Mfumo – Sauti

By , in Sarufi na Utumizi Wa Lugha on . Tagged width:

Mfumo – Sauti

Maarifa ya mjua lugha yanajitokeza katika viwango vingine vile vile. Kwa mfano ikiwa mjua Kiswahili atapewa neno baba, na akaambiwa aweke sauti nyingine (au herufi katika maandishi) badala ya ile ya kwanza, haya ni baadhi tu ya maneno ya Kiswahili anayoweza kuunda:

(17) kaba, saba, shaba

Ikiwa atabadilisha sauti ya pili, atapata:-

(18) beba, buba

Na ikiwa atabadilisha sauti ya tatu, anaweza kupata:-

(19) bata, bapa, baka, n,k.

Katika kuunda maneno ya hapo juu, kuna kanuni maalum ambazo mjua lugha anazifuata, na anajua kuwa mifuatano fulani inakubalika, na mingine haikubaliki kwa sababu haiwezi kuunda maneno ya Kiswahili. Hivyo kutokana na baba hawezi kuunda (20):-

(20) *abba, *bbaa, *aabb, *baab.3

3 Kila alama * inapotumika ina maana kuwa tungo hiyo haikubaliki katika lugha inayohusika.

Maarifa haya ya lugha yanamwezesha mjua lugha kutambua kuwa ingawa anaweza kufananisha sauti katika maneno tofauti ya lugha yake, si kila mahali anaweza kuzibadilisha, kama tulivyofanya hapojuu katika neno baba. Kwa mfano, hadhi ya sauti /a/ ya kwanza katika tungo ifuatayo ni tofauti na ile ya sauti /a/ za neno “baba”:-

(21) anaweza

Mzungumzaji anajua kuwa hadhi za sauti hizo ni tofauti kutokana na kutambua kuwa /a/ ya (21) inaweza kubadilishwana vipashio vingine vya kisarufi kama katika (21a):-

(21a) ninaweza; unaweza; tunaweza, n.k.

Hivyo mjua lugha anatambua kuwa sauti za lugha zinafanya kazi tofauti, hata kama hawezi kueleza kitaalamu kazi hizo ni zipi.

Hayu tuliyojadili hapo juu ni baadhi tu ya mambo ambayo tunamtarajia mjua lugha yeyote kuyamudu. Wala ujuzi huu si wa mtu mmoja, au wa mtu maalumu, bali ni wa kila mtu katika jamii ya watu wanaozungumza lugha moja; na kwa hakika, ni ujuzi ambao tunamtegemea mtu yeyote anayejiua lugha (ya wanandamu) kuwa nao. Lakini mpaka hapo, bado hatujajibu swali muhimu ambalo ni Ujuzi huu wa lugha ukoje? Na tukishajibu swali hilo, itabidi tujibu maswali mengine mawili ya ziada: Je, mwanadamu anaupataje ujuzi huo, na akishaupata, anautumiaje? Taaluma inayoshughulikia maswali haya inaitwa ISIMU.