SHAIRI : KUMBE NANGOJWA NISEME

By , in Ushairi on .

Heri hapa nipahame, nirudi kwetu wenzangu
Nikalishe nikalime, nikafinyange na vyungu
Lakini musinipime, kutaka undani wangu
Kumbe nangojwa niseme, nipashwe vidonge vyangu

Ni kimya sitolalama, nilonalo siwambii
Bora nirudie nyuma, ingawa siyakimbii
Naitafuta salama, ninaradhiwa kudhii
Kumbe kwa kutokusema, pia haisaidii

Kila nikiyaungama, yasiwe mambo ya ngumi
Wao wakiniandama, kunisingizia mimi
Hudhania yatazima, kwa kuufyata ulimi
Kumbe wao watasema, ingawa mimi sisemi

Wao wananizingira, wanibanangia boma
Napigwa kama mpira, waniteka wanizoma
Siwafanyii hasira, ingawa yananichoma
Naamuwa kuwazira, watajibiwa na koma

Hapa najifanya bubu, sineni wanganinena
Najitoa taratibu, haya si ya nyemi tena
Nacha zipande ghadhabu, tuanze kujibizana
Wakisema niwajibu, ibaki kutukanana

Mohamed Khamis
Takaungu
03.04.2019

Facebook Comments
Recommended articles