Mwongozo kwa waandishi wa Kiswahili sanifu (BAKITA, 1994)

By , in Sarufi na Utumizi Wa Lugha on . Tagged width:

UTANGULIZI

Mojawapo ya njia za kueneza na kukiimarisha Kiswahili ni ile ya kuandaa maandishi ambayo yatasomwa na watu wengi. Upo msemo usemao “Watu hupenda kusikia, lakini zaidi hutaka kuona.” Hapa Tanzania Lugha ya Kiswahili huzungumwa kila siku na watu mbalimbali na ni kwa jinsi hiyo kinazidi kuenezwa na kuimarishwa zaidi. Lakini ni wazi kwamba njia hiyo peke yake haitoshi. Upo umuhimu wa kutayarisha maandishi ili yapate kusomwa na watu wengi.

Baraza la Kiswahili la Taifa linaamini kuwa, kwa njia ya vitabu vilivyoandikwa katika mtindo mzuri wa uandishi, lugha ya Kiswahili itaendelea kukua na kuimarika zaidi. Vitabu hivyo ambavyo kama vikitunzwa vizuri, vitaendelea kusomwa na vizazi vijavyo.

Kitabu hiki cha MWONGOZO KWA WAANDISHI WA KISWAHILI SANIFU kitakuwa msaada mkubwa sana kwa waandishi wa vitabu na magazeti, wataalamu wa lugha, wanafunzi wa shule na vyuo, wachapishaji, wahariri, na wasomaji kwa ujumla, katika kufahamu matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili pamoja na kujua namna ya kukiandika kwa usahihi.

Kitabu hiki kina sehemu nne muhimu. Sehemu ya kwanza inahusu matumizi ya herufi kubwa, vituo mbalimbali vya uandishi na jinsi ya kutumia tarakimu katika makala. Sehemu ya pili inaelezajinsi ya kuunda na kuandika (pamoja na kukata) maneno ya Kiswahili kwa usahihi. Vilevile, uundaji na uandikaji wa finyazo umepewa uzito wa pekee katika sehemu hii. Sehemu ya tatu inahusu vipengele muhimu ambavyo kila mwandishi wa Kiswahili sanifu hana budi kuzingatia ili aweze kuandika kwa ufasaha. Sehemu ya nne, ambayo inahusu uandikaji wa fafanuzi na marejeo, inampa mwanga mwandishi jinsi ya kuandika kazi yake kitaalamu na kuwaelekeza wasomaji wake kuielewa zaidi mbali ya kujua vyanzo vya taarifa alizozitumia.

Pamoja na kutoa mwongozo huu, BAKITA linapenda kuwajulisha wananchi kuwa BARAZA hili limekabidhiwa mamlaka ya kuthibitisha kazi zote za maandishi ya Kiswahili. Katika kufanya kazi hii BARAZA litatumia zana zifuatazo:

· Kamusi ya Kiswahili sanifu
· Machapisho ya Tafsiri Sanifu
· Machapisho ya BAKITA
· Machapisho mengine yatakayokuwa yametolewa kama uamuzi wa BAKITA kutokana na kazi za utafiti kuhusu usanifu au ufasaha wa lugha ya Kiswahili.

Kwa hiyo, kazi zote za maandishi ya Kiswahili zitakazokuwa zimesomwa na kuthibitishwa na BAKITA zitapigwa muhuri wake wa ithibati. Muhuri huu utapigwa baada ya hatua zote muhimu za uhariri wa muswada kukamilishwa ili kutoruhusu mabadiliko zaidi yatakayohusu maandishi yaliyothibitishwa.

Kazi ya utayarishaji wa Mwongozo huu ilibuniwa kwa mara ya kwanza mwaka 1982 na kuanza kutekelezwa na Ndugu P.C.K. Mtesigwa wa Idara ya Sarufi na Ithibati ya BAKITA wakati huo, ambaye alitayarisha rasimu ya mwanzo. Baadaye kazi hii ilipamba moto wakati Kamati ya Uchapishaji ilipoisimamia na kuitilia mkazo mwaka 1987. Ni katika mwaka huo ndipo Kamati hiyo ilipokutana mjini Morogoro kwa siku mbili, Novemba 26 na 27, 1987 ili kupitia Mwongozo huu na kufanya marekebisho muhimu. Kamati hiyo ilikuwa na watu wafuatao:

Ndugu Dk. T.S..Y. Sengo

Chuo Kikuu cha D’Salaam (Mwenyekiti)

Ndugu Prof. E. Kezilahabi

Chuo Kikuu cha D’Salaam (Makamu wa Mwenyekiti)

Ndugu S.A. Kibao

UKUTA

Ndugu F. Rajabu

UHURU NA MZALENDO

Ndugu E. Mahimbi

Ofisa Utamaduni (Iringa Mjini)

Ndugu S.K. Msuya

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima

Ndugu B.M. Khatibu

Pemba

Pia watumishi wa BAKITA wafuatao walihudhuria warsha hiyo:

Ndugu S.J. Maina

Katibu Mtendaji

Ndugu A.J. Kishe

Idara ya Lugha na Fasihi

Ndugu S.D. Irira

Idara ya Istilahi na Kamusi

Ndugu M. Mwinyi

Idara ya Uchapishaji

Ndugu F.F. Mpoyola

Idara ya Uchapishaji

Aidha, warsha hiyo ilihudhuriwa na wataalamu wawili kutoka kwenye mashirika ya uchapishaji:

Ndugu E. Lema

Shirika la Uchapishaji la Tanzania (T.P.H.), D’Salaam

NduguJ.M.K. Mallya

Shirika la Uchapishaji la Chuo Kikuu cha D’Salaam (D.U.P.)

BARAZA linachukua nafasi hii kuwashukuru hawa pamoja na wengine ambao hawakutajwa hapa kwa ajili ya mchango wao mkubwa walioutoa wa hali na mali katika kufanikisha utoaji wa kitabu hiki muhimu. BAKITA linatoa shukrani maalumu kwa Prof. E. Kezilahabi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kazi nzuri aliyoifanya ya uhariri wa awali. Kadhalika, BAKITA linatoa shukrani kama hizo kwa Ndugu S.A. Mapunda wa Idara ya Istilahi na Kamusi ya BAKITA kwa kufanya uhariri wa mwisho wa kitabu hiki. Shukrani nyingine za pekee ziwaendee Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) na Shirika la Uchapishaji la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUP) kwa mchango wao katika kugharimia uchapaji wa kitabu hiki. Ni matumaini ya BAKITA kwamba kitabu hiki kitakuwa msaada mkubwa kwa wote watakaokisoma. Aidha, wao pia watakuwa wajumbe wa kukieneza Kiswahili.

Tujivunie Kiswahili

Prof. G.A. Mhina
MWENYEKITI

SEHEMU YA KWANZA

Matumizi ya Herufi Kubwa, Vituo na Tarakimu

Matumizi ya herufi kubwa

Herufi kubwa zitatumika kwa usahihi katika mazingira yafuatayo:

1. Wakati wa kuandika herufi ya kwanza ya neno la kwanza la sentensi. Neno hili laweza kuwa la kwanza katika sentensi ya kwanza ya habari au aya au pia baada ya mojawapo ya vituo vikuu vya uandishi vifuatavyo: nukta, kiulizo, mshangao, alama za mnukuo na nuktapacha.

2. Wakati wa kuandika herufi ya kwanza ya majina yafuatayo:

· Majina ya watu, mji, nchi, bara, n.k.
Mifano: Siwema, Dodoma, Tanzania, Afrika.

· Majina ya pande za dira.
Mifano: Kaskazini, Kusini, Mashariki, Maagharibi, Kusini Mashariki.

· Majina ya vyeo au heshima.
Mifano: Sheikh Mkuu, Rais, Diwani, Meya, Jiji, Kamati Kuu

· Majina au sifa zinazoandamana na majina ya pekee.
Mifano: Ziwa Nyasa, Bahari ya Hindi.

· Neno lolote litakapopewa hadhi ya pekee.
Mifano: Chama (haya ni malengo ya Chama), Vita vya Majimaji, Ukuta Mkuu, Njaa Kuu.

· Sifa itokanayo na jina la pekee.
Mifano: Mtanzania, Mwafrika, Mchina, Mkenya, Mwingereza, Mmarekani, Mjerumani.

· Finyazo kama vile za vyama, mashirika, jumuia, n.k.
Mifano: UNO, OAU, TANESCO, BAKITA, UWAVITA.

· Majina ya siku na miezi.
Mifano: Jumatatu, Februari, Mfunguo Mosi.

· Majina ya vitabu na mada.
Mifano: Kiu, Mashetani, Diwani ya Mnyampala, “Uhuru wa Mwandishi”.

· Majina ya sayari.
Mifano: Pluto, Zuhura, Zebaki.

· Majina ya Sikukuu.
Mifano: Iddi Kubwa, Muungano, Pasaka, Krisimasi.

· Majina ya nafsi yatakapotumika kuleta maana maalumu.
Mifano: Mpaji ni Yeye (Mungu)

Matumizi ya vituo mbalimbali

Vituo mbalimbali vya uandishi vitatumika kwa usahihi kama ifuatavyo:

Nukta (·)

Kituo cha nukta kitatumika kama ifuatavyo:

· Mwishoni mwa neno, tungo au kifungu chenye kuleta maana kamili.
Mfano: Tulipofika, tulimwona.

· Wakati wa kuandika herufi za vifupisho.
Mifano: N.B., A.D., B.Sc., Ph.D., k.v., k.m.

· Wakati wa kuandika ili kutenga kiasi cha fedha, vipimo mbalimbali vya desimali, na pia kutenga saa na dakika.
Mifano: shillingi 82.55, saa 12.15, kilogramu 2.73.

Matumizi ya nukta katika mazingira ya vituo vingine

Kituo cha nukta kitaandikwa NDANI ya vituo vingine iwapo kitatumika katika mazingira yafuatayo:

· Endapo alama za mnukuo zitakuwa zimetumiwa kuonyesha sentensi au maneno yanayounda maana kamili.
Mfano: alisema “Nitahudhuria tafrija hiyo.”

· Endapo mabano yatakuwa yametumiwa kufunga kifungu cha maneno kinachojitosheleza kwa maana.
Mfano: (Mambo haya tumekwishayaeleza hapo awali.)

Kituo cha nukta kitaandikwa NJE ya alama za mnukuo na mabano endapo vituo hivyo vitakuwa vimetumika kufungia vifungu vya maneno ambavyo havileti maana kamili vikitazamwa kama vilivyo.

Mifano:

a) Wajibu wa kulinda taifa ni wa kila mwananchi (hasa mzalendo).
b) Polisemia kwa mujibu wa Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha ya TUKI (1990) ni “hali ya neno au kikundi cha maneno kuwa na maana zaidi ya moja”.

Zingatia: Nukta isitumike mwishoni mwa mada au vipengee vilivyoorodheshwa.

Mfano: Katika kipindi kijacho tutajadili mada zifuatazo:

a) Ufugaji
b) Ukulima
c) Kisomo chenye manufaa

Nuktapacha (:)

Kituo cha nuktapacha kitatumika kama ifuatavyo:

· Baada ya neno au kifungu cha maneno kinachofuatwa na maelezo au ufafanuzi zaidi. Hali hii hasa hujitokeza kwa kutaka kutaja idadi au maelezo yaliyopangiliwa hatua kwa hatua.
Mifano: Alipofika sokoni alijipatia mahitaji yafuatayo: nyanya, vitunguu, nyama na matunda; Ili kufika huko, fuata njia ifuatayo: pita kushoto, vuka mto, na pinda kulia.

· Katika kukamilisha jina la mada au sura.
Mifano: “Mashujaa wa Tanzania: Mkwawa wa Uhehe”; “Lugha ya Kiswahili: Chimbuko lake”

· Baada ya kuandika jina la mhusika katika tamthiliya.
Mfano: JUMA: Unatoka wapi?; MUKI: Popote tu!

· Wakati wa kutenganisha tarakimu katika mazingira yafuatayo:

a) Kutenganisha sura na aya, hasa katika Maandiko Matakatifu.
Mifano: AL – MAIDA: 96 – 100; LUK. 7: 10-18

b) Kutenganisha dakika na sekunde.
Mfano: Saa 2.24:05

· Kuonyesha dhana ya uwiano baina ya nambari.
Mifano: 3:5 7:11

· Kuonyesha sababu ya tendo au tukio.
Mfano: Maisha ya mjini yalimshinda: mshahara wake ulikuwa mdogo sana.

Zingatia:

Nuktapacha zaweza kufuatwa na deshi (kistari kirefu) hasa kabla ya kutaja mambo yanayokusudiwa kuorodheshwa.

Mfano: Jarida la Kiswahili hushughulikia nyanza zifuatazo:-

(i) Isimu

(ii) Leskografia

(iii) Fasihi

(iv) Mashairi

(v) Mapitio ya vitabu

Mkato (,)

Kituo cha mkato kitatumika kama ifuatavyo:

· Kutenga vifungu vya maneno au sentensi tegemezi kutoka kifungu kikuu, ili maana ya sentensi nzima ieleweke vema na kwa urahisi zaidi.

Mifano:

– Ukitaka kukarimiwa, jifunze kuwa mkarimu
– Si lazima sheria zote zifuatwe, ingawa kusudi ni kuzifuata, ili ushirikiano wetu udumu.
– Nyumba ya Ibrahimu, uliyotaka kununua mwaka jana, imeungua moto.

· Wakati wa kuorodhesha mambo, hasa kama yako katika mfululizo wa sentensi na hivyo hayakupangwa hima.
Mfano: Huko sokoni nilinunua: samaki, ndizi, matunda, na mboga.

· Kuonyesha vyeo, anwani au maskani baada ya jina la mtajwa.
Mifano: Juma Bakari, Meya wa Jiji, Dar es Salaam. Musa Mgombeki, S.L.P. 51, Ujiji, Tanzania.

· Kuondoa utata katika maana ya sentensi.

Mifano:

(i) Aliwaona: Juma Shaaban, John Mkali, na Asha Athumani
Aliwaona: Juma, Shaaban, John, Mkali, na Asha Athumani.

(ii) Wageni wale, chakula chao kizuri.
Wageni, wale chakula chao kizuri.

(iii) Hawakushikwa kwa bahati mbaya.
Hawakushikwa, kwa bahati mbaya.

· Baada ya vina vya kati na vya mwisho katika uandishi wa mashairi.

Mfano:

Raha ya kweli kinaya, kukinai yako hali,
Ukaepuka mabaya, na mema ukayajali,
Kisha usione maya, utosheke na akali,
Ya upatacho halali, ndipo utaona raha.
(Amri Abedi)

Baadhi ya washairi hawaweki mkato mwishoni mwa kina cha mwisho.

Dunia ukiihisi, mwenendo inayokwenda
Yaenda kama msasi, mawindoni akiwanda
Khususa kwa wadinasi, haikawi kutenda
Ina ladha na utesi, huthubutu kuishinda
Ukiona yakupenda, dunia uiogope
(Khamis Amani Nyamaume)

· Baada ya kutumia maneno ya jumla ili kufupisha kazi ya kuendelea kuorodhesha au kutaja mambo.

Mifano:

– Na kadhalika, na mengineyo
– Waliwapigia kura madiwani, meya, n.k., kabla ya kumpigia kura Rais.

· Badala ya kurudiarudia neno katika sentensi.
Mfano: Watoto mchana hucheza sana; usiku, hulala na asubuhi, huamka mapema.

Hapa neno watoto ambalo lingerudiwarudiwa limewakilishwa na mkato.

Mshangao (!)

Kituo cha mshangao kitatumika kama ifuatavyo:

· Baada ya neno au usemi wa kushangaa au kushtuka.

Mifano:

– Kumbe alikuwa mwizi wa siku nyingi!
– Lo! Maskini mjomba wangu!

· Wakati wa kusisitiza mshangao, kero, kuita, kubeza, kukanusha au kuamuru.

Mifano:

– Hii ni kweli!
– Ondokeni hapa! La! Sikwenda
– Mwone alivyo!
– Njoo!
– Alikuwa mweupe pee!
– Alitembea ng’wanyu! ng’wanyu!

· Kuonyesha uchungu, huzuni au majonzi.

Mifano:

– Mama yoo! Mama yoo maskini! (Amri Abedi)
– Hae! Msiba mzito amefishwa shaaban (Amiri Andanenga)
– Ai! Ulimwengu jifu njileo vumbivumbi (Muyaka)

Kiulizo (?)

Kiulizo, au alama ya kuuliza, kitatumika kama ifuatavyo:

· Kuonyesha neno au sentensi iliyokusudiwa kuwa swali.

Mifano:

– Sawa? Kweli? Ndivyo?
– Je, tuondoke lini?

Ili kuzingatia matumizi sahihi, kiulizo kiwekwe mwishoni mwa sentensi na si baada ya neno Je. Mkato unaweza kuwekwa baada ya Je. Pia Je yaweza ikawekwa mwishoni mwa neno au usemi unaokusudiwa kuwa swali.

Mifano:

– Je, hujambo?
– Unasemaje? Ulikujaje?

· Kuonyesha hali ya kutokuwa na hakika yaani swali lililochanganyika na mshangao.

Mifano:

– Sukari imepanda bei tena?
– kweli hukuwako?

Zingatia:

Hali hii ya kutokuwa na hakika yaweza kuonyeshwa kwa kutumia mshangao (!). Kamwe zisitumike zote mbili kwa wakati mmoja.

Mfano: *Kweli?!

* alama ya nyota kabla ya neno/sentensi inaonyesha kuwa neno/sentensi inayohusika ina ila ya kisarufi.

Matumizi ya Kiulizo katika mazingira ya vituo vingine

Kiulizo kitatumika na mnukuo (alama za usemi) kama ifuatavyo:

a) Kiulizo kitaandikwa NDANI ya mnukuo iwapo maneno yaliyokaririwa yanajitosheleza katika maana na hayakaririwi na mtumiaji au msemaji mwingine.
Mfano:Baba alimwuliza mtoto wake,“Je, ulikwenda shule leo?”

b) Kiulizo kitandikwa NJE ya mnukuo iwapo maneno yaliyokaririwa yakikaririwa tena na mtumiaji au msemaji wa pili kwa lengo la kusisitiza au kuyatafakari zaidi.

Mifano:

– Hebu tueleze una maana gani kusema “Mimi ni sheria na sheria ni mimi”?
– Je, sote tunakubaliana na wazo hili la “Uhuru wa mwanamke”?

Mabano (·)

Kituo cha mabano kitatumika kama ifuatavyo:

· Kuhifadhi usemi, taarifa au maelezo ya nyongeza katika sentensi. Nyongeza yaweza kuwa bezo, mshangao au msisitizo wa mwandishi.

Mifano:

– Nchi yetu (yaani Tanzania) ina utajiri mwingi wa maliasili.
– Yuleyule muuaji (ni ajabu na kweli!) alipandishwa cheo.

· Kutoa maelekezo ya mwandishi hasa katika tamthilia.

Mfano: JUMA: (Huku akipaza sauti na kutupa mikono) sitaki kwenda!

· Kuonyesha fikira za ndani za mwandishi au msemaji wakati anapokuwa anaandika au anasema yanayoifikia hadhira yake.

Mfano: Mkutano ulipofunguliwa akasema “Wananchi, (laiti wangejua nia yake hasa, wasingemshangilia) kwa heshima zote nahitaji kura zenu zote!”

Wakati wa kutumia kituo hiki yafaa pia kuzingatia yafuatayo:

a) Alama ya deshi huweza kutumika badala ya Mabano. Tofauti ni kwamba Mabano hutumika zaidi katika maelezo ya ziada yanayohusiana sana na sentensi kuu, ambapo deshi hutumika kwa maelezo yasiyohusiana sana na sentensi hiyo kuu.

Mifano:

– Tutakuja sote (mimi, mke wangu na watoto wetu wanne) kesho asubuhi.
– Inawezekana – na pengine yaweza ikawa lazima – tutoe amri kwa wakulima wa sehemu fulani kulima eka kadha wa kadha za zao fulani la chakula ili kuzuia njaa.

b) Iwapo itabidi kutumia mabano kuhifadhi tena taarifa nyingine mbali ya ile iliyowekwa katika mabano tayari, italazimu kutumia mabano ya msitatili kwa ajili ya hiyo taarifa ya pili.

Mfano: Mkewe (aliyemzalia mtoto mmoja tu [naye kafa bado mchanga] wa kiume) alifarikijana usiku.

Zingatia: Kwa kuwa Mabano huweza kuondolewa na maana ya sentensi ikabaki ileile, ni muhimu kuzingatia kwamba Mabano yatumike pale tu inapolazimu.

Mnukuo (“ “)

Mnukuo, au Alama za usemi, utatumika kama ifuatavyo:

· Zitatumika alama mbilimbili mwanzoni na mwishoni mwa usemi ulionukuliwa au kukaririwa.
Mfano: Mwalimu alisema, “Wanafunzi wazembe ni sumu kwa shule yetu.”

· Zitatumika alama mbilimbili mwanzoni na mwishoni mwa usemi, neno au maneno maalumu au jina la kupanga.
Mfano: Kampuni ilifilisika baada ya yule “kizito” wao kuhama.

· Zitatumika alama mbilimbili wakati wa majibizano au mazungumzo baina ya wasemaji wawili.

Mfano:

“Wewe Kocho unanijibu mimi maneno hayo leo!”

“Kama unaweza nifumbe mdomo wangu.”

“Wewe uliyezowea kunita mimi bwana, leo …”

“Mabwana zaidi kuliko wewe sisi tuliwaondoa … na penye haki sioni uzito kukwitajina lolote unalostahili. Na ujuwe kuwa wakati utafika pia wanawake kuonekana watu, ala!”

(Utengano: S.A. Mohamed)

· Zitatumika alama mojamoja wakati wa kuonyesha usemi uliokaririwa au kunukuliwa katika usemi mwingine uliokaririwa au kunukuliwa pia.

Mfano: Juma alisema, “Musa alisema, ‘nitakwenda leo’.”

Zingatia:

a) Katika mazingira ya kunukuu katika usemi mwingine, vituo vitatumika na kuandikwa mwishoni mwa sentensi kama ifuatavyo:

i) Alama moja ya Mnukuo ya kufunga usemi uliokaririwa ndani ya usemi mwingine.
ii) Nukta kuonyesha mwisho wa sentensi au usemi.
iii) Alama mbili za Mnukuo za kufunga semi zote mbili zilizokaririwa.

(Tazama mfano uliotolewa hapo juu kudhihirisha hali hii).

b) Katika kazi za nathari na ushairi, iwapo maneno yanayonukuliwa ni zaidi ya mistari mitatu, basi maneno hayo hayalazimiki kuwekwa katika mnukuo mradi tu (katika kazi za nathari) mstari mpya uanze kwa kuingizwa ndani kama ifanyikavyo wakati wa kuanza kuandika paragrafu mpya.

Mfano:

Alhaji Karimu alikuwa wa asili ya Kingazija.
Alitokea Moroni, kisiwa cha Grande Comoro miaka mingi iliyopita, kabla ya kuoa mke wake wa kwanza

(Harusi: A.J. Saffari)

Kwa nini kwao kwa nini, kuwa kwetu kwa nini?
Na kwetu pia kwa nini, kuitwa kwao kwa nini?
Kwa nini ina yakini, kwetu ni kwao kwa nini?
Kwetu ni kwao kwa nini, na kwao kwetu kwa nini?
(Mashairi ya Saadani: S. Kandoro).

Deshi (—)

Kituo cha deshi, pia huitwa kistari kirefu, kitatumika kwa usahihi kama ifuatavyo:

· Kama kitumikavyo kituo cha mabano, kituo cha deshi hutumika ili kuongeza taarifa au maelezo mengine yahusuyo usemi, neno au sentensi iliyotangulia. Kwa kawaida deshi mbili hutumika, yaani mwanzoni na mwishoni mwa maelezo ya nyongeza, iwapo maelezo hayo yapo katikati ya sentensi.

Mifano:

– Nchi yetu  yaani Tanzania  ina utajiri mwingi wa mali asili.
– Alipoingia nyumbani akajitupa kitandani  kumbe mlango uko wazi.

· Badala ya nuktapacha katika mazungumzo hasa mahojiano.

Mfano:

MHOJAJI  Kwa nini ulianza kuandika? Jambo gani lilikusukumauanze kuandika?
MHOJIWA  Maisha yenyewe pamoja na vitabu vya waandishi wengine niliowasoma.

· Badala ya nuktapacha kama alama ya kuorodhesha mambo.

Mfano:

Nilinunua  samaki, ndizi, viazi, n.k.
badala ya: Nilinunua: samaki, ndizi, viazi, n.k.

· Kuonyeshajina la mwandishi au msemaji ambaye usemi, dondoo au kitabu chake kimekaririwa. Deshi itaandikwa mbele ya jina la mhusika.

Mfano:

“Ukiwa na fedha utajuta, ukiwa huna utajuta. Cha nini kitu kama hiki!”
(Utubora Mkulima – Shaaban Robert)

· Kuonyesha maneno yaliyosemwa lakini hayakukamilika. Mathalani katika mahojiano, maelezo n.k. katika mazungumzo.

Mfano:

MHOJAJI

– Unafikiri baa la njaa litakwisha Afrika?

RAIS

– Ninaweza kusema  kama nilivyo-kwishaeleza  ndiyo na hapana  sijui. Hapana, kama nchi zilizoendelea zitazidi kuinyonya Afrika. Ndiyo, kama nchi za Kiafrika zenyewe zitakataa kunyonywa.

· Badala ya mkato katika kuonyesha taarifa au maelezo ya nyongeza katika sentensi.

Mfano: – Si lazima sheria zote zifuatwe, ingawa ndilo kusudi la kuzitunga, ili kudumisha ushirikiano wetu.

Kuwa – Si lazima sheria zote zifuatwe  ingawa ndilo kusudi la kuzitunga — ili kudumisha ushirikiano wetu.

· Baada ya kuorodhesha mambo kadhaa ambayo hufuatwa na, maelezo ya nyongeza.
Mfano: Njaa, vifo, vita, ubaguzi wa rangi – yote haya yanadhihirisha kuwa ulimwengu ni mgumu.

· Katika kuonyesha mkazo katika usemi.
Mfano: Jambo moja lazima likumbukwe – sote tutakufa.

Zingatia: Katika mahojiano, deshi inapotumika alama za mnukuo hazitumiki.

Kiungo (-)

Kituo hiki pia huitwa kistari kifupi au kistariungio hasa kukitofautisha na deshi ambayo pia hujulikana kama kistari kirefu.

Kiungio kitatumika kwa usahihi kama ifuatavyo:

· Wakati wa kukata neno, hasa kwenye ukingo wa kulia wa karatasi, kutokana na kukosekana nafasi ya kuliandika zima.

(Maelezo zaidi juu ya suala hili yametolewa chini ya kichwa cha “Ukataji wa Maneno” uk.26)

· Wakati wa kuonyesha kipindi, umbali, au muhula baina ya nyakati mbili. Katika mazingira haya kiungio hutumika badala ya maneno “hadi” au “mpaka”.

Mifano:

Mwaka 1914 – 1918
Kurasa 5 – 17.

· Wakati wa kupanga au kuorodhesha vipengele au mawazo makuu kwa muhtasari. Kiungio huwekwa mwanzoni mwa kila sentensi.

Mifano:

Mwaka ujao tutafanya yafuatayo:

– kulima pamba
– kufuga kuku
– kujenga zahanati ya kijiji
– kujenga shule.

Apostrofi (‘) Kituo hiki kitatumika kwa usahihi kama ifuatavyo:

· Kuonyesha matamshi ya king’ong’o.
Mifano: ng’ombe, ng’ambo, mgong’oto, ng’ang’ania, mkong’oto, n.k.

· Kuonyesha nafasi ya herufi au tarakimu iliyoachwa.

Mifano:

‘79 = 1979
N’sharudi = nimekwisharudi.

Nuktakatishi (…)

Kwa kawaida kituo hiki hutumia nukta tatu au zaidi zenye kufuatana. Kituo hiki huonyesha dukuduku la usemi uliokatishwa na zitatumika kwa usemi uliokatishwa lakini unaojulikana kwa wengi; mathalan methali, nahau, kibwagizo, n.k.

Mfano: Mtoto wa nyoka …. (Methali).

· Kuonyesha maelezo, mazungumzo, n.k. yaliyochanganyika na hali ya kuvuta maneno au kuvuta subira katika tabia ya msemaji.

Mifano:

– Mu … mu … mukinipacha … chakula nitasema (kigugumizi)
– Mara mwanzishaji akasikika: Tayari… moja … mbili… tatu …! (Mashindano ya mbio).

· Kuonyesha kwamba kuna maneno yaliyotangulia au yanayoendelea licha ya haya yaliyokaririwa.

Mfano:

… Wadhalimu na wajanja ndio wanaoendewa sawa na wao; watu waaminifu na wanyonge utawaona daima wako chini.
… wajumbe wote wataanza majadiliano mara baada ya kufungua mkutano…

Nuktamkato (;)

Kituo hiki kitatumika kwa usahihi kama ifuatavyo:

· Kuunga mawazo mawili mbalimbali katika sentensi ambatano zilizotumika.
Mfano: Sisi si panya; wao si paka.

· Kutenga vifungu vya sentensi ambatano moja ambayo ni ndefu mno na ambayo kwa kutumia kituo cha Mkato peke yake maana yake bado isingeeleweka kwa urahisi.
Mfano: Huku akihakikisha kwamba haonekani, alikwenda pale mlangoni; akaufungua polepole.

· Kabla ya maneno kama: Baadaye, halafu, basi, hivyo, kwa hiyo, ndipo, n.k. iwapo maneno hayo yanaunganisha sentensi ndefu.
Mfano: Tulilima asubuhi na mchana kutwa bila kuwaona viongozi wa kijiji shambani; baadaye, tuliamua kuwafuata nyumbani; ndipo, tulipowaeleza ukweli.

Kinyota (*)

Kinyota, ambacho pia hujulikana kama Asteriki, ni kituo ambacho kitatumika kwa usahihi kama ifuatavyo:

· Kuonyesha kuwa neno lililotiliwa alama hiyo limepewa maelezo zaidi. (Tazama “Uandikaji wa Fafanuzi”). Alama hii itawekwa baada ya herufi ya mwisho ya neno linalohusika, kwa juu.
Mfano: Kimwaga* huyu!

· Kuonyesha maneno au maandishi ambayo yanakosekana, si kwa kukatisbwa, bali kwa kupotea au sababu nyingine.

Mfano:

“Sababu zifanyazo shairi liwe zuri au baya; hoja za wahakiki na majibu yahojahizo.***”

(Poetics – Aristotle)

(Hii ni sentensi ya mwisho ya kitabu cha Aristotle kinachohusu taaluma ya ushairi. Vinyota vyaonyesha kuwa maandishi yaliyofuata yalipotea. Mpaka leo hayajaonekana).

· Kuonyesha mambo ya undani au siri ambayo si vema kutajwa hadharani.
Mfano: Taa ilizimwa*** Harusi Haikujibu… (Katika matumizi haya kinyota hutumika kama nuktakatishi).

· Kudhihirisha uhusiano baina ya matukio kati ya sura moja na nyingine hasa katika mtindo wa uandishi wa riwaya wa kutumia kirejeshi (flashback).

Mfano:

Makusudi alikuwa kaganda hapa kama pande la barafu. Alikuwa akijaribu kuzizuia hamasa zake. Alihisi baridi kali, lakini kijasho chembamba kilimtoka. Nadhari yake ilianza kufanya kazi upesiupesi. Alijua la kufanya. Alitia uso matuta. Joto likampanda, damu ikamchemka. Alikuwa mtu mwingine sasa, tayari kwa lolote. Kishampandisha wa kwao. Alihonyeza kengele.

* * *

Kwa wakati huu, nyumbani mwa Makusudi umeshaingia mtafaruku wa kupotea Maimuna. Wasiwasi, hofu na wahka umemvaa kila mtu. Na wote hao si lolote kama mwenyewe mama mtu. Alikuwa karukwa na roho. (Utengano – S.A. Mohamed).

(Kabla ya vinyota tunamwona Bwana Makusudi akirejea nyumbani kwake. Baada ya vinyota tunaelezwa yaliyotokea nyumbani mwake wakati yeye hayupo).

Zingatia: Tarakimu au alama nyingine yoyote huweza kutumika badala ya kinyota kwa lengo hilohilo pia.

Matumizi ya tarakimu

Katika uandikaji, tarakimu au namba zitatumika kwa kufuata misingi ifuatayo:

Matumizi ya Jumla

Kwa kawaida tarakimu zitaandikwa badala ya maneno katika mazingira yafuatayo:

· Wakati idadi au namba mbili zitakapolinganishwa katika sentensi au kifungu kilekile cha habari.
Mifano: Katika kila watoto 100 wanaozaliwa duniani, 13 huzaliwa huko India.

· Wakati wa kutumia hesabu za vipimo.

Mifano:

– Hesabu za asilimia: 10% ya watanzania ni wafanyakazi wa kuajiriwa.
– Hesabu za desimali: Kilogramu 16.8 za sukari zimenunuliwa.
– Hesabu za sehemu: 3/10 ya watoto wetu hufa kwa surua kila mwaka.

· Wakati wa kuandika tarehe – yaani tarehe ya siku, mwezi na mwaka.
Mfano: 09.12.61 au 09/12/61 au 09-12-61.

Matumizi ya maneno badala ya tarakimu

Maneno yatatumika badala ya tarakimu katika mazingira yafuatayo:

· Katika kuonyesha idadi yoyote itakayotumia namba zilizo chini ya 100.

Mfano:

“Idadi ya watu duniani itafikia bilioni tano mwakani.”
Japokuwa 5,000,000,000 (bilioni tano) ni kubwa kuliko 100 katika wingi, tarakimu hiyo itaandikwa kwa maneno kwa kuwa idadi ya bilioni hizo ni tano tu ambayo haizidi 100.

· Katika kuonyesha jina la mwaka kikamilifu.
Mfano: “Tulikutana mara ya kwanza mwaka elfu moja mia tisa sabini na saba.”

· Wakati wa kuandika idadi ya kukadiria tu.
Mfano: Shule ina watoto wapatao mia saba hivi.

Matumizi ya tarakimu za Kirumi

Tarakimu za Kirumi zitatumika kwa usahihi kama ifuatavyo:

· Wakati wa kupambanua vyeo, hadhi au nasaba za wakuu.

Mfano:

Mfalme George wa VI
Mwami Ntare wa I
Rais wa XXXVI

· Wakati wa kupambanua sehemu kuu za jambo, makala au tukio ambazo kwazo vifungu au mfululizo wa matukio madogomadogo hufuata. Katika mazingira haya tarakimu za kirumi huonyesha mafungu, sehemu au sura; mathalan katika katiba, sheria, taarifa ya utafiti n.k.
Mfano: “Maidhinisho na sahihi” katika Katiba ya Umoja wa Mataifa sura ya XIX.

· Wakati wa kuandika kurasa za dibaji au utangulizi wa muswada au kitabu ili kuzipambanua kwa urahisi na zile za kisa chenyewe. Tarakimu ndogo za Kirumi zitatumika kwa kazi hii.

Mtumiaji anao uhuru wa kuziweka tarakimu hizo ndani ya mabano au la.

Mfano:

uk. iii au (iii)
uk. xiv au (xiv)

Matumizi ya tarakimu za Kiarabu

Tarakimu za Kiarabu zitatumika kwa usahihi kama ifuatavyo:

· Kupambanua vifungu au mada ndogondogo zinazojitokeza kutokana na fungu kuu au sehemu kuu ileile.
Mfano: Sehemu ya III, kifungu cha 33.4.

· Kuandika namba za kurasa za kisa au kazi yenyewe katika kitabu au muswada.

· Kuorodhesha kwa kawaida mambo yote yasiyohitaji kutumia herufi za Kirumi ili kupambanuliwa.

Zingatia: Katika makala ndefu au taarifa, ili kurahisisha upambanuzi wa sehemu na vifungu vyake, matumizi ya tarakimu za Kirumi na za Kiarabu na pia herufi za alfabeti hutumika kufuata daraja kama ifuatavyo:

I

1

a

(i)

Anza

II

halafu

2

ndipo

b

kisha

(ii)

III

3

c

(iii)

Uundaji na Uandikaji wa Maneno, Istilahi na Finyazo

Uendelezaji na ukataji wa maneno

Uendelezaji wa maneno

Uandikaji sahihi wa maneno utafuata misingi ifuatayo:

Tahijia sahihi kwa neno mojamoja:
Ili kuandika neno mojamoja uamuzi ufuatao utazingatiwa:

1. Uwakilishwaji sahihi wa sauti (fonimu) za Kiswahili. Herufi zifuatazo zitatumika kuwakilisha fonimu za Kiswahili kama ifuatavyo:

Fonimu

Itakavyowakilishwa

Mifano yake

q /

th

thamani, thelathini, n.k.

 I

dh

dhambi, dhidi, dhahabu, n.k.

g /

gh

ghala, lugha, gharama, n.k.

ò /

sh

shamba, mshale, n.k.

a /

ch

chunga, cheza, n.k.

p /

ng’

ng’ombe, ng’ambo

/ x /

h

hasara, hamsini, alhamisi, n.k.

h /

ny

nyanya, nyama, n.k.

Zingatia:

Fonimu /x/ itaandikwa “kh” wakati wa kuandika majina ya watu kadiri ya utashi wao.

Mifano: Khamis, Khalid, Khalfan, n.k.

2. Usawilishwaji wa irabu katika mazingira ya “mu-”: “mu-” itaandikwa kama “mw-” iwapo itafuatwa na irabu za “a”, “e”, “i” na “o”. Lakini “mu-” itaendelea kuandikwa kama “mu-” iwapo itafuatwa na irabu “u”.

Mifano:

Mu + aliko

mw

=

Mwaliko, mwalimu, mwali.

Mu + embe

mw

=

Mwembe, mwezi, mwehu.

Mu + izi

mw

=

Mwizi, mwiko, mwisho.

Mu + ongo

mw

=

Mwongo, mwombaji.

Mu + u

muu

=

Muumba, muuguzi, muungano.

3. Upachikaji wa “w” na “y” kati ya irabu mbili za mwishoni mwa neno:

Isipokuwa kama neno lilelile litaleta maana zaidi ya moja na ikusudiwe kwamba maana hizo zitofautishwe kwa urahisi, “w” au “y” hazitapachikwa kati ya irabu mbili za mwisho wa neno.

Mifano:

Uandikaji sahihi

Uandikaji usio sahihi

Mayai

Mayayi

Tembea

Tembeya

Zuia

Zuwiya/zuiya

Jumuia

Jumuiya

Tamthilia

Tamthiliya

Oa

Owa

Ua

Uwa

Zingatia:

Ua (sehemu ya mmea)

ua (uzio)

Kua (ongezeka kimo)

Kuwa (toka hali moja hadi nyingine).

Maneno yenye maana ileile yaandikwayo tofauti katika lahaja mbalimbali za Kiswahili.

Kwa lengo la kuzingatia Kiswahili sanifu maneno kadhaa yatumikayo katika lahaja mbalimbali za Kiswahili na kuandikwa tofauti, ingawa yana maana ileile, yataandikwa ifuatavyo:

Tahijia ya Kiswabili Sanifu
(uandikaji sahihi)

Tahijia ya lahaja nyingine
(uandikaji usio sahihi)

Dhoruba (upepo mkali)

Dharuba (Upepo mkali)

Heshima

Hishima

Methali

Mithali

Ishirini

Ashirini

Nasi

Naswi

Lakini

Ilakini/Lakin

Nyinyi Hesabu

Ninyi Hisabu

Merikebu/marikebu

Markeb

Hekima

Hikima

Tisini

Tisaini

Au/Lau

Ao/Lao

Hasa

Haswa

Nchi

Inchi

Sheria

Sharia

Ofisi

Afisi

Kadiri

Kadri

Sabini

Sabaini

Fikira/fikara

Fikra

Desturi

Dasturi

Muda

Mda

Hitilafu

Ikhitilafu

Tekinolojia

Teknolojia

Zingatia:

Endapo neno litakuwa na zaidi ya maana moja katika lahaja mbalimbali lakini linaandikwa kwa tahijia mbalimbali katika lahaja hizo, basi liandikwe kwa tahijia tofauti ili kurahisisha kutofautisha maana hizo.

Mfano: “harufu” huandikwa pia “herufi” katika lahaja mbalimbali. Pia laweza kuwa na maana ya “andiko” katika baadhi ya lahaja na “nmuko” katika lahaja nyingine. Hivyo, “harufu” litapewa maana moja tu ya “mnuko” na “herufi” litapewa maana ya “andiko” katika Kiswahili Sanifu.

Uzingatiaji wa tabla za lugha zenye asili ya Kibantu katika kuandika maneno yenye asili ya lugha za kigeni:

Kwa kuwa Kiswahili ni Kibantu, kwa kadiri iwezekanavyo maneno yenye asili ya lugha za kigeni yataandikwa kwa kuzingatia tabia za lugha za kibantu na hasa katika vipengele vifuatavyo:

· Neno lisiishie na konsonanti hata kama halitakuwa na matatizo katika utamkwaji wake.

Mifano:

Salamu, mtaalamu, taabu, maalumu, n.k.
Isipokuwa: “Rais” litaandikwa “Rais”.

· Mwambatano wa herufi mbili au zaidi za konsonanti uepukwe isipokuwa iwapo mwambatano huo unahusisha: m, n, sh, ch, y, w na konsonanati zenye asili ya maneno ya lugha za kigeni ambazo hazina matatizo ya utamkwaji, kama vile: st, sk, kt, n.k.
Mifano: mmomonyoko, mnong’ono, mnyonge, mnywaji, kichwa, lishwa, stakabadhi, trekta, hekta, stesheni, sketi, n.k.

Zingotia:

a) Baadhi ya maneno ambayo yamekwisha kukomaa kwa tahijia yanavyoandikwa yaendelee kutumia tahijia hiyo k.m. sharti, labda.

b) Urudiaji wa konsonanti au irabu ileile uepukwe isipokuwa tu ikiwa kwa kufanya hivyo neno litaleta maana tofauti.

Mifano:

“Bassi” liandikwe “Basi”
“Hatta” liandikwe “Hata”
“Illa” liandikwe “Ila”
“Burre” liandikwe “Bure”
“Boonde” liandikwe “Bonde”
“Paango” liandikwe “Pango”
“Muungu” liandikwe “Mungu”
“Maada” liandikwe “Mada”.

Uunganishaji wa maneno:

Kwa kuwa uendelezaji wa neno utazingatia sana maana ya neno litakaloandikwa, maneno mawili (au zaidi) yataandikwa kama neno moja katika mazingira yafuatayo:

· Neno litakapoandikwa kwa kurudiwarudiwa.
Mifano: mbalimbali, ndogondogo, mojamoja, kupigapiga, n.k.

· Kitenzi au kifungutenzi chenye mofimu au kiambishi cha urejeshi.

Mifano: Utakalotenda, aliyeondoka, atakapokuona. Pia maneno yote yenye kutumia Kivumishi cha pekee cha urejeshi -o -ote.

Mifano: yeyote, wowote, lolote, n.k.

· Maneno mawili yenye maana tofauti yatakapounda maana moja mpya yakitumika pamoja.

Mifano:

Mwana

+ Siasa

= Mwanasiasa

Mfanya

+ Kazi

= Mfanyakazi

Embe

+ Mafuta

= Embemafuta

Kibiriti

+ Ngoma

= Kibiritingoma.

Zingatia:

Katika fungu hili pia yataingia baadhi ya maneno yatakayoambatana na Kivumishi cha pekee mwenye 

Mifano: Mwenyekiti, Mwenyezi.

Ukataji wa maneno

Misingi ifuatayo itatumika katika kukata neno ambalo halitaweza kuandikwa kamili kutokana na upungufu wa nafasi:

1. Neno lenye asili ya lugha za Kibantu litakatwa kufuatana na silabi zitakazoliunda. Kwa kuwa silabi katika lugha za kibantu huishia na irabu basi herufi ya mwisho ya neno litakalokatwa itakuwa haina budi iwe irabu.

Kwa mfano:

Neno

Ukataji sahihi

Ukataji usio sahihi

Maneno

Ma-ne-no

Man-en-o, manen-o

Kukata

Ku-ka-ta

kuk-at-a, kukat-a

Ng’ombe

Ng’o-mbe

Ng’-ombe, Ng’om-be

Nyumba

Nyu-mba

Ny-umb-a, Nyum-ba

Mnong’ono

M-no-ng’o-no

Mn-ong’-on-o, Mnong’-ono

Kukimbia

Ku-ki-mbi-a

Kuk-im-bia, kukim-bia

· Kwa maneno yenye asili ya lugha za kigeni ukataji wa neno utazingatia zaidi urahisi wa kutamka silabi kuliko irabu mwishoni mwa neno au silabi. Kwa sababu hii neno lenye asili ya lugha ya kigeni litakatwa mwisho wa silabi hata kama silabi hiyo haitaishia na irabu.

Mifano:

Labda

Lab-da

Alfajiri

Al-fa-ji-ri

Maktaba

Mak-ta-ba

Kortini

Kor-ti-ni

Ustaarabu

U-sta-a-ra-bu

Stakabadhi

Sta-ka-ba-dhi

Stesheni

Ste-she-ni

Zingatia: Neno halitagawanyika litakapokuwa katika mazingira yafuatayo:

– Neno lenye silabi moja.
Mifano: na, ni, si, ya, cha, wa, n.k.

– Neno ambalo ni finyazo ya maneno mengine.
Mifano: OAU, CELTA, UNO, UNESCO, n.k.

– Jina la mtu
Mifano: Juma, Maganga, Manje, n.k.

– Tarakimu, nambari au idadi.
Mifano: 6, IV, 20, 40, 100, n.k.

Uundaji na uandikaji wa istilahi sanifu

Uundaji wa istilahi

Kwa kuwa chanzo kikubwa cha istilahi kitakuwa ni kupata visawe vya istilahi za Kingereza za nyanja mbalimbali, basi istilahi (maneno maalumu kwa shughuli maalumu) za Kiswahili sanifu zitaundwa kwa kutumia mbinu zifuatazo ambazo zimepangwa kulingana na mfuatano jinsi zitakavyokuwa zikitumika:

1. Kutafuta maneno yaliyo katika lugha ya Kiswahili chenyewe – yaani Kiswahili sanifu na lahaja nyingine za Kiswahili.

2. Kutafuta na kutohoa maneno yenye dhana inayokusudiwa kutoka lugha za Kiafrika zenye asili ya kibantu.

Mifano:

Sinovial fluid

= Giligili (Kinyakyusa)

Bone – marrow

= Uloto (Kizaramo)

Faculty

= Kitivo (Kipare)

Landslide

= Ngoko (Kichagga)

State House

= Ikulu (Kinyamwezi)

Parliament

= Bunge (Kiganda) Bulange

Soil texture

= Unamu (Kigogo) n.k.

3. Kutafuta na kutohoa maneno yenye dhana inayokusudiwa kutoka lugha nyingine za Kiafrika zisizo za asili ya Kibantu.

Mifano:

Duodenum

= Mbuti (Kimasai)

Lung fish

= Kamongo (Kijaluo)

Blank verse

= Sukui (Kisusu – Guinea)

Griot

= Yeli (Kimaninka – Guinea)

Ballad

= Rala (Kiyoruba – Nigeria)

Kola nut

= Kola (Lugha za Afrika Magharibi).

4. Kutohoa maneno ya lugha za kigeni:

Mifano:

Carbohydrate

= Kabohaidreti

Quarantine

= Karantini

Tractor

= Trekta

Campaign

= Kampeni

Maktab

= Maktaba

Fasih

= Pasihi

Ism

= Isimu

Vinho

= Mvinyo

Television

= Televisheni.

5. Kuunganisha vipashio vya maneno, hasa maneno ya Kiswahili.

Mifano:

Mnyama mfu

= Nyamafu

Mkato kama tao

= Mkatotao

Delta kama tao

= Deltao

Chakula chajioni

= Chajio

Mtu asiye na kwao

= Msikwao.

Wakati mwingine maneno mazimamazima yataungwa kuunda istilahi.

Mifano:

Ghala

+

Banda

= Ghalabanda

Jiwe

+

Sabuni

= Jiwesabuni

Kipaza

+

Sauti

= Kipazasauti

Kani

+

Eneo

= Kanieneo n.k.

Uandikaji wa istilahi

Misingi ifuatayo itazingatiwa wakati wa kuandika istilahi sanifu:

1. Istilahi itaandikwa kama neno moja katika mazingira yafuatayo:

· Iwapo maneno mawili au zaidi mbalimbali yanapoungwa yataunda maana mpya moja.

Mifano:

Umbo

+

punje

= Umbopunje

Sukari

+

tata

= Sukaritata

Ngozi

+

nje

= Ngozinje

Kani

+

eneo

= Kanieneo

Kitega

+

Uchumi

= Kitegauchumi.

· Iwapo istilahi iliyoundwa itatokana na kuunganisha vipashio vya maneno mbalimbali. Mifano: Deltao Chajio Msikwao n.k.

2. Istilahi itaandikwa kama maneno mawili yaliyotengwa katika mazingira yafuatayo:

· Iwapo maneno yanayoiunda istilahi ni zaidi ya mawili na iwapo yataunganishwa, istilahi itapoteza uangavu wake.
Mifano: Kipima pembe ubapa = Kipimapembe ubapa.

· Iwapo istilahi inayotumika inaelekea zaidi kuwa maelezo kwa sababu ya kukosekana neno moja fupi.

Mifano:

Bata mchanga

= Duckling

Simba jike

= Lioness

Hundi iliyochina

= Stale cheque

Utembo mrefu

= Filament.

Uundaji na uandikaji wa finyazo

Uundaji wa finyazo

Finyazo za maneno ya Kiswahili zitaundwa kwa usahihi kwa kuzingatia misingi mikuu ifuatayo:

1. Usahihi wa mpangilio wa maneno yatakayounda finyazo. Maneno hayo yatakuwa hayana budi yapangwe katika mfuatano ufuatao:

– Jina, Jambo, Tukio.
– Shughuli ifanywayo na Jina, Jambo au Tukio lililotajwa katika finyazo.
– Mwenye kutawala, kumiliki au kuendesha shughuli hiyo.

Kutokana na msingi huo finyazo zifuatazo ni sahihi:

Kampuni ya Mabasi ya Taifa

= KAMATA

Kiwanda cha Uchapaji cha Taifa

= KIUTA

Shirika la Vyama la Taifa

= SHIVYUTA

Shirika la Habari la Tanzania

= SHIHATA

Baraza la Kiswahili la Taifa

= BAKITA

Benki ya Maendeleo

= BEMA

Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania

= UWAVITA n.k.

2. Urahisi wa kutamka finyazo kufuatana na tabia na muundo wa lugha ya Kiswahili. Ili kurahisisha utamkaji wa finyazo zitakazotokana na maneno ya Kiswahili yaliyofupishwa, finyazo zisiundwe kwa mfuatano wa herufi za konsonanti ambazo hazitamkiki kwa urahisi katika Kiswahili. Ili kuzingatia tabia ya matamshi ya Kiswahili, finyazo itaundwa kwa kutumia silabi badala ya kuchukua herufi kubwa za mwanzo wa neno tu.

Mifano:

Shirika la Habari la Tanzania: lifupishwa kama SHIHATA badala ya SHT.

Usafiri Dar es Salaam: lifupishwe kama UDA badala ya UD.

Baraza la Muziki la Tanzania: lifupishwe kama BAMUTA badala ya BMT.

Wakati mwingine ili kurahisisha utamkaji wa finyazo baadhi ya silabi zaweza kudondoshwa na herufi moja tu kubakia mradi kwa kufanya hivyo finyazo bado itatamkwa kwa urahisi.

Mifano:

Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili = TUKI badala ya TAUKI.

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania = BAKWATA badala ya BAKUWATA.

Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania = UKUTA badala ya UKIUTA.

3. Uteuzi wa neno moja muhimu na kulitumia kama finyazo.

Mifano:

Chama cha Wafasiri Tanzania

= WAFASIRI

Jumuia ya wazazi Tanzania

= WAZAZI

Umoja wa Vijana

= VUANA

Muungano wa Vyama vya Ushirika

= USHIRIKA

Zingatia: Zipo finyazo zilizoundwa kwa kuteua herufi za mwanzo tu za maneno yaliyoziunda.

Mifano:

Chama cha Mapinduzi – CCM
Umoja wa Wanawake Tanzania – UWT

· Mashirika, Vyama na jumuia vinashauriwa kuhakikisha kuwa fmyazo zao hazifanani. Mbinu mbalimbali zilizoorodheshwa zitumike kuepusha tatizo hili.

Uandikaji wa finyazo

Finyazo zitaandikwa kwa herufi kubwa zote kama ifuatavyo:

Finyazo zitaundwa kutokana na maelekezo yaliyotolewa katika kifungu kinachohusu uundaji wa finyazo hapo juu, na herufi zake zote zitaandikwa kwa herufi kubwa.

Mifano:

Kampuni ya Usafirishaji Dodoma

= KAUDO

Shirika la Habari la Tanzania

= SHIHATA

Finyazo hazitalazimika kuwekewa alama ya nukta baada ya kila herufi.

SEHEMU YA TATU

Vipengele Kuhusu Ufasaha wa Lugha

Baraza la Kiswahili la Taifa linasimamia matumizi fasaha ya Kiswahili sanifu. Ili kutekeleza suala hili, misingi ifuatayo, pamoja na mingine itakayoonekana inaweza kusaidia utekelezaji huu, itazingatiwa.

Vipengele vya kisarufi

Upatanishi wa kisarufi

Mara nyingi kuna mgogoro wa kisarufi, na hivyo kupotosha ufasaha, kutokana na majina au viambishi vya ngeli zake kutopatana na jinsi ya kuvihusisha katika matumizi na kifungutenzi. Ili kuondoa tatizo hili misingi ifuatayo itatumika hasa kwa vipengee vitakavyohusika.

Majina ya ngeli ya N – N

Majina yote ya viumbe vyenye uhai yaliyo katika ngeli ya N – N, mathalani: ng’ombe, mbuzi, ndege, mamba n.k., yatachukua upatanishi kwenye kifungutenzi kadhalika na vivumishi kama yalivyo majina ya ngeli ya M- Wa- (yaani, yu-, a-, wa-).

Mifano:

Ng’ombe mdogo amepotea
Ng’ombe wadogo wamepotea
Samaki mkubwa anammeza samaki mdogo
Samaki wakubwa wanawameza samaki wadogo

Sawasawa na:

Mtoto mdogo amekuja
Watoto wadogo wamekuja

Upatanishi huu pia utakuwa vivyohivyo upande wa vimilikishi.

Mathalani:

Mbuzi wake mweupe amepotea
Mbuzi wake weupe wamepotea

Sawasawa na:

Mtoto wake mrefu ameonekana
Watoto wake warefu wameonekana

Majina ya uhusiano wa kifamilia

Majina yaonyeshayo uhusiano wa kifamilia japokuwa yako katika ngeli ya N – N yatapewa upatanishi tofauti na majina mengine katika ngeli hii. Haya yatapewa upatanishi tofauti hasa katika vimilikishi katika wingi.

Mifano:

Baba yangu
Baba zangu
Rafiki yangu
Rafiki zangu

Majina yatakayohusika katika fungu hili ni: baba, mama, dada, bibi, babu, jirani, rafiki, shangazi, ndugu, shemeji, wifi, n.k.

Majina ya viumbe visivyo hai

Majina ya viumbe visivyo na uhai yatatumia kimilikishi cha umoja (-ake) bila kujali majina hayo yatakuwa katika umoja au katika wingi.

Tazama jedwali lifuatalo:

UMOJA

WINGI

Mfano

Matumizi sahihi

Matumizi yasiyo sahihi

Ukuta huu rangi yake ni nzuri

Kuta hizi rangi zake ni nzuri

Kuta hizi rangi zazo ni nzuri

Sanduku hili alama yake haionekani

Masanduku haya alama zake hazionekani

Masanduku haya alama zayo hazionekani

Maktaba hii vitabu vyake havifai

Maktaba hizi vitabu vyake havifai

Maktaba hizi vitabu vyazo havifai

Wimbo huu mdundo wake unapendeza

Nyimbo hizi midundo yake inapendeza

Nyimbo hizi midundo yazo inapendeza

Nvumba hii ukuta wake ni imara

Nyumba hizi kuta zake ni imara

Nyumba hizi kuta zazo ni imara

Kalamu hii wino wake ni mbaya

Kalamu hizi wino wake ni mbaya

Kalamu hizi wino wazo ni mbaya

Matumizi ya “-nge-” na “-ngali-”

Matumizi ya “-nge-” na “-ngali-” yatapambanuliwa ili vipashio hivyo vitumike kwa usahihi kama ifuatavyo:

“-nge-” itatumika kuonyesha matamanio kwa wakati uliopo au ujao.

Mifano:

– Ningekuwa mfalme ningemtendea haki kila raia
– Ningejua siku ya kufa ningejiandaa.

“-ngali-” itatumika kuonyesha matamanio kwa wakati uliopita tu

Mifano:

– Tungalikuwa na silaha, tusingalitawaliwa na wakoloni.
– Tungalijua, tungalijiwekea akiba ya uzeeni.

Zingatia:

Si sahihi kuchanganya matumizi ya vipashio hivyo.

Mathalani:

*Tungalijua, tusingekwambia

*Ningekuja, ningalimwona

Athari kutokana na lugha za kigeni na lugha za makabila

Vipo vipengee kadhaa vitokanavyo na lugha za kigeni na pia za kikabila ambavyo huathiri ufasaha wa Kiswahili. Vifuatavyo hujitokeza mara nyingi katika matumizi:

Matumizi ya nyakati

Tazama mifano ifuatayo:

Matumizi yasiyo sahihi

Matumizi sahihi

· Mimi huendaga kumwona mara kwa mara

Mimi huenda kumwona mara kwa mara

· Yeye halagi nyama n.k.

Yeye hali nyama/Yeye huwa hali nyama.

Athari za muundo wa maneno au mpangilio wa maneno katika sentensi Mifano:

Matumizi yasiyo sahihi

Matumizi sahihi

· Nimealikwa Kilimanjaro hoteli

Nimealikwa hoteli ya Kilimanjaro

· Nilisoma Kigoma sekondari

Nilisoma shule ya sekondari, Kigoma

· Kanjia haka ni kazuri

Kijia hiki ni kizuri/Ujia huu ni mzuri

· Sasa ninapandisha na mlima n.k.

Sasa nlnapanda mlimani n.k.

Mazoea mabaya ya kuchanganya lugha

Mara nyingi maneno ya lugha za kigeni, hasa lugha ya Kiingereza, au ya lugha za kikabila hutumika bila sababu nzuri ya kufanya hivyp. Matokeo yake ufasaha wa Kiswahili hupotoshwa na lugha inayozungumzwa huwa si Kiswahili wala Kiingereza.

Mifano:

Hii ndiyo ofisi ya “District Commissioner”, badala ya:
Hii ndiyo ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Mwaka huu hatukufikia “target” yetu, badala ya;
Mwaka huu hatukufikia lengo letu.

Wa aidha katika kipengele hiki ufasaha wa Kiswahili hupotoshwa na watumiaji wanapotumia maneno au misemo ya Kiingereza iliyofasiriwa sisisi kutoka katika lugha hiyo.

Mifano:

– Baada ya kununua tiketi nilikamata basi, badala ya:
Baada ya kukata tiketi nilipanda basi.

– Wote mnaulizwa kuhudhuria, badala ya:
Wote mnaombwa kuhudhuria.

Matumizi mabaya ya maneno

Kipengele hiki hutokana hasa na kuchanganya matamshi ya maneno yanayokaribiana katika matamshi lakini yenye maana tofauti.

Mifano:

“wasilisha”

na “wakilisha”

“pasha”

na “pasa”

“kalamu”

na “karamu”

“ghali”

na “gali”

“thibiti”

na “dhibiti”

“mrima”

na “mlima”

Vilevile ufasaha hupotoshwa kutokana na neno kubadili maana kadiri ya tofauti ya mazingira ya matumizi.

Mifano:

“kukodi” badala ya “kukodisha”
“kupokea” badala ya “kupokelewa”
“maziko” badala ya “mazishi”

Ufasha hupotoshwa pia kwa kutozingatia usahihi wa jinsi maneno/semi yanavyotumika.

Mifano:

Matumizi sahihi

Matumizi yasiyo sahihi

hapana budi

ni budi

aidha (pia)

aidha aidha (ama … au)

Zingatia: Ili kutoa maelekezo ya matumizi fasaha ya Kiswahili sanifu, BAKITA litakuwa likichapisha mara kwa mara toleo maalumu liitwalo Jifunze Kiswahili Uwafunze Wengine.

SEHEMU YA NNE

Uandikaji wa Fafanuzi na Marejeo

Katika kuandika kazi zote za kitaaluma au taarifa ya utafiti wa kitaaluma, mwandishi hana budi pia kuandika ufafanuzi na marejeo katika kazi hiyo.

Uandikaji wa fafanuzi

Maana ya fafanuzi

Fafanuzi ni marejeo pamoja na maelezo yote ya nyongeza, mathalani, taarifa za ziada kuhusu chanzo cha taarifa au mwandishi mwenyewe, kama vile maoni yake n.k. Fafanuzi hutolewa, kwa mfano, kitabu ilikopatikana taarifa kitajwapo kwa mara ya kwanza katika makala au sura inayoandikwa. Alama maalumu, aghalabu kinyota au tarakimu, huwekwa juu kidogo baada ya mwisho wa jina la kitabu.

Mifano: Diwani ya Mnyampala* au Diwani ya Mnyampala1

Mambo ya kuzingatia

1. Mwishoni mwa makala, sura au taarifa inayoandikwa, fafanuzi kamili itaandikwa kwa kurejea alama au tarakimu iliyoonyeshwa mwanzo katika makala yenyewe. Fafanuzi kamili pia yaweza kuandikwa mwishoni mwa kila ukurasa chini kutegemea utashi wa mwandishi.

2. Fafanuzi kamili inapaswa kuwa na maelezo kamili ambayo ni: jina kamili la mwandishi, jina kamili la kitabu, nambari yajuzuu au toleo la kitabu/jarida hilo, mahali kilikochapishwa (mji), jina la mchapishaji, mwaka kilipochapishwa, ukurasa au kurasa zilizotumiwa au kunukuliwa ili kupata taarifa ambayo mwandishi anaiandika katika makala yake, Juu ya haya, mwandishi aweza kuandika taarifa nyingine ya nyongeza.

Fafanuzi itaandikwa kwa kutumia “nafasi”, yaani, umbali kadhaa kutoka ukingoni mwa karatasi. Mwandishi’ anaweza kuchagua nafasi moja, mbili, nne au tano.

3. Kwa kila kitabu, jarida au chanzo kingine chochote kitakachoandikiwa fafanuzi, nambari ya fafanuzi iwe moja tu. Matumizi yatarakimu na herufi kwa wakati mmoja, kwa mfano, la, Ib, lc, n.k., hayaruhusiwi.

4. Kitabu kitakapokwisha kutajwa mara ya kwanza na kupewa nambari ya fafanuzi, hakuna haja ya kupewa nambari nyingine iwapo kitatajwa tena katika sura au makala yaleyale.

Hata hivyo, kitabu kitapewa nambari nyingine kama kitarejewa au kunukuliwa tena katika sura nyingine. Katika kufanya hivyo, maelezo yake yatakuwa mafupi tu kama ifuatavyo:

· Iwapo nambari za kitabu kinachorejewa mara nyingi zinafuatana, tumia k.h.j. (kama hapo juu) na nambari za ukurasa au kurasa zilizonukuliwa au kurejewa. Mfano: k.h.j. uk. 40

· Iwapo nambari za kitabu kinachorejewa mara nyingi hazifuatani, andika tu jina la mwandishi na ukurasa au kurasa zilizorejewa au kunukuliwa. Mfano: Mulokozi, uk. 6.

· Iwapo vitabu kadhaa vya mwandishi mmoja vinarejewa mara nyingi na nambari zake hazifuatani, andika jina la mwandishi, jina la makala na jina la kitabu au jarida pamoja na ukurasa au kurasa zilizorejewa au kunukuliwa.

Mfano: J.S. Mdee, “Matatizo ya kuunda Istilahi kama Yanavyojitokeza katika Kiswahili, “KiswahiliNa. 55/1 uk. 115.

Zingatia: Katika kuandika majina ya makala, maneno yote yaanze na herufi kubwa, isipokuwa viunganishi kama na, ya, katika, kama, n.k.

5. Fafanuzi zitaorodheshwa na kupangwa kufuata nambari kama zilivyojitokeza katika makala yenyewe, na orodha hiyo itawekwa kila mwisho wa sura, na kila sura itaanza na nambari mpya. Ndani ya fafanuzi, nambari za kurasa zinazorejewa zitaandikwa kwa ukamili kama ifuatavyo:
Kur. 325 – 330 na siyo Kur. 325 – 30

6. Iwapo katika aya moja waandishi kadhaa wametajwa kuhusu suala lilelile moja wanalohusiana, basi wote watapewa nambari moja ya ufafanuzi itakayowekwa mwishoni mwa kauli.

Mfano:

Mugyabuso Mulokozi1, Kutikoyela Kahigi2 na Theobald Mvungi3 ni baadhi ya washairi waandikao bila kutawaliwa na urari wa mizani. (Siyo sahihi)

Mugyabuso Mulokozi. Kulikoyela Kahigi na Theobald Mvungi ni baadhi ya washairi waandikao hila kutawaliwa na urari wa mizani1 (Sahihi)

Katika fafanuzi patawekwa maelezo kamili ya vitabu walivyoandika.

7. Neno tazama kwa kifupi taz. litatumika katika fafanuzi ambazo mwandishi amerejea kwa muhtasari au kwa maneno yake mwenyewe bila kunukuu neno kwa neno, kauli au maandishi ya watu wengine. Maelezo katika fafanuzi yawe kamili. Kama maneno halisi ya mwandishi yamenukuliwa, nambari ya fafanuzi iwekwe mwishoni mwa maneno yaliyonukuliwa na siyo juu ya jina la mwandishi.

8. Iwapo kitabu kimoja kinajadiliwa kwa kirefu na kinanukuliwa mara nyingi (hasa katika makala za kifasihi), nambari za fafanuzi zisitumike. Andika nambari ya ukurasa ulionukuliwa katika mabano.

Mfano:

Katika tamthilia hii tunaona uhakiki uliofichama Juma anapouliza swali hili:

Ule mfano wa mashua ulikuwa si mzuri. Katika jahazi hakuna nahodha tu; kuna abiria vilevile. Je abiria wanataka kwenda upande gani? (uk. 23). (Kitabu kinachojadiliwa hapa kwa kirefu niMashetani)

9. Kunukuu maneno katika makala

Maneno kama hayana budi kukidhi haja na kuandikwa ifuatavyo:

· Yawe yanaoana vizuri kimantiki na kimtiririko na makala ili yaonyeshe umuhimu wa kunukuliwa kwake kwa sababu yanasukuma mbele hoja kwa kutoa mwanga zaidi kuhusu hoja inayojadiliwa.

· Maneno hayo yanayonukuliwa yataingia ndani ya msitari, nafasi tano kutoka ukingoni (pambizoni) na yatachapwa nafasi moja kati ya msitari na msitari, kmyume na nafasi mbili kati ya msitari na mstari katika makala.

· Maneno hayo lazima yafanane na jinsi yalivyo katika maandishi ya awali, kwa mfano, katika matumiziya herufi kubwa, matumizi ya vituo, n.k.

· Maneno ambayo mwandishi anataka kuyasisitiza ndani ya kauli iliyonukuliwa, yatapigiwa msitari chini, na maneno “msisitizo ni wangu” yatawekwa mwishoni mwa kauli katika mabano.

· Iwapo maandishi yaliyo katika lugha za kigeni yatanukuliwa, basi, yatanukuliwa kama yalivyo katika lugha hiyo na kisha tafsiri yake ya Kiswahili itafuata chini. Nambari ya fafanuzi itawekwa mwishoni mwa kauli ya awali na siyo juu ya tafsiri. Tafsiri itawekwa ndani ya mabano mraba. Mwishoni mwa tafsiri pataongezwa maneno (tafsiri ni yangu) iwapo tafsiri ni yako. Kama tafsiri si yako, maelezo kamili yatawekwa katika fafanuzi. Kamwe, usinukuu tafsiri yako mwenyewe ya maneno yaliyonukuliwa. Kama unanukuu maneno yaliyonukuliwa na mtu mwingine na hukuweza kupata kitabu hicho, ongeza maneno “kama ilivyonukuliwa na…”

10. Mpangilio wa kuandika vipengee katika fafanuzi

Fafanuzi zitaandikwa kwa mpangilio ufuatao: Nambari ya Fafanuzi, Jina kamili la mwandishi likifuatiwa na mkato, Jina la kitabu ambalo litapigiwa msitari chini yake. Alama ya kufungua mabano ambayo itafuatiwa na jina la mji ambako kitabu hicho kilichapishwa. Kisha jina hilo litafuatiwa na nuktapacha na kufuatiwa na jina la wachapishaji. Weka mkato baada yajina la mchapishaji, kisha andika mwaka wa kuchapishwa na alama ya mabano ya kufunga. Weka mkato, halafu neno uk. au kur, kwa kifupi, na weka nukta mwisho kabisa. Kama kuna maelezo mengine, yaandikwe baada ya hapo.

Mfano: 1. Amri Abedi, Sheria za Kutunga Mashairi (Nairobi: East African Literature Bureau, 1954), uk., 60.

11. Upungufu wa vipengee katika kuandika Fafanuzi
Iwapo miji kadhaa imetajwa, chagua mji mmoja (hasa wa kwanza). Iwapo mahali kilikochapishwa kitabu hapakuandikwa, basi andika h.m., yaani, hakuna mji. Iwapo tarehe (yaani mwaka) ya kuchapishwa hakuna, andika h.t., yaani, hakuna tarehe. Iwapo mchapishaji hakuandikwa, basi andika pia h.m., yaani, hakuna mchapishaji. Nafasi itaonyesha kinachokosekana ni nini: mji au mchapishaji. Iwapo hakuna tarehe lakini mwandishi katika utangulizi au dibaji ameweka tarehe, basi tarehe hiyohiyo itumike lakini pamoja na alama ya kiulizi baada ya tarehe hiyo ili kuonyesha shaka juu yake.

12. Finyazo za majina ya mashirika ya kimataifa na kitaifa yanayojulikana zinaweza kutumika katika fafanuzi, (Majina kama UNESCO, TUKI, BAKITA, na mengine ambayo ni marefu mno kimaandishi). Pia badala ya kuandika kwa kirefu k.m. Heinemann Educational Books Inco, 1977, unweza kuandika: Heinemann, 1977.

13. Majina ya makala yawe ndani ya alama za mnukuo. Vitabu, vijitabu, majarida magazeti na filamu ndivyo vinavyopigiwa msitari chini yake.

14. Barua, majedwali, orodha mbalimbali vikionekana kwamba vinaingilia au kuharibu mtiririko wa mawazo viandikwe mwishoni kama viambatishi.

Mifano mbalimbali ya uandikaji fafanuzi

Kitabu ambacho kimeandikwa na mtu mmoja

Mfano: Abdilatif Abdalla, Sauti ya Dhiki (Nairobi: Oxford University Press, 1973), uk. 8.

Kitabu kilichoandikwa na watu wawili au watatu

Mfano: Amandina Lihamba, Ndyanao Balisidya na Penina Mhando, Harakati za Ukombozi (Dar es Salaam: Tanzania Publishing House, 1982), uk. 7.

Iwapo waandishi ni zaidi ya watatu, basi andika jina lililotajwa kwanza kitabuni, kisha ongeza maneno “na wengineo” baadayajinahilo, halafu, endelea kuandika vipengee vingine kama ilivyoelekezwa. Waandishi wawili au watatu wanaweza kutajwa wote au mmoja “na wengineo”.

Kitabu kilichochapishwa na shirika, twne n.k.

Mfano: Chama cha Washairi wa Kiswahili Tanzania, Mashairi ya Hekima na Malumbano ya Ushairi, Yamekusanywa na Mathias Mnyampala (Dar es Salaam: Chama cha Washairi wa Kiswahili, Tanzania, 1965?), uk. 1.

Makala kutoka kitabu kilichohaririwa

Mfano: M.A. Maganga, “Maisha ya Shaaban Robert na mawazo yake”, katika Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili: Kitabu cha Kwanza, (mh) Farouk Topan (Dar es Salaam: Oxford University press, 1971), kur. 33-54.

Iwapo makala ya mhariri mwenyewe ndiyo yaliyonukuliwa

Mfano: Farouk Topan (mh) “Michezo ya Kuigiza”, katika Uchambuzi wa Maandishiya Kiswahili (Dar es Salaam: Oxford university press, 1971), kur. 66-79.

Iwapo idadi ya wahariri ni wawili au watatu, andika majina yao wote na neno (wah.) yaani wahariri.

Iwapo makala ya mwandishi mwenyewe ndiyo yaliyonukuliwa kutoka kitabu chake

Mfano: Julius K. Nyerere, Ujamaa (Dar es Salaam: Oxford University Press, 1968), kur. 73-88.

Makala kutoka kitabu chenye juzuu (kwa kifupi Juz.)

Mfano: E. Kezitahabi, “Mashairi ya Kiswahili”, katika uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili Juz. 2 (mh) Farouk Topan (Dar es Salaam: Oxford University Press, 1979), kur. 13-27.

Makala kutoka kwenye kitabu chenye juzuu zenye majina ya nyongeza tofauti

Mfano: Daniel J. Mkude, “Uchambuzi wa Sentensi za Kiswahili”, katika Lugha ya Kiswahili, Juz. 1 la Makala za Semina ya Kimataifaya Waandishi wa Kiswahili (Dar es Salaam: TUKI, 1983), kur. 219-243.

Zingatia: Jina la nyongeza linatangulia kwanza na majina yote mawili yanapigiwa msitari chini.

Mfano mwingine:

L.A. Cormican, “Milton’s Religions Verse” katika From Donneto Marvell, Vol. 3 la The Pelican Guide to English Literature, (mh) Boris Ford (Harmond-Sworth: Penguin Books, 1956), kur. 173-192.

Makala kutoka vitabu vya rejea

Mfano: “Abraham Lincoln”, Encyclopedia Americana, 1976 ed.

Iwapo mwandishi ameweka jina lake mwishoni mwa makala, jina lake linaweza kutajwa kwanza na kurasa zaweza kuwekwa mwishoni.

Kitabu kilichofanyiwa mabadiliko katika toleojipya

Inabidi toleo hilo jipya litajwe.

Mfano: F.E.M.K. Senkoro, Fasihi, Tol. la 2, (Dar es Salaam: Press and Publicity, 1982).

Kitabu kilichofasiriwa (kwa kifupi taf.)

Mfano: Ngugi wa Thiong’o, Njia Panda, taf. ya John Ndeti Somba, (Nairobi: EastAfricanPublishingHouse, 1974).

Utangulizi ulionukuliwa (Kwa kifupi Utang.)

Mfano: Abdilatif Abdalla, Utang., Diwani ya Nyamaume, Mkusanyaji Shaaban Gonga, Mhariri AbdilatifAbdallah, (Nairobi: East African Publishing House, 1974).

Tasnifu ambayo haijachapishwa (kwa kifupi Tas.)

Mfano: E. Kezilahabi, “Riwaya za Shaaban Robert”, tas. ya M.A. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 1974, uk. 30.

Angalia: Jina la tasnifu halipigiwi msitari chini. Hata hivyo iwapo tasnisfu imekwishachapishwa, basi itapewa hadhi ya kitabu na uandishi wa fafanuzi yake utafuata kanuni zote zinazohusu kitabu. Yawezekana kuongeza maelezo ya ziada kuwa awali kitabu hiki kilikuwatasnifu iliyotolewa katika chuo kikuu cha

Makala toka kwenye jarida

Jina la makala litatajwa likiwa katika alama za mnukuo. Jina la jarida litatajwa likiwa limepigiwa mstari chini yake. Kadhalika namba yajuzuu na mwaka hutajwa.

Mfano:

Said A. Khamis, “Nafasi ya Fasihi Simulizi katika Jamii ya Kitanzania”, Mulika Na. 15 (1983), kur. 3-13.

S.S. Salehe, “Nyimbo za Taarab Unguja”, Lugha Yetu, Na. 37 (1980), kur. 35-48.

Makala au kauli toka magazetini

· Kutoka gazeti lichapishwalo mara moja kwa juma.
Mfano: Jumanne Shaibu, “Lugha za Mitaani”, Mzalendo, 15 Feb. 1987, uk. 5 saf. 3.

· Kutoka gazeti la kila siku.
Mfano: Mwandishi wa Uhuru, “Uzembe unaletea Afrika hasara”, Uhuru, 27 Feb. 1993, uk. 5, saf. 4-5.

· Makala yanayoendelea kwenye ukurasa mwingine wa gazeti.
Mfano: Jacob Kambili, “Viongozi wenye tamaa wadhibitiwe – Wabunge” Uhuru, 18 Feb. 1993, uk. 1 saf. 4-5; uk. 3, saf. 2.

· Maoni ya Mhariri.
Mfano: Maoni Yetu, “Kasumba ya Kiingereza Chuo Kikuu ni ya nini?” Uhuru, 22 Feb. 1993, uk. 1, saf. 1-4.

· Makala ambayo hayana jina la mwandishi.
Mfano: “Wanafunzi Chuo Kikuu wakataa mtoa hoja kuzungumza Kiswahili”, Uhuru, 22 Feb. 1993, uk. 1, saf. 1-4.

· Barua kwa Mhariri.
Mfano: A.J. Nyiti, Barua, uhuru, 13 Jul.1987, uk. 4, saf. 2.

Makala ya mapitio ya vitabu

· Makala yaliyo najina la mwandishi
Mfano: Ismael R. Mbise, “Hatia”, Mapitio ya kitabu cha Hatia, mwandishi Penina Muhando Kiswahili, Vol. 41/1 (Machi 1971), lcur. 165-167.

· Makala ambayo hayana jina la mwandishi
Andika jina la makala katika alama za mnukuo, kisha endelea kundika vipengele vingine kama ilivyoonyeshwa katika kifungu cha makala yenye jina la mwandishi hapo juu.

· Barua
Katika kunukuu barua iliyoandikwa, andika:
Mfano: Barua niliyoandikiwa na Shaaban Robert, 15 Februari, 1955.

· Mahojiano
Ni muhimu kutaja: Jina la mhojaji, mhojiwa, tarehe ya mahojiano – tarehe, mwezi na mwaka. Yawezekana pia kutaja mji na mahali mahojiano yalikofanyika.

Mfano: Mahojiano kati yangu na Ngugi wa Thiong’o, 16 Mei, 1979, mjini London.

Mihadhara na vyombo vya mawasiliano

· Mihadhara na hotuba.

Inabidi kuonyesha jina la mzungumzaji, mada (katika alama za mnukuo), hadhira, mahali, tarehe, mwezi na mwaka.

Mfano: Julius K. Nyerere, “Ujamaa una Njia Nyingi”, hotuba iliyotolewa katika Chuo Kikuu cha Cairo, 10, Aprili, 1967.

· Vipindi vya Redio au Televisheni

Inabidi kuonyesha: jina la kipindi (katika alama za mnukuo), jina la kituo au idhaa, mji na tarehe kiliposikika hewani. Unaweza pia kutaja majina ya mtangazaji na mtayarishaji wa kipindi hicho kama ni muhimu.

Mfano: “Taarifa ya Habari”, saa 2 usiku, msomaji Eda Sanga, Redio Tanzania, Dar es Salaam, 10 Mei 1988.

· Kanda na Rekodi

Maneno yaliyo kwenye kanda au rekodi zinazouzwa yanaponukuliwa, andikajina la mwimbaji, jina la wimbo, jina la msanii au mtayarishaji na kampuni iliyotoa rekodi au kanda hizo, mji, nambari ya katalogi na pia mwaka.

Mfano: Juma Kilaza, “Mariamu”, Cuban Marimba Band, Mtoaji rekodi A.P. Chandarana, Kericho, Na. MPC 2088, 1971.

Kama maneno yako kwenye kanda za utafiti tu, fafanuzi zake zitaandikwa kama za mahojiano – Mahojiano. Unaweza kuongezajina la wimbo, n.k. kama ni muhimu.

· Filamu

Katika kuandika fafanuzi za filamu, andika jina la mtayarishaji, jina la filamu, na msambazaji. Unaweza pia kuwataja wahusika, na maelezo mengine kama yanahitajika.

Mfano: Martin Mhando, (mtay.), Mwna Twnaini, Waandishi: Martin Mhando na T.M. Mollel, Mhusika Mkuu Penina Mlama kama Mama Tumaini, Kampuni ya Filamu Tanzania na SIDA, 1986.

· Maonyesho na Maigizo

Katika kuandika fafanuzi za maigizo ya tamthilia au sanaa maopyesho, andika fafanuzi kama ilivyoelekezwa kuhusu filamu hapo juu, ila inabidi kuongeza pia jumba au mahali onyesho lilipofanyika na pia mji.

Mfano: Amandina Lihamba (mtay.), Pambo, Mwandishi Penina Muhando, Mhusika Mkuu Ibrahim Ngozi kama Pambo, Kikundi cha Paukwa, Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dar es Salaam, 20 Julai, 1985.

Uandikaji wa marejeo (bibliografia)

Maana ya Bibliografia

Bibliografia ni orodha ya marejeo yote, yaani, vitabu na makala yote yaliyotumika katika kuandaa makala, muswada, tasnifu, n.k. na pia vitabu vyote vilivyorejewa katika kuandika fafanuzi. Wakati mwingine bibliografia, kwa jumla, huitwa marejeo. Ni muhimu kutambua kuwa neno marejeo ni pana zaidi, na hivyo yafaa litumike tu iwapo mwandishi amerejea kwenye vitu kama filamu, radio, televisheni, picha, n.k. mbali ya vitabu na maandishi mengine mbalimbali aliyoyasoma na kwa jumla vikaathiri mawazo yake katika makala aliyoyaandika.

Mambo ya Kuzingatia

Tofauti kuu kati ya uandikaji wa fafanuzi na bibliografia ni:

1. Katika kuandika bibliografia, orodha ya marejeo hupangwa kadiri ya mpangilio wa herufi za alfabeti; tarakimu hazitumiki. Katika fafanuzi mpangilio hufuata jinsi mwandishi alivyoyatumia marejeo yake kulingana na mantiki ya makala anayoyaandika. Ndiyo sababu marejeo hayo hupewa tarakimu katika makala yenyewe na kuorodheshwa vivyo hivyo katika orodha ya fafanuzi.

2. Katika kuandika bibliografia hakuna maelezo ya nyongeza yanayohitajika. Maandishi ambayo hayakurejewa hayaorodheshwi kabisa, na kurasa zilizorejewa (isipokuwa kama ni makala) hazionyeshwi.

3. Katika kuandika bibliografia orodha yake lazima ianze na ukurasa mpya mwishoni mwa makala kabla ya ukurasa wa fahirisi, najina la ukoo (au la mwisho) la mwandishi ndilo hutangulia kuandikwa. Mfano:A.J. Saffari litaandikwa: Saffari, A.J.

4. Mwandishi wa bibliografia, kutegemea mtindo atakaotumia, anayo hiari ya:

· Kuonyesha mwaka ambao maandishi yanayorejewa yalichapishwa, mara tu baada ya jina la mwandishi.

Mfano: Nkwera, F.V.M., (1978) Sarufl na Fasihi: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam, Tanzania Publishing House.

AU kuonyesha mwaka huo mwishoni mwa vipengele vyote vinavyohusu kubainisha marejeo.

Mfano: Nkwera, F.V.M. Sarufl na Fasihi: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam, Tanzania Publishing House, 1978.

· Kupiga msitari chini ya jina la kitabu au jarida linalorejewa.

Mfano: Saffari, A.J., Harusi. Dar es Salaam, BCI Publishers, 1984.

AU kutopiga msitari chini ya jina la kitabu au jarida linalorejewa.

Mfano: Saffari, A.J., (1984), Harusi. Dar es Salaam, BCI Publishers.

MIFANO MBALIMBALI YA UANDISHI WA BIBLIOGRAFIA

Bibliografia inayohusu vitabu

Kitabu ambacho kimeandikwa na mwandishi mmoja

Mfano:

Mvungi, Martha, Lwidiko. Dar es salaam: Tanzania Publishing House, 1975.

Nurru, Said, Mtango wa Kiswahili. Nairobi: East African Literature Bureau, 1975.

Kitabu kilichoandikwa na watu wawili au watatu

Mfano:

Sengo, T. na Saifu K., Hisi Zetu 1. Dar es Salaam: Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili, 1973.

Lihamba, Amandina, na wengineo. Harakati za Ukombozi. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House, 1982.

Kitabu kilichoandikwa na waandishi watatu au zaidi ya watatu
Jina la mwandishi aliyetajwa kwanza ndilo litakaloandikwa likifuatiwa na maneno na wengineo badala ya kutaja waandishi wote. Waandishi wawili au watatu wanaweza kutajwa wote kisha maneno na wengineo yakafuata.

Kitabu kilichochapishwa na Shirika, tume n.k.

Mfano: Chama cha Washairi wa Kiswahili Tanzania, Mashairi ya Hekima na Malumbano ya Ushairi. Dar es Salaam: Chama cha Washairi wa Kiswahili Tanzania, 1965.

Kitabu kilichofasiriwa

Mfano: Dickinson, Margaret. (Mh) Risasi Zianzapo kuchanua. Taf. ya Paul Sozigwa. Nairobi: East African Publishing House, 1972.

Kitabu kilichohaririwa

Mfano: Topan, Farouk (Mh) Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili. Dar es Salaam: Oxford University Press, 1971 na 1979.

Zingatia: Mhariri hupewa hadhi kuliko waandishi wa makala zilizo ndani ya kitabu kwa sababu jina la mhariri ndilo hujitokeza kwenye jalada la kitabu. Hata hivyo, yawezekana kuonyesha jina la mwandishi wa makala iliyorejewa kama ifuatavyo:

Mfano: Shija, A.N. “Wahusika wa Shaaban Robert” katika Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili: Kitabu cha Kwanza. (Mh) Farouk Topan. Dar es Salaam Oxford University Press, 1971.

Kitabu ambacho utangulizi wake tu ndio wnerejewa

Mfano: Mwaduma, S.Z. utang. katika kitabu chake Simbayavene. London: University of London Press, 1974.

Bibliografla inayohusu makala

1. Makala kutoka kitabu

Mbali ya vipengele vingine vya bibliografia, ukurasa wa makala inayohusika sharti uonyeshwe.

Mfano: Shija, A.N. “Wahusika wa Shaaban Robert”. katika Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili (1). (Mh) Farouk Topan. Dar es Salaam: Oxford University Press, 1971, kur. 1-5.

Iwapo kitabu kimehaririwa na watu wawili au watatu, andika majina yao wote na kuonyesha (wah.), yaani, wahariri.

2. Makala ambayo mwandishi wake hajulikani.

Mfano: BAKITA. “Istilahi za Agronomia na Ufugaji”. Katika Lugha Yetu. Tol. Na. 35 na 36, 1980.

3. Makala kadhaa au vitabu vya mwandishi yuleyule vilivyorejewa.

Vitabu au makala vitapangwa kwa mfuatano wa kuchapishwa. Vile vilivyochapishwa kwanza vitaorodheshwa kwanza. Jina la mwandishi litaandikwa kwa kitabu au makala ya kwanza tu, na msitari ukifuatwa na kituo cha nukta utawekwa kwenye nafasi ya jina la mwandishi kwa makala au vitabu vyote vifuatavyo.

Mfano: Abdulla, Mohamed Said.

– Mzitnu wa Watu wa Kale. Nairobi: East African Literature Bureau, 1960.
– Kisima cha Giningi. London: Evans, 1968.
– Duniani Kuna Watu. Dar es Salaam: East African Publishing House, 1973.
– Siriya Sifuri. Dar es Salaam: Est African Publishing House, 1974.

4. Makala au kitabu kilichochapishwa na mashirka mbalimbali.

Inabidi ionyeshwe nani alikichapisha kwa mara ya kwanza. Hivyo, maneno Kimetolewa kwa mara ya kwanza nayaongezwe mwishoni pamoja na jina la mchapishaji wa awali na mwaka. Nyongeza hiyo itawekwa mabanoni.

Mfano: Robert, Shaaban. Pambo la Lugha. Nairobi: Oxford University Press, 1966. (Kimetolewa kwa mara ya kwanza na Witwatersrand University press, 1947.)

5. Makala ya mapitio ya vitabu

Mfano: Mochiwa Z.S.M. “Hatia ya Hatia”. Mapitio ya kitabu cha Hatia, mwandishi Penina Muhando. Mulika,Na. 8, 1976, kur. 11-16.

6. Makala yaliyotolewa kwenye semina.

Mfano: Msokile, Mbunda. “Waandishi chipukizi na Matatizo yao”. Makala yaliyotolewa kwenye Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Vitabu, Dar es Salaam, Oktoba 26-29, 1987.

7. Mihadhara na Hotuba.

Mfano: Nyerere, Julius. “Kazi ya Wizara Mpya ya Utamaduni.” Hotuba iliyotolewa Bungeni, 10 Des. 1962.

8. Makala kutoka magazetini.

Mifano:

Hassan Salum. “Mwongozo wa BAKITA” Mfanyakazi, 1 Nov. 1987, uk. 10 saf. 6.
Maoni ya Mhariri
“Maoni Yetu”. Maoni ya Mhariri. Uhuru, 17 Nov. 1987.
Barua kwa Mhariri
Sefu Mohamed. Barua Uhuru. 13 Jul. 1987, uk. 4, Saf. 2.

Zingatia: Ikumbukwe tu kwamba tofauti kubwa katika utumiaji wa alama za vituo kati ya uandikaji wa fafanuzi na bibliografia ni matumizi ya mkato na nukta. Uandikaji wa bibliografia unatumia zaidi nukta ambapo ule wa fafanuzi unatumia mkatb ili vipengele visomeke kama maelezo ya sentensi moja yenye kueleweka. Mwandishi huchukua nafsi kama anayezungumza na msomaji. Tofauti kubwa ya pili ni kwamba katika uandikaji wa bibliografia jina la ukoo (au jina la pili) la mwandishi ndilo hutangulia kuandikwa. Katika uandikaji wa fafanuzi utaratibu kinyume cha huu ndio unaofuatwa. Jambo lingine la kuzingatia ni kwamba iwapo wapo waandishi zaidi ya mmoja waliochangia katika uandishi wa kitabu, makala n.k. yaweza kutosha kuandika jina la mwandishi mmoja tu halafu kuongeza maneno na wengineo.

Kila taaluma (k.m. tiba, sayansi, sheria n.k.) ina mtindo wake wa kuandika fafanuzi na bibliografia. Mwongozo wa BAKITA unahusu lugha ya Kiswahili, taaluma za Isimu, Fasihi na masomo mengine yaliyomo katika fani ya sanaa na sayansi za jamii.

VIFUPISHO VITUMIKAVYO KUANDIKA BIBLIOGRAFIA NA FAFANUZI

Uandikaji wa vifupisho

Vifupisho vitaandikwa kwa herufi ndogo na pia vitalazimika kuwekewa alama ya nukta baada ya kila herufi.

Mifano:

kwa niaba ya

= k.n.y.

Kupitia kwa

= k.k.

ipitie kwa

= i.k.

na kadhalika

= n.k.

kwa mfano

= k.m.

kama vile

= k.v.

maili kwa saa

= m.k.s.

Zingatia:

Baadhi ya vifupisho, hasa vinavyohusu vipimo, vitaandikwa kwa herufi mbili.

Mifano:

kilomita = km

kologramu = kg

Hivyo, kilomita kwa saa = km.k.s.

Orodha ya vifupisho ambavyo kwa kawaida hutumika katika uandikaji wa bibliografia na fafanuzi ni hii ifuatayo:

h.m.

hakuna mchapishaji au hakuna mji

h.t.

hakuna tarehe

juz.

juzuu (vol.)

k.h.j.

kama hapo juu (ibid)

k.m.

kwa mfano

k.n.y.

kwa niaba ya

k.v.

kama vile

mh./wah.

mhariri, wahariri

mtay.

mtayarishaji

Na.

Nambari

n.k.

na kadhalika

saf.

safu

seh.

sehemu (sec.)

sic.

sic (kama ilivyo)

taf.

tafsiri (trans.)

tas.

tasnifu

tol.

toleo (edn.)

uk. & kur.

ukurasa, kurasa.

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)

Printed by Dar es Salaam University Press