UAMBISHAJI

By , in Sarufi na Utumizi Wa Lugha on .

Neno uambishaji linatokana na kitenzi kuambisha ambalo nalo latokana na kitenzi kuamba. Kuamba maana yake ni kukifunga kitu fulani kwenye kitu kingine ili kibakie hapo; au kukinatisha kitu fulani kwenye kitu kingine. Neno kuambisha lina maana ya kukifanya kitu kinate mahali fulani.  

Katika Kiswahili, uambishaji unafanyika kwa kuongeza mofu fulani mwanzoni au mwishoni mwa mzizi wa neno. Kwa mantiki hii, maneno yanayoundwa hupewa maana ama mpya, au ya ziada au hata yakageuza hali yake ya asili na kuchukua nafasi nyingine katika muundo wa kishazi. Kinachoambishwa huitwa kiambishi ambacho, aghalabu, hubeba maana katika lugha; na kwa mantiki hiyo, kiambishi ni sawa na mofu.

Kwa mfano, katika neno piga, pig ni mzizi, na a ni kiambishi/mofu ishilizi au tamatishi katika kila kitenzi asilia cha Kiswahili.           

           

Tunaweza kunatisha viambishi kadhaa mwanzoni mwa mzizi pig kama ifuatavyo:

           

            tu-ta-m-pig – a,

lakini pia tunaweza kunatisha viambishi kadhaa mwishoni mwa mzizi uo huo pig kama ifuatavyo:

                 

            pig-an-ish-a

au hata pengine tunaweza kuvinatisha viambishi vya mwanzoni na vya mwishoni mwishoni mwa mzizi huo huo pig na kupata tungo kama ifuatavyo:

            tu-ta-m- pig –an-ish-a; au

            tu-ta-m-pig – an-ish-a-je ?  (na wenzake).

Facebook Comments
Recommended articles