Matumizi ya Dhana na Sanaa za Maonyesho za Jadi katika Tamthiliya za Leo

By , in Fasihi Simulizi on . Tagged width:

Matumizi ya Dhana na Sanaa za Maonyesho za Jadi katika Tamthiliya za Leo

E. Mbogo

Nia ya makala haya ni ku ma na kuchambua jinsi waandishi wa tamthiliya walivyozitohoa na kuzi ia dhana na fani mbalimbali za sanaa za maonyesho za jadi ili kuumoa tamthiliya zinazoakisi maisha ya leo. Fani tutakazozitazama ni zile za utambaji wa hadithi na nyimbo. Pamoja na fani hizi makala yatachambua matumizi ya dhana au ‘sayansi’ za uganga na uchawi katika tamthiliya hizi. Aidha makala haya yatachukua mifano kutoka tamthiliya chache tu ikiwa ni pamoja na zile zilizoandikwa na E. Hussein na Penina Muhando – waandishi wawili waliokwishachapisha tamthiliya nyingi kuliko waandishi wengine hapa Tanzania. Lakini swali letu la kwanza ni: sanaa za maonyesho za jadi zilikuwaje?

Hoja ya Taban kwamba sanaa za maonyesho ni fani ngeni na wala haikuwepo Afrika kabla ya ukoloni1 ni madai ambayo yameshakanushwa na wataalamu wengi. Sanaa za maonyesho za jadi zilikuwepo. Zilistawi katika mazingira ya mfumo wa uchumi wa kabla ya ubepari/ukoloni. Uwindaji, kilimo, ufugaji na hata kazi za ufundi ndizo zilikuwa njia kuu za kuzalisha mali. Katika misingi hii ya uchumi tasasi, falsafa, itikadi, itikeli, matambiko, dini, uchawi na sanaa mbalimbali zilistawi na kuakisi hali halisi ya maisha ya kipindi hiki. Maandishi hayakuwepo hivyo jamii iliwasiliana na kuhifadhi amali zao mbalimbali toka kizazi hadi kizazi kwa njia ya fasihi simulizi.

Sanaa za maonyesho za kipindi hiki, kama fani nyingine zote, zilikuwa sehemu ya maisha; sehemu ya uzalishaji mali. Hivyo sanaa za maonyesho za kipindi hiki zilitoa huduma katika shughuli za matambiko, kama vile maombezi dhidi ya magonjwa ya kutisha, mvua, njaa, n.k. Pia zilijitokeza katika shughuli za jando, unyago, arusi, tanzia na sherehe mbalimbali. Katika shughuli hizi watu walirindimisha ngoma na kucheza, waliimba, walitamba mashairi na kujigamba. Na wakiwa majumbani watoto na hata wakubwa walimzunguka bibi kumsikiliza akisimulia hadithi, visasili na matukio mbalimbali kuhusu historia ya kabila ama jamii yao. Lakini ukoloni ulikuja.

Walipofika wakoloni, serikali na taasisi zake za shule na dini zilifanya kila jitihada ili kudhalilisha na hata kuua utamaduni wetu. Wale Watanzania wachache waliokuwa na bahati ya kwenda shule walijifunza lugha ya kikoloni – aidha Kiarabu, Kijerumani au Kiingereza. Na mintaarafu mada yetu, walijifunza na kuigiza tamthiliya za Shakespeare na za waandishi wengine wa Kizungu. Huko vijijini na mijini watu waliendelea kuimba na kucheza ngoma zao. Waliendelea kutambika, kuwalea watoto wao katika jando na unyago, n.k. Zilikuwa tamaduni mbili katika jamii moja. Lenin anasema kuwa katika jamii yoyote yenye matabaka kuna utamaduni wa mnyonyaji kwa upande mmoja, na utamaduni wa anayenyonywa kwa upande mwingine. Na mikinzano hii ilibidi itafutiwe jibu, na jibu hilo lilikuwa katika mapambano ya kujikwamua toka makucha ya ukoloni wa Mwingereza.

Mapambano ya kujikwamua na ukoloni mkongwe yalikuwa na ncha mbili: ya kisiasa, na ya kiutamaduni. Ya kisiasa kwa maana kuwa tulikuwa tunatawaliwa na taifa la nje huku tukinyonywa uchumi wetu. Na kiutamaduni kwa sababu, mintaarafu kukandamizwa kwetu kisiasa na kiuchumi, kulikwamiza utamaduni, mila, sanaa na historia yetu kama Waafrika. Hivyo mapambano ya kuukombna utamaduni wetu yalikuwa ni mapambano ya kurejea katika mizizi yetu ya mila, desturi, falsafa na sanaa zetu za Kiafrika. Wakati huohuo tulipiga vita kila kitu chenye kuakisi utamaduni wa Kizungu na hata rangi ya Kizungu. Sanaa na sanaa za maonyesho za jadi zilijizatiti katika mapambano dhidi ya ukoloni. Nyimbo zilitungwa na ngoma zikachezwa. Kwa mfano, Makongoro alitunga wimbo akasema:

Majitu ya ng’ambo
Yenye ubeberu
Hatunayo haja tena
Tumekwisha yacheua, maisha!

Na hakika, kama asemavyo Makongoro 1961 Tanzania iliwacheua Waingereza na uhuru ukapatikana. Uhuru wa bendera ulifungua ukurasa mpya katika suala la utamaduni, ikiwa ni pamoja na medam ya sanaa za maonyesho na tanzu zake mbalimbali.

Katika tamthiliya mabadiliko na maendeleo hayakuja haraka. Wakitumia muundo uleule waliorithi toka kwa kina Shakespeare, waandishi wetu waliandika tamthiliya zao kwa lugha ya Kiswahili. Zaidi ya hayo tamthiliya hizi zilihusu masuala ya jamii zetu wenyewe.3 Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika tamthiliya, na hata riwaya na mashairi hapa nchini, ilikuwa ni bahati kubwa kwetu kwani nchi nyingine za Afrika kama vile Kenya, Uganda, Zaire, n.k., zilikuwa zinaelemea zaidi katika kutumia lugha ya Kimgereza au Kifaransa kuliko lugha zao za Kiafrika.4 Wakati wa mkoloni drama ilikuwa kwa ajili ya Wazungu na Waafrika wachache waliojua kukisema na kukielewa Kizungu. Lakini wanatamthiliya wazalendo polepole walianza kung’amua kuwa ili drama yao iwe na maana, ili waweze kuwasiliana na umma wa wakulima na wafanyakazi, iliwabidi watunge tamthiliya zao kwa lugha ya Kiswahili.

Lakini juhudi za kuusogelea na kuwasiliana na umma kisanaa hazikuishia katika matumizi ya lugha ya Kiswahili bali pia katika kuzitazama, kuzichunguza na hatimaye kuzifanyia majaribio sanaa za maonyesho za jadi zilianza. Tamthiliya za awali kama vile Wakati Ukuta, Heshima Yangu, n.k., hazina utohozi wa matumizi ya fani mbalimbali za sanaa za maonyesho za jadi. Lakini tamthiliya za kuanzia mwishoni mwa miaka ya sitini na mwanzoni mwa miaka ya sabini zilianza kuonyesha mwelekeo mpya, yaani matumizi ya fani za jadi kama vile utambaji wa hadithi, majigambo, ngoma na nyimbo. Pamoja na fani hizo falsafa na imani za Kiafrika (au za kipindi kabla ya ubepari) kama vile matambiko, miviga, visasili, uchawi, uganga, mashetani, miungu, mizimu, kupagawa, utabiri,5 n.k., zilitumika na waandishi wetu wa tamthiliya. Waandishi walikuwa wanaufuata na kuutumia mzizi wao wa jadi. Lakini je, wameutumiaje mzizi huo?

Tutazigawa fani na falsafa za sanaa za maonyesho za jadi katika makundi mbalimbali, lakini mgawanyo huu ni wa bandia, kwa kiasi fulani, kwani katika hali halisi fani hizi huingiliana. Hata hivyo tutautumia kwa matumaini kwamba utasaidia kufafanua suala hili.

Utambaji wa Hadithi

Hadithi zilitambwa na bibi au mama, aghalabu wakati wa usiku wa mbalamwezi. Watoto na hata wakubwa walimzunguka mtambaji sio tu katika kumsikiliza bali pia katika kuviona vitendo vya mwili wake vilivyogeza na kuigiza vitendo na vituko mbalimbali vya wahusika waliomo katika simo, kama vile watu, mazimwi, wanyama, fisi, sungura, n.k. Pamoja na burdani hii watazamaji, ambao walishiriki kwa namna moja au nyingine katika kumsaidia mtambaji, walipata mafunzo na maadili mbalimbali yaliyokuwemo katika hadithi hizi. Hussein anasema:

In the folktale there is common sense, reason, restraint and profound wisdom. There is the good, there is the evil. There is the struggle between the two and often, there is the triumph of the good and the defeat of the evil. There is poetry that is sung and prose that is narrated, all in an epic form where strings of drama are gently touched upon by instruments of magic and fantasy to effect pleasure and aesthetic education which is the enchantment of both child and adult.6

Aidha waandishi wetu wameandika tamthiliya zao kwa mtindo au umbo lilelile la KiAristotle na kupachika fani ya utambaji katika mtiririko wa drama, au wengine wamejaribu kuifanyia marekebisho madogo ili pamoja na upya walioutia, ibakie, kwa kiasi kikubwa, katika mtindo na umbo lake la asili.

Tutazame mifano kadhaa ya tamthiliya zilizotumia mtindo na umbo hili la utambaji wa hadithi.

Penina Muhando, katika Lina Ubani7 na Nguw Mama8 ametumia fam hii. Pamoja na tamthiliya hizo mbili, tamthiliya ya Harakati za Ukomooziiliyotungwa kwa ushirikiano kati ya Lihamba, N. Balisidya na Muhando mwenyewe pia imetumia fani ya utambaji.

Nguzo Mama ni tamthiliya inayohusu suala la ukombozi wa mwanamke: umoja wao, chama chao. Kwa hakika nguzo yao imelala chini na ni lazima waiinue na waisimike ili iweze kuwalinda, kuwatetea na kuwapa haki na maendeleo sawa na wanaume. Wanawake hawa wa Patata wakiwemo wakulima, wasomi, walimu, makahaba, n.k., wanaungana kuimarisha umoja na maendeleo yao. Wamefungua miradi mbalimbali kama vile kushona, kupika pombe, n.k., lakini kila mara miradi hiyo inavunjika kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na tofauti zilizopo kati yao kama vile uzembe, majungu, fitina na kutoelewana. Kama mwandishi anavyosema kupitia kwa Chizi:

Tuseme hii ni njaa iliyoingia Patata
Njaa ya kukosa umoja
Kukosa ushirikiano
Kuoneana wivu na uzembe kuzidia (uk. 32)

Tufikapo mwisho wa mchezo tunaiona Nguzo Mama bado imelala palepale; wanawake wameshindwa kuisimika. Kuna matatizo kadhaa ya kiitikadi katika tamthiliya hii, lakini tutalizingatia suala hilo baadaye. Sasa hivi tutazame jinsi Muhando alivyotumia fani ya utambaji wa hadithi katika tamthiliya yake.

Katika tamthiliya hii kuna watambaji wawili: nunoja ni Bi Msimulizi, na wa pili ni Chizi. Bi Msimulizi anaanza hadithi yake kwa mtindo uleule wa kale, bila shaka anaisimulia hadhira:

BI MSIMULIZI:

Hadithi! Hadithi!

HADHIRA:

Hadithi njoo!

BI MSIMULIZI:

Hadithi! Hadithi!

HADHIRA:

Hadithi njoo!

BI MSIMULIZI:

Hapo zamani za kale
Tena kale za mababu na mababu
Waliishi watu wema
Katika kijiji cha Patata (uk. 3)

Matumaini yetu na yale ya mwandishi ni kwamba hadhira ya leo itaitikia:

‘Hadithi njoo’. Lakini mara nyingi si hivyo. Ni jambo la kubahatisha tu.

Mazingira yamebadilika. Zamani mtambaji hadithi ni mtu aliyekuwa anafahamika na hadhira yake. Hadithi na hata nyimbo zilikuwa zinafahamika na wasikilizaji, kama siyo kwa wote basi kwa baadhi yao. Hadhira ilikaa karibu na kumzunguka mtambaji. Kulikuwepo na uhuru wa kuingilia kati mtiririko wa hadithi, watoto wakauliza maswali huku wakila mahindi ya kuchoma au karanga, ama wakifanya kazi nyingine ndogondogo za mikono. Zaidi ya yote Penina hapa ametumia muundo wa tamthiliya ya kigeni – thamthiliya iliyoundwa ili ichezwe katika jukwaa la kisasa lenye kuitenga hadhira upande mmoja (ukumbi), na waigizaji jukwaani. Na juu ya yote watazamaji wamewalipa waigizaji hawa ili wawaburudishe. Kwa maneno mengine kiungo kati ya msanii na mtazamaji ni pesa. Katika hali kama hii kuitaka hadhira iitikie. “Hadithi njoo!” au ishiriki katika nyimbo zilizomo katika hadithi ni muhali. Kuichukua fani hii na kuileta katika jukwaa la kisasa, kama asemavyo Hussein, “however imaginatively done is to subordinate taletelling as an art form into the one or the other art form”10 na matokeo yake yatakuwa tofauti.

Mtambaji katika Nguzo Mama anatumika kama kiungo kati ya waigizaji na watazamaji. Anafafanua matukio, hisia na mawazo mbalimbali yaliyomo katika igizo:

BI MSIMULIZI: Maandamano yakafanywa

Kwa vifijo na vigelegele
Kwa maelfu walimiminika
Gombe sugu likachezwa
Mkwajungoma na ngokwa
Roho zikasafishika za wao
Wana wa Patata
Lakini NGUZO MAMA katu haikusimama.

Hadhira haionyeshwi jukwaani maandamano haya yaliyojaa nderemo na vigelegele, badala yake wanayaona katika macho ya bongo zao kwa msaada wa Bi Msimulizi. Penina amemtumia Chizi kama mhakiki wa jamii juu ya yale yanayosimuliwa katika tamthiliya hii. Katika jamii za jadi na hata za leo mtu ‘chizi’ husema mengi ya kweli yanayoihusu jamii yake. Masuala nyeti kama vile utawala mbaya, dhuluma zinazofanywa na wakubwa, uonezi, ubarakala na masuala mengine ya kisiasa na kiuchumi ambayo watu wengine huogopa kuyasema hadharani chizi, msanii, au mtani huyasema waziwazi mbele ya kadamnasi. Bi Msimulizi anatufahamisha Chizi alikuwa ni mtu wa aina gani:

BI MSIMULIZI: Lakini alikuwepo mmoja hodari msanii

Walizoea Wapatata kumwita eti Chizi
Si kama kweli Chizi walimwengu huwawezi
Walimpa bilo jina kwa vile bila kujali
Mkubwa au kabwela, uwanjani au ufichoni
Ukweli alijisemea.
Kwa kupiga lake rimba
Maneno kuyapamba na Ngoma kujichezea
Ukweli alitoboa. (uk. 30)

Baadaye Chizi anatokea na kueleza kiini cha wanawake kushindwa kusimamisha Nguzo Mama na kuleta maendeleo: wivu na uzembe, na ukosefu wa umoja na ushirikiano. Chizi haingii ndani kuweza kuona kiim hasa cha unyonge wa mwanamke wa Patata. Kule kushirikiana, wivu, uzembe na ukahaba si msingi au chanzo cha matatizo ya unyonge wao. Msingi wa unyonge wao ni historia ya muda mrefu – tangu jadi – ya kukandamizwa na mfumo wa kiuchumi wa jamii za kipindi hicho, ikiwa ni pamoja na kugandamizwa na wanaume. Wakoloni walipoingia jamii nzima ya Watanzania iligandamizwa na kunyonywa, lakini mwanamke aligandamizwa na kunyonywa mara mbili; kwanza na hao wakoloni, na pili na wanaume. Leo katika Tanzania yenye mfumo wa uchumi wa ukolonimamboleo unaopiga kite chini za makucha ya ubeberu mwanamke bado ndiye anayeumia zaidi. Penina haonekani kuzingatia masuala haya ambayo ndiyo kiini cha unyonge wa mwanamke. Siyo Chizi tu, hata wahusika wengine, na hasa Bi Nane ambaye msomaji anapata hisia kuwa ndiye msemaji mkuu wa mwandislp, katika kutatua tatizo la mwanamke bado anapwaya sana, hayapigii mbizi za kisayansi masuala haya:

BI NANE: Kila mmoja afunge vizuri ikaze kabisa ili

wakati wa kuvuta kamba isifunguke. Tayari!
Haya sasa kila mtu ashike kamba yake. Hebu
tusogee kila upande (WANAJIPANGA) Loo!
kamba yako Bi Pili naiona fupi sana. Nisubiri
nikalete nyingine ambayo ni ndefu (anatoka (uk. 12)

Hicho ndicho kiwango cha kiongozi wa kina mama katika kutafuta mikakati ya kujikwamua na unyonge wao. Mtambaji hadithi anamaliza igizohivi:

BI MSIMULIZI: Kwa vile Chizi kakimbia

Hadithi tamalizia
Wakainua, wakainua
NGUZO MAMA palepale
Wakainua wakainua
Usiku na mchana
Siku ya pili ikapita
NGUZO MAMA palepale

(Kwa hadhira)

Sasa leo ni siku ya tatu
Niendelee, nisiendelee
Niendelee, nisiendelee
Niendelee, nisiendelee

(kimya)

HADITHI YANGU IMEKWISHA (uk. 59)

Ni kweli tukitumia fani hizi za jadi tunakuwa tumesogea karibu zaidi na hadhira yetu ya Kiafrika – ya wakulima na wafanyakazi – kwani mbinu na fani hizi za mawasiliano si ngeni kwao. Lakini hiyo peke yake haitoshi. Yatubidi tuongozwe na nadharia sahihi inayoweza kutufafanulia kiyakinifu masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, la sivyo tutakuwa ‘machizi’ tukipigana na vivuli badala ya matatizo halisi ya jamii yetu.

Katika tamthiliya ya Lina Ubani, Penina ametumia pia fani hii. Nyuma ya jalada la kitabu tunasoma kuwa Lina Ubani ni:

…tamthiliya ya kisasa ambayo maudhui yake yamechipua kwenye matatizo ya kiuchumi na kijamii yaliyojitokeza baada ya vita vya Kagera vya mwaka 1978-79. Vurugu, nugogoro na mikanganyiko inayosawiriwa katika tamthiliya hii, inadhihirisha wazi kwamba jamii hii ina uvundo, lakini kama linavyoonyesha jina la kitabu, uvundo huu ‘una ubani’, kinyume kabisa na la uvundo la Waswahili lisilo na ubani… Tamthiliya hii imejengwa katika misingi ya kisasa na kijadi huku ikitumia mtindo wa masimulizi, nyimbo na maombolezo (msisitizo E.M.)

Daudi ni mmoja wa wale askari wazalendo waliokwenda Kagera ili kukomesha uvamizi wa Idi Amin na hatimaye kumng’oa kabisa katika kiti cha uraisi fashisti huyo. Lakini katika harakati hizo Daudi hakurudi, alifia vitani. Mama yake (katika tamthiliya: Bibi) alipatwa na majonzi na kuweweseka, maradhi yaliyozidishwa na hali mbaya ya uchumi na mori wa kujenga ujamaa kwa kuwabomolea wakulima majumba, kung’oa mazao yao ya chakula na kisha kuwaswagia katika maeneo yaliyokuwa karibu na barabara hata kama ardhi yake ilikuwa imechakaa na gumba. Wakati Bibi akiomboleza na kuugua, tunaonyeshwa mabepari uchwara na wasomi wanavyofanya ‘juhudi’ ya kuinasua nchi yao katika janga hili la kiuchumi.

Nchi za Afrika, Asia na Latin Amerika zinalazimika, kwa namna moja au nyingine, kushirikiana na kupata misaada kutoka nchi za kibepari. Lakini kumekuwepo misimamo tofauti katika kuamua ni misaada ya aina gani na itumikeje. Mhusika Huila ni msomi anayeelekea kutaka nchi yake ichukue misaada ile tu itakayoifanya ijitegemee yenyewe katika nishati na maendeleo ya watu kwa jumla. Lakini Zoeni, kiongozi – bepariuchwara – ana mtazamo tofauti. Anadhani kuwa nchi yake itaendelea ikiwa itapata misaada mingi iwezekanavyo bila kujali matokeo na athari zake za baadaye. Katika mkutano wa kimataifa tofauti na mgongano kati ya Huila na Zoeni unajitokeza.

SAUTI:

Tutaendelea kupokea maoni ya wajumbe.

HUILA:

Mheshimiwa Mwenyekiti. Ujumbe wangu ungependa kutoa hoja kuunga mkono ulazima wa kuanzisha miradi itakayoziwezesha nchi zinazoendelea kuendeleza nishati zilizomo nchini mwao. Miradi iliyoorodheshwa katika muswada 2D ukurasa 312 hadi 415 haizisaidii nchi zinazoendelea kwa sababu inahusu nishati zinazohitaji teknologia ya hali ya juu na gharama kubwa sana. (Anaingia Zoeni na kukaa na kushangaa kuwa HUILA anazungumza). Tunaomba kutoa hoja kuwa miradi hii ifutwe na badala yake iingizwe miradi inayohusu kila nchi na nishati zake za ndani ya nchi. Ama sivyo nchi zinazoendelea daima hazitajitegemea. (Anakaa)

ZOENI

(Anachukia): Kakupa ruhusa nani kuzungumza? Wewe sio kiongozi wa ujumbe huu bwana Huila. Sasa umesema maneno gani mimi sipo? Hujasikia kitu protokali? Umesema nini? … Ndiyo maana mimi huwa nakataa kutangulizana na wasomi, fujo tupu. Sasa nitafanya nini eeh!

(uk. 9)

Migogoro hii inaendelea hata warudipo nyumbani toka mkutanoni, na mwisho tunaambiwa kuwa maradhi ya Bibi yalizidi akapelekwa hospitali ambako alifariki dunia. Tutarudia baadaye kuchambua msimamo wa kiitikadi wa Pemina lakini kwanza tutazame jinsi gani ameitumia fani ya utambaji hadithi. Kuna Mtambaji na kuna Bibi. Mtambaji ndiye mwenye hadithi akwasimulia watazamaji. Mtambaji anaanza hadithi kijadi:

MTAMBAJI: Paukwa
HADHIRA: Pakawa
MTAMBAJI: Paukwa!
HADHARA: Pakawa!
MTAMBAJI: Hapo zamani za siku hizi

Palitokea huyo bibi
Kama mnavyomuona
Peke yake kazaliwa
Wazaziwe wamekufa
Na nduguze kalelewa
Vizuri kaolewa, wanawe kajizalia
Madume mawili, Huila na Daudi
Huyo wa pili Daudi
Jeshini kajiunga
Kapten akawa
Sasa habari zimefika
Kule vitani alikokwenda
Daudi kajifia (uk. 2)

Mtambaji akisaidiwa na waigizaji anasimulia visa vya hadithi hii mpaka mwisho. Lakini mawasiliano yake ya moja kwa moja (ya kujibizana na hadhira) yanaishia katika ‘Paukwapakawa”, na mwisho wa mchezo anapowauliza watazamaji: “Niendelee nisiendelee!” (uk. 58). Hata katika nyimbo anazoziimba Bibi ni vigumu kwa hadhira kushiriki hasa tukizingatia kuwa hadhira haizijui nyimbo hizo.

Ili hadhira iweze kushiriki katika utambaji na uigizaji wa maigizo kama haya – hasa katika fani ya nyimbo, kucheza ngoma, kupiga makofi, kuitikia n.k. – yatubidi tuondoe tatizo la ‘ugeni’. Uigizaji usionekane kama ni kitu kisichoweza kufahamika au kueleweka kwa urahisi. Mazoezi na hata utunzi wa mchezo kwa kushirikiana na wananchi ni jambo muhimu katika kufanikisha fani hizi. Ngugi aliona na kulitatua tatizo hili katika lile jaribio maarufu la Kamiriithu. Katika igizo hili wananchi walishiriki katika kutunga na kuucheza mchezo wa Nitaolewa Nitakapopenda.12 Nyimbo, ngoma, na dhamira ya igizo yalikuwa mambo yaliyokuwa katika historia na utamaduni wa maisha yao. Kuhusu kuwashirikisha wananchi katika utunzi wa igizo la Kamiriithu Ngugi anaeleza:

The content of the play was asking many questions about the nature of Kenyan society and this generated ever more heated discussions of form and content during the entire period of the play’s evolution. Sometimes these involved not just the actual participation but the ever widening circle of the audience.

Auditions and rehearsals for instance were in the open. 1 must say that this was initially forced on us by the empty space but it was also part of the growing conviction that democratic participation even in the solution of artistic problems, however slow and chaotic it at times seemed, was producing results of a high artistic order and was forging a communal spirit in a community of artistic workers.13

Matumizi ya mtambaji katika tamthiliya yana faida na kazi yake nyingine. Mtambaji ni mtazamaji, ni ‘sehemu’ ya hadhira; hivyo hapa na pale, kadri mchezo unavyoendelea, hutoa maoni yake, huuliza maswali na kuchochea fikra za watazamaji ili waweze kuwaza na kuyapima yale yanayosemwa katika igizo. Katika kufanya hayo Mtambaji huzizuia bongo za watazamaji zisitopee na kujiainisha moja kwa moja na mangazimbwe yanayotokana na waigizaji ambao, aghalabu, nao pia huingia katika nafsi za wahusika wao. Hadhira na waigizaji wakishikana katika hisia za aina hii basi fikra huwa mtumwa wa vivuli. Brecht,14 yule mshairi maarufu wa karne yetu, aliitumia sana mbinu hii ya ukengeushi. Alitumia utambaji, nyimbo, filamu, mabango, slides katika maigizo yake aliyoyaita epiki ili kuwafanya watazamaji wayatafakari wanayoyaona.

Utambaji wa Mwanahego katika Lina Ubani umechangia vizuri katika kuleta mkengeuko huu wa kuuliza maswali, kutoa mawazo, kueleza woga na fikra za watazamaji kuhusu matatizo yajamii yao. Mwanahego, japo mlevi, anatumika na mwandishi kuyasema yale ambayo mtu mwenye “akili zake” ataogopa kuyasema kwa kuchelea rungu la dola:

MTAMBAJI:

Kilima cha Kusini

SAUTI:

Tufanye kazi kwa bidii maana naona tunalegalega. Tuzalishe mali zaidi ndipo tutaondokana na balaa…

MWANAHEGO:

(Kalewa kibao): Kamwambie baba yako hayo maneno ya ugoro. Usituambie sisi kutugeuza mabwege. Asiyefanya kazi wewe uliye juu ya kilima. Juu ya kilima kuna mashamba? Asiyefanya kazi baba yako, anayekula vya bure, unavyomletea wewe, unavyotuibia sisi… Shenzi taipu… Kama kuzalisha mali ni kusema kwa maneno yako tungeunda ndege. Basi niache Mwanahego niseme… kwa maneno yangu chakula kitoke hapa, mke wangu anirudie… Haya sema…” (uk. 45)

Huo ni uhakiki mkali wa “mlevi” kuhusu serikali yake, na kwa kweli maoni hayo ya mlevi ndiyo hasa maoni ya hadhira kwa jumla. Lakini je woga wa hadhira anauonyesha nani?

MTAMBAJI:

Watu wakatahayari

Huyu Mwanahego vipi?

Atafungwa walahi

(uk. 47)

Na woga wa mwandishi?!!Aaa! mlevi huyo

Mwacheni mlevi
Kama si mlevi, punguani (uk. 47)

Mwisho Penina anasema: lenye uvundo lina ubani, na ubani huo ni nini?

MTAMBAJI: Vibwebwe wamevifunga

Ngoma kuicheza
Wakapiga yowe
Ngoma tutaicheza
Itakuwa ubani
Uvundo kutuondolea
Wakaimba wakaimba
Ngoma wakazishika
Mikuki! Mishale!
Sime! Shoka! Mawe!
Huku wanaimba
“Hayoo, madyamini hayooo”(uk. 58)

Iwapo kucha za udhalimu na unyonyaji zimegota katika maisha ya wanyonge, dawa ni kuzing’oa ili kuikwamua jamii. Na mbinu ya mwisho na yenye uhakika ni ya kushika silaha. Hivyo ndivyo anavyotuambia Mtambaji wa Penina. Lakini kwa bahati mbaya mwandishi hatuonyeshi harakati na nafasi ya watu hawa wa chini katika kufusha mavumba ya uvundo ila maombolezo ya Bibi.

Hussein ni mwandishi mwingine ambaye ametumia fani mbili za fasihi simulizi katika Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi.15 Akiandika utangulizi wa kitabu hiki Shihabuddin Chiraghdin alisema, “Hizi tungo mbili mpya za Ebrahim Hussein ni mchanganyiko wa fasihi simulizi na fasihi andishi. Yaani katika tungo hizi mwandishi amechanganya miundo ya kiasili ya ngano na vitendawili na kuyageuza kivyake ili kututolea maandishi haya.16” Kinyume na Penina, Hussein hatumii fani hizi za fasihi gimulizi katika muundo wa tamthiliya, badala yake amesimulia tu akianza na paukwapakawa na kumalizia katika mtindo wa kitendawili akidai mji ili alifumbue fumbo. Utambaji wa hadithi, aghalabu, hutumia mazungumzo ya nathari lakini katika tungo hizi Hussein ametumia ushairi. Fauka ya hayo katika utambaji huu baadhi ya vituko na matukio ya hadithi yana athari ya majigambo. Kwa mfano: Mtemi aliyepewa jukymu la kumuua Sesota – joka la vichwa sabini – anasimuliwa hivi:

MTAMBAJI HADITHI
Basi
Kijana mkuki chini kaukita
Kaukita
Lile Joka Sesota’kaliita
Kaliita
Akaliita

Tena akaliita

Lakini Sesota kimya hakuitikia

Mtemi akaanza kuranda
Mkuki chini ‘nda ukadinda
‘Kutafuta mahali pakujichomea
Huku atanda
Huku aranda
Huku adanda

Pale kama mpira akijinyambukia
Mkuki mkononi ukachomoka
Ukachomoka
Kiwinguni nda’ ukajichomeka
Machozi y’kiwingu
Roho za watu zikajiburudishia (uk. 39)

Katika sehemu kama hizi Mtambaji (mwigizaji) anatakiwa aonyeshe kwa vitendo ufundi, mbinu na ushujaa alioutumia Mtemi kupambana na Sesota. Na katika kufanya hivyo atakuwa anachukua nafasi ya shujaa na kujigamba kama shujaa. Kwa kuchanganya fani tatu za fasihi simulizi: vitendawili, utambaji wa hadithi, na majigambo Hussein amepiga hatua kadhaa mbele katika kutumia utamaduni na dafina ya jadi ili kujadili masuala ya maisha ya leo.

Lakini ufundi wa Hussein hauishii katika ufinyanzi na sanaa, bali upo pia katika mtazamo na mkabala sahihi wa masuala ya kiitikadi. Tutumie mfano huuhuu wa Ngao ya Jadi kufafanua hoja hii.

Ngao ya Jadi ni hadithi ya asili kutoka kabila la Waganda. Tunaambiwa kwamba katika haditni hiyo kulikuwa na Waswa, mkulima, aliyejitokeza kumuua Sesota lililokuwa likikishukia kijiji cha Kalungu kila siku kukamata watu na kuwala. Waswa aliingia mwituoi kumtafuta Sesota na zumari na mtungi wake. Akaenda akamwimbia hata akamvuta kwa nyimbo mpaka mtungini – maneno matamu humtoa hyoka pangoni – akauziba mtungi akawaondoshea watu baa hilo, nao wakamshangilia sana na Waswa akapewa ujumbe wa Kalungu (uk. 4). Hussein anafanya mabadiliko mawili muhimu katika hadithi hii. Kwanza Sesota anafanywa kuwa na vichwa sabini; na pili, shujaa aliyepewa jukumu la kumuua Sesota hakutumia zumari na mtungi bali mkuki. Kwa nini?

Katika nusu ya pili ya karne hii suala la ukoloni mkongwe, ukolonimamboleo na ubeberu kwa upande mmoja, na ukombozi kutokana na makucha hayo kwa upande wa pili, limetoa changamoto kubwa kwa wapenda uhuru, amani na maendeleo kote duniani. Hapa Afrika, Dar es Salaam ilikuwa kitovu cha ukombozi wa nchi za Afrika zilizokuwa bado zinatawaliwa, hususan nchi za kusini mwa Afrika. Akiwa kama zao la jamii hii, maandishi ya Hussein yameakisi masuala hayo kwa undani wake unaostahiki. Suala la ubeberu, kwa mfano, linajitokeza wazi katika tamthiliya ya Mashetani kitabu tutakachokishughulikia baadaye.

Katika Ngao ya Jadi, Sesota, joka la vichwa sabini linawakilisha udhalimu, ukoloni, ukolonimamboleo na ubeberu. Waafrika walipigania uhuru wao wakaupata, wakashangilia:

‘Kaingia kitongojini
Shuwari na nyingi amani
Watu wakawa furahani
Watu wote kitongojini kila mmoja

Nyunyusa

Ngomaze ‘kazikaanga

Kina dada

Vibwebwe’ kavifunga… (uk. 45)

Lakini huo ulikuwa uhuru wa bendera, joka lile kwa hakika halikufa, lilitokomea:

Likatoa kelele zake
Miti yote karibu yake
‘Kivurunga kisha likatokomeya (uk. 45)

Hivyo baada ya muda nchi za Kiafrika ziligundua kuwa lile joka bado tulikuwa nalo, na sasa lina vichwa vingine vyenye vitimbwi na maangamizi makubwa zaidi. Huo ndio ubeberu anaouzugumzia Hussein. Ubeberu mgumu kupigana nao kwani unakuja na kunyonya nchi changa kwa kutumia mbinu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mashirika kama IMF, Benki ya Dunia, n.k., na hata kuwanunua viongozi wa serikali. Na hivyo ndivyo vichwa sabini vya ubeberu. Kama Hussein angelifuatisha na kunakili tu ile hadithi ya asili ya Kiganda kuwa Sesota ana kichwa kimoja, basi mtazamo huo ungekuwa finyu; suala la ubeberu lingerahisishwa. Harufu, hisia na unajisi wa ubeberu unatambwa kama hivi:

Punde si punde
Wakati si wak’ti
Alibaini
Tena alibaini
Sumu ya Joka
Kumbe ilibakia pale kijijini
Mwake mwili
Harufu chafu na najisi ilibakia! (uk. 46)

Jambo la pili la kimtazamo tulilolitaja ni uchaguzi wa mkuki badala ya zumari au filimbi na mtungi. Tunajiuliza: Kwa nini Hussein asitumie zumari kama ilivyo katika hadithi asilia ya Kiganda? Zaidi ya yote zumari na muziki zingekuwa tanzu mwafaka katika kulifanya igizo hili livutie macho na masikio ya hadhira. Lakini Hussein kageuza: kampa mkuki shujaa wake. Sababu iko wazi: jamii haibadilishwi kwa zumari. Mapinduzi na maendeleo hayawezi kuletwa na nyimbo, ngonjera, riwaya, mashairi, michezo ya kuigiza, n.k. Mapinduzi na maendeleo huletwa kwa kuzalisha mali katika misingi ya usawa. Wakati tungo hizi mbili zinamea katika bongo la Hussein, mapambano ya silaha kusini mwa Afrika yalikuwa yamepamba moto. Nyimbo, mashairi, ngoma, n.k., vilichangia kiasi kikubwa katika kufafanua, kuhamasisha na kuwatia mori wapigania uhuru na wapenda amani na haki kote duniani, lakini kwa hakika ni mtutu wa bunduki uliokomesha kiburi cha mkoloni na kuleta uhuru katika nchi za Angola, Msumbiji, Zimbabwe, Guinea Bissau, n.k.

Tunalo somo moja la kujifunza: kuwa fani za jadi zipo kwa ajili yetu, sio sisi kwa ajili ya fani hizo. Wandishi wanayo haki na uhuru wa kuzitumia wapendavyo ilimradi matumizi katika tungo zao yasaidie katika kuwatanabahisha, kuwahamasisha na kuinua mwamko sahihi wa kisiasa na Kiitikadi wa mamilioni ya Waafrika ambao hadi sasa bado maisha yao ni ya kimasikini, ya kutisha, na ya kusikitisha.

Sayansi ya Vchawi na Uganga

Ustadhi Safari Jumbe katika makala yake juu ya “Uchawi Katika Riwaya za Kiswahili” amejaribu kuthibitisha kuwepo kwa uchawi na uganga katikajamii yetu ya jana na hata ya leo. Mimi, katika makala haya, nitajifunga tu katika matumizi ya ‘sayansi’ hii katika tamthiliya.

‘Sayansi’ hii, kama zilivyo imani na falsafa nyingine za jadi, ilitamalaki na kutumika zaidi katika kipindi cha kabla ya maendeleo ya sayansi na teknologia na mfumo wa kibepari kwa jumla. Waafrika wa kipindi hiki walitumia uchawi na uganga kama vyombo, elimu na maarifa muhimu katika kupambana na mazingira yao. Ni maarifa yaliyokuwa yakitekelezwa kufuatana na sheria, utaratibu na miiko maalumu. Kama mwanasayansi wa leo, mganga ama mchawi alifanya ugunduzi na majaribio yake katika misingi ya kisababisha na matokeo. Kama mwanasayansi wa leo anasema: Hidrojeni na oksijeni matokeo yake ni maji; basi mchawi alisema kwa kufananisha: maiti au msiba unavuta watu wengi hivyo kipande cha maiti/sanda n.k. katika biashara matokeo yake ni kuvuta wateja wengi!! Hivyo misingi ya utendaji kazi ya mchawi/mganga na mwanasayansi inakubaliana hadi kiwango fulani.

Kuhusu mwelekeo wa kisayansi wa waganga na wachawi LeviStrauss anasema:

…to work out techniques, often long and complex, which permit cultivation without soil or alternatively without water; to change toxic rpots or seeds into foodstuffs or again to use their poison for hunting, war or ritual… There is no doubt, that all these achievements required a genuinely scientific attitude sustained and watchful interest and a desire for knowledge for its own sake.17

Uvumbuzi na maendeleo ya sayansi/ni maarifa mapya yaliyochukua pahala pa ‘sayansi’ ya uchawi na uganga. Leo, katika nchi za Ulaya, suala la uchawi na uganga halipo, na kama lipo ni hafifu mno. Lakini imani na matumizi ya uchawi na uganga katika jamii zetu bado vipo. Pamoja na hayo, kama nilivyosema nia ya makala haya ni kuchambua ufundi, uvakinifu na udhanifu wa tamthiliya zetu mintaarafu matumizi ya taaluma hii ya uchawi na uganga. Tuanze na Kinieketile.

Mapambano dhidi ya unyonyaji na ukatili wa Mjerumani katika mashamba yaliyolimwa kwa viboko na wazalendo kusini mwa Tanzania yalileta umoja kati ya makabila na kuzua mapambano ya silaha yaliyojulikana kama Vita vya Maji Maji. Hii ilikuwa sayansi ya jadi dhidi ya ile ya Mzungu. Kinjeketile alifahamika na kukubalika na jamii yake kuwa ni mganga mwenye uwezo wa kutibu, kutabiri na kufanya miujiza. Kwa kutumia vipaji hivi aligundua na kutengeneza uganga ambao alidai kuwa ungeweza kubadili risasi kuwa maji.

KINJEKETILE: Haya ni maji – maji ya maisha. Hii ni silaha yetu. Huu ni usinga wa nguvu. Mwenye kunywa na kupakaa maji haya hatadhurika na chochote. Risasi itakuwa maji juu ya mwili wa mwenye kutumia dawa hii. Sasa nguvu tunazo. Hizi za dawa, haya maji ni nguvu zetu. Radhi za mizimu tunazo. Waliopo huko Bokero wanasema neno moja. Mfukuzeni udongo mwekundu (uk. 15)

Itikadi ya maji iliwaunganisha wazalendo ili kupambana na ukoloni. Lakini uganga peke yake usingemng’oa mkoloni. Kinjeketile, au tuseme Hussein, anatambua mkabala sahihi wa suala hili. Mkoloni hang’oleki kwa uganga na uchawi bali kwa mapambano halisi. katika muktadha huu wa wakati wa uganga silaha na uchawi ni vitu viwili visivyoweza kutenganishwa; vinakinzana na kusaidiana ili kufanikisha lengo moja: kuung’oa ukoloni. Akisisitiza umuhimu wa mazoezi ya silaha kabla kina Kitunda hawajajitumbukiza katika medani ya vita, Kinjeketile anaonya:

KINJEKETILE: Tutampigaje?

Tujifundishe njia za vita. Tujifundishe kutumia bunduki. Tujipange tuwe askari – askari wetu wenyewe. Tukishakuwa na nguvu – nguvu zetu wenyewe – ndio tupigane na udongo mwekundu. Kitunda

KITUNDA: Nipo hapa
KINJEKETILE: Juu yako kufundisha vijana wetu, na wote wanaotaka, namna ya kupigana. (uk. 17)

Kwa maneno mengine ni kuwa katika dunia yetu ya leo, dunia anayoizungumzia na kuiandikia Hussein, mabadiliko, mapinduzi na maendeleo ya wanyonge hayataletwa na uchawi ama uganga bali kwa kuyakabili matatizo yetu kiyakinifu. Hussein ‘hakupagawa’ na mvuto wa nguvu na imani za uganga kama kichocheo cha bongo lake na ubunifu ili afinyange drama ya kuvutia, bali ameuchukua uganga wa jadi, uendao kichwa chini, na kuusimamisha utembee miguu ardhini! Na hiyo ndiyo moja ya kazi ya mwandishi wa leo.

Kuhusu matumizi ya hazina ya utamaduni wetu wa jadi Cabral anasema:

A return to the source can only signify the return to Africans the power to produce the means of their own welfare and hence the opportunity to recreate social and spiritual harmony at a higher level.19

Kama tutageuka nyuma na kuakisi kama kioo utamaduni wetu wa jadi bila kujiuliza mamilioni ya wanyonge watafaidikaje leo, basi tutakuwa tunapoteza muda. Katika igizo moja liitwalo Chakatu20 lililoonyeshwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkanganyiko katika matumizi na tafsiri ya uchawi na uganga katika fasihi ulijitokeza.

Igizo linahusu mfalme anayekabiliwa na wapinzani wa himaya yake – wapinzani ambao ni miongoni mwa baraza lake la mawaziri. Wapinzani hawa wanatumia uchawi kuupindua uongozi wa mfalme. Na mfalme naye anatafuta na kumtumia mchawi mwingine kuwagundua wapinzani wake. Mchawi wa mfalme anapiga ngoma ya uchawi (mkonikoni) na mara wachawi wanaanza kuathirika na kucheza ngoma ya kichawi. Kwa njia hii tishio la kuvuruga usalama na amani ya nchi linatoweka. Igizo hili, ambalo linatetea tabaka tawala, linauchukua uchawi kama ulivyo, wala juhudi hazifanywi za kujenga fikra na tafsiri mpya na yakinifu inayolingana na hali halisi ya leo. Wahujumu uchumi na wanyonyaji hawawezi kubainishwa na kung’olewa kwa kutumia mchawi au uchawi, lazima mwandishi afikirie zaidi ya hapo.

Soyinka, katika tamthiliya zake nyingi ambazo zimejikita katika utamaduni, dini, visasili, n.k., vya Wayoruba, ametokea kuwa na mwelekeo huu finyu kama mhakiki mmoja asemavyo:

One central difficulty is that he sees no distinction between wholly participating in a traditional culture and currently understanding such a culture. Although it would result in absurdities if such distinction were to be understood in an absolute sense, it is clear that immediately we want to understand and explain in a manner appropriate to 20th century con’-cerns, we must go beyond the concepts of participation in tradition. Such understanding is essential to revolutionary transformation.21

Tukirudi tena kwa Kinjeketile, Hussein anaona kuwa hata kama wazalendo watashinda vita hii, lakini kimsingi watakuwa bado hawajajikomboa, watakuwa watoto wa Seyyid Said. Seyyid Said anawakilisha ukoloni, ukoloni – mamboleo na hatimaye ubeberu – uwe wa Mwarabu, Mjerumani au mgeni mwingine yeyote. Fikra na utabiri huu sahihi hautokani na ubongo na fikra zake mwenyewe Kinjeketile. Ni ‘wahayi’ unaotoka kwa Hongo na yeye Kinjeketile anatumika kama “mtume”.

Dhana ya kupagawa, kukaliwa na mizimu, miungu, (majini – Waarabu?) ni matendo yanayotamalaki zaidi katika kipindi kilekile cha kabla ya maendeleo ya sayansi, teknolojia na viwanda. Mganga akipagawa huwa si yeye tena. Hajui analolisema; lakini jamii yake inajua na inaamini kuwa yale yatokayo katika kinywa chake ni maneno ya kweli. Akisisitiza na kufafanua hali ya bongo la mganga aliyepagawa Soyinka anasema:

Nor would we consider that such a communicant withdraws from conscious reality, but rather that his consciousness is stretched to embrace another and primal reality.22

Hali ya kupagawa ya Kinjeketile aliyompa mwandishi wake haikumfanya awe chapwa kimtazamo bali mhusika aliye tajiri wa haiba, sifa, fikra na falsafa zilizobobea na kuifanya kazi hii ya fasihi kuwa pevu na yenye kuhimili dharuba na tufani za wakati.

KITUNDA: Kama ulivyokuwa ukisema wewe unapohutubia, na unapofundisha, unasema lugha ngeni kama Kialabalabu

KINJEKETILE: Mimi
KITUNDA: Wewe
KINJEKETILE: Mimi?
KITUNDA: Ulisema kuwa sisi sote tutakuwa watu wa Seyyid Saidi.
KINJEKETILE: Mimi? Nieleze nilivyosema. Kila kitu tafazali.
KITUNDA. Ukasema tukisha shinda tutakuwa watu wa Seyyid Saidi.
KINJEKETILE: Tukishinda vita alafu tutakuwa watu wa Seyyid Said?
Chini ya Seyyid Said? Nilisema ivyo?
KITUNDA: Ndiyo. Je, unaumwa uso wako? Unakwenda wapi?

KINJEKETILE: Nimedanganywa. Wameniuwa, nimejiuwa mimi mwenyewe. Ilikuwa ndoto nikiota! Apana! Wamenidanganya! (Anapiga ukelele unafika mbinguni na kuanguka chini – GIZA) (uk. 19)

Tamthiliya nyingine inayotumia dhana ya uganga na uchawi ni Ngoma ya Ng’wanamalundi. Tamthiliya hii imejikita katika uchawi wa ndondocha au msukule. Msukule ama kizuu ni mtu “aliyekufa” kiuchawi, akazikwa, na usiku mchawi akaja kaburini kumfufua! Mchawi huyu humchukua mtu huyu hadi nyumbani ambako hufanya mambo makubwa matatu: Kwanza, kumkata ulimi asizungumze; pili, kumlisha madawa ya kuharibu ubongo wake ili asijijue, asifikiri wala kukumbuka alikotoka; na tatu, kumfuga na kumtumikisha kama mtumwa au mnyama. Inaaminika kuwa mtu akisha kuwa kizuu hatibiki. Lakini uchawi huu wa msukule unalingana kwa kiasi kikubwa na jamii inayokandamizwa, ikinyonywa na kutumikishwa, ikipigwa marufuku kutoa mawazo yake kwa hali yoyote ile. Udhalimu wa aina hii unaweza kuonekana katika nchi nyingi duniani. Lakini labda mfano uliokithiri hapa barani ni ile siasa ya ubaguzi wa rangi huko Afrika ya Kusini. Waafrika wamefanywa vizuu.

Katika lamthiliya ya Ngomaya Ng’wanamalundi mchawi aitwaye Chidama anamiliki idadi kubwa ya vizuu akiwatuma na kuwatumikisha katika miradi yake mbalimbali. Lakini kwa upande mwingine anatokea mganga Ng’wanamalundi ambaye anatumia ‘uganga’ wake kuwafanya vizuu hawa wajikomboe. Uganga huu si tunguri wala mavumba yatokanayo na mizizi na wadudu bali vita vya kutumia silaha. Hata tafsiri ya Ng’wanamalundi kwa Chidama si ya kiuchawi. Anamwona Chidama kama nguvu zinazowakihsha unyonyaji na udhalimu wa kila hali dhidi ya wanyonge. Anasema:

NG’WANAMALUNDI: (Kutoka chumbani. anakuja pale ukumbini kwa

fosi, anampiga yule nyoka kwa mgwisho wake. Anatulia. Sasa anamkamata na kuanza kunuiza na kusema naye)
Najua aliyekutuma
Lakini huyu si mume sawasawa ni mwanamke
Wewe ni tonga, hujawa tui bado Hu chochote bali garasa-
Shushu la nyoka mgonjwa (anamtemea mate)
Lakini nakutambua wewe u nani,
Najua ndiye wewe yule anukae damu ya maskini
Huwezi kunizuga kwa mavazi uliyovaa
Kwani sabuni na manukato
Havitoshi kutoharisha nuksi iliyoko Ndani ya kichwa, roho na matendo yako
Kwani nani hajui kuwa wewe ni Mchawi wa Msukule?
Nani hajui kuwa: wewe hupika vitumbua
Kwa maji ya kuoshea wafu ili vitoke?
Nani hajui kuwa: wewe hutumia
Kiganja cha mtoto aliyetanakali
Kuchotea na kuuzia vitumbua vyako
Nani hajui kuwa: wewe umeshonesha
Talasimu ya vinofu na vinyama vya
Uke wa yule hayati kigoli wa damu yako
Ili unate na kunatisha biashara zako
Kwa kufyonza damu za binadamu wenzako!(uk. 53)

Penina Muhando katika tamthiliya ya Hatia24 na Pambo25 ametumia waganga. Katika Hatia mwandishi anajadili suala la matatizo yawapatayo vijana waishio katika miji mikubwa kama Dar es Salaam; na kwamba baada ya yisa na mikasa hurudi au hushauriwa warudi vijijini wakalime. Cheja, msichana mhusika mkuu, anapewa mimba na kijana aitwae Juma ambaye anakana kuhusika na mimba hiyo. Cheja anaamua kurudi nyumbani. Huko nyumbani badala ya kumtaja Juma kama mhusika wa madhambi hayo anamtaja Sembuli aliyekuwa mlezi wake huko mjini.

Sembuli naye anawaambia wazee wa kijiji kuwa hahusiki. Ubishi huu unawarudisha katika imani na uganga wao wa jadi, yaani kiapo! Mganga (mwapishaji) anatayarisha kiapo cha mafuta yanayotokota: Sembuli atumbukize mkonowake humo. Kama hahusiid hataungua lakini kama kweli alimpa mimba Cheja basi atakiona cha mtema kuni. Wazee wanaamini hivyo lakini Sembuli haamini hivyo; kwa hiyo anagoma kutumbukiza mkono wake katika mafuta yanayotokota na badala yake anamtaja, kwa makusudi Mkami, kaka yake Cheja, kuwa ndiye aliyempa mimba dada yake! ‘Matusi’ haya yanazua mtafaruku na ugomvi mkubwa pale kijijini na mwisho Cheja mwenyewe anasema kweli na anaahidi kutorudi mjini bali kujiunga na kijiji cha ujamaa.

Suala la kurudi kijijini katika tamthiliya hii ambayo nadhani ndiyo iliyoandikwa kwa ustadi kuliko tamthiliya zake nyingine, liko nje ya muktadha wa makala haya, na fauku ya hayo wahakiki wengi wameshalishughulikia vya kutosha. Yatosha tu kutazama nafasi ya uganga na mganga katika tamthiliya hii.

Penina anatumia uganga kwa namna mbili: kwanza, kama ‘kitegezeo’ cha drama; na pili, kama tashititi dhidi ya uganga. Katika kitegezeo hiki tunajiuliza: Je, kama onyesho la kiapo lingeondolewa drama hii ingefika katika kilele chake cha mapigano? Jibu ni ndiyo: lile ‘tusi’ la Sembuli lingetosha kuamua ugomvi. Lakini hii haina maana kuwa onyesho la kiapo siyo muhimu; ni muhimu kwani ni kidokezo kinachoongezea taharuki katika igizo hili, taharuki inayochangia kulipa ‘tusi’ la Sembuli kwa wazee wa jadi uzito wake. Na Muhando hakuruhusu tambiko la kiapo litekelezwe. Kiapo kimebezwa na usasa:

MWAPISHAJl: (anamtolea macho ya ukali) Sembuli, usilete mchezo hapa. Sisi siyo watoto wadogo tunacheza.

SEMBULI: Na minri sina madhumuni ya kucheza vile vile. Ila nataka kusema neno litakalomaliza huku kutokuelewana. Mimi nasingiziwa tu.

MZEE I: Sasa apa basi halafu tuone ukweli wenyewe.

SEMBULI: Sina imani na mambo haya.

WOTE: Eeeeh!

SEMBULI: Lakini bila kuwabishia na mila zenu mimi nataka kuwaambia kuwa namfahamu mtu aliyemkosea mtoto wenu na mtamtaja hapa hapa (uk. 27).

Katika Pambo Mganga amepewa uwezo zaidi wa kutatua matatizo ya jamii yake. Pambo, mhusika mkuu, baada ya kusoma na kupata digrii yake Chuo Kikuu na kuingia ulimwengu akiwa amejawa na matumaini ya kupata fedha nyingi na kuishi maisha ya juu, anafadhaika kuona kuwa umbali kati ya hali halisi na ndoto zake ni mkubwa mno. Kichwa cha msomi huyu kinavurugika, anapata kichaa. Lakini ni kichaa gani hicho?

SAUTI:

Kichaa… Kicha… Kichaa

Lakini siyo kichaa cha kutumia nguvu kufanya madhara, bali zaidi kichaa cha mawazo. (uk. 34)

Katika hali halisi ya nchi kama Tanzania msomi mwenye shahada hahesabiwi katika tabaka la watu wa chini: yeye ni mmoja wa wale wachache, chambilecho Nyerere, wenye bahati kubwa ya kupata elimu ya juu. Katika Pambo, Pambo na rafiki zake wawili Pesa na Raha (vijana wadogo) ambao nao wameathiriwa na fikra za Kipambo wanatoweka majumbani na kukimbilia maporini huko wakicheza ngoma za kiwendawazimu. Wazazi na ndugu zake, ambao wanawakilisha tabaka la chini la wafanyakazi na wakulima, wanawafuata; wakifanya kila juhudi ya kuwaokoa. Pamoja na mbinu nyingine nyingi, inayofanikiwa kuwaokoa ni ya mganga:

BABA PAMBO: Au labda tujaribu kupata msaada wa mganga.
BABA PESA na
BABA RAHA: Eheee! Wewe umesema kweli kabisa.
BABA RAHA: Kwa nini hatukufikiria jambo hili tangu awali?
BABA PESA: Mganga anaweza kuwazinga na kuwarudisha nyumbani (uk. 30)

Wazee hawa wanampata Mganga na kurudi porini kuendelea kuwasaka akina Pambo. Nyimbo za wagonjwa hawa zinaposikika Mganga anawatayarisha wazazi kwa kuwavalisha njuga:

(Wote wanasikiliza. Akina Pambo wanasikika wanaimba kwa mbali)

BABA PESA: Ndiyo wenyewe, hata mimi nasikia
BABA PAMBO na
BABA RAHA: Kweli! Hao! Hao!

MGANGA: Sasa kazi inaanza (Anatoa filimbi kama ile ya Pambo… Anatoa na njuga anawapa wote) Vaeni hizi upesi. Tutawafuata nyuma nyuma. Kila wakiimba na sisi tutaimba kuwaitikia na tukiimba tutachezesha njuga hizi na mimi nitapiga hii filimbi kama wanavyofanya.

WOTE: (Wanashangaa) Hee! Nini!

MGANGA: Vaeni hizo njuga upesi na mfuate ninavyowaambia. Sisi tutaimba tuni tu, siyo maneno, fanyeni upesi kabla hawajatupoteatena (wanavaa njuga zao miguuni) (uk. 40).

Katika kuimba na kucheza wanawavuta akina Pambo hadi nyumbani. Huko nyimbo na ngoma zinachezwa kwa nguvu zaidi. Wagonjwa wanacheza hadi wanazirai:

KIKUNDI B: Pambo niko shidani leo
Rafiki mmoja simwoni
Pambo gani
Wa wa wa ewaa

(Pambo anaendelea kwa unyonge) Pambo! Pambo! Pa… Pambo! eee! eek! Paaambo! (Anazirai)

Baadaye nyimbo zinaendelea, Pambo anazinduka. “Amechoka” na ile sura ya kichaa imemtoka. Halafu polepole anaanza kuimba” (uk. 55) Mwishoni mwa mchezo Mganga anamaliza kwa kusema haya:

MGANGA: Na hapa ndipo matumaini na jitihada zetu zinapopata uso mpyauso wa matumaini, uso wa ushindi. (uk. 56)

Matatizo ya kina Pambo ni matatizo ya mfumo wa elimu, pamoja na hali halisi ya kiuchumi na kisiasa iliyopo nchini. Ili kuzuia vichaa vya aina hii visitokee inabidi mfumo wa uchumi na elimu vibadilishwe. Tuwe na mfumo wa uchumi unaoweza kuleta maendeleo sio tu kwa kina Pambo wenye madigrii, bali pia kwa tabaka la wakulima na wafanyakazi. Lakini Penina anafikiri kuwa matatizo haya yanaweza kutatuliwa nchi ikapata ‘uso mpya, uso wa matumaini, uso wa ushindi’ kwa kutumia uganga na uchawi. Kichaa cha Pambo ilikuwa ni ishara ya kueleza matatizo halisi ya jamii yetu wala si kichaa halisi kilichohitaji mganga.

Hussein naye alikuwa na ‘kichaa’ wake (Kitaru) katika Mashetani.26 Lakini kinyume na Penina Muhando, Hussein hayatibu maradhi ya Kitaru kwa kutumia mganga au daktari, japo njia hizo zinagusiwa hapa na pale. Hussein anamtibu kwa vitendo:

KITARU: Juma, iko njia
JUMA: Njia! Njia gani?
KITARU: Yote yalianza katika mchezo…
JUMA: Yote yalianza katika hadithi.

KITARU: Ukitaka hivyo basi, yote yahanza katika kitendo. Kilianza kitendo, zikaja hadithi. Hadithi zikafanya mchezo ambao ni kitendo… Ikiwa yote yalianza katika mchezo huu ambao ni kitendo, basi iawabu iko katika mchezo huu huu. Tukiucheza, na kuucheza, na kucheeza, mwisho wake itatoka sumu yake. Natukiweza kuucheza bila ya kuuhisi maumivu vake, basi…

JUMA (anatikisa kichwa). Unajua kama hayo unayoyasema ni maneno tu? Sumu haitoki katika mchezo, bali katika kitendo – kitendo cha kila siku.

KITARU: Kitendo cha kila siku, maisha ya kila siku yanabadilishwa na watu.

JUMA: Lakini siyo vijitu viwili. Kwa heri (uk. 56) (msisitizo wangu)

Maradhi ya Pambo, Kitaru, uozo wa jamii, umasikini, n.k., vinaweza kuondolewa kwa vitendo, na sio vitendo vya watu fulani wachache bali tabaka la umma wa wakul’-ma na wafanyakazi.

Hitimisho

Katika makala naya tumetazama jinsi waandishi wa tamthiliya walivyozitonoa na kuzitumia fani za fasihi simulizi, utambaji wa hadithi, na nyimbo. Pia malumizi ya sayansi ya uganga na uchawi yametazamwa. Mizam ya mjadala kuhusu suala hili imeonyesha mambo mawili: kwanza, kuwa ili sanaa zetu za maonyesho ziwe karibu zaidi na wananchi, ziweze kuwaburudisha na kujadili matatizo yao kinagaubaga, haitoshi tu kutumia sanaa hizi za jadi bali pia zitumike kwa ubunifu na uyakinifu zaidi. Pili, kuwa ili kuendeleza matumizi na utohozi wa fani hizi za jadi, kila inapowezekana waandishi wetu washirikiane na wajifunze zaidi kutoka kwa wenye kuelewa sanaa hii – yaani wakulima na wafanyakazi.

Tanbihi

1. Taban lo Liyong (1983) katika The Drama Review, Volume 25 No. 4 (T 92) Winter 1981, uk. 3.

2. Wimbo huu niliupata toka kwa Mama Pala, mmoja wa waimbaji wa zamani wa Mzee Makongoro.

3. Tamthiliya za mwanzoni zilizoandikwa kwa Kiswahili na Watanzania ni Wakati Ukuta na Alikiona.

4. Miaka ya karibuni Ngugi wa Thiong’o amekuwa anatetea sana matumizi ya lugha za Kiafrika katika kazi za fasihi. Soma Ngugi (1986) Decolonising the Mind – The Politics of Language in African Literature. Heinemann, Nairobi.

5. Tunaweza kuzungumzia pia tanzu kama vile: methali, vitendawili, nahau, n.k., lakini makala haya hayajadili suala hili.

6. E. Hussein (1976) “TaleTelling as a Performing Art,” katika Semina “Theatre and Social Reality” iliyofanyika kuanzia tarehe 14 hadi 27 Juni, 1976 uk. 50.

7. Penina Muhando (1984) Lina Ubani, DUP, Dar es Salaam.

8. Penina Muhando (1982) Nguzo Mama. DUP, Dar es Salaam.

9. A. Lihamba, Ndyanao Balisidya na Penina Muhando, (1982) Harakati za Ukombozi. TPH, Dar es Salaam.

10. Hussein, m.y.k. uk. 51.

11. Penina Muhando (1984). Maelezo yaliyoandikwa nyuma ya jalada la kitabu.

12. Neugi wa Thiong’o (1982) Nitaolewa Nikipenda. HEB, Nairobi.

13. Ngugi wa Thiong’o (1986) m.y.k., uk. 56.

14. J. Fiebach, (1975) Von Graig bis Brecht. Henschelverlag, Berlin.

15. E. Hussein (1976) Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi. OUP, Dar es Salaam.

16. Shihabuddin Chiraghdin (1976) “Utangulizi” katika Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi. OUP, Nairobi, uk. 1.

17. C. LeviStrauss, (1968) The Savage Mind. The University ofChicago Press, Ghicago, uk. 14.

18. Hussein E. (1969) Kinjeketile. OUP, Dar es Salaam.

19. B. Jeyifo (1985) Tragedy, History and Ideology in Marxism and African Literature, ed. Guge Iberger. James Currey Ltd., London, uk. 74.

20. Chakatu. Watunzi na Waigizaji: Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo, 1986/87.

21. Jeyifor m.y.k., uk. 75.

22. Wole Soyinka (1976) Myth, Literature and theAfrican World. Cambridge University Press, London, uk. 33.

23. E. Mbogo (1986) “Ngoma ya Ng’wanamalundi”, (MS).

24. Penina Muhando (1976) Hatia. East African Publishing House, Dar es Salaam.

25. Penina Muhando (1975) Pambo. Foundation Books Ltd. Nairobi.

26. E. Hussein (1971) Mashetani. OUP, Dar es Salaam.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!