukaji wa sheria unaweza kutokea bila kugundulika mintarafu ya maadili ya uandishi, uchapishaji, uchapaji, ununuzi na uuzaji wa bidhaa hizo zitokanazo na karatasi.