SHAIRI : NIRUDISHIYE UJANA

By , in Ushairi on .

SHAIRI : NIRUDISHIYE UJANA
—————————-
1.
Subukhana wa Taala, Mwenyi-enzi Maulana.
Nakujiya Mtawala, kwa unyenyekevu sana.
Hakika hakuna suala, kwako lisowezekana.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
2.
‘Kinirudisha ujana, vema nitautumiya.
Sikuwi mvivu tena, yalopita najutiya.
Nitachapa kazi sana, nguvu nikizitumiya.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
3.
Shuleni nikirudiya, masomo sin’tachezeya.
Hivi ninashuhudiya, baba alon’elezeya.
Kuwa somo n’kichukiya, mbele sintaendeleya.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
4.
Sasa nimedhoofika, mwili wote watetema.
Moyo kama wapasuka, tumbo kichwa vyaniluma.
Ni mapombe yaninyuka, na tumbaku niso’koma.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
5.
Rai za wangu wazazi, miye nilipuuziya.
Mwalimu mwema mlezi, yake sikuzingatiya.
Sasa ndiyo namaizi, yote waloniwambiya.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
6.
Uliopita mlongo, mahela nililokota.
Yote nikanyweya gongo, sikujenga banda hata.
N’tatumiya kwa malengo, leo pesa nikipata.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
7.
Nguvu za mwili zaisha, mawazo ndo yapevuka.
Ninaelewa maisha, nimefika mingi miaka.
Leo najisahihisha, bila hata pa kushika.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIYA VEMA.
8.
Hivi ndiyo naelewa, ma’na ya kuwajibika.
Niliishi nikilewa, yangu vilewo kusaka.
Hadi sasa ninakuwa, jamii imenichoka.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
9
Nilikuwa sikujali, hata weye Mu’mba wangu.
Nikipuuza kauli, inayomtaja Mungu.
Sasa ‘meanza kuswali, n’kiwa na mwingi uchungu.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
10.
Vema nitautumiya, ujana nikiurudi.
Mno nitakazaniya, kazini kuwa mshindi.
Maisha ‘menipatiya, masomo mengi zaidi.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA..
11.
”Ni kama moshi ujana, uk’enda h’urudi chini”.
Ni tamko alinena, mshairi Shaabani,
Ila kwako Maulana, nini hakiwezekani?
NIRUDISHIE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
12.
Hapa nimeufikiya, wa thenashara ubeti.
Mola umeyasikiya, maombi yangu ya dhati.
Jawabu ‘tanipatiya, naandaa mikakati.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.

**************

Rwaka rwa Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda)
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare,RWANDA.

Recommended articles