SHAIRI : LOLIONDO KWA BABU

By , in Ushairi on . Tagged width:

Habari natangazia, Kuwapatia uhondo

Nchini Tanzania,   Kijiji cha  Loliondo

Watu viguu na njia, Wanoenda kwa vishindo

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Siku imepambazuka, Naamshwa kwa kelele

Najifunga yangu shuka, Kutazama walo mbele

Tayari washazunguka, Kwa Kasisi Ambakile

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Miujiza imefika,  Babu yeye keshaota

Wote mloathirika, Anzeni kujikokota

Loliondo mkifika,  Mizizi inatokota

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Iwapo una nafasi,  Usiende mhimbili

Ondoa na wasiwasi, Loliondo kuna dili

Dawa bei ni rahisi, Kikombe ni buku mbili

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Kashinda madakitari, Walosoma hadi ng’ambo

Magonjwa yote hatari, Yalokuwepo kitambo

Eti mpaka kisukari,  kweli babu ana mambo

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Ukimwi unatutisha, Ugonjwa kama adhabu

Waganga wamechemsha, Kutafuta matibabu

Kama mbinu zimekwisha, Kajaribuni kwa babu

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Kwa babu kuna vioja, Kabla kutoa tiba

Hutangaza yake hoja, Dawa msije kuiba

Mnapata mara moja, Sio kunywa mkashiba

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Wala msifanye pupa,  Walokwenda ni umati

Babu dawa akikupa,  Kunywa  kwa kombe la bati

Usipeleke na chupa, Ukayavunja  masharti

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Aponya kila madhara, Hili wengi wanakiri

Pengine ni  biashara, Katumia muhubiri

Kujitoa  ufukara,  Ajipe na utajiri

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Mara bibi wa tabora, keshaibuka na yake

Kujiona ndio bora, Na yeye afaidike

Watu kweli ni wakora, Jamani tuwajibike

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Sijui kama ya kweli, Msije mkasusia

Mi nahisi utapeli,  Mbuzi ndani ya gunia

Dawa sijaikubali,   Maajabu ya dunia?

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

Namefika kaditama,  Dawa zinanitatiza

Babu ataniandama,  Malenga kuniapiza

Ninaogopa lawama,  Shairi nimemaliza

Kiongozi wa kanisa, Siku hizi anaganga

HAMZA A. MOHAMMED