SIFA ZA MAIGIZO

By , in Fasihi Simulizi on .

Maigizo ya fasihi simulizi yana sifa zifuatazo:

  1. Huzingatia mtiririko wa visa na matukio: Igizo lolote ni lazima vitendo, visa na matukio vipangwe katika mtiririko sahihi wa mawazo au fikra ili hadhira ipate ujumbe ipasavyo.
  2. Huhusisha ubunifu: Fanani au mtunzi wa igizo lazima awe na ujuzi mkubwa wa kubuni mambo yanayowagusa wanajamii moja kwa moja ili kufundisha, kuelimisha,kuonya, kuasa, kuhimiza, n.k.
  3. Huwa na uwanja maalumu wa kutendea: Igizo hutendwa eneo maalumu lililoandaliwa kama vile jukwaani ambapo hadhira hutazama matendoya watambaji na kusikia maneno yao ili wapate ujumbe.
  4. Huwa na dhana inayotendeka: Igizo lazima lizingatie dhana maalumu iliyokusudiwa kutendwa ili iwasilishwe kwa hadhira. Dhana hiyo huwasukuma watambaji kuandaa igizo husika.
  5. Huzingatia muda au wakati: Muda ni kipengele muhimu sana katika igizo kwani hudhibiti urefu na ufupi wa igizo, huangalia igizo linatendwa wakati gani, na huangalia kama igizo linaendana na wakati uliopo wa jamii inayoishi.
  6. Huwa na wahusika wanaotenda (watambaji/fanani): Igizo huwa na watambaji wanaotenda matendo jukwaani ili wafikishe ujumbe kwa jamii iliyokusudiwa. Wahusika hao huweza kubeba dhamira fulani.
  7. Huwa na hadhira (watazamaji na wasikilizaji wa igizo): Hadira ni watazamaji na wasikilizaji wa igizo ambao ndio wanaopokea ujumbe kutoka kwa watambaji.Hadhira huona matendo na husikia sauti za watambaji na huweza kushiriki kwa kucheka na hata kushangilia (kupiga makofi).
  8. Huwa na upekee wa mtindo: Igizo hutungwa kwa namna inayoruhusu majibizano (dayalojia) baina ya watambaji. Kila mhusika huwa na nafasi yake ya kujitokeza kuzungumza (kutamba) na kutenda kwa hadhira.
  9. Huhusisha utendaji: Sifa moja kuu ya igizo ni kuhusisha utendaji wa wahusika. Matendo ndio uhai wa igizo lolote. Wahusika huigiza jukwaani matendo ambayo ni halisi kwa jamii waliyomo. Kupitia matendo ya wahusika, hadhira hujifunza mambo mbalimbali.
Recommended articles