SHAIRI: MAMA CHURA NA NG’OMBE

By , in Ushairi on . Tagged width:

MAMA CHURA NA NG’OMBE

Amkeni amkeni, ndugu ninawaamsha,
Kwa utulivu kaeni, nataka kuwakumbusha,
Naomba sikilizeni, kisa cha kuhuzunisha,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Alikuwa mama chura, pamoja na watotowe,
Alo mpole wa sura, sijaona mfanowe,
Kandoni mwa barabara, aliishi na wanawe,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Mama chura siku zote, watoto aliwapenda,
Alifanya mambo yote, watotowe kuwalinda,
Lengole wakuwe wote, hawano watoto kenda,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Mama huyo kawaida, kila siku huondoka,
Na kurejea baada, shambani anapotoka,
Ilikuwa yake ada, chakula kwende kusaka,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Siku moja ‘lirejea, akayakuta maafa,
Nyumbani yametokea, wana kadha wamekufa,
Hivyo pasi kuchelea, akataka taarifa,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Wana waliobakia, ikawabidi waambe,
Yakuwa aliingia, mnyama mwenye mapembe,
Nao mrefu mkia, ndipo kikawa kimbembe,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Chura akataka juwa, huyo mnyama ajile
Namna alivyokuwa, sawa na lake umbole?
chura akajifutuwa, ili wana wamuole,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Akazidi wauliza, huku amekasirika,
Chura akikisitiza, waone alivyofika,
kwani amejituniza, karibia kuchanika,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

jibu wakampatia, atambue kwa haraka,
Mnyama alowajia, ni mkubwa kwa hakika,
Hawezi kulingania, na panya wala na paka,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Hasira zikamzidi, tena akatutumka,
Kaongezeka zaidi, ili ng’ombe kumvuka,
Masikini! mkaidi, ghafula akapasuka,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Tama naishia hapa, namaliza kisakale,
Hadithi niliyowapa, inayo mafunzo tele,
Ili msitoke kapa, fikirini kwa makele,
Kisa cha azali, cha chura na ng’ombe.

Mshairi Machinga,
mfaumehamisi@gmail.com,
+255716541703/677620312,
Dar es salaam, Kkoo.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!