MUHTASARI, AZIMIO LA KAZI NA ANDALIO LA SOMO

By , in WALIMU on . Tagged width: , ,

MUHTASARI, AZIMIO LA KAZI NA ANDALIO LA SOMO

4.1       Utangulizi

Maneno “Muhtasari, Azimio la kazi na Andalio la somo” sio mageni kwa walimu ambao sasa hivi wanafundisha shuleni au vyuoni. Kila somo lifundishwalo shuleni au vyuoni lina muhtasari wake. Mwalimu wa darasani anapta mada za kufundisha kutoka kwenye muhtasari wa somo. Akipata mada hizo anatengeneza azimio la kazi. Kabla ya kwenda kufundisha darsani anaandaa atakachokwenda kufundisha (andalio la somo) Muhadhara huu unachambua mahitaji hayo matatu ya ufundishaji.

Malengo mahsusi

Baada ya kusoma muhadhara huu utaweza:
1. kufafanua muhtasari wa lugha na muundo wake.
1. kueleza vipengele vya maazimio ya kazi.
1. kuandika andalio la somo la Kiswahili ipasavyo.

4.2       Muhtasari

            Muhtasari ni nini?

Muhtasari ni utaratibu wa vipengele mahsusi katika somo lolote lile (Mbunda, 1996). Katika muhtasari vipengele vimepangwa kwa ufupi na kimantiki kwa ajili ya mafunzo katika ngazi maalum. Vipengele hivyo vinajumuisha madhumuni ya somo husika, maudhui, mbinu za jumla za ufundishaji, pamoja vitabu na vifaa mbalimbali ambavyo vitaenda sambamba na maudhui yaliyomo.

Muhtasari unaandaliwa kufuatana na mada na ngazi ya elimu inayohusika. Hapa Tanzania kwa hivi sasa tuna Muhtasari wa Kiswahili wa miaka saba ya elimu ya msingi; Muhtasari wa Kiswahili wa miaka mine ya kidato cha kwanza hadi cha nne; muhtasari wa Kiswahili wa miaka miwili wa kidato cha tano na sita na muhtasari wa Kiswahili wa miaka miwili wa vyuo vya ualimu.

4.2.1    Muundo wa Muhtasari wa Kiswahili

(i)   Madhumuni ya lugha

Madhumuni yaliyoko kwenye muhtasari lazima yahusishwe na malengo ya elimu pamoja na sera ya elimu ya taifa, na yatofautiane kutoka ngazi moja ya elimu hadi nyingine.

(ii)    Maudhui ya mada mbalimbali

Mada mbalimbali zitatumiwa katika kutekeleza madhumuni yaliyotolewa. Mada zote zinawekewa malengo yake maalum, na katika nagazi zake tafauti. Kwa mfano, mada ya utungaji ina msisitizo wake katika vidato mbalimbali kama ifuatavyo:

Kidato cha Kwanza    –           kumwezesha mwanafunzi kufikiri, kuzungumza na

kuelewa kwa kusema na kuandika Kiswahili kwa mtungo fasaha.

Kidato cha Tatu          –           Kuendeleza kumwongoza mwanafunzi aweze

kutumia lugha katika fani na njia mbalimbali kwa ufasaha.

Kidato cha Nne           –           Kuwapa wanafunzi fursa ya kujadiliana juu ya

mambo mbalimbali ya maendeleo ya nchi pamoja na yale yanayotendeka nchini siku hata siku.

Kwa kawaida mada moja kuu itagawanywa katika mada ndogondogo kufuatana na wingi wa shughuli k.m. mada kuu ya kuzungumza inaweza kuwa na mada ndogo za:

 • Kujibu maswali ya ufahamu kutokana na hotuba
 • Majadiliano
 • Hotuba
 • Kutamba hadithi
 • Midahalo
 • Majigambo
 • Tenzi.

(iii)   Mbinu za ufundishaji

Muhtasari utakuongoza mwalimu jinsi ya kukabili ufundishaji wa mada fulani k.m. kuanza na kutoa maana kabla ya mifano mbalimbali. Pamoja na mbinu zilizoko kwenye muhtasari, mwalimu unapaswa kubuni mbinu zitakazoendana na mazingira ya darasa lako.

(iv) Tathmini

Muhtasari unaonesha jinsi gani unalenga kupima mafanikio yake, na hasa kuangalia jinsi gani unalenga kupima mafanikio yake. Jinsi gani mwalimu atapima, tuseme, ukuzaji wa utu wote, yaani akili, viungo vya mwili na tabia.

(v)  Vifaa vya kufundishia

Muhtasari lazima uoneshe vitabu vyake vya kiada, baadhi ya vitabu vya ziada na rejea na zana za kufundishia mada mbalimbali.

4.3  Maazimio ya Kazi

Mwalimu unapopewa muhtasari wa somo lako (k.m. Kiswahili) kabla ya kuingia darasani una kazi ya kuzipanga mada kwa juma, mwezi, muhula au mwaka ili uweze kuzifundisha. Shughuli hiyo inaitwa kutayarisha maazimio ya kazi au kama ni moja ni kutayarisha azimio la kazi.

Azimio la kazi ni nini?

Azimio la kazi ni mpango wa muda mrefu wa mwalimu unaoonesha anachotazamia kufundisha katika juma, mwezi, muhula au hata mwaka mzima. Inategemea shule ambayo mwalimu anafanya kazi. Mara nyingi azimio la kazi linaandaliwa na walimu wa idara husika kwa pamoja k.m. idara ya Kiswahili.

4.3.1    Vipengele vya Azimio la kazi

 • Mwezi
 • Juma
 • Vipindi
 • Madhumuni
 • Mada kuu
 • Mada ndogo
 • Kazi za mwalimu
 • Kazi za mwanafunzi
 • Rejea
 • Vifaa vya kufundisha
 • Maoni.

4.4       Maandalio ya Somo

            Maandalio ya somo (au moja-andalio la somo) ni nini?

Andalio la somo ni mpango wa muda mfupi wa mwalimu anaoufanya usiku wa kabla ya somo. Andalio la somo linaeleza kinaganaga kitakachoendelea darasani. Mwalimu unachora jedwali kuonesha somo, mkondo, tarehe, saa, idadi ya vipindi na  idadi ya wanafunzi waliopo.

            Halafu unaandika

(a)    Mada kuu

(b)   Mada ndogo

(c)    Lengo kutokana na mada kuu

(d)   Madhumuni mahsusi kutokana na mada ndogo

(e)    Vitabu/makala ya rejea

(f)    Vifaa vya kufundishia

(g)   Hatua za somo zinazoonesha kazi za mwalimu na kazi za mwanafunzi

(h)   Maoni ya mwalimu baada ya somo.

Kila somo lina hatua za somo tofauti. Kwa mfano hatua za somo la Jiografia ni tofauti na hatua za somo la Kiswahili. Katika somo la Kiswahili mfano wa hatua za somo katika kazi za mwalimu ni:

 1. Utangulizi
 2. Maarifa mapya
 3. Hitimisho
 4. Tathmini.

Kwa mfano kama una mada ndogo: Utangulizi wa maelezo

Lengo kuu: Kufundisha namna ya kuandika utungaji wa maelezo

Madhumuni Mahsusi:

Baada ya dakika 80 kila mwanafunzi aweze:

(a)     Kutaja maswazo mbalimbali kutokana na kielelezo cha utungaji wa juu ya matunda.

(b)   Kujadili muundo wake.

(c)    Kuorodhesha maneno (msamiati) yaelezayo dhana ya matunda.

(d)   Kuandika utungaji wa maelezo juu ya mada watakayochagua kutokana na misingi iliyojadiliwa.

*Jadili na wenzako jinsi kazi za mwalimu zitakavyokuwa ili kutimiza madhumuni mahususi hapo juu.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!