SHAIRI: NIJILE TAKA IDHINI

By , in Ushairi on . Tagged width:

NIJILE TAKA IDHINI

 

Nijile ndimi nijile, nijilepo pa kujiwa

Nami sijile na kele, zitazozusha beluwa

Nijile tuteze lele, na shingo tukizitowa

Kama idhini ‘tapawa

 

Nijile tuteze lele, na masogora wenzawa

Na ngoma hizi na zile, zipibwapo kutezewa

Nami ‘tateza vivile, midundo hiinyakuwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Nami ‘tateza vivile, uwandani sitakawa

Na watezewa waole, wafurahi watezewa

Na ijapo mizingile, ‘tangiya kuizinguwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Na ijapo mizingile, izingayo wazingiwa

Hata yangawa ni mile, ‘tajit’atuwat’atuwa

Nazo kumbi zilo tele, ‘tazingiya za kungiwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Nazo kumbi zilo tele, ziso matango na t’uwa

‘Tazingiya nizikale, nikeleti kwa sitawa

Kwa hayano na hayale, nizishize zangu ngowa

Kama idhini ‘tapawa

 

Kwa hayano na hayale, na mengine sitotowa

Mhariri nikujile, ufanye vya kufanyiwa

Na ambavyo vilekele, ni hayano kuchapiwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Na ambavyo vilekele, naweta wa kuwajuwa

Zuberi Lesso nijile, nawe nalishawishiwa

Ahadi nitimizile, ‘siwe mbwa kulaumiwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Ahadi nitimizile, Shabani Gonga tambuwa

U miyongoni mwa wale, walio wana welewa

Numa numa ‘siketile, nikaja nikakutiwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Numa numa ‘siketile, John Komba wagotewa

Mwandani wako ningile, nataraji kupokewa

Sambe nikusahawile, ukanipakaza towa

Kama idhini ‘tapawa

 

Sambe nikusahawile, J. Mayoka pumuwa

Hilino halilekele, la nami kusahawiwa

U mwenzangu mwenginele, upokee ujiliwa

Kama idhini ‘tapawa

 

U mwenzangu mwenginele, siwi mbwa kukuk’utuwa

Salim Ali yuyule, “Kibao” wafahamiwa

Ni mlangoni nikele, nangoja kufunguliwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Ni mlangoni nikele, watunzi nawamkuwa

Wa Ngurumo musikile, salamu nyote mwapawa

Na ambako nitoshile, ‘tanena mupate juwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Na ambako nitoshile, ni Mvita mwakwelewa

La zaidi sitashile, kwongeza mengi yakawa

Nikomilepo komele, nangoja kuchapishiwa

Kama idhini ‘tapawa

 

Nikomilepo komele, sendi nyengine hatuwa

Na ambalo lisalile, ni kwombeyana afuwa

Tupate liteza lele, mitima kufurahiwa

Kama idhini ‘tapawa

 

 

Abdilatif Abdalla

Dar es Salaam

Aprili 7, 1973

 

______________

Hili lilikuwa ni shairi langu la pili kulitunga Tanzania, tangu nilipohamia Dar es Salaam kutoka Mombasa, Kenya, mwezi wa Agosti 1972; na ambako nilifanya kazi Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili (baadaye Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mpaka mwaka 1979. Madhumuni yake yalikuwa ni kuwaomba idhini washairi wa Tanzania wanikubali mimi mgeni kuwa matengoni mwao. Maombi yangu yalikubaliwa, na nikakaribishwa kwa mashairi na washairi kadha wa kadha. Lilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Ngurumo la tarehe 12 Aprili, 1973, na gazeti la Uhuru la tarehe 19 Mei, 1973.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!