SHAIRI : BUSITANI NI MWANANA, WACHENI KUIHARIBU

By , in Ushairi on .

SHAIRI : BUSITANI NI MWANANA, WACHENI KUIHARIBU
———————————————————————
1.
Busitani hino wazi, imefika mashakani,
jamii ya zama hizi, kwake haina thamani.
Mnaichimba mizizi, kwani kuiharibuni?
mwapandikiza magugu,yanayochafua shamba
2.
Busitani tumerithi, toka kale ya mababu,
ni wa jamii urithi, muwache kuuharibu.
Isibakie hadithi, isokuwa na sababu,
kama vile Kilatini, ile lugha ya Warumi.
3.
Busitani ni mwanana, matundaye mubashara,
kwayo twajadiliana, tukifanza biashara.
Ndani ye tunakutana, kwa kheri si masihara,
Visiwa na mwambaoni, hadi bara mbali sana.
4.
Ni shamba linatufaa, kwalo twawasiliana,
hili limekuwa taa, kwazo fani nyingi sana.
Ni mbali limetandaa, kwalo tunashikamana,
busitani ni mwanana, wacheni kuiharibu.
5.
Msione vyaelea, vinakuwa vimeundwa,
inajitoshelezea, busitani ilokuzwa.
Acheni kuichezea, kwa mambo yasiyo sawa,
mnapoivangavanga, kuichanga na kimombo.
6.
Inakuwa ni hatari, hata wetu viongozi,
jopo la wanahabari, wasanii welekezi,
pasi na kutafakari, kuwa huu upuuzi,
mnapozivanga ndimi, Kiswahili kwa kimombo.
7.
Viongozi yetu taa, Kiswahili msivange,
wanahabari ni nyota, ulimi wetu mchunge.
Wasanii wetu nyota, lugha msivangevange,
Kiswahili chajitosha, kimombo hakihitaji.
8.
Fikiri upo Ulaya, unalonga Ki’ngereza,
huku unagwayagwaya, Kiswahili kuongeza,
niambie pasi haya, aonaje Mungereza?
hata hapa Afurika, wenzio watakupu’za.
9.
Kiswahili laazizi, ni busitani mwanana,
tusikichimbe mizizi, kwacho tunaelewana.
Ni gundi ya pande hizi, yatufanya kushikana,
ni ulimi mtukuka, tuwache kuuharibu.
10.
Shukurani Subukhana, kalamu chini naweka,
umeniwezesha tena, beti hizi kuandika.
Kwako naamini sana, tungo litaeleweka,
busitani ni mwanana, wacheni kuiharibu.
————————————

Rwaka rwa Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda)
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare, RWANDA.

Facebook Comments
Donate
Recommended articles