Namba ya moduli 3: Uhamasishaji wa mawasiliano katika lugha ya ziada : Sehemu ya 5: Kusaidia ujifunzaji wa lugha ya ziada

By , in DIPLOMA/CHETI on .

Sehemu ya 5: Kusaidia ujifunzaji wa lugha ya ziada

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kujenga mahusiano ya kusaidiana katika lugha ya ziada?

Maneno muhimu: mawasiliano ya mtu binafsi; marafiki wa kalamu; kupeana taarifa za ndani.

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • kuanza kukuza mahusiano baina ya wanafunzi ambayo yatasaidia ujifunzaji wao wa lugha ya ziada na kuwasaidia katika kutafakari juu ya ujifunzaji wao wenyewe;
  • kutoa nafasi kwa wanafunzi kuwasiliana kwa kutumia maarifa ama wazungumzaji wa lugha ya ziada amabao kwao hiyo ni lugha mama kuweka nafasi kwa ajili ya mawasiliano na wanafunzi nje ya shule yako.

Utangulizi

Wanafunzi wengi Afrika wana nafasi chache za kushirikiana na wazungumzaji wa lugha yao ya ziada ambao kwao hiyo ni lugha mama.

Mara nyingi welewa kwenye lugha unapatikana kwa njia za kusoma, kusikiliza redio na kutazama televisheni.

Hata hivyo, zipo njia zitakazowasaidia wanafunzi wako kuzungumza na kuandika kwa watu wenye ufasaha katika lugha ya ziada. Unaweza pia ukawasaidia wanafunzi wako kuwasiliana kwa kutumia lugha ya ziada na wanafunzi wa shule nyingine

Sehemu hii inaangalia njia zitazotumika kufanikisha jambo hili.

Somo la 1

Kwa watu ambao hujifunza lugha katika mfumo wa kawaida wa darasani, misemo ambayo watu hutumia kila siku katika maingiliano yao mara nyingi huwa ni kitu cha mwisho kujifunza.

Zipo njia ambazo zinaweza zikatumika kuwasaidia wanafunzi wako kupata ustadi katika misemo na sentensi ambazo wanaweza kuzitumia pindi wanapokutana na watumiaji stadi wa lugha ya ziada. Kila seti ya misemo au sentensi zinatakiwa:

ziwe fupi na rahisi kujifunza;

ziseme kitu ambacho wanafunzi wanataka;

ziwe zinatumiwa na watu wengi;

ziwaruhusu wanafunzi kuanza majibizano na kujenga mahusiano;

ziwaruhusu wanafunzi kujifunza zaidi kuhusu lugha kutoka kwa watu wanaozungumza nao;

zisichochee majibu marefu toka kwa watu wengine.

Uchunguzi kifani ya 1: Kujifunza kiZulu kupitia katika mahusiano

Liz Botha aliyepo Mashariki mwa London, Afrika Kusini, alijifunza kiZulu kama lugha ya ziada kupitia mradi wa lugha za ndani uitwao TALK. Kauli-mbiu ya mradi wa TALK ilikuwa, ‘Jifunze kidogo, na utumie SANA!’

Alianza kwa kujifunza namna ya kusalimia kwa kiZulu, na kuwaeleza watu kuwa alikuwa anajifunza kiZulu. Alijifunza pia kuwataka wao wamsemeshe kwa kiZulu na kumsaidia katika zoezi lake la kujifunza lugha hiyo.

Aliwatafuta watu ambao anaweza kuzungumza nao kiZulu, na kubaini kuwa kuna idadi kubwa ya wazungumzaji wa kiZulu wanaofanya biashara ya kutembeza matunda na mbogamboga katika mtaa wa karibu na nyumbani kwake. Alifanya mazoezi ya sentensi zake kwao na kuanza kuwaelewa.

Alikuwa na rafiki aliyekuwa anamfundisha misemo mipya, na kujifunza kutoka kwake namna ya kuuliza bei ya kitu fulani na kukinunua. Hizi ndizo sentensi alizozitumia wakati uliofuata alipowaona rafiki zake wanaotembeza biashara.

Kadiri muda ulivyozidi kwenda, alijifunza kujieleza kwao kuhusu yeye mwenyewe na familia yake. Baadaye aliwasimulia hadithi fupi kuhusu nini kilichotokea kwake siku moja kabla, au mwisho wa wiki. Mmoja wa watembeza biashara aliyeitwa Jabu, akawa rafiki yake wa karibu sana na kumfundisha maneno na sentensi nyingi. Mwishowe akawa anawasaidia watu wengine kujifunza kiZulu katika mradi wa TALK.

Shughuli ya 1: Kujenga mahusiano ya kujifunza lugha

Waulize wanafunzi wako ni wapi wamesikia lugha ya ziada ikizungumzwa. Ni watu gani pia wanaowafahamu kuwa wanaitumia vizuri? Ni nani wanaweza kuzungumza naye lugha ya ziada? Zingatia watu waliopo nje na ndani ya shule na pia watu ambao unaweza ukawaalika katika darasa lako. Fikiria ushirikiano na shule ya karibu kama unaweza kukuza mtagusano katika lugha ya ziada.

Sasa wanafunzi wako wanafahamu ni akina nani wanataka kuzungumza nao, pangilia mambo wanayotaka kusema nao.

Kwa utaratibu maalum, wasaidie kujifunza msamiati kama mradi wa muda mrefu. Weka uzito katika sauti na matamshi bayana.

Waache wafanye mazoezi wawiliwawili.

Mawazo juu ya vitu vya msingi vya kujifunza yanajumuisha:

salamu na kuagana;

kutaja na kuuliza majina na taarifa binafsi na za familia;

kueleza kuwa wao ni watu wanaojifunza lugha na kuwa wanahitaji msaada wa kujifunza;

kununua vitu;

kuzungumzia kuhusu hali ya hewa;

kuelezea mambo yalitokea jana;

kuomba radhi, kuomba kitu au jambo, kusifu, n.k

Wahimize wafanye mazoezi na watu waliowapendekeza (hapo juu).

Tenga muda fulani kila wiki ili kufuatilia maendeleo yao.

Je kuna mafanikio na matatizo gani wamekumbana nayo? Ni lugha ipi mpya wamejifunza?

Nini kingine walichojifunza?

Somo la 2

Katika sehemu hii,tunapendekeza kuwa uwahamasishe wanafunzi waandike barua kwa kutumia lugha ya ziada. Hii inaweza kuwa na maana ya kuweka mhusiano ya mbali na wazungumzaji wa lugha ya ziada, ama wanaweza kuwaandikia rafiki zao wa karibu.

Unaweza kuanzisha utaratibu wa rafiki wa kalamu na darasa lingine (tazama Nyenzo-rejea 1: Marafiki wa kalamu ). Hili linaweza kuwa darasa katika nchi yako au nchi nyingine.

Kama wanafunzi watakuwa waandishi na wasomaji wanaojiamini wakingali shule ya msingi, kuna uwezekano mkubwa kuwa waandishi wa barua wenye mafanikio hapo baadaye katika maisha yao. Kadiri wanavyoandika barua binafsi kwa marafiki zao, unaweza pia ukafundisha mtindo mwingine wa uandishi wa barua. Hili litawaandaa kwa ajili ya mahitaji ya baadaye, kama vile, kuomba kazi, barua kwenda magazetini, barua za pongezi au rambirambi.

Uchunguzi kifani ya 2: Kuandika kwa ajili ya kufariji au kulalamika

Wanafunzi wa darasa la 5 la Bibi Linda Shigeka walikuwa katika mfadhaiko na hawakuweza kushiriki vema katika kazi zao za shule. Mwanafunzi mwenzao mmoja, Mandisa, alifariki katika ajali ya basi. Walimkumbuka sana rafiki yao.Walikuwa pia na hasira kwa sababu walisikia kuwa basi halikuwa na breki.

Bibi Shigeka aliwahimiza wanafunzi kueleza namna wanavyojisikia. Alibaini kuwa wanataka kufanya jambo fulani, akawauliza kama wanataka kuiandikia familia ya Mandisa barua. Akapendekeza kuwa waandike barua mbili, moja kwa Kiswahili kwa ajili ya wazazi na wazee (babu na bibi) na nyingine kwa Kiingereza kwa ajili ya kaka na dada ambao wamekulia London wakati wazazi wao walipokuwa uhamishoni. Wanafunzi walisema kuwa wanataka kuieleza familia ya Mandisa kuwa wapo pamoja nao na pia wanataka kuwaeleza mambo mazuri kuhusu Mandisa.

Bibi Shigeka aliwasaidia kwa kuwapa dondoo za maandishi yao. Wanafunzi waliandika barua binafsi kwa Kiswahili. Katika somo lililofuata, Bibi Shigeka aliwasaidia kuandika barua moja kwa Kiingereza kwa ajili ya darasa zima na kisha kila mwanafunzi aliweka saini yake

Kwa msaada wa Bibi Shigeka, waliandika pia barua kwa Kiingereza kwenda kwenye kampuni ya basi wakiomba kuwa mabasi yakaguliwe vema kuhakikisha kuwa ni salama na yanafaa kutembea barabarani.

Wanafunzi walipata majibu ya barua zote mbili walizoandika. Bibi Shigeka akazibandika barua hizi kwenye ubao wa matangazo uliopo darasani.

Bibi Shigeka alibaini ni kwa namna gani suala hili limewahamasisha wanafunzi na kuwapa stadi muhimu ya kijamii. Imewasaidia pia kuona lengo la kujifunza lugha ya ziada.

Shughuli ya 2: Barua ya kwenda kwa rafiki au rafiki wa kalamu

Soma Nyenzo-rejea 1 kwanza, na anzisha uwenza na shule jirani.

Mpe kila mwanafunzi darasani mwako jina la rafiki wa kalamu ambaye wanaweza kuanzisha uhusiano. (Kama haitawezekana, jaribu kumfanya kila mwanafunzi kumtambulisha mwanafunzi wa darasa lingine au jamaa au rafiki wa mbali na nyumbani ambao wangependa kuandikiana barua). Kama una shule nyenza tayari au ndiyo unaiasisi ( angalia Nyenzo-rejea 1 kwa namna ya kulitekeleza hili ), dumisha mawasiliano ya karibu na mwalimu mwenza wako, kujadili matatizo nyeti na kuyatafutia suluhisho kwa pamoja.

Jadili na darasa lako juu ya vitu ambavyo wangependa kuzungumzia katika barua yao ya kwanza. Wakati huo huo wanaweza kubadilishana habari juu ya maisha yao, familia zao, rafiki zao, mambo wayapendayo na matarajio yao.

Ridhia muundo wa barua (angalia Nyenzo-rejea 2: Kuandika barua ), na waache waanze kuandika. Zungukazunguka ukiwasaidia maneno na virai wanayohitaji.

Waache wapitie na kuhariri barua zao katika jozi. (angalia Nyenzo-rejea 3: Kupima ubora wa barua za marafiki wa kalamu ). Zichukue barua, na toa mrejesho saidizi na wenye kujenga.

Waache wanafunzi waandike toleo la mwisho la barua yao, andika anuani juu ya bahasha na uitume (kwa njia ya posta).

Kwa wanafunzi wadogo, hii yaweza kuwa shughuli ya darasa zima na andika wanayotaka kusema. Wanaweza kuwaandikia darasa jingine hapo shuleni.

Je, unawezaje kusaidia maendeleo ya huu uhusiano wa kuandikiana barua?

Je, unawezaje kusaidia pale unapohitajika, wakati wa kutoa nafasi kwa mahusiano kukua?

Somo la 3

Kuzalisha vitabu ambavyo wanafunzi wameandika na kuvitengeneza, sio tu kunawaongezea kujisifu, lakini pia kunakupatia Nyenzo-rejea nzuri darasani.

Sehemu hii hujengwa na mawazo ya Kitabu Kikubwa katika Moduli 1, Sehemu 5. Inapendekeza kuwa uwape moyo wanafunzi wako kuyaleta maandishi na michoro yao katika hatua ya mwisho kwa kutengeneza kitabu. Hii wanaweza kushirikiana darasani, au na watu, kikundi au shule nyingine.

Unatakiwa ufikirie ni kwa jinsi gani unaweza kupanga na kuendesha zoezi kama hili. Utatakiwa kufikirikiria juu ya aina ya kitabu cha kutengeneza (mfano kitabu cha kukunja), vielelezo na mpangilio wa kitabu, na aina ya kitabu (k.m kitabu cha nyimbo, kitabu cha hadithi au kitabu cha hadithi isiyo ya kubuni).

Utapaswa kufikiria juu ya nyeno rejea zitakiwazo na wapi pa kuzipata. Uanweza kuwashirikisha wanafunzi katika kukusanya baadhi yake kabla hujaanza kabisa kazi darasani. Aina hii ya upangaji na uandalizi ni muhimu kama darasa lako ni kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kujifunza (angalia Nyenzo-rejea muhimu: Kuwa mwalimu mwerevu katika mazingira (hali) yenye changamoto .)

Uchunguzi kifani ya 3: Kutengeneza kitabu cha darasa

Bibi Ndekule, ambaye anafundisha wanafunzi 44 wa darasa la 5 huko Zanzibar, alitaka kuwatia moyo kama waandishi na wasomaji na aliamua kutengeneza nao kitabu kwa kutumia lugha yao ya ziada ya Kiingereza.

Aliwambia kuwa alitamani kuanzisha hifadhi ya vitabu kwa ajili ya darasa, na ingestawi tu kama wangezalisha baadhi ya vitabu vyao wenyewe. Walijadili aina gani ya vitabu walipenda kusoma na aliviorodhesha ubaoni. Orodha ilijumuisha, riwaya, mashairi na vitabu juu ya michezo na mavazi. Halafu aliwambia wanafunzi waunde makundi madogo yasiyozidi watu sita wenye kupenda aina fulani ya kitabu.

Bibi Ndekule ailjadiliana na kila kundi juu ya aina ya kitabu watakachoandika. Kundi moja liliamua kujigawa katika makundi mawili ya watu watatu kutengeneza vitabu viwili vya michezo, kimoja cha mpira wa miguu na kingine cha riaadha. Kundi jingine lilitaka kuandika kitabu cha hadithi juu ya hadthi za mapokeo. Bibi Ndekule aliyapa makundi muda kupanga dondoo zao kabla hajawaambia wajadiliane na wengine. Darasa lilitoa mwitikio kwa kila kundi. Katika wiki iliyofuata, aliwapa muda wa darasani na wa kazi za nyumbani kuadika kazi zao.

Walipomaliza rasimu zao za mwanzo, Bibi Ndekule alizipitia na kutoa mwitikio juu ya njia za kuboresha vitabu vyao. Rasimu zao za mwisho zilikuwa ziameisha katika wiki iliyofuata na ziliwekwa kwenye maonesho kwa ajli ya darasa zima kuvisoma.

Shughuli muhimu: Kutengeneza kitabu cha ubia

Pendekeza kwa darasa lako watengeneze kitabu kwa ajili ya shule nyenza (au kwa lengo jingine) kikiwa na nyimbo, mapishi na habari nyingine za nyumbani. Kama una kitabu cha mapishi, waoneshe. Baadhi ya vitabu vya mapishi huwa na picha , habari na hadithi juu ya mahali na watu wanaohusiana na mapishi.

Amua ni nyimbo zipi au mapishi yapi yatajumuishwa na jinsi yatakavyo wasilishwa. (angalia Sehemu 1).

Amua kwa pamoja ni mambo gani zaidi yatakuwemo ndani ya kitabu. Angalia Nyenzo-rejea 4: Nyimbo na hadithi kuhusu michakato –nyimbo hizo hizo na hadithi zinaweza kujumuishwa. Mashairi na maelezo kutoka kwenye shughuli zilizopo katika Sehemu 2 na 4 zinaweza kuhusishwa. Fikiria kuhusu vielelezo(michoro), picha, maelekezo ya michezo ya asili, riwaya au mashairi.

Panga na wanafunzi wako ambao watafanya kila sehemu ya kazi, nani atahariri kazi na lini kila sehemu ya kazi itakuwa iimekamilika. (Moduli 1, Sehemu 5, Nyenzo-rejea 1: Jinsi hadithi zinavyotengenezwa kitabu. Huonesha jinsi kitabu kinavyoandaliwa na watu tofauti.)

Andaa mpango. Kama inawezekana, toa nakala ya kitabu ili kimoja ubaki nacho na kingine ukipeleke katika shule nyenza. Waombe pia shule nyenza kama wanaweza kukutumia kitabu walichotengeneza.

Pale nyenzo zinapokuwa chache, karatasi zilizotumika, kalenda za zamani, magazeti ni vifaa ambavyo unaweza kuvikusanya kirahisi kutengenezea kitabu. Kwa mawazo zaidi, angalia Rejea muhimu: Kuwa mwalimu mwerevu katika mazingira yenye changamoto.

Nyenzo-rejea ya 1: Marafiki wa kalamu

 Taarifa ya usuli / maarifa ya somo kwa mwalimu Wewe!

Kama unapenda kuwa na mawasiliano na shule katika nchi yako au nchi nyingine ambayo pia hutumia vifaa vya TESSA , tafadhali wasiliana na Jane Devereux wa Open University, kwa kutumia j.b.devereux@open.ac.uk au tumia anuani ifuatayo: The Open University, P O Box 77, Walton Hall, Milton Keynes MK7 6BT, UK.

Pia unaweza kuasisi uhusiano kati ya darasa lako na darasa la rika sawa kutoka shule nyingine na panga kila mmoja wa wanafunzi wako kuwa na rafiki wa kalamu. Hii itawapa wanafunzi wako faida ya kuwa na rafiki wa kumwandikia na kupokea majibu kutoka kwake, juu ya maswala yanayowapendeza, kutumia lugha ya ziada au lugha ya biashara/maasiliano. Watapata mazoezi katika kusoma na kuandika kwa lengo maalum, na kujifunza zaidi juu ya watu wengine, familia zao, shule, nchi na mtindo wa maisha.

Kabla hujawaingiza wanafunzi wanafunzi wako kwenye mpango/mradi, hakikisha umeshachanganua vizuri mambo kama ville mgawo na malipo ya bahasha na stampu. Unaweza ukaweka barua zote kwenye bahasha kubwa na kuituma kwa mwalimu.

Nyenzo-rejea 2: Uandishi wa barua

 Taarifa ya usuli / maarifa ya somo kwa mwalimu

Wanafunzi wana mwelekeo wa kufurahia zaidi uandishi wa barua (katika ama lugha ya mama au lugha ya ziada) kama wanahisi kuna sababu halisi ya kuandika na kwamba watu wengine watavutiwa kuzisoma. Kutakuwa na hali kadhaa ambapo utumizi wa lugha ya ziada utakuwa ni mwafaka zaidi. Kwa kila hali, unapaswa kujadili lugha ipi ya kutumia.

Unaweza kupanga na walimu katika shule nyingine ili wanafunzi wa shule moja wawaandikie barua wanafunzi wa shule nyingine (taz. Nyenzo- rejea 1). Unaweza pia kuwasaidia wanafunzi kuandika barua kwenye kampuni kuomba mchango wa fedha, vitu au huduma kwa ajili ya shule. Kama umewapeleka kwenye ziara katika jumuiya yako kwa mfano kliniki, mradi wa kilimo au kiwanda, unaweza kuwasaidia kuandika barua ya shukurani. Kunaweza kuwepo matukio ya furaha au huzuni ambapo ingekuwa vyema kwao kumwandikia mtu barua ya pongezi/hongera au rambirambi.

Kwa aina yoyote ya barua utakayotaka kushughulikia, kwanza jadiliana na wanafunzi kwa nini watu huandika barua na mambo wanayotaka kusema katika aina hiyo ya barua. Andika mawazo yao ubaoni, na uwasaidie kuyapanga katika aya. Ukitaka unaweza kutumia vidokezo vilivyo hapa chini.

Pindi wanafunzi wamalizapo barua zao, zitume kwa mtu au shirika lililolengwa. Unaweza kukusanya barua zote na kuziweka kwenye bahasha moja kubwa ikiwa na anwani husika. Kama wewe na wanafunzi mna bahati, mtapata jibu!

Vidokezo vya barua kwa ‘rafiki wa kalamu’ katika shule nyingine (au nchi nyingine).

 

Mpendwa ……………….

 

Nimefurahi sana kwamba tutakuwa marafiki wa kalamu. Katika barua hii lengo langu ni kujitambulisha kwako.

Jina langu kamili ni ………………………………. Nina umri wa miaka …… Kwa kuwa sina picha ya kukutumia sasa hivi, nitaeleza ninavyoonekana. [ikifuatwa na sentensi zenye maelezo haya]

Ningependa kukuambia juu ya familia yangu [ikifuatwa na sentensi kuhusu familia]

Tunaishi ………………… [ikifuatwa na sentensi juu ya mahali ]

Haya ni baadhi ya mambo ninayopenda. Chakula ninachokipenda ni….muziki ninaoupenda ni ……………. Somo ninalolipenda zaidi shuleni ni ……..

Wakati wa wikendi mimi hupendelea……….

Nitakapomaliza shule ninatarajia ……………….

Ninatarajia kupata jibu kutoka kwako hivi karibuni……………

Ninakutakia kila la heri,

Wako,

[Jina na saini]

Vidokezo vya barua ya shukurani baada ya ziara ya shule

 

Mpendwa ……………….

Kwa hakika nilifurahia ziara yetu hapo.……………….

Kilichonivutia kuliko vyote kilikuwa …………………………….

Nilifikiri hili lilikuwa na mvuto kwangu kuliko vitu vingine kwa sababu……………………

Kama shule yetu itapata nafasi ya kufanya ziara nyingine, ningependa ……………….

Ninakushukuru sana kwa ……………………………………………….

Wako mwaminifu,

 

[Jina na saini]

Vidokezo vya barua kwa kampuni kuomba mchango

 

Bw./Bi ……… [jina la mtu]

Ninaandika barua kuomba msaada wako. Shule yetu inahitaji …………………

Tunahitaji hili kwa sababu ……………………………………………………….

Ninakuandikia kwa sababu …………………. [sababu kwa nini kampuni hii inaweza kusaidia]. Ninatumaini utaweza kutusaidia. Wako mwaminifu

 

[Jina na saini]

Nyenzo-rejea 3: Kutathmini barua za urafiki wa kalamu

Kwa matumizi ya mwanafunzi

Je, barua inaunda picha hai na ya kuvutia ya mwandishi? Taarifa gani zinatakiwa kuongezwa ili kuifanya ivutie zaidi?

 

 

 

Je, maelezo yametolewa kwa ufasaha? Je, barua inasomeka kwa urahisi?

 

 

 

Je, mada tofauti zimeshughulikiwa katika aya tofauti?

 

 

 

Je, barua iko katika njeo sahihi? (Maelezo yanaweza kuwa katika njeo iliyopo.) Je, kila kitenzi kiko katika njeo iliyopo au, kama si hivyo, kuna sababu ya msingi ya kutumia njeo tofauti? (Unaweza kuamua kuhusu aina za miundo unayotaka kukazia katika shughuli hii.)

 

 

 

Je, barua inaonekana ni nzuri? (Safi, imepangiliwa vizuri.)

 

 

 

Nyenzo-rejea 4: Nyimbo na hadithi kuhusu michakato

Nyenzo-rejea za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi

Hapa kuna wimbo wa kijadi wa Kiswahili unaofafanua michakato mbalimbali ambamo nafaka hupitia kabla ya kuliwa. Uliambatishwa katika kijitabu cha ‘Michakato na Uchakataji’. Wimbo huo unaweza kuingizwa kwenye kitabu cha mapishi. Hadithi zinafuatia, ambazo nazo zinatoka kwenye chanzo hicho hicho, zinaweza pia kujumuishwa kwenye kitabu hicho cha mapishi au cha mchakato.

Ninakipenda chakula

Chakula cha asubuhi,

Makande, uji na viazi

Ugunduzi wa mtama

Hapo zamani za kale palikuwa na mwanaume aliyekuwa na wake wawili. (Katika baadhi ya sehemu za Afrika, wanasema, ‘Mke mmoja – tatizo moja. Wake kumi na mbili – matatizo kumi na mbili!’) Mke mkubwa hakuweza kuwa na watoto, kwa hiyo alipogundua kuwa mke mdogo alikuwa mjamzito, aliona wivu sana. Lakini hakuwa na la kufanya.

Mume na mke mdogo wakapendana sana. Na hili likamfanya mke mkubwa aone wivu zaidi. Kwa hiyo mke mkubwa aliamua kusubiri mpaka baada ya mke mdogo kujifungua.

Lakini mtoto alipozaliwa, alikuwa ni mtoto wa kiume. Kwa mujibu wa mila, mke mkubwa alitakiwa kuwatunza mtoto mchanga na amariya (mke mdogo) kwa miezi michache. Mke mkubwa aliamua kwenda msituni kutafuta kitu cha kumpikia mke mdogo ambacho kingemdhuru. Alitarajia kwamba mke mdogo angekufa, na hapo angeweza kumlea mtoto mchanga kama mtoto wake mwenyewe.

Kule msituni, mke mkubwa aliona mmea ambao ulikuwa na vichwa vyenye punje zikuazo juu yake. Hajawahi kuona kitu kama hiki hapo awali. ‘Hii itamfanya alale, usingizi mzito hasa, kiasi kwamba hataweza kuamka siku itakayofuata. Kisha nitaandaa mazishi mazuri sana.’

Alipika mtama na kumlisha amariya. Alipata mshangao, amariya hakulala usingizi mzito wala kufa. Badala yake, alinenepa na kuonekana mwenye afya na kupendeza kila uchao. Vilevile, mtoto mchanga alinawiri.

Mke mkubwa alipoona matokeo ya kitu alichokuwa anakipika na kumlisha mke mdogo, aliamua kukionja yeye mwenyewe. Aliipenda ladha yake, na aliendelea kukipika na kukila kitu hicho kipya. Yeye pia, alianza kunenepa na kuwa na afya zaidi.

Sawa, mume alishindwa kujizuia kuona kuwa wake zake wawili walipendeza sana, na mtoto alikuwa na afya. Alitaka kukionja, kwa vyovyote kilivyo kitu hicho, ambacho wakeze walikuwa wanakula. Kwa hiyo, wote wakawa wanene na wenye afya.

Na, kwa hakika, katika kijiji, neno husambaa kwa haraka sana, Kabla muda haujapita, wanakijiji wote waliobaki walitaka kujua kitu ambacho familia hii ilikuwa inakula. Na ndivyo ikawa kwamba mtama ukagunduliwa.

Ugunduzi wa jibini

Hapo kale palikuwa na wanandoa vijana waliokuwa na kundi kubwa la ng’ombe na kundi kubwa la kondoo. Mume aliilisha familia yake kwa kukamua ng’ombe. Nyakati hizo, walihifadhi maziwa kwenye vibuyu.

Wanandoa hao wakati mwingine waligombana; na mke alionekana akikimbilia kwa mama yake, huku mumewe akikimbia kumfuata, kwa kufoka na kupiga ngumi hewani.

Siku moja wakati walipokuwa wakigombana, mume alikuwa ameshika kimojawapo kati ya vibuyu vyenye maziwa mazito yenye malai. Wakati mke wake alipokimbia, mume alimkimbiza, kama kawaida. Lakini safari hii alisahau kuweka chini kibuyu cha maziwa mazito yenye malai. Kadri alivyokuwa akikimbia na kumfokea mkewe, alikunja ngumi yake huku akiwa amekishika kibuyu hewani. Kwa hakika, mume alikimbia upesi sana kiasi kwamba kibuyu cha maziwa kilitikisika kwa nguvu hasa.

Aliposhindwa kumkamata mkewe, hali ya kuwa ameishiwa na pumzi, mwanaume alikaa chini. Alikuwa anasikia joto na kiu baada ya kumkimbiza mke wake na kumfokea. Kwa hiyo aliweka kibuyu mdomoni ili anywe kinywaji cha maziwa mazito yenye malai. Lakini hayakuwa maziwa yaliyomwagika toka kwenye kibuyu. Yalikuwa vitu kama maji! Haya yote yalikuwa ni makosa ya mke wake!

Mume alipigwa na butwaa. Alikaa chini na kuangalia ndani ya kibuyu. Kitu gani kimetokea kwenye maziwa mazito yenye malai? Kwa nini yamegeuka kuwa kitu cha majimaji? Akajaribu kuweka funda lingine mdomoni. Ikawa hivyo hivyo. Akaweka mkono wake ndani ya kibuyu na kugundua kwamba kulikuwa na bonge fulani. Nina hakika unaweza kukisia kitu alichokiona. Ndiyo, ni sawa, ilikuwa ni bonge la jibini laini yenye mafuta. Wakati mume aliporamba vidole vyake, aliona kwamba bonge la kitu hicho lilikuwa na ladha nzuri. Ilikuwa kama mafuta.

Alirudi nyumbani kwake haraka, akatafuta mkate wa mahindi, na kuupaka kiasi cha mafuta toka kwenye kibuyu kwenda kwenye kibonge cha mkate. Mkate ulikuwa na ladha nzuri zaidi kuliko kawaida. Hasira yake ikayeyuka. Wakati mkewe aliporudi baada ya kitambo kidogo, alimwonesha kilichotokea, na alimpa kiasi cha mafuta ili ajaribu kukionja kwenye mkate.

Kwa muda mrefu baada ya hapo, kila jibini inapokuwa imemalizika, mume alianzisha ugomvi na mkewe ili aweze kuchukua kibuyu cha maziwa mazito yenye malai anapomkimbiza. Alielewa kwamba kwa namna hiyo, maziwa mazito yenye malai yatatengeneza jibini.

Siku moja wakati jibini kidogo sana ilikuwa imebakia, mke alichukua kibuyu cha maziwa mazito yenye malai na kukitikisa kwa nguvu kadri alivyoweza. Alikitikisa, na kukitikisa. Alipoacha kukitikisa zaidi, alikiweka chini. Unaweza kukisia alichokiona ndani ya kibuyu, huwezi? Aliona jibini, na kiasi cha majimaji ya maziwa.

Jioni hiyo mume aliporudi nyumbani, mkewe alimgeukia na kusema, ‘Labda kama tutatingisha kibuyu kilichojaa maziwa mazito yenye malai kwa nguvu, tutatengeneza jibini nyingi zaidi. Hivyo hatutalazimika kugombana tena.’

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa, kwamba waliishi kwa raha mustarehe, na kuwa familia yenye afya kwa kupiga maziwa mazito yenye malai kutoka kwenye mifugo yao, na jibini, ambayo wamejifunza kuitengeneza.

Imetoholewa kutoka: Ngtetu, C. & Lehlakane, N., Inqolowa, The Discovery of Amazimba and The Discovery of Butter, Umthamo 3, University of Fort Hare

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!