SHAIRI: UNANISHINDA MSHONO

By , in Ushairi on .

UNANISHINDA MSHONO

Wenzangu twaeni neno, mlio bara na pwaa

Wa vijiji ja Ugweno, wa miji hata mitaa

Yananiwazisha mno, kukicha nataataa

Nimepata kitambaa, unanishinda mshono

 

Unanishinda mshono, ila nina kitambaa

Naranda huko hukuno, sipati la kunifaa

Naomba mnipe meno, nami niweze kung’aa

Nimepata kitambaa, unanishinda mshono

 

Fuluge hii si ngano, ni kweli ulipo twaa

Ponera sina usono, ni gizani washa taa

Macho hayana uono, kwa hiki kizaazaa

Nimepata kitambaa, unanishinda mshono

 

Shadidu shika ndoano, ni wewe mkubwa jaa

Usiitoe miguno, na kuniona kinyaa

Mambo yangu si mswano, ndiyo kwanza natambaa

Nimepata kitambaa, unanishinda mshono

 

Sovu nishike mkono, chonde sije niambaa

Mlaga lete sindano, kijalizwacho hujaa

Tuutafute mshono, tukishone kitambaa

Nimepata kitambaa, unanishinda mshono

 

Swahibu Amarisono, fukia hili balaa

Ulfat penye tano, weka moja itafaa

Tusitupe maagano, tutachekwa na jamaa

Nimepata kitambaa, unanishinda mshono

 

Tamati natunza wino, Hassani chini nakaa

Kutotajwa siwe neno, ndugu zangu tafadhaa

Nyote mwahusika mno, ya utungoni kuvaa

Nimepata kitambaa, unanishinda mshono

Hassan R. Hassan

Nikiwa Tanga

Mwl Mfaume: UNANISHINDA MSHONO(jibu)

Niletetee Mimi Fundi, Fundi wa yote mashono,

Na sitashona kwa gundi, nitatumia sindano,

Huwa ujinga sipendi, nikiwa kwenye agano,

Nilitee Mimi Fundi, Fundi wa yote mashono.

 

Kozi haukumaliza, ufundi unajitia,

Ona  unavyokuliza, mshono ulotulia,

Inabidi kujikaza, sio unalialia,

Niletee Mimi Fundi, Fundi wa yote mashono.

 

Lete hicho  kitambaa, nikichane kwa muwala,

Bure umetunduwaa, hicho  hukiwezi wala,

Acha sisi mashujaa, tukitendee jamala,

Niletee Mimi Fundi, Fundi wa yote mashono.

 

Kabla hujamaliza, kozi usiombe kazi,

Sasa unaona kiza, inakushinda sakazi,

Leo hii nakujuza, lete kwa sisi wajuzi,

Niletee Mimi Fundi, Fundi wa yote mashono.

 

Nitaishona vizuri, mianya nitaiziba,

Sindano Yangu ni nari,  inachoma kama mwiba,

Ikishakuwa tayari, utakuja kuibeba,

Niletee Mimi Fundi, Fundi wa yote mashono.

 

Mafundi tunatamani, himahima tuletewe,

Wewe waitupa chini, umeingiwa kiwewe,

Ufundi hauna mboni, lete hima ushonewe,

Niletee Mimi Fundi, Fundi wa yote mashono.

 

Nikishona kwa urari, ila  usitie ngoa,

Nyuzi zangu za hariri, na sindano nilonoa,

Tachomeka kwa uzuri,   Mwishowe nitakohoa,

Mimi ndiye yule Fundi, Fundi wa yote mashono

Mwl Mfaume: Mwl R.R. Mfaume(Kivuli cha Mvumo)

 

Morogoro Sekondari

SLP 240

Morogoro

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!