SHAIRI : CHUMBA CHA GIZA

By , in Ushairi on .

Wengi mmekusanyika, nduzangu na majirani
Sauti zinasikika, zilo na tele huzuni
Yanenwa nimeitika, wito wa Mola Manani
Gogo mwataka lizika, mimi ni chumba cha giza

Vilio mnavyolia, havinipi afuweni
N’nazidi didimia, n’naona hamuoni
Lau mnganisikia, mngazama ugangani
Gogo msije lizika, mimi ni chumba cha giza

Amenifanya ndondocha, izidi yake thamani
Zinanirefuka kucha, hususa za mikononi
Wallahi kila kukicha, mabadiliko mwilini
Gogo msende lizika, mimi ni chumba cha giza

Meno nayo yanyooka, yanaelekea chini
Mdomoni yashatoka, sasa yapo kidevuni
Ili niwe mkomboka, gogo lisende mavani
Gogo msende lizika, mimi ni chumba cha giza

Mama yangu hajiwezi, yuwalia kama nini
Na ajala toka juzi, ale ana raha gani?
Wasaidie Mwenyezi, ukweli waubaini
Gogo wasende lizika, mimi ni chumba cha giza

Ustadhi anenayo, kaegama kwenye dini
Nami yaniumizayo, ni haya ya uchawini
Hakika uchawi ndiyo, uloniweka chumbani
Gogo msende lizika, mimi ni chumba cha giza

Lau ndugu mtashika, ya mnyonge mnyongeni
Yote alosema kaka, Makame yakubalini
Huku ndipo ntatoka, n’tarudi duniani
Gogo msende lizika, mimi ni chumba cha giza

Nasikia m’mepanga, mkanizike nyumbani
Kwenye mkoa wa Tanga, Moa kwetu kijijini
Haya n’nashusha tanga, nenda kufa udongoni
Gogo bure mtazika, mimi ni chumba cha giza

Kwaheri ya kuonana, mkono wangu shavuni
Haingalipo namna, ningalia ifaeni
Moto hauwaki tena, umezimwa na jirani
Gogo linaendazikwa, mimi ni chumba cha giza

Mbaruku Ally
Moto wenu
Abtali
Mjaala
03:12 usiku
19/05/2019
Nikiwa Kigogo Dsm
Mzaliwa Moa
Tanga

Facebook Comments
Donate
Recommended articles