SHAIRI : JADI ZETU

By , in Ushairi on .

*****
1.
Tuzienzi jadi zetu,
kale ya jamii zetu,
tuendeleshe ya kwetu,
ni utambulisho wetu.
2.
Kuthamini jadi yako,
si kutunza kila mwiko,
ka’ ilivyokuwa huko,
mwenye mimba yai mwiko.
3.
Wala si kuigizia,
babu waliyopitia,
tuwache nguo valia,
na ngozi kuzirudia.
4.
Bali kuyaendeleza,
mazuri waliyofanza,
na halafu kuyatunza,
kadiri tunavyoweza.
5.
Siyo tuwache viatu,
sababu si jadi yetu,
ni dhahiri hivi vitu,
vinayo mafao kwetu.
6.
Utamaduni hakika,
ni dhana yabadilika,
yaliyopita miaka,
kwa leo yanageuka.
7.
Dunia yabadilika,
mila zinabadilika,
ila tunakokutoka,
siyo kwadharaurika.
8.
Zione zetu sanaa,
fani tafauti sana,
ona zilivyo mwanana,
na tena zinavyofana.
9.
Pulika nyimbo za jadi,
na ngoma zetu zaidi,
tafiti dawa za jadi,
ya kale yetu zawadi.
10.
Angalia Wajapani,
na Wachina majirani,
sana wanauthamini,
wa kwao utamaduni.
11.
Jadi zao wakazana,
kuzitafiti kwa kina,
wakiendeleza sana,
mila zao kwa mapana.
12.
Jadi zetu wajameni,
wengi hatuzithamini,
yale ya ughaibuni,
ndiyo tunayatamani.
13.
Jama tujikomboeni,
tujitoe utumwani,
uliojikita ndani,
ndani sana akilini.
14.
Naona upunguwani,
ya babu kudharauni,
huu ni umasikini,
uko ndani ubongoni.
15.
Mazuri ya jadi zetu,
tuyajali wanakwetu,
yawe ni msingi wetu,
wa maendeleo yetu.

*****
Rwaka rwa Kagarama,
(Mshairi Mnyarwanda)
Jimbo la Mashariki,
Wilaya ya Nyagatare,RWANDA.

Facebook Comments
Recommended articles