TOFAUTI KATI YA LUGHA YA BINADAMU NA MAWASILIANO YA WANYAMA

By , in Sarufi na Utumizi Wa Lugha on . Tagged width:

Kwa mujibu wa Masamba na Wenzake Mwaka (1999: 1) “Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo hutumiwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao”.

Pia kwa mujibu wa NKWERA F.M.V (1979) “Lugha ni utaratibu (mfumo) maalumu wa sauti za nasibu zenye maana ambazo hutumiwa miongoni mwa binadamu kwa madhumuni ya mawasiliano miongoni mwao sauti hizi lazima ziwe za kutamkika”.

Hivyo basi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali walioeleza maana ya dhana ya Lugha. Lugha ni utaratibu maalumu wa sauti za nasibu ambazo huodhi maana katika jamii fulani sauti hizi hutumiwa na wanajamii hao kwa kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao.

Binadamu hutumia lugha kama nyenzo kuu ya mawasiliano tofauti na wanyama wengine. Kwa mujibu wa kamusi ya karne ya 21 kamusi ya Kiswahili. “Mawasiliano ni upashanaji wa habari kwa kutumia barua, simu au vyombo vya habari kama vile redio na televisheni’

Mawasiliano ni kubadilishana ujumbe (habari) baina ya wawasilianaji mfano, mtu na mtu ama mtu na kikundi. Pia wanyama huwa wanawasiliana na mawasiliano yao yana husisha ishara na sauti tofauti na binadamu ambaye hutumia lugha. Hivyo kuna tofauti baina ya Lugha za binadamu na mawasiliano ya wanyama kama ifuatavyo;-

 

Uwili; Lugha ya binadamu huwa na uwili yaani inajitokeza katika viwango viwili Sauti na Maana katika sauti Mofu, Fonimu, na Lekisimu viwango hivi huunganishwa ili kupata neno lenye maana tofauti, kwa mfano fonimu    maneno    sentensi lakini katika mawasiliano ya wanyama hayawezi kuchanganuliwa kwa kuanzia kipashio kidogo hadi kikubwa

Lugha ina sifa ya ubunifu au uzalishaji; Binadamu katika kuzungumza anauwezo wa kubuni na kuweza kuunda maneno mapya na hata kuzungumza maneno mengi katika kuelezea jambo au mada fulani kwa wakati mmoja kwa mfano, kutokana na neno lima tunaweza kupata maneno kama vile limia, limiana, limika, limisha. Maneno haya yana maana tofautitofauti na zinaeleweka. Tofauti na  mawasiliano ya wanyama ambapo wanyama wanaidadi mahususi za ishara na sauti. kwa mfano ng’ombe anapohisi njaa hawezi kutoa mlio tofauti na ule aliozoea kuwasilisha ujumbe kuwa ananjaa anahitaji chakula.

Lugha ya binadamu hutumika ghafla na kuna kubadilishana zamu; lakini katika mawasiliano ya wanyama hamna kubadilishana zamu binadamu anaweza kuzungumza maswala mbalimbali kwa wakati mmoja, pia binadamu hawazungumzi kwa pamoja bali huzungumza kwa zamu, kunakuwapo msemaji na msikilizaji kwa mfano mahojiano kati ya daktari na mgonjwa mgonjwa anapomuelezea daktari, daktari huwa ni msikilizaji na wakati daktari anapomshauri mgonjwa, mgonjwa huwa msikilizaji hivyo hali ya kubadilishana zamu hutokea. Hali hii ni tofauti na mawasiliano ya wanyama. Mfano nguruwe wanapoitaji chakula hulia wote kwa pamoja

Umakinikaji; binadamu huweza kuendelea kuzungumza ilihali anaendelea na jambo lingine mfano anaweza kuwa analima huku anaongea masuala tofauti na kilimo mfano siasa ,michezo na afya  lakini wanyama huzama katika kile wanachokitenda tu , kwa mfano mbwa anapobweka husitisha shughuli zote na kuzama katika kitendo cha kubweka.

Unasibu; lugha ya binadamu haina uhusiano halisi wa dhana ya  kirejelewa au kitajwa na hutumia sauti, ishara, alama na maneno. Mfano neno nyumba halina uhusiano wa  moja kwa moja na kirejelewa chake ndio maana hurejelewa kwa majina tofauti mfano house (kiingereza), enju (kihaya ) na ekhaa (kiganda) lakini mawasiliano ya wanyama yana uhusiano kwani ishara wanazotumia mfano paka hukunjua makucha yake kuashiria utayari wake kumshambulia adui wake . Aidha ni maneno macheche tu yenye uhusiano wa moja kwa moja na virejelewa vyake mfano nyoka (umbo) na pikipiki (sauti).

Viwango vya uundaji; katika Lugha binadamu huwa na viwango maalumu vya uundaji kwa mfano, sauti/b/ huunda fonimu/ba/ na fonimu huunda mofimu au maneno/baba/ ambayo nayo pia huunda kirai (kisu kikali) ambacho huunda kishazi kinachounda sentensi ambayo huunda kifungu cha habari au habari kamili (kisu kikali kimeibiwa) tofauti na mawasiliano ya wanyama hakuna viwango vya uundaji.

Lugha ya binadamu huwa na sifa ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali; utekelezaji huu unaweza kuwa kama vile kusali, kuimba, kutoa nasaha, kutoa hotuba, ahadi kwa mfano,  baba alimwahidi mwanae kumsomesha. Ila  kwa upande wa mawasiliano ya wanyama huwa ni kufikisha ujumbe tu haitekelezi majukumu tu.

Usambavu; Lugha ya binadamu huwa na sifa ya usambavu ambayo humsaidia mwanadamu kuelezea juu ya vitu vilivyombali kijografia na kihistoria, pia matumizi ya maandishi, maneno na ishara, Binadamu hutumia maandishi, Ishara na maneno kuzungumzia dhana yeyote kwa upana wowote ule bila upeo au kikomo pamoja na kuelezea yaliyopita, yaliyopo na yajayo.hii ni tofauti na mawasiliano ya wanyama kwa sabababu hawana uwezo wa huu wa usambavu kwa mfano panya hawezi kuwahadisia watoto wake alivyonusulika kuliwa na paka mwezi uliopita  binadamu huweza kurejelea matukio yaliyopita ya sasa na yajayo.

Hufungamana na utamaduni wa jamii husika; lugha ya mwanadamu hurithishwa kizazi kimoja kwenda kizazi kingine kupitia utamaduni wa jamii husika au utamaduni  na mazingira ambayomtu amekulia , mfano motto yeyote ana uwezo wa kuzungumza lugha yeyote duniani kutegemeana na mazingira auutamaduniambayo amewekewa kukuliamfano  motto wa kimasai anapozaliwa ,anapolelewa na kukulia katika utamaduni na mazingira ya kizungu tofauti na wanyama ambao huzaliwa na mlio ambayo wanaitoa na wala hawawezi kubadilishana utamaduni na mazingira , mfano hata ng’ombe akiwekwa na mbuzi hawezi kujifunza utamaduni wa mbuzi wala sauti na ishara za mbuzi japo wako katika mazingira  yapamoja.

Hitimisho; kwa mtazamo huu lugha ya binadamu hutofautiana na mawasiliano ya wanyama, hivyo utofauti hizo zinatokana na sifa bia za lugha. Hata hivyo  ni vigumu kuelewa vipengele mbalimbali vya mawasiliano ya wanyama kwa uwazi unaodhihirika tofauti na lugha ya  binadamu kwani wanyama hawana lugha halisi iliyodhahiri bali huwasiliana kwa ishara tu.

 MAREJELEO

Matinde R.S (2012) Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, Serengeti Editor Publishers (T) Ltd, Mwanza –Tanzania.

J.S.Mdee,K. Njogu,Shafi,A. (2011) .Kamusi ya kiswahili ya  karne ya  21,Longhorn Publishers (T)  Ltd, Dar es salaam –Tanzania.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!