TANZU ZA FASIHI SIMULIZI (NUKUU ZA KIDATO CHA V-VI)

By , in Fasihi Simulizi Kidato V-VI on . Tagged width:

TANZU ZA FASIHI SIMULIZI (NUKUU ZA KIDATO CHA V-VI)

 

 1. Hadithi

Hadithi ni tungo za Fasihi za masimulizi zitumiazo lugha ya nadhari (lugha ya ujazo, ya maongezi ya kila siku). Masimulizi hayo hupangwa katika mtiririko wa vituko unaokamilisha kisa. Ili kisa hiki kikamilike, hadithi huwa na wahusika ambao ndio nyenzo ya kukiendeshea kisa chenyewe, vivyo hivyo hadithi huwa na maudhui.

Aina za hadithi

 • Ngano: hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kueleza au kuonya kuhusu maisha. Kwa kawaida ngano ni hadithi za maadili ambazo husimuliwa katika mazingira ya starehe nazo huadili kwa kutumia istiara, kharifa, hekaya, kisa, mbazi, n.k.

Ngano huwa na wahusika wa aina mbalimbali, wadudu, wanyama, binadamu, mizimu na miungu au viumbe visivyo na uhai kama vile mawe, miamba, n.k. wahusika hawa hupewa urazini wa binadamu ili kuadilisha.

 • Tarihi:ni hadithi ambazo husimulia kuhusu matukio ya kihistoria. Matukio haya yanaweza kuwa ya kweli au ya kubuni. Matukio haya yanafumwa kisanii ili kuwavutia watu. Mara nyingi wahusika wake ni binadamu ila hupewa uwezo mkubwa au mdogo mno kulingana na matukio yanayosimuliwa.
 • Visasili: ni hadithi zinazotumia wahusika wa aina mbalimbali, pamoja na miungu na binadamu. Hadithi hizi husimulia mambo yanayohusiana na maumbule ya watu, wanyama, miti na vitu visivyo na uhai. Pia huhusisha maumbile hayo na ada au taratibu za jamii inayohusika. Kwa mfano ili kukanya ukosefu wa heshima masimulizi hueleza kuwa tabia ya sungura ya kunusa nusa vitu iliwaudhi watu hata wakamkata mkia. Ndiyo maana sungura ana mkia mfupi. Pia hadithi hizi hueleza vyanzo na taratibu za miviga,imani na dini za jamii fulani. Mara nyingi hadithi hutambwa kwenye miviga.
 • Kigano: ni hadithi fupi zinazoeleza makosa au uovu wa watu fulani na kueleza maadili yanayofaa. Kigano mara nyingi hutumia methali kama msingi wa maadili yake. Kwa mfano, kigano kinaweza kueleza kuhusu mzazi anayempenda mno mwanawe wa pekee. Kwa hiyo hakuthubutu kumkemea au kumrudi yule mtoto. Hatimaye mtoto alijenga tabia nyingi mbaya. Basi simulizi husema kwa methali ‘mchelea mwana kulia hulia yeye’. Kwa kawaida kigano hujengwa kwenye kisa kimoja tu. Hali hii inasaidia hadhira kuelewa jambo lile na kulikumbuka.
 • Soga: Ni hadithi fupi za kuchekesha na kukejeli. Wahusika wa soga ni watu wa kubuni. Hata hivyo kwa kuwa soga inakejeli hali inayohalisika, wahusika wanapewa majina ya watu walio katika mazingira hayo. Soga husema ukweli unaoumiza, lakini ukweli huo unajengewa kichekesho ili kupunguza ukali wa ukweli huo.

Fani Katika Hadithi

Muundi

Muundo wa hadithi za Fasihi simulizi ni wa moja kwa moja ambao una mwanzo-kati-mwisho.

Mwanzo Msimulizi: Hadithi, hadithi….Wasikilizaji: hadithi njooo……Msimuliaji: Kaondokea chenjagaa kajenga nyumba kaka mwanangu mwanasiti kijino kama chikichi cha kujengea kikuti na vilago vya kupita, hapo zamani za kale…
Kati Hapa habari zote huelezwa kwa kifupi na kwa kufuata mambo muhimu tu. Mara kwa mara huwa ni maelezo ya moja kwa moja. Kwa mfano kuzaliwa                      kukua           kuoa/kuolewa
Mwisho Hapa kufa au kuishi raha mustarehe ndiyo miisho ya kawaida. Wakati mwingine, msimuliaji humalizia kwa kusema “Hadithi yangu inaishia hapo”

 Mtindo

Hadithi za Fasihi simulizi hutumia mbinu za monolojia (masimulizi). Msimulizi husimulia masimulizi yote yaliyomo hadithi. Katika kuutajirisha mtindo wake msimuliaji vilevile anaweza kuingiza nyimbo au ushairi kwa lengo la kusisitiza kile anachosimulia na kushirikisha hadhira yake.

Wahusika

Wahusika wa Fasihi simulizi ni wanyama, mimea, miti, wadudu, n.k. kadiri siku zilivyoendelea matumizi ya wahusika binadamu yaliingizwa. Hata hivyo hawa wahusika wa hadithi walichanganywa na wahusika wanyama au miungu. Kutokana na jadi ya kimaadili, wahusika hawa hugawanywa katika mafungu makuu mawili: wahusika wema na wahusika wabaya. Kwa kawaida wahusika hawa ni bapa na hawabadiliki kama vile kukua, kuugua, ama kufa katika mkondo mzima wa hadithi.

Matumizi ya lugha

Katika hadithi matumizi ya lugha yako ya aina aina. Humo kuna matumizi ya:

 • Misemo
 • Nahau
 • Methali
 • Tamathali za semi
 • Mafumbo
 • Mbinu nyingine za kisanaa
 • Taswira na ishara mbalimbali, n.k

Mandhari

Kwa ujumla katika hadithi mandhari hayapewi nafasi kubwa, ila tu pale ambapo yamehitajiwa yaongezee undani wa maudhui (hasa kiishara) na wakati mwingine hatuelezwi kabisa kuhusu mandhari katika hadithi. Hii inatokana na ufupi wa hadithi zenyewe.

Umuhimu wa Hadithi

 1. Kujenga jamii na kuipa mwelekeo- Hadithi zimekuwa zikisimuliwa tangu zamani kwa lengo la kuifanya jamii iwe na mwelekeo mzuri unaozingatia falsafa ya jamii inayohusika.
 2. Hadithi huelimisha, huadibu na kuionya jamii-katika hadithi kuna maadili na ujumbe unaotolewa kwa jamii. Kwa njia hii kizazi hadi kizazi kimekuwa kikitumia njia hii ya hadithi kama njia moja wapo ya kuelimisha jamii. Mara nyingi hadithi husimulia watu wenye tabia za uchoyo, uzembe, wizi na wivu baina ya ndugu.
 3. Hadithi husisitiza ushirikiano katika jamii- hadithi zimekuwa zikisimulia sana mambo ambayo yanahusu ushirikiano katika shughuli mbalimbali za jamii. Kwa mfano ushirika katika kazi kama vile kilimo, misiba, mazishi, harusi, uwindaji, ufugaji, n.k
 4. Hadithi ni chombo kimojawapo kinachorithisha amali za jamii kutoka kizazi hadi kizazi kingine. Hadithi hurithisha mila na desturi za jamii fulani kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
 5. Hadithi hutumika kama chombo cha kuliwaza au kuondoa majonzi kwa watu waliopatwa na majonzi au wale ambao wako katika hali ya kuchanganyikiwa kutokana na matatizo. Hadithi pia huweza kuburudisha watu waliochoka baada ya kufanya kazi mchana kutwa.

Semi

Semi ni fungu la tungo la Fasihi simulizi ambazo ni fupi fupi zenye kutumia picha, tamathali za semi na ishara. Aghalabu ni mafunzo yanayokusudiwa kubeba maudhui yenye maana zinazofuatana na ibara mbalimbali za matumizi.

Aina za Semi

 1. Methali

Ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa muhtasari fikra au mafumbo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Mara nyingi mawazo hayo huelezwa kwa kutumia tamathali hasa sitiari na mafumbo. Methali ni utanzu tegemezi ambao kutokea kwake hutegemea fani zingine. Kwa mfano maongezi au majadiliano mazito katika miktadha maalumu ya kijamii. Baadhi ya methali huwa ni kielelezo au vifupisho vya hadithi fulani inayofahamika kwa wanajamii.

Vipengele vya Fani katika Methali

Methali hutawaliwa na maudhui na fani. Vitu hivi viwili huathiriana, hukamilishana na hutegemeana katika utanzu huo. Methali hudhihirisha ukuu wake kifani katika muundo, tamathali za semi, picha za kisanaa (taswira), ishara na vipengele vingine vya kifani vya kifasihi. Fani na maudhui vikikamilishana hadhira hupata ujumbe unaotakiwa.

 

 1. Muundo

Methali nyingi huwa na muundo wenye sehemu mbili. Sehemu ya kwanza huanzisha wazo fulani na sehemu ya pili hukanusha au kulinganisha wazo hilo.

Mfano: Haraka haraka/haina Baraka

            Tamaa mbele/mauti nyuma

            Haba na haba/hujaza kibaba

            Bandu bandu/humaliza gogo

Sehemu ya kwanza kila wakati inakuwa ndefu zaidi ya sehemu ya pili. Urefu huo unasababishwa na kuwa kwake chanzo cha methali. Kama chanzo cha methali hiyo inapaswa kufafanua zaidi hali ambayo inatendeka na inastahili kuangaliwa ili irekebishwe. Ni kiini cha methali na hapo ndipo yalipo mambo ambayo hayastahili kutendwa aua yanayostahili.

Sehemu ya pili ni fupi kuliko ya kwanza, hapa ndipo kwenye matokeo ya kufanya vile ilivyoelezwa kwenye sehemu ya kwanza. Ni jibu la matendo au maono ya sehemu hiyo ya kwanza. Hivyo basi tunaweza kusema jamii ya Kiswahili kwenye methali huangalia pande mbili za maisha ili kufanya hitimisho na kufanikiwa kumpa mtu maono na mwangaza wa mwisho na fundisho.

 1. Matumizi ya Lugha

(a) Tamathali za Semi

Methali hutumia tamathali semi na kila methali ina ustiari kwa kiasi fulani ndani yake. Ustriari katika methali huzipima pande mbili za methali na kuzifananisha kwa jambo ambalo zote zinalichangia. Tunaweza kuchambua ustiari wa methali kutokana na jinsi tamathali mbalimbali za usemi zilivyotumika. Methali nyingi huangukia katika mafungu yafuatayo ya tamathali za usemi.

 1. Sitiari

Hii hulinganisha kitu na kingine kwa kuvifanya viwe sawa bila kutumia viunganishi. Methali za tamathali za aina hii ziko nyingi. Baadhi yake ni:

 • Mgeni ni kuku mweupe
 • Kufai kikondoo ndio kufa kiungwana
 • Mke ni nguo mgomba kupaliliwa

  

 1. Kejeli

Methali nyingi huwa na kejeli katika maudhui yake mfano:

 • Ganda la muwa la jana chungu kaona kivuno
 • Uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti
 1. Msisitizo Bayana

Hii inaonesha ushindani wa mawazo. Hii inasisitiza maana ya sentensi kwa kutumia kinyume. Katika methali kuna aina mbalimbali za msisitizo.

 • Msisitizo uwili: methali zenye tamathali za aina hii hurudia neno moja mara mbili ili kusisitiza dhana fulani ya tahadhari au onyo fulani. Mfano:
 • Hayawi hayawi, huwa
 • Hauchi hauchi, unakucha
 • Mzaha mzaha, hutumbua usaha
 • Msisitizo utatu: methali za aina hii huwa na neno moja linalorejelewa mara tatu katika tungo moja ya kimethali. Mfano:
 • Awali ni awali, awali mbovu hapana
 • Mla mla leo, mla jana kala nini
 1. Tamathali zinazokinzana

Hapa methali hubeba jozi za maneno yanayokinzana. Kuna tamathali zinazokinzana kwa kuingiliana na zile ambazo zina ukinzani wa pekee.

 • Ukinzani mwingiliano
 • Kukopa harusi, kulipa matanga
 • Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza
 • Ukinzani pekee
 • Mtu hakatai wito, hukataa aitiwalo
 • Upendalo hupati, hupata ujaliwalo
 1. Tashihisi

Hizi ni tamathali ambazo vitu hupewa uwezo wa kutenda kama mtu, methali za kitashihisi ni kama vile:

 • Kiburi si maungwana
 • Siri ya mtungi mwulize kata
 1. Tashibiha

Hii inalinganisha vitu viwili kwa kutumia viunganishi linganishi. Mfano wa methali za kitashibiha ni kama vile:

 • Kawaida ni kama sheria
 • Jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza

(b) Mbinu nyingine za Kisanaa

 • Onomatopea (Tanakali sauti)

Ziko methali zinazoigiza sauti mbalimbali

Mfano:

 • Chururu si ndo! ndo! ndo!
 • Bandu bandu, huisha gogo
 • Takriri

Pia kuna methali zenye maneno yanayojirudiarudia kwa ajili ya kusisitiza

Mfano:

 • Asiyejua maana, haambiwi maana
 • Mtoto wa nyoka ni nyoka
 • Kokoto huzaa kokoto
 • Mfululizo sauti

Methali za aina hii zinabeba sauti maalumu mara nyingi hutawaliwa na sauti –ha-, -ba-, na –pa-

Mfano:

 • Haba na haba, hujaza kibaba
 • Haraka haraka,haina Baraka
 • Padogo pako si pakubwa pa mwenzako
 • Maswali

Baadhi ya methali hujenga sanaa yake kwa kuuliza maswali. Kimsingi maswali hayo hayahitaji majibu lakini jambo lile linalokusudiwa kulengwa kwa hadhira hufika huko.

Mfano:

 • Pilipili usizozila zakuwashia nini?
 • Umekuwa bata akili kwa watoto?
 • Mchezo wa maneno

Methali nyingine hucheza na maneno huleta maana mahususi hasa katika kutoa onyo.

Mfano:

 • Pema ujapo pema ukipema si pema tena
 • Ukiona neno usitie neno ukitia neno utapatwa na neno

(c) Picha au Taswira katika methali

Sifa ya methali ni kule kujenga picha au taswira ambazo huchotwa katika mazingira. Picha hizo zaweza kuhusu wanyama, ndege, samaki, wadudu au mazimwi.

 • Picha za wanyama
 • Paka akiondoka panya hutawala
 • Mzoea punda hapandi farasi
 • Picha za wadudu
 • Mtupa jongoo hutupa na mti wake
 • Maji ya kifuu ni bahari ya chungu
 • Picha za ndege
 • Kuku mwenye watoto halengwi jiwe
 • Kunguru mwoga hukimbiza mbawa zake
 • Picha za silaha
 • Vita vya panga haviamuliwi kwa fimbo
 • Mshale kwenda msituni haukupotea
 • Picha za viungo vya mwili
 • Ulimi unauma kuliko meno
 • Heri kufa macho kuliko kufa moyo
 • Picha za samani
 • Kitanda usichokilalia hujui kunguni wake
 • Uzuri wa mkakas ndani kipande cha mti
 • Picha za matunda
 • Mchagua nazi hupata koroma
 • Koko haidari maji

(d) Wahusika

Wahusika katika methali ni muhimu sana. Hawa ndio wanaojenga kazi hii. Wahusika wake ni binadamu na wako wa aina mbili.

 • Mtoa methali
 • Wasikilizaji

(e) Mazingira

Methali hufuatana na mazingira ya watu pamoja na silka. Ni vigumu kwa mtu kupata uzito wa maana au jibu na dhana ya picha za maneno yaliyotumika katika methali iwapo mtu hana asili mahali methali ilipozaliwa.

 1. Vitendawili

Kitendawili ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili uifumbue. Fumbo hilo kwa kawaida huwa linafahamika katika jamii hiyo na mara nyingine lina mafunzo muhimu kwa washiriki mbali na kuwa chamsha bongo zao. Vitendawili ni sanaa inayotegemea uwezo wa mtu kutambua, kuhusisha na kulinganisha vitu vya aina mbalimbali vilivyomo katika maumbile. Ni sanaa inayotendwa inayojisimamia yenyewe hivyo ni tofauti na methali ambazo ni sanaa tegemezi au elezi.

Vipengele vya Fani katika Vitendawili

Muundo

Vitendawili vina muundo wake maalumu tofauti na tanzu nyingine za Fasihi simulizi. Muundo wa kitendawili unaweza kuwa kama ifuatavyo:

Kitangulizi (mtambaji au mtendaji)

Mfano: Kitendawili…..tega….(mtegaji)

 • Kitendawili swali/fumbo lenyewe
 • Swali la msaada (nini hicho)
 • Kichocheo – toa mke, mji, lipa mbuzi au lipa binti.
 • Jibu lenyewe

Mume mrefu lakini mke mfupi, lakini wanashirikiana sana (mteguaji hujibu) “mchi na kinu”

Mtindo

Vitendawili vina mtindo wa majibizano (dayalojia) kati ya mtambaji na msikilizaji. Mtambaji hutoa kitangulizi kwa kusema: “Kitendawili,” msikilizaji hujibu “tega” kisha hutoa kitendawili chenyewe yaani swali au fumbo lenyewe. Wasikilizaji wanatakiwa kutoa jibu na wakinshindwa wanamshawishi mtambaji atoe jibu mwenyewe kwa kumpa mji yaani kichocheo. Namna na aina ya kichocheo hutegemea sana mahali na mahali.

Matumizi ya lugha

Vitendawili hutumia lugha ya sitiari na mara nyingi lugha hii huwa na aina ya ushairi ndani yake. Vilevile vitendawili vya Kiswahili vina utajiri mkubwa ndani yake wa lugha. Vina utajri wa tamathali za semi zinazotawala vitendawili vingi.

Tamathali za semi

Sitiari

 • Samaki wangu anaelea kimgongomgongo (merikebu)
 • Nyumba yangu haina mlango (yai)
 • Mwarabu wangu mkali sana, ukimshika hashikiki, hana panga hana shoka, hana kisu, hana mshale (moto)

Tabaini

 • Mkubwa ananiamkia mdogo haniamkii (kunde kavu na mbichi)
 • Futi kufunika futi kufunua (kumbi, fuu, nazi, maji )
 • Yeye anatuona sisi hatumuoni (Mungu)

Kejeli/Dhihaka

 • Uzi mwembamba umefunga dume kubwa (usingizi)
 • Upara wa mwarabu unafuka moshi (chai-maziwa)
 • Kitu kidogo kimemtoa mfalme kitini (haja)

Tashihisi

 • Popo mbili zavuka mto (macho)
 • Popote niendapo ananifuata (kivuli)

Mbinu nyingine za kisanaa

 1. Onomatopea (Tanakali sauti)
 • Huku pi na kule pi (mkia wa kondoo atembeapo)
 • Chubwi aingia chubwi atoka (jiwe majini)
 • Pa funua pa funika (nyayo wakati wa kutembea)
 • Prrrrrrrrr! Mpaka maka (utelezi)
 1. Takriri
 • Huku fungu huku fungu katikati bahari (nazi)
 • Mama kazaa mtoto na mtoto kazaa mtoto (kuku na yai)

Taswira au picha

 • Kuku wangu katagia mibani (nanasi)
 • Mzazi ana miguu bali mzaliwa hana miguu (kuku na yai)
 • Mnazi wangu uko mlimani lakini nayanywa madafu hapa (mvua)
 • Mti mmoja una matawi saba: manne mabichil, mawili makavu, moja linawazimu (ng’ombe miguu minne-matawi mabichi, pembe mbili-matawi makavu na mkia mmoja-jani lenye wazimu)

Umuhimu wa vitendawili na methali

Katika maudhui tunaangalia jinsi vitendawili na methali vinavyojishughulisha katika kuonesha silka itikadi, utamaduni, tabia, uchumi, siasa, na uhusiano wa matabaka. Thamani ya methali na vitendawili ni ule ujumbe utolewayo na tanzu hizi mbili katika kuielekaza jamii.

Methali na vitendawili vingi hushughulikia mazingira yanayowazunguka watu wa kawaida huchunguza maisha ya kawaida ya binadamu na mazingira yake. Kwa hivyo basi maudhui ya vitendawili na methali hutofautiana kutoka jamii na jamii kuhusiana na mazingira na mahitaji ya jamii hizo. Maudhui ya kazi hizi huathiriwa pia na kazi ama dhima ya methali na vitendawili vinavyohusika. Methali na vitendawili vina matumizi mengi kwa jamii inayohusika kama vile:

 1. Kuelimisha

Maudhui yanayotolewa na tanzu hizi huelimisha wanajamii. Mfano methali isemayo “mali bila daftari hupotea bila habari” huelimisha wanajamii umuhimu wa kuweka kumbukumbu hasa katika maandishi. Uelimishaji kutokana na methali na vitendawili unajihusisha pia na kuwafundisha watoto historia ya jamii na mazingira yanayoizunguka jamii hiyo ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Vile vile hufunza watoto ujuzi wa kuchunguza, kuhakiki, kuhusisha mambo kuuliza na kujibu maswali pamoja na kukuza ufundi wa lugha ya jamii yao.

 1. Kuburudisha

Kama kiburudisho methali na vitendawili hufurahsha na kustarehesha ndio maana methali na vitendawili huendeshwa mara nyingi wakati wa jioni. Huu ni wakati wa baada ya saa nyingi za kazi nzito-kazi ya kutwa. Kwa hiyo watoto au wakubwa methali na vitendawili kwao huwa ni kama kitu cha kuburudisha yaani kustarehesha akili zao.

 1. Kuonya, kuadibu na kuishauri jamii

Kwa kawaida watu katika jamii: wakubwa au vijana huaswa na kuonywa kuwa na tabia na mwenendo mzuri na kufuata maadili mema ya jamii kwa mfano methali isemayo “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu” au “majuto ni mjukuu”. Hutolewa kwa madhumuni ya kuwataka watoto wawaheshimu wakuba wao na kusikiliza au kuzingatia wapewayo/waambiwayo na wakubwa. Vilevile “Ana mali nguo havai” (kinu), “Kusuka nasuka mwenyewe nakaa chini” (boga) huwafunza watu wapende kujiangalia na kujimiliki yaani waache tabia ya kuwa wabahili.

 1. Kukosoa na kukejeli

Methali na vitendawili hukosoa na kukejeli jamii-wale wafanyao kinyume na utaratibu wa jamii. Mfano: vitendawili kama: wazungu wawili wanachungulia dirishani (kamasi) mzungu amembeba mwafrika (moto na chungu) au mwarabu wangu nimemtupa bwawani (machicha ya nazi). Ni mifano mizuri ambayo ndani yake mna hisia za kejeli. Vitendawili hivi vilitumiwa kimteto na watawaliwa kuwapa chuki na dharau kwa watawala wa kikoloni. Kuwafanya wasiabudu watu hao bali wawaone kuwa ni sawa na makamasi au machicha ya nazi yasiyotakiwa katika jamii zao na ambayo mahali pake panapostahili ni katika jalala palipojaa uchafu na uozo mwingi. Kwa upande mwingine vitendawili hivi vinatoa mwito kwa watawala kupinga kutawaliwa na kuungana pamoja ili kumtimua mkoloni. Vile vile methali kama vile, ganda la muwa la jana chungu kaona kivuno au uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti, ndani yake mna hisia za kejeli na dharau.

 1. Hutunza historia ya jamii

Methali na vitendawili kwa upande mwingine hutunza historia ya jamii kwa sababu hirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Mabadiliko ya methali na vitendawili

Methali na vitendawili hubadilika kulingana na mabadiliko yanayojitokeza katika jamii katika Nyanja zote.mabadiliko ya wakati na utamaduni yanaathiri sana mabadiliko ya methali na vitendawili kimaudhui na matumizi ya lugha.

Vile vile mambo mapya yajitokezapo katika jamii hulazimisha kuunda methali na vitendawili vinavyosawiri mambo hayo. Maendeleo ya sayansi na teknolojia nayo pia yanaleta mabadiliko ya methali na vitendawili hasa upande wa uwasilishaji yaani kuhusu uhusiano wa fanani na hadhira.

Vipindi vya Chei chei shangazi, mama na mwana, na watoto wetu katika redio Tanzania ni mifano ya mabadiliko ya uwasilishaji huo kwa methali na vitendawili sasa vyaweza kupata hadhira pana zaidi kwa kusikia redioni. Hadhira hii husikia tu bila kumwona mtegaji au mtoaji wa vitendawili na methali.

Misimu

Misimu ni semi a muda na mahali maalumu ambazo huzuka na kutoweka kutegemeana na mazingira maalumu. Msimu ukipata mashiko ya kutosha katika jamii huweza hatimaye kuingia katika kundi la methali au misemo ya jamii hiyo.

Misimu ina matumizi mengi yakiwemo ya kupamba lugha, kuibua hisia mbalimbali za wazungumzaji, kufurahisha, kuasa, kuchochea, kuchekesha, kukuza lugha, kutunza historia ya jamii, n.k. Kwa ujumla misimu haina maana ya mafumbo bali inaeleza maana ya kauli mojamoja.

Mafumbo

Ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Fumbo hubuniwa na msemaji kwa shabaha na hadhira maalumu hivyo ni tofauti na methali na vitendawili ambavyo ni semi za kimapokeo.

Lakabu

Ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipa kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo.majina haya huwa ni matendo au mafungu ya maneno yenye maana iliyofumbwa. Mara nyingi majina haya huwa na sitiari. Baadhi ya majina humsifia mtu husika lakini mengine humkosoa au hata kumdhalilisha. Mfano wa lakabu ni kama vile:

 • Baba wa taifa – Nyerere
 • Mkuki uwakao – Jomo Kenyatta
 • Samba wa Yuda – Haile Selassie
 • Nyundo – Von Zelewiski
 • Mti Mkvu – Jenerali Mayunga
 • Mzee ruksa – Ally Hassan Mwinyi

Misemo

Misemo ni fungu la maneno linalotumiwa na jamii ya watu kwa namna maalumu kutoa maana fulani. Au misemo ni kauli yenye ukweli wa jumla inayotumiwa kusemea mambo mbalimbali yanayoafiki ukweli huo. Mfano:

 • Mtu kwao
 • Piga msasa mtu
 • Misitu ni mali
 • Mjini shule

Kwa ujumla misemo haina maana ya mafumbo bali inaeleza maana ya kauli moja moja.

Nahau

Nahau ni misemo ya picha ambayo huleta maana iliyofichika. Nahau ni lugha yenye uzito zaidi kuliko semi za Kiswahili au lugha ya kawaida ya moja kwa moja. Nahau ni semi zenye undani. Undani ambao wageni wanaoijua lugha hiyo juu juu tu huambulia patupu wanapoambiwa nahau hizo. Kwani nahau licha ya kuwa lugha ya mkato pia ina ujumbe mzito wenye mafumbo.

Mathalani Mswahili akisema fulani ana ndimi mbili mgeni wa lugha hii atatafsiri kwamba huyo mtu fulani kazaliwa na ndimi mbili. Kumbe maana iliyomo kwenye kauli hii yenye maneno mepesi sana ya Kiswahili ni kwamba fulani yu kigeugeu au ni ndumila kuwili.

Sifa za kutambulisha Nahau

 1. Nahau kuwa sawa na neno kimaana
 • kupata jiko ———kuoa
 • kushika hatamu———-kuongoza
 • Mtoto wa kikopo——-muhuni
 • Kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa——kudanganya

Nahau nyingine zinazokaribia kuwa neno moja kwa umbo lake badala ya fungu la maneno mara nyingi huandikwa kama neno moja. Mfano:

 • Kidudu mtu —————–mfitini
 • Ndumilakuwili ————–mnafiki

Jambo jingine lenye kuthibitisha sifa za kineno za nahau ni uwezo wa nahau kuwiana miongoni mwao kwa njia zifuatazo.

 • Nahau zenye mfanano wa maneno lakini zilizoundwa kutokana na maneno tofauti.

Mfano:

Kupata jiko

Kuasi ukapera —————-kuoa

Kukunja jamvi

Kufunga virago ————–kumaliza shughuli

Nahau zilizo na maana ya kinyume lakini zenye umbo sawasawa isipokuwa neno moja (ambalo husababisha kinyume hicho).

Mfano:

 • Kula unga ————kupata kazi
 • Kumwaga unga——-kuachishwa kazi
 • Kukaza kamba ——–kuongeza juhudi
 • Kulegeza kamba ——-kupunguza juhudi
 • Ndege mzuri ————-ishara njema
 • Ndege mbaya ———–kisirani/bahati mbaya
 • Nahau zenye mfanano wa umbo na muundo lakini zilizo na maana mbalimbali
 • Kuzunguka mbuyu ————kutoa rushwa

           Kwenda kinyume/kudanganya

 • Kushika miguu —————–kutoa shukrani

                                                Kupiga mbio

                                                             Kuomba radhi

 1. Nahau huwa na maana ya Kisarufi

Nahau za Kiswahili huweza kulinganishwa na kitenzi, jina, kiwakilishi au kielezi. Nahau za kiswahii tunaweza kuzigawa katika makundi manne ya msingi.

 • Nahau majina

Joka la mdimu

Donda ndugu

Ndege mbaya

Mkia wa mbuzi, n.k

 • Nahau vitenzi

Kukaanga mbuyu

Kufua dafu

Kuvimba kichwa

Kwenda joshi

Kukalia kuti kavu

 • Nahau vivumishi

a- miraba minne

a- kufuatia machozi

a- kijungu jicho

 • Nahau vielezi

Kufa kupona

Kufumba na kufumbua

Shingo upande

Bega kwa bega

Katika sentensi kama ilivyooneshwa nahau huchukua maana ya neno moja na kuhusiana na maneno mengine kama neno moja. Kwa hiyo ni sawa na jina au kitenzi ambacho kinaweza kuchukua ujumbe wa nafasi ya kitendwa, kielezi au kiarifu. Nahau pia inaweza ikachukua majukumu mbalimbali katika sentensi.

Mfano:

 • Mimi langu jicho hapa – kiarifu
 • Baada ya kupata kifungua kinywa alikwenda kazini (kitendwa)
 • Walipigana kufa kupona. Kielezi maana
 1. Nahau na umbo lake

Sifa nyingine muhimu katika kutambulisha nahau ni kule kuwa fungu la maneno zaidi ya neno moja na lenye muundo maalumu

Nahau hujumuisha maneno yaliyopoteza sifa za kawaida na kuchukulia kimaana kama neno moja. Nahau huzuka kutokana na fungu la maneno ya kawaida kwa kuchukua maana yake asilia na kupanua lugha ya kisasa. Nahau nyingine hupatikana sambamba na mafungu ya maneno yaliyokuwa chanzo cha nahau hizo.

Mfano:

 • Kutonesha kidonda
 • Kuzunguka mbuyu
 • Kukalia kuti kavu
 • Kuweka boya
 • Bega kwa bega, n.k

Sifa za umbo la Nahau

 1. Idadi ya maneno yenye kulinda Nahau

Nahau hujumuisha maneno si chini ya mawili. Tukitambua idadi ya maneno ya nahau tutaweza kuipambanua nahau ya sentensi kwa urahisi zaidi. Mfano:- Hakupenda kwenda lakini alikubali shingo upande.

Neno alikubali lipo karibu sana na kuhusiana moja ka moja na nahau shingo upande ambayo ina maana ya bila kupenda na kutimiza ujumbe wa kielezi katika sentensi. Kwa hiyo tunaweza kusema kwamba nahau (kukubali) shingo upande ina maneno mawili tu.

Majitu yaking’amua kuwa uko hapa utakiona cha mtema kuni.

Katika sentensi hiyo tunayo nahau kuona cha mtema kuni ikiwa na maneno manne, katika umbo lake ambayo yote kwa pamoja yanachukua maana maalumu na ujumbe wa kiarifu kama kauli moja ndani ya sentensi.

 1. Mipaka ya Nahau

Ili kuelewa barabara umbo la nahau na uwiano wake pamoja na maneno mengine ya sentensi hatuna budi kutambua idadi ya maneno yenye kuiunda nahau na mipaka yake pia. Maneno mengine yanaweza kuingia katika mipaka ya nahau na kuhusiana na nahau hiyo. Kutokana na ujumbe wake katika sentensi. Lakini maneno hayo hayaingii ndani ya nahau yenyewe. Mfano. mtangazaji alizua uongo kwa kutia chumvi nyingi alipotangaza pambano la mchezo kati ya Yanga na Simba. Neno nyingi linatia nguvu tu nahau kutia chumvi nalo limo katika mipaka yake. Lakini haliingii katika nahau yenyewe.

 • Mzee huyu amekula chumvi nyingi

Hapa neno nyingi linaingia moja kwa moja katika nahau.

Mitindo ya muundo wa Nahau

Nahau za Kiswahili zinaweza kuundwa kwa mitindo mbalimbali. Mitindo hiyo maarufu zaidi ni kama hii ifuatayo:

Kitenzi + Jina        – kukaanga mbuyu

                                – kuwa macho

                                – kutia mdomo

                                – kushikilia mkia

T+E+N+E au V    – Kuwa na mkono mrefu

                                – kufunga pingu za maisha

                                – kula chumvi nyingi

                                – kumvika kilemba cha ukoka

TS+T                      – Kufa kupona

                                – kufumba na kufumbua

                                – pata shika

T+E                        – kujikaza kisabuni

                                – kutokea puani

                                – kufa kikondoo

                                – kufa kiofisa

N+T                        – Donda ndugu

                                – domo kaya

N+U+W                 – Ana kwa ana

                                – bega kwa bega

                                – kiguu na njia

                                – chanda na pete

N+V                       – Ndege mbaya

                                – nyota njema

                                – bahari kubwa

Umuhimu wa Nahau/Misimu/Lakabu/Misemo

 1. Kukuza lugha: matumizi ya nahau mbalimbali hukuza lugha inayohusika
 2. Kupunguza ukali wa maneno: Nahau hupunguza ukali wa maneno au uzito wa jambo linalotakiwa kusemwa. Ikiwa pengine neno hilo likitumiwa kama lilivyo litaleta hali ambayo haipendezi kwa watu wanaolisikia au kuleta aibu fulani kwa kwa wasikilizaji.
 3. Hutumika kama kikolezo katika lugha: hapa nahau huongeza madoido fulani na ladha ya pekee katika mazungumzo. Kwa mfano mtu anaposema fulani Amevaa miwani atakuwa na maana fulani kuwa amelewa. Hali hii inaleta utamu wa pekee katika mazungumzo hayo kupata mvuto/kupenda aendelee kuzungumza.
 4. Hutumika kuficha maana iliyokusudiwa kwa manufaa ya watumiaji: Kwa mfano mtu akisema fulani Amekula mwendo mtu mwingine anaweza asielewe kinachoongelewa kumbe maana ni kwamba amekosa alichofuata.
 5. Ushairi

Ushairi katika Fasihi simulizi ni fungu linalojumuisha tungo zote zenye kutumia mapigo kwa utaratibu maalumu. Mapigo ya kimuziki mathalani mapigo hayo yanaweza kupangwa kwa muwala wa urari. Baadhi ya fani za ushairi huambatana na muziki wa ala. Maana, hisia na hali ya kishairi hutokana na mwingiliano huo wa maneno na mazingira ya utendaji.

Aina za Ushairi

Kundi la ushairi lina tanzu nyingi lakini tunaweza kuzigawa katika mafungu mawili ambayo ni: nyimbo na maghani.

 1. Nyimbo

Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Hivyo hii ni dhana pana inayojumuisha tanzu nyingi. Hata baadhi ya tanzu za kinathari kama vile hadithi, huweza kuingia katika kundi hili la nyimbo pindi zinapoimbwa.

Mambo muhimu yanayotambulisha nyimbo

 • Muziki wa sauti ya mwimbaji au waimbaji
 • Muziki wa ala (kama upo)
 • Matini au maneno yanayoimbwa
 • Hadhira inayoimbiwa
 • Muktadha unaofungamana na wimbo huo kwa mfano sherehe, ibada, kilio, n.k

Tanzu za nyimbo

 • Tumbuizo

Hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama ngoma au harusi.

 • Bembea (Pembejezi): hizi ni nyimbo za kubembelezea watoto, mifano ni mingi, kila kabila huwa nazo.
 • Kongozi: ni nyimbo za kuaga mwaka
 • Nyimbo za dini: huimbwa makanisani au misikitini kwa mfano kaswida za kumsifu Mtume, nyimbo za Wakristo, za ibada za jadi, n.k
 • Wawe: hizi ni nyimbo za kilimo
 • Kimai: hizi ni nyimbo za wavuvi
 • Tenzi: nyimbo ndefu za kimasimulizi au za mawaidha
 • Tendi: nyimbo ndefu za masimulizi ya matendo ya mashujaa mf. Utendi wa Fumoliyongo
 • Mbolezi: nyimbo za maombolezo
 • Nyiso: nyimbo za jando
 • Nyimbo za vita: huimbwa na wanajeshi waendapo au warudipo toka vitani
 • Nyimbo wa wawindaji: huimbwa na wasasi wakati wa sherehe zao au wawapo mawindoni hasa wanapofanikiwa kupata kitoweo.
 • Nyimbo za taifa: huimbwa kusifia taifa hasa kwenye matukio muhimu
 • Nyimbo za watoto: huimbwa na watoto katika michezo yao
 1. Maghani

Maghani ni ushairi unaotolewa kwa kalmia badala ya kuimbwa. Zipo aina mbili za maghani ambazo ni maghani ya kawaida  na maghani ya masimulizi.

Maghani ya kawaida

Hapa huingia fani mbalimbali za ushairi simulizi, kwa mfano, ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini, harusi, n.k. ilimradi ushairi huo unaghanwa badala ya kuimbwa au kusemwa tu.

Maghani ya masimulizi

Hizi ni ghani zinazotambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani na ambazo mara nyingi huambatana na muziki wa ala. Mtambaji wa ghani hizi huitwa Yeli na kwa kawaida huwa ni bingwa wa kupiga ala fulani ya muziki. Hapa Tanzania ala zinazotumika zaidi kwa shughuli hii ni zeze, marimba, ngoma na njuga.

Fani katika Ushairi

Ushairi wa Fasihi simulizi una vipengele mbalimbali vya kifani kama vile:-

Muundi

Miundo ya ushairi wa Fasihi simulizi ni ya aina mbalimbali. Idadi ya mistari katika kila ubeti hutofautiana na kwa kawaida ushairi wa Fasihi simulizi unakuwa na beti pamoja na kibwagizo chake na mpanhilio wa beti ndio unaofanya wimbo uweze kuimbika.

Mtindo

Mashairi mengi ya Fasihi simulizi hayafuati urari wa vina na mizani na baadhi hufuata kanuni hizo. Kinachozingatiwa hapa ni mapigo ya kimuziki, uimbikaji au ughanwaji.

Matumizi ya lugha

Vipengele vya lugha vinavyotumika sana katika ushairi wa Fasihi simulizi ni:

 • Misemo na nahau
 • Methali
 • Tamathali za semi
 • Mbinu nyingine za kisanaa
 • Taswira na ishara mbalimbali

Vibainishi vya ushairi wa Fasihi simulizi

Ushairi wa Fasihi simulizi mara nyingi huwa na aina fulani ya madoido ambayo hukamilisha ushairi huo kwa kuufanya ushairi huo upendeze na uweze kuchezeka. Madoido hayo ni kama vile:

 1. Mkarara

Ni ule mstari au ubeti ambao hurudiwarudiwa mara nyingi na washiriki. Mkarara ndio hasa unaofanya kila msikilizaji ashiriki na mara nyingi huchukua wazo zito la wimbo. Vilevile husaidia kuondoa udhia wa kumsikiliza mtu mmoja kama ilivyo katika ushairi wetu wa Kiswahili. Huondoa usingizi na kumpa mghani nafasi ya kupumzika na kumeza mate.

 1. msindo

Ni mapigo ambayo hupigwa kwa mwendo uleule katika nyimbo zetu hasa zile za kucheza. Mapigo haya hufanywa na mguu mmoja au miwili, kwa baadhi ya makabila miguu ya wachezaji mara nyingi hufungwa njuga au vijikengele vidogo au makopo na kengele hizo hasa husababisha mlio ambao huleta uzuri wa aina fulani masikioni. Zipo aina mbili za kengele- zipo zenye mlio mzito na zile zinazotoa mlio wa juu. Mchanganyiko wa milio hii huleta muoano wa aina fulani kati ya wachezaji na mpiga muziki au mwimbaji. Milio hii husaidia katika kuuwekea alama za mapigo wimbo unaochezwa na kutambua kama mwendo wa wimbo huo ni wa polepole au harakaharaka.

 1. makofi

Kazi ya makofi kukata shauri juu ya mwendo wa wimbo (polepole au harakaharaka). Katika makabila mengi makofi huchukua nafasi kubwa katika nyimbo ambazo watu huimba wamekaa au wamesimama bila kucheza. Vilevile hutumika sana kumpa nguvu mchezaji aliye katikati na kadiri makofi yanavyoongezeka ndio vilevile mchezaji huchemka. Makofi pia hutumiwa sana na wanawake katika nyimbo za harusi. Makofi huwekea wimbo alama ya mwendo, huwaongezea nguvu wachezaji na kuwashirikisha watu wote katika mchezo. Mara nyingi huambatana na manyanga na haya hutingishwa kwa mikono.

 1. vigelegele

Ni mlio wa sauti ufanywao kwa kutembeza ulimi mdomoni haraka haraka. Katika wimbo vigelegele hutumika:

 • Kuonesha upeo wa juu wa furaha. Huweza kupigwa pia kumpongeza mchezaji ambaye amecheza vizuri au mwimbaji kwa kuimba vizuri.

Kuna vyombo ambavyo hupigwa na midomo vilivyo muhimu katika nyimbo. Vyombo hivyo ni kama vile filimbi, pembe, vibuyu, n.k. vyombo hivi vina matumizi sawa na yale ya vigelegele na ndivyo mara nyingi husaidia kuita watu walio mbali waje kutazama wimbo au mchezo.

Umuhimu wa ushairi wa Fasihi simulizi

 • Kuelimisha, kukosoa na kuirekebisha jamii inapoelekea kuzama katika dimbwi la upotofu
 • Kufurahisha na kustarehesha jamii
 • Kutia hamasa na kumfanya mtu asikate tamaa
 • Kuiongoza jamii mf nyimbo
 • Kuionya jamii
 • Kueleza falsafa ya jamii inayohusika.