TAFRANI: TAMTHILIYA YA VITA BAINA YA UKALE NA USASA

By , in Tamthiliya on .

 

Jamii ya Kizanzibari
inapitia kwenye vipindi vyake vya mabadiliko kama zilivyo jamii nyengine zozote
za kibinaadamu. Kubadilika kwa jamii huwa ni sehemu muhimu ya maisha na,
kwa hakika, si adui wa maisha ya mwanaadamu.
Lakini ili mabadiliko
yawe na maana kwa maisha ya jamii inayohusika, yanapaswa kuakisi ipasavyo
misingi iliyoijenga jamii hiyo katika imani yake, falsafa yake, na taasisi
zake. Taasisi kuu ya malezi ya kila jamii duniani ni familiya, majirani, skuli
au madrasa, na masuhuba ama marafiki.
Familiya ndio chimbuko
la jamii, ndio skuli na madarasa ya mwanzo ambayo mwanaadamu huhudhuria na
kujifunza. Familiya ikikaa sawa, kwa kiasi kikubwa sehemu nyengine za jamii
hufuata njia hiyohiyo. Jamii ya Kizanzibari, ikiwa sehemu ya jamii pana ya
Waswahili wenyeji wa Upwa wa Afrika Mashariki – inatoa nafasi ya pekee kwa
familiya katika maisha ya watu.
Kuna hadithi, methali,
misemo na masimulizi mengi kuhusiana na hayo, kwa mfano, nafasi ya wazazi
kwenye maisha yetu, malezi ya mtoto, na mahusiano baina ya wanafamiliya.
Waswahili huadhiana: “Mama ni mama, japo akiwa rikwama” kuonesha nafasi ya mama
kwenye maisha ya mtu. Hutunga piya kitendawili: “Titi la mama litamu wala
halinishi hamu” ambalo jawabu lake nij usingizi, kuonesha ladha ya malezi
ya mama zetu. Lakini piya kwa wazazi huaswa kwa misem kama vile: “Samaki mkunje
angali mbichi” kuwataka wawape mafunzo mazuri watoto wao tangu wakiwa wadogo,
na au “Ukicha mwana kulia, utalia weye” unaoonya kuwa mzazi asiyetaka
kumrekebisha mwanawe tangu akiwa mdogo, basi atakuja kulia kwa kumkuta mwanawe
huyo amepotea ukubwani.
Baada ya familiya,
taasisi za malezi ni majirani. Namo piya Waswahili wana hekima kubwa na
nyingi sana zinazoutukuza ujirani na kuupa haki yake. Husemwa, kwa mfano, “Wema
mtendee jirani” au “Jirani ndiye ndugu”, tukihimizwa nafasi ya jirani
kwenye maisha yetu, maana ni yeye ndiye tunayemkimbilia tunapopatwa na matatizo
au faraja, kabla ya hata ndugu wa damu, ambaye anaishi mbali nasi. Piya, kwa
sababu ya umuhimu wake huo, ndipo piya wahenga hutuasa kwa kutuambia: “Hala
hala na jirani”, yaani tuchukuwe tahadhari sana kwenye kuishi na majirani zetu
kusudi tusije kuwakera na kuondosha mapenzi baina yetu.
Katika mapokezi ya Dini
ya Kiislamu, ambayo ndiyo dini inayofuatwa na zaidi ya asilimiya 98 ya
Wazanzibari, tunasimuliwa kuwa kiongozi wa dini hiyo, Mtume Muhammad (S.A.W)
alikaribia kumuweka jirani kuwa mmoja wa warithi wetu kutokana na namna ambavyo
alikuwa akihimizwa kumtendea ihsani na Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, ujirani mwema
ni taasisi muhimu ya malezi na ujengaji wa maadili.
Ukiondoa familiya na
majirani, malezi hufanywa piya na vituo vya elimu ambavyo watoto wetu huhudhuria,
iwe ni elimu ya skuli au ya madrasa. Mote humo huwa munapandikizwa misingi
muhimu kwenye vichwa vya watoto wetu, ambavyo ndivyo baadaye vinavyojenga jengo
zima la ubinaadamu wao.
Wajapani husema:
“Ukitaka kujuwa kinachoendelea mitaani, tazama kinachoendelea darasani”. Usemi
huu unamaanisha kuwa, elimu wanayopata watoto wetu huakisika moja kwa moja na
maisha watakayokwenda kuyaishi huko mbele ya maisha yao. Kutengenea kwa taasisi
za kielimu huwa ni kutengenea kwa jamii zetu na kuporomoka kwake, huwa ni kuporomoka
kwa jamii hizo.
Mbali ya familiya,
ujirani na taasisi za elimu, nafasi nyengine muhimu ya malezi na makuzi ya
jamii inatekelezwa na masuhuba walionao watoto wetu. Waarabu husema kuwa:
“Nioneshe marafiki zako, nikuambie wewe ni mtu wa aina gani”, wakimaanisha kuwa
masuhuba wanaombatana kwenye maisha huwa wana tabia ya kuathiriana na hatimaye
khulka zao huwa moja. Kama wasemavyo Waswahili kuwa “Mkaa karibu na waridi,
hataacha kunukia”, basi piya ni sawa kuwa mkaa karibu na karo, hatakosa kunuka
uvundo!
Tamthiliya hii ya Tafrani inawahusu
vijana wa Kizanzibari na namna wanavyoyaishi maisha yao katika jamii hii
iliyojengwa kimaadili. Inalitazama kundi hili muhimu kwenye jamii na namna
ambavyo taasisi zake za malezi – familia, majirani, skuli na masuhuba –
zinavyoyagusa na kuyaathiri maisha hayo kwa namna ya kukinzana, kuachana na
piya kushikana. Inauchambua uwezo na nguvu za kila taasisi kwenye yote mawili –
kheri na shari – na kisha inatuongoza kwenye jawabu lake.
Kupitia mazungumzo na
matendo ya wahusika wa tamthiliya hii, suali kubwa linalojaribu kujibiwa ni:
Nini hasa kilichosababisha hata baadhi ya vijana hawa waliofunzwa maadili mema
wakawa katika tafrani?   SOMA ZAIDI HAPA >>>>>>>

 

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!