UCHAMBUZI WA KITABU: NINAWEZA, NI LAZIMA, NITAFANYA (“I CAN, I MUST, I WILL” ) Na: Dkt. Reginald Mengi

By , in Riwaya on .

UCHAMBUZI WA KITABU: NINAWEZA, NI LAZIMA, NITAFANYA/NITAFANIKISHA/NITAKUWA (“I CAN, I MUST, I WILL” ) Na: Dkt. Reginald Mengi

Mwandishi wa kitabu hiki Dkt. Reginald Mengi ni moja kati ya watanzania wa mwanzo kabisa kusoma UK, Scotland na kufanikiwa kuwa Mhasibu anayetambulika na Taasisi ya Wahasibu ya Uingereza na Walesi. Aliporudi Tanzania, alijiunga na kampuni ya Coopers Brothers (ambayo baadaye ilikuja kujulikana kama Coopers and Lybrand na sasa PriceWaterhouseCoopers) ambayo aliweza kukua na kufikia kuwa Mshirika Mkuu na Mwenyekiti.

Dkt. Reginald Abraham Mengi ni mwanzilishi, mmiliki na Mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP Limited na Taasisi ya teknolojia na ugunduzi ya IPP(IPP Institute of Technology and Innovation). IPP imewekeza katika vyombo vya habari vya magazeti kama The Guardian, Nipashe na magazeti mengine, pia katika vyombo vya habari vya kielekroniki (ITV, East Africa na Capital televisions pamoja na vituo kadhaa vya radio). Chini ya IPP pia kuna Bonite Bottlers inayoongoza kwa kinywaji cha Coca-Cola na maji ya chupa ya Kilimanjaro. Dkt. Mengi pia amewekeza katika madini, mafuta, gesi, gesi asilia, madawa, kilimo cha mboga mboga katika maeneo makubwa, magari(kuunganisha magari ya umeme), saruji na mambo mengine zaidi katika sekta ya utengenezaji(manufacturing sector).

Dkt. Mengi amewahi pia kuwa katika nafasi kadhaa za uongozi wa umma ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa magazeti Tanzania(Chairperson of Tanzania Standard Newpapers); Kamishna wa kamati inayoshughulikia mishahara(Commissioner of Salary Review Commission); Mwenyekiti wa bodi ya Wahasibu na Wakaguzi Tanzania(NBAA); Mwenyekiti wa Baraza la Taifa La Mazingira Tanzania(National Environmental Council of Tanzania(NEMC); Mwenyekiti wa Vyombo vya habari vya Jumuia ya Madola Tanzania(Chairman of the Tanzania Chapter Commonwealth Press Union(CPU)); Mkurugenzi wa bodi ya LEAD(Leadership for Environment and Development International); Kamishna wa kamati ya Ukimwi Tanzania (Commissioner of Tanzania Commission for AIDS(TACAIDS); Mwenyekiti wa Muungano wa viwanda Tanzania(Chairman of the Confederation of Tanzania Industries(CTI);  Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki(Chairman of the East African Business Council); Mwenyekiti wa ICC Tanzania (a National Committee of the Intenational Chamber of Commerce); Na Mkurugenzi wa Bodi Ya Baraza la Biashara la Jumuiya ya Madola(Director of the Board of Commonwealth Business Council).

Dkt. Mengi kwa sasa ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania(Chairman of the Media Owners Association of Tanzania(MOAT) na Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania(the Tanzania Private Sector Foundation (TPSF)).

Dkt. Mengi ni mtu anayejulikana sana kwa kutoa sana misaada ya kijamii(philanthropist).  Amepewa tuzo mbalimbali kitaifa, kikanda na kimataifa akitambulika sana kwa kazi yake ya kujitolea kwa watu. Amepewa tuzo ya “The Order of the United Republic of Tanzania” mwaka 1994 na “The Order of The Arusha Declaration of the First Class” zilizotolewa na Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania mwaka 1995. Amepewa tuzo ya “The Martin Luther King Jr. Dktum Major for Justice iliyotolewa na Marekani mwaka 2008. Amepewa tuzo ya “The International Order of the Lions Club iliyotolewa na Jumuiya ya Kimataifa ya Lions Club mwaka 2014; na “The 2012 Business For Peace Award” iliyotolewa na Taasisi ya Oslo Sweden ya “Business for Peace Foundation” baada ya kupendekezwa na kamati inayotoa tuzo za Nobeli.

Dkt. Mengi alizaliwa katika kijiji cha Nkuu huko Machame, Kilimanjaro, Tanzania. Baba yake Mr. Abhraham Mengi alizaliwa Marangu, Kilimanjaro, Tanzania lakini baada ya babu yake kufariki ilitokea mivutano juu ya urithi hasa kwenye masuala ya ardhi alilazimika kuhamia Machame ambapo napo licha ya kukutana na changamoto nyingi lakini aliweza kukaa akatulia. Baba yake Mzee Abraham Mengi na mama yake Ndeekyo walibarikiwa watoto saba yeye Dkt. Mengi akiwa kama mtoto wa tano kuzaliwa ambao ni Apaanisa, Elitira, Asanterabi, Karileni, Dkt. Mengi mwenyewe, Evaresta na Benjamin. Familia yao ilikuwa ni familia ya maisha ya chini iliyokuwa inapata mahitaji yake kwa kujihangaisha sana, lakini bado ilikuwa ni familia yenye kujitolea sana katika kujali familia nyingine ambazo zilikuwa duni zaidi kiuchumi.

Dkt. Mengi anasema moja kati ya watu waliomvutia sana katika utoto wake ni kaka yake Elitira aliyekuwa mchapakazi sana na mjasiriamali ambaye alikuwa kati ya watu mwanzoni sana kujenga jengo la ghorofa Moshi mjini.

Dkt. Mengi alianza shule katika shule ya msingi Kisereny Village Bush School, kisha akajiunga Nkuu District School, kisha Siha Middle School, na baadaye Old Moshi Secondary School. Katika maisha yake ya shule tukio kubwa analolikumbuka ni wakati shule yao ya Old Moshi ilipohamishwa kutoka Old Moshi, Kolila na kuhamia Moshi mjini ambapo wanafunzi walikuwa wakitoroka sana shule na kwenda mjini kwa kiwango kikubwa sana. Hivyo yeye kama kiongozi alishauri wanafunzi wasikatazwe kwenda mjini bali wahimizwe kusoma na kuwa na mitihani ya mara kwa mara, ambapo ushauri ulifanyiwa kazi na tabia hiyo ikapungua kabisa.

-Wakati akiwa kidato cha sita katika shule ya sekondari Old Moshi aliona tangazo la KNCU(Kilimanjaro Native Cooperative Union) katika gazeti la pale Moshi la miaka hiyo lililoitwa “KOMKYA” linaita maombi ya watu wanaotaka kwenda kusoma kozi ya miezi sita ya ukarani nchini Scotland UK. Alijua kabisa kuwa ukarani ni jambo la chini sana kwake na endapo angesubiri kumaliza kidato cha sita moja kwa moja angejiunga na chuo kilichokuwa maarufu na kinachokubalika sana miaka ile cha Makerere nchini Uganda moja kwa moja kusoma digrii ya uchumi. Lakini wazo la kwenda kusoma Ulaya lilimvutia sana na pengine lingemvutia mtanganyika mwingine yeyote wa kipindi chake. Japo kulikuwa na changamoto kwamba alikuwa ni mwanafunzi bora sana wa kidato cha sita na mkuu wake wa shule Mr. Mundy alikuwa akilitambua hilo na walikuwa wameshajadili kuhusu yeye kwenda kusoma digrii Makerere College Uganda baada ya kumaliza kidato cha sita. Kwa hiyo alikuwa na hofu kwamba mkuu wake wa shule na familia yake haitakubaliana na uamuzi wake wa kwenda kusoma Ulaya, hivyo alifanya siri kuomba huo udhamini wa masomo ya ukarani ambapo alifanikiwa kuchaguliwa.

Siku chache kabla ya kuondoka aliondoka shuleni Old Moshi na kwenda kujificha katika hostel iliyokuwa inalipiwa na rafiki wa familia yao na kufikiri atajificha hapo mpaka siku anaondoka. Hata hivyo kaka yake mkubwa Elitira alikuwa mjanja na aligundua mipango yake na kumwambia atalazimika kuiweka wazi kwa familia na mkuu wake wa shule ili kupata baraka zao, alifanya hivyo na kilichomshangaza ni kwamba walimshamehe na kumpa baraka zao kwenda kufanya kile alichoamua.

Mwandishi anasema hapa unaweza kuona mchango uliotolewa na vyama vya ushirika Tanganyika katika elimu.

Mwandishi Dkt. Mengi anasema ukiangalia mchango uliotolewa na taasisi kama KNCU Tanganyika hasa katika kuendeleza watu, mtu unaweza kushangaa kwa nini Nyerere alizipinga taasisi hizi kuanzia katikati ya miaka ya 1970. Au labda ni kwa kuwa alikuwa anatafuta kuwa na nguvu kubwa nchi nzima na kwa vile vyama vya ushirika vilikuwa vinaungwa mkono na vilikuwa vina ngavu kubwa kwa watu hasa wa maeneo husika na kama jinsi ilivyokuwa inaonekana vingepingana na mipango yake ya kijamaa, hasa ile ya vijiji vya ujamaa?. Au ni maoni juu ya  yale maendeleo aliyokuwa anasema yanayogusa watu. Haya ni maswali ambayo yamebaki bila majibu.

Vyoyote ilivyokuwa hivi vijiji vya Ujamaa ambavyo Nyerere alivianzisha mwaka 1975 na kupewa hadhi ya vyama halali vya ushirika, vilianguka vibaya mwishoni mwa miaka ya 1980 baada ya sera za mrengo wa kiliberali zilivyoingia chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi chini ya maelekezo ya Benki ya Dunia. Anasema Dkt. Mengi kwamba hata yeye mwenyewe vyama vya ushirika vilimvutia jinsi vilikuwa vinafanya shughuli zake namna yeye mwenyewe binafsi anaisaidia jamii na vyama hivi vilisaidia sana kuinua maisha ya watu vijini yeye mwenye akiwa mnufaika.

Dkt. Mengi baada ya kufika Uskochi(Scotland) alimwambia mwalimu wake Professor Ray kwamba kozi ya ukarani haikuwa lengo lake na kwamba ndoto zake ni kuwa Mhasibu anayetambulika(Chartered Accountant). Professor Ray alistaajabu na kumuuliza kwa nini amesafiri kote huko kutoka Tanganyika mpaka Scotland na kujiweka kwenye mazingira magumu kwani kama lengo lake ni kuwa Mhasibu na anahitaji kuachana na kozi ya ukarani atahitaji fedha za ada ya kulipia uhasibu pamoja  na mahitaji mengine. Aliamua kuachana na kozi ya ukarani na kuomba kujiunga na masomo ya juu ya sekondari A-level kwa njia ya masomo ya jioni(evening class). Alijaribu kuwarudia KNCU kuwaomba kama wanaweza kumpatia ufadhili wa masomo ya juu ya Sekondari lakini walikataa wakasema ni bora wamfadhili mtu mwingine kozi ya ukarani. Ilimbidi kutafuta kazi ya kufanya kwa muda ili aweze kujilipia ada pamoja na gharama nyingine za kuishi. Ilikuwa ni vigumu sana kufaulu vizuri masomo ya Sekondari wakati anayasoma kwa muda mchache wa jioni. Alipitia kipindi kigumu sana akifanya kazi muda mrefu sana na  bado ana ukata wa pesa na presha kubwa ya masomo ya jioni.

Ni mpaka pale kaka yake mkubwa Elitira alipoingilia kati na kumsaidia kifedha na yeye kuweza kuweka muda mwingi kwenye kusoma. Bila hivyo ingemuia vigumu sana kumaliza masomo yake ya sekondari lakini aliweza kumaliza na kufaulu vizuri kiasi cha kuweza kusoma kozi ya Uhasibu aliyoidhamiria sana.

-Dkt. Mengi baada ya kumaliza masomo yake alichangua kurudi Tanzania uamuzi ambao ni tofauti na watu wengi wa kiwango chake cha elimu ambao walichagua kibaki Ulaya ambapo kulikokuwa na fursa za kazi nyingi nzuri na zenye mishahara minono. Alirudi Tanzania mwaka 1971 na kukuta baba yake mzazi alishafariki na hakuweza kushuhudia mafanikio yake hayo. Alipangiwa kufanya kazi ofisi ya waajiri wake ambao ni Cooper Brothers iliyokuwa Nairobi lakini hakukaa muda mrefu akaomba kurudi kufanya kazi katika mji wa nyumbani akapata uhamisho kuhamia ofisi za Cooper Brothers zilizokuwa Moshi. Baadaye aliamua kuhamia ofisi za Dar es Salaam ili kukabiliana na kupata uzoefu kwenye ofisi kubwa zaidi. Alikuja kugundua kwamba Tanzania imegeuka kuwa nchi ya kijamaa inayoongozwa na chama kimoja tofauti na alivyoiacha wakati anaondoka kwenda Scotland.

Utaifishaji wa mali za watu kuzifanya za umma uliofanywa na serikali uliumiza sana watu, mali za kaka yake mkubwa Elitira zilizokuwa Moshi nazo zilitaifishwa na likawa pigo kubwa sana kwa kaka yake mkubwa ambaye alikuwa amemsaidia sana Dkt. Mengi kielimu pamoja na familia yote ya kina Mengi kwa ujumla.

-Mwaka 1973 kampuni aliyokuwa anafanya kazi ya Cooper Bothers iliungana na kampuni ya Lybrand na kuunda kampuni ya C & L expatriates ambapo yeye na Godfrey Urassa walichukua nafasi za juu. Mwaka 1974 wafanyakazi wengi wa C & L expatriates waliondoka Tanzania kwa sababu ya kutofurahia mazingira ya mfumo wa ujamaa na kodi kubwa iliyokuwa inatozwa katika mishahara yao huku yeye akiendelea kupanda vyeo kwenda nafasi za juu zaidi.

Mwandishi wa kitabu hiki Dkt. Reginald Mengi anasema alikuwa ana ndoto za kuandika kitabu juu ya safari yake ya mafanikio, mambo aliyojifunza kwa miaka yote hiyo ili iwe chachu kwa vijana wa kitanzania na Africa kwa ujumla kupata ari ya kuingia kwenye ujasiriamali. Dkt. Mengi anatuambia kwamba mtoto wake wa kiume Rodney ambaye alifariki dunia mwezi Oktoba mwaka 2005 alikuwa akimhimiza sana aandike kitabu kama mtanzania mwafrika aliyeweza kupiga hatua kubwa kibiashara katika mazingira yenye changamoto nyingi kisiasa na kiuchumi.

Dkt. Mengi anatuambia kila mmoja anaweza kufanikiwa anapokuwa ameiweka akili yake katika mtazamo wa “Ninaweza, Ni Lazima, Nitafanya/Nitakuwa/Nitafanikisha”(I can, I must, I will). Nitaweza(I can) mtu anatakiwa kuanza jambo lolote akiwa amehamasika kwamba atafanikisha kwa kujiamini na ujasiri wa hali ya juu. Bila kuwa na ari hiyo ya I Can ni rahisi mtu kushindwa hata kuchukua tu hatua mwanzoni. I must(Ni lazima), hapa mtu anajijengea sababu za kwa nini lazima afanikisha ambayo itasaidia kumjengea nidhamu itakayomsaidia katika kuvumilia anapopitia nyakati ngumu kwani biashara ina changamoto sana. Nitafanya/Nitakuwa/Nitafanikisha(I will), nitabadilisha namna mambo yatakavyokuwa mbeleni kwamba nimedhamiria na nitafanya hivyo kwa uhakika na bila kuacha.

Dkt. Mengi alianza biashara katikati ya miaka ya 1970, wakati huo mfumo wa ujamaa na njia za kiuchumi zikiwa zimeshikiliwa na serikali.

Uongozi wa kisiasa wa wakati huo ulitukuza sana usawa wa kijamaa kwa gharama za maarifa sahihi, maamuzi bora na ubunifu.

Ukweli ulikuwa kwamba wazo tu la mtanzania mwafrika au mtanzania mweusi kuingia kwenye biashara lilikuwa halikubaliki kisiasa. Kinyume chake watanzania wenye asili ya kiasia na kiarabu hawakuonekana kuwa tishio kisiasa ambapo walikuwa wanaruhusiwa kuingia kwenye biashara na hata kusaidiwa kabisa kufanikiwa, ndio maana kufanikiwa katika mazingiri haya ilikuwa ni changamoto hasa.

Mwandishi wa kitabu hiki Dkt. Mengi anasema ile historia na mitazamo ya kijamaa bado inaendelea kuonekana kuiathiri nchi mpaka wakati huu ambao wengi wetu tumepata fundisho kutoka kwenye ujamaa na tunaamini kwamba uchumi wa soko huria ndio njia mpya sahihi inayokubalika kwa sasa. Lakini bado tunaendelea kuona serikali ikisimama kwa sehemu kubwa kama dereva badala ya kuwa mshauri na mwangalizi katika kusimamia uchumi wa nchi. Lakini licha ya changamoto zote za kukosa uhakika wa mwelekeo wa mazingira ya kiuchumi kwa miaka mingi bado Dkt. Mengi ameweza kufanikiwa kibiashara na pengine leo hii sio tu kwamba ni mfanyabiashara mkubwa na maarufu Tanzania bali hata Afrika Mashariki.

Dkt. Mengi anatuambia kwamba bado kuna changamoto sana Tanzania ni bahati mbaya zaidi kwamba imani za kishirikina bado ziko kwa kiwango cha juu sana, ambayo ni ishara ya kwamba bado tuko nyuma sana kijamii kwa matendo kama vile mauaji ya vikongwe, walemavu wa ngozi(albinos) n.k.

Mwaka 1984 Dkt. Mengi alichaguliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa bodi ya wahasibu na wakaguzi wa mahesabu NBAA ili kusaidia kukuza kiwango cha taaluma hii ya uhasibu nchini. Pia mwaka 1985 alichaguliwa kuwa mmoja wa makamishna wa kamati ya mishahara.

Dkt. Mengi anasema namna yoyote ya serikali kuingilia sana biashara na sekta binafsi kwa ujumla ni mbaya kwa biashara iwe biashara hizo zinamilikiwa na serikali au watu binafsi.

Dkt. Mengi anasema kiongozi yeyote kutoka sekta binafsi nchini anayesimama kuikosoa serikali kwa mambo muhimu ya kitaifa kijamii, kiuchumi na kisiasa anaonekana kama adui kwa baadhi na baadhi ya watu wa serikalini.

Tanzania kulianza kupambazuka upya wakati Rais Ali Hassan Mwinyi alipochukua madaraka ya urais kutoka kwa mtangulizi wake  Mwalimu Julius Nyerere na akafungua ukurasa mpya Tanzania ambapo alijulikana na kuwa maarufu kama “Mzee Ruksa” wakati wa Urais wake na hata baada ya kuondoka.

Baada ya kuona watanzania wanateseka sana na mifumo ya kijamaa Rais Mwinyi aliamua kufanya kitu juu ya hilo. Alifikia maamuzi ya kuamua kwamba ilimradi mtu hajavunja sheria basi yuko huru kufanya jambo lolote. Dkt. Mengi anasema “Ruksa” ilimpa furaha na hamasa kubwa, alijua sasa Tanzania inapambazuka upya kiuchumi na sasa anaenda kupata jibu lake la kuonyesha kipaji na uwezo ulioko ndani yake(self actualization).

Hata hivyo Dkt. Mengi anasema kabla ya hapo alikuwa ameshajaribu kuonja nini maana ya kufanya biashara, ambapo mwaka 1983 kalamu ziliadimika sana katika maofisi mengi nchini na alipojaribu kufuatilia akagundua kalamu zimeadimika kabisa nchini. Alijiuliza kwanza ni kwa nini bidhaa hizi zinatoka nje ya nchi na pia kulikuwa na bidhaa nyingine nyingi kama vile dawa za meno, sabuni n.k. ambazo nazo zilikuwa zinategemewa kutoka nje ya nchi na zilikuwa zimekwisha pia.

Karibu kila bidhaa mtu uliyokuwa unaweza kuifikiria iliadimika na uadimu wakati huo ndio ilikuwa habari ya mjini. Hatua ambayo serikali ilichukua juu ya hali hiyo ilikuwa ni kupitisha msako mkali wa polisi kwa kutafuta wale waliosemekana wameficha bidhaa hizi muhimu kwa mahitaji ya kila siku. Wafanyabiashara wengi wakubwa kwa wadogo walikamatwa, kudhalilishwa na kuwekwa kizuizini kwa sheria ambayo ilitumika wakati huo kwa wanasiasa waliokuwa wanaonekana kupingana na serikali.

Njia zilizotumika za kufuata hizi sheria hazikuwa njia sahihi, baadhi ya watu walikamatwa baada ya nyumba zao kukutwa na bidhaa kutoka nje ya nchi kama vile sabuni, dawa za meno, toilet paper n.k. Taratibu za kisheria ziliwekwa pembeni na kunyimwa dhamana kinyume cha sheria ilikuwa ni sehemu ya adhabu badala ya kufuata sheria za kawaida ambapo watu hao walipaswa kufikishwa mahakamani.

Baadhi ya watanzania waliteswa sana vizuizini kwa muda mrefu wakisubiri kufikishwa mahakamani lakini hawakufikishwa. Baadhi waliwekwa mahabusu. Ilikuwa ni kipindi kigumu sana cha kihistoria katika nchi yetu. Kinachosikitisha ni kwamba hali hii ilikuwa ya muda tu lakini baada ya muda nchi ilirudi tena kwenye uhaba wa mkubwa wa bidhaa kwa sababu ya ukweli kwamba hatukuwa na mipango madhubuti.

Kwa maana hiyo biashara ya kalamu aliyoianzisha Dkt. Mengi ilipata mafanikio na kampuni yake ya kwanza ya Tanzania Kalamu Company Limited ilianza kupiga hatua kubwa sana kimafanikio. Hata hivyo biashara hii alikuwa anaifanya kama sehemu tu ya mambo yake(part time) kwani alikuwa bado anafanya kazi kampuni ya C& L expatriates Company lakini baadaye aliamua kuacha na kujiingiza kwenye biashara moja kwa moja.

Dkt. Mengi anasema hata hivyo mazingira ya kibiashara bado hayakuwa rafiki sana Tanzania licha ya “Ruksa” aliyoileta Rais Ali Hassan Mwinyi kwa sababu Nyerere bado alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama na serikali na hakufurahia kuona watanzania wenye asili ya kiafrika(watanzania weusi) wakipiga hatua kibiashara. Mwaka  1987 Nyerere alikosoa waziwazi kuanzishwa kwa kiwanda cha Bonite Bottlers Moshi kwa sababu baadhi ya malighafi ya kiwanda hicho yalitoka nje ya nchi ambapo Mwalimu Nyerere aliita ni “ubepari wa kimarekani”, japo yeye binafsi Dkt. Mengi anafikiri haikuwa sawa kwani kiwanda cha Fahari Bottlers Limited kinachomilikiwa na watanzania wenye asili ya Asia kilichoanzishwa 1983 kilikuwa kimeshaanza kutengeneza bidhaa za Pepsi wakati yeye Nyerere akiwa ni Rais madarakani.

Mwaka 1992 Dkt. Mengi alianzisha makampuni mengi zaidi yaliyokuwa yanazalisha bidhaa mbalimbali za kawaida ambazo zilikuwa ni adimu sana kwa wakati huo. Alikuwa tayari anamiliki biashara kadhaa ambazo ni;- Tanzania Kalamu Company Limited, Anche-Mwedu Limited, Tanpack Industries Limited, Industrial Chemicals Limited ambacho baadaye ilibadili jina na kuitwa Bodycare Limited pamoja na Bonite Bottlers Limited.

Mwaka 1981 Dkt. Mengi alianzisha kampuni kubwa ya uwekezaji iliyokwenda kwa jina la Mengi Associates Limited ambayo mwaka 1988 ilibadili jina na kuitwa Industrial Projects Promotion Limited na baadaye IPP Limited. IPP Limited kwa sasa ni jina linalojulikana sana Tanzania. Dkt. Mengi anasema karibia fedha yote anayotumia kuanzisha makampuni haya inatokana na faida inayopatikana katika kampuni zilizopo.

Dkt. Mengi anasema alikuwa anasita sana kuwekeza katika vyombo vya habari kutokana na uhalisia wa mazingira ya kitanzania kisiasa lakini kufikia mwaka 1993 aliamua kuingia huko kwa kuanzisha Radio One, Itv kisha magazeti kama vile Nipashe, The Guardian n.k.

Dkt. Mengi ni mmoja wa waanzilishi wa CTI(Confederation of Tanzania Industries) Shirikisho la viwanda Tanzania ili kusaidia kujadili na kushirikiana na serikali mambo kadhaa kwa faida ya pande zote mbili. Dkt. Mengi anapongeza uamuzi wa Rais Benjamin Mkapa kuanzisha Tanzania National Business Council(TNBC) mwaka 2004 ambayo ni taasisi ya kitaifa iliyowekwa kisheria kabisa ambayo inaongozwa na Rais mwenyewe kujadili masuala ya kibiashara kwa makampuni ya umma na binafsi. Hata hivyo Dkt. Mengi anaeleza kwamba baada ya Mkapa kuondoka Taasisi hii sambamba na taasisi nyingine za kukuza biashara kama vile TCCIA, CTI, TPSF hazikupewa kipaumbele sana.

Dkt. Mengi anasema kilimo ni sekta ambayo inaweza kutumika kuondoa umaskini Tanzania na kupambana na tatizo sugu la ajira kwa vijana Tanzania. Anasema Ethiopia ni mfano mzuri wa namna sera nzuri za kilimo na utekelezaji wake unavyoweza kufanikiwa. Anasema wote tunafahamu jinasi miaka ya 1980 Ethiopia ilikuwa inakumbwa na tatizo la njaa na utapiamlo kiasi cha kupelekea jamii ya kimataifa kuingilia kati kuisaidia. Leo hii Ethiopia ile ile imefikia hatua inazalisha mpaka ziada na inauza mpaka China na nchi za Magharibi. Anasema haoni sababu kwa nini Tanzania ishindwe kuzalisha kwa kiwango hicho, kwa sababu bila mashaka yoyote linapokuja swala la kilimo Tanzania kuna fursa kubwa(sleeping giant).

Dkt. Mengi anatuambia kwamba tafiti zinaonyesha kwamba bonde la mto Ruvu peke yake linaweza kulisha Afrika Mashariki yote, eneo la Kilombero linaweza kulisha kulisha Afrika ya Kati yote kwa mchele, wilaya ya Kyela peke yake inaweza kuzalisha mchele wa kulisha Afrika Magharibi yote, bonde la Rufiji linaweza kulisha Afrika ya Kaskazini ikijumuisha Sudan, Ethiopia na Somalia, na maeneo ya Wami na Arusha Chini yanaweza kuzalisha mchele wa kutosha kulisha Kusini ya Afrika yote. Kwa kifupi ni kwamba Tanzania ina ardhi yenye rutuba na maji ya kutosha kuzalisha chakula cha kulisha Afrika nzima. Dkt. Mengi anasema haya mambo sio yakufikirika tu bali yanaweza kufanyika kabisa. Hata hivyo kipindi cha ukoloni Tanganyika ilikuwa ndio ghala la Afrika Mashariki.

Dkt. Mengi kutokana na kwamba pia alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki(Chairman of the East Africa Business Council(EABC)) na yeye kama mtanzania anaweza kuona kwamba serikali yetu na baadhi ya viongozi na watu wa kawaida wanafikiri kwamba kwa sababu Kenya imepiga hatua zaidi kiuchumi kuliko Tanzania, ushirikiano utapelekea Kenya kufaidika zaidi. Kwa mtazamo wake anasema ni mawazo ya ajabu kwa watanzania kufikiri kwamba Kenya itaendelea kutawala kiuchumi Afrika Mashariki muda wote. Anasema Tanzania ina fursa na nafasi kubwa zaidi ya kufaidika sana na ushirikiano wa ukanda huu kwa sababu ina rasilimali nyingi zaidi kuliko majirani zake ambao ni msingi mzuri wa kujenga uchumi imara, hasa elimu bora na kuendeleza rasilimali watu vikipewa kipaumbele. Namna anaona hili shirikisho ni kwamba kila mtu atashinda/atafanikiwa(win-win) na nchi zinazoonekana kuwa nyuma kiuchumi ndizo zitafaidika zaidi baada ya muda mrefu kidogo. Unatakiwa uwe ushirikiano mzuri ambapo washirika wanasaidiana kutengeneza pesa na sio mmoja kuvuna kwa mwingine.

Dkt. Mengi anasema kuhusu maswala ya uwekezaji tunatakiwa kuongeza umakini kwa sababu kwa sasa wawekezaji ndio wananufaika zaidi na sio wazawa. Tunahitaji/tunapaswa kuwawezesha watu wetu watazanzania waafrika zaidi kuliko watu kutoka nje.

Dkt. Mengi anaamini kwamba biashara sio kwa ajili tu ya kupata faida tu bali pia kwa ajili ya majukumu ya kijamii kama vile ujasiriamali wa kijamii n.k. Dkt. Mengi anasema mfano wa namna mchango kidogo kwa jamii unaweza kuleta matokeo makubwa unamhusisha yeye mweyewe alipotembelea vijiji viwili mkoani Kilimanjaro vya “Kimashuku” na “Mbokomu Korini”. Alitembelea kijiji cha Kimashuku miaka ya 1990 na kukuta msitu wa uoto wa asili uliokuwa umefunga sana umepotea na kwa vile ndio ulikuwa unasababisha chemchemi za maji basi nazo zimekauka na zilizobaki ni za msimu tu. Anasema aliamua kuchangia pesa kidogo kwa ajili ya mradi wa upandaji miti na miaka michache baadaye uoto ule wa msitu uliofunga ulirudi kama ulivyokuwa awali, wanyama wa msituni nao walirudi na chemchemi zile za milimani zilianza tena kuteremsha maji. Mchango wake huo mdogo uliweza kusaidia kuondoa ukame huo.

Kwa upande wa kijiji cha Mbokomu Korini ilikuwa ni kikundi cha wanawake waliokuwa na miradi yao binafsi ya kiuchumi kwa ajili ya kujiendeleza. Alipotembelea kikundi hiki alihitajika kuwasaidia katika mradi wao wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Msaada huo ulitolewa kwa kuwanunulia ng’ombe wa maziwa, vifaa pamoja na gharama za kujifunza ufugaji wa ng’ombe. Anasema msaada ulikuwa ni mdogo lakini matokeo yalikuwa makubwa. Wanawake hawa waliweza kujenga nyumba zao wenyewe, kusomesha watoto na kuboresha maisha yao kwa ujumla.

Dkt. Mengi anasema ujasiriamali wa kijamii na kusaidia miradi ya kukuza na kuiendeleza jamii ndivyo vinatambulisha maisha yake. Kuanzia mwaka 1987 Dkt. Mengi amekuwa akisaidia upandaji miti kuzunguka mlima Kilimanjaro kwa sababu amekuwa akiona msitu ukipungua katika mlima Kilimanjaro. Anasema mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 2014 zaidi ya miti milioni 24 ilikuwa imepandwa na anategemea kuanzisha mradi mwingine wa upandaji miti kuanzia mwaka 2018. Kwa mchango huu katika mazingira Rais Mkapa alimchagua kuwa Mwenyekiti wa Baraza la kusimamia Mazingira Tanzania(NEMC)National Environmental Management Council licha ya kwamba anatokea katika sekta binafsi.

Baada ya kuona uharibifu wa mazingira ya mlima Kilimanjaro yanavyoathiri maisha ya kiuchumi na kijamii ya watu wanaoishi kuzunguka mlima Kilimanjaro Dkt. Mengi ametambua kwamba kulinda mazingira ni kwa maslahi ya kibiashara, yaani kiuhalisia ni kwa maslahi ya uhai wa biashara.

Kila mwaka kuanzia mwaka 1994 kampuni ya IPP imekuwa ikiandaa na kudhamini tukio kubwa la kitamaduni sambamba na chakula cha mchana, ambapo lengo lake ni kujenga ujasiri na kutambulika kwa raia wenye ulemavu kufurahia kama wengine wasio na ulemavu ambapo wanapata sehemu ya kukutana kubadilishana mawazo na kuzungumzia changamoto zao lakini pia na matumaini yao na matarajio ya mbele. Dkt. Mengi anasema watu hawa ni wa thamani na wanaweza kujengewa kujiamini kama sisi wote tutawaheshimu na kuthamini utu wao.

-Mwaka 2014 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alimpatia Dkt. Mengi  tuzo ya taifa katika mambo ya kuisaida na kuiwezesha jamii hasa katika ujasiriamali wa kijamii “The National Philanthropy Award” katika sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Dkt. Mengi anasema anamwamini Mungu na anaamini Mungu ndiye aliyemsaidia kufanikisha yote hayo.

Dkt. Mengi anasema falsafa yake ipo katika kuwajenga vijana kufanikiwa kwa kwa kuwajengea kujiamini wajiendeleze na kujiwezesha wenyewe.

Dkt. Mengi anasema watanzania waafrika(watanzania weusi) walinyimwa fursa ya kuendelea kutokana na kwamba miaka hiyo ya mwanzo ya nchi hii iliaminika kwamba endapo watanzania waafrika(watanzania weusi) watapata nguvu kupitia sekta binafsi wanaweza kuyumbisha siasa za nchi hii na matokeo yake pia nguvu za kisiasa zinaweza kuchukuliwa na matajiri watanzania waafrika(watanzania weusi)

Dkt. mengi anasema yeye kukubali kwa Mwenyekiti wa sekta binafsi Tanzania(Chairman of TPSF) ni kwa sababu aliamini atakuwa na uwezo wa kuhamasisha na kuamsha ari mpya katika sekta binafsi Tanzania kuweza kuwawezesha wazawa/raia wakitanzania kumiliki na kuendesha uchumi wa Tanzania.

Dkt. Mengi anasema uwekezaji wa ndani una matokeo makubwa kuliko uwekezaji kutoka nje. Anasema kwamba kukosa mitaji ya kutosha, teknolojia na ujuzi katika mambo ya usimamizi hakutakiwi kuwa visingizio vya kuweka sera za kuwapendelea wawekezaji kutoka nje. Anasema pale ambapo inapoonekana kwamba inatakiwa kuwaruhusu wawekezaji kutoka nje basi inapaswa kuwe na ubia kati ya wawekezaji wa ndani na wawekezaji hao kutoka nje.

Dkt. Mengi anasema moja kati ya sababu za yeye kuamua kuwekeza katika tasnia ya vyombo vya habari ni pamoja na kuweza kupambana na rushwa ambayo ina madhara makubwa katika ustawi wa jamii. Mwezi Aprili mwaka 2009 Dkt. Mengi aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea jinsi rushwa imefikia hatua ya hatari na kutaja majina ya watu watano ambao kila mara wamekuwa wakihusishwa na ufisadi mkubwa ambao walitajwa kama “mapapa wa ufisadi mkubwa” na kuhoji kwa nini serikali haiwachukulii hatua watu hao.

Kwa kutambua juhudi zake hizo za kupambana na rushwa na ufisadi nchini mwaka 2008 serikali ya Marekani ilimpatia tuzo ya “Martin Luther King Jr. Dktum Major Award”

Dkt. Mengi yeye kama Mwenyekiti wa wamiliki wa vyombo vya habari Tanzania (MOAT) Media Owners Association of Tanzania katika kukemea na kulinda waandishi wa habari ambao wamekuwa wahanga wa kudhuriwa wakiwa katika kazi zao kwani amekuwa akiwachukulia kama mashujaa, ambapo pia amekuwa akisaidia matibabu yao ndani na nje ya nchi.

Katika kuchagua nani wa kufanya naye kazi Dkt. Mengi anasema anaamini kwamba licha ya kwamba kipaji na uwezo siku zote vimekuwa ni vitu muhimu sana vya kuviangalia lakini amekuwa akivilinganisha pia na uaminifu na kujituma/kujitoa sana(trust and commitment). Hii ni kwa sababu anaamini uwezo mkubwa unaweza kuendelezwa/kujengwa lakini huwezi kujenga uaminifu na kujitoa sana kwa mtu. Dkt. Mengi amewataja Zoeb Hassuji wa Bonite Bottlers Limited na Joyce Mhaville wa Itv na Radio One kama wakurugenzi wake bora zaidi wanaofanya vizuri na wenye sifa alizozitaja.

Dkt. Mengi anasema kutoa nafasi ya kusikia nini wengine wanasema, ambapo inamaanisha kusikiliza wateja au watu unaofanya nao kazi au wakati mwingine hata washindani wako wa kibiashara ni njia bora sana ya kufanikiwa. Anasema mtoto wake Rodney alikuwa na uwezo mkubwa katika kusikiliza na matokeo yake aliweza kuja na mapinduzi makubwa katika kuwafikia vijana wa Afrika Mashariki ambapo yeye kama Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa East Africa televisheni na Radio alijua kwamba vijana wa Afrika Mashariki wanahitaji kuwa na chombo cha kuwakilisha vyema na kukuza/kuendeleza utamaduni wao na maslahi yao ya kijamii.

Dkt. Mengi anamalizia kwa kusema maoni yake ambayo ataendelea kuyasimamia na kuhamasisha kwa nguvu zote, ni kwamba haiingii akilini kuwakatalia raia wa nchi hii haki ya kumiliki na kuendesha uchumi wa nchi yao eti hawana mtaji wa kutosha, mbinu na teknolijia ya kisasa. Kama tunajua hivyo inakuwaje sasa tunaweka sera na sheria hizi kumwezesha mzawa? Bado tuna tatizo kati ya sera na utekelezaji.

Haya ni machache sana kati ya mengi ya kufundisha, kuelimisha na kuhamasisha sana yaliyopo katika kitabu hiki bora sana na ambacho mimi binafsi kimenifungua sana hasa ukizingatia ni kijana ambaye mengi niliyoyasoma sikuyajua kabisa hivyo yamenipa mtazamo wa tofauti na nilivyokuwa kabla.

Napenda kukuhimiza na kusisitiza utafute kitabu hiki ukisome mwenyewe utajifunza mengi usiyoyajua hasa kama wewe ni kijana mwenzangu na una ndoto kubwa katika maisha yote

Ahsanteni sana

Uchambuzi Na:

 Mary A. Assenga +255672508523 Whatsapp/Piga

Facebook Comments
Recommended articles