MWANANGU: WATAKUJA WATALIA LAKINI MWISHO ATABAKI MKEO NA WANAO!

By , in ELIMUJAMII on .

Baba alinisisitizia kuchukua likizo, kazini nilikuwa na mambo mengi sana lakini aliniambia kuwa mwezi mmoja wa kutokuwa kazini naweza kujutia maisha yangu yote kwani yeye hatavuka mwezi atakufa. Kwa namna alivyokuwa anaongea mpaka niliogopa, Baba yangu hakuwa mtu wa kudekadeka mara nyingi alijifanya mgumu hata alipokuwa anaumia sana, nilipomsikia anaongea vile nilijua kuwa kuna kitu na ninahitajika kwenda kumuona.

Nilichukua likizo na kwenda nyumbani, kweli alikuwa anaumwa, alikuwa kaisha, alikuwa kakonda afya imedhoofu na alikuwa hawezi hata kunyanyuka. Alikuwa mpole anaongea taratibu mnyonge sana, kwa mtu aliyekuwa anamfahamu Baba yangu angemuonea huruma na hata kutoa machozi kwa kumuona vile. Nilimuangalia kwa huruma lakini alilazimisha tabasamu, hakutaka kuonekana mnyonge.

Aliniambia kuwa wewe ndiye mtoto wangu wa kwanza, una wadogo zako sita na wakike wawili na wanaume wanne, kuna kitu nataka nikufundishe kabla sijafa ili uje kuwa Bora na si kuwa kama mimi. Nilimuitikia nikidhani kuwa kuna kitu ataniambia, lakini mpaka likizo inaisha hakuniambia kitu chochote, nilishangaa na kumuuliza mbona kaniahidi kuniambia kitu lakini hajaniambia na likizo inaisha natakiwa kurudi kazini.

Alitabasmau na kuniambia kuwa ameshaniambia. Nilifikiria sana nikijaribu kukumbuka kama kuna kitu labda aliniambia nikakisahau lakini sikukumbuka, nilifikiri sana na sana sikukumbuka chochote, nilishindwa nikamuambia Baba mbona sikumbuki chochote. Alitabasmau tena, huku akiongea kwa shida aliniuliza nimekaa pale siku ngapi, nilimuambia siku 23, akaniuliza wewe una Shangazi wa ngapi nikamuambia wawili na Baba wadogo nikamuambia watatu.

Akaniuliza tangu nikae hapo walishakuja mara ngapi, nilimuambia Shangazi mmoja alikuja mara tatu, kuna mwingine kila baada ya siku mbili anakuja, Baba wadogo aliyekuja ni mmoja mara moja kwani wote wapo mjini na familia zao. Alitabasamu tena na kuniuliza vipi Mama yako tangu uje hapa yeye kaja mara ngapi? Nikashangaa sana nikidhani labda Baba kachanganyikiwa nilimuambia.

“Baba Mama mbona kila siku yuko hapa, ndiyo anakupikia, anakusafisha, anakufanyia kila kitu? Inamaana umesahau?” Nilidhani Baba akili zimeanza kupotea lakini alitabasamu na kuniambia “Hapana mwanangu, sikusahau leo kuwa Mama yako hayupo, nilisahau kipindi namuoa kuwa hayupo. Niliendekeza ndugu na kuwajali, niliwapa kila kitu huku Mama yako nikimfungia ndani, nilikuwa nikimpiga kwa maneno tu ya ndugu zangu.

Alivumilia kila kitu kwakua hakua na pakwenda lakini leo yeye ndiye yuko na mimi na ananihudumia kwa kila kitu wakati mimi sina pakwenda. Ndugu zangu wana maisha mazuri lakini wapo na familia zao wanakuja kunisalimia wakati Mama yako ananiogesha na kunilisha. Nyie wanangu mpo huko mna maisha yenu, siwalaumu lakini ukweli nilikuwa mimi si jukumu lenu hata kuja kunisalimia mnapangiana zamu.

Lakini Mama yako hana cha zamu, akilala akiamka yuko na mimi, akigeuka ni mimi, akila ni mimi, akipumua ni mimi, nikijisaidia ni yeye, nikitapika ni yeye, nikidondoka ni yeye. Wakati zamani nilikua namuambia kama umenichoka bado ondoka lakini leo siwezi hata kujisaidia bila yeye. Mwanangu wapende ndugu zako lakini kama hutaki kufa kwa unyonge kama mimi basi Mpende mke wako zaidi, huyo ndiye Mungu akipanga utazeeka naye.

Ndugu watakuja kukusalimia tu na kukupa pole lakini wakubeba kinyesi chako ni mkeo. Mfanye abebe huku akikumbuka mema uliyomfanyia na si mateso uliyompa, mwanangu ukimnyanyasa mwanamke lazima utateseka tu, akitangulia kufa yeye atabaki na watoto wanaokuchukia kwakua ulimtesa Mama yao, hata kama hawakuona lakini utakua unaumia kila siku ukiwaona na ukitangulia wewe basi yeye ndiye atakua karibu kukuhudumia, mheshimu sana mke wako.”

Baba alimaliza kuongea, akaniambia nimuache apumzike. Siku iliyofuata niliondoka kurudi mjini lakini sikufika, nilipigiwa simu kuwa Baba yangu kafariki dunia. Nilirudi kwenye msiba, ndugu zake walikuja na kulia tena sana. Lakini baada ya siku mbili wote walirudi kwao na familia zao, alibaki Mama tu, nilijikuta badala ya kulia natabasamu kwani Baba alinifundisha kuwa watakuja watalia na mwisho wa siku atabaki mkeo na wanao.

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!