TAMTHILIYA YA MKUTANO WA PILI WA NDEGE

By , in Tamthiliya on . Tagged width:

WAHUSIKA

MTANI:

Mpiga hadithi

MGANGA WA JADI

MTUA

SHANGAZI:

Dadake Mtua

MAMA:

Mke wa Mtua

MSHERI:

Mtoto wa Kiume wa Mtua

MAISA:

Mtoto wa kike wa Mtua

WATU

NDEGE

MAELEZO YA JUMLA

Wakati: Ni huu

Mahali: Tulipo

Sehemu ya Kuchezea: Uwanja wowote ambao utawawezesha wachezaji wasiwe mbali na hadhira. Upande wa katikati lakini nyuma ya uwanja kuwe na mfano wa nyumba. Hii ni nyumba ya mtu lakini isijengwe kama nyumba kweli, hata hivyo itambulike kama makazi ya watu.

Wachezaji: Ni muhimu mchezo uchezwe kwa mfululizo na wachezaji waweze kubadilisha wahusika upesi upesi katika sehemu zile zinazotakiwa. Idadi ya wachezaji inategemea na matakwa ya watayarishaji lakini ni muhimu kuwa nafasi za wahusika kadhaa zichezwe na mtu huyohuyo. Kwa mfano wale wahusika ndege wawe ni wale wale wanaocheza nafasi za binadamu katika sehemu nyingine za mchezo.

Onyesho la Kwanza

(MTANI anaingia huku anaimba na kupiga manyanga, anaecheza kuzunguka uwanja mzima.)

MTANI:

Mwanangati kafumaniwa
Leo Mwanangati atakiona
Kafukuzwa, kapigwa
Mwanangati uchi amekimbia,
Nguo ya kuazima haistiri
Aliambiwa Mwanangati,
Usiibe, wizi ni mbaya zaidi ya kuazima
Aliambiwa Mwanangati
Mke wa mwenzio haramu
Mwanangati aliambiwa
Fanya kazi uoe
Mkono mrefu mbaya
Mwanangati eeh.
Mwanangati kafumaniwa
Leo mikono yote kakatiwa
Mwanangati asiyesikia mkuu
Kacharazwa, kafukuzwa mbali sana
Mwanangati kafumaniwa
Leo Mwanangati
Mwanangati eeh!

(Anaendelea kucheza mpaka mwisho wa wimbo.)

MTANI: Husemwa, siku njema huonekana alfajiri. (Ananusa hewa.) Huumph!!! humph! Hewa nzito hapa!

(Kutoka pande zote wanaingia watu waliojifunika gubigubi. Wanaisogelea nyumba na kuilemea mate, wanaitupia lakataka na kuitukana. Wanailaani nyumba na wakazi wake. Wanaioka.)

MTANI: Nilifikiri niliitwa niwapigie hadithi lakini naona mandhari yamejengwa kwa vituko vingine. Ukweli lakini ni kuwa hakuna neno lisilo na mwenzie au kituko cha peke yake. Hata hadithi zina ncha mbili tatu. Hadithi hii ina mizunguko. Ncha mbili lakini uelekeo ule ule. Kituo cha mwisho kile kile. Katika mwanzo wa mmoja kuna mwisho na mwingine, naye huyo ni mwanzo wa mmoja. (Ananusa hewa.) Hewa nzito! Shuzi? Harufu mbaya iliyoachwa na wale waliokuja? (Ananusa hewa) Hata. Sio shuzi wala harufu mbaya ya mdomo ulioukwepa mswaki. Hewa nzito zaidi. Si mnaisikia hiyo? Imejaa uwanja mzima. Nuseni! Hamuamini? Nuseni! Aaaah! (Anashika pua.)

Kutoka ndani ya nyumba sauti za manyanga na kuimba kunasikika. Mikiki ya miguu kama vile washiriki wanacheza ngoma kufuatana na nyimbo na manyanga pia inasikika. Zote hizo zinafikia kileie halafu zinakatika ghafla. MAMA na SHANGAZI wanaingia. Wanasimama kuelekea mlango wa nyumba. MGANGA analoka. Ameskika manyanga na vitu vyake vya kuagulia. Anakaa karibv na mlango kuelekea hadhira. MAMA na SHANGAZI wanachuchumaa kungojea MGANGA atafanya nini. Kimya. MGANGA anaimba peke yake kvanza halafu baada ya muda waliopo wanamsaidia.)

Hilelee, hilele, Hilele hiieleleeee’!
Aliliaya
Samaki wa wenyewe
Aliliaye
Atanyimwa fyu
Aliliaye
Imama
Hilelee, hilele, Hilele, hilelelee!!

(Ngoma ya kuagua inazuka na kuchezwa mpaka wole wamechoka.)

MGANGA: Ugonjwa huu ni mbaya. Ni mbaya sana. Si mmeuona?

WOTE: Ndiyo.

MOANGA: Mmeunusa?

WOTE: Ndiyo!

MGANGA: Ugonjwa wa hatari sana.

SHANGAZI: Sasa tufanyeje?

MGANGA: Ni juu yenu. Inawezekana mmekwishachelewa. Si niliwaambia mara ya mwisho?

SHANGAZI (kwa mkazo): Sasa tufanyeje?

MGANGA: Ile dawa maalum lazima kwanza ipatikane.

SHANGAZI: Tumekwishanituma mtu.

MGANGA: Mmempa miiko yote?

SHANGAZI: Usitie shaka anajua wajibu wake. Kingine?

MGANGA: Mtayarishe mbuzi mwekundu, kuku watano: mweupe, mwekundu, rangi ya udongo, madoadoa na mweusi. Chakula cha mgonjwa na Mganga cha wiki nzima, nguo mpya za wote wawili na kipangusajasho cha shilingi elfu kumi.

SHANGAZI: Elfu kumi?

MGANGA: Kama hamtaki basi. Huu ni ugonjwa mbaya sana. Si waganga wengi wako tayari kumtibu. Kama hamtaki basi. (anaanza kuondoka.)

SHANGAZI: Siyo hivyo. Hali yetu mbaya siku hizi.

MGANGA: Msinipotezee wakati.

SHANGAZI: Hapana. Labda Maisa atafanikiwa.

MGANGA: Maisa?

MAMA: Huyo tuliyemtuma akatafute yale majani unayohitaji.

SHANGAZI: Atapita kwa rafiki zake Mtua na kuwaomba wasaidie.

MGANGA: Pesa?

SHANGAZI: Ndiyo.

MGANGA: Mtoto wa kike? Mmemtuma kazi hiyo mtoto wa kike?

SHANGAZI: Hakukuwa na mwingine. Tuliobaki ni wazee na safari hiyo ni ndefu na labda ina hatari.

MAMA: Lakini Maisa amezoea hayo. Ameshaishi huko na kufanya kazi.

SHANGAZI: Na ameahidi kupitia akiba zake alizoziacha huko.

MAMA: Anaelewa wajibu wake. Atafanya kazi na kuleta vyote vinavyohitajika.

SHANGAZI: Mtua ana rafiki wengi, watasaidia tu.

MGANGA: Msiniite kabla hamjazipata pesa wala vitu. Mna hiari ya kumtafuta Mganga mwingine.

SHANGAZI: Mwingine tumpate wapi? (MGANGA anaondoka.)

MTANI: Mtaluona leo: Mtaka cha uvunguni ni sharti ainame. Tembo kaziona nyasi kainama mpaka kavunjika mgongo.

SHANGAZI: Yule mtoto asiporudi na vitu tulivyomtuma, ataluona.

MAMA: Utamfanya nini?

SHANGAZI: Ungemfunza mtoto wako ipasavyo sasa tusingekuwa na wasiwasi – wewe na mwanao.

MAMA: Niache mimi na mwanangu. (Wanaiazamana kwa chuki.)

(MTANI anapiga manyanga na kucheza. MAMA anacheka na kwenda kukaa karibu naye.)

MTANI: Niambie juu ya Maisa.

MAMA: Ni mtoto kama wengine.

SHANGAZI: Jeuri, kalelewa vibaya.

MTANI: Mkubwa na ana kazi.

MAMA: Hodari wa kazi.

MTANI: Ana kazi gani?

MAMA: Sijui.

MTANI: Hujui?

MAMA: Ninajua ana kazi. Hiyo inatosha.

MTANI: Na mradi aleta unga na akiba benki yaongezeka sivyo? Hmm!! Ni karani. Mwezi shilingi mia nane. Hapana. Baada ya kodi, matumizi, hawezi kuweka akiba. Kazi gani nyingine. Ualimu. Hmmmm! Hakusoma sana yeye. Labda mchuuzi.

SHANGAZI: Una maana gani mchuuzi?

MTANI (anaimba):

Nunua viatu
Vikuletee mikogo ya sikinde na msondo
Utanepa, utaongezeka urefu si kidogo.
Juu yao sketi ya kulingana
Imebana kiuno, imebana goti
Inasawazisha tako kwa maringo
Usisahau juu, ziwa lachungulia kwa mwito.
Tia hereni, tia bangili
Malizia na nywele za bandia kichwani
Rangi ichungulie vidoleni na kupiga kelele mdomoni.
Kungu si lazima, wanja utabadili jicho na nia.
Nunua viatu, nunua gauni
Vishangiliwe na hereni na bangili
Kumulika Mdomo, ziwa, kiuno na paja la mwili.
(Anamaliza kuimba.)

MTANI: Mjini kuna wanunuzi wa aina nyingi na mtu anaweza, kwa kutumia akili, kuuza chochote kile na kuwa mchuuzi. Si mjini tu hata hapa.

MAMA: Maisa hana kitu cha kuuza

MTANI (anacheka mpaka machozi yanamtoka): Mie nafikiri kazi ya uchuuzi inamfaa sana huyo Maisa wenu.

SHANGAZI: Acha mzaha. Matatizo yametusonga lakini wewe Unaleta mzaha.

MAMA: Hatuna chochote. Pesahamna. Vitu vyote vimeuzwa au vimekwenda. Hamna chakula, hamna nguo.

MTANI: Hamna dawa.

SHANGAZI: Maisa akirudi…?

MTANI: Ndiyo mnamngoja Maisa

MAMA: Tutamngoja Maisa.

(Kimya.)

MTANI: Njaa inauma.

MAMA: Hakuna chakula nimekwambia.

MTANI: Aah, ndiyo, tumngoje Maisa.

MAMA: Atarudi

SHANGAZI: Una hakika?

MAMA: Tungoje. Tumngoje Maisa (Kimya.) (Anaguna) Na baridi hii mtaniambia…

SHANGAZI: Hakuna blanketi.

MAMA: Labda Maisa ataleta.

MTANI: Tumngoje Maisa.

SHANGAZI: Tutamngoja Maisa.

MTANI: Ndiyo, tumngoje Maisa. Haya ngojeni mie nakwenda.

MAMA: Usiondoke Mtani!

(Kutoka ndani, sauti ya maumivu inasikika. Wote wanashika pua.)

MTANI: Maiti hanuki hivi.

SHANGAZI: Fukiza hiyo miti shamba tena. Inasaidia (MAMA anafukiza.)

MTANI: Ameanza lini kunuka hivi?

MAMA: Tangu mwanzo wa ugonjwa. Kila siku harufu inazidi.

SHANGAZI: Tumeshaizoea.

MTANI: Samaki aliyeoza hafui dafu.

MAMA: Ugonjwa mbaya.

MTANI: Ugonjwa wa namna hii sijapata kuuona, huusikia tu. Hata mgonjwa akipona harufu humwandama, nasikia.

SHANGAZI: Ugonjwa gani huo?

MTANI: Kama huu, usio na jina. (Kwa MAMA) Fukiza, fukiza kabla pua hazijakatika (MAMA anafukiza).

MAMA: Sasa twangoja. Mgonjwa hana dawa anangoja kutibiwa. Yuko taabani. Miguu imepooza, mgongo umefyatuka. Vidole havikunji wala kukunjuka. Hawezi kula lakini vidudu vyamla yeye. Hawezi kunusa wala kusikia lakini kila kiumbe cbamnusa na kumsikia yeye.

MTANI: Taabani. Yuko katikati. Nyuma kuna uzima, mbele kuna mauti. Wa nyuma wamwita; “Rudi. Bado siku zako. Ahera bado si yako.” Wa mbele wamvuta, “Karibu! Umemaliza kazi yako. Pumzika. Toa orodha yako.” Yu katikati. Lakini uwezo si wake. Nyuma au mbele ni Maisa atamtoa kihere. “Nenda” au “Njoo” dawa ya Mganga itamwita. Na sisi? Twangoja. Njaa inatuuma, baridi imetukumbatia, taabu zimetuegemea. Twangoja matibabu ya Mtua. Eeeh, naelewa.

MAMA: Twamngoja Maisa.

MTANI: Twangoja pesa za Maisa.

SHANGAZI: Twangoja mganga na dawa yake.

MTANI: Twamngoja mganga huku pua tumezishika. Wao ni wana ndugu. Miye je? Aah, miye unaweza kusema ni ndugu pia. Damu husemwa ni nzito. Sijulikani lakini ni ndugu. Napenda jina la Mtani lakiui Mtua alitupa mbegu yake upenuni siku moja. Ikaota. Kaipuuza. Ikakua. Kaikataa. Ikakomaa. Kaikana. Nipo. Hanijui lakini namjua. Upofu wa kuku haumfuti mwewe. Jamani! Hii harufu itanishinda.

(Kimya.)

MAMA: Hadithi!

MTANI: Hadithi!

SHANGAZI: Hadithi?

MAMA: Wakati tunangojea.

SHANGAZI: Hapana. Tunapiga hadithi wakati wa matanga na….

MTANI: Haya ni matanga.

SHANGAZI (kwa ukali): Sitaki hadithi!

MTANI: Mimi ni mtani.

SHANGAZI: Wewe ni shetani.

MAMA: Ndiyo, wewe ni mtani. Neno lako ni amri. Tamka upate maamuma.

(MWANAMKE anaingia.)

MWANAMKE: Hodi, hodi wenyewe!

MAMA: Karibu!

MWANAMKE: Hamjambo?

MAMA: Hatujambo

(MWANAMKE anaangalia huku na kule. Anasikia harufulakini anajikaza. Anataka kukaa lakini anaona hakukaribishwa. Kimya.)

MWANAMKE: Eee…, habari za hapa?

MAMA: Nzuri.

MWANAMKE: Hamjambo wote?

MAMA (kwa mkazo na polepole): IIatujambo!

(Kimya.)

MWANAMKE (anasafisha koo): Hamjambojambo, sijui?

SHANGAZI (kwa ukazi): Una shida gani?

MWANAMKE: Shida? Aaa (anacheka) ndiyo! Nilikuwa na shida na Mtua.

SHANGAZI: Hayupo.

MWANAMKE: Hayupo? Nilifikiri…

SHANGAZI: Hayupo!

MWANAMKE: Hmm! Lo, bahati yangu mbaya.

(Kimya.)

SHANGAZI: Sasa?

MWANAMKE: Atarudi lini, sijui?

SHANGAZI: Sijui.

MWANAMKE: Basi nitarudi baadaye. (Anaanza kuondoka halafu anakumbuka.) Nitauacha mzigo wake, karibu nisahau.

SHANGAZI: Nini?

MWANAMKE: Mtua mwenyewe atafahamu. Alikuwa ananidai. (Anaacha kifurushi na kuondoka. Kimya kidogo).

MAMA: Hadithi.

MTANI: Mtauficha ugonjwa huu mpaka lini?

SHANGAZI: Haikuhusu.

MTANI (anacheka): Huwa nasahau mara nyingi.

MAMA: Hadithi.

MTANI: Ndiyo, hadithi.

MAMA: Hadithi.

SHANGAZI: Haya hadithi, mie simo.

MTANI: Hadithi, hadithi!

MAMA: Hadithi njoo!

MTANI: Hadithi! hadithi!

MAMA: Hadithi njoo!

MTANI: Barabara. (Anaimba kidogo bila maneno halafu anacheza ngoma yake mwenyewe akizunguka uwanja wa kuchezea.) Ehee! Kaondoka chenjagaa.

WOTE: Kajenga nyumba kakaa.

MTANI:

Mwanangu mwana siti
Kijino kama chikichi
Cba kujengea kikuta
Na vilango vya kupita.

MAMA: Naam twaib.

MTANI: Eehe! Waswahili husema ni mtu mpumbavu anayeacha mavi kizingitini ili akirudi asikie harufu na nzi wengi nyumbani. Utavuna unachopanda, na usikwee mti kujificha baada ya kutukana watu kwani siku moja…

SHANGAZI: Ndiyo hadithi yenyewe hiyo?

MTANI: Subira. Polepole ya kobe, husemwa, humfikisha mbali.

MAMA: Nataka kulia.

MTANI: Lia, lakini sikiliza hadithi yangu.

SHANGAZI: Hana hadithi.

MTANI: Eehe hadithi. Hapo zamani za kale palitokea ndege. Ndege walikaa raha mustarehe kama viumbe wengine duniani. Kulikuwa na ndege wengi zaidi wakati ule kuliko sasa. Hao kanga, chiriku, tai, mwewe, kuku, tausi, mwali, tumbusi na mbayuwayu hawakuhesabika; wala njiwa, mbuni, bundi, kunguru na korongo. Hao na wengine wengi ambao majina yao yametoweka kama walivyopotea wenyewe. Ndege wakubwa, ndege wadogo. Ndege walioruka kwa kasi ya upepo na ilikuwa vigumu kuwafuata kwa macho. Ndege waliokuwa wazito kuruka lakini wepesi wa mbio zilizowashinda wanyama wote. Ndege wazuri na wabaya kwa tabia na umbo. Ndege waliokuwa na sauti nyororo za kushawishi sikio lolote. Ndege waliobeba rangi mbalimbali zilizoshindana na pinde za mvua.

MAMA: Naam twaib.

MTANI: Eehe. Basi ndege hao wakakaa raha mustarehe kwa karne na karne. Vizazi na vizazi. Siku zikapita. Na siku nyingi zikapita. Hata siku moja katika mwaka usio na jina, ndege wakajikuta hali yao imebadilika sana. (Anaimba ombolezo amhalo linapokelewa na washirikt wengine. MTANI anawakatiza.) Kunanini? Kifo? Ndiyo, lakini zaidi ya kifo. Kifo ni cha mara moja lakini njaa ni kifo kinachorudi kila siku. Ndiyo, ndege walikabiliwa na baa la njaa. Inasemekana njaa si mchezo. Humfanya kiumbe ale vya mwiko. Jirani humsahau jirani, kiumbe mmoja huiga tabia za mwingine na kujipoteza. Baba hamtambui mwanae na mama hujificha uvunguni kula alicho nacho. Njaa. Njaa husaliti. Ndege walikabiliwa na njaa. Si wote, bali wale waliojikuta sehemu kama hizi zetu walipata shida hiyo.

(Filimbi ikiimba wimho wa kusikitisha inasikika. MTANI na washiriki wengine wanaiga ndege wakiruka huku na kule lakini pole pole nguvu zinawaishia, wengine wanakufa, wengine hawajiwezi na wanalala tu. Mwishowe, woie wanatoweka isipokuwa ndege watatu wadhaifu, wawili wamekaa, wamejikunja. Hawa ni MWEWE na CHIRIKU. Ndege wa tatu ambaye ni mzee, TAUSI anawakaribia. Kimya.)

TAUSI: Hmmmm!

MWEWE: Hmmmm!

TAUSI (anakaa): Mgonjwa nini?

MWEWE: Nani?

TAUSI (akimwonyesha CHIRIKU): Huyo!

MWEWE: Hata. Njaa tuu.

TAUSI: Hmmmm!

MWEWE (huku akimwamsha CHIRIKU): Hee Hee! Amka bwana! Unafikiri usingizi utakushibisha!

TAUSI: Aah, unasaidia, ukilala na chango linalala.

MWEWE: Wapi. Amka bwana wee!

CHIRIKU (anaamka na kugutuka): Hmmmm! mpunga eeh! pumba!

(MWEWE na TAUSI wanacheka.)

MWEWE: Chakula, chakula, chakula tu. Sikukwambia kuwa usingizi hausaidii? Hata njozini njaa yakuandama.

CHIRIKU (anawaona MWEWE na TAUSI. Anakasirika): Kumbe ni nyinyi? Mtu hata hawezi kulala kwa amani?

MWEWE: Mwangalie. Eti anataka amani! Utapata wapi amani wakati kama huu? Kila uendako…

CHIRIKU: Kwani mtu hawezi kujaribu lakini…

MWEWE: Kujaribu hakufai kitu. Unaweza kusema kuwa hatukujaribu kila kitu kutatua matatizo yetu? Tuangalie sasa. Tuko wapi? Hata nguvu za kufikiria sasa hatuna.

TAUSI: Unajua, nilikuwa nafikiria matatizo haya yetu ya njaa yametukabili mwaka hata mwaka. Kama si jua kali, ni mvua nyingi; na kama si upungufu wa vidudu, ni ujanja wa binadamu kuficha vyakula vyao. Nimesikia hata ndugu zetu kuku wanaofugwa wamedhoofika kwa kukosa chakula. Nilikutana na TAI juzi. Huko kwao Mikumi hakuna cho chote. Amejaribu kweuda hata Serengeti. Inaonekana kuwa akina Simba na wauaji wengine hula bila hata kubakisha mifupa, na ukiona mmoja basi ujue hakuna hata uzi wa nyama.

MWEWE: Najua utadhani kuwa dunia imekata shauri kututokomeza sisi ndege.

CHIRIKU: Sijui wenzetu na mahala pengine wana shida hii hii?

TAUSI: Eeehe, ndivyo nilivyokuwa nafikiria. Kama kuna sehemu ambazo shida hii hakuna labda tunaweza kwenda huko.

CHIRIKU: Niondoke nyumbani, niende nikakae sehemu nyingine? Hata! Afadhali nifie hapa kuliko…

MWEWE: Mwache amalize basi – wee umekazana na pupa tu.

(CHIRIKU ananyamaza.)

TAUSI: Asante. Tukikata shauri kwenda, itakuwa kwa muda tu mpaka…

CHIRIKU: Hata. Nimesikia sehemu nyingine zina baridi ya barafu na manyoya yetu wengine hayawezi…

MWEWE: Mbona wee hovyo? Mwache amalize bwana wee!

TAUSI: Jawabu lingine ni kuwaalika ndege wenzetu kutoka sehemu mbali mbali kuona kama wanaweza kutusaidia. Inawezekana nao wana shida kama hii na tunaweza kushirikiana kutafuta njia. Husemwavyo, vichwa viwili ni bora.

CHIRIKU: Sasa wewe bwana unataka kutuita sisi wapumbavu. Yaani kuna mambo ambayo hayajaingia vichwani mwetu?

MWEWE: Mwenzetu amesema vyema na nia yake si kututukana. Hao ndege wengine wa dunia ni ndugu zetu, ingawa tumesambazwa sehemu mbalimbali. Maumbile yetu, damu, na ile hali ya kindege ni moja. Kwa hiyo, hilo ulilosema Tausi ni jambo zuri sana.

CHIRIKU: Sijui; mimi naona tuendelee tu wenyewe kutafuta kwa ubongo wetu njia za kutuponya.

TAUSI: Lakini mwaka wa ngapi tunajaribu tu? Ndege wengine wamekufa sana hata sijui kama kuua yeyote aliyebakia wa kabila yao, mathalan Kanga.

CHIRIKU: Shida zao ni wanadamu. Wanapenda sana kuwakaanga hao ndugu zetu.

MWEWE: Lakini njaa imewaua wengi zaidi. Kama hutaki mawaidha yake, lete yako basi. (Kimya.) IIaya kichwa kitupu…

CHIRIKU: Unanitukana?

MWEWE: Sasa?

CHIRIKU: Ngoja nitakuvunja shingo yako (anajaribu kumvamia – wanajaribu kupigana, lakini nguvu hawana.)

TAUSI: Jamani Tuangalie! Hili ndilo jawabu letu? (Anawatenganisha.)

CHIRIKU (akihema): Amenitukana!

MWEWE: Ulikitaka!

TAUSI: Basi jamani. (Baada ya muda wanaanza kutulia na kukaa chini tena.)

(Kimya kidogo. MWEWE anajanbu kuimba halafu ananyamaza.)

TAUSI: Nafikiri tuite mkutano. Tuwaalike siyo ndege wetu tu bali na wenzetu wa pande nyingine za dunia. (CHIRIKU anacheka kwa dharau na mshangao.)

CHIRIKU: Tutawaweka wapi wote hao?

TAUSI: Tutawaomba wawachague wajumbe.

MWEWE: Basi hakutakuwa na taabu.

CHIRIKU: Nyinyi watu sijui namna gani. Hata kama wakija wajumbe tu, mtawalisha nini?

MWEWE: Hilo ni swala halisi.

TAUSI: Hmmm Sikulifikiria.

CHIRIKU: Fikiria sana basi!

TAUSI (baada ya muda): Kwa nini tusiwaombe walete vyakula vyao wenyewe?

MWEWE: Vipi?

TAUSI: Tutawaeleza kuwa sisi huku tuna shida ya vyakula kwa hiyo ingetusaidia kama wangeleta chochote wawezacho.

CHIRIKU: Na labda tuongeze kuwa walete kwa wingi na sisi tuambulie.

TAUSI: Hiyo itakuwa shauri yao.

CHIRIKU: Na wale wasioweza je?

TAUSI: Hili litakuwa tatizo. Labda tutaweza kukusanya kwa wale walioweza kuweka akiba.

CHIRIKU: Akina nani hao?

TAUSI: Sijui, lakini tutaona.

MWEWE: Mimi naona tulijaribu shauri hilo na tukishindwa basi.

CHIRIKU (analalamika): Itatuchukua nguvu zetu zote zilizobaki.

MWEWE: Ni kweli, lakini wewe ungependa zaidi kukaa hapa na kufa kidogo kidogo?

TAUSI: Lazima tufanye kitu na tukifanye sasa la sivyo tutachelewa.

CHIRIKU: Jambo la kwanza ni kuwa na mpango maalum wa mkutano.

TAUSI: Kwanza mbiu. Tumpeleke mtu akapige mbiu za kutangaza habari za mkutano.

MWEWE: Huyu Chiriku ana sauti kali.

CHIRIKU (karibu kugombana): Unanitukana tena!

TAUSI: Hapana. Ni kweli. Sauti yako itafaa sana katika kazi hii. Na wewe mwewe kwa kuwa una nguvu sana utakuwa kiongozi wa kutayarisha mahali pa mkutano, kukusanya chakula na kadhalika.

MWEWE: Ndiyo kazi ninazozipenda, za kutoka jasho. (Anamwonyesha kidole CHIRIKU.) Usidokoe dokoe huko na kusahau kazi.

CHIRIKU: Na wewe kumbuka tunataka hata vifaranga waje mkutanoni. Usiwamalizie njiani.

MWEWE: Unamwona ananichokoza?

CHIRIKU: Weweje?

TAUSI: Basi, basi, tuna kazi kubwa rnbele yetu. Haya Chiriku, ondoka ukaanze.

(CHIRIKU anaanza kuondoka na kuimba lakini anakatizwa na mlio unaoloka chumhani kwa mgonjwa. Wote wanaziba pua na kungoja. Mlio unaendelea halafv unatulia. Majani yanachomwa kufukiza harufu mbaya. Wote wanaanza kutulia.)

MAMA: Hadithi!

MTANI: Naam twaib. Tulikuwa wapi?

MAMA: Chiriku anaondoka huku anaimba.

MTANI: Ehee!

(CHIRIKU anaonekana akipiga ngoma ndogo. Anaipiga huku anaimba na kucheza akizunguka uwanja. Ataendelea kufanya hivyo wakali wote MTANI anapozungumza.)

MTANI: Mbiu ikalia. La mgambo likapelekwa kutoka mashariki mpaka magharibi, adhuhuri mpaka alasiri. Chiriku aliimba; Chiriku alipaza sauti mpaka pembe moja ya dunia ikairudisha sauti itue pembe ya pili. Ujumbe ulichukuliwa na mawimbi na kutupwa katika pwani za dunia. Sauti ya Chiriku ilisafiri na mchanga wa majangwa na kutua kwenye milima. Waliozikwa siku zile waliuchukua ujumbe kaburini ukatokea upande wa pili wa dunia ya mizimu. Bila kuchoka, biia kupumua Chiriku alifanya kazi yake.

(CHIRIKU anaimba kwa sauti kubwa huku anapiga ngoma.)

CHIRIKU: Nakuita golegole mwenye ujuzi wa kale. Utuonyeshe kilele, kwa hekima na upole. Tuangaze macho mbele, tusipotee milele. Nawaita ndege wote, mkutanoni, njooni. Ndege wote nawaita, mje bila ya subira. Mjikusanye kivita, mzisahau hasira. Toka pwani za Mvita, hadi jangwa la Sahara. Nawaita ndege wote mkutanoni njooni. Nakuita yangeyange, kasuku nawe tumbusi. Kanga kutoka Mahenge, popo, tai na tausi. Mbayuwayu simtenge, njiwa walio weusi. Nawaita ndege wote, mkutanoni njooni.

(CHIRIKU anacheza na ngoma yake na kuimba bila maneno. Anaita kindege na ndege wengine wanampokea.)

TAUSI:

Enyi wa mashariki
Rukeni Ogeleeni
Ingieni safarani
Leteni hekima
Ujasiri
Msimamo mwema
Sitiri
Mtutoe fadhaani.

CHIRIKU:

Ko ko likoo! ooooh! oooh!
Magharibi sisahau
Kengewa wenye nguvu
Muishio kwa mabavu
Na werevu wa nahau

MWEWE:

Ndugu zetu wa kusini
Amkeni
Changamkeni
Muufukuze umasikini
Mpige teke
Karaha
Muicheke njaa na ngurumo za ughaibuni.

MTANI: La mgambo likapigwa kuwaita wa kaskazini; bara, pwani, na waliopotea angani. Saa hadi saa, siku hadi siku, mbiu ikapigwa. Iliwaamsha makinda chini ya uvungu wa mama zao na kuwabembeleza kulala tena. Ndege waliokuwa wakila waliisikia na kusahau kumeza. Vicheko vilikatizwa katikati na walioruka walidandia hewani kusikiliza. Waliolala waliota habari hizo; wagonjwa walimeza habari hizo na dawa zao; na waliokuwa mahututi walipata nguvu za mwisho kuzipokea na kuzipeleka habari ahera. Sauti zikapeperusha habari kutoka nchi hadi nchi. Miluzi ikaimba kutoka tundu hadi tundu na njiani ikajipenya katikati ya miamba na mapango, ikazunguka kasri za vichuguu, na kuvamia milima mikubwa na midogo.

(Ngoma na kelele zinafikia kilele halafu zinanyamaza kwa ghafta. Kimya.)

MTANI: Ndege wakaulizana! Pst, pst, pst! Pst, pst pst!

(Ndege wanaupokea mnong’ono na kuukuza na unapofikia kilele MTANI anawapa ishara, Kimya.)

MTANI: Tetere akamuuliza kipanga, kipanga alimuuliza tomboro ambaye naye alimgeukia kitwitwi. Mkutano gani huu, walijiuliza. Unatutaka nini huu?

NDEGE 1: Twakumbuka vizuri mkutano wa kwanza. Historia, hadithi na fasihi zasimulia. Mkutano ule wa kwanza wa ndege. Ndio; kulikuwa na mkutano wa kwanza. (Filimbi inalia pole pole.)

NDEGE 2: Kama hivi sasa, wakati ule ndege waliitwa kutoka pande zote za dunia. Wasio wana walibeba mawe. Wote walifika mkutanoni. Mkutano ule wa kwanza.

NDEGE 1: Ndege waliambiwa watafute kiini cha hekima.

NDEGE 2: Walihimizwa wafunge safari kuisaka roho ya uhai.

NDEGE 3: Waliamriwa washinde aliposhindwa Adam na Hawa.

NDEGE 1: Ndege walionywa;

NDEGE 2: “Njia ni ndefu….”

NDEGE 3: “Njia ni ngumu….”

NDEGE 1: “Ni njia hatari…”

NDEGE 2: Hata hivyo waliifunga safari. Kwa miaka mingi walisafiri kupitia milima na mabonde, nyika na misitu, bahari na majangwa.

NDEGE 1: Wachache walifika mwisho wa safari ile.

MTANI: Mkutano gani huu wa pili? Ndege walijiuliza.

NDEGE 3: Kati ya maelfu walioanza safari ile ya kwanza karibu wote walipotea. Wengi walipotelea baharini, wengine juu ya milima. Waliteswa na kiu na wengi waliungua mabawa na mioyo. Wengine waliliwa na chui na duma; kati yao wengi walikufa kwa uchovu na joto. Na wale waliosalia kati yao walipata wazimu wakauana wao kwa wao; wengine wakafadhaika na waliyoyaona, wakapata bumbuazi. Wakafa bila ya kujua walinuia kitu gani.

NDEGE 2: Waliobaki walimfuata golegole katika kumtafuta Ndege Mkuu Mjua Yote, Mweza Yote, na ubawa wake huko China. Walipofika walimwona. Lakini katika kumwona, wakajitambua wenyewe.

NDEGE 1: “Tafuteni shina la mti na hamtababaishwa na uhai wa matawi.”

NDEGE 2: Ndege walitambua. Njia ya ukweli na hekima ni njia ya ndani ya roho, ridege waligundua.

NDEGE 3: Vizazi na vizazi sasa vimepita.

NDEGE 1: Ni historia.

NDEGE 2: Ni hadithi.

NDEGE 3: Ni kumbukumbu kati ya Agano la Kale na Jipya.

MTANI: Pst! pst! pst! pst! pst! pst! Je ni mwito wa Majnun kumtafuta Laila wake? Ndege walisikiliza! Ndege walisita!

(Kimya. Kelele za sauli za ndege zinasikika zinapanda na kukaiika kwa ghafla. Kimya. Wanangoja. Kwa mbali ndege wanasikika wakianza safari. Mmoja, mmoja, na katika’ makundi wanaonekana waktiembea, kuruka, kukimbia, kuogelea, n.k. Vitendo hivi vitajiingiza katika makundi tofauti na ndege wote watamalizia kwa kucheza pamoja. Ngoma hiyo inaanza polepole na kuwa na mapigo ya haraka sana mwishowe ili kuonyesha ile hamu ya ndege kufika upesi kwenye mkutano. Ngoma inakwisha kwa mkato. Na mara hiyo mlio wa mgonjwa ttnasikika. Baada ya kusita kidogo, MAMA na SHANGAZI wanaingia ndani.)

MTANI (baada ya kimya kidogo): Simulizi zatuambia juu ya wenzetu wanaokufa si kwa ajili ya ugonjwa bali jamii inawaruhusu waende huko ahera. ‘Mkutano hufanywa. “Huyu na yule wakati umefika”! Au, “Na rnimi jamani nataka kwenda kwani kazi yangu imekwisha!” Watawala walioshindwa vitani nao walijua lini kutoweka. Wagonjwa hawakutaka kungoja mpaka nguvu ya mwisho. Ngoma zilipigwa. Nyimbo zikaimbwa. Katika mkesha wa matambiko mtu alisindikizwa ahera. Aya! aya! yaya! Mambo yamebadilika.

(MSHERI ameingia kimya kimya na anainsikiliza MTANI ambaye baada ya muda anageuka na kumwona. Wanatazamana.)

MSHERI: Ehh, habari!

MTANI: Nzuri.

MSHERI (kwa kusita): Wenyeji sijui wako wapi?

MTANI: Mwenyeji ni mimi.

MSHERI: Mbona sikufahamu?

(MSHERI anamwangalia MTANI.)

MTANI: Na mimi sikujui!

MSHERI: Jina langu Msheri, na wewe?

MTANI: Naitwa majina mengi lakini kwako ni Mtani.

MSHERI: Mtani wa nani?

MTANI: Mtani tuu! Msheri umesema? Ha!!

MSHERI: Unanijua?

MTANI: Kama kiganja cha mkono wangu kifunikacho na kuanika siri. Usishangae! Nimekwambia majina yangu ni mengi. Watu wengine hupalilia mazao, mimi napalilia siri za watu, wanyonge na wafalme. Jina langu Mtani (Wanaangaliana.)

MSHERI: Wenyewe wako wapi?

MTANI: Wenyewe wenye nini? (MSHERI anajifanya kana kuingia lakini MTANI anamzuia.) Mabavu eeh?

MSHERI: Niache nipite.

MTANI: Unakwenda wapi? Hujachoka kusafiri? Au unamtafuta mama unyonye! (Anacheka.)

MSHERI (kwa hasira): Hata kamajina lako Mtani, huna haki.

MTANI: Eeh! Kaja na hasira mwenzenu! Hasira kapu tele! Nini kingine umeleta? Chakula? Pesa? Au hasira tu? Umeleta hasira unafikiri ni mvua kwa ardhi yenye kiu? Au umesikia kuna ukame wa miti shamba kwa hiyo umeleta marobota na marobota? Aah, hapana. Najua, nyie vijana siku hizi mnapenda kusafiri kama unyoya – wepesiii!!!! Ukipulizwa huku na kule huna kipingamizi.

MSHERI: Umemaliza?

MTANI: Ndiyo kwanza tumeanza.

MSHERI: Wewe hasa ni nani?

MTANI: Aaah, ninajua kwa nini umerudi na magunia yako ya hasira. (Anacheka.) Husemwa ndege walao mizoga husikia harufu ya chakula chao kabla hata kiumbe hajakata roho. Mmeanza kukusanyika. Mmetua kwenye matawi ya karibuni ili muwe wa kwanza kudonoa. Mnamkodolea macho na kujifunika buibui za kilio ili aone haya kuchelewa kuondoka. Aaah, naujua mtindo wenu.

MSHERI: Nafikiri una kichaa.

MTANI: Umekuja kumwona Mtua?

MSHERI: Hayakuhusu.

(Mara wanasikia sauii za mgonjwa na harufu ya uvundo unawashambulia.)

MSHERI (baada ya muda kidogo): Kumbe ni kweli? Labda unaweza kuniambia.

MTANI: “Unakwenda wapi?” mtu alimwuliza Kobe. “Hayakuhusu,” alijibu Kobe kwa majivuno. Lakini alipofika njia panda haku – taka kupoteza wakati. “Eti,” alimwuliza mtu, “Njia ipi itanipeleka mtoni haraka?” “Hainihusu,” Kobe alijibiwa.

(MAMA anaioka. Kwanza hamwoni MSHERI lakini anapomwona wanaangaliana kwa muda bila maneno wakaii MTANIanazungumza.)

MTANI: “Shtkamoo mama.”

MAMA:

“Marahaba mwanangu.”
“Habari za safari mwanangu.”
“Si mbaya mama mradi nimerudi.”
“Mradi umerudi mwanangu.”
“Habari za hapa mama?”
“Si mbaya mwanangu. IIasa sasa umerudi.”
“Nataka kumwona Mtua mama.”
“Pumzika kwanza baba.”
“Nataka kumwona Mtua.”
“Nakupenda marnangu wee mzazi.”
“Nakupencla pia wangu wa utumbo wangu.”

MSHERI: Nataka kumwona sasa hivi!

MAMA: Unajifanya kama baba mwenye nyumba anayekuja kukusanya kodi.

MTANI: Hmmmm! Ni bwana harusi asiyetaka kucheleweshwa kuingia ndani.

MSHERI: Haya hayakuhusu wewe!

MAMA: Nenda kamwone baba yako.

(Baada ya kusita kidogo, MSHERI anaingia ndani.)

MTANI: Baba tai kamwona intoto wake akija kwa haraka. “Aaah baba afadhali umeniletea dawa nipone.” “Nimekuja kuchukua urithi wangn,” alijibu rntoto. “Nipe urithi wangu sasa hivi au sivyo nitakufanya ingonjwa zaidi ya hapo. Huu ni wakati wangu. Nataka urithi wangu, ili niishi zaidi ya ulivyoishi. Nipae kupita mbingu ulizopitia. Nataka siri ya utai mzee na usinichezee.” Sauti nyonge ilimjibu “Aaah, mwanangu, damu ya damu yangu, mbawa zangu zimevunjika, nisaidie kuniponyesha.” “Huo ni ujanja tu. Nipe. Nimefika hapa kwanza, kwa hiyo nipe nipate kufaidi kabla ya wengine kukusanyika. Uliniahidi kuwa mimi ni mtoto wako mpendwa, nitarithi kila kitu.”

(MSHERI na SHANGAZI wanatoka ndani wakifukuzana. MSHERI anaanguka na vitu kadhaa alivyovishikilia.SHANGAZI ameshika fimbo kvbwa lakini kabla hajawai kumpiga MSHERI, MTANI anamshika.)

SHANGAZI: Mwache nimuue! Mwanaharamu.

MTANI: Mwache. Hahitaji msaada.

MAMA: Mtoto wa nyoka ni nyoka

MTANI: Uwi, uwi!

(SHANGAZI na MSHERI wako mbalimbali.)

MAMA (anaonekana amechoka): Msheri na Maisa. Giza na mwanga. Hata walipokuwa watoto. Msheri ndiye aliyekuwa na haraka. Takwa lake amri. Chake ni chake na cha mwenziwe ni chake pia. Mtua alifurahi: “Mtoto wa nyoka!” Alimvalisha kama yeye. “Huyu ndiye mrithi wangu,” alisema Mtua. “Sio balaa hili la Maisa ulilozaa.” Maisa. Aliyekimbia mbali aepukane na mateke, matusi na karaha ya Mtua: “Mtoto mwanamke hana faida.” Maisa aliyevunjika mgongo kupika chakula cha Mtua. Aliyevunjika shingo kumtekea maji Mtua. Aliyelala na njaa ili Mtua acheze na chakula kilichobaki na kuwapa mbwa zake. Maisa!

MTANI: Maisa aliyefanywa kijakazi, akapata shukrani za punda na kufukuzwa. Mwishowe akakata shauri kuwa mchuuzi. Ni huyo tunamngojea. Amuokoe Mtua.

SHANGAZI: Ni wajibu wake, mtoto kwa mzazi.

MTANI: Asiporudi je?

SHANGAZI: Hawezi!

MAMA: Wewe Msheri umekuja inikono mitupu halafu unadai…

MSHERI: Kwa kwpli mimi sijali kama Mtua ataishi. Ninachotaka ni kupata chote kilicho changu.

MAMA: Umeupata.

MTANI: Nini? Urithi?

(MSHERI anajikunja kama vile ana maumivu. Woie wanamwangalia.)

MTANI: Vipi?

MSHERI (Kimya): Kichomi kidogo.

(MAMA baada ya muda ktdogo anaomboleza kwa sauti kama mtu aliycfumbua macho kwa stri iliyofichuka vibaya. Analia na kuzunguka polepole kama aliyebeba mzigo mzito).

MTANI: Vipi?

MAMA: Mnuse!

(MTANI anamnusa MSHERI.)

MSHERI: Toka hapa!

MTANI: Pole! Umeingia katika ufalme wa baba yako.

MAMA: Nilijua tu. Toka alipokuwa mdogo, yeye na baba yake. Humsikii sauti? Ya baba yake. Mwangalie alivyovaa. Nafikiri hii ni laana.

MSHERI (anacheka): Sijui ninyi mnazungumza nini. Lakini wewe mama najua tangu zamani hunipendi kwa kuwa baba alinipenda sana.

MAMA: Hapana. Nilijawa na wasiwasi uovu wa baba usimwangukie mwana.

MSHERI: Uliona wivu.

MAMA: Kuwaonea wivu?

MSHERI: Watu wadhaifu kila mara hawadharau wenye nguvu. Lakini unalalamika nini?

MAMA: Nilimwonya. Hizi ni mali za watu unazopora, hizo roho za watu unazochezea; siku moja zitakushtaki. Watakuloga. Na sasa Msheri…

MTANI: Mmrn! Miye simo. Sihusiki. Lakini msikate tamaa, Mganga kasema ugonjwa huu una dawa.

MSHERI: Mie sitaki maneno mengi. Nimerudi kuchukua haki yangu. Mtua aliniahidi zamani na kila mtu anajua mirni ni mrithi wake.

MTANI: Na Mtua sasa anakufa.

MSHERI: Nataka nichukue kilicho changu niondoke.

SHANGAZI: Una hakika Maisa atarudi?

MAMA: Atarudi.

MSHERI: Sasa najua ujanja wenu. Mnataka Maisa arudi halafu mninyang’anye urithi wangu. Sijali kama baba anakufa. Nataka aniambie urithi wangu. (Anajaribu kuingia ndani lakini SHANGAZI anamwahi. Wanatazamana kwa chuki. MAMA anacheka kama mwenye kichaa.)

MTANI: Tofaa halizai embe na mbweha katu hageuki farasi. Akina Mtua walikuja kama wezi usiku wa manane. Wakanyemelea. Walibomoa, waliua na kunyang’anya ovyo. Waliwaita wenyeji washenzi, lakini waliiba ardhi ya washenzi hao.

MSHERI: Mababu zangu walikuja hapa. Walikuta nini? Nyasi pori na washenzi wengi. Ni sisi akina Mtua wapasua Nyika, wapasua pori. Miti ilijikata yenyewe iliposikia kelele za panga zetu. Nyasi zikajikusanya mabiwi. Mawe na vichuguu vilikuwa mchanga chini ya jernbe letu. Tulipogusa inajabali yalihema na kutetemeka.

MAMA: Lakini Mtua huyu aliwapita wote. Alivaa ukatili kama joho la dhahabu. Alimfukuza mtu kutoka nyumbani kwake na mume kutoka kitandani mwake. Chakula hakilivvi bila ruhusa ya Mtua. Maji hayanywewi kabla ya Mtua kuyanusa. Ufunguo wa kisima kaufutika kwapani. Ncno la Mtua ni amri. “Fanya hivi! Fanya vile! Nencla kule, au umechoka kupumua?”

MSHERI: Mtua huyu ni zaidi ya Watua wote. Mtua wa Watua. Sauti yake mlio wa simba unaompa kinyonga mbio za swala. Ukimya wa Mtua ni kelele zinazoziba masikio. Kelele zake ni ukimya wa kifo. Na mimi mrithi wa Mtua huyo. Nitampita. Mtua wa Watua kupindukia.

MAMA: Watu hawakustahimili, “Tunaonewa!” “Tunanyanyaswa!” Walipiga kelele mpaka sauti zikawakauka. Chuki na basira zilipandwa, zikachipuka, zikachanua.

MTANI: Siku moja watu wakakumbuka laana ambayo nguvu yake ni umoja wa watu kwa adui yao. Walitia nguvu zao zote katika laana hiyo. Wakarudi makwao na knngoja.

MAMA: Mtua alicheka aliposikia watu wanataka kumwangamiza.

MTANI: Labda ni siku, labda ni miaka, lakini watu walingoja.

MSHERI: Walijisumbua bure. Sisi akina Mtua, tumetawala miaka mingi. Tumeota mizizi mirefu na imara, hatung’oleki. Hatusogezeki. Tumevaa hirizi zisizogusika. Nyimbo zimeimbwa, ngoma zimechezwa jiua la Mtua. (Anaimba katika mtindo wa wimbo wa taifa.)

Mtua Mtua, mfalme wetu
Pokea salamu na shukrani
Utawala toka karnc hadi karne
Ukumbukwe kizazi hadi kizazi
Mtua Mtua, Mola akulinde
Akujazie neema
Mali katika sheheua Mtua
Leo na Milele daima

(MAMA anauimba wimbo huo huo lakini kwa hasira na mwisho wote wawili wanaimba kama katika mashindano. Ktmya, ghafla wanatazamana kwa chuki.)

MTANI:

“Ilaaniwe siku yako ya kuzaliwa.”
“Ilaaniwe siku ulipochaguliwa kuwa mama yangu.”
“Sikukuomba uzaliwa kwangu.”
“Sikushauriwa nitungwe wapi.”

(MAMA na MSHERI wanaacha kutazamana.)

MTANI: Mtua alijua njia za dunia.

MSHERI: Alizoea vipenyo vyote vya utawala.

MTANI: Alijua kuuma na kupuliza.

MSHERI: Alielewa kuzusha na kuchipuza.

MTANI: Yule lakini alikuwa Mtua mwingine. Si huyu. Wakati huo Mtua huyu alikuwa bado kijana. “Niko upande wenu!” Mtua aliwaambia watu. “Nipeni mkuki tuwatokomeze hawa akina Mtua. Toka leo mimi si wa akina Mtua bali ni mwenzenu.

MAMA: Hmmmm. Watu wakampa mikuki na mishale. Akapigana na adui mstari wa mbele.

MTANI: Ushindi ulikuja. Alelelelele! “Watu wote ni sawa!” “Uhuru na kazi!” “Wanyonyaji wote ziiii!!” “Mali ni ya wote wanaotoka jasho!”

MAMA: Haikumchukua muda Mtua kukata shauri kuwa kibanda cha uhuru ambamo wote walikimbilia kutoka katika mvua za utumwa ni kidogo rnno kwa watu wote, kilimtosha yeye tuu!

MTANI: Watu wakajikuta katika hali mbaya zaidi kuliko awali.

“Mtua umetudanganya.”
“Nyoka wee, ndimi zako mbili.”
“Mwizi wee, unayenyatia mali za watu usiku wa manane.”
“Tulikuwa jahazini pamoja lakini umekata shauri kututumbukiza ufike ng’ambo peke yako.”
“Laana wee.”

(Wakati MTANI akiendelea, sauli za waiu zinasikika kila upande zikimlaani na kumtukana MTUA.)

“Shetani wee.”
“Kwa kntudanganya twakulaani.”
“Kwa kutuimbia, kutuvika kilemba cha ukoka twakulaani.”
“Kwa mateso yetu.”
“Njaa na uchi wa watoto wetu twakulaani.”
“Twaknlaani kwa kujifanya Mungu kuongoza nyota zetu.”
“Laana.”
“Laana.”
“Laana.”
“Usilale usingizi tena kwa madhambi uliyotenda.”
“Upate ukoma na magonjwa yote ambayo duniani bado hayajaonekana.”
“Uoze.”
“Unuke kuliko maiti ya samaki.”
“Laana.”
“Laana.”

(Watu wanaonekana wakizunguka sehemu yote ya kuchezea wakilaani kwa vitendo na kusema “Laana” mpaka inafikia kiwango cha juu sana. Sauti zinakatika ghafla. Kimya. Kutoka ndani MTUA anasikika akipiga kelele. Anafoka. Anatapalapa kama miu aliyepagawa. Amevaa majoho machafu machafu yenye “magonjwa.” Wanajaribu kumkamata. Kwa muda hakamatiki. Wanapomkamata anakuwa kama mbwa mwenye kichaa.)

SHANGAZI: Kamwite mganga.

MAMA: Hatuwezi mpaka Maisa aje.

SHANGAZI: Nasema, kamwite mganga.

MAMA (kama hakusikia): Nini?

(MSHERI na MTUA Wanaangaliana. Wamevaa karibu sawa isipokuwa nguo za mmoja ni mpya. MTUA anajaribu kumvamia MSHERI lakini anashikwa.)

SHANGAZI: Kamwite mganga.

MAMA: Haiwezekani. Maisa hajafika.

SHANGAZI: Tutauza vitu vilivyobaki.

MSHERI: Thubutu! Kutoka sasa hakuna kitu kuuzwa au kutoka humu.

MTANI: Maji yanachemka.

SHANGAZI: Kamwite mganga! (Kimya. MTANI anaanza kuondoka.)

MSHERI: We rudi! (MTANI anaondoka). Hata kama huyo mganga akija mtajisumbua bure. Hakuna kumlipa. (MWANAMKE anaingia. Wote wanajaribu kuonekana kama kawaida.)

MWANAMKE: Habari za hapa jamani.

SHANGAZI: Nzuri.

MWANAMKE: Nina shida na Mtua.

SHANGAZI: Sasa hivi anapumzika.

MWANAMKE: Haitachukua muda mrefu. Nilitaka kujua kama tunaweza kuanza kuchoma mabiwi. Mashamba tayari lakini mabiwi…

MSHERI: Wee kiziwi? Umeambiwa anapumzika!

MWANAMKE: Aah. Mbona yuko hivi? Ni mgonjwa?

MSHERI: Mgonjwa mwenyewe. Ondoka hapa.

MWANAMKE: Sasa lakini…

MSHERI: Ondoka, ondoka! Shenzi, Ondoka!

MWANAMKE: Haya basi nakwenda. Lakini… mzigo huu wa Mtua.

SHANGAZI: Kuna nini?

MWANAMKE: Aaah, Sijui, lakini ni cha kufungua mwenyewe.

(SHANGAZI: anauchukua mzigo. Anataka kuufungua, anasila halafu anauingiza ndani.)

MWANAMKE: Haya nakwenda.

(Anatoka. MSHERISHANGAZI: na MAMA wanajaribu kumwingiza MTUA ndani lakini anachomoka na kuhaha kwenye uwanja. Kutoka kila upande sauii za watu zinasikika zikimlaani na kumtukana MTUA. Yeye anaonekana kama anajaribu kuzikimbia hizo sauli lakini zinamzinga kila upande. Anapiga kelele. Anapigana na watu wasioonekana. Analia na kujikokota ndani. MGANGA anaingia akifuatana na MTANI. Anaingia ndani na baada ya muda manyanga na kuimba kunasikika. Baada ya kitambo MGANGA anatoka.)

SHANGAZI: Vipi? (MGANGA anamwangalia bila kujibu.) Asante kwa kuja. Utalipwa baadaye.

MGANGA: Siwezi kungoja. Dawa hii ni ya muda tu. Hamjatimiza masharti.

SHANGAZI: Tutauza vitu. Halafu Maisa anakuja. (MGANGA anamwangalia bila kusema neno.)

MAMA: Anataka kulipwasasa hivi (SHANGAZI anavua nguo zake. Baada ya muda anamvua MAMA nguo zake kwa nguvu. MSHERIanakataa. SHANGAZI anazifunga nguo zake na za MAMA pamoja na kumkabidhi MGANGA.)

SHANGAZI: Mpaka hapo baadaye!

MSHERI: Hizo nguo si zenu za kugawa ovyo ovyo. (Anajaribu kumnyang’anya MGANGA furushi. Kwa muda furushi linavuiwa huku na kule mwisho MGANGA analipala na kukimbia.)

MSHERI: Mwizi huyo! Mkamate mwizi huyo! (Anatoka akimkimbiza MGANGA.)

(SHANGAZI anachukua majani na kuanza kufukizia kila mahali. MAMA amekaa tu.)

SHANGAZI (akimwangalia MAMA): Umekaa tu hapo, huna kazi? (Kimya) Au unaiomba miungu yako imchukue Mtua upesi? Wewe na watoto wako mmetuletea balaa sisi akina Mtua.

MAMA: Mimi ni zumari. Kila anayejua na kujitia kujua amenipiga bila kuniuliza. Ninyi kina Mtua ni mumiani. Mnafyonza na kufyonza na kufyonza…

SHANGAZI: Wakati umepita wa kufikiria hayo. Sasa wewe ni mmoja wetu.

MAMA: Anayekula najambazi ni mwizi sivyo?

SHANGAZI: Kitu kama hicho.

MAMA: Hata kama chakula kimeshurutishwa kooni kwa mtu?

SHANGAZI: Acha hayo. Kazi yetu ni kuona kuwa Mtua anapona na kuendelea.

MAMA: Hajafika mwisho wa barabara?

SHANGAZI: Hata, njia panda tu. Unasikiliza mno maneno ya maadui zake. Usikae tu, kamwangalie mgonjwa labda anahitaji kitu. (Pole pole MAMA anainuka lakini baada ya kuchukua hatua chache anabadili nia na kukaa chini).

SHANGAZI: Nini?

(MAMA anabakia kimya. Wanawake wawili waliobeba mizigo wanaingia na kumwangalia).

SHANGAZI: Mnachokishangilia ni nini?

MWANAMKE 1: Aka, tulikuwa tunapita njia tu.

MWANAMKE 2: Tukaona ingekuwa vizuri kuja kumwamkia Mtua na kumwombea heri.

SHANGAZI: Hajambo.

MWANAMKE 1: Hajambo?

MWANAMKE 2: Hajambo eeh?

SHANGAZI: Mnataka nini?

MWANAMKE 2: Si tumeuliza tu? Hajambo?

MWANAMKE 1: Maana’ke haonekani siku hizi.

MWANAMKE 2: Panya wamewaingilia nini?

MWANAMKE 1: Maana’ke wakishakufa hao na usipowawahi kuwatupa wanaoza hao!!!

MWANAMKE 2: Umefanya vizuri kufukizia na hayo majani.

MWANAMKE 1: Tunasikia harufu kweli.

SHANGAZI: Hebu piteni, nina kazi nyingi.

MWANAMKE 1: Hiyo harufu isipotoweka, ninajua dawa nzuri…

MWANAMKE 2: Twende bwana, tusije tukaambiwa tumekula mpaka tukalamba sahani.

MTANI (ambaye mpaka wakaii huu wole alikuwa akiangalia tu): Hivyo mnangojea mpaka mfukuzwe na fimbo?

WANAWAKE: Tunakwenda, tunakwenda. Aah, mzigo wa Mtua huu.

(MSHERI anarudi anawaangalia wanawake, wanatoka)

MSHERI: Mbona watu hivi, utafikiri kuna harusi?

MTANI: Au matanga?

SHANGAZI: Aha! Ndiyo! Tutawaambia watu Mtua anajitayarisha kwa harusi. Anaoa mke mwingine.

MSHERI: Nini?

SHANGAZI: Sherehe! Watu wakiona kuna furaha hawazidi kuchunguza. Sasa hivi hapa nyumbani kumepooza.

MAMA (anacheka): Sherehe ya harusi eeh? Si mbaya.

SHANGAZI: Wanamwogopa Mtua lakini wakijua ni mgonjwa au anakufa…

MTANI: Utakuwa mwisho wenu wote.

SHANGAZI: Haya, nyimbo, ngoma. (Anainuka na kufundika matawi, vipande vya nguo, maua. Anaimba nyimbo na kucheza ngoma ya harusi. Wengine wanamwangalia. Anapomaliza, kimya).

MSHERI: Kwa kweli siamini kuwa katika karne hii ambako kuna matibabu chungu nzima, Mtua hawezi kutibiwa. Hospitali je?

SHANGAZI: Huu si ugonjwa wa hospitali.

MSHERI: Basi hamtaki apone.

MTANI: Kama wewe.

MSHERI: Angalau mimi si mnafiki.

MAMA: Nimechoka. Lete hadithi Mtani.

MSHERI: Msianze upuuzi hapa.

SHANGAZI: Hadithi zisizo na mwisho?

MAMA: Kwenye matanga watu hupiga hadithi.

MTANI: Au harusini.

MAMA: Mkutano wa pili wa ndege.

SHANGAZI: Hii imenichosha.

MAMA: Ndege wamefika.

MTANI: Wanangojewa kufika.

MAMA: Kama masika baada ya ukame.

MTANI: La mgambo limelia. Chiriku, Mwewe na Tausi wanangoja kama sisi hapa. (Ndege waliotajwa wanajitokeza).

CHIRIKU: Sasa wako wapi?

MWEWE: Watakuja.

CHIRIKU: Mmenisumbua bure. Watu…

MWEWE: Acha ukorofi Chiriku. Umeshafanya kazi yako sasa ngoja.

CHIRIKU: Nimepayuka weee mpaka sauti imenikauka. Kumbe kazi bure.

MWEWE: Hebu sikiliza kwanza…

CHIRIKU: Nisikilize nini? Ndiyo faida ya kukaa na watu wapumbavu.

MWEWE: Nani unamwita mpumbavu?

TAUSI: Basi jamani!

CHIRIKU: Tangu mwanzo sikupendelea mkutano huu.

MWEWE: Unaniita mimi mpumbavu?

CHIRIKU: Sasa?

MWEWE: Aaah.

CHIRIKU: Utanifanya nini?

MWEWE: Nitakufanya nini? (Anamvamia CHIRIKU, wanaangushana miereka na kudonoana. TAUSI anajaribu kuwaamua. Kwa fujo za mayowe na kelele za ngoma anawaingilia. CHIRIKU na MWEWE wanaachana lakini hado wamenuntana. Wanapeana migongo. TAUSI hajui la kufanya. Kimya.)

MTANI: Kazi kubwa ya uzazi si uchungu bali kungojea huo uchungu uanze. Mvumilivu hula mbivu lakini si wote tunaoweza kungojea utamu. Hakuna njia nyingine isipokuwa kungoja. Chambo kikitupwa mtoni si juu ya samaki kukata shauri atauma lini? (Anakaa. Kimya).

TAUSI: Mnajua, kuna kuku nunoja aliyekataa kuwa ndege? Alitaka kuogelea kama samaki. Basi siku moja… (Anaona hakuna anayesikiliza. Ananyamaza. Kimya kidogo. MWEWE anaimba kwa kupiga miluzi)

CHIRIKU: Shhhh!

(MTANI anapiga marimba polepole. TAUSI anatembea huku na kule. Anasimama kwa mbah. Muziki unasikika. Anasikiliza. Muziki wa MTANI unakatizwa. Woie wanasikiliza. CHIRIKUMWEWETAUSI wanajiandaa kuwapokea wageni. Ndege wanaingia, kila kundt na ngoma yake inayowakilisha sehemu wanazotoka. Kundi la kwanza kuingia ni ndege kutoka magharibi ya dunia: tai, njiwa na zawaridi. Wanacheza ngoma aina ya ktsasa ya huko magharibi, kati ya disco na jazz. Kundi la pili ni la ndege kutoka kaskazini ya dunia: korongo, kipanga na hua. Wanacheza ngoma aina ya “waltz.” Kundi la (atu ni la ndege kutoka mashariki ya dunia: kuku mwitu, kasuku, miombo. Wanacheza ngoma aina ya Kichina na Kihindi. Kundi la nne ni la ndege kutoka kusini mwa dunia: tumbusi, tetere na inbuni. Wanacheza ngoma ya mchanganyiko wa Afrika na Carrtbean. Ngoma hizi zote zinachezwa kwa muda wa dakika 3-5. Kikundi cha nne kinapomaliza kucheza ndege wanapiga makofi na kutawanyika).

MTANI: Inasemwa, kufika ni mwanzo wa safari. Ndege wamefika lakini mgonjwa wetu bado hana dawa. Pesa za kumwita mganga hazijapatikana. Maisa hajafika. Waliokwishafika wameleta matumbo matupu na macho yenye tamaa na uchoyo. (Kisha) Sikilizeni! (Wanasikiliza)

MAMA: Wanakusanyika nao kama hao ndege zako. Hivi ni vita vyao. Ugonjwa wa Mtua ndio uwanja wa mapigano. Sasa nao wanangoja.

MTANI: Wamevishika vicheko na vigelegele wakingojea ishara ya ushindi kuviangua.

MSHERI: Ushindi wao utakuwa wa muda. Mimi nitakuwa zaidi ya Mtua.

MAMA (anacheka): Mtoto haamini kuwa yeye ni mfuasi anayemfuata bwana wake jehanam.

MTANI: Macho yameangalia katikati ya jua. Amepofuka macho. Mwache afe na ujinga wake (Anaimba bila maneno).

(Watu wawili wanaingia wamebeba sanduku kubwa kama jeneza. SHANGAZI anawaona na kuama Kupiga vigelegele. Anajaribu kuwafanya waliopo wajiunge na sherehe hiyo. MTANI anajiunga. MSHERI analazimishwa. MAMA amekaa. SHANGAZI anawashirikisha “wageni” katika ngoma huku bado wamebeba sanduku. Ngoma hainogi, inalazimishwa. Kimya)

SHANGAZI: Sherehe ya harusi.

MTU 1: Oh!

MTU 2: Aah!

SHANGAZI: Mtua anaoa mke mwingine.

MTU 1: Oh!

MTU 2: Aaah…

MTU 1: Tulifikiri…

SHANGAZI: Anaoa mtoto huyoo, hajaonekana sehemu hizi.

MTANI: Mbichi.

SHANGAZI: Mwaliwajuzi.

MTANI: Si mweusi, si mweupe, maji ya kunde hajayafikia.

SHANGAZI: Meno, taa kali katika giza.

MTU 1: Oh!

MTANI: Urefu na ufupi washindana katika kimo chake.

MTU 2: Aaah! Eeeh!

SHANGAZI: Uzuri wake hauna kifani.

MTANI: Kicbeko chake hukunjua nyuso hadharani.

WATU: Mtua aliagiza sanduku hili.

SHANGAZI: Ndiyo, la harusi.

MTANI: Labda la kubebea mizoga. (MAMA anacheka)

SHANGAZI: La harusi hilo.

MSHERI: Harusi gani?

(Kimya)

MSHERI: Mnangoja uini sasa?

WATU: Hata! sisi…

(MWANAMKE anaingia amebeba kuni)

MWANAMKE: Nimesikia…

MTANI: Kuna harusi. Umeleta kuni bwana harusi aote moto?

MSHERI: Nimechoka na hizo soga zenu. Ondokeni hapa.

SHANGAZI: Msheri, unafanya nini?

MSHERI: Mnangojea nini?

MWANAMKE: Hiyo harusi je?

MSHERI (kwa hasira): Bwana harusi anapambwa sasa. Mikono ameinyoosha kumkumbatia mgeni wake.

MTANI: Mwenye masikio na asikie. MSHERI: Atakapofika Bi harusi mtaalikwa. Sasa ondokeni.

SHANGAZI: Siyo kama tunawanyima sherehe lakini tuna mambo mengi ya kutayarisha. (Anawasindikiza wageni nje halafv anarudi).

SHANGAZI: We Msheri utatuaogamiza. (MSHERI hamsikilizi bali anajishughulisha na kufungua sanduku.)

SHANGAZI: Hee! Acha hilo.

MTANI: Zawadi za harusi mwiko kufungua kabla.

(SHANGAZI na MSHERI wanagumbea sanduku mpaka linavunjika. Ndani yake kuna marapurapu, takalaka na kitambaa kimoja cheupe: Kimya. MAMA anacheka. MTANI anaimba bila maneno halafu…)

MTANI:

Mwanangati eeh
Mwanangati kafumaniwa
Leo mikono yote kakatiwa
Mwanangati asiyesikia mkuu
Mwanangati eeh.

MAMA: Mtani!

MTANI: Naam!

MAMA: Ndege…

MTANI: Naam twaib.

MAMA: Wamekusanyika.

MTANI: Ehe, ndege wamekusanyika lakini watu husema hadharani har pakosi vituko. Mtego wa panya huingia waliomo na wasiokuwamo. Kama vile palipo na mgonjwa hapaishi dawa. Wenye njaa wana matumaini na wageni wana matumaini tofauti. Wameleta macho, matumbo na fikra kemkem za siri. (Sauti za ndege zinasikika kila mahali. Shughuli za mkutano zi tayari kuanza).

BINADAMU (kutoka nje): Hodi! Hodi! (Anaingia. Ndege wanamkodolea macho). (Mara FISI anaingia huku anachekachcka. NDEGEFISI na BINADAMU wanaangaliana. Mara sauli ya SIMBA inasikika. Wote wanatawanyika haraka sana. SlMBA anaingia huku bado ananguruma.)

TAUSI: Eeh… aaah… Bwana Simba, huu ni mkutano wa ndege.

SIMBA: Sasa?

TAUSI: Wanyama wengine hawakualikwa.

SIMBA: Nini? Hujui mimi ni Simba, mfalme wa mwitu? (Ananguruma na kutamba uwanja mzima).

CHIRIKU: Umeambiwa kwa upole kuwa hutakiwi, au unataka…

SIMBA (anacheka na kutamba):

Mimi ni mfalme, sihitaji mwaliko.
Mimi ni Simba
Mfalme wa mwitu, mfalme wa viumbe
Nilitawazwa ndani ya tumbo la mama yangu.
Nilipolia ng’aa jua likafifia na mwezi haukuonekana
Mpaka nilipopiga ukope wa jicho langu.
Simba wa ukoo wa simba
Nguvu zetu zajulikana tangu milele
Zikasifiwa, zikaimbwa vizazi hadi vizazi.
Sisi Simba, twanyanyua miamba twasogeza milima.
Gololi zetu ni majabali. Pumzi yetu ni tufani,
Tunapotema meli huzama ovyo kwa dhoruba ya mawimbi,
Ukimya wetu ni kelele kali. Sauti yetu haisikiki
Yatoboa masikio na kusimamisha upepo usifanye kazi.
Wengi wanatupenda
Wengi wanatuogopa
Hatumpendi wala kumwogopa yeyote
Rafiki na adui ni kitoweo tukichagua
Njaa yetu kubwa ya upana na marefu ya maili moja.
Kulungu kumi ni kifungua kinywa.
Tule, tusbibe
Tulikula paa, pofu na nyati mia
Tukamalizia na ngamia watano kila mmoja wetu.
Ni mimi Simba…

CHIRIKU (anapiga kelele za kumkatiza): Tumekaa tu tunamsikiliza huyu jamaa aliyetuingilia mambo yetu! (Anamgeza) Ni mimi Simba… ni mimi Simba… tutamsikiliza mpaka lini?

(Ndege wanaitikia)

TAUSI: Simba, sisi ndege hatutaki shari. Tafadhali nenda zako kabla…

SIMBA: Siondoki!

(Ndege wanalalamika)

MWEWE: Simba, wewe una heshima zako. Kwa nini unafanya mambo ya kitoto?

SIMBA; Kwanza ninyi ndege, nani amewapa ruksa ya kuita mkutano, mkutano ambao hata mimi mfalme wa viumbe vyote sina habari nao?

TAUSI: Sikiliza Simba, hii si mara ya kwanza. Unakumbuka nyani walivyokutana mwakajana? Na sisimizi?

SIMBA: Waliniomba ruksa.

CHIRIKU: Wewe siyo mfalme wetu sisi ndege.

TAUSI: Sasa Chiriku hilo ni swalajingine, lakini hivi sasa tunao mkutano wa ndege.

CHIRIKU: Tunataka kuzungumza yanayowahusu ndege tu.

SIMBA (anacheka): Najua ujanja wenu. Mnataka kupindua uongozi wangu.

TAUSI: Bwana simba…

SIMBA: Nazyua hila zenu. Siondoki.

(Ndege wanazungumza kati yao).

CHIRIKU: Asiyesikia la mkuu…

(Kimya kidogo, Ndege wanaanza kuruka hapa na pale. Kwanza SIMBA halingishiki lakini baada ya muda anakuwa na wasiwasi kwa sababu hajui nia yao, Ndege wanamshambulia SIMBA. Wanamdonoa kwa midomo yao na kumpiga na fimho za miti. SIMBA anashambuliwa kila upande. SIMBA anafukuzwa, Ndege wanafurahi. Mambo yanapotulia kidogo wanamwona BINADAMU bado yuko juu ya mii. Wanamwangalia. Kwa hofu BINADAMU anakimbia. FISI alikwisha toka zamani, Haya yole yafanywe kwa “choreography” na yawe kwa muda wa dakika tatu hivi. Ndege wanakaa. Mabango yanasawazishwa. Moja kubwa linasema “Mkutano wa Pili wa Ndege”. Mengine, “Umoja ni Nguvu,” “Ndege Juu, Juu, Juu Zaidi!” Mabango yanaonyesha pia kama wawakilishi wanaioka wapi).

TAUSI: Sisi ndege wenyeji tuna furaha sana kuwakaribisha wageni wetu mliotoka sehemu mbalimbali za dunia. (Hapa ngoma inaanza kupigwa na ndege wenyeji wanacheza ngoma ya kuwakarihisha wageni wao. Wakali ngoma hiyo bado inaendelea. MTANI anajitokeza.)

MTANI: Ndege wenyeji waliwasalimu wageni wao. Waliigusa ardhi kwa shukrani na kuangalia hewani wakiomba dua warudi kama walivyokuja – salama. Waliwaonyesha viganja vyao vya amani na kutumaini wageni hawakufutika silaha mikononi mwao. Waliushangilia umoja wa ndege na kuwatolea heshima kwa kupiga goti. Tausi, Chiriku, Mwewe walitumaini mkutano utafanikiwa. Palipo nia, njia i wazi. (Ngoma inaendelea kuchezwa kwa muda mfupi inapokwisha ndege wageni wanaipiga makofi).

MSHERI: Hivyo nyie badala ya kufikiria mambo muhimu mmekazana tu na hadithi zenu za ndege?

MTANI: Umealikwa?

MSHERI: Njaa inauma, baridi inatuua lakini ninyi…

(MAMA anaanza kucheka mpaka anakuwa kama amepagawa; anainuka na kuhaha ovyo kwenye jukwaa. SHANGAZI naMTANI wanajaribu kumtuliza na inabidi wamkamale kwa nguvu. Kimya.)

MAMA: Mnajua… Mtua alinioa kwa hila na kwa nguvu. Na sasa laana yake imepita kwa watoto wangu. Nalaani siku niliyowazaa.

SHANGAZI: Acha wee! Mwiko! Jilaani mwenyewe.

MTANI: Baada ya kuamkiana ndege walianza mkutano wao. Wali…

MAMA: Mtua alifika mjini kwa baba yangu kama dhoruba ya kiangazi.

MTANI: Haitegemewi. Haitakiwi.

MAMA: Alituvamia kama makundi ya nzige.

MSHERI: Bila shaka aliwatetemesha. “Mimi Mtua.”

MAMA: Alisema, huku akila chakula chetu.

MSHERI: “Mimi Mtua.”

MAMA: Aliimba, huku akiiba mali yetu.

MSHERI (amekuwa MTUA sasa): “Lete hiki, hicho sitaki”.

MAMA: “Nataka kuwaona wasichana wenu wote! Hamkusikia? Nawapeni saa moja.

MSHERI: Maneno yake matamu yaliwanogea.

MAMA: “Aaah baba, wanawake wote wameolewa. Wasichana wana wachumba.”

MSHERI (anaigiza): “Wewe, njoo hapa. (Anamwita MAMA kwa nguvu. Anamchunguza meno, nywele, macho, anampapasa kutoka chini mpaka juu). Nione mikono yako ina nguvu kiasi gani. Nikande miguu. (Anakaa na kunyoosha miguu) We! Unafikiri nina siku nzima kukungojea! (Anampigisha inagoti mbele yake. Pole pole MAMA anamkanda) Aaah! Hmmm! Barabara! Ongeza nguvu kidogo! Aaah! Sasa sawa. Utanifaa. Utanifuata niendako. Utanikanada, utanitumikia. Aah! Barabara! Hebu nisikie sauti yako. (Kimya) Imba nasema! (Polepole MAMA anaanza wimbo wa kuomboleza) Wimbo gani? Hee! Imba wimbo wa kuinua moyo, wa kunifurahisha. Na wewe uonyeshe furaha. Hakuna kilio hapa.”

(MAMA kwafuraha ya kulazimisha. Anapoona “MTUA” anasinzia anaendelea na wimbo wa mwanzo. Baada ya muda muziki wa guitar unaingia na kumfuata katika hadithi. Mara anasimulia, mara anaimba.)

MAMA: Hapo zamani za kale, zamani za sasa hivi, ndege wote waliishi mahali pamoja kwa raha mustarehe. Waliruka walikotaka, walikula walichopenda, walifauya kazi kwa wakati wake. Miaka ikapita, na miaka ikapita. Siku moja: He! he! he! kelele. Nini? Yule! Wapi? Pale! Ndege ambaye hajaonekana katika dunia ya ndege alijitokeza. Ndege wakashnama. Wakatazamana na kuulizana. Huyu Ndege gani? Ndege gani huyu, asiyeweza kuruka, bali atambaa angani kwa uwezo wa silika? Umbo gani hili? Hatujauona huu mwili! Kichwa cha ndege kamili lakini, sesota, kajaa kiwiliwili?

Ndege, ndege gani huyu anayewika, anayepayuka kama jogoo wa masika? Atoka mto gani, bahari au nyika ya wapi isiyofahamika?

“Naitwa Lyanamandyenga”
Alijibu yule ndege
Niliumbwa na nyie hapo kale
Ninaruka
Ninatambaa
Ninajitandaza nitakavyo
Hakuna wa kuniletea fujo
Sina baba
Sina mama
Wala ndugu wa ovyo
“Lyanamandyenga ndiye mimi.”

Aliwika ndege yule. Aliwaambiajinsi alivyosafiri usiku na mchana kwa miaka na miaka ili kuwafikia. Amechoka. Ametota. Anaomba kupumzika.

Ndege wakampokea kwa mikono miwili wakamtengenezea kitundu na manyasi ya kuegemea. Wakamlisha, wakamvalisha, wakamtunukisha raha na utajiri. Miaka ikapita, miaka ikapita. He! kumetokea nini’? Imewapata laana gani? Walijaribu kukumbuka kama katika ule mkutano wa kwanza walionywa juu ya janga hili. Hapana. La sivyo wangekuwa tayari.

Maskini ndege, maskini. Janga gani limewafikia? Walimkaribisha mgeni. Kumbe ni mumiani. Lahaula, masikini ndege. Walikosa nini kupagazwa na hili jini?

Likawanyonya damu. Chakula likawapokonya, Nao kwa woga wakajikunyata (Msheri anaota na kujipurukusha. Mama anaimba.)

Miaka ikapita.
“Tumeonewa kiasi cha kutosha”
Wakaimba ndege mahali pote.
“Tumenyonywa kiasi cha kutosha”
Ndege wakajitia vitani.
Walikusudia bila utani
Lyanamandyenga kulitokomeza angani.
Wakalicharaza, wakalifukuza.
Lyanamandyenga likasikika “Huu si mwisho!”
Nitarudi, akacheka kwa sauti ya kutisha na ya chuki.
“Nitarudi! Nitarudi!: Akapotea angaui.

MSHERI (anaamka); Nani atarudi! Sikukuambia unikande na uniimbie wewe? Kwa nini umesimama? (MAMA anarudia kuimba kama mwanzo) Argh! Ondoka hapa!

MAMA: Haya, mimi na Mtua. “Njoo hapa, rudi pale! Nitekenye hapo!”

MTANI: Nilishe, nivishe.

MSHERI: Taabu ya wanyonge kila siku kulalamika.

MTANI: Ulimwiga Mtua kama vile ulikuwapo Msheri.

MSHERI: Mimi ni kina Mtua.

MTANI: Aah ndiyo, nilisahau (SHANGAZI anatoka chumbani kwa MTUA) Vipi?

SHANGAZI: Hali mbaya.

MSHERI: Muda gani? (Kimya. MSHERI anacheka.)

MTU: Hodi!

SHANGAZI: Maisa?

MAMA: Sio Maisa!

MTU: Nimeleta… mzigo

MSHERI: Nipe! (Anakichukua kifurushi kwa nguvu, MTU anaondoka. Anaanza kukifungua kifurushi. Ndani mna nguo nyeupe). Afadhali. (Anachukua moja na kujifunika).

SHANGAZI: Lete hizo nguo. (Anachukua zilizosalia na kuingia nazo ndani).

MSHERI: Upuuzi huu ukiisha ndiyo maisha yataanza.

MAMA: Mtani, ule mkutano wa ndege uliishaje?

MTANI: Mnanikatizakatiza hata nimesahau.

MSHERI: Sitaki kusikia upuuzi huo. (Anaondoka)

MAMA: Ndege walianza mkutano wa pili.

MTANI: Naam. Baada ya fujo za kindege kuendelea kwa muda, gongo likapigwa kuwanyamazisha ndege.

TAUSI: (anagonga gongo asikilizwe): Tusikilizane jamani.

MAGHARIBI: Hatutaki kukaa mkono wa kushoto.

TAUSI: Magharibi….

MASHARIKI: Na sisi hatutaki kuondoka hapa.

KUSINI: Mzozo huu haueleweki.

MAGHARIBI: Kwa nini Mashariki wameruhusiwa kukaa pale?

TAUSI: Hakuna mtu aliyewaruhusu.

KASKAZINI: Tutatue swala hili bila kelele zote hizi!

MAGHARIBI: Nakwambia sisi tunataka tukae upande wa kulia katikati.

MASHARIKI: Nyie ni akina nani mjichagulie nafasi yenu wenyewe? Wenyeji walitupanga, basi.

MAGHARIBI: Kama hatuwekwi katikati kulia, tutafunga virago vyetu tu…

TAUSI (anajaribu kuwanyamazisha): Tusikilizane jamani!

MASHARIKI: Tupe sababu muhimu kwa nini upewe sehemu hiyo.

MAGHARIBI: Tuna sababu zetu.

MASHARIKI: Toa!

TAUSI: Kimya, tafadhali!

KASKAZINI: Tusikilizane kama waungwana.

MASHARIKI: Watu wengine hata hawajui neno hilo.

MAGHARIBI: Una maana sisi!

TAUSI: Tafadhali wajumbe….

MASHARIKI: Sina maana yoyote.

MAGHARIBI: Unatutukana siyo?

KASKAZINI (anaingilia kati): Mambo haya hayafai. (MAGHARIBI na MASHARIKI ambao walikuwa karibu kupeana vibao vya mbawa wanasonya na kutengana.)

KUSINI: Labda tungetumia bahati nasibu kupanga watu.

KASKAZINI: Shauri zuri.

MAGHARIBI: Sikubali.

TAUSI: Wanaopendelea shauri hili waseme ndiyo.

NDEGE WENGI: Ndiyo!

TAUSI: Wasiopendelea.

MAGHARIBI: Siyo!

TAUSI: Haya. Mawe haya matano kila moja lina umbo na uzani tofauti. Tutachukuliajiwe dogo sana kuwa ndiyo namba moja. (Wawakilishi wa kila sehemu wanachukua jiwe lao.)

TAUSI: Sasa tuone. Mashariki amepata katikati kulia, Kusini pembeni kushoto, Kaskazini katikati kulia na Mashariki pembeni kulia.

MAGHARIBI (hajaridhika): Mimi naona…. aha! ah! ah! ah! sitakikukaa karibu na…. (Anamwonyesha MASHARIKI.)

KUSINI: Jamani, tukiendelea hivi hatufiki popote.

TAUSI: Tuendelee! (MAGHARIBI anakaa kwa shingo upande.)

MAGHARIBI: Mambo haya yanaenda kinyume cha utaratibu. Lazima kwanza tumchague mwenyekiti.

TAUSI: Sawa. Ndiyo nilikuwa naelekea huko. Uchaguzi wa Mwenyekiti.

KUSINI: Mimi nampendekeza Tausi.

MASHARIKI: Ndiyo.

MAGHARIBI: Sikubali (Mzozo unazuka TAUSI anaingilia kati.)

TAUSI: Tusikilizane jamani. Mmoja, mmoja. Sasa, kuna mapendekezo mengine kabla hatujapiga kura?

MAGHARIBI: Nampendekeza Kaskazini.

TAUSI: Haya sasa tupige kura.

MAGHARIBI: Mimi nafikiri kwanza wajumbe waeleweshwe kufaa au kutofaa kwa ndege waliopendekezwa.

(Mzozo unazuka tena.)

KUSINI: Mambo haya yatatuchelewesha jamani!

CHIRIKU: Nilijua tu!

TAUSI: Haya, labda tungesikia kwa ufupi tu maelezojuu ya waliopendekezwa.

MAGHARIBI (kwa pupa):

Sisi tungetaka Kaskazini awe mwenyekiti. (Anaimba)
Ndege wa Kaskazini
Ni viongozi bora
Nahodha wenye ujuzi
Wasiopepesuka na mawimbi na dhoruba
Wasioangalia kulia au kushoto
Katika kufikia lengo lao.
Wao ni wafalme
Walioamka asubuhi na kuona
Wengine wote wamelala
Wakachukua
Wakanunua
Wakaimeza nchi mpaka wakatawala
Kutoka machweo moja hadi nyingine
Wao ni Wanawali werevu
Waliowasha taa zao kwa hekima
Njaa alipopiga “hodi”
Alichimbiwa kaburi kabla hajafika kizingitini
Wapenda amani
Wajua tarehe za kupatwa jua na kujikinga vipasavyo
Kaskazini ni chaguo letu.
Huyu Tausi!
Tausi ni nani?
Mtoto wa jana mwenye meno ya kibogoyo
Atawezaje kuutafuna mfupa wa wadhifa.
Uzuri si hekima
Ulimi haujalegezwa na maneno ya busara.
Wala akili kukomazwa na ulaghai

ubahili
ubepari
ukatili wa siasa na maendeleo

Tausi?
Tausi ni nani?

CHIRIKU (kwa hasira): Mmekuja hapa kututukana….

KASKAZINI: Ngoja kwa…

CHIRIKU: Ngoja nini?

MAGHARIBI: Tausi nani?

KASKAZINI: Magharibi!

KUSINI: Tutaondoka sisi, tutaacha mkutano! (Wanaanza kuondoka lakini wengine wanajaribu kuwapoza na kuwarudisha.)

TAUSI: (anagonga kibao): Tusikilizane jamani? (Zogo halafu kimya).

CHIRIKU: Ndege mwenyekiti…

MAGHARIBI: Hakuna mwenyekiti… (CHIRIKU anamtupia jicho la hasira.)

CHIRIKU: Tausi, ni maoni yangu kuwa ndege wengine wemekuja hapa kuleta fujo. Hawataki…

MAGHARIBI: Nani analeta fujo! Tunachotaka ni utaratibu ufuatwe.

CHIRIKU: Utaratibu mnaotaka ninyi!

TAUSI: Basi ndege! Chiriku labda ungengoja kidogo tumalize swala hili.

CHIRIKU: Tunapoteza wakati kwa vitu visivyo muhimu. Lini tutaanza kuzungumza…

MAGHARIBI: Utawezaje kuanza kujadili mambo bila mwenyekiti!

TAUSI: Basi ndege wenzangu. Tumchague huyo mwenyekiti.

MAGHARIBI: Wanaomtaka kaskazini, ubawa juu! (Magharibi anaonyesha.)

KUSINI: Tausi? (Kusini na Mashariki wanaonyesha mbawa.)

KASKAZINI: Tumekata shauri tusipige kura.

CHIRIKU: Tausi basi ndiye mwenyekiti.

MAGHARIBI: Hatukubali!

KUSINI: Hamkubali vipi?

MASHARIKI: Tausi amepata kura mbili.

NDEGE: Tausi! Tausi! Tausi! (Magharibi anataka kulalamika lakini sauii za wengine zinazamisha maneno yake.)

TAUSI: Asante sana ndege wenzangu kwa heshima hii. Nitajaribu kuubeba wadhifa huu bila upeudeleo. (Anapigiwa makofi). Sasa basi, tuendelee na shughuli zilizotuleta hapa.

(Taa zinafifia na katika giza, giia linasikika likipiga wimbo kama wa maombolezo. Baada ya muda unabadilika na kuwa wimbo mchangamfu na mwanga unapokuja tunawaona ndege wanaruka huko na huko kwa furaha. Chakula tele, lakini hali hii inabadilika. Kwa kadiri chakula kinavyokuwa haba nyuvu zao zinapunguwa. Ndege wanaonekana wagonjwa na wadhaifu. Wanagombana. Wanaporana chakula. Wanaibiana. Wanapigana. Wanakufa. Wanaobaki wamevunjika moyo. Muziki wa gita unafuaia matendo ya ndege. Ndege wanapomaliza, muziki unaendelea. Taa zinafifia. Kimya kidogo. Kaskazini anasafisha koo.)

MAGHARIBI: O.K. tumeelewa. Mna tatizo sasa mnataka mkutano huu ufanye nini? (Mwewe ansimama.)

TAUSI: Mwewe!

MWEWE: Asante ndege mwenyekiti! Tumeita mkutano huu ili tufikirie njia ya kutuokoa kutoka janga hili la njaa kwa hivi sasa na kwa wakati ujao. Vichwa vyetu pamoja vinaweza kutupa mwelekeo unaofaa.

KUSINI:

Shida hii hata sisi twaijua
Mwaka huu neema
Mwaka huu njaa
Hapa jua kali
Pale mvua nyingi
Matokeo ni sawa
Hali isiyopangika
Kwa uhaba na neema za nafaka.
Adui pia ni kakaka
Watulia hata mapumba na maua ya migomba.

KASKAZINI: Tumeshasikia hayo. Sasajawabu ni nini?

KUSINI: Misaada mingi na yenye ziada.

MASHARIKI:

Ndege mwenyekiti, naomba ukumbi.
Jawabu si kushibisha matumbo kufukuza njaa.
Njaa ina sababu zake.
Si invua najua tu.
Kuna adui wanaosababisha njaa.
Swali ni hili:
Adui hao ni nani?
Tutapambana nao vipi?

MAGHARIBI: Huko ni kupoteza lengo. Mimi ninaona kuna adui mmoja tu!….

MTANI: (MAGHARIBI anaimba bila maneno wakati MTANI anazungumza.)

Ni maoni yangu, alisema Magharibi, adui wa ndege ni ndege wenyewe.

Wanazaana tele tele bila fikra, bila mpango na subira Wao ndio waletao kihere. Msaada! wangapi utawasaidia Wangapi utawaachilia

Katika idadi hii mia mia, aliuliza Magharibi.
Kamwe hatutatoa msaada, aliwakatalia.
Kamwe hatutatoa msaada alisisitzia.
Misaada huwafanya watu kuwa wavivu.
Huwatawanya nguvu na ubovu kugawanya.
IIulemaza mikono na miguu.

Magharibi aliendelea kumwambia kuwa kutegemea misaada ni kujizoeza kula bila kutoka jasho. Ndege wengine hufanya kazi kwa bidii, hukusanya, huweka akiba mwaka hadi mwaka. Ndiyo, hata huko kwenye anga za magharibi kuna matatizo ya chakula. Ndege hawana nafasi kubwa ya kuchagua—nafaka tano badala ya kumi, matunda kumi badala ya ishirini, wadudu aina hii na ile badala ya chungu nzima isiyo na idadi. Aliongeza, Magharibi haiwezi kutoa misaada. Alisisitiza, Magharibi ina matatizo yake. Jawabu ni kutozaa sana. Jawabu ni kutozaa kabisa. “IIaiwezekani!” Walilia ndege wa Kusini. “Haiwezekani!” Walilia Tausi, Chiriku na Mwewe! “Ni kinyume cha maumbile! Haiwezekani!” walisema wote kwa pamoja. “Ngoja niwaambieni habari za kiumbe Binadamu,” aliendelea Magharibi. “Binadamu, alikabiliwa na njaa, alikabiliwa na msongamano.”

MAGHARIBI:

Siku moja Binadamu kaamka
Hofu ikamshika
Kakumbuka njozi ya usiku ule
Iliyomtia kiwewe
Kaona njozini
Mamilioni na milioni ya wakubwa na wadogo
Waliojibana kama mchanga baharini.
Watu wamebebana
Wengi wamepangana kama muhogo tengani!
Nguo hawana
Njaa imewabana
Huku na kule maji hamna
Hewa nayo ya kupimiana
Jawabu ni nini? Kawaza binadamu
Dua au knua wasio timamu
Saa ni saa
Siku si siku katokea mganga wa miti shamba
“Kutozaa,” akaimba, ndiyo jawabu la kufaa.
“Ndiyo!” wakasema wenye siasa
“Ndiyo!” wakaitikia kwa hamasa
Walio na watoto na walio tasa.
Mtoto mmoja kwa mtu
Zaidi ya hapo asitliubutu adhabu si faini ya hela
Bali jela iliyotengwa kwa misitu
Binadamu wamestarehe
Wangojea baadaye kwa sherehe bila hofu
Bila woga kwa utulivu

KUSINI: Haya yamewezekana kwa binadamu, lakini sisi ni ndege!

KASKAZINI: Labda tuwaache hao wenye matatizo wahame, anga yetu ni kubwa na ingawaje ni tofauti, huko tutawafundisha tena kuishi na kufa. Tutawafundisha kujikinga na baridi na kupekua juu ya theluji. Mlango u wazi. Leo, kesho, sasa hivi tutawakaribisha na kuwageuza wawe kama sisi. Mtakula, mtavimbiwa. Tutawaimbia nyimbo msizozijua na muda mfupi mtaziimba nanyi kuwabembeleza watoto wenu kulala. Tutawapaka rangi mpya kwenye mbawa zenu. Tutawafundisha miondoko mipya ya kuruka. Mtasahau njaa. Mtasahau mlikotoka. Mbele yenu ni ngoma mpya tutakazowapigieni na kuwafundisheni na mtanenepa, mtanawiri.

TAUSI: Samahani, ndege kutoka Kaskazini, sidhani kama tunataka kuhama. Tumezoea huku ndiyo nyumbani.

KASKAZINI: Mkikaa hapa mtakufa!

MASHARIKI: Adui lazima ashambuliwe aangamizwe. Na adui mkubwa ni fikra isiyo sawasawa. Mimi…

MAGHARIBI: Jawabu ni kutozaa!

MWEWE: Mnataka tutoweke kabisa duniani?

KUSINI: Sasa hivi misaada ndiyo jawabu!

(Zogo linazuka, na linakaiishwa na CHIRIKU anayepiga kelele. Wote wananyamaza na kumwangalia. CHIRIKU anatoka jasho. Amekasirika. Kimya kidogo.)

CHIRIKU: Sijui kama waheshimiwa mnaelewa kuwa kuna ndege wanakufa? Sasa hivi nyinyi mnapoichafua hewa na maneno yenu ndege mamia kwa mamia wanakufa njaa. Kama hamtaki kutusaidia, basi rudini kwenu!

TAUSI: Chiriku tafadhali! (Zogo jingine linazuka. TAUSI anajaribu kuwanyamazisha kimya.) Nafikiri ni wakati wa kupumzika kidogo. Baada ya hapo tutaeudelea.

(Ndege wanaiawanyika kwa kelele na kujikusanya katika vikundi vikundi. Wengine wanaruka kutoka kikundi kimoja hadi kingine. Mazungumzo makali ya kichinichini yanaendelea. Mazungumzo yanafanywa kwa vitendo iu navyo vinaigwa kwa ukubwa bila kiasi. Wakati hua wote “Flute” inaom’ boleza. Baada ya muda, ndege wanatawanyika tena. Wanajiweka katika makundi yao kuanza kula vyakula walivyoleia. MAGHARIBI wana chakula kingi sana na wanakula kwa fvjo na ulafi. KASKAZINI wamejiienga pembeni kabisa, wakiwapa ndege wenzao mgongo. MASHARIKI wanakula taratibu. Wanapomaliza punje moja moja iliyobakia wanawapa akina TAUSIMWEWE na CHIRIKU ambao wamekaa wakiwaangalia walaji. Wao hawana kitu. KUSINI wana punje kidogo tu ambazo wanazila zote. Wote wanapomaliza wanajinyoosha kujipumzisha. Kimya. TAUSI anainuka, CHIRIKU anamvuta chini, wanasemezana bila wengine kusikia. TAUSI anasafisha koo.)

TAUSI: Ndege wawakilishi…

MAGHARIBI: Ndege mwenyekiti, hakuna haja ya kupoteza wakati. Sisi tuna mapendekezo ambayo yanaungwa mkono na ndege wa kaskazini.

TAUSI: Haya tuyasikie.

MAGHARIBI: Tunakubali kuwa mna tatizo na mnahitaji msaada. Sasa sisi tumekubali kuwaleteeni msaaada wa chakula kwa muda wa siku chache mpaka mjiweze. Tutawaleteeni samaki na wadudu wakubwa wakubwa. Tutawaleteeni vile vyote ambavyo hatuwezi kula. Tuna maharagwe mengi na nafaka nyingi zilizobaki miaka iliyopita.

CHIRIKU: Ndege mwenyekiti. Tutawalaje samaki na wadudu wakubwa wakubwa? Ni ndege wachache tu wanaoweza! Toka lini ndege wote….

MAGHARIBI: Mtajifunza.

TAUSI: Lakini nyinyi mna vyakula vingine mnavyoweza kutupa.

MAGHARIBI: Tutawapeni tunavyotaka kuwapa.

MWEWE: Ombaomba hachagui.

MAGHARIBI: Ngojeni nimalize! Tutawapeni msaada huu mkikubali masharti yafuatayo.

KUSINI: Hee! Ndege wanakufa na nyie mnatoa masharti?

MAGHARIBI: Masharti ni haya: Moja, kila ndege akubali kutozaa zaidi ya kinda moja. Mayai mengine yote yaletwe kwetu na tutayala. Pili, makinda yatakayoanguliwa kutoka sasa yaletwe magharibi au kaskazini. Tutawafundisha mbinu mpya za kuishi. Tatu, kila mwaka mtatupelekea manyoya ya Tausi wote wa huku ili tupambe vitundu vyetu.

CHIRIKU: Ndege Mwenyekiti, kwa nini tunasikiliza mambo haya?

TAUSI: Ngoja kidogo Chiriku.

MAGHARIBI: Nne, tutawaleteeni ndege mabingwa wa kuwinda na kuhifadhi chakula. Hao itabidi watiiwe kwa kila hali.

KASKAZINI: Twakubaliana na maoni hayo.

TAUSI: Sasa, kwa kweli sielewi. Ila kupata manyoya ya Tausi wote hapa itabidi tuwaue ndege.

CHIRIKU: Au kwa kuwanyang’anya manyoya tutawaua!

MAGHARIBI: Hayatuhusu! Sisi tunataka manyoya. Mtakavyoyapata shauri yenu.

MASHARIKI: Ndege Mwenyekiti, sisi pia tuna mapendekezo yetu.

TAUSI: Endelea!

MASHARIKI: Asante. Mapendekezo yetu ni hivi. Sisi tungependa kuwafundisheni fikra mpya. Tutaleta waalimu wa itikadi mpya. Tatizo si njaa bali fikra ambazo zinaweza kuzaa njaa.

CHIRIKU: Ndege Mwenyekiti!

KUSINI: Ndege Mwenyekiti!

MAGHARIBI: Ndege Mwenyekiti!

MASHARIKI: Sijamaliza, Ndege Mwenyekiti (Zogo linazuka.)

MTANI: Mambo yakawaka kwa haraka isiyo na baraka. Ndege wakatupiana maneno, matusi yakaruka kama mishale ya vita. Kukurukakara, hakuna lililopatikana. Mbawa zikakamatwa, Shingo zikavutwa. Sokomoko la mchana kutwa likazuka.

(Ndege wote wamesimama na kubishana. Ugomvi unazuka kati ya kikundi na kikundi mpaka wengine wanaanza kuondoka kwa hasira. Hii itaendelea mpaka woie wameloka. Filimbi inaomboleza. MAISA anaingia ameshika mkoba.)

SHANGAZI: Maisa!

MAMA: Maisa!

MTANI: Mchuuzi kaja! (MSHERI anamkaribia MAISA. Wanatazamana. MSHERI anamnyang’anya MAISA mkoba. SHANGAZIanajaribu kumnyang’anya MSHERI. Wanagombea. MAISA anauchukua mkoba.)

MTANI: Mwewe hao. Wamekutana jalalani.

SHANGAZI: Kamwite Mganga.

MGANGA (anaingia): Hamna haja. Nimefika.

MTANI: Mwizi na mganga wajuana kwa mikono mirefu. (MSHERI anamvuta mganga pembeni, Mazungumzo makali. MSHERI anacheka kwa uvivu.) Mimi simtaki raganga. Anatufilisi bure tu.

SHANGAZI: Mganga, pesa zimefika. Endelea na kazi.

MAISA: Eti mganga unafikiri Mtua atapona?

MGANGA: Haswa. Hasa sasa baada ya kuleta pesa za kutosha. (Anaingia ndani.)

MAMA (wanatazamana na MAISA): Maisa, habari za safari mwanangu.

MAISA: Nzuri mama.

MAMA: Umefanikiwa huko ulikotoka?

MAISA: Ndiyo mama.

MAMA: Umetuletea nini mwanangu?

MAISA: Nimeleta dawa ya Mtua.

MAMA: Umeleta pesa za mganga?

MAISA; Nimeleta yote mama.

MAMA: Tumekungoja siku nyingi Maisa.

MAISA: Kazi zilikuwa nyingi. Ilibidi nifunge hapa, nifunge pale. Nilikesha siku hadi siku bila kupumzika.

MAMA: Ulifanya vyema mwanangu. Baba yako sasa atapona.

MAISA: Niliuza usiku na mchana bila kupumzika!

MAMA: Uliuza nini mwanangu?

MAISA: Maskini ana nini ila yeye mwenyewe. (Kimya.)

MAMA: Na sasa umerudi mwanangu.

MAISA: Ndiyo mama. Nimeleta kila kitu.

MSHERI: Hii dawa afadhali ifanye kazi sasa. Mganga, mganga njoo!! (anapuliza mikono kama mcheza kamali.)

MTANI: Utapata urithi wako.

MAISA: Unanuka Msheri.

MSHERI: Nini?

MAMA: Mtoto wa nyoka ni nyoka.

MSHERI: Usinisemeshe, malaya we!

MAISA (anacheka): Aah, Msheri weupe kuliko weupe.

MSHERI: Lete huo mfuko Maisa. Ukinilazimisha nitatumia nguvu (anajaribu kumpora na baada ya kugombea kidogo anaupala. Anaufungua. Kimya.)

MSHERI: Maisa, umeleta pesa nyingi kweli! Mfuko mtupu! Hapana, sio mtupu, kuna kiberiti. Kawa mvuta sigara Maisa. (Anacheka kama mwenye wazimu, Anakiiupa kiberiti chini.) Maisa hizo pesa umezificha wapi? Ninajua unazo. Lete. Sitakudhuru. Ama unataka nije nizichukue kwa nguvu? (Anamsogelea polepole. MAISA anaona hatari inakuja anakimbia. Kisha wananyatiana kama wapiga ndondi.) Umezificha mahali eeh! Maisamtoto mzuri, umeziletaeeh! Mtua anangoja kupona. Hutaki Mtua apone? Hee? Hee! Hizo pesa zina shughuli na mganga, kwa hiyo lete (MSHERI anamshika MAISA na anajaribu kutafuta pesa kuenye mwili wake. Kaiika kukurukakara MAISA anavuliwa nguo. MAMA na MTANI wanamshika MSHERI.)

MTANI: Bibi harusi kafika nyumbani kwa mumewe “Aah” akasema, alipoangalia huku na kuona kuta za mbavu za mbwa. “Aaah” alilia, aliposogezewa mkeka wa kulalia. “Bwana wee! Uliniahidi kitanda cha samadari, nyumba ya sementi, mikate ya siagi na wali wa pilau,” “Acha wee,” kamjibu bwana harusi huku ananyosha miguu. “Ukivitaka hivyo, uvitokee jasho mwenyewe. Mie simo.”

MAISA: Mie siyo punda wako Msheri (Anaokota kiberiti na kuingia ndani kwa MTUAMAMA na MTANI wanamuachia MSHERI. Baada ya muda MAISA anatoka na kwenda kvkaa karibu na MAMAMSHERI amesimama kimya.)

MAISA: Nipigie hadithi mama. Zile ulizonipigia nilipokuwa bado naweza kukaa mapajani mwako.

MAMA: Sina hadithi. Zimekwisha zote.

MSHERI (kwa kejeli): Kuna hadithi ya ndege hapa ambayo haina mwisho. Imekuchosha mara?

MAISA: Kweli, Mtani, nipigie hiyo hadithi.

MTANI: Hadithi imezunguka na kufikia mwanzo. Ndiyo mwisho wa hadithi. Katika mwanzo wangu uko mwisho wangu, alisema Mshairi.

MAISA: Ndege gani hao?

MTANI: Viumbe wa dunia.

MAISA: Wengine wenye busara, wengine wajinga?

MTANI: Wenye nguvu na wanyonge.

MAISA: Walionacho na wenye mikono mitupu?

MTANI: Wamejigawa katika tabaka hili na lile.

MAISA: Mtua?

MTANI: Ndege.

MAISA: Wale wanyonge siku moja walichoka. Wakapanua mbawa zao na kusema potelea mbali.

MTANI: Wakasema husaidiwa anayejisaidia. Wakakodoleana macho na adui zao ana kwa ana.

MAISA: Hadithi ya Mtua hiyo.

MTANI: Hadithi ya ndege hiyo. Mkutano wao uliposhindwa, wale waliouitisha; wale wenye njaa wale, wakajikuta peke yao. Isipokuwa labda wawili watatu nao wenye njaa kutoka kusini au mashariki; ndio walioungana nao.

MAISA: Ndege wenye njaa wakakata shauri kuwa na mfumo mpya?

MTANI: Kurarua dunia na kuiwekajuu chini.

MSHERI: Ama ndege kweli. Na njaa yao?

MAISA: Palipo nia pana upenyo. (Moshi unaonekana ukitoka chumbani kwa MTUA. Unaongezeka mpaka unajaza jukwaa.)

SHANGAZI (kutoka ndani): Moto!!

MAISA (kimya kimya): Moto, ndiyo.

MTANI (kwa kilio cha kulisha): Motoooo!!

MSHERI: Aaah! (Anakimbilia chumbani kwa MTUAMAMA na MTANI wanajaribu kumzuia.)

MAMA: Una wazimu!

MTANI: Wee!

MSHERI: Niachie! Vitu vinaungua, urithi wangu. (MAISA anacheka kichinichini.)

MAMA: Usiende ndani!

MSHERI: Niachie! Wajinga! Pumbavu! (Anachopoka na kutoweka ndani. Anatoka na furushi moja halafu anarudi ndani. SHANGAZIanamfuata. MAMA analia kwa sauti na kumfuata SHANGAZI lakini anavutwa nje. Wakati huohuo, watu wanaingia huku wakilia “moto!” na kucheza ngoma ambayo mapigo yake ni ya kasi sana. Kutoka ndani, milio ya kutisha inasikika na kvchanganyika na kelele za ngoma. Baada ya muda milio na ngoma zinakatika ghafta. Wole wanaioweka isipokuwa MAISAMAMA na MTANI. Kimya.)

MTANI: Katika mwisho wangu uko mwanzo. (Anaomboleza.)

MAMA: Maisa!

MAISA: Mama!

MAMA: Kwa nini?

MAISA: Ilibidi kutupa nafasi ya kupumua.

MTANI: Aah ndiyo, kiberiti. Cheche moja huletajoto la uhai au huleta mauti.

MAISA: Tumaini katika kizazi kipya. Mfumo mpya ni wakati wa kupanda.

MAMA: Umebaki peke yako. Ungeniacha na mie niende.

MAISA: Na wewe ni msingi, udongo unaolisha mbegu mpya.

MTANI: Mie simo, kazi yangu kutazama tu. Niliyoyaona hapa nimeyashuhudia sehemu nyingine. Nitakuwepo kuona kona hii mpya na kusimulia hadithi na visa vingine vya ndege.

MAMA: Mkutano ule wa ndege ulikwishaje vile Mtani?

MAISA: Ndege hawakuwa na chaguo. Kufa na njaa daima au kujitosa kwenye hekaheka.

MTANI: Hiyo umemalizia wewe. Niliwaacha ndege hawajui la kufanya.

MAISA: Kutojua la kufanya siyo kitendo cha kumaliza matatizo.

MTANI: Cheche za kiberiti ndiyo mwongozo?

MAISA: Ndiyo. (Kimya kidogo.)

MAMA: Maskini Msheri!

MTANI: Maskini Shangazi!

MAMA: Maskini Mtua!

MAISA: Waarabu wa pemba.

MAMA: Husikii chochote?

MAISA: Maumivu ya mkono uliokatwa kwa sababu umeambukizwa na kansa.

MAMA: Hiyo tuu?

MAISA: Ulitegemea nini zaidi? Punda anayenyanyaswa akipiga mateke utashangaa? (MAISA na MAMA wanasimama kuangalia masalia ya vitu na watu.)

MTANI: Hata hadithi za ndege zina mwisho. Hakuna kungoja tena. Mchuuzi kachoka na kazi yake, kavunjavunja bakora inayomlazimisha kulala chini. Kakata shauri yeye ni Pronnethea wa sasa. Kwa ujiti wa kiberiti kapasua njia mpya. Ndege mmesikia? Kesho hadithi yenu nitaisimulia, upya. Katika mwisho huu mwanzo unabainika.

MAMA: Lazima nianze ombolezo la mfu (Anaanza kuomboleza na kulia bila machozi.)

MAISA: Nisaidie Mtani kufagia majivu haya. (Wanachukua majani ya miti na kuanza kufagia. MAISA anaimba wimbo si wa furaha si wa huzuni. Nyuma yake inasikika sauti ya MAMA inaomboleza. Watu wengine wanaingia mmoja mmoja na kuanza kufagia na kudakia wimbo wa MAISA na sauti zinapanda mpaka zinafunika sauti nyingine zote.)

MTANI: Nitarudi. Hadithi yangu ilitekwa nyara lakini nitarudi na mpango mzuri zaidi. Nitashauriana na ndege na kuona baada ya mkutano wao wa pili, ulifuatia wa tatu? Labda. Au wamejifunza mitindo mipya ya maneno? Nitawaleteeni hadithi hiyo siku nyingine. (Anaanza kuimba.)

Mwanangati kafumaniwa.
Leo mwanangati atakiona
Kafukuzwa, kapigwa.
Mwanangati uchi amekimbia.
Mwanangati eeh

(Watu wanaingia na miti ya kujenga nyumbo. Ngoma zinaanza kupigwa na wachezaji wanaiga vitendo vya kujenga nyumba mpaka imemalizika.)

MTANI: Sasa?

MTU: Wakati mpya.

MTANI: Hadithi mpya?

MTU: Wakati wa hadithi umekwisha.

MTANI: Aaah!! Vitendo vipya.

MTU: Haya jamani tuanze! (Wote wanajipanga kwenye duara wakaii ngoma zinasikika kwa mbali. Mchezo wa Kidari* unaanzapolepole na mwisho kuchezwa kwa haraka haraka.)

* Mtu mmoja yuko katikati ya duara. Shabaha yake ni kumgusa mtu mwingine. Walio kwenye induara wanajaribu kumkwepa bila kuvunja mduara. Anayeguswa, anaingia katikati.

MTANI: (Wakati mchezo unaendelea) Mchezo wa watoto. Atakayekuwa nacho mwisho ndiye atalala macho. Ndiye Mtua. Hapana, watabadilisha jina. Ndiye Mtemi, kiongozi, Rais, Kamuzu, Jenerali, Waziri, Mwenyekiti, si kitu. Atakayelala nacho ndiye. Ataanza nyayo mpya.

(Mchezo unamalisika kwa ghafla na watu wameganda kaiika ‘tableau’. Juu ya ‘tableau’ ni MTUA aliyenyanyuliwa kwenye mabega ya wengine. Wole wanakenya kwa kutabasamu.)

Kinyume

Mkutano wa Pili wa Ndege ni tamthiliya inayosawiri visa viwili vinavyohusiana: Kisa cha Mtua, na kisa cha Ndege. Kisa cha Mtua ambacho ndicho kikuu, kinaonyesha uhusiano kati ya mtawala dikteta na watu wake na madhara yanayotokea kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Hadithi ya Ndege ambayo inasimuliwa sambamba na kisa cha Mtua, ni istiara ya kisa kikuu. Vilevile, hadithi ya Ndege inaashiria tofauti za kiitikadi baina ya mataifa kwani licha ya “mageuzi” yanayotokea hivi sasa ulimwenguni, inabashiriwa kwamba bado athari za muda mrefu za tofauti hizi zitaleta hitilafu za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Tamthiliya hii ya kisasa inatumia masimulizi, ngoma na nyimbo katika kuwasilisha na kuimarisha ujumbe wake. Aidha itawafaa sana walimu na wanafunzi wa fasihi katika vyuo na hata vidato vya 5 na 6.

AMANDINA LIHAMBA ni Profesa Mshiriki na Mkuu wa Idara ya Sanaa, Muziki na Sanaa za Maonyesho katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ana shahada ya Ph.D kutoka Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza.