SIMULIZI: JUA LISILOKUWA NA MWANGAZA

By , in Simulizi on . Tagged width:

Pazia la maisha yake muda wote lilikuwa wazi kila aliyepita aliyaona maisha yake, maisha ambayo hayakuwa na usiku wala mchana, kwake hakika alijiona yeye si wa thamani zaidi na zaidi alisema kuwa bora angelifariki angali mdogo labda asingelikumbana na shida zote zile zilizomkumba sasa tofauti na umri wake aliofikia, sasa alipata kuwa na takribani miaka 19 hakuwa na imani kwamba atafika aendapo kwani safari yake ya maisha muda wote aligandwa na kutembea na umaskini kama kivuli cha umbo lake la mwili. Muda wote alitembea nao hakika hapakuwa na mzani unaoweza kupima uzito wa matatizo yake, siku zote kwenye maisha yake alikuwa anasubiri ile kauli ya kulala hali ya kuwa ni maskini na kuamka akiwa tajiri ifike kwake na kila alipojaribu kujitua mzigo uliomwelemea alishindwa kwani mzigo alioubeba ulikuwa mzito sana na hakika hapakuwa na wa kumsaidia kumtua mzigo ule.

Kila aliyekutana naye alimhisi kuwa yeye ni chizi au kichaa fulani maana nywele zake zilikuwa sawia kabisa na rangi ya udongo ulio mwekundu tena zilizosokotana na kukamatana kama mkanda uliofungwa barabara kwenye suruali. Machozi kwenye mashavu yake yalizoea kuchirizika na mara zote alikuwa akijiuliza maswali mengi sana na kufikiria juu yaje, ina maana Mungu amenisahau kabisa? Na kama hajajisahau juu yangu je lini ataninolea kisu changu name nianze kula nyama kama ilivyo kwa wengine. Kwa hakika alikosa jibu. Mara zote alikuwa akikumbuka ile siku alipojiwa na mtu ambaye alizungumza kwa sauti ya chini kabisa na kumwambia siku moja lazima ubadili maisha yako na baadaye yule mtu akatoweka, kauli hii hupoza vidonda vya moyo wake na husimamisha machozi ambayo mara zote yalizoea kutiririka mashavuni mwkae. Mtu huyu hakuwa hohe hahe bali ni zaidi ya hohe hahe katika maisha yake, hakuwahi kuwaona wazazi wake kwani walikuwa hawaonekani tena kwenye kioo.

Jua lilipozama kutokana na mawazo aliyokuwa nayo usingizi ulimchukua lakini siku moja aliamini kuwa ataacha kurusha mawe na kuangua matunda yaliyo juu kabisa ya mti na ataanza kula matunda yadondokayo bila ya kutumia nguvu nyingi hatimaye Mungu akamuangazia nuru kwenye maisha yake, je ni nani aliyemfanya akumbuke kauli ile aliyoambiwa na na yule mtu ambaye kwa muda mchache alimpotea na kumfanya aamini kumbe kuna wakati virefu vinaweza kuonekana vifupi hapo ndipo maisha yake yalipojichochea kuni na kuanza kuiva kabisa. Hakika penye nia pana njia maisha yake yalikuwa mazuri kabisa alimiliki nyumba yake na maisha yake aliyatamani yale maisha.

Siku moja alipokuwa safarini alifikiri mengi sana na kujiuliza kwanini Mungu amemzawadia maisha mazuri kama yale na kwanini sio wengine, maswali yale yalikuwa hayana majibu kamili kama yale ya kujiuliza kuwa kuku na yai kipi ni cha kwanza kuja duniani. Hakika hakupata jibu hatimaye akajikuta akitabasamu kwa muda mfupi mara ghafla honi ilisikika kwa ukulele mkali na ikamfanya aamke na kuinuka pale alipokuwa kwani ilikuwa ni njia ya magari na hata watembea kwa miguu, alipojiinua pale alipo ndipo maswali mengi yakaanza kumjia kichwani mwake akaanza kujiuliza kwanini Mungu aliamua kumfikirisha ndoto kama ile pale alipokuwa usingizini, basi hueda nikawa najutia juu ya umaskini wangu lakini siku ambayo Mungu ataamua kunipa utajiri vivyo hivyo nitajutia juu ya utajiri wangu.

Ewe Mungu asante kwa hiki ulichonipa maana kwa hikihiki kidogo kinaweza kikawa kikubwa atakaponiweka na watu wenye shida zaidi yangu na nimeamini kuwa siwezi kufikiria kufungua mlango wa sebuleni ikiwa nimefungiwa chumbani, kwa hiyo ni lazima nianze kufikiria kufungua mlango wa chumbani na baadaye ndipo nifikirie kuhusu mlango wa sebuleni ili niweze kujitoa hapa nilipo.

MTUNZI: Chande Said

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!