SHAIRI : BARUA KWA MBARUKU ALLY

By , in Zote on . Tagged width:

SHAIRI : BARUA KWA MBARUKU ALLY

Hakusimama njiani,tarishi ulo mtuma.
ajile hadi nyumbani,na kutekeleza dhima.
ujumbewo mkononi.akanipa kwa heshima.

Usemayo ni yakini,na wala sitolalama.
naona haya usoni,ndiposa nnaungama.
kweli niko lawamani,nduguyo nimekuhama.

Nakiri nimakosani,nilokutenda si vyema.
viumbe sote ni duni,tu dhaifu wanadama.
nakuomba samahani,radhizo sijeninyima.

nisikiza kwa makini,ewe wangu muadhama.
udugu kwetu nishani,alituvika karima.
utele mwangu moyoni,hadi siku ya kiyama.

Kuchwa kucha nimbioni,sikai nihima hima.
mkono wende kinywani,tushibe tuwe wazima.
mwenzio nijukumuni,kulea baba na mama.

Nilipo sina amani,sipati na kuterema.
kwa majonzi fuadini,na hamu imenivama.
tukitiana matoni,tapoa wangu mtima.

Nakhitimisha uneni,nimefikiya khatima.
yatosha nilobaini,Sarai hapa nakoma.
wasalimie nyumbani kifika Darisalama.

SARAI MAULID.
MOMBASA,KENYA.