SHAIRI : MAMA SIKU IMEFIKA

By , in Zote on .

Mama siku imefika, ya wewe ulonizaa.
Pia sasa ni miaka, tangu walipokutwaa.
Mwaka uliokauka, nusura niwe kichaa.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Ukitaabika mno, kwa nguvu zilobakia.
Ukayasema maneno, wakati ukijifia.
Kwa mithali na mifano, mie ukaniusia.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Mosi kua uyaone, nilidhani maghorofa.
Sikuwazia mengine, ila sherehe na dhifa.
Kumbe usiku mbele, wenywykuleta maafa.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Pili dunia jukwaa, waja wote wasanii.
Haya Maisha Sanaa, tena hayana chalii.
Mwanangu sije shangaa, fasiqi ndiye walii.
Mama sana nayaona, mwanao nimeshakua.

Tatu aso fanya kazi, chakula kwake haramu.
Kila afanyaye wizi, huishia jahanamu.
Jela mwanangu makazi, ya viumbe madhalimu.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Nne swali kwa wakati, kama wataka salama.
Ni faradhi kwa umati, toka kwa wetu karima.
Omba kauli thabiti, mwisho wako uwe mwema.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Ulosema nimeshika, uchao nayatumia.
Ila bado ni mashaka, mwanao ninaumia.
Kwenye panda nimefika, niongoze yangu njia.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Mkono umenitupa, sina nyuma wala mbele.
Maisha yamenichapa, madeni ninayo tele.
Yaani ninakopa hapa, ili nikalipe pale.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Mikosi yaniandama, sina raha nateseka.
Nikaamua kulima, walovuna ni vibaka.
Lipo jambo laniuma, jikoni kulala paka.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Yeyote akiibiwa, ninafuatwa nyumbani.
Maovu nasingiziwa, nisofanya asilani.
Jina baya nimepewa, hapa kwetu mtaani.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

Si punde ulipo naja, Mama yangu nipokee.
Tena jifunge mkaja, na mbeleko jiwekee.
Yote ninayobwabwaja, naomba yakuelee.
Mama sasa nayaona, mwanao nimeshakua.

MTUNZI:DOTTO RANGIMOTO

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!