TATHIMINI YA MATINI ILI  KUTAMBUA UBORA NA UDHAIFU WAKE KATIKA TAFSIRI

By , in TAFSIRI/UKALIMANI on .

TATHIMINI YA MATINI ILI  KUTAMBUA UBORA NA UDHAIFU WAKE KATIKA TAFSIRI

Tuanze  na maana ya matini kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali kama vile ;Wamitila (2003) ameeleza kuwa matini inaweza kueleezwa kama kifungu cha maandishi au usemi wa lugha. Huweza kuelezwa  kwa kuangalia maumbo  ya kazi yake.

Oxford dictionary (2000) inaeleza matini kuwa ni andiko au chapisho linalohusu maudhui zaidi kuliko fani. Kutokana na maana hii tunaweza kusema kuwa si matini zote huzingatia zaidi kipengele cha fani na kuacha maudhui bali zipo ambazo huweka usawa katika vipengele hivyo na nyingine kama za kisiasa na zile za kisayansi zinahusisha zaidi kipengele cha maudhui kuliko fani. Hivyo kutokana na fasili zilizotolewa na wataalamu tunaweza kufasili matini kuwa;

Ni wazo au mfululizo wa mawazo ambao unajitosheleza kimaana. Au matini yaweza  ni neno moja, kirai, kishazi, sentensi, aya, au kifungu cha habari ambacho kinajitosheleza kimaana chenye ujumbe au wazo linalojitosheleza.

Katika tafsiri tunafanya tathimini ili kujua ubora na upungufu wa tafsiri husika. Neno tathini wataalamu wanatueleza kama ifuatavyo:

Wamitila (2003) anaeleza kuwa; kimsingi tunapotaja tathmini kuhusina na kazi za kifasihi humanisha kupima ubora na udhaifu wa kazi inayohusika. Mhakiki anaweza kupima kazi hiyo kwa kuiangalia maudhui yake au muundo wake kwa ujumla.

Lakini kutathmini tafsiri ni zoezi la kupima kiwango cha ubora wa tafsiri husika kwa kutumia mbinu zilizokubalika. Hivyo tunavyofanya tathmini ya tafsiri tunaweza kupata makundi makuu manne. Makundi hayo ni kama yafuatayo;

  • Tafsri bora
  • Tafsiri tenge
  • Tafsiri finyu
  • Tafsiri pana.

Katika kufanya tathmini kuna aina kuu mbili za matini ambazo zinaweza kufanyiwa tathmini, matini hizo ni kama  zifuatazo;

Matini lengwa zilizo katika mchakato wa kutafsiriwa. Matini hizi ni zile ambazo hazijafikishwa kwa mteja. Katika matini hizi mfasiri anaweza kutathmini tafsiri yake kwa lengo la kuiboresha kabla ya kuipeleka kwa mteja.

Matini lengwa zilizo katika mikono mwa mteja. Matini hizi mfasiri hufanya tathmini kwa lengo la kutoa maoni ambayo yatamwezesha mfasiri kuboresha kazi nyingine atakazozifanya baadae au kama atatoa toleo jingine.

Katika kufanya tathmini,  tamthiliya hii ya “Black Hermit” iliyoandikwa na Ngugi wa Thiong’o (1968) na kutafsiriwa kama “Mtawa Mweusi” na East African Educational Publishers Ltd. (2008), tumetathmini kwa kuangalia vipengele vifuatavyo;

Sarufi; katika kipengele hiki tumeangalia uzingativu wa vipengele vya kisarufi kama vile upatanisho wa kisarufi na upotoshaji wa maana.

Jukumu la kwanza la mfasiri ni kuhakikisha kwamba anazingatia na kuhifadhi upatanisho wa kisarufi wa matini chanzi. Lakini wakati mwingine jukumu hili halitekelezeki mfano wafasiri wa tamthiliya ya “Black Hermit” iliyotafsiriwa kama “Mtawa Mweusi” hawajazingatia upatanisho wa kisarufi na kufanya matini ya tafsiri ipoteze ubora wake.

      Mfano : Matini chanzi:  sorting out beans spread  in a basin. (Uk 1)

                   Matini lengwa:  akichagua harage katika bakuli. (Uk1)

                   Matini chanzi: if this be a curse put upon me (uk4)

                   Matin lengwa: kama hili ndilo laana nililopewa…(uk4)

Katika tafsiri ya kiswahili neno la kiingereza “beans” limefasiriwa kama “harage” badala ya “maharage” na pia katika tungo ya kiingereza “if this be a curse put upon me” limetafsiriwa kama “kama hili ndilo laana nililopewa”badala ya“kama hii ndio laana” tungo hizi zimefanya kukosekana kwa upatanisho wa kisarufi katika matini lengwa.

Katika suala la maana yawezekana mfasiri akachagua maana isiyo sahihi kati ya maana nyingi zilizo katika lugha lengwa za neno katika lugha chanzi. Mfano

Matini chanzi:                                                             Matini lengwa

… in a basin (uk1)                                                  : …katika bakuli(uk1)

 …carrying                                                            …akichukua

Do without husband                                          siwezi kuishi bila mwanaume

I have tasted the pains of beating               nimeona maumivu ya mapigo.

Katika tafsiri ya Kiswahili neno la kiingereza “basin” limefasiriwa kama “bakuli” badala ya “beseni”, neno “carrying”limetafsiriwa kama “akichukua” badala ya “akibebelea”, neno “do” limetafsiwa kama “kuishi” badala ya “kufanya” na neno “tasted” limetafsiriwa kama “nimeona”  badala ya “nimeonja”. Uteuzi wa maana za  msamiati katika matini legwa umepotosha maana iliyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi.

Kipengele cha pili ni muundo; kipengele hiki kinahusu ulinganifu wa mpangilio kati ya matini chanzi na matini lengwa. Tamthiliya ya “Black Hermit” ambayo ni matini chanzi imetumia muundo sahihi wa tamthiliya ambapo majina ya wahusika yanatokea kushoto. Lakini matini lengwa ambayo imetafsiriwa kama “Mtawa Mweusi” wafasiri wameitafsiri kwa muundo wa filamu, ambapo majina ya wahusika yamejitokeza katikati ya maelezo ya wahusika hivyo kukiuka muundo wa matini chanzi.

Vipengele vingine ambavyo tunaweza kuvifanyia tathmini katika tafsiri hii ya “Mtawa Mweusi” ni kama vile udondoshaji, upunguzaji na uteuzi mbaya wa maneno.

Udondoshaji; wafasiri wa matini hii kuna baadhi ya maneno ambayo ni ya msingi kukamilisha wazo au habaha ya msanii au mwandishi hayajitokeza ambayo yalikuwapo katika matini chanzi. Kwa mfano;

                Matini chanzi:  This temptation harping on weak flesh (uk4)

                Matini lengwa; Jaribu hili linalirudia rudia mwili wangu (uk.5)

                                                                      

Neno “weak” ambalo lipo kwenye matini chanzi halijafasiriwa katika matini lengwa na lilipaswa kufasiriwe kama “dhaifu”.

Uongezaji; katika matini lengwa kuna baadhi ya misamiati imeongezwa na wafasiri wakati katika matini chanzi haijatokea.

Mfano;

Matini chanzi:  A woman without a child is not a woman.  Uk. 4

Matini  lengwa:  Mwanamke bila mtoto si mwanamke timamu.   Uk 3

Neno “timamu” lililotumiwa na wafasiri wa matini lengwa halipo kabisa katika matini chanzi.

Uteuzi m’baya wa msamiati; katika tafsiri ya “Mtawa Mweusi” wafasiri wameteua na kutumia visawe ambavyo vimesababisha upotoshaji wa ujumbe katika matini lengwa. Mfano wa viswe hivyo ni pamoja na :

Matinichanzi:  Have seen sunrise and sunset. (pg. 3)

                        I have tested the pains of beating. (pg. 3)

                        Together with power of the tribe. (pg. 10)

Matini  lengwa: Yameona  kuchomoza na kuingia kwa jua. (uk. 3)

                           Nimeona maumivu ya mapigo. (uk. 4)

                           Pamoja na nguvu ya taifa. (uk. 10)

Katika matini ya lengwa wafasiri wameteua na kutumia visawe visivyokubalika kulingana na visawe vilivyotumika katika matini chanzi. Wafasiri wametumia neno “I have tested” kama “nimeona” badala ya “nimeonja” pia neno “tribe”likafasiliwa kama “taifa”.

Katika kufanya tathmini hususani katika kazi hizi mbili za tamthiliya tafsiri iliyofanyika ina mapungufu katika kila kipengele ambavyo ni msingi kuvizingatia wakati wa kufanya tafsiri. Vipengele hivi vimewakumba wafasiri wa tamthiliya labda kutokana na sabau za kutofatiana kiutamaduni, ujuzi wa lugha hizi kwa wafasiri wenyewe.

Marejeo

East African Educational Publishers Ltd (2008) Mtawa Mweusi. Kenya: Sitima Printers  Stationers Ltd

Ngugi wa Thing’o (1968) Black Hermit. Kampala-Uganda: East African Educational Publishers Stationers Ltd

Oxford Dictionary (2010) Oxford Advanced Learner’s Dictionary of Current English. New York: Oxford University Press.

Wamitila, K.W (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi-Kenya:Focus: Publication Ltd.

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!