UCHAMBUZI WA UTENZI WA MWANAKUPONA: MAWAIDHA KATIKA TENDI

By , in Ushairi on .
 UTANGULIZI.
Katika uchambuzi huu wa
UTENZI WA MWANAKUPONA tunatarajia kuangalia vipengele kadhaa vya uchambuzi kama
vile historia fupi ya mwandishi, vipengele vya  fani na maudhui, na
vingine vitakavyojitokeza. Katika uchambuzi huu tutaonesha moja kwa moja nafasi
ya mwanamke katika kumtunza mumewe. Hii ni kazi ya uchambuzi kwa hiyo
itahusisha vipele mbalimbali vya uchambuzi. Kisha tutaonesha hitimisho na
marejeo

HISTORIA FUPI YA
MWANDISHI.

Mulokozi (1999)
anatueleza kuwa Mwanakupona binti Mshamu Nabhany alizaliwa Pate mwaka 1810.
Mwaka 1836 aliolewa na bwana Mohammed Is- Haq bin Mbarak. Lakini inasemekana
kuwa alijulikana zaidi kwa jina la Mataka. Mwanakupona aliolewa na Bwanaa
Mataka katika ndoa ya wake wengine watatu. Yasemekana kuwa Mataka alikuwa ni
mtawala wa Siu na mpinzani mkubwa wa utawala wa waarabu huko Zanzibar.
Mwanakupona alipata kuzaa watoto wawili na bwana Mataka ambao ni Mwana Hashimu
bint Shee Mataka (1841-1933) na ndiye aliyetungiwa utenzi huu, na Mohammed bin
Shee Mataka aliyezaliwa baina ya mwaka 1856 na 1858.
Tunendelea kuelezwa
kuwa Shee Mataka alikuwa na watoto wengine watatu kwa wake wengine ambao ni
Bakari alieyekufa vitani Pate mwaka 1855, Mohammed (mkubwa) ambaye ndiye
aliyerithi utawala wa baba yake mwaka 1855 na kuendeleza upinzani uliokuwa
umeanzishwa na baba yake dhidi ya utawala wa waarabu wa Zanzibar. Tunaelezwa
kuwa baadaye Sayyid Majid, Sultan wa Unguja alimfanyia hila hadi alifanikiwa
kumkamata na kumfungia katika Ngome ya Yesu, Mombasa ambako alifia huko mwaka
1868. Pia yasemekana kuwa baada ya kifo cha Mohammed (mkubwa) Omari alirithi
utawala na kuishi hadi miaka ya mwanzo ya karne ya ishirini na alishiriki
katika kupinga ukoloni wa Waingereza huko Kenya.
Pia yasemekana kuwa
Mohammed (mkubwa) alikuwa mshairi na alitunga tungo za ILELE SIU ILELE na
RISALA WA ZINJIBARI ambazo zilihusu mapambano yake na Sultani wa Unguja, na
fitina za baadhi ya raia zake wa Siu. Baadaye tunaelezwa kuwa Mwanahashimu
aliolewa mara mbili na kufanikiwa kupata watoto wawili ambao waliishi hukohuko
Lamu. Alikuwa ni mshairi na alitunga mashairi kadhaa. Baadaye tunaelezwa kuwa
kuna maafa yalimkuta bibie Mwanakupona na yaliisibu familia yake na hata
aliiamua kuondoka Siu na kuhamia Lamu ambako ndiko alikotungia utenzi wake wa
mwaka 1858. Inasemekana kuwa Mwanakupona aliuandika utenzi huu akiwa ni mgonjwa
akisumbuliwa na maradhi ya tumbo la uzazi. Alihisi kuwa asingepona, hivyo
akaamua kutunga utenzi huu ili uwe ni wosia kwa binti yake ambaye angebaki bila
ya uongozi wa mama.

MUHTASARI WA UTENZI.

Kijamiii, Mwanakupona ni
utenzi wa kimawaidha uliotungwa na Mwanakupona Binti Msham kwa ajili ya binti
yake aliyeitwa Mwanahashimu bint Mataka mwaka 1858. Utenzi huu unaonakena
kuwakilisha vyema tungo za utamaduni na maonyo ya wakati huo. Mtunzi aliutunga
ili kumlenga binti yake aliyeitwa Mwana Hashimu kwa lengo la kumuonya lakini
pia aligusia kwa vijana wengine wa kike wapate kuusoma utenzi huu ili nao
wapate maonyo hayo (Ubeti wa 94 na 95). Utenzi huu unaonekana kuibadilisha
jamii ya uswahilini baada ya kuona kuwa unafaa hasa kwa malezi ya kijadi hasa
kwa watoto wa kike kwa kuwafunda. Yawezekana Jambo hili ndilo linaloufanya
utenzi huu uonekane kuwa msaada wa jamii hata leo hii.
Kihistoria, tunaelezwa
kuwa huu ni utenzi wa kale uliokuwa unaendana na mazingira ya wakati huo.
Mwandishi aliuandika kwa kuilenga jamii ya wakati ule hasa kwa kufuata mila,
desturi za jadi za wakati huo kama vile heshima ya ndoa, wanawake kuwekwa
utawani, kutoonesha sura zao mbele ya watu, kumtukuza mume kama Mungu wao wa
pili. Pia unaonekana kuwa ulikuwa ni utenzi wa kitabaka la utawala.
Kifasihi, UTENZI
WA MWANAKUPONA
 ni utenzi pekee wa kishairi uliotungwa na mwanamke
ambao unaonekana kuleta athari kwa waandishi wengine hata kuiga mfano wake wa
kutunga tungo za kimawaidha kama vile Said Karama WASIA WA BABA,
Shaaban Robert katika utenzi wa HATI NA ADILI, Zainab bint
Humud, HOWANI MWANA HOWANIUTENZI WA ADAMU NA HAWA.

FANI NA MAUDHUI.FANI.

Senkoro (2011),
anaeleza kuwa fani katika fasihi ni ule ufundi wa kisanaa anaotumia msanii
katika kazi yake. Mpangilio wa vitushi, (episode) UTENZI WA MWANAKUPONA ni
utenzi wenye jumla ya beti 102 ambao unaanza kwa mtunzi kumwita binti yake
akaribie akiwa na wino na karatasi ili asikiilize wosia. Anasema kuwa yeye
alikuwa ni mgonjwa hivyo hakupata muda wa kumpa wosia binti yake. Anamwambia
binti yake kuwa aanze kwa kumtukuza Mungu wake na kumwomba rehema zake. Baada
ya hapo anamwambia anataka kumpa hirizi ya kinga yake na kidani cha kujipambia.
Halafu anaanza kumpa maonyo aliyokuwa ameyakusudia kama vile kuheshimu mume,
kumheshimu mungu, kuwa mwaminifu, kuepuka umbeya, kushika dini na mengineyo.
Hayo ni kuanzia ubeti wa (1-25).
Na kuanzia (ubeti.
26-36) mtunzi anaeleza namna mwanamke anavyotakiwa kumfanyia bwana yake.
Miongoni mwa mambo hayo ni kutojibizana naye, kumpa kila anachokihitaji,
kumuaga vizuri kila anapoondoka, kumpokea vizuri kila anapokuja, kumpapasa na
kumpepea usiku, kumkanda mwili, kumsifia kwa watu wengine, kumwandalia chakula,
kumnyoa ndevu, na kumpendezesha.
 Kuanzia (ubeti
37-56), mtunzi anaonesha namna mwanamke anavyopaswa kuwa yeye binafsi yaani
mwanamke aliyeolewa inatakiwa awe msafi kimwili, avae vizuri na kujipamba kila
siku, aombe ruhusu kwa mumewe kabla ya kutoka na akitoka asikawie kurudi na
anapotembea asijifunue buibui lake na asiongee wala kunena na mtu yeyote njiani
na aridhike kila anachopewa na mumewe.
Kuanzia (ubeti. 57-66)
mtunzi anamwonya binti yake namna ya kuishi na watu wote kwa ujumla, yaani awe
na upendo kwa watu wote bila kuangalia hadhi zao, afanye ushirikiano na
wanandugu, marafiki na watu wengine pia awasaidie wanaohitaji msaada. Na
atakapofanya hivyo malipo yake yatakuwa ni mbinguni.
Kuanzia (ubeti. 67-102)
mtunzi anafanya dua ndefu ya kuwaombea watu wote wakiwemo watoto wake, anajiombea
yeye mwenyewe, anawaombea waislamu kwa ujumla, na kisha anamalizia kwa
kuwaombea wanawake wote wauosome utenzi huu ili wanufaike nao.
Hivyo tunaona kuwa
japokuwa mtunzi amejitahidi kupangilia vitushi lakini inaonesha wazi kuwa
amechanganya baadhi ya beti, yaani beti ambazo zilitakiwa ziwepo mwishoni
amezipeleka kati ama mwanzoni mwa utenzi, na za mwanzoni kuzipeleka mwishoni
ikiwa zingepaswa kuendana na beti fanani ili kukamilisha wazo. Kwa mfano beti
za 92 na 93, zilipaswa kuwekwa mwanzoni maana zina mawazo ya mwanzoni kama vile
maonyo kwa ujumla, ubeti 22 na 23 zingepaswa kuwekwa kati ya ubeti wa 11na 14
ili kusisitiza suala la dini, na ubeti wa 40 na 42 zingepaswa kuwekwa kati ya
ubeti wa 36 na 37 ili kumwonya mtoto wa kike kuwa na tabia nzuri hasa kwa bwana
yake kwa kuwa msafi na kufanya kazi.
Matumizi ya lugha,
mwandishi huyu hajatumia sana lugha ya picha kama vile sitiari, tashibiha,
tashihisi, methali nahau hata vitendawili na taswira japokuwa kwa kiasi fulani
anaonekana kutumia lugha ya taswira kama vile hirizi, akionesha kuwa ni kinga
ya kujikingia mtu aliyepatwa na matatizo ubeti ( 8-10), kidani,kama lulu au
pambo (ubeti. 40) Anasema kuwa;
Na
kidani na kifungo
Sitoe
katika shingo
Muili
siwate mengo
Kwa
malashi na dalia
Hapa tunaona kuwa
mwandishi ametumia taswira ya kidani inayomaanisha kuwa ni pambo au lulu
inayovaliwa shingoni.
 Misamiati,
aliyoitumia sio migumu sana inaeleweka japokuwa kwa kiasi kikubwa ametumia
lahaja ya Kiamu na anaonekana kuimudu vyema lugha yake, lakini kwa mtu asiye
mmilisi wa lahaja hiyo anaweza kupata mkanganyiko pindi anapousoma utenzi huu.
Muundo, kwa upande wa
muundo mwandishi anaonekana kujitahidi kwa kiasi kikubwa kwani ametumia ushairi
wa kufuata urari wa vina na mizani kwa kiasi kikubwa, na kila mshororo
unaonekana kuwa na mizani 8.
Motifu, iliyojitokeza
katika utenzi huu ni motifu ya msako wa peponi, yaani ile ya
kumsaka Mwenyezi Mungu hasa kwa kutenda matendo mema, kutii maagizo yake pamoja
na mwanamke kumheshimu mume. Mfano (Ubeti. 26-27) unasema;
26. Siku
ufufuliwao
Nadhari
ni ya mumeo
Taulizwa
atakao
Ndilo
takalotendewa
27.     Kipenda
wende peponi
Utakwenda
dalhini
Kinena
wende motoni
Huna
budi utatiwa
Beti hizi mbili
zinatudhihirishia kuwa Mwanakupona aliona kuwa safari ya kufika peponi ni kubwa
kwani kinachotakiwa ni kujipanga ili tuweze kuepuka adhabu ya jehanamu.
Anamwambia mwanaye kuwa ili kushinda hilo ni vyema kumpenda mumewe na kumtii
maana huko mbinguni Mungu atamuuliza kama alimpenda na kumtii huku duniani
(Ubeti.28).
Keti
naye kwa adabu
Usimtie
ghadhabu
Akinena
simjibu
Itahidi
kunyamaa.
Ushujaa, wahusika
wanaoelezwa katika utenzi huu sio mashujaa kama ilivyozoeleka katika tenzi
zingine kama vile FUMO LIONGO, SUNDIATA, MAJIMAJI na zinginezo. Huu unaonekana
kuwa ni utenzi wa kimawaidha ambao hauonyeshi ushujaa au unguli kwa sababu
unatoa mawaidha mengi ya kijadi hasa kwa wanawake pamoja na binti yake. Hivyo
tunaweza kusema kuwa utenzi huu haujasadifu ushujaa bali umekuwa na wahusika
ambao ni binti yake anayeitwa Mwanahashimu, (ubeti .37), wanawake wengine
(ubeti 94), Mungu ambaye anatajwa katika (ubeti. 5, 23, 36,72,73,82, 87 na 88)
na mume (ubeti. 42, 47, 48).
Mianzo na miisho ya
kifomula, mwandishi ameanza na sala au dua kama kawaida ya tendi za Kiswahili,
katika sura ya kwanza (ubeti.4-7) anamwambia mwanaye aketi chini na Mungu wa
rehema atasaidia katika kufanikisha jambo hilo. Mfano (ubeti.4) anasema;
Ukisa
kutaqarabu
Bismillahi
kutubu
Umsalie
Habibu
Na
sahabaze pamoya.
Pia anamalizia kwa
shukrani ya kumshukuru Mungu kwa kumfanikishia shughuli nzima ya utunzi wa kazi
yake na kuufanya usomwe na watu wengi ili uje kuwa nyenzo ya maisha yao. Mfano
(ubeti.101-102)
101.
Mola tutasahilia
Kwa
Baraka za Nabia
Na
masahaba pamoya
Dini
waliotetea
102.
Nahimidi kisalia
Kwa
Tume wetu nabia
Ali
zake na dhuria
Itwenee
sote pia.
 MAUDHUI.
UTENZI WA MWANAKUPONA
unaonekana kujadili masuala ya itikadi ya kijinsia yaani yakukubali na
kuheshimu ngazi za mamlaka kama zilivyo bila kuzivunja kwa kuwa ni amri ya
Mungu. Hata hivyo mawazo yake yanaonekana kuwa yalitokana na vyanzo kadhaa kama
vile, mafundisho ya dini ya kiislamu, yanatokana na  mila na desturi
za Waarabu zinazofuatwa na wenyeji wa pwani, mtazamo na ozoefu wa tabaka tawala
la pwani. Mawazo yote haya yanaunganika na kutupa dhima kadhaa kama zifuatazo.
Dhima za utendi huu
Katika uchambuzi wa
kazi yoyote ya kifasihi tunaona kwamba huwa na dhima mbalimbali ambazo huweza
kuwa za kijamii, kihistoria na kiutamaduni. Lakini dhima hizo kwa kiasi kikubwa
hutegemea muktadha na wakati wa utunzi wake. Kwa mfano utenzi huu ulikuwa na
dhima zake nyingi kwa wakati ule lakini kwa sasa hauwezi kuwa na dhima ileile
kwa kiwango chote kama ilivyokuwa wakati ule.
Kijamii, inaonyesha
kuwa Mwanakupona aliuandika utenzi huu kwa kuzingatia tabaka lake na jamii
yake. Kwani alikuwa katika jamii ya tabaka la Kifalme na hivyo dhima zake
zilionekana kumsaidia zaidi binti aliyopo katika uwanja huo sio zaidi ya hapo.
Kwa mfano alijaribu kuzungumzia masuala ya kutojichanganya na watumwa
wakati wa kazi 
(ubeti. 20),kuepuka wajinga wasiojichunga (ubeti.21), kuwa
mwaminifu na mpenda haki,(
ubeti.14) kujinyenyekeza mbele za wakubwa,
(ubeti. 15) kuepuka uropokaji (ubeti.19) kumheshimu
Mungu na mtumewe
 (ubeti .23),kumheshimu mume (ubeti
.31), kuheshimu wazazi, kuwa na upendo kwa wote (ubeti61-64), kuwa
mtiifu
 (ubeti.13), kushika dini. Pia baadhi ya dhima hizo
zinaonekana kuwa mwongozo kwa watoto wa kike mpaka kwenye jamii ya leo hii, na  labda
ndio maana tunauona unafaa mpaka sasa. Pamoja na kugusia hayo hakujaribu
kuzungumzia maswala ya tabaka la chini kama vile kulima, pamoja na maisha ya
tabaka la chini kwa ujumla ila tu, anamwambia mwanaye awasaidie watu
wasiojiweza mfano (ubeti.64) Anasema;
Na
ayapo muhitaji
Mama
kwako simuhuji
Kwa
uwezalo mbuji
Agusa
kumtendea
Hapa anadhihirisha wazi
kabisa kuwa yeye anatoka katika tabaka la juu na kila kitu anacho.
Kihistoria, utenzi huu
unatuonesha kuwa ni utenzi wa kale yaani wa miaka ya 1858 ambao ulitungwa na
Mwanakupona kwa lengo la kumwonya binti yake na wanawake wengine. Ulikuwa na
mashiko zaidi kwa wakati huo na kwa kiasi fulani mpaka sasa unaonekana kushika
chati kwani unatoa maonyo na maadili kwa wanawake wa kisasa kama vile kuepuka
umbeya, kuacha uvivu (ubeti .37), kuwa na adabu (ubeti.13),  kushika
dini, upendo kwa wote, wanawake kuwaheshimu waume zao pamoja waume kuwaheshimu
wake zao.
Kiutamaduni pia utenzi
huu unaoneka kuwa kwa kiasi kikubwa unazungumzia mambo ya kitamaduni hasa
utamaduni wa kufuata mila, desturi na jadi za Waswahili, na kwa kiasi kidogo
unagusia pia tamaduni za Kiarabu. Kwa upande wa Waafrika kama tunavyojua kuwa
wao wana mila na desturi zao za kijadi ambazo hutokea baada ya kijana kuonekana
anafikia hatua ya makuzi. Hivyo jamii huchukua jukumu la kuwafunda vijana wa
kike na kiume. Kwa mfano hufundwa kuhusu mambo ya ndoa (namna ya kuishi na
mume) na maisha kwa ujumla. Hata ndani ya utenzi huu tunaona hayo yakifanywa na
mtunzi kwa binti yake, akimwonya juu ya mambo kadhaa ya kiutamaduni kama vile;
adabu na heshima, kuepuka umbeya, kuepuka fitina, kuepuka uchoyo (ubeti.64),
kuepuka uvivu (ubeti .37), kuwa msafi na kujipamba ili kufurahisha na kumvutia
mume ubeti. (40-42), kutomnyima mume chochote anachokitaka (ubeti.29) na kumhudumia
kitandani mfano. (ubeti.31) anasema.
Kilala
siikukuse
Mwegeme
umpapase
Na
upepo asikose
Mtu
wa kumpepea.
Funzo hili liko katika
mila za ndoa kwani utamaduni wa Waswahili husisitiza sana masuala kama hayo
hasa kwa kudumisha ndoa kwa kupendana na kutimiziana mahitaji mbalimbali ili
kuishi kwa furaha na amani ndani ya nyumba mfano kutabasamu kwa mke kila
anapomwona mume wake (ubeti.50).
Pia utamaduni wa
Kiarabu  ulioguswa ni kama vile; namna ya mwanamke anapovaa na kutoka
nje ya nyumba yake inatakiwa aweje, mwandishi anatuonyesha kuwa Waarabu
wanatamaduni zao ambazo wanazifuata na kuzitekeleza lakini kwa sasa zinaonekana
kabisa kuingia katika utamduni wa waswahili na tunazifuata. Kwa mfano masuala
ya kutawishwa kwa mwanamke pamoja na mavazi (ubeti 44-45), pia mwanamke
anaambiwa kuwa anapotoka asiangalie wala kuongea na watu njiani, (ubeti .46)
anasema
Wala
sinene ndiani
Sifunue
shiraani
Mato
angalia tini
Na
uso utie haya.
Tunaona kuwa hizi ni
mila za kiarabu ambazo kwa sasa zinaonekana kuleta athari mpaka kwetu mpaka
sasa.
Suala la dini, sehemu
kubwa ya UTENZI WA MWANAKUPONA unaonekana kujadili zaidi kuhusu maudhui ya
kidini na kusisitiza haja ya kuzingatia mafunzo ya dini ya kiislamu. Kama vile,
kumtii Mungu na mtume wake (ubeti.23), kupenda na kutenda haki kama dini
inavyotaka (ubeti. 12), kumtii mume na kuishi naye kwa upendo kama dini
inavyotaka. (Ubeti.26-27), pia utenzi huu unatufundisha kuwa Mungu pekee ndiye
anayeweza kutenda chochote unachohitaji na kama ni hivyo basi hatuna budi ya
kutanguliza maombezi yetu kwake popote tunapofanya jambo fulani hata baada ya
kumaliza shughuli yoyote ni vyema pia kumshukuru. Mfano huu tunauona pia kwa
Mwanakupona mwenyewe ambaye alianza kwa dua na kumalizia tena na dua ubeti.
(4-7, 66-102).
Falsafa ya mwandishi
juu ya utenzi huu inaonekana kuwa mwanamke hawezi kufika mbinguni kama
hajamtendea mume wake mambo anayopaswa kufanyiwa katika maisha ya ndoa.
Hivyo tunaweza
kuhitimisha kwa kusema kuwa UTENZI WA MWANAKUPONA unaonekana kuwa nguzo ya
mafunzo na maonyo kwa wanawake hata wa kizazi cha sasa lakini kwa kuangalia kwa
baadhi ya mafunzo ambayo yanaendana na wakati huu maana mafunzo mengi
yaliyoelezwa ni ya wakati wa zamani na hayana maana kwa wakati huu. Pia utenzi
huu unaonekana kumdidimiza sana mwanamke hata kutopewa uhuru wa kuweza kufanya
mambo mengine ya kimaendeleo kwani unamfanya mwanamke muda wote awaze namna ya
kumriwaza mume tu.
MAREJEO
Mulokozi, M.M.
(1999) Tenzi Tatu za Kale. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili: Dar
es Salaam.
Senkoro, F.E.M.K
(2011) Fasihi. Dar es salaam. KAUTTU.

 

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!