Namba ya moduli 3: Uhamasishaji wa mawasiliano katika lugha ya ziada : Sehemu ya 3: Kuunda Fursa za Mawasiliano

By , in DIPLOMA/CHETI on .

Sehemu ya 3: Kuunda Fursa za Mawasiliano

Swali Lengwa muhimu: Unawezaje kuunda shughuli za kukuza mawasiliano katika lugha ya ziada?

Maneno muhimu: tofauti katika taarifa; maingiliano ya kimawasiliano; umaanifu; kuunda shughuli; makundi

Matokeo ya ujifunzaji

Mwishoni mwa sehemu hii, utakuwa umeweza:

  • umeunda shughuli za mawasiliano halisi katika darasa lako la lugha ya ziada;
  • umeendeleza ‘maktaba’ ya nyenzo za kuchochea mazungumzo asilia;
  • umetumia kazi za vikundi na za wanafunzi wawili wawili ili kukuza mawasiliano ya lugha ya ziada.

Utangulizi

Ukiwa mwalimu, unapaswa kutumia matokeo ya tafiti kuhusiana na kitu unachokifanya. Tafiti za hivi karibuni zinaonesha kwamba watu hujifunza lugha kutokana na kushiriki katika mawasiliano yenye maana ya lugha husika, katika mazingira asilia. Hoja hii inamaanisha nini?

‘Kushiriki’: Kila mwanafunzi lazima ashiriki –au ahusishwe kikamilifu.

‘Umaanifu’: Shughuli lazima iwe inalandana na mazingira halisi na ilete maana kwa wanafunzi.

‘Maingiliano’: Mawasiliano lazima yahusishe njia-mbili (au njia tatu au nne).

‘Mazingira asilia’: Lugha inayotumiwa lazima iwe lugha ya kawaida ya mawasiliano ya kila siku.

Katika sehemu hii, tunaangalia jinsi ya kuchochea maingiliano ya kimawasiliano ya aina hii darasani kwako, hususan kwa kutumia picha. Tunashauri kwamba uunde uteuzi wa zana.

Kwa kawaida, darasa lenye kazi za maingiliano ya kimawasiliano hufanywa katika makundi madogo madogo. Itasaidia kusoma Nyenzo-rejea Muhimu: Kutumia kazi za vikundi katika darasa lako .

Somo la 1

Kuwatia hamasa wanafunzi ili wawasiliane miongoni mwao kunahusu uandaaji wa shughuli wanazoweza kuzifanya pamoja, na ambazo ni ‘halisi’. Makundi yanasaidia kutiana moyo na yanawawezesha wanafunzi kujaribu lugha mpya.

Mawasiliano ‘halisi’ huhusisha ‘tofauti za taarifa’; kwa maneno mengine, wanafunzi hugundua kitu ambacho hawakukifahamu awali kutoka kwa wenzao. Zamani, wanafunzi wangeweza kuagizwa kumwuliza mwanadarasa mwenzao, ambaye jina lake wanalifahamu vizuri, ‘Jina lako nani?’ Hapa hakuna tofauti ya taarifa, kwa hiyo mawasiliano haya si ‘halisi’.

Uchunguzi-kifani 1 na Shughuli 1 zinaonesha jinsi utafutaji wa taarifa zinazokosekana unavyoweza kutumika kwa lengo la kuunda makundi au kazi za watu wawili wawili. Vile vile, angalia Nyenzo-rejea 1: Mifano zaidi kuhusu Shughuli za tofauti za taarifa .

Uchunguzi kifani ya 1: Shughuli za tofauti za taarifa katika kuunda makundi

Liz Botha wa East London, Afrika ya Kusini, alitaka kugawanya kundi la walimu 40 katika makundi manne, kwa namna ambayo ingewasaidia kuwasiliana miongoni mwao.

Alitafuta jumla ya picha 16 zote katika ukurasa mmoja wa kitabu (angalia Nyenzo-rejea 2: Mawazo katika picha ). Alitengeneza nakala nne za ukurasa huo na kukata picha kumi kutoka katika kila ukurasa ili apate makundi kumi yenye picha nne nne: viatu; bendera, nk. Kisha alizichanganya picha.

Walimu walipofika, alimpatia kila mmoja picha moja, na kuwaambia wasiioneshe kwa mtu yeyote. Kisha akawaagiza watembee kuzunguka darasa, wakiuliza maswali ya aina hii:

Swali: Una picha ya (n) …. ?

Jibu: Hapana, sina./Ndiyo, ninacho.

Waliendelea namna hii mpaka wakaunda kundi la watu wanne wenye picha zinazofanana.

Baada ya makundi kuundwa, wanavikundi wakaanza kusemezana, na wakagundua, kwa njia ya majadiliano, kwamba wana kitu kimoja kilicho sawa kwa wote: labda wote wanne wana dada wadogo, au wanapenda au hawapendi aina fulani ya chakula au muziki, nk.

Walifurahia mno shughuli hii, na waliikamilisha kwa kufahamiana zaidi miongoni mwao.

Ni kwa jinsi gani unaweza kufanya shughuli kama hii katika darasa lako?

Shughuli ya 1: Tafuta mwenzi wako

Andika orodha ya maneno yanayohusiana na somo la hivi karibuni (angalia Nyenzo-rejea 3: Maneno na maana ili kuona baadhi ya maneno).

Wape kila wanafunzi wawili wawili neno moja kutoka kwenye orodha na vipande vidogo viwili vya karatasi. Waambie waligawe neno lao katika sehemu mbili/nusu, na waandike nusu moja katika kila kipande miongoni mwa vipande hivyo vidogo vya karatasi.

Kusanya na changanya vipande vyote vya karatasi. Sasa mpe kila mwanafunzi nusu-neno.

Waambie wanafunzi wamtafute mwanafunzi ambaye ana nusu nyingine ya neno lao, na kisha wasimame naye.

Kundi la wanafunzi wawili wawili lisome maneno yao mbele ya darasa.

Kisha, kila kundi la wanafunzi wawili wawili liandike maana ya neno lao katika kipande kingine cha karatasi. Kusanya maana hizo na maneno yaliyo nusu.

Wape tena maneno yaliyo nusu na rudia mchakato wa kuoanisha.

Baadaye, taja kila maana kwa zamu na liambie kundi la wanafunzi wawili wawili likae chini litakaposikia maana ya neno lao. Mtu yeyote asiseme kama wamekaa chini kwa kukosea au kwa usahihi. Mwishoni maana zitafafanuliwa.

Jaribu mchezo huu tena na angalia kama wanaweza kuucheza kwa haraka na kwa usahihi zaidi.

Je, shughuli hii iliwasaidia wanafunzi wako kuelewa maana za maneno? Unajuaje?

Somo la 2

Ukiwa mwalimu, mara zote unapawa kutafuta shughuli ambazo zinakuza ujuzi wa kusikiliza kwa kuelewa.

Hapa, Shughuli 2 inahusisha kusikiliza na kuchora, au kubadili lugha ya taarifa kwenda katika kielelezo cha taarifa. Ina faida inayofanana na mwitikio wa mwili wote (total physical response); kwa sababu wanafunzi hawalazimiki kutumia lugha katika kuonesha welewa wao. Hata hivyo, inatakiwa yule anayeelezea awe fasaha na sahihi sana –vinginevyo, athari zinaweza kuonekana kwenye picha ya mwanafunzi mwenza.

Uchunguzi kifani ya 2: Kueleza na kupanga mawasiliano yasiyofahamika kwa njia ya posta

Aghalabu, Lulu alikuwa akipata ‘mawasiliano asiyoyafahamu’ yaliyowekwa kwenye sanduku lake la barua: matangazo kutoka kwenye maduka mbalimbali yanayoonesha picha za bidhaa zao. Siku moja aliamua kuyaweka, badala ya kuyatupa kwenye pipa la taka.

Alikata sehemu tofauti tofauti za bidhaa za nyumbani: pakiti za vyakula, sukari na unga; maboksi ya sabuni za unga na nafaka, nk. Alikuwa na nakala nyingi.

Alichora picha sita za vinafasi vya kabati la jikoni, na kuchomeka bidhaa za nyumbani katika vijinafasi vitatu ( Nyenzo-rejea 4: Eleza na panga sinaonesha mifano). Kila moja kati ya picha hizo tatu ilikuwa tofauti na nyingine. Kisha alikata nakala za bidhaa zote kwenye vijinafasi vya kabati la jikoni. Bado alibakiwa na vijinafasi titatu visivyo na kitu.

Siku iliyofuata, kwenye Darasa lake la 4, makundi matatu ya wanafunzi sita sita au saba saba yalipewa picha za vijinafasi vya kabati vilivyojaa vitu. Vile

vilivyokuwa vitupu, viligawiwa kwa makundi mengine matatu, na wanafunzi tofauti katika makundi haya walipata nakala za bidhaa.

Aligawa makundi hayo katika sehemu mbili, na kulifanya sehemu ya 1 (ililo na picha zilizokamilika) kukaa karibu na sehemu ya 2 (yenye vijinafasi visivyo na kitu na bidhaa tofauti). Wanakundi la sehemu 1 walieleza jinsi bidhaa zilivyopangwa kwenye vijinafasi, na wanakundi la sehemu 2 walizipanga katika vijinafasi vilivyokuwa vitupu. Waliuliza maswali pale ambako hawakuwa na uhakika. Mchezo huu uliwapa zoezi la kutumia maneno kuhusu nafasi mbalimbali katika mazingira ‘halisi’.

Somo lilikwenda vizuri. Lulu aliamua kwamba wakati mwingine atakuza msamiati wa wanafunzi wake kwa kuwaambia wachambue na kueleza taswira za –au, kama itawezekana, ngoma-halisi na vitu vilivyobuniwa kutoka katika jumuiya ya mahali hapo.

Shughuli ya 2: Eleza na chora

Shughuli hii hufanywa katika makundi au na watu wawili wawili. Mtu mmoja anaeleza na mwingine/wengine anachora/wanachora. Darasa lenye wanafunzi wa viwango mbalimbali, wanafunzi wakubwa wanaweza kutoa maelezo, na wadogo wachore.

Tafuta picha au michoro rahisi sana au chora ya kwako, m.f. mchoro wa vistari wa picha ya nyumba au mti. Utahitaji picha moja kwa kila jozi au kundi la wanafunzi. Picha zinaweza kuwa sawasawa au tofauti.

Anza kuwafundisha wanafunzi msamiati na aina za sentensi ambazo watahitaji kuzitumia, mfano, ‘Chora mraba katikati ya ukurasa’. ‘Chora kuku wawili kando ya nyumba.’

Toa picha moja kwa kila jozi (au kundi) la wanafunzi, huku ukiwaambia ‘watoa maelezo’ kutowaonesha wenzao picha hizo. Mwanafunzi aliyeshika picha anaielezea picha hiyo kwa wanafunzi wengine/mwanafunzi mwingine, ambaye anajaribu kuchora kitu kinachotolewa maelezo. Hawatakiwi kusema picha hiyo ni nini.

Mwishoni, mtoa maelezo na mchoraji wanalinganisha picha zao. Anza mjadala wa darasa zima: Duara la ‘Asanda’ ni dogo kuliko lililoko katika picha’. Kuku wa Amina wana vichwa vikubwa, lakini kuku walioko katika picha wana vichwa vidogo.’ Wakiwa wanafanya mazoezi, wataifanya vizuri zaidi shughuli ya aina hii.

Nyenzo-rejea Muhimu: Kufanya kazi katika madarasa makubwa/madarasa ya mchanganyiko kunatoa mawazo zaidi kuhusu mbinu za kufanya kazi.

Somo la 3

Ukiwa mwalimu, unapaswa kukumbuka kwamba aghalabu, binadamu (pamoja na wanafunzi) hutaka kujua maana ya kitu wanachokifanya. Kila shughuli unayowapa wanafunzi lazima iwape fursa ya kutafuta maana.

Uchunguzi-kifani 3 na Shughuli Muhimu vinatalii njia za kutafuta maana katika aya au matini. Wanafunzi wafanye mazoezi ya baadhi ya maarifa muhimu yaliyomo katika maandishi hayo: utabiri na utazamiaji (kukisia kitu gani kitatokea baadaye). Walitakiwa pia kuwasiliana miongoni mwao ili kutatua tatizo. Kila mmoja alikuwa na nafasi ya kuchangia ili kutatua ‘fumbo’ na kutafuta maana.

Uchunguzi kifani ya 3: Hadithi: kutoka vyanzo tofauti na kuwekwa pamoja

Darasa la 6 la Bibi Ndaba lilileta hadithi kutoka majumbani na kuzieleza kwa ufafazi. Katika kila ukurasa, waliandika sentensi na kuchora picha inayoona na sentensi husika. Kurasa hizo zilipachikwa kwenye magamba ya plastiki ya kurekodia na kuunda jarida ambalo ili kutengeneza kitabu.

Mfanyakazi mwenzie, Bibi Mapande, ambaye anafundisha darasa la 3 aliziona hadithi zilizofafanuliwa, na akaomba kuziazima kwa ajili ya shughuli ya kusoma katika darasa lake. Bibi Ndaba alifika kuangalia darasa la mwenzie.

Bibi Mapande aliligawa darasa lake katika makundi matano. Alilipa kila kundi hadithi lakini alizitoa kurasa kutoka kwenye jarida na kuliweka jarida hilo katikati ya meza. Alimpa kila mwanafunzi katika kundi ukurasa mmoja wa hadithi, huku akihakikisha kwamba amechanganya mpangilio wa kurasa hizo. Kila mwanafunzi alitakiwa kusoma sentensi iliyo kwenye ukurasa wake mbele ya kundi lake. Kwa njia ya majadiliano, kundi liliamua sentensi ipi ikae mwanzo wa hadithi, na kuweka sentensi nyingine zote katika mpangilio unaostahili; na kurudishia kurasa katika jarida kwa mpangilio sahihi.

Bibi Mapande alimwambia mwanafunzi mmoja kutoka katika kila kundi, asome hadithi ya kundi lake mbele ya darasa; na wanadarasa walitoa maoni kuhusu mpangilio wa sentensi. Wakiwa katika darasa, walichagua hadithi waliyoipendelea zaidi, na igizo la dakika tano likaandaliwa kuonesha hadithi hiyo.

Shughuli muhimu: Sehemu za kitu kizima

Unaweza kutumia shughuli ya aina hii kwa darasa la kiwango chochote

Chagua hadithi fupi, iliyoandikwa vizuri, au aya ambayo wanafunzi wako wanaweza kuielewa na kuihusisha na ukweli. Unaweza kutumia hadithi, hadithi au aya za/ya picha kama zile zilizoko katika Nyenzo-rejea: Kuunda maana , au aya ambayo ni changamano zaidi ya lugha au mada yoyote. Kila kundi linaweza kuwa na hadithi hiyo hiyo au tofauti ya kushughulikia.

Ikate hadithi katika vipande sita au saba. Vipande vyaweza kuwa aya, sentensi au kundi la sentensi, kulingana na umri na uwezo wa wanafunzi wako. Pachika kila kipande kwenye kadi.

Lipe kila kundi seti ya sehemu za aya zilizokatwa.

Kila mwanakikundi ana kipande cha aya, na anawasomea wengine kipande chake. Wakiwa kama kundi, wanaziweka aya zao pamoja katika mpangilio wake sahihi.

Kwa wanafunzi ambao wana uwezo au uzoefu zaidi, waambie waeleze jinsi walivyofanya mpaka kupata mpangilio sahihi.

Soma aya au hadithi hizo mbele ya darasa.

Nyenzo-rejea ya 1: Shughuli zaidi zihusuzo tofauti za taarifa

Nyenzo za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi

Kufanana ni nini?

Chagua seti za picha sita au nane. Kila seti ya picha lazima iwe na kitu kinachofanana kwa picha zote. Kwa mfano, unaweza kuwa na picha sita ambazo zote zina kitu kimoja ambacho kimetengenezwa kwa kioo, au seti ya picha sita ambazo katika kila picha kuna mtu anakula. Pengine una picha sita ambazo zinaonesha mtoto, au zinaonesha umaskini, au ukarimu.

Gawa darasa lako katika makundi ili kila kundi linaweza kuwa na seti ya picha kadhaa. Hakikisha kwamba una baadhi ya picha za akiba, kwa ajili ya kundi lolote litakalomaliza kazi haraka. Mara kundi linapomaliza, unaweza kukusanya seti za picha zao na kuzigawa kwa kundi lingine ambalo limemaliza.

Wanakikundi wasioneshane picha zao. Wanatakiwa kuulizana na watu wengine katika kundi aina ifuatayo ya maswali:

Je, kuna (kitu)…. katika picha yako?

Je, kuna (vitu)…. katika picha yako?

Je, picha yako inaonesha …. ?

Wanakikundi wengine wanajibu:

Hapana, hakuna. Au, Ndiyo, ipo/zipo.

Hapana, haioneshi. Au, Ndiyo, inaonesha.

Mtu ambaye anabainisha sifa ya ufanano ndiye mshindi.

Mchezo huu ni rahisi au mgumu zaidi kutegemeana na kiwango cha udhahania kilichomo kwenye sifa ya ufanano.

Unafanya nini ili kujipatia kipato?

Andika orodha ya kazi ubaoni, kama hii iliyopo hapa chini.

Daktari Daktari wa Meno Mwalimu
Muuza duka Muuguzi Meneja
Karani Rubani Mhandisi
Mtunza Bustani Mkutubi Askari polisi
Mkulima Mchuuzi wa samaki Fundi wa ngamizi
Mhudumu katika ndege Mfamasia Mama Ntilie/Lishe
Mtaalam wa maua Mwanasayansi Mwanamuziki
Mtaalam wa ngamizi Mhudumu wa dukani Fundi gereji

Waambie wanafunzi waseme wangependa kufanya nini watakapomaliza masomo yao. Wanaweza kuongeza kazi nyingine katika hizo zilizoorodheshwa.

Toa kadi kwa jozi za wanafunzi na waambie waandike jina la kazi kwenye kadi hiyo. Kwenye kadi nyingine, wanatakiwa waandike fasili ya kazi hiyo.

Mwambie mwanafunzi mmoja kutoka katika kila jozi kutoa ripoti mbele ya darasa kuhusu kazi waliyonayo, na fasili yake. Wanafunzi wengine lazima watoe maoni kama wanadhani fasili ni sahihi.

Kusanya kadi za kazi na maana zake, zisambaze kwa wanafunzi bila kufuata utaratibu wowote. Waambie wanafunzi wazunguke darasani na kutafuta mwenza ambaye ana fasili au neno sahihi.

Wenza wanapopatana, wanatakiwa wasimame pamoja mpaka kila mmoja hapo darasani amalize shughuli hiyo.

Kisha waambie waunde sentensi kwa kutumia kazi walizozifasili.

Nyenzo-rejea 2: Madokezo kwa ajili ya picha

Nyenzo za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi

Chanzo asilia: Books on display: New Day-by-Day English Course

Line drawings: Modern English Teacher, 10

Nyenzo-rejea 3: Maneno na maana – mifupa katika mwili

Nyenzo za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi

Neno Maana
Muungabega/Hu merus Aina ya mfupa iliyopo sehemu ya juu ya mkono
Fuu la kichwa/Cranium Fuvu, ambalo huhifadhi ubongo
Fibula/goko Mfupa mdogo kati ya mifupa miwili iliyopo sehemu ya chini ya mguu
Radias/Radius Mmoja kati ya mifupa ya kwenye kiwiko ambao huzunguka kadri unavyouzungusha mkono wako
Fema/Femur Mfupa mmoja uliopo juu ya mguu na ulio mrefu kuliko yote mwilini
Pingilimgongo/Ve rtebrae Mifupa ambayo huunda uti wa mgongo na inayoshikilia neva zipitazo sehemu hiyo
Kifupakono/Meta carpals Mifupa iliyopo kwenye mkono
Kifupakidari/Ster num Mfupa wa kwenye kidari, ambao unahifadhi moyo
Skapula/Scapula Mfupa ambao unajulikana kama bapa la bega sehemu ya nyuma
Muundi goko/Tibia Mifupa mikubwa miwili iliyopo sehemu ya chini ya mguu
Tarisas/Tarsus Mkusanyiko wa mifupa inayounda sehemu ya juu ya kiwiko na goti

Nyenzo-rejea 4:

Nyenzo za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi

Unaweza kuandaa michezo kama hii kwa kutumia mpangilio wa nyumbani na picha za samani. Viweke katika sanduku lako la zana kwa matumizi ya baadaye, au ili wanafunzi watumie wakati watakapokuwa na nafasi kwa ajili ya shughuli za kujisomea na ujifunzaji binafsi, na kufanya mazoezi ya msamiati. Unaweza kuhitaji kutumia vitu na bei za mahali hapo.

Nyenzo-rejea 5: Kuunda maana

Nyenzo za mwalimu kwa ajili ya kupanga na kutumia na wanafunzi

Aya kwa ajili wanafunzi wa madarasa ya juu: Wafalme wa Zulu

Wafalme wa Zulu walianzisha utawala wa kinasaba wenye nguvu kuliko tawala zote za watu weusi katika Afrika. Mkuu Shaka, ambaye alianzisha utawala wa kinasaba mwanzoni mwa karne ya 19, aliunganisha taifa la Wazulu na kuunda kikosi cha kijeshi kilichokuwa cha kuogopesha. Kufuatia kujulikana kwake kama ‘Napoleon Mweusi’, mfalme huyu wa kwanza wa Wazulu alikuwa katili, ingawa pia alikuwa kiongozi mwerevu sana. Kutokana na sifa yake ya kuwa mshindi na asiye na huruma katika vita, aliongoza watu wake kujipatia umashuhuri na aliwatawala kwa nidhamu ya ukali. Mauaji aliyomtendea nduguye aliyechangia naye mzazi mmoja ambaye alimsaliti, Dingane, hayakusaidia kupunguza utawala wa kigaidi. Lakini Dingane, aliyejiingiza matatani, ijapokuwa alikuwa katili na dikteta, hakuwa mwanajeshi, na utawala wake uliishia katika maafa. Baada ya kuzidiwa nguvu na Makaburu katika vita ya Mto wa Damu, hatimaye Dingane alilazimika kuikimbia nchi ya Zulu, na alifia uhamishoni. Baada ya kifo chake eneo la jirani la Natal likawa makazi ya wazungu, na mkondo wa historia ya Zulu ukabadilika.

Vyanzo asilia:

Matini iliyoandikwa – imetoholewa kutoka ‘The Zulu Kings’, na Brian Roberts, Hamish Hamilton, 1974. imekaririwa katika Rodseth, V. na wengine. 1992. Think Write: A writing skills course for students, teachers and business people. Randburg: Hodder and Stoughton Educational. ISBN 0 947054 87 1

Hadithi ya picha – Standard 2 Language Book, Maskew Miller Longman

Recommended articles