MASWALI YA MAJADILIANO (USHAIRI)

By , in Ushairi on . Tagged width:

Maswali ya Majadiliano

1. Kwa maudhui yake TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA SAADANI na MASHAIRI YA CHEKA CHEKA ni vitabu vilivyopitwa na wakati”. Thibitisha au kanusha kauli hii ukitumia vitabu viwili kati ya hivyo.

2. Chagua vitabu viwili kati ya TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA SAADANI na MASHAIRI YA CHEKA CHEKA kisha chambua kila kimoja kwa kuunyesha mafanikio katika fani na maudhui.

3. Mwandishi anatazamiwa kuelimisha jamii. Chagua vitabu viwili kati ya TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA SAADANI na MASHAIRI YA CHEKA CHEKA, ueleze kila kimoja kilivyofaulu au kushindwa kuelimisha jamii.

4. Fasihi hujengwa kwa fani na maudhui. Chagua vitabu viwili kati ya TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA SAADANI na MASHAIRI YA CHEKA CHEKA, ujadili jinsi matumizi ya lugha yalivyosaidia kujenga au kufifisha kazi hizo.

5. Jadili msimamo wa kisiasa wa washairi wawili kati ya Semghanga (TEUZI ZA NFASI), Kandoro (MASHAIRI YA SAADANI) na Mvungi (MASHAIRI YA CHEKA CHEKA).

6. Fafanua matumizi ya lugha katika vitabu viwili kati ya TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA SAADANI na MASHAIRI YA CHEKA CHEKA.

7. Kwa kutumia vitabu viwili kati ya TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA CHEKA CHEKA na MASHAIRI YA SAADANI, jadili suala la mapenzi juu ya nchi yao waonyeshayo washairi.

8. Linganisha na/au tofautisha fani ya mashairi na tenzi zilizomo katika vitabu viwili kati ya TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA SAADANI na MASHAIRI YA CHEKA CHEKA.

9. Jadili dhamira na ujumbe wa vitabu viwili kati ya MASHAIRI YA SAADANI, TEUZI ZA NAFSI na MASHAIRI YA CHEKA CHEKA.

10. Fafanua fani iliyotumika katika vitabu viwili kati ya vilivyotajwa vya TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA CHEKA CHEKA na MASHAIRI YA SAADANI, ukizingatia muundo na matumizi ya lugha.

11. Ushairi wa Kiswahili kama tanzu nyingine za fasihi una kazi ya kuadilisha, kuadibisha na kuelimishajamii inayoandikiwa. Kwa kutumia vitabu viwili kati ya TEUZI ZA NAFSI, MASHAIRI YA SAADANI na MASHAIRI YA CHEKA CHEKA, jadili usemi huu.

12. Washairi uliosoma vitabu vyao wanaonekana wana uwezo mkubwa kiutunzi na hazina kubwa ya lugha. Kwa kutumia MASHAIRI YA SAADAN, TEUZI ZA NAFSI au MASHAIRI YA CHEKA CHEKA jadili kauli hizo kwa kyzingatia muundo na matumizi ya lugha.

13. Eleza maana ya istilahi zifuatazo:

· Takriri,
· Methali
· Sitiari
· Tashihisi
· Tashibiha
· Onomatopeia
· Tasifida
· Nahau
· Vitendawili
· Utenzi na Ushairi

14.

(a) Eleza kazi za takriri

(b) Taswira ni nini?

(c) Kuna aina ngapi za taswira.

 

Mbinu za Kujibu Maswali

Wanafunzi na watahiniwa wanapopata swali katika mitihani wanajukumu kubwa la kulielewa kabla ya kulijibu.

Endapo mtahiniwa atakuwa anajibu swali lolote bila kulielewa matokeo yake ni hasara; atashindwa mitihani! Kushindwa si lengo la mtahiniwa yeyote yule. Ili kukwepa hilo, mtahiniwa lazima awe makini.

Mara nyingi maswali yanayoulizwa kwa watahiniwa ni yale yanayozingatia mkondo maalum. Mtahiniwa anaweza kuambiwa aanzishe, abainishe, ajadili, aeleze, alinganishe, ajadili, aeleze, alinganishe, afafanue, aonyeshe, atofautishe na kadhalika. Tunadokeza mbinu kadhaa ambazo ni za msingi katika kujibu maswali ya mtihani.

· Maswali ya Kujadili

Kujadili ni kuhoji, kuuliza au kusaili. Suala la kujadili linahusu pande mbili. Kwa nini jambo limetokea? Kwa kawaida hutolewa kauli fulani ambayo mwanafunzi anatakiwa akubali au akatae; au yote kwa pamoja. Ni muhimu kuelewa yafuatayo:

· Swali linataka nini hasa?
· Je, kuna mambo chanya?
· Je, kuna mambo hasi? Yepi ambayo yanatakiwa kutajwa?

· Maswali ya Kulinganisha

Kulinganisha kunahitaji mambo makuu mawili. Mambo haya ni

(a) Yale yanayoeleza kufanana kwa vipengele vilivyo katika vitu tofauti na

(b) Kutofautiana kwa mambo katika vitu hivyo viwili. Baada ya kulinganisha kama swali linavyotaka, hatua nyingine muhimu ni kuangalia ufanisi wa kazi zote/vitu vyote viwili.

Maswali yanatakiwa yajibiwe kwa kufuata mtindo wa insha. Kila kipengele kinachojadiliwa kinatakiwa kihusishwe katika vitabu vyote ambavyo vinahusishwa katika swali.

Sasa tutoe mifano ya maswali na majibu ambayo mawanafunzi anatakiwa kuyatoa. Maswali yote yanayojadiliwa yapo katika sehemu III hapo juu.

· Swali Na. 4

·Jibu

FANI ni jumla ya mambo mengi yanayoiunda kazi ya sanaa ya fasihi. Mambo hayo ni pamoja na matumizi ya lugha, wahusika na ujenzi wake, matumizi ya mazingira na muundo na mtindo. Aidha, kwa minajili ya swali letu, tutaangalia matumizi ya lugha.

Matumizi ya lugha ndiyo yanayofanya kazi ionekane ya kisanaa na wala si vinginevyo. Katika Mashairi ya Cheka Cheka na Teuzi za Nafsi matumizi ya lugha katika vipengele kadhaa yamesaidia kuimarisha kazi hizo za kifasihi. Lakini kuna pia nyakati ambapo lugha imedunisha kazi ya fasihi.

Tukianza na Teuzi za Nafsi, kwa mfano, kwanza tunaona mshairi ametumia mbinu mbalimbali za kisanaa. Mbinu hizo ni pamoja na takriri, matumizi ya tanakali sauti [anomatopeia], mkato wa maneno, matumizi ya tamathali za usemi na kadhalika.

Kwa upande wa takriri za maneno, Teuzi za Nafsi imezitumia kwa kiasi kikubwa. Takriri za aina hii zimejitokeza sana hasa katika utenzi wa Ewe Mama Mpenzi. Japokuwa mbinu hii ya takriri – neno inaweza kuchukuliwa kama mbinu mojawapo ya kisanaa, katika utenzi huo mbinu hii imekithiri kiasi cha kuonekana kuwa ni udhaifu wa msanii katika kazi yake.

Diwani ya Mashairi ya Cheka Cheka nayo inatumia pia mbinii hii ya kurudiarudia maneno. Mfano unaoweza kutolewa hapa ni wa shairi la “Moyo” (uk. 13) ambalo lina takriri neno moyo. Katika shairi hili, takriri neno moyo limeipa nguvu za kisanaa kubwa shairi zima.

Mbinu nyingine inayojitokeza katika Teuzi za Nafsi ni ile ya matumizi ya Onamatopeia [tanakali sauti]. Mbinu hii huiga sauti au mlio wa chombo chochote katika kuimarisha sanaa ya kazi ya fasihi. Mfano ni ule unaojitokeza katika ubeti wa 95, ambapo inaelezwa kuwa bunduki ililia “tusu”, na kisha ‘sina habari ya “ndusu”. Maneno haya tusu na ndusu yanaiga mlio wa bunduki.

Mashairi ya Cheka Cheka yanatumia mbinu hii ingawa siyo kwa kuonekana sana. Kipengele hiki kimetanya nguvu ya kisanaa ipungue katika diwani hii ya Mashairi ya Cheka Cheka.

Suala la ukataji wa maneno linajitokeza pia katika Teuzi za Nafsi. Maneno mengi katika Teuzi za Nafsi yanakatwa hasa pale yanapotumiwa ili kuunda mizani na vina. Kwa mfano katika ubeti wa 188, tunasoma neno akinuiza badala ya kuniuliza. Hali hii ya kuunda maneno kwa mbinu za ukataji maneno ina athari zake, zikiwemo zile za kuunda maneno ambayo yanaweza yasiwe na maana, au yanaweza kuwa ni matusi. Hali hii inasaidia kudunisha hadhi ya Teuzi za Nafsi.

Mashairi ya Cheka Cheka ni diwani ambayo nishairi wake ametumia pia mbinu hii ya ukataji wa maneno kama ilivyo katika Teuzi za Nafsi. Ukataji wa maneno unafanywa kwa lengo la kulinganisha mizani na pengine kuunda vina maalumu ambavyo mshairi wake anavihitaji. Imethibitika kuwa maneno yanayoundwa katika Mashairi ya Cheka Cheka yanatoa athari mbili muhimu: neno linaloundwa linaweza kupotosha maana, na pili, neno linaloundwa linaweza kuonekana kimaumbile kuwa ni jipya.

Baadhi ya maneno katika diwani zote mbili yametolewa kutoka maneno mbalimbali ya lugha za kikabila au lugha nyingine ambazo si Kiswahili. Kwa mfano, katika Teuzi za Nafsi, ubeti wa 124 kuna neno liitwalo mkalola. Neno lola linatokana na lugha za kibantu likiwa na maana ya ona au tazama. Maneno mengine yanayojitokeza na ambayo yanatumika katika Teuzi za Nafsi yana asili ya Kiarabu na kadhalika.

Kwa upande wa Mashairi ya Cheka Cheka tunayakuta maneno ya aina hii katika shairi la “Chunguzeni walo Mbele” (uk. 17). Aidha, mashairi mengine yana maneno yatokanayo na lugha za Kibantu. Aidha kuna matumizi pia ya tashtiti.

Lugha imeimarishwa zaidi na matumizi ya tamathali za usemi. Katika diwani zote kuna matumizi ya tashbiha, sitiari, tashihisi, n.k.

Tukianza na tashibiha, tamathali hii ambayo hulinganisha vitu viwili au zaidi kwa kutumia maneno “kama” mithili ya “mfano wa” “kama kwamba” n.k. imetumiwa na washairi wote. Mashairi ya Cheka Cheka kwa mfano ina mifano kadhaa katika (uk. 5) “Na wasiothaminiwa, wapimwao kama nyasi”. (uk. 7) “Mlevi akakolea, kama matumbakuya toza” (uk. 13), “Moyo kiburi hatari, mfanowe kama radi”, na mengineyo.

Katika Teuzi za Nafsi tashibiha inajitokeza katika beti kadhaa. Mifano dhahiri inajitokeza katika ubeti 48, “Vile vile nazo nyusi, Mithili wino mweusi”, ubeti 55 “Shingo isiwe nyembamba, wala ndefii kama kamba”, ubeti 56, “Awe na chema kiunzi, kisicho kama cha penzi”, na kadhalika.

Tamathali nyingine ni tashihisi ambayo kwayo vitu hufanywa vitende kama binadamu. Mbinu hii, kama zilivyo tamathali nyingine, zikitumiwa huleta nguvu za kisanaa katika kazi ya kifasihi inayohusika. Katika diwani ya Mashairi ya Cheka Cheka kwa mfano, mifano michache tunaweza kuitaja hapa. Angalia kwa mafano. Katika “Wewe kimoyo sikia mbona unanipa tabu?” (uk….12) “Moyo jifunze busara, iwe ndiyo taa yako”, (uk. 13) “Moyo usiwe jeuri, makini kwa hekima” (uk. 13) “Unayofanya si kweli, njiwa wacha tafrani”.

Teuzi za Nafsi ni diwani yenye tamathali hizo pia. Kwa mfano katika ubeti wa 105 tunasoma mwandishi akisema.

Ewe ua la upole
Mlezi wa tangu kale

Kifungu cha maneno Ewe ua ni tashihisi. Mifano ya aina hii iko mingi kitabuni.

Sitiari ni tamathali nyingine muhimu inayolinganisha vitu viwili au zaidi vyenye sit’a tofauti, kama ilivyo katika tashbiha, lakini tofauti yake ni kuwa tamathali hii haitumii maneno ya viungo. Katika diwani ya Mashairi ya Cheka Cheka mifano tunayoweza kuitoa ni kama:

Dhuluma ndiyo hekima…..
Utu umekuwa kima…..
Hafai huyo Mnyama….
Kadhalika, tafakari mshairi uwe nyati
Nchi takumbwa najuto la watu kuwa farasi (uk. 3)

Kwa upande wa Teuzi za Nafsi, yako matumizi kadhaa ya aina hii. Kwa mfano katika ubeti wa 186 ambako mshairi anasema:

Nasema aya kwa raha
Ewe yangu tashbiha
Sitiari hapa ni Ewe yangu tashbiha.

Vipengele vilivyojadiliwa hapa ingawa ni vichache, vinaonyesha jinsi ambavyo washairi wamejitahidi kuvitumia katika kujenga athari mbalimbali. Matumizi ya tamathali za usemi kwa mfano yamefanya waandishi kujenga taswira kwa upande wa msomaji. Ingawa taswira za Mashairi ya Cheka Cheka si nyingi, lakini zinajipambanua waziwazi katika mafungu ya taswira zionekanazo [Tuambae Ukasuku (uk. 31)] taswira za hisi [Kuna Nini Huko Ndani? (uk. 4)] na mwisho zile za mawazoni [Kimoyo u.k. 12]

Katika Teuzi za Nafsi taswira zenye athari mbalimbali nazo zimejengwa. Aidha, ikilinganishwa na Mashairi ya Cheka Cheka tenzi hizi zina taswira nyingi za kihisi.

Matumizi ya lugha kwa upande mwingine hayakuwa ya kiwango cha juu sana katika kazi zote mbili. Jambo hili limesababisha kazi hizo zionekane kutofanikiwa kwa kiwango chajuu.

Maoni:

Swali hili lilihitaji mjadala unaohusu vipengele vya fani katika vitabu vyote viiwili. Juhudi imetanywa kufafanua vipengele hivyo na kwa hali hii kuwapa welewa wanafunzi.

Swali la 3

Jibu

SUALA la mwandishi wa fasihi kuelimishajainii limekuwa hapa kama mwavuli. Jambo lililotakiwa pengine litamkwe hapa ni lile linalohusu nat’asi ya fasihi katikajamii; kwamba inaweza kujenga au kupotosha. Kitendo hiki kinaweza kuchukuliwa katika undani wake kuwa fasihi huelimisha.

Vitabu vya Teuzi za Nafsi na Mashairi ya Cheka Cheka vina mambo muhimu katika jamii na kimsingi yako mambo mengi yanaielimisha jamii. Kwa mfano, suala la kisiasa linajadiliwa kwa mapana katika vitabu vyoteviwili. Katika Mashairi ya Cheka Cheka suala la siasa limejitokeza na kutoa welewa mpana kwa wananchi. Kitabu hicho kinaelezea mbinu za wananchi za kutetea haki. Mashairi ya Cheka Cheka ni diwani inayomhimiza Raisi Mwinyi kutetea haki, na wananchi wamejifunza kuwa kumekuwa na ukiukaji wa haki miongoni mwa jamii. Mshairi anawaelimisha wananchi kwa kusema kwa mtano:

Tumaini la wanyonge, kwamba ipo serikali
Ila nchi ya inazonge, ya mwenye meno makali
Wanyang’anyao matonge, Wanyonye hawana hali
Mwinyi ukiwa mkali, ndio raha ya raia.

Kwa upande wa demokrasia, jamii inazidi kuelimishwa kuwa baadhi ya watu wanakuwa wakandamizaji, wengine, wanapenda kuzungumza zaidi kuliko vitendo.

Suala la kuwepo kwa vyama vingi au chama kimoja ni jambo jingine linalojadiliwa pia. Mshairi anaeleza kuwa kitendo cha kung’ang’ania kuwa na chama kimoja cha kisiasa ni cha kumnyima mtu demokrasia. Mhariri katika shairi moja anasema:

Mezikwa deinokrasi, Chaina kiinoja ndo’ ngao
Watu hawana nafasi, kutetea nchi yao
Mawazo ya ukakasi, inawazo ya mtitio (uk. 2)

Mshairi alishaona umuhimu wa kuwa na vyaina vingi. Alishaonya na kuwaelimisha wale walioogopa vyama vingi (kabla havijaruhusiwa) kwa kusema:

Waogopa vingi vyama, ni hofu ya kumbuka
Maovu yanayofuma, kwa dharau na dhiliaka
Vyama vingi vingcpewa, na kutwea madaraka
Pasipo uhuru huo, ulu upo mashakani (uk. 2)

Elimisho hilo lilishawafikia na linaendelea kuwafikia wananchi. Tunasubiri utekelezaji kama ulivyokwisha onekana.

Suala la rushwa na ulanguzi linakemewa pia na mshairi. Jambo hili linajadiliwa kwa mapana katika diwani mbalimbali za mshairi huyo. Kutokana na rushwa na ulanguzi, watu wameweza kupata magari, majumba ya kifahari, maisha ya anasa wakati mkulima na wavuja jasho wengine wanazidi kudidimia na kuteseka katika maisha yao.

Dawa ya jambo hili, mshairi anashauri na kuelimisha kuwa:
……. walaji wapigwe vita,
…. hawa dawa yao radi.
Mwinyi unda zako mbinu, iwe dawa ya kudumu (uk. 1)

Pamoja na maelezo hayo, kuna pia dhamira nyingine kama vile uzembe na ukasuku, matumizi ya fedha ovyo na kadhalika.

Kwa upande wa siasa Teuzi za Nafsi nayo imechambuajamii na kutoa mafiinzo mengi. Katika kitabu hicho, kuna tenzi mbili: Siasa Yetu na Vjamaa Kijijini ambazo zinachambua jamii kisiasa. Utenzi wa Siasa Yetu unajaribu kulinganisha siasa ya Tanzania katika kipindi cha baada ya uhuru. Siasa ya msingi inayojadiliwa hapa ni ya wakati wa vijiji vya ujamaa na ile ya kuheshimu usawa wa binadamu. Siasa hii imesaidia sana kuleta utulivu na amani miongoni mwa wanajamii ambao wameelimishwa na mazingira yao.

Teuzi za Nafsi inajaribu kuonyesha pia nafasi ya mwanamke na haki yao katika jamii. Aidha, kuna hoja kwamba mtu asiwe mtumwa wa kuwafanyia kazi wengine.

Kama Uivyo katika Mashairi ya Cheka Cheka kuna dhamira nyingine kama vile mapenzi, elimu na malezi, na kadhalika katika diwani hiyo.

Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kuwa waandishi wote wamefanikiwa kuwaelimisha wanajamii kwa viwango mbalimbali na katika vipengele mbalimbali.

Jambo la muhimu kulieleza nikuwa waandishi wote wamefanikiwa kuvielezea baadhi ya vipengele vizuri kuliko vingine. Kwa mfano, katika kipengele cha siasa Mashairi ya Cheka Cheka mwandishi amefafanua vyema, wakati katika Teuzi za Nafsi hajafanya uchambuzi wa kina. Tofauti hizo zimesaidia kutoa athari mbalimbali kwa kazi hizo. Tunasema kwa kuhitimisha kuwa waandishi wamejitahidi kuielimisha jamii kwa viwango mbalimbali.

Maoni

Swali hili lilikuwa la kimjadala. Lilihitaji kujadiliwa vipengele kutoka vitabu vyote viwili kama ilivyoonyeshwa katika mjadala. Aidha, mwanafunzi anaweza kupanua mjadala bado kwa kuelezea kwa kirefu dhamira na mafunzo kutoka kila kitabu.

Swali la 10

Jibu

FANI ya Teuzi za Nafsi na Mashairi ya Cheka cheka katika vipengele vya muundo na matumizi ya lugha inaweza kuelezwa kwa ufasaha na kwa uftlpi kila pale panapowezekana.

Tukianza na mjadala wajumla, Teuzi za Nafsi ni ushairi wa utanzu wa tenzi wakati Mashairi ya Cheka Cheka ni ushairi wenye misingi ya unne au tarbia. Kimuundo, utenzi na shairi ni kazi zinazotofautiana.

Katika utenzi kama ilivyo katika Teuzi za Nafsi, kuna vifiingu mbalimbali vinavyoitwa beti. Beti za utenzi hugawanyika katika mistari iliyo sawa. Wakati mwingine kunaweza kuwe na tenzi zenye mistari zaidi ya ile ya kawaida minne iliyozoeleka kama katika ule utenzi wa Siasa Yetu ambao una mistari mitano. Mashairi ya Cheka Cheka ni diwani yenye mashairi yaliyogawanyika katika vifungu vinavyoitwa beti. Kila ubeti kimsingi una mistari minne.

Kwa upande wa vina na mizani, Teuzi za Nafsi ni kitabu chenye tenzi ambazo zina vina vya mwisho tu. Aidha, tenzi zote, ukiondoa ule wa Siasa Yetu zina mizani minane kwa kila mstari. Mstari wa nne una kituo maalum kinachopatikana kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho wa kila titenzi. Kituo hicho huitwa bahari. Mashairi karibu yote katika diwani ya Mashairi ya Cheka Cheka ni yale yenye vina vya kati na mwisho. Vina hivyo vinajitokeza kila baada ya mizani minane. Kwa kawaida, kila mstari wa shairi au utenzi hugawanyika katika vipande au silabi ambazo huitwa silabi. Mstari wa kawaida wa shairi la unne una mizani kumi na sita, wakati utenzi wa kawaida una mizani minane.

Tenzi za Teuzi za Nafsi ni ndefu kuliko mashairi yale ya diwani ya Mashairi ya Cheka Cheka. Unaweza kupata shairi la ubeti mmoja. Katika hali ya kawaida, tenzi nyingi zina beti zisizopungua mia moja, wakati shairi refti sana kwa kawaida halizidi beti hamsini. Aidha, beti za tenzi hazijitoshelezi. Huwezi kwa mfano kupata utenzi wa ubeti mmoja, wakati katika ushairi kama ule wa Mashairi ya Cheka Cheka ni jambo linalowezekana kabisa.

Washairi wa tenzi mara nyingi huanza uandishi wao kwa kuomba dua kwanza. Jambo hili si la kawaida sana katika ushairi. Hivi kimsingi ni vipengele vya kimuundo katika Teuzi za Nafsi na Mashairi ya Cheka Cheka.

Baada ya kuangalia vipengele vya kimuundo, sasa tuangalie kipengele kingine cha kifani kinachohusu matumizi ya lugha. Katika Teuzi za Nafsi mwandishi wake ametumia mbinu za kisanaa za jumla na tamathali za usemi. Jambo hili limefanywa pia na Mashairi ya Cheka Cheka.

Tukianza na mbinu za kisanaa za kawaida, mshairi arnetumia mbinu za takriri – mbinu ile ya kurucliarudia maneno, miundo na kadhalika ili kusisitiza jambo. Kuna takriri za aina nyingi – takriri mistari, vina, mizani na kadhalika. Mashairi ya Cheka Cheka pia imetumia mbinu hizo.

Matumizi ya Onomotopeia, yaani mbinu ile ya kuiga sauti mbalimbali za watu, wanyama na vyombo ni mbinu ambazo zimetumika katika kazi hizo pia.

Suala la ukataji wa maneno na washairi linajitokeza pia miongoni mwa kazi hizo mbili. Ukataji wa maneno unafanywa ili kujenga vina au kupunguza mizani ikibidi.

Kwa upande mwingine, yako matumizi ya maneno ambayo si sanifu, au yale ambayo yana asili ya lugha nyingine. Teuzi za Nafsi kwa mfano kuna matumizi ya maneno kama lola (mkalola) na kadhalika, si sanifu, ni neno la Kibantu. Mashairi ya Cheka Cheka nayo imetumia maneno ya namna hii. Kuna baadhi ya maneno ambayo yana asili ya lugha nyingine kama vile Kiarabu na kadhalika.

Matumizi ya tamathali za usemi katika kazi zote mbili yamefanya yasaidie kujenga taswira mbalimbali. Tamathali zinazojitokeza katika Teuzi za Nafsi ni pamoja na tashihisi, yaani tamathali ile inayokipa kitu uwezo wa kimtu (mf. Ubeti 106. Ewe Nyota, ubeti 101: Ewe Ua n.k.) Tamathali hizo zinajitokeza mara kwa mara katika tenzi hizo. Aidha, Mashairi ya Cheka Cheka nayo yana tamathali za aina hii. Tamathali nyingine ni ya tashibiha. Hii ni tamathali ambayo hulinganisha vitu viwili au zaidi kwa kutumia vitu viwili au zaidi kwa kutumia maneno: kama, mfano wa, mithili ya, na kadhalika. Teuzi za Nafsi na Mashairi ya Cheka Cheka vimetumia tamathali ya aina hizo. Kwa mfanb, Teuzi za Nafsi ina mfano kutoka ubeti 48 Mithili wino mweusi, ubeti 55, wala ndefu kama kamba ubeti 56, Kisicho kama cha panzi na kadhalika kutoka Mashairi ya Cheka Cheka kuna mifano kadhaa, kwa mfano, wapimwao kama nyasi, (uk. 5), kama tumbaku ya toza, (uk. 7) mfanowe kama radi, (uk. 132) na kadhalika.

Tamathali ya sitiari, yaani tamathali inayolinganisha vitu viwili au zaidi kama ilivyo tashibiha, lakini haitumii maneno ya viungo kama ilivyo katika tashibiha, inajitokeza katika kazi zote mbili za Teuzi za Nafsi, na Mashairi ya Cheka Cheka. Katika Mashairi ya Cheka Cheka tuna mifano: Dhuluma ndiyo hekima utu umekuwa kima. Au mifano mingine: Kadhalika tafakari, mshairi uwe nyati (uk. 3) Nchi takumbwa na juto, la watu kama farasi (uk. 3). Tunaweza kusema kuwa ziko tamathali nyingine mbalimbali ambazo zinasaidiakujengataswira mbalimbali katika ushairi mzima. Katika Mashairi ya Cheka Cheka kwa mfano tuna tamathali zinazojenga taswira za aina tatu. Taswira zionekanazo, taswira za hisi na taswira za mawazoni. Mifano na maelezo ya taswira hizo yametolewa katika sehemu ya uchambuzi. Katika Teuzi za Nafsi taswira za aina hii pia zinajengwa. Jambo linalowatofautisha washairi hawa wawili ni mtindo wa lugha wanayotumia na muundo wa kazi zao za kishairi.

Tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa ingawa Teuzi za Nafsi na Mashairi ya Cheka Cheka ni kazi za kishairi zilizo ehini ya mwavuli mmoja wa ushairi, mtindo na muundo wake, pamoja na matumizi ya lugha kwa ujumla umezifanya kazi hizo kuwa na upekee kwa kila mojawapo.

Maoni

Swali hili limejibiwa kwa kugusia vipengele muhimu vilivyoulizwa. Aidha, jambo linalojitokeza katika jibu hili ni kuwa limekuwa refti, huenda wanafunzi wasiweze kujibu kirefu kama ilivyofanywa hapa. Jambo la msingi ni kupata nini kinatakiwa na kisha kujibu kwa haraka na kifupi inavyowezekana.

Swali la 5

Jibu

SIASA ni dhamira ambayo imepata kujadiliwa kwa mapana na wanafasihi mbalimbali, wakiwemo washairi Saadan Kandoro, F. Semghanga, na T. Mvungi. Misimamo ya washairi hawa inakubaliana na kutofautiana katika vipengele mbalimbali. Ili lcuthibitisha hoja hiyo, tuangalie vitabu viwili vya Mashairi ya Saadani (S.A. Kandoro) na Mashairi ya Cheka Cheka (T. Mvungi) kuhusiana na dhamira ya siasa.

Tukianza na Mashairi ya Saadani diwani hiyo ina msimamo wa kuitetea jamii ya Tanzania katika misingi ya uzalendo. S.A. Kandoro anaiangalia siasa ya Tanzania katika hatua mbili: hali wakati wa ukoloni na hali baada ya uhuru.

Wakati wa ukoloni mkongwe, mazingira ya wananchi hayakuwa ya kuridhisha kwa watu wengi wa Tanzania. Kwa kuzingatia hali hiyo S.A. Kandoro alitumia kalamu yake kuandika mashairi yaliyotoa mwito wa kuwaunganisha wananchi wapambane dhidi ya ukoloni huo mkongwe. Msimamo wa Kandoro ni kutetea unyonge kwa kila hali. Yako mashairi kadhaa yanayosimama kama mfano, likiwemo shairi la “Ondoka Nchini Mwetu” (uk. 141).

Raia wamekutana, mbelc ya wakubwa wetu
Raia tumeungana, kuunda taifa letu
Na sisi tuwe inabwana, kutawala nchi yetu
Ondoka nchini mwetu, mwishoni mwa mwaka nuu.

Mshairi katika shairi hili la beti saba anawahimiza Waingereza kuondoka nchini mwetu wakati kipindi cha kupata uhuru kilipokaribia.

Msimamo mwingine wa Kandoro ni ule wa kutaka amani na mshikamano na umoja. Kwa mfano katika shairi la “Siafu Wamekazana” (uk. 138), mshairi anawashauri watanzania kuwa na umoja katika mapambano ili kuweza kufanikiwa.

Msimamo wa mwandishi wa Mashairi ya Cheka Cheka kabla ya ukoloni hauonekani kutamka lolote la msingi. Labda hii inatokana na kweli kuwa kwa kiasi kikubwa utendaji wake, yaani mwandishi wake ameanza kuandika ushairi wake baada ya uhuru.

Baada ya uhuru, tunaona mabadiliko yakifanywa na jamii na hivyo kuathiri kazi ya usanii. Kandoro mara alipoteuliwa kuwa Area Commisioner ushairi wake umehusishwa na siasa zaidi. Hii ilikuwa baada ya kufanya kazi sehemu mbalimbali sfirikalini na mashirikani. Katika kuonyesha mapambano yao, Kandoro anasema kumpongeza J.K. Nyerere wakati alipokuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika:

Mola wetu muongoze, kisitoke kiti hicho
Vikingo sisikingize, Nyerere panua macho
Kusudi tusipooze, tuchangamke tumacho
Nyerere pokea hicho, kiti cha nchi kitunze (uk. 145)

S.A. Kandoro anaendelea kusisitiza masuala mbalimbali, mengine yanaendelezwa kuanzia wakati wa ukoloni. Tunaweza kuhitimisha kwa kutaja mambo ambayo yanaonyesha msimamo wake, ambao ni:

Ili kuwa na amani na maendeleo ni lazima pawepo na umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa nchi hii.

· Kandoro anatetea haki; na msimamo wake ni kuwa kama mtu atanyimwa haki yake ataipigania.

· Msimamo wake kuhusu maisha ya watanzania ni kuwa wanatakiwa kulinda uhuru na usiwe na ubaguzi wa rangi.

· Kandoro anaamini na ana msimamo kuwa hakuna mapambano yasiyo na wasaliti. Baadhi ya watu wanasaliti juhudi za wananchi, jambo ambalo ni lazima lipigwe vita.

Kuna upande wa Mashairi ya Cheka Cheka mshairi anaonekana akitetea haki kwa wananchi wa Tanzania. Mshairi anamshauri Raisi kuwa mkali anayelinda haki kwa nchi yetu. Msimamo wa mshairi unapitia ubeti ufuatao:

Tumaini la wanyonge, kwamba ipo serikali
Ila nchi ya mazonge, ya wenye meno makali
Wanyang’anyao matonge, wanyonge hawana hali
Mwinyi ukiwa mkali, ndio raha ya raia

Suala la demukrasia pia linajitokeza sehemu mbalimbali katika diwani hii. Lakini mshairi anaona demokrasia lazima iambatane na ukweli na sio maneno matupu tu!.

Msimamo wake kuhusu vyama vingi au chama kimoja ni kuwa mshairi anapendelea kuwe na vyama vingi. Msimamo huu ni mpya kwani wakati mrefu uliopita Tanzania ilikuwa chini ya chama kimoja. Hali hii, yaonyesha mshairi haikumftirahisha, ndipo akataka pawepo na vyama vingi katika msimamo wake wa kisiasa.

Kwa kubitimisha, tunaweza kusema kuwa washairi wote wana misimamo ambayo inatetea maslahi ya jamii yao. Ni misimamo sahihi inayotakiwa kwa wasanii.

Maoni

Swali hili limejibiwa kwa kugusia vipengele mbalimbali. Vipengele hivyo si lazima viwe vyote, lakini vinatosha kwa kutoa mwanga kwa wanafunzi ambao wanatumia jibu hili kama mwongozo wa kupanua mawazo kuhusu swali hili.

***

· TEUZI ZA NAFSI
· MASHAIRI YA CHEKA CHEKA
· MASHAIRI YA SAADAN

DAR ES SALAAM UNIVERSITY PRESS

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!