SHAIRI: UPAMBAUKAO  HUTWA

By , in Ushairi on . Tagged width:

UPAMBAUKAO  HUTWA

(KWAHERINI!)

 

Upambaukao hutwa, na kutwapo huwa giza

Mtana hupetwapetwa, ukanyang’anywa mwangaza

Nyoyo zikawa kukotwa, japo mwezi waangaza

Laliza hili laliza!

 

Na sisi ule mtana, uliotupambauza

Ulotupa kujuwana, na mengi kuyafanyiza

Leo waanza kununa, mitima kuiumiza

Laliza hili laliza!

 

Hikumbuka tangamano, vyema tulivyolikuza

Mi nanyi ‘kawa mfano, wa lulu katika shaza

Kisha leo saa hino, hiona twalikatiza

Laniliza! Laniliza!

 

Hikumbuka ukarimu, na wema wenu nduguza

Jinsi mulivyonikimu, myaka saba hatimiza

Nahisi najidhulumu, Tanzania kuipeza

Ndipo hamba laniliza!

 

Ingawa ‘menilazimu, na nyinyi kujiambaza

Yondokayo ni sehemu, sehemu najibakiza

Moyo wangu umo humu, Tanzania ‘tausaza

Japo hivyo – laniliza!

 

Ni yangu matumaini, kwenu nayapendekeza

Kwamba hwenda si jioni, nuru ingajipunguza

Pengine wingu angani, ndilo lilojitandaza

Litakoma kutuliza?

 

Na iwapo si hakika, hili nalowaambiza

Jambo moja liso shaka, tusoweza lipuuza:

Utwao hupambauka, hauwezi ukaiza

Hapo halitatuliza!

 

 

Abdilatif Abdalla

Dar es Salaam:

Septemba 8, 1979

 

____________________

Shairi hili nililitunga kuwaaga Watanzania nilipokuwa naondoka Tanzania, baada ya kufanya

kazi Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa miaka sabaa.

Lilichapishwa katika Lugha Yetu, jarida la Baraza la Kiswahili la Taifa  (BAKITA), Toleo la 35/36 (1979-1980), na katika magazeti ya Uhuru, Ngurumo na Mzalendo.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!