SHAIRI : UTANDAWAZI

By , in Ushairi on .

SHAIRI : UTANDAWAZI (Globalization)
—————————————
1.
Shukurani Maulana, kun’gea nafasi hini,
u mkarimu Rabana, Mwenyenzi Mungu makini.
Mola nakuomba sana, wanyonge utulindeni,
na huu utandawazi, uloundwa nchi papa.

2.
Kwa huu utandawazi, mapapa wanatumia,
kwendeleza waziwazi, mfumo uharamia.
Hawa damu hawalazi, nafasi huitumia,
utandawazi ni chombo, mwafaka cha mabepari.

3.
Kipindi hakitakuwa, bepari kuwa na utu,
siku zote atakuwa, kama ”nondo mla watu”.
Zama hizi anakuwa, anakula wengi watu,
kwa huu utandawazi, poleni sana wanyonge.

4.
Utandawazi sikia, ni globolaizesheni,
imefungiwa dunia, ndani yake moja sheni.
Sayansi teknolojia, ni matumizi yakini,
ya mfumo haramia, wake huo ufisadi.

5.
Vita leo duniani, vinawamaliza watu,
wote tuko mashakani, mtu anakula mtu.
Ni wafadhili makini, wa kuwagawanya watu,
mapapa hawa hasidi, kupitia ‘tandawazi.

6.
Libya leo angalia, pia Somali na Mali,
Iraki pia Siria, na kwingine tahadhali.
Leo dunia yalia, wanyonge hawana hali,
ni matokeo ya huu, utandawazi fisadi.

7.
Rwanda yaliyotokea, mauaji ya kimbali,
sana yanaelezea, ya ubepari makali.
Unyama uloenea, ni matokeo dhahiri,
ya huu utandawazi, leo tun’okumbatia.

8.
Palipokuwa salama, umeingia unyambi,
dawa za kulevya jama, uhuru wa tabia mbi.
Zile mila zetu njema, mbadala wake dhambi,
uchi sawa hadharani, ndo huo utandawazi.

9.
Ushoga ‘metufikia, kutoka ughaibuni,
debe wanaupigia, sana wakiuthamini.
Kwao wanafaidia, na mambo ya ushetwani,
kupita utandawazi, unyambi watumwagia.

10.
Mola sana utulinde, zama ‘zi tupitilize,
utandawazi tulinde, wanyonge usitumeze.
Una nguvu kila ‘pande, bepari ndogo nguvu’ze,
tupatie hekima’zo tupone utandawazi.

______

Rwaka rwa Kagarama, Mshairi Mnyarwanda,
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare,RWANDA.

Facebook Comments
Recommended articles