TAMTHILIYA YA USHUHUDA WA MIFUPA

By , in Tamthiliya on . Tagged width:

Utangulizi

Historia ya uwajibikaji wa wasanii kwa Mipango mbalimbali ya Taifa hili haiwezi kusahaulika wala kupuuzwa na mtu yeyote. Msanii ni kioo cha jamii. Jamii hujiona na kujikosoa kwa kuangalia sanaa. Katika kuitikia wito wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI nchini, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na wasanii wa fani mbalimbali kote nchini, walia-zimia kuanzisha kampeni maalum ya kutumia sanaa katika kuelimisha jamii kuuelewa ugonjwajinsi unavyoenea na athari zake; hatimaye waweze kubadilisha mwenendo wao wa maisha ikiwa ni njia ya kujikinga na ugonj-wa huo. BASATA, kama Mratibu Mkuu wa kampeni hii likisaidiana na Wakuza Sanaa kote nchini limejenga misingi imara ya utekelezaji kuan-zia ngazi za Taifa hadi vijijini, ili kuwasaidia Wasanii waweze kufikisha elimu hii kwa wanajamii wotc. Kampeni hii ilizinduliwa kwa maonyesho yaliyofanywa na wasanii wa fani mbalimbali wa Mkoa wa Dar es Salaam. Fani zilizoshirikishwa ni pamoja na ngoma, muziki (Kwaya, Dansi. Taarab), Tamthiliya, Sarakasi, Mashairi, Ngonjera pamoja na maonyesho ya picha za kuchora. Maonyesho haya yalianza tarehe 29 Mei, 1989 na kuzinduliwa rasmi tarehe 2 Juni 1989 na aliyckuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Ndugu Salim Ahmed Sal-im. Ambaye katika uzinduzi wake alisema:
(Nanukuu).

“Kampeni hii ya wasanii dhidi ya UKIMWI isiwe ya mwaka mmoja tu bali iwe ni ya kudumu kwani dawa haijapatikana na jamii yetu ya Tanza-nia na dunia ikingali inatafuta dawa aidha bado watu wengi hasa vijijini hawajaufahamu ugonjwa huu vyema.”

(Mwisho wa kunukuu – gazeti la Uhuru tarehe 3 6.1989).

Licha ya Maonyesho hayo yalifanyika mashindano ya Uandishi wa Tam-thiliya. Mashindano haya yalitangazwa tarehe 21 Mei 1989 na tarehe ya mwisho ikawa 31 Julai 1989. Jumla ya miswada 160 kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara ilipokelewa. Usahihishaji wa miswada hiyo uligawanyika katika awamu mbili na kila awamu ilifanywa na jopo tofauti la waamu-zi. Jopo la kwanza lilipewa jukumu la kuchagua miswada 10 bora kati ya miswada 160. Jopo la pili lilitakiwa lipate mswada ulio bora kati ya rniswada 10. Baada ya kazi hiyo ngumu iliyochukua muda mrefu mswaada huu “USHUHUDA WA MIFUPA” ulipata ushindi wa kwanza.’

Ni imani yetu maudhui ya tamthiliya hii bado yana thamani kubwa, ugonjwa haujatoweka na bado unaendelea kuenea, hivyo kwa kusoma na hasa kuigiza tamthiliya hii kutaikumbusha jamii juu ya dalili, ueneaji na jinsi ya kuepukana na ugonjwa huu. Pia itakuwa ni kumbukumbu ya kihistoria kwa vizazi vijavyo.

Wahusika

MIFUPA NA WATU

Ingawaje baadhi ya wahusika wametajwa kwa majina, kama vile Ngariba, Mtambaji, Meneja Dokoa, Toza, Makalikiti, Korido-Dokta, n.k., wahusika wote wanaweza kuigiza sehemu tofauti tofauti na kuchukua uhusika wowote. Hivyo, watayarishaji wameachiwa kuamua idadi ya waigizaji watakayo, wa kike au wa kiume. Kadhalika, mchezo huu un-aweza kuigizwa na watu wengi au wachache, hata watatu au wawili, kadiri ya mahitaji ya watayarishaji. Hivyo hivyo, kwa vifaa: vinaweza kuwek-wa vingi, vichache au hata visiwekwe kabisa.

MAIGIZO JUKWAANI

Mchezo huu una onyesho moja tu na wahusika wachache ambao itabi-di wabadilishe wadhifa wao mara kwa mara kutokana na kile wanachok-ionyesha. Hivyo kutakuwa na kufaragua kwingi na maonyesho-bubu mengimengi. Mifupa inaweza kuonyeshwa kwa wahusika kuvaa gubigu-bi majoho meusi ambayo yatakuwa na mistari myeupe kuonyesha alama za mifupa ya binadamu kamili pamoja na fuvu kichwani. Ili kupunguza ghasia za kutoa vitu na kuviingiza jukwaani, vifaa vyote vya wahusika vinaweza kuwekwa ndani jukwaani kwa nyuma au pembezoni na kuvut-wa au kuondolewa kadiri vinavyohitajika. Kadhalika waigizaji wanawe-za kukaa pembeni tu mwa jukwaa na kuingia na kutoka katikati ya jukwaa kadiri, inavyohitajika.

Onyesho

Ngurumo, radi na sauti nyingine kalikali. Milio ya ngoma la Mgambo likilia lina jambo na saufi nyingine zinasikika kwa muda. Ghafla sauti w watu wanaolia, kwanw taratibu kisha kwa nguvu sana. Maombolezo ya nguvu sana ya fujo yanafanyika. Hakuna kusikillzana. Jukwaani wanainuka (au wanaingia) Mifupa kwa taratibu. Wanazunguka jukwaani kwa huzuni, wanajinyonganyonga kwa maumivu wakiomboleza. Pole pole sauti w maombolezo zinafifia, lakini haziishi, wakati ikijinyonganyonga….n.k.

MFUPA I:

Viini… Viinii… VIIINI! Virus – H.I.V. VIRUS – Viini. Hivyo…. Hivyo…. Hivyooooo….!

Vinazagaa, vinazagaa, vinazagaaa…..! Vinasafirishwa kwa sindano na vifaa vingine vya kuchanjia visivyochemshwa, miswaki ya kuchangia, vifaa vya kutogea na, hasa zaidi, kwa zinaa na kulawiti! Hivyo… Hivyo…. Hivyooooo!

Vinazagaa: Vinaingia katika damu yajamii…. Vinaingia! vinapigana na chembechembe za mwilini. Vinaua! Viini! Hivyo… Vinazaaana… Vinazaana. VINAZAANA!

(Kilio. Sauti za maombolezo zinaongezeka taratibu)

Vinaingia mwilini pote mpaka kwenye ubongo. Vinazaana katika jamii… Vinamaliza chembechembe za kulinda mwili… Mwlii unadhoofu…. Jamii inadhoofu…. Mwili unadhoofu….. Jamii inadhoofu…. MWILI UNADHOOFU! JAMII INADHOOFU. Madonda! Nywele zinapunyuka! Mapele! Kuhara! Vichaa! Vifua! Nini jamani……? Nini…..? NAULIZA NINI?

MIFUPA:

(wote kwa pamoja) UKIMWI

MFUPA I:

He! Na mimi….?

MIFUPA:

(wote) Ndiyo, umeupata! Na wewe umeupata! Na mimi nimeupata! Na yule ameupata! Na yule! Na yuleee…..! Ni wewe umeniambukiza. Ni wewe…. Ni wewe….. Ni wewe….. Wewe..

(Zogo. Mifupa wanasutana. Sauti kaliya vilio, mwanzo kwa mbali, kisha inaongezeka)

MFUPA I:

Kifo hicho jama! Kifo!

MIFUPA:

(wote) Kifo! Kifo!

(Sauti za maombolezo, kwanza kwa nguvu, kisha zinafifia polepole)

MFUPA I:

Ukimwi…….. vijana wanapukutika…. Viini… Wazee wanapukutika…. Viini…. Vinasambaa….. Jamii zinasambaa…

Nani amzike nani, jama eeh….? Jamii inadhoofika…. Jamii inadhoofika…. Jamii inakufa….. Inakufa….. INAKUFA!

MIFUPA:

(wote); INAKUFA!

(Wote wanaanguka chini. Kimya. Taratibu ngoma inalia, lamgambo. MFUPA I anasimama polepole na kuan za kuongea)

MFUPA I:

Hivyo ndivyo jamii yetu ilivyokwisha. Balaa…… Balaa… Nasema balaa kubwa! Hivyo ngoja tuwasimulie ilivyoku-wa. Sikilizeni: liwe onyo! Na pia, iwe kinga. Kinga kwa balaa isiyokuwa na kinga. (Anawageukia wenzake na kuwaamrisha)

Hey! Nyie kina Mifupa, Amka! Amkeni tutoe ushuhuda. (Mifupa wote wanainuka wakifurahia kutoa ushuhuda)

MIFUPA:

(wote): Haya, sawaa… Tutoe ushuhuda! Ushuhuda wa mifupa iliyofishwa; ili iwe kinga! Tunawaletea Ushuhuda wa Kinga ya Mifupa ya Watu Iliyofishwa….

MFUPA I:

Yaani nini?

MIFUPA:

(wote): Ukimwi!

MFUPA II:

Sasa tufanyaje?

MFUPA III:

Tufanyeje namna gani? Ni mashtaka tu. Naam, fugun-gue mashtaka tu: nani aliyesababisha vifo vyetu na jamii yetu kutokomea…

MFUPA IV:

Viini…..

MFUPA III:

Ndiyo, viini; lakini tulivipataje? Kupata jibu la hili tuweke baraza hapa hapa katikati, kila mmoja wetu atoe maelezo yalivyokuwa na sisi sote tutashuhudia. Lakini, tusihukumiane, mnaonaje?

MIFUPA

(wote): Sawaa….!

MFUPA III:

Sawa. Sasa itabidi tuonyeshe kama watu, kama tulivyokuwa kweli hapo awali kabla ya mji wetu kuteketea… Haya, sote tukae kando. Katikati mahali pa ushuhuda. Wewe, Namba moja, tukupe kazi ya kuon-goza, uwe Mtambaji. Mnaonaje?

MIFUPA:

(Wote): Sawa… Leo ndiyo leo… Siri zitafichuka…. Leo nitamwona mbaya wangu….

(Wanavua majoho yao na kubakia na nguo au mavazi kaina watu walio hai kweli, si mifupa tena. Mtambaji anapoanza masimulizi yake, wengine wanayaigiza kwa vitendo yale anayoyasema)

MTAMBAJI:

Nitaanza mwanzo kabisa katika masimulizi yangu ili tuone ilivyotokea. Katika mji wetu kulikuwa na watu wa kila aina kama miji mingine. Walikuwapo vijana……wazee…. watoto….. vikongwe….. akina baba na akina mama….. Na wote tukifanya shughuli za kawaida mbalimbali…… Wakulima….. Wafanyakazi, viwandani, maofisini, kila sehemu…. Wafahya biashara, kila namna…. Malaya wa mji, wa kiume na wa kike.. Wanasiasa… wazururaji…. Na kadhalika…..

(Wakati MTAMBAJI akisema, watu wanapita mmoja mmoja, kila mmoja akionyesha kuwa ndiye mtendaji wa shughuli hiyo inayotajwa wakati huo; kwisha wote-wanakwenda kuganda pembeni)

Basi tuliishi kwa raha mustarehe kwa miaka mingi, laki-ni ikafika mwaka mmoja huo tukaona ghafla vifo vya ajabuajabu vingivingi vikaanza kutokea. Kadhalika tukaanza kusikia habari za ajabu.. ajabu…

MTU 2:

Sisi Marekani tumefanya utafiti. Ndiyo! Tumefanya utafiti na tumegundua Acquired Immune Deficiency Syndrome – kwa ufupi AIDS. Tumeridhika kabisa kuwa kuna viini visivyokuwa na dawa. Vinasababisha nguvu za mwili zisiweze kujikinga na maradhi. Na chanzo chake tunakijua. Ndiyo. Tunakijua chanzo cha virus – H.I.V. Tunakijua…. Mnataka niwatajie?

(Anawaangalia kulia na kushoto)

Ndiyo…Er…kuna masokwe…… Masokwe haya ndiyo yaliyompatia binadamu ugonjwa huu. Na masokwe haya yapo! Ndiyo. Yapo Afrika!

MTU 3:

Wewe Marekani msenge nini? Sisi ndiyo tumeleta ugonjwa huu?

MTU 2:

Er… Tuseme huko kwenu Afrika ndiyo umeanzia…. Er. …kwa rnasokwe..

MTU 3:

Sasa kama ulikuwa kwa masokwe, unataka kusema nini? Sisi tulungiliana na hao masokwe ndiyo tukaupata?

MTU 2.

Lazima mkubali ukweli Bwana Jujumani. Kumbuka huu-ni utafiti si haban ya kubuni.

MTU 3:

Mnamsikia? Wamezoea hawa Marekani; kila kitu kibaya, ni cha Mwafrika. Maluuni hawa! Hata huko kwenye mwezi wanakokwenda siku wakikuta mavi watasema sisi ndiyo tuliokunya huko. Mabaradhuli wakubwa!

MTU 4:

Wamezoea! Wapashe! Sisi Wakyuba tumewachoka.

MTU 2.

Bwana, sisi tumefanya utafiti… Acha ubisni wa Kijinga Madevu.

MTU 5:

Hata sisi Warusi tuinefanya utafiti… Usitutishe Bwana Doladola.

WOTE:

Tupe ripoti: Leta ripoti……….

MTU 5:

Ripoti yenyewe bwana, ni kwamDa Kuna watu wameten-geneza hivi viuu kwenye lebu……. Er…… Yaani kwenye maabara. Sijui kwa makusudi au kwa nasibu, viini hivi” mwishowe vikatoka huko kwenye maabara, vikasambaa Vilisambaa toka wapi? Toka kwenye maabara moja huko Marekani.

MTU 2:

Shenzi taipu, Majungu matupu!

MTU 4

Utafiti wa Mrusi kiboko: Hekoo: Bwana Vodka heko zako.

Utafiti madhubuti wa hali ya juu kabisa huo.

MTU 3:

Msitutishe! Na sisi Waafnka tumetazamia: Msinikodolee macho kama vyura! Ndiyo. Tumefanya utafiti Nasi tunavyo viona mbali! Waone macho! Ninyi hamjui jujuoloji? Tumefanya utafiti nawaambia.

WOTE:

Tupe ripoti.

MTU 3:

Safi. Jujuoloji imeonyesha kuwa ugonjwa huu umean-zia kwa wafungwa waliokuwa wanabashiana huko Marekani.

MTU 2:

Shit!

MTU 3:

Shit mwenyewe: Bata – Mzinga wee

MTU 2:

Akili mbovu kama ya Mrusi. Huna adabu Sokwe wee (anampiga kofi). Shenzi!

MTU 3:

Shenzi mwenyewe…! Nitakuroga nikugeuze fisi, mahamri wee! (Anamsukuma MTU 4 ambaye naye anam-gonga MTU 2. Ugomvi unazuku):

Kwa nini umenipiga….? Wewe ndiveumeletaAIDS.. Wewe…. Wewe…..” n.k. (Ghafla sauti za vilio, Wanaganda).

MTAMBAJI:

Wakati wanabishana, watu wanaendelea kupukutika katika mji watu…(Vilio). Watu wanaendelea kuteketea (Viliovinazidi).

MTU 4:

Jama, tuache kubisha. Kila mtu mahali alipo, afanye utafiti wa kutafuta dawa tu, basi. Tutakwisha wote…. Acheni kubishana, tutakwisha!

WOTE:

Sawa! Haina haja. Wote tufanye utafiti, tutafute tiba tu, basi.

MTAMBAJI:

Basi, wakati utafiti wa tiba unaendelea, hamna dawa za kinga. Viini vikaendelea kusambaa kwa namna mbalimbali, kama vile kwenye vituo vya matibabu… (Wote katiku foleni. Mbele yao kwa pembeni kuna wauguzi).

MUUGUZI:

(Akitingisha jiko la mafuta): Ah! Hili stovu halina mafuta hata tone. Hizi sindano tutapigaje leo jamani? Hii zaha nati yetu nayo imezidi kwa matatizo.

MTU 2:

Kwani hamkupata mafuta ya; taa ya kaya?

MUUGUZI II:

He! Mzee wangu, unakuwa kama mgeni hapa kijijini. Mgao wa kaya wa mafuta ya taa wiki iliyopita wamepata watatu tu. Miye nimejidamka saa kumi usiku, wauzaji wenyewe wamekuja saa tano mchana. Foleni maili nzima! Dakika kumi tu wamekaa:

“Mafuta ya taa yamekwisha! Sasa mgao wa sabuni…”

MTU 3:

Ah, kawaida yao hiyo…

MTU 4:

Mie siku hizi natumia dizeli kwenye kibatari changu.

MTU 3:

Hee! hiyo mpya teria, Dizeli?

MTU 4:

Sasa? Bila ya hivyo nitalala giza kama wewe. Ukizidiwa usiku unaenda unapapasa viambaza kama kipofu.

(Wanacheka)

MUUGUZI I:

Sasa hizi sindano tutapigaje leo?

MTU 2:

Nesi, kwani ukipiga hivi hivi tu haziingii?

MUUGUZI I:

Na kweli. Tena nilichemsha kiasi jana, kabla mafuta hayajaisha kabisa.

MTU 2:

Basi tudunge tu hizo sindano mama, hamna taabu.

MUUGUZI I:

Basi aingie mmoja mmoja…

(Watu wanaanza kudunga sindano, kwafoleni. Wauguzi wanatumia sindano zilezile. Inasikika sauti ya mtoto akilia)

MTU 2:

Mtoto mwoga wa sindano huyo.

MTU 3:

Eee. Sindano si mchezo. Zinauma hata kwa mtu mkubwa.

MTU 4:

Na wewe mtani wangu kwa woga! Hivi hapo ulipo, unatamani kukimbia hizo sindano, baba zima na midevu chakala! Leo nitakushikilia mpaka wakuchome.

MTU 2:

Ulishike hilo baba zima!

MTU 4:

Joga je. Leo nitakushika mtani wangu.

MTU 3:

Kamshike mkeo.

MUUGOZI I:

(Akaita kwa nguvu): Nimesema mwingine!

MTU 3:

Haya, mwingine nenda….

(Mara inasikika sauti ya mtu anayegugumia kwa maumivu; ni mgonjwa aliyezidiwa)

MTU 2:

Jama tumsaidieni’mwenzetu kumwingiza, kwa daktari.

(Wanamsaidia mgonjwa mahututi kuingia kwa daktari. Daktari anamchunguza)

DAKTARI:

Loh! Mgonjwa mwenyewe huyu anahitaji kuwekewa damu mara moja. Hakuna ndugu yake yeyote hapa anayeweza kujitolea damu?

MTU 2:

Naona hakuja na ndugu yake yeyote.

MTU 3:

Bwana Mganga, katika hali kama hiyo, sisi sote hapa ni nduguze. Mimi najitolea kutoa damu.

DAKTARl:

Sijui umeshawahi kutoa damu?

MTU 3:

Zamani. Nilipokuwa shule.

DAKTARl:

Unaweza kukumbuka grupu yako.

MTU 3:

Sana. Ni grupu -0. Nakumbuka sana.

DAKTARI:

Vizuri sana, maana damu yako anaweza kupewa mgonjwa yeyote.

Sogea huko kwa manesi utoe ili tuweze kuokoa maisha ya mwenzetu.

(Anasogea. Manesi wahamtoa damu, hapo hapo DAKTARI anamwekea mgonjwa halafu wanampeleka kando)

MTAMBAJ 1:

Pole maskini Daktari. Alidhani anaokoa maisha, kumbe anapoteza maisha. Damu ile ingepimwa kwanza, ingegu- duliwa kuwa ina viini vya Ukimwi. Lakini si hapo tu viini vilipoenea.

(sauti za vilio)

Katika mji wetu pia kulikuwa na akina Korido-Dokta….

KORIDO-DOKTA:

Ah! Maisha gani haya! Dokta mzima, na huduma zan gu zote hizo ninazozitoa kwa wananchi usiku na mchana, mimi mwenyewe kwenda kulala na njaa! Upuuzi mtupu! Muni nakesha wodini, emergency cases chungu nzima. Nakesha kuokoa maisha ya watu wakati mimi mwenyewe wanayatoa maisha yangu taratibu kwa njaa. Nimeenda hata ng’ambo kuspeshalaizi, nimerudi hapa sipumui kwa kuwahudumia wagonjwa waliorundikana. Halafu wananipa mshahara wanaoita wa mwezi, Lakini nakula siku tatu tu, umekwisha! Sasa nitafanyaje? Basi kila mtu mahali pake. Na mimi mahali pangu ni kwenye begi hii. Begi hii ina kila kitu… Ndiyo tutakavyoishi na sisi. Kila mtu mahali pake. Na mimi mahali pangu kwenye begi hii… Ndiyo hata kuhani chakula chake anapata hekalu- ni, ati, hivyo nitaji….

MTU 2:

Dokta!

KORIDO-DOKTA:

Haloo…..!

MTU 2:

Samahani, Dokta, nilikuwa nakusaka. Nimefika pale kwenye autipeshenti, sijakuona.

KORIDO-DOKTA:

Ha! Ha! Ha’ Utaniona wapi? Tumo kwenye korido kido- go kidogo…. Vipi kuna tatizo?

MTU 2:

Si kubwa sana…. Er….. Nilikuwa nahitaji rangi-mbili! Unajua tena Dokta, sisi wengine ujana bado unatusumbua.

KORIDO-DOKTA:

Wewe….! Umepatikana ten’a? Utakatika hiyo ndude yako. Chunga sana.

MTU 2:

Ah! Nilikuwa ni nesafiri tena kupeleka mizigo Zambia kwa malori yetu.

Basi nikaona nipunge upepo kidogo. Unajua tena dereva lazima uwe na spea taya.

KORIDO DOKTA:

Matokeo yake kuumwa na nge! Gono si zuri kulipata mara kwa mara

MTU 2:

Ah, ujana Dokta….

KORIDO-DOKTA:

Sasa leo naona nikudunge sindano tu. Ni.na dawa komesha yake. Sindano moja tu itakaasha.

MTU 2:

Safi, Hivyo nikutafute wapi dokta?

KORIDO-DOKTA:

Unitafute wapi, utaniona? Wach nikudnnge hapa hapa; uchepuke kidogo hapo. Umejizatiti lakini?

MTU 2:

(Akitaka kutoa fedha mfukoni): Ninazo mia tano? Dokta…

KORIDO-DOKTA:

Ah! Usinipee hapa, watu wote hao huwaoni, Tuchepuke kando, kwenye huo upenyu…

(Wanachepuka kando. Anafungua begi lake, anupokea kwanza fedha zake, anavfutika. Anamchoma sindano na kuanza kuondoka)

MTU 3:

Dokta!

KORIDO-DOKTA:

Yeees!

MTU 3:

Nilikuwa nakutafuta!

KORIDO-DOKTA:

Aaah! Unanitafuta hivi nivi hivi tu? Nina haraka kidogo, Namuwahi mgonjwa wangu wodini…..

MTU 3:

Samahani Dokt?… Lakini tafadhali sana, naumba unisaidie. Nimekuja hapa tangu asubuhi, lakini wala faili langu halijaingizwa ndani kwa daktari.

KORIDO-DOKTA:

Aaa! Mafaili mengi mno siku hizi.Nina haraka lakini…

MTU 3:

Tafadhali Dokta….

KORIDO-DOKTA:

Haya, hebu basi njoo tuongelee hapa pembeni nisikilize shida yako haraka haraka…. Labda tunaweza kueleana lugha……..

(Wanachepuka kando na kuanza kuongea lakini hatusikii. Tunaona tu kuwa anafungua begi lake tena, unapokea fedha na kumdunga sindano. Kisha wanapeana mikono na kuagana. Sauti za vilio zinasikika kwa mbali)

MTAMBAJI:

Mambo hayo. Viini ndiyo vinavyosambaa hivyo.

(Mara kicheko kinasikika toka pembeni).

Khe! Na huyo anayechekelea huko ni nani? Hebu aso-gee tumwone naye shughuli zake…. ahaa… Ngariba: Mmmh! Ngariba naye alikuwaje katika mji wetu…..? (Anatokea NGARIBA na mkasi n’kononi).

NGARIBA:

Mimi si Nganba tu, usinishushie cheo. Nina kazi nyingi miye. Nikipumzika za kutairi wanaume basi huwasaidia akina mama kazi za kutoga masikio na pua. Nayo hii na’fahamu kazi hiyo kuwazidi hata akina mama; akina mama wao mikono yao hutetema, yangu mikavu, inatuna na nnara kuzidi chuma Nikikubana hutoki, wacha wee! Lakini siku hizi hiyo si kazi, ninayo bora zaidi: Ah! Msinipotezee muda wangu wa kazi. (Anaongeza sauti) Eee! Wateja wangu.. Mambo tayari! Ingieni kwa foleni na msifanye fujo. Kila anayeingia asisahau kumpa ada yake huyo kijana hapo nje. Mmoja mmoja tafadhalis (Watu wanaingia, Kelele za vikohozi na sauti za watoto wakilia).

NGARIBA:

(Kwa mtu wa hwanza): Haya fungua mdomo wako! Kwa nguvu! Eee, unacho baba. Unacho! Usinitolee ulimi kama kenge! Nimesema kimeo unacho.

Fungua mdomo wako zaidi. Zaidi….

(Anachukua mkasi wake na kumkata kimeo).

MTU 2:

(amembeba mtoto) Oh Mwanangu, baba, anakohoa tangu ainezaliwa.

Na kutapika ndio hakumwishi. Amechoma misindano hospitali weee… Mpaka sasa niitako imekuwa migumu kama mawe!

NGARIBA:

Mtungulishe mdomo. Eeheee….zaidi…. Naam, anacho (anamkata) Hiki hapa!

MTU 3:

(hali anakohoa): Ngariba: sikuwezi kwa kukata vimeo!

NGARIBA:

Si vimeo tu. Kutairi watoto na hata wakubwa ndiyo mwenyewe mimi. Kama bado nieleze tu

MTU 3:

Aaah. Labda yule aliyetoka hapa na mtoto ndiyo bado. Siye jadi yetu kwenda ngomani. Basi tuache utani, nimekuja hapa kuangalia kama nina kimeo maana nakohoa mno!

NGARIBA:

Fungua mdomo ehee! Unacho (anamkata). Hiki hapa (Anawaangalia wateja waliobakia). Ee, naona leo mko wengi sana wateja wangu. Hivyo bora nyote mfungue midomo na kuachama. Nitapita haraka haraka zaidi. Msiwe na wasiwasi. Na watoto wafunguzeni midomo. Msihofu ndio kazi yangu.

(Watu wanafungua vinywa wazi. NGARIBA anapita akikata vimeo kwa mkasi wake lie ule kwa haraka hara-ka mno. Kelele w vikohozi na watoto wakHia kwa nguvu. Inakuwa ghasia na makelele ya vilio, ikifuatiwa na maombolezo).

MTAMBAJI:

Khe! Hata mimi sikujua kwamba Ngariba alikuwa pia mkata vimeo. Salale! Haya tena, mwenye macho haambiwi ona. Ndiyo viini vilivyoenea hivyo. Lakini yote hayo ni upuuzi ukilinganisha na sababu yenyewe hasa il-iyosababisha mji wetu kuteketea.

(Wanatokea MAKALIKITI na TOZA, Malaya wa kike na wa kiume. Wole wamejirembesha mno kwa mavazi, na marembo ya kike).

TOZA

(Sauti ya kiume inayogeza ya kike): Vipi Makalikiti sho-ga yangu, mambo vipi leo…

MAKALIKITI:

(Sauti ya kike asilia) Ah, ndiyo kwanza nimeanza kazi. Vipi wewe, umekuja zamani?

TOZA

Aa, sasa hivi tu, kama tumefuatana tuseme. Hapa nao-na kama pazuri. Wale njagu hawawezi kutuona.

MAKALIKITI

Washenzi wale! Wanadhani sisi tutakula nini wakifunga maduka yetu?

TOZA

Sijui labda magwanda yao!

MAKALIKITI:

Lakini waongo watupu! Haja yao vya bure tu. Ukiwaon-jesha kidogo, wanasahau walivyoagizwa…

TOZA:

Ssssh!!! Naona wateja hao……

(Wateja wanaingia. Igizo-bubu linafuata. Wateja wanap-ita wanatoa fedha, na kufuatana na malaya walepembe-ni, au nyuma ya jukwaa na kwa muda kidogo hawaonekani. Wanaporejea, wateja wanaonekana wakijilengeneza vema mavazi yao kama kurekebisha makoti, kufunga vifungo, zipu n.k. shughuli imekwisha. MAKALIKITI na TOZA, baada ya kila wateja kuondo-ka, wanarudi na kujiweka sawa mapambo yao tayari kuwavutia wateja wengine. Wateja wengine wanakuja na inakuwa kama mwanzo. Hali hii inaendelea kwa muda mrefu hatimaye MAKALIKITI na TOZA wanaonekana wamelewa kwa uchovu. Wanaondoka baada ya sauti za vilio kuanza kusikika kwa mbali; halafu sauti za maom-bolezo zinafuata).

MTAMBAJI:

Mh! Mamho hayo yalivyokuwa kwenye mji wetu. Sina haja ya kuwasimulia. Mmmeona wenyewe! Tulidhani kuwa katika mj wetu watu wakisikia habari za viini watashtuka, kumbe wapi, ndiyo, kwanza mambo yakazidi, pamwe na vishawishi vyake…..

(Sauti ya nguvu ya muziki ghafla. Disco. Watu wote wanaanza kucheza dansi, igizo la pombe kunywewa, n.k. Anaingia MAKALIKITI akiwa amevaa sketi fupi mno kiasi cha kuyaacha mapaja katika hali ya utupu. Meneja DOKOA anaanza kumnyemelea. Sauti ya Muziki inafifia na wengine wakiendelea kucheza pembeni).

MENEJA-DOKOA:

Halo binti, Vipi? Mbona unacheza peke yako?

MAKALIKITI:

Aaa, niko peke yangu…

MENEJA-DOKOA:

Loo, haifai hivyo dunia wawili wawili eti. Njoo tusakate rumba pamoja.

MAKALIKITI:

Asante.

MENEJA-DOKOA:

Eeer…. mimi naitwa Meneja-Dokoa, Eeer…. ni meneja wa Kampuni ya Kondomu….. Ha! Ha! ha! Ni mtu mkubwa kidogo… Tunanunua na kuuza kondomu nchi nzima. Na kama ikianzishwa Wizara ya Kondomu, eeerrr…. naona kuna dalili kuwa naweza kuambulia chochote. Ha! ha! ha!…. Eeeeer…… Ha! ha! ha! Nimekuambia, eeer.. ni mkubwa kidogo, eeer… sijui wewe kisura unaitwa nani mwenzangu?

MAKALIKITI:

Naitwa Makalikiti…. Nasoma Kidato cha Sita.

MENEJA-DOKOA:

(Akionyesha furaha): Ohoooo…,. Msomi, Vizuri sana Bi-Msomi. Saafi sana, Unajua…er….sisi watu wakubwa hatupendi wale….er….wa mitaani…. Unajua tena siku hizi, mambo yamevurugika kidogo. Hivyo hupendelea dogodogo za shule kama wewe….. Ha! ha! ha!.

MAKALIKITI:

Uwongo tu…

MENEJA-DOKOA:

Kweli kabisa. Unajua, lazima tahadhari kabla ya hatari, eeerr… kuna viini siku hizi…….

MAKALIKITI:

Viini

MENEJA-DOKOA:

Huwezi kuelewa mambo hayo bado uko shule…. Utapenda bia kidogo?

MAKALIKITI:

Ah! Nimejinunulia mwenyewe soda zimenitosha. Ah! kwanza naona bora nirudi nyumbani sasa hivi. Karibuni tutaanza mitihani, nikajisomee kidogo.

MENEJA-DOKOA:

Oh! Hapana shaka…. Nina gari hapo nje. Wacha nikupe lit’ti kidogo.

MAKALIKITI:

Asante sana, nitashukuru…

MENEJA-DOKOA:

Nami nitashukuru saana kama lugha zetu zitaelewana kidogo. Usiogope mtoto, tunaweza kwenda. Usiwe na shaka na Meneja-Dokoa. (Wanacheka. Wanashikana mikono na kuondoka pamoja. Muziki unaendelea kwa muda hali watu wakitawanyika polepole kila mtu na wake… Sautiya muziki inafifia, kwa mbali mlio wa ngoma la mgambo – inapozimika vilio kwa mbali…..)

MTAMBAJl:

Jama… Viini hivyo… Masiku yanakwenda.. vinasam-baa… (Ghafla vilio vya nguvu kabisa).

MTAMBAJI:

Kuna nini tena hapa?

MTU 1

Baba kwani hujasikia kilio!

MTAMBAJI:

Kwa kweli nami hili sijalisikia. Kilio, nani amefariki

MTU 1

Amefariki yule binti yetu.

MTAMBAJI:

Binti yenu!

MTU 1

Ndiyo. Yule mkubwa. Makalikiti.

MTAMBAJI:

Lahaula: Makalikiti!

MTU 1

Na leo ndiyo mazishi yake.

MTAMBAJI:

Poleni sana, vipi alikuwa anaumwa nini?

MTU 1:

Eh! Mwanangu hata vinaeleweka! Mtoto alianza tu kuwa anachokachoka tu kila wakati. Ghafla akawa vijihomahoma havimwishi, mara kuharisha mara kutapika. Kutapika ndiyo kutapika mwanangu, dawa na dawa tumemaliza. Waganga na waganguzi! Wapi! Mtoto anazidi kunyang’onyea tu. Khe! maia tukaanza kumwona anapata utando mweupe mdomoni. Nywele zikaanza kumng’oka kichwani. Sisi tukafikiri labda kwa ajili ya yale madawa yao ya kutengeneza nywele, maana nasikia huwa yanaharibu nywele mwishoni. Khe! Mara matezi shingo nzima baba’. Mwishowe yakaanza kumtambaa makwapani. Lo! Mwanangu matezi balaa! Maana yalim-wenea mpaka sehemu zake za siri. Mtoto akawa hali chakula. Kitu chochote hakipiti kooni. Kunywa uji kunywa na wewe! Kila akipimwa damu inazidi kupungua tu. Kila anapoongezewa wapi inazidi kupungua tu. Maajabu baba, ngozi yake ikaanza kuota ukurutu. Ukurutu, ukurutu. Ngozi ya mwanangu. Makalikiti iliyokuwa laini, ilivyokuwa inawaka – leo kuota ukurutu! kutahamaki madonda! Mbona ilikuwa kazi baba. Wa kumsogelca kwa kuwa ni damu yako. Madonda mwili mzima. Uji haupiti! Hapa mwishoni baba, Makalikiti alibaki ufito mtupu. Ufito baba. Eh! Mwishowe tena Mwenyeezi Mungu akamchukua mja wake…. Mwanan-gu mie… Makalikiti katutoka…. Mwanangu mie jama cech…. (vilio tena. Mara anaingia Meneja-Dokoa na begi lake mkononi)

MTAMBAJI:

Ohoo Meneja – Dokoa!

MENEJA-DOKOA:

Oh! Kumbe unanifahamu …er… Ndiyo. Jina langu ni Meneja-Dokoa… lakini siku hizi nimepata uwaziri mdogo kwenye Wizara mpya ya Kondomu. Kwa-ni bado hujasikia…?

MTAMBAJI:

Ah! kumbe ndiyo wewe mwenyewe uliyeapishwa mwezi juzi! Mimi nilidhani majina tu kufanana. Hongera.

MENEJA-DOKOA:

Asante. Er…Na hivi unavyoniona, natoka Sweden, er… tulikuwa na mikutano yetu ya kimataifa.

MTAMBAJI:

Ahaa, Kumbe umetoka safarini.

MENEJA-DOKOA:

Ndiyo kwanza hivi unavyoniona nimetoka Airport. Gari yangu nimeegesha pembeni kidogo. Er…. Nimepitia sehemu hii kumwona binti mmoja anakaa jiraninahapa. Lakini naona hapa mambo si ya kawaida er….. umesema kuna msiba, nani amefariki?

MTAMBAJI:

Ee, amefariki binti wa mwenyc nyumba ile pale… Binti yake mkubwa!

MENEJA-DOKOA:

Binti yake?

MTAMBAJI:

Ndiyo, yule aliyekuwa anaitwa Makalikiti.

MENEJA-DOKOA:

Oh! No! Makalikiti! My God! (Kimya kidogo) alikuwa mgonjwa?

MTAMBAJI:

Ndiyo ameugua kwa muda kiasi…. kiasi cha miezi mitatu hivi….

MENEJA-DOKOA:

Alikuwa akiumwa nini?

MTAMBAJI:

Ah! Bwana hata haieleweki vizuri. Lakini nimesikia watani wanapitapita hapa wanasema kuwa amekufa kwa Slimufiti…

MENEJA-DOKOA:

Slimufiti! Ndiyo ugonjwa gani huo?

MTAMBAJI:

Hata mimi, Mheshimiwa sijui. Hebu tumwite yule pale mtani wao labda atacuelewesha…. Aloo Mtani…. Mtani! Hebu njoo utueleweshe vizuri (Mtani anakuja).

MTANI:

Enhe, Mnasemaje Mabwana.

MENEJA-DOKOA:

Er….. nilikuwa naulizia, ugonjwa aliokuwa akiumwa marehemu Makalikiti….

MTANl:

Ahaaa! Alikuwa akiumwa Acha Iniue Dawa Sina!

MENEJA-DOKOA:

Ndiyo ugonjwa gani huo?

MTANI:

Ndiyo Acha Iniue Dogodogo Siachi!

MENEJA-DOKOA:

Mwananchi hebu uache utani… Maana mimi ni jamaa ya hawa waliofiwa… hivyo…

MTANl:

Ahaaa! Nakuona tu kuwa kilio hiki kinakuhusu…. Na wewe unamunasaba nao sio? Ndugu yao? Sema upesi tukutoze faini ya kuchelewa kufika………

MENEJA-DOKOA:

Hapana, mimi er…. jamaa tu.

MTANI:

Anhaaa! Jamaa! Basi jamaa yangu nikupashe upashike. Makalikiti alikuwa anaumwa eidisi! Unajua eidisi wewe….. Ukimwi:! (Meneja-Dokoa anaanguka ghafla chini. Watu wanamzunguka na kuanza kumpepea…. sauti za); “Imekuaje jamani… Amezirai…. Vipi tena….. Ameanguka tu mwenyewe….Loh! Ajabu…. Lete Maji tumwagie atainuka.” (Wanaendelea kumhudumia)

MTANI:

Jama ajabu hi (Anacheka) Tangu Makalikiti amekufa, najionea vioja vinatokea! Juzi mabwana watatu, majina yao nayahifadhi, watu wenye heshima kidogo, waliposikia kuwa Makalikiti amekufa, wameacha kazi na kurudi makwao! Ghafla tu! Mh! vituko haviishi. Mzee Dezo naye tangu amesikia Makalikiti kafa akili zimemduru! Anatapatapakuzidi kuku anayetaka kutaga. Anataka hata kucholopoa nguo! Jana jioni nimeinwona anakwenda mikojo inamporomoka, suruali lote chepechepe! Mwenyewe hana hili wala lile! (Anacheka). Kha! Na kuna watu kama wanne hivi, nasikia wamehamia kwa waganga! Mjomba wangu naye ameenda kung’ang’ania hospitali! “Nipimeni nipimeni!” Makubwa haya! Haya, sasa tena huyu bwana. Hata kusema nashindwa! Tumek-wisha jama.

MTAMBAJI:

Nasikia ulimpeleka Toza Kwa Mganga!

MTANl:

Eh! Kwani mganga mmoja! Siku hizi Toza kawa mtu! Mabadiliko makubwa! Basi fedha zake zote zitaishia kwa waganga. Juzijuzi hapa, kama mwezi mmoja hivi uliop-ita, tulimwona mtu mmoja (Anaanza kugeza) “Mimi nimeepushwa na shetani…. nilikuwa naumwa tumbo, natapika usaha, waganga wote nimemaliza – wapi sikupona! Mwishowe nikalazwa hospitali nifanyiwe operesheni… Basi nikiwa nikisubiri huku nikiomba, usiku wa tatu tangu nilazwe, nikaamka na kuona mwanga mkubwa! Nikaambiwa imani yako imekuponya! Na si hivyo tu, umepata uwezo wa kuponya Wagonjwa, viwete, wakoma, wenye vichaa, vipofu, mabubu waliopooza na wagonjwa wote wengine. Njooni kwangu mpate tiba…. Nina uwezo! Nina Nguvu!…. Nina Uwezo…..” Basi mimi nikamwambia Toza, bwana Toza tumpeleke Makalikiti shoga yako kwa yule bwana muombeaji. Akasema, ah, bwana mimi mwenyewe vilevile nina matatizo. Twende wote. Basi tukawaambia wazazi wa Makalikiti tukaenda nao kwa huyu bwana. Basi akaomba, akaomba Alipoona anashindwa, kaanza “Ah, Huyu ana pepo mbaya huyu. Na huyu mwanamke, unaona macho yake. Kipofu! Lazima atubie dhambi zake. Na afadhali ashukuru amekuwa kipofu kwani angekuwa na macho angekuwa mwovu sana huyu…” Na sisi tukaanza kumeka! Mhubiri wa uongo! Ati ana uwezo! uwezo gani? Mpigeni mawe! wee… alifyatuka kama risasi! Ha! ha! ha! Nawaambieni makubwa! Ugonjwa huu hauna tiba hata va kuombewa! Na tangu Makalikiti amekufa…. (MENEJA -DOKOA anazinduka. Anainuka anajikung’uta) Loh! Pole bwana, naona huyu marehemu anakuhusu sana…

MENEJA-DOKOA:

Aah! Ndiyo, nina ugonjwa wa moyo oa huyu aliyefariki, ananihusu kidogo…………

MTANI:

(Kwa chati) Anha….. anakuhusu kidogo….. La! Nasikia na huu ugonjwa hauna tiba!

MENEJA-DOKOA:

No! No! Tiba ipo! Lazima ipatikane. Mimi ni Waziri-Mdo’go Nitaagiza kondomu bilioni mia mbili!

MTANI:

Khe! zote hizo, watu wanafanya mara ngapi kutwa!

MENEJA-DOKOA:

(Bila kumsikiliza) Na tutatekeleza maazimio yote ya Sweden. Hatuwezi kyacha watoto wa shule kama Makalikiti wafe ovyo!

MTANI:

(Akicheka) Ama kweli Makalikiti aliwaokota wengi. Eti mtoto wa sbule, Makalikiti alikuwa na duka.

MTAMBAJl:

Duka?

MTANI:

Ndiyo! Duka la mwili wake. Akiuza kwenye mabaa, madisko, majumbani, mitaani na kwenye gesti.

MENEJA-DOKOA:

Lazima juhudi zote za utafiti zifanywe! Nitapita nikiwahamasisha mimi mwenyewe binafsi waganga wa jadi watafute tiba. Nitahakikisha wanapata misaada….

MTU 1

(Kwanguvu) JAMANI! Nimesema tusikilizane! Nimesema mazishi kesho, hivyo tunaweza kusambaa mpaka kesho…. (Wanaenda kando. Maombolezo).

MTAMBAJI:

Kampeni alizoanzisha Meneja-Dokoa si mchezo. Kondomu ziliuzwa mno. Watu wakafungua viwanda vipya vya kutengenezea kondomu. Utafiti ukazidi, lakmi utatuzi ukazidi kuwa tata, kwa nini tusijiepushe na mzizi wa tatizo – Uasherati?

MTANl:

Nzi kufia kwenye kidonda si haramu, acha ushamba.

MTAMBAJ 1:

Tutakwisha jama lazima tuzingatie kampeni. Vikundi vya sanaa visaidie….(Anaingia Daktari na kundi la wauguzi).

DAKTARl:

Kufa kufaana ndugu! Haya jama Manesi. Kama mlivyosikia pesa za msaada wa kampeni hizi zimekuja toka nje. Asante kwa waziri – mdogo wa kondomu! Hekoo (makofi) Sawa, sasa jukumu letu ni kubwa, lazima tuzichangamkie.

Haina haja ya kutafuta vikunda vya kwaya au maigizo toka nje sisi wenyewe kwayaa… (Anapanga sauti ovyo ovyo) Haya tyuni… Wote kwa pamoja! (Wanaimba vibaya mno lakini wanajishangilia) Hekoo… Basi tuimbe wimbo wetu special Moja! Moja! Mbili! Tatu!

(wanaimba)

Tumia mipira, ni kinga bora!

Tumia mipira ni kinga bora!

Tumia mipira ni kinga boia!

Mabibi na Mabwana, tumieni nupira! Hii ni kiaga ni kingaa bora ya Ukimwi. Vaeni hivi (wanavaa wote mipira kwenye vidole)

Tuaua mipira, ni kinga bora!

Tumia mipira, ni kinga bora!

Tumia mipira, ni kinga bora!

Hekoo (Wanajishangilia kwa nguvu)

DAKTARI:

San kabisa. Hebu sasa tujaribu mdundiko wetu wa AIDS). (Ngoma ya mdundiko inarindima wutacheza kila mtu vyake wakishangilia na kujipongeza kwa nguvu) Mambo safi, safari yetu tutazuru miji yote na kwaya yetu. Naiti zake si mbaya, haya tupumzike kidogo (wanaenda pembeni)

MTAMBAJI:

Ama kweli kufa kufaana. Lakini pamoja na hayo viini vikaenea….

MTANI:

Jama hii balaa! Hivi viini hatari, nasikia ukikanyaga tu mavi au matapishi ya mgonjwa wa ukimwi tayari umeshaupata!

MTAMBAJI:

Chumvi hizo zimeanza!

MTANI:

Akikupigia chafya tu, basi umeshakukumba na wewe.

MTAMBAJI:

Uzushi huo!

MTANI:

Tena ukimpa mkono tu ndiyo umekwisha…,

MTAMBAJI:

Maneno ya watu!

MTANl:

Ukishirikiana nao wenye Ukimwi vyombo vya chakula, yoo au vinywaji ndiyo tena umeshanunua sanda!

MTAMBAJI:

Bwana acha kupotosha watiu!

MTANI:

Na ukimtunza mgonjwa wa ukimwi basi kachimbe kabisa na kaburi lako, usitupe shida sisi watani….

MTU 1:

(Amfukuze Mtani) Toka hapo afriti mkubwa. Sisi tunaumwa halafu wewe unatupigia makelele! Yala kichomi…. Yalaa…. Nam anisaidie nakufa mie jama ee. (Anajikunyata)

KORIDO-DOKTA:

(Anasogea na kumtazama) Loh…. Pole sana mwananchi. Ngoja nikuchunguze. Vaa… Nywele zako zimekuwa nyekundu naona.

MTU 1:

Ah! sijui kwa nini….

KORIDO-DOKTA:

Na unakohoa kidbgo.

MTU 1:

Kidogo? Usiku silali dokta! Na mapele yamenianza mwilini

KORIDO-DOKTA:

Vipi umewahi kufika hospitalini?

MTU 1

Siku zote. Wananiambia ati ugonjwa hawauoni.

KORIDO-DOKTA:

Umekwisha ndugu, siwezi kukutibu. Una Ukimwi!

MTU 1:

(Akikimbia) Yalaaa… Tumekwisha!

MTANl:

(Anaingia na kumfukuza Korido-dokta) Wewe shetani kabisa! Unatangaza Ukimwi hadharani unadhani togwa! Hili ni balaa! Sawa na Gharika. Uchunguzi gani unaofanya! Kazi kuzurura tu! Ukimwona mtu anavipele kidogo basi ameshakuwa na Ukimwi.

MTAMBAJI:

Kumbe ana matetekuwanga!

MTANI:

Unaona basi. Mtu akikohoa saana unasema ana Ukimwi.

MTAMBAJI:

Kumbe ana kifua kikuu!

MTANI:

Unaona basi. Konfyusheni tupu. Mtu akichongeka kwa gongo, likamuua utasema Ukimwi.

MTAMBAJI:

Kumbe amekufa kwa maflgo kushindwa kufanya kazi. Na watu wataogopa hata kuisogelea maiti yake bure tu!

MTANI:

Mnaona basi! Konfyusheni tupu! Hatujui lile wala hili. Ah! Aisey, Mtambaji hivi ni kweli Meneja-dokoa naye alikufa… kwa nini ile… “Kidini-feilia” kami wanavyotucleza!

MTAMBAJI:

Eh! Ngoja nikueleze alivyokufa halafu utajaza mwenyewe, sitaki majungu mimi!

MTANI:

Enhe!

MTAMBAJI:

Meneja-dokoa alizunguka nchi zima kutafuata dawa! Karuka maji, kajaribu MM II wapi. Kajaribu Morokuna-mambo, haikufua dafu. Mwishowe akarudishwa hospitalini. Kwa kuwa yeye ni mtu wa kufahamika, Manesi walikuwa wanashinda kutwa nzima kumsafisha na kumpa dripu! Lakini wapi! anazidi kukonda na kuishiwa nguvu.Wakawawanashika migozi kwa mikasi kumwingiza mdomoni. Wanamchokonoa wee, ndiyo wanajaribu kumpa viuji. Wapi, vinarudi tu! Haja kubwa na ndogo hapo hapo – Nguvu hana tena. Kutwa nzima akiharisha. Wanabadili mashuka mpaka wanachoka.. Mwishowe mgonjwa mwenyewe akaungama.

MTANI.

Eh! Kamtaja nani? Makalikiti huyo!

MTAMBAJI:

Hapana! Hakusema Makalikiti.

MTANI:

Kumbe?

MTAMBAJI:

Toza!

MTANI:

Yalaa – tumekwisha! Wote! Hakuna cha Bwana Vodka wala Doladola, wala jujumani, wala Yohana mtembezi, wala nani! Tumekwisha!

WOTE:

Yalaa Tumekwisha!

Yalaa meja Dezo!

Yalaa Toza!

Yalaa Mtani!

Yalaa sisi wote!

MTAMBAJI:

Jamanisiri zote zimefichuka. Mimi na Dezo tumekula chungu kimoja hamna atakayesalia. Hamna mtu wa kumzika mwenzie! Sote tulitopea mno kwenye uasherati. Sote tulivunja masharti. Sote tulizikejeli kampeni. Kila mtu ajichimbie kaburi lake. Kila mtu avae sanda yake!

MTANI:

Ngojerii kidogo jama msife. Nasikia ndugu zetu wamegundua KEMRONI. Kiboko ya Ukimwi!

MTAMBAJI:

Bwana Doladola anaitilia mashaka lakini…..

MTANI:

Kama kawaida yake. Dharau tupu. Anaona aibu kwa kuwa hajaigundua yeye. Wivu unamsumbua.

MTAMBAJI:

Tusiseme wivu tu. Utafiti bado unaendelea. MTANI: Hata hivyo ni dalili nzuri. Hekoo utafiti wa ndugu zetu…

WOTE:

Hekoo!

MTAMBAJI:

Lakini mji wetu unahitaji KINGA siyo tiba! Jihad-hari kabla ya hatari. Nasi hatukutahadhari! Tumekwisha!

MTANI:

Sielewi…

MTAMBAJI:

Huelewi! Kemroni itaponyesha wengine siyo wewe! Wewe ulihitaji kinga kuacha uasherati wako! Sasa umechelewa. Vaa Sanda! Chimba kaburi lako! VAENI SANDA! Tulidharau kinga. TUMEKWISHA!

MTANI:

Yalaa Tumekwisha!

WOTE:

Yalaa Tumekwisha! TUMEKWISHA! TUMEKWISHA! (wanavaa nguo zao za mifupa. Wanaanza kujinyonganyonga kama mwanzo wa mchezo. Sauti za vilio zinazidi mno. Wanajinyonganyonga. Ngoma kwa mbali inasikika – la mgumbo. Makelele mengi ya vilio na ghasia za maombolezo. Ngoma inalia kwa nguvu sana na kuzimika ghafla, wote wanaanguka chini. Kimya).

MWISHO


Taswira

ISBN NO. 9976 971 0 28

Baraza la Sanaa laTaifa
Kimepigwa Chapa na Inter Press of Tanzania Ltd.
P.O. Box 6130 Tel: 72051/72283 Dar es Salaam