UCHAMBUZI WA TAMTHILIYA YA MASHETANI

By , in Tamthiliya on .

UCHAMBUZI WA TAMTHILIYA YA MASHETANI

MTUNZI :   Ebrahim N. Hussein

MWAKA:   1971

MCHAPISHAJI : Oxford University Press East Africa

 

UTANGULIZI

Maana ya Tamthiliya

Wamitila (2003)

Tamthiliya ni utanzu ambao hutegemea mazungumzo na uigizaji ili kuwasilisha ujumbe wake. Tamthiliya ni neno linalotumiwa kurejelea utanzu bila ya kuwa na msisitizo mkubwa kwenye suala la uwasilishaji wake jukwaani.

 

Penina Mhando Mlama (1983)

Tamthiliya ni ule utungo ambao unaweza kuwa umeandikwa au haukuandikwa, ambao unaliweka wazo linalotaka kuwasilishwa katika umbo la tukio la kuliwezesha kutendeka mbele ya hadhira.

Kutokana na fasiri hizo tunaweza kusema kuwa, tamthiliya ni mchezo ambao huwasilishwa ana kwa ana jukwaani kwa madhumuni ya kuwasilisha wazo ama tukio fulani kwa hadhira.

Katika kuchambua vipengele vya tamthiliya kwa ujumla tumetumia tamthiliya ya Mashetani iliyoandikwa na Ebrahim N. Hussein, mwaka 1999.

Vipengele vya tamthiliya kwa ujumla

Tamthiliya ina vipengele vifuatavyo;

 1. Mtiririko wa matukio ama Ploti
 2. Wahusika
 3. Maudhui
 4. Maneno
 5. Muziki
 6. Kionwa (Spectacle)
 1. MTIRIRIKO WA MATUKIO (Ploti)

Mtiririko ni mpangilio wa tamthiliya yote na una mwanzo, kati na mwisho.

 

(i) Mwanzo– Unaonekana baada ya Juma na Kitaru walipokutana chini ya mbuyu wenye pango.

Tukio- Juma na Kitaru wanaonesha mchezo wa shetani na binadamu.

Wahusika: Juma na Kitaru

 Hali – Walikuwa katika hali ya kawaida.

(ii) Katikati

Sehemu hii imegawanyika katika vipengele vidogo vifuatavyo;

Ugunduzi wa habari njema

Baba Kitaru anamwambia mama Kitaru kwamba kuna ‘poultry farm’ inauzwa. Familia ya kina Kitaru inaonekana wana maisha mazuri mfano: wana gari, nyumba ya kifahari.  Hii inajidhihirisha wazi baada ya baba yake Kitaru aliporudi nyumbani na kusema kuwa njooni nikuonesheni kitu kumbe alikuwa amenunua gari mpya aina ya Benzi (uk,22) na kuwachukua wakatembee.

Upinzani usiotegemewa kutoka kwa wahusika

Ni mabishano kati ya mama yake Kitaru na baba yake Kitaru kuhusu kumpeleka kwa mganga kwa sababu Kitaru alipokuwa anaumwa madaktari walikuja kumtibu lakini hakupona kwa hiyo mama yake aliamua wampeleke au wamwite mganga lakini baba yake alikuwa anapinga kumwita mganga.

Upinzani mwingine ulitokea baada ya mama yake Juma alipomwambia Juma amwangalizie chungu chake kama kinachemka lakini Juma alionekana kukataa na bibi yake alikuwa anamtetea kwamba amwache asome asimsumbue mtoto.

Kilele cha Utata

Unaoneshwa pale Juma anapoamua kuondoka kwao kwa hasira na kwenda hotelini na kukaa chini na kuanza kunywa soda.

Ni pale Kitaru naye alipoanza kuumwa Ugonjwa usiojulikana kwa sababu Madaktari walikuja nyumbani kwao kumtibia lakini haikufua dafu bado Kitaru alikuwa haponi na ugonjwa anaoumwa ulikuwa haujagundulika.

Uchaguzi usiotegemewa

Umejitokeza pale mama yake Kitaru alipoamua watumie mitishamba kuwa waite mganga wa kienyeji ili amtibu Kitaru kwa sababu madaktari wamejaribu wameshindwa kwa hiyo huo ni uchaguzi ambao hakuutegemea. Mwishowe baba yake Kitaru alimruhusu mkewe afanye anachotaka.

(iii) Mwisho

Sehemu ya mwisho ni ufumbuzi, baada ya Juma kwenda kwa kina Kitaru, alimkuta ameamka usingizini akionekana kujishangaa na hajielewi kama yupo ndotoni au ni fikra. Lakini Juma anamtoa wasi wasi kuwa yupo katika hali ya kawaida na hakua ndotoni ndipo Kitaru alipoamua kumsimulia Juma ndoto aliyoiota.

Baada ya Kitaru  kumsimulia Juma mambo aliyoota alimshauri wakacheze mchezo wao pia Kitaru alitaka aigize sehemu ya Shetani ambayo mwanzo iligizwa na Juma. Walianza kubishana taratibu lakini mwishowe ugomvi kabisa hadi kuburuzana chini. Mwisho ni wa taharuki kwa sababu baada ya ugomvi Juma aliondoka bila kucheza mchezo wao, hivyo kumuacha Kitaru asijue la kufanya, na msomaji asijue kuwa mchezo ungeishaje.

 1. WAHUSIKA

Katika tamthiliya ya Mashetani kuna wahusika wa aina zifuatazo;

Wahusika Ishara

Wahusika ishara katika tamthiliya hii ni Shetani na Binadamu

Wahusika bapa

Wahusika bapa ni Juma na Kitaru kwani wahusika hawa hawakubadilika tangu mwanzo wa tamthiliya hadi mwisho.

Mhusika Mfoili

Bibi yake Juma ndiye mhusika mfoili kwani anampamba mjukuu wake Juma na anamtetea katika mambo na tabia anazofanya.

Wahusika wa Tamthiliya hii wanatofautiana kwa namna mbalimbali.

Umri:  Wahusika wanatofautiana kiumri, kuna vijana ambao ni Juma na Kitaru, kuna wazazi ambao ni wazazi wa Juma  na Kitaru. Pia kuna bibi yake Juma.

Kiuchumi:  Wahusika wanatofautiana  kiuchumi kwani kina Kitaru wana maisha mazuri kuliko kwa familia ya kina Juma.

Kitabia:   Juma anaonekana mtu mwenye hasira, dharau, kiburi wakati Kitaru anaonekana mtu mwenye kupenda kukaa ndani na kusoma vitabu.

Mtazamo:  Kitaru alikuwa hasomi ili apate hela lakini Juma alikuwa anaonekana kuwa anasoma ili apate hela.

Mawazo:  Baba yake Kitaru anatofautiana na mkewe alipomwambia kuwa kuna ‘poultry farm’ linauzwa lakini mama Kitaru hakuridhika na maoni pamoja na ushauri wa mume wake. Pia mama Kitaru anatofautiana na mumewe katika wazo la kutumia miti shamba na kumwita mganga. Baba Kitaru anamwambia mkewe afannye anachotaka katika hilo. 

 1. MAUDHUI

Maudhui ni jumla ya masuala na mambo yanayozungumzwa katika kazi ya fasihi. Hivyo katika kuikuza dhamira yake mwandishi anaibua na kuyagusia masuala mengine haya ndiyo yaitwayo dhamira. Katika tamthiliya ya Mashetani, mwandishi ameibua dhamira zifuatazo;

 

Uonevu na Unyanyasaji

Shetani anamnyanyasa Binadamu kwa kumtaka afanye mambo yote anayomuamrisha, binaadamu analazimika kuyafanya bila ridhaa yake.

Shetani anamfundisha Binadamu kutamka neno “Gashalazeritwas” ambalo lina mnyanyasa Binadamu kila mahali katika mwili.

SHETANI    :  Liseme neno nililokufunza

BINADAMU:  Gashalazeritwas

SHETANI     : sasa acha likuumize

BINADAMU: (Linamuumiza) gashalazeritwas

SHETANI     : Sasa likuvunje maini

BINADAMU: (Linamvunjavunja maini) Gashalazeritwas

SHETANI     : Ndani ya hali yako.

BINADAMU: Gash….Gasha…aah. (kwa maumivu, kimya kazirai. Shetani huku      anakuja. Anamnyooshea mikono anatapatapa Binadamu kwa huruma) (uk.4)

Katika jamii yetu ya leo kuna uonevu na unyanyasaji wa namna mbalimbali unaofanywa na wenye nguvu katika jamii. Viongozi na wenye nguvu za kiuchumi, kisiasa na kijamii wanawaburuza waliochini yao. Wanatoa maelekezo na amri ambazo ni kandamizi kwa wanyonge na nguvu hawana budi kufanya yote yaliyotolewa na wakubwa.

Kujitoa mhanga

Binadamu anaamua kujitoa muhanga kujitetea baada ya kunyanyaswa na Shetani; hamwogopi tena.

BINADAMU: Jitokeze, (kimya) jitokeze kama wewe mwanaume kweli, jitokeze unaogopa? Ushujaa wako wote unayeyuka ukimwona mtu kashika silaha? Tokeza, mwoga mkubwa we.  Tokezaaa.

SHETANI: …Huna la kunifanya eh? (Anacheka) Wewe huogopi kugombana na mtu usiyemwona na ambaye anakuona? (Uk. 5)

BINADAMU: Acha kunitisha sitishiki hivyo. Kama mwanaume kweli jitokeze.

Mashetani ni wengi katika jamii yetu leo, watu wenye nguvu za kiuchumi, kiutawala, Kielimu, Kisiasa na hata Kiutamaduni wanawanyanyasa wanyonge wasio na nguvu hizo.

Wanyanyasaji wanafika mahali na kuamua kujitetea kwa kupambana na watu hao kwa malengo ya kujitetea baada ya kuchoshwa na unyanyasaji wa kila namna.

Umuhimu wa Elimu

Mwandishi ameonesha umuhimu wa elimu kwa jamii, na amewasilisha mawazo yake kupitia wahusika Juma na Kitaru wanaosoma katika Chuo Kikuu, Wote wana mitazamo tofauti baada ya kumaliza chuo kikuu.

KITARU:  Hata kidogo, siamini, Basi ikiwa nimekwenda University kwa  sababu ya mshahara tu, basi afadhali niache na huko kusoma kwenyewe pia.  Mawazo ya ovyo kwelikweli.  Mimi nilipata kazi Shell; Pesa chungu nzima, nikaiacha, nikaja University.  Ningetaka pesa tu si ningefanya kazi tu?

JUMA: …Unajua; fanya kazi leo, pata pesa nyingi.  Mi ninatoka kesho University, na kukanyaga chini.

KITARU:  Sikubali hata kidogo, University siyo factory inayotoa vipande vya kupatia mshahara mkubwa au inayotoa tikiti ya kuingia katika nyumba ya Ubwana.

University ni mahali pa elimu, pa ujuzi.  Ukitaka kujijua hasa…(uku. 17)  Jamii kubwa ya wasomi leo hasa katika nchi yetu, matumaini na matarajio yao ni kwamba baada ya kumaliza viwango vya elimu wanavyosomea waajiriwe serikalini.  Wengi hawana mawazo ya kujiajiri.  Ni vema wasomi wakatambua kuwa elimu wapatayo ni kwa ajili ya kuwaangazia waweze kupambana na maisha yao.

Kadhalika, Elimu nayo iwaelekeze vijana katika kujitegemea, kujiajiri wenyewe na sio kuajiriwa.  Kwani hakuna uthibitisho kwamba kuna mtu aliyeajiriwa na kuwa tajiri.  Matajiri wana ajira Binafsi.

Nafasi ya Mwanamke katika familia

Mama Kitaru anajihusisha na kazi mbalimbali hasa za mikono kama vile ushonaji wa nguo.  Hii ni ajira ya kujipatia kipato na kulea familia yake.  MAMA:… Lakini hapana, kusema kweli nimeshikwa na kazi mpaka kopeni mwanangu. Nguo za watu chungu nzima na mkono wenyewe huu mmoja. Sijui nimshonee nani, nimwache nani…(uk.14)

Wanawake wengi wanajikita katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kwa madhumuni ya kuinua hali zao kiuchumi, kutunza familia na kupambana na umasikini kwa ujumla.

Hata  hivyo, wanawake nao wanapaswa kutambua nafasi zao katika familia na jamii kwa ujumla.  Kadhalika, wanaume wanapaswa kuthamini na kutambua kuwa kwa kushirikiana wanaume na wanawake kutaleta maendeleo.  Wanawake wajitahidi kufanya kazi zote bila kuchagua.

 

Imani juu ya Mashetani

Kitaru anaamini kuwa mashetani wapo, kadhalika Mfaume (Mtumishi wao) anaamini kuwa mashetani wapo.

MFAUME:  Mimi…Mimi ninaamini kama mashetani wapo.  Juzi juzi hapa, dereva mmoja bwana. anatoka sehemu za huko Magomeni huko.  Basi kafika kule karibu ya jangwani. He! Mara peke yake bwana, kachepuka njia akaenda kujilaza basi miguu juu chini, Kaulizwa kwani kasema nini? Kasema shetani; kazi ya shetani (uk.29-31)

Imani juu ya mashetani ni kubwa hata katika jamii yetu. Watu wanajiingiza katika vitendo visivyofaa kisha wanapoulizwa wanasema Shetani kawapitia. Watu wanajihusisha na wizi, ajali wanasingizia ni shetani.

Sote hatuna budi kuchukua tahadhari kwani kila tunalofanya tunajua matokea yake, hivyo shetani asisingiziwe kwa uzembe ambao ungezuilika.

Kutii na Kuthamini Wazazi

Juma anaonekana kutomtii mama yake.  Yeye anatumwa na mamaye anaitika bila kutekeleza kazi hiyo.  Anaonekana kiburi na anaamua kukimbia kusikojulikana.  Baba yake anamtafuta akae dukani haonekani wala hajulikana alipo.

Bibi yake Juma anaona kuwa anachofanya mjukuu cha kutomsikiliza mama yake kuwa sio neno.  Anamtetea kiasi cha kuzozana na mwanae (mama Juma) hadi kufikia mama Juma kutaka kuishi peke yake bila mama yake (uk. 39).

Vijana na watoto wengi wamepunguza utii kwa wazazi wao, wanaagizwa, wanatumwa na wanaelekezwa bila kutekeleza wala kufuata.  Ni jambo baya kutotii wazazi kwani wanayotuelekeza ni kwa manufaa yetu katika jamii.  Tukumbuke kuwa “Asiyesikia la Mkuu huvunjika guu” na tena tunapaswa kufuata mafundisho yatolewayo na wazazi hasa mama kwani “Asiyefunzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu”

Vile vile tusisahau kuwatunza wazazi na wazee wetu.  Tusipende kuishi peke yetu bila kutoa msaada kwa wazazi hawa.  Tusikate tamaa na wala tusichoke kuishi nao hata kama tunapingana nao katika mawazo na mitizamo kama Juma alivyokuwa anapingana na mama yake (uk.39) na kufikia hatua ya kutaka kuishi peke yake.

Suala la Ulevi

Ulevi umeonekana katika tamthiliya ya Mashetani.  Hata hivyo inaonekana kuna sehemu tofauti za kunywea , zile za watu wa chini na za watu wa juu, MTUMISHI 2: …Wacha wakae kwanza…Nao wanaacha kwenda uswahilini huko wanakuja kutupa taabu hapa…(uk 40).

Watu wawili wanakwenda, baa lakini hawapewi huduma vizuri kwa kuwa ni weusi (waafrika) hivyo hata wahudumu wanachelea kutoa huduma kwa watu hao.

Suala la ulevi lipo hata katika jamii yetu, Ulevi unaweza kumfanya mtu kujisahau hasa anapolewa kupita kiasi.  Kadhalika ulevi huweza kusababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kifo. Hivyo basi hatuna budi kuchukua tahadhari dhidi ya ulevi ili kuepuka madhara yatokanayo na ulevi hasa ule wa kupindukia.

Matabaka

Mwandishi wa tamthiliya hii, ameonyesha kuwepo kwa matabaka katika jamii, tabaka la juu, kati na chini. Mwandishi anasema kuwa wazungu wanapohitaji huduma hupewa mapema kuliko waafrika. Mwandishi anasema;

MTU 1: Hatukusema namna gani. Tumesema hapa mumesikia bwana. Lakini nyinyi ndio tabia yenu: Mnatudharau, Waafrika wenzenu. (Ingekuwa mzungu hapa, hata hungethubutu kubishana bishana namna hii. (uk. 41)

Umoja na mshikamano

Mwandishi anaonyesha kuwa kuna umuhimu wa umoja na mshikamano. Mwandishi amewatumia wahusika Juma na Kitaru,  walioshirikiana katika mambo mengi pale waliposhindwa kuelewa jambo Fulani na walikuwa wanapendana. (uk.47)

 

 1. MANENO

 Maneno ndio nyenzo muhimu inayotumiwa katika kuwasilisha mawazo kwa hadhira. Lugha ya tamthiliya ni tofauti na lugha ya kila siku. Tamthiliya ya Mashetani ina maneno yenye uzito, ya mkato, yenye kikomo na ya kisanaa.

Mfano wa maneno mazito

Gashalazeritwas ( uk.4)

Neno hili ni fungu la Kingereza yaani “Gush it all as it was” Maana yake kwa Kiswahili ni kuwa mtawaliwa anapaswa kuzitupa mila zake zote jaani kasha ajivishe vazi la kikoloni  awe kiumbe anayestahili machoni mwa shetani. Hapa shetani ni taswira inayoonyesha tabaka tawala (ukoloni kipindi hicho kabla ya mapinduzi) wakati binadamu ni tabaka tawala.(Wafula,1983)

Mbuyu wenye pango- ina maana ya nchi za kiafrika

Shetani– Ukoloni mamboleo

Binadamu– Wananchi wa Afrika

 

Uzungumzia nafsi- Ni njia mojawapo iliyotumika kufikisha hisia za mwandishi, kwa kurejelea maneno ya Binadamu;

BINADAMU: Amekufa. Amekufa! Nimemuua! Nimemuua, au alitaka nimuue? … mawazo gani… mawazo mabovu kabisa. …Fikira gani hizi zinazonijia? Ninagombana na kuzungumza na nafsi yangu kama mwenye wasiwasi, nisiye na imani na kitendo nilichofanya? (Kimya.)

Dayalojia ndio imetumika zaidi katika kuwasilisha mawazo kwenye tamthiliya hii mfano.

SHETANI    :  Liseme neno nililokufunza

BINADAMU:  Gashalazeritwazs

SHETANI     : sasa acha likuumize

BINADAMU: (Linamuumiza) gashalazeritwas

SHETANI     : Sasa likuvunje maini

BINADAMU: (Linamvunjavunja maini) Gashalazeritwas

SHETANI     : Ndani ya hali yako.

BINADAMU: Gash….Gasha…aah. (kwa maumivu, kimya kazirai. Shetani huku      anakuja. Anamnyooshea mikono Anatapatapa Binadamu kwa huruma) (uk.4)

Maneno yenye kikomo na ya kisanaa

Mpanda ngazi na mshuka ngazi hawawezi kushikana mikono (uk. 56)

Wewe unaishi leo. Mimi ninaishi jana .(uk. 56)

Na kila leo yako ni kidato cha kesho yako (uk.56)

Kila kipitacho moyoni sio lazima kionekane usoni (uk.2)

Uzungumzia nafsi- Ni njia mojawapo iliyotumika kufikisha hisia za mwandishi, kwa kurejelea maneno ya Binadamu;

BINADAMU: Amekufa. Amekufa! Nimemuua! Nimemuua, au alitaka nimuue? … mawazo gani… mawazo mabovu kabisa. …Fikira gani hizi zinazonijia? Ninagombana na kuzungumza na nafsi yangu kama mewnye wasiwasi, nisiye na imani na kitendo nilichofanya? (Kimya.)

 1. MUZIKI

Muziki huhusisha sauti za wahusika. Kupanda na kushuka kwa sauti za wahusika hutengenezewa muziki katika tamthiliya. Muziki katika tamthiliya ya Mashetani unaonekana katika mifano  ifuatayo;

SHETANI: (Kicheko kirefu) Unataka kuniua? Stihizai kubwa hii! (uk.6)

SHETANI: …Shetani anaanguka lakini kicheko kinaendelea. Mara

                   Kinaendelea. Mara kinanyamaza ghafla. Kimya. Na

                   Kimya kinatisha kama kicheko au zaidi. Binadamu

                   Hakuna kitokeacho. Binadamu anapumua… (uk.8)

Nyimbo zimetumika katika tamthiliya hii (uk.9-10)

                    Mfano: Wako wapi walio wakijitapa?

                                 Sasa twawataka.

                                 Wako wapi  walio wakijitapa?

                                 Sasa twawataka… (uk.9)

Wimbo mwingine pia umeimbwa na baba Kitaru katika (uk.21- 22) wa tamthiliya hii.

 1. KIONWA

Kionwa ni vitu vionekanavyo jukwaani, vitu hivi huhabirisha wapi, na lini kitendo kilifanyika au kinafanyika. Pia huonesha wakati na kujenga wahusika kwa kuonesha hali ya uchumi wao, utamduni utabaka, vyote vipo chini ya kionwa, pia huonesha hali ya onesho. Vipo vionwa vingi katika tamthiliya hii vimeonekana katika sehemu zote na maonyesho yote.

Mwanzo

Sehemu ya 1

Onyesho la kwanza Juma na Kitaru – Wakiwa katika matembezi yao kasha baadae walikutana katika Mbuyu wenye pango ili kucheza mchezo wa Shetani. Juma anaonekana akiitangazia hadhira iliyofika kuangalia mchezo(uk.1).

Sehemu ya II- Hakuna kinachoonekan zaidi ya giza. Sehemu hii nzima inachezwa gizani, na kuna ukungukungu katika yote. Sehemu hii inachezwa katika akili ya Kitaru na mandhari(setting) yake imewekwa mbele au ndani ya picha ya kichwa chake.

Onyesho la I

Nyumbani kwa Kitaru mama yake anonekana anapiga pasi. (uk 13)

Onyesho la ii

Familia hii inaonekana ya kitajiri nyumbani kwao Kitaru. Baba anasoma gazeti. Mama anashona nguo kwa mkono. Kitaru amekaa kitabu mapajani, macho angani . Wana mtumishi wa ndani, jiko la umeme(oven), gari na mazungumzo yao ndio yanathibitisha maisha yao(uk.23)

Onyesho la iii.

Kitaru anaonekana yupo kimya na mwenye fikra, lakini anonekana pia mwenye kungojea matokeo ya kitu Fulani na mwenye tahadhari. Kimya kilikatishwa na mama yake alipoanzisha mazungumzo (uk.27)

Onyesho la iv. Katika onyesho hili mwanga unaonekana hafifu, ingawa kabla ya kuanza  onyesho inaonekan spotlaiti imetulia kwa muda mrefu juu ya kichwa cha Kitaru aliyelala.Baba na Mama wapo katikati ya mazungumzo na mazungumzo kuhusu tiba itakayomsaidia Kitaru.

Sehemu ya iii.

Onyesho la 1. Maisha ya familia ya kina Juma inaonekana yenye hali duni, Kwani hata vitu vimejaa hadi mlangoni. Juma anaonekana anasoma, mama yake anakuna nazi na abibi yake amejinyoosha katika kijitanda cha kamba(uk.36).

Onyesho la ii.

Onyesho limechezwa hotelini. Juma anaonekana yuko peke yake mezani anakunywa soda. Baada ya muda wanakuja watu wawili. Wanakaa meza ya pili. Pembeni watumishi wanaongea(uk.40.)

Sehemu ya iv.

Onyesho la 1

Nyumbani kwa Kitaru mama yake anapiga pasi, Juma anaingia baada ya muda Kitaru anatoka akiwa mwenye sura ya kutisha. Kitaru na Juma wanaonekana wakiwa katika mazunguzo (uk.45)

Onyesho la ii.

Juma na Kitaru wanaonekana mahali pale pale pa kwanza chini ya mbuyu wenye pango, wanautazama Mbuyu. Onyesho hili ndio la mwisho kutokana na ugomvi uliotokea kati ya Juma na Kitaru baada ya kila mmoja kutaka acheze nafasi Shetani (uk.53.)

HITIMISHO

Mwandishi Ebrahim Hussein ametumia vizuri taswira ya Shetani kama mkandamizaj,mnyanyasaji na mnyonyaji. Shetani anawakilisha dhana mbalimbali za uovu ufanya na binadamu dhidi ya mwanadamu mwingine. Mwandishi analenga kumuathiri mwnadamu kimawazo.Ikiwa mwanadamu atajidadisi, atajiuliza na kujihakiki mawazo yake yatapevuka. Msanii katika mchezo huu pamoja na dhamira yake ya kuifurahisha jamii pia analenga kuikomboa jamii kwa kuiamsha kupinga ukoloni mamboleo na kupigana kwa nguvu dhidi ya ukandamizaji wa kila namna. Hata hivyo msanii anaiasa jamii kutokuwa malimbukeni wa kupokea kila kitu kinacholetwa na Ukoloni mamboleo.

MAREJELEO

Hussein, E. N. (1996). Mashetani. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.

Kamusi ya karne ya 21 (2010).  Nairobi: Longhorn Publishers Ltd.

Wafula R. M. (1999). Uhakiki wa Tamthiliya, Historian a Maendeleo yake. Nairobi: Jomo Kenyata Foundation.

Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya fasihi, Istilahi na Nadharia, Nairobi: Focus publication Ltd.

Facebook Comments
Recommended articles