NYANYA SHUKA BEI

By , in Ushairi on . Tagged width:

🍒🍒”NYANYA SHUKA BEI”🍒🍒

Nyanya umeleta shida, kipi tulichokukwaza
Kila soko we ndo mada, watu wakuzungumza
Umetoweka kwa muda, na bei ukajikweza
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei.

Nyanya moja hadi jero, utadhani Coca-Cola
Unasakwa ngarenaro, bongo hadi ilemela
Waumiza wapogoro, chaga na kila kabila
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei.

Nakumbuka enzi zako, nyanya kumi mia mbili
Tukaangua vicheko, ukioza hatujali
Leo sasa zamu yako, umetupiga kabali
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei.

Kweli tulikudharau, tukakutupa jaani
Kumbe we hukusahau, ukayaweka moyoni
Leo umepanda dau, ndio tunakuthamini
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei.

Hatuli tena michuzi, tumebaki kulumanga
Zimekosa bei nazi, hunogi tena mpunga
Metunyima usingizi,vitambi vinatuchenga
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei.

Kukukata kachumbari, hakuna wa kuthubutu
Walala kwa matajiri, hutaki kurudi kwetu
Umekuwa mashuhuri, na hutukumbuki katu
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei.

Rafikizo bilinganya, kitunguu na karoti
Hawajui Cha kufanya, mbona umewasaliti
Na adui yako panya, kakumisi Sana eti
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei.

Lile chuzi shatashata, tulilomezea mate
Limekuwa pwatapwata, mradi tonge lipite
Kwa manji tunakukuta, na nyumbani kwa dangote
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka bei.

Ewe nyanya shuka bei, ili tuheme wanyonge
Kwa michuzi tujidai, yasitukwame matonge
Mama lishe wapo hoi, yanadorora magenge
Tunakukumbuka nyanya, tafadhali shuka beiii…!

Dada D.
Malenga wa Uhehe

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!