MAMBO YA MSINGI  KUFANYA ILI KUMUDU MTIHANI WA FASIHI

By , in Kidato I-IV Kidato V-VI on . Tagged width: ,

MAMBO YA MSINGI  KUFANYA ILI KUMUDU MTIHANI WA FASIHI

UFAHAMU wa muda mrefu nilionao katika kufundisha, kutahini na kuusahihisha mtihani wa fasihi katika kiwango cha kitaifa unaniaminisha kwamba hakuna swali lolote ambalo halijawahi kutungwa na Baraza la Mitihani nchini (NECTA) katika miaka yote ya uwepo wa Hati ya Kuhitimu Kisomo cha Sekondari (CSEE/ACSEE).

Kubwa zaidi ambalo NECTA imefanikiwa kufanya ni kubadili mbinu za utahini mwaka hadi mwaka, nami nikiamini kwamba hakuna mwalimu na mwanafanzi ambaye hajaigundua siri hiyo. Wajuzi wa lugha husema, hamadi kibindoni silaha mkononi.

Nasema hivi kutokana na uhakika kwamba mfumo na mtindo wa kutahiniwa kwa maswali ya NECTA umesalia ule ule kwa miongomingi iliyopita na sidhani kama kutakuwa na tofauti yoyote mwaka huu.

Ili nisiyakoseshe dira makala haya, ningependa kutumia jukwaa hili kusema na watahiniwa wote wa mwaka huu kwa kuwadokezea vipengele watakavyokutana navyo katika karatasi ya mtihani wa fasihi, jinsi ya kuyahimili maswali yenyewe na kisha niwashajiishe kwa kuwahakikishia kwamba hakuna geni watakaloliona hapa lililo tofauti na yote ambayo tayari wamesisitiziwa na walimu wao tangu watie miguu katika kidato cha kwanza.

Ninalenga kufafanua vitengo ambavyo mtahiniwa wa mwaka huu akivizingatia kwa makini atakuwa katika nafasi nzuri ya kuzoa alama nyingi katika fasihi.

Mara nyingi wanafunzi hufanya vibaya katika karatasi hii kwa kutojua ni vipi karatasi yenyewe hutahiniwa na kusahihishwa.

Mtihani wa fasihi hushirikisha Riwaya, Tamthiliya, Ushairi na Fasihi Simulizi.

Mtahiniwa anatarajiwa kusoma, kuelewa maagizo yote na kuchukua muda wake kuyateua maswali vizuri kabla ya kuihusisha mbinu ya kalamu yake.

Usiwe na pupa ya kuyakimbilia maswali ambayo huna uwezo wa kuyajibu kwa usahihi na ukamilifu.Kutulia kabla ya kuanza kujibu maswali kutakupa muda wa kuyazamia maswali yenyewe, kuyafasiri vilivyo na kuandaa vidokezo muhimu vitakavyokuongoza katika kuyawasilisha majibu yako kwa mtindo ufaao.

Inatarajiwa kwamba uwe umevisoma vitabu teule na kuvielewa vilivyo kabla ya mtihani wa fasihi. Ufahamu finyu wa yaliyomo ni hatari na aghalabu humfanya mtahiniwa kukosa kutambua baadhi ya vipengele kama vile dondoo fiche na wahusika wadogo au wajenzi.

Katika hali hii, mtahiniwa huishia kukariri tu msuko wa matukio kwenye hadithi fupi, riwaya au tamthiliya nzima bila ya kuwasilisha hoja zinazostahili kulijenga jibu lake.

Utaratibu wa kuwasilisha jibu

Ni sharti mtahiniwa azingatie utaratibu mwafaka katika kuwasilisha jibu lake. Anza kwa hoja, ifafanue hoja yenyewe na kisha uitolee hoja hiyo mifano kwa kurejelea kitabu husika. Hoja hizo zinastahili kupangwa kwa uwazi katika aya. Kwa kifupi utaratibu huu tuuite (HOMAMI-yaani Hoja, Maelezo na Mifano).

Kila aya itangulizwe kwa hoja. Usichanganye vipengele katika aya au kuzitaja hoja nyingi kwa pamoja katika aya moja. Ufichaji wa hoja utakunyima alama muhimu hasa ikizingatiwa kwamba ‘huenda mtahini asizione hoja hizo ulizozificha’.

Unashauriwa kuepuka matumizi ya lugha chafu itakayokubainisha kama mtovu wa nidhamu. Badala yake zingatia matumizi ya lugha fasaha iliyosheheni tafsida.

Epuka kuwarejelea wahusika kwenye kitabu kwa ujumla. Mtaje mhusika kwa jina lake kamili jinsi lilivyoandikwa kitabuni au kwa cheo na nafasi anayoishikilia katika jumuiya ya utunzi.

Pania kuelewa tofauti baina ya sifa au tabia za wahusika na umuhimu wao katika kazi ya fasihi. Umuhimu wa mhusika hubainika unapoirejelea dhima anayoitekeleza.

Sifa za wahusika ziwe kwa hali yakinishi

Unapotaja sifa za wahusika, ni muhimu kuziweka katika  uyakinishi. Mtahiniwa ataadhibiwa iwapo atatumia ‘vikanushi’.

Ni kosa kusema kwa mfano ‘Bw. Ecko’ ‘hana huruma’. Badala yake, sema Bw. Ecko’ ni ‘katili’. Usiseme Amani ‘si mwoga’ badala yake sema ni ‘mkakamavu’ au ‘jasiri’.

Epuka matumizi ya istilahi za jumla katika kubainisha sifa za mhusika kama vile ni ‘mkandamizaji’, ‘dhalimu’, mwenye utu na huruma’, ‘mnyanyasaji’, nk.

Zitumie vyema kurasa za kijitabu cha majibu huku ukiepuka kufutafuta sana kazi yako. Kufuta kwingi kuna maana ya kubabaika, kukosa umakini, kunakili kazi ya mwingine au kukosa uhakika wa kile unachokifanya.

Ni vizuri kwa mtahiniwa kutenga muda mwafaka kwa maswali anayoyajibu. Dakika 30 zinatosha kwa mtahiniwa kuwasilisha jibu la swali moja kwa umakini unaostahili.

Hii ina maana kwamba saa tatu zinatosha kuyajibu kwa ukamilifu maswali yote yaliyokusudiwa na hatimaye kuyapitia majibu kwa minajili ya kuyahakiki vilivyo.

Mtahiniwa aelewe kwamba ‘maswali huru’ (ya insha) katika fasihi ni hatari zaidi kuliko yale ‘funge’ (ya muktadha au dondoo). Kwa hivyo, ni muhimu kuandika na kufafanua hoja zote anazozijua wakati wa kuyakabili maswali ya aina hiyo.

Usijitegemeze kwa idadi ya alama zilizotolewa kwa swali, nawe ukatoa idadi sawa ya hoja. Fahamu kwamba baadhi ya maswali huhitaji kuzamiwa kwa kina zaidi ili kuridhisha matarajio ya mtahini.

Unapowasilisha jibu lako, zifafanue hoja katika aya huku ukizitanguliza zile muhimu na zenye uzito wa mawazo.

Dhana ya kwamba ‘kanuni za sarufi hazizingatiwi katika usahihishaji wa fasihi’ ni potoshi kabisa.

Usitegemee sana maelezo ya ‘miongozo’ uliyoisoma au ‘utabiri potofu’ wa maswali yanayotarajiwa kwenye mtihani.

Mara nyingi NECTA hurudia kutahini sehemu zilizofanywa vibaya na watahiniwa waliotangulia na kwa hivyo ni kosa kuchukulia kwamba swali lililotungwa mwaka jana haliwezi kurudiwa mwaka huu. Pitia kadiri iwezekanavyo maswali ya mitihani ya nyumba ili kujipa uzoefu mkubwa zaidi.

Azimia kuelewa visawe vinavyotumiwa katika kuuliza maswali ambayo aghalabu huhitaji majibu sawia.

Maana na matumizi ya istilahi

Elewa maana na matumizi ya istilahi elekezi kama vile ‘taja’, ‘eleza’, ‘thibitisha’,  ‘jadili’, ‘fafanua’, ‘onesha’, ‘dondoa’, ‘toa’, ‘tambua’, ‘dhihirisha’, ‘andika’, ‘tofautisha’, ‘pambanua’, ‘linganisha’, ‘orodhesha’ na kadhalika.

Ifahamike kwamba mfumo wa kutahini ushairi wa Kiswahili siku hizi unaelekea kufanana na ule wa Kiingereza. Mtahiniwa anaweza kuulizwa kutambua ‘Falsafa ya mtunzi’, ‘ Mgogoro wa shairi’, ‘Msimamo au Mtazamo wa mshairi’, Nafsi-neni au Nafsi-nenewa katika shairi.

Katika kueleza maana ya neno jinsi lilivyotumiwa katika shairi au kuandika ubeti fulani wa shairi kwa lugha nathari, ni muhimu kuhifadhi nafsi iliyotumiwa katika neno au ubeti husika. Vinginevyo, huwa ni kosa linaloadhibiwa vikali na watahini.

Kujifunza hakuna mwisho, na kufaulu hakuna mjanja ila mtiifu wa maelekezo muhimu.

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!