MAELEZO YA METHALI ZA KISWAHILI

By , in Fasihi Simulizi on . Tagged width:
 1. Mwenye pupa hadiriki kula tamu
 • Mtu mwenye haraka asiye na uvumilivu huwa hafanikiwi
 1. Mwenye tumbo ni tumbole, angafunga mkaja
 • Mkaja ni aina ya mkanda aghalabu hufungwa tumboni na mwanamke hasa baada ya kujifungua. Methali hii inatumiwa kuasa kuwa mwenye kupata tumbo kalipata tu asijisumbue kufunga mkaja atajiumiza bure. Wanawake wengi hupenda kufunga mkaja baada ya kujifungua ili kuzuia tumbo lisiwe kubwa na kuharibu muonekano.
 1. Mwibaji na watwana, mlifi ni mwungwana
 • Mwenye kuiba ni mwizi tu japo Mlifi (mlipaji), huuwa ni muungwana. Ukiiba unapoteza sifa ya uaminifu uliyokuwa nayo hata kama utalipa ulichoiba bado utabaki na sifa ya wizi.
 1. Ndege mjanja hunaswa na tundu bovu.
 • Ujanja ukizidi mwisho huondoa maarifa na hatimaye mtu huweza kuangukia asipotegemea kama inavyokuwa kwa ndege mjanja
 1. Ndugu wakigombana, chukua jembe ukalime, wakipatana chukua kikapu ukavune
 • Ndugu huwa hawagombani na hata ikitokea wakagombana ujue ugomvi wao hauvunji undugu wao hivyo usiingilie maana utapoteza muda wako bure ni bora ukalime ili siku wakipatana uwe na ulichovuna.
 1. Nifae na mvua nikufae na jua
 • Methali hii inasisitiza umuhimu wa kusaidiana kwa kujua kuwa kila mmoja ana umuhimu wake kwa wakati fulani, mtu asipokufaa kwa jambo hili ipo siku atakufaa kwa jambo lingine
 1. Lila na fila hazitangamani.
 • Lila ni wema au uzuri na fila ni ubaya/uovu,kutangamana ni kukaa pamoja/kuchangamana. Mambo mema hayakai pamoja na mambo maovu hivyo hata watu wema hawakai pamoja wala kufungamana na watu wabaya/waovu.
 1. Kuzima koleo si mwisho wa uhunzi
 • Koleoni zana ya ufundi na uhunzi ni ufuaji vyuma. Kuvunjika kwa koleo sio sababu ya kuacha kazi ya uhunzi, methali hii inahimiza kutoacha kufanya mambo kwa visingizio
 1. Jambo usilolijua, usiku wa giza
 • Kutolijua jambo humnyima mtu maarifa juu ya jambo hilo sawa na jinsi ambavyo mtu hushindwa kuona iwapo kuna giza. Mtu asiyefahamu jambo kwa kina hawezi kuwa na maarifa ya kutosha kwa jambo hilo
 1. Jino la pembe si dawa ya pengo.
 • Jino la pembe ni jino la bandia ambalo mtu huweka kuziba sehemu iliyotoka jino. Jino hili huwa haliwezi kushika kama ilivyo kwa jino halisi la kuzaliwa nalo. Methali hii huasa kutotegemea vitu vya muda kwani huwa havidumu.
 1. Jitihadi haiondoi kuduru
 • Jitihada ni bidii na kudura ni nguvu au uwezo wa Mungu. Hivyo bidii haiondoi uwezo wa Mungu, methali hii hutumiwa kuwatahadharisha watu wasiopenda mafanikio ya wengine hasa inapotokea aliyefanikiwa ni kwa uwezo wa Mungu tu.
 1. Jungu kuu, halikosi ukoko.
 • Jungu kuu ni chungu kikubwa, chungu kikubwa kikipikiwa hakikosi ukoko hata kama chakula kitakuwa kimekwisha. Methali hii inatujulisha kwamba mtu aliyekuwa tajiri hata akiharibikiwa na kufilisika, hakosi akiba yoyote japo ndogo.
 1. Jununu fununu.
 • Fununu ni habari za mnong’ono; habari zisizo na hakika. Jununu ni sawa na jambo. Mambo mengi huanza kufahamika kwa fununu kabla ya kusikika kwa ukweli wake, methali hii inahusiana kabisa na ile isemayo lisemwalo lipo kama halipo laja.
 1. Kafiri akufaaye, si muislamu asiye kufaa
 • Kafiri huhesabiwa kuwa ni mtu asiye na dini, asiyeamini Mungu. Methali hii inatumika kuonesha umuhimu wa kutenda mema bila kujali unaimani au la kwa sababu matendo mema humpa mtu thawabu, lakini usialmu usioambatana na wema hauna tofauti na ukafiri.
 1. Kafiri akufaye si Isilamu asiyekufaa.
 • Kafiri huhesabiwa kuwa ni mtu asiye na dini, asiyeamini Mungu. Methali hii inatumika kuonesha umuhimu wa kutenda mema bila kujali unaimani au la kwa sababu matendo mema humpa mtu thawabu, lakini usialmu usioambatana na wema hauna tofauti na ukafiri.
 1. Kanga hazai ugenini.
 • Kanga ni ndege jamii ya kuku, kwa desturi kanga huishi porini ingawa hutokea akafugwa majumbani mwa watu. Kanga awapo ugenini nje ya mazingira yake huwa vigumu sana kutaga kwa sababu hukosa mazingira aliyoyazoea huko porini. Methali hii hutumiwa kuonesha ugumu wanaoupata watu wawapo katika mazingira mapya.
 1. Kibuzi na kibuzi hununua jahazi.
 • Methali hii inaonesha umuhimu wa kuweka akiba kidogokidogo, watu hudharau vitu vidogo bila kujali kuwa vinaweza kuwa vingi na kuleta faida kubwa.
 1. Kichango kuchangizana.
 • Methali inahimiza ushirikiano katika masuala mbalimbali hasa yanayohusu kuchangiana, baadhi ya jamii huwa na utaratibu wa kupitisha harambee ili kufanikisha jambo la mtu mmoja na utaratibu huo huendelea kwa kila atakayepatwa na haja kama hiyo.
 1. Kikulacho ki nguoni mwako.
 • Kikulacho ni aina fulani ya mdudu anayeuma na mwenye maumivu makali sana huwa anapenda kujificha kwenye nguo. Aghalabu mtu mbaya kwako huwa hatoki mbali na wewe ni mtu anayekufahamu vizuri.
 1. Kikushindacho kukila usikitie ila.
 • Kutia ila ni kutoa sifa mbaya juu ya kitu, methali hii inaitaka jamii kutosema vibaya kuchafua sifa ya kitu ambacho unahisi hakikufai au kukunufaisha huku ukitambua kuwa huwezi kukitumia.
 1. Kila chombo kwa wimblile.
 • Wimbi ni mvumo mkali wamaji unaosababishwa na upepo hasa baharini, kila chombo cha kwenye maji hudhuriwa na wimbi kutegemea na uwezo wa chombo chenyewe, methali hii inataka watu wasifanye mambo kwa kuiga bali kupima uwezo kwanza juu ya jambo lenyewe ili kujiridhisha kama litawezekana ama la.
 1. Kila mwamba ngoma ,ngozi huivuta kwake.
 • Kuwamba ngoma ni kule kuivuta ngozi ili ienee kwenye kibao cha kutengenezea ngoma na huwezi kuwamba ngoma bila kuivuta ngozi kuja kwako. Methali hii hutumiwa kwa watu ambao huonekana kujipendelea wao zaidi ya wengine na kutaka vitu vizuri viwe kwao tu mf. mafisadi hujilimbikizia mali bila kujali watu wengine huwa sawa na wawamba ngoma.
 1. Kila shetani na mbuyu wake.
 • Shetani ni kiumbe kisichoonekana na huogopwa sana, shetani huaminika kuwa anapenda sana kuishi kwenye mibuyu na huwa akichagua mbuyu mmoja ndiyo huo huo. Methali hii hutumiwa kwa watu wanaoonekana kupenda sana vitu fulani au mtu fulani kiasi cha kuwa tayari kufanya lolote kwa ajili ya mtu huyo, yani huwa kama shetani ashikiliavyo mbuyu na asitake kuuachia kwa namna yoyote.
 1. Kilimia kikizama kwa jua, huzuka kwa mvua, na kikizama kwa mvua, huzuka kwa jua
 • Kilimia ni kikundi cha nyota zinazoambatana na majira ya mvua. Kuibuka na kuzama kwa nyota hizi huendana na majira. Methali hii inatufundisha kuwa kila jambo huwa na wakati wake hivyo tusilazimishe mambo kabla ya wakati wake kwani huweza kutokea yakaharika kabisa.
 1. Kipofu hasahau mkongojo wake.
 • Kipofu ni mtu asiyeona ambaye hutegemea mkongojo (aina fulani ya fimbo inayomuongoza) kutambua njia. Methali hii hutumiwa kuonesha jinsi watu wanavyokuwa makini na kukumbuka vitu wanavyovithamini kutokana na umuhimu wa vitu hivyo kwao sawa kabisa na mkongojo kwa kipofu.
 1. Kipya kinyemi ingawa kidonda.
 • Kinyemi ni kitu cha kupendeza, chenye kufurahisha. Methali hii hutumiwa kwa mtu aliyepata kitu kipya ambacho si kizuri hivyo, lakini akakienzi zaidi kuliko kizuri alichokuwa nacho tangu zamani. Pia, watu hutumia methali hii wanapomwona mtu anapenda kuvaa nguo hiyo hiyo mara nyingi kwa sababu ni mpya.
 1. Kisebusebu na kiroho papo.
 • Kisebusebu ni mtu mwenye tabia ya kuonyesha watu kwamba jambo fulani hana haja nalo na kumbe analitaka. Methali hii hutumiwa kuwasema watu wenye tabia ya kujifanya hawataki vitu fulani na kumbe wanavitamani.
 1. Kisokula mlimwengu,sera nale.
 • Kisichofaa kwa mwanadamu hufaa kwa shetani na hicho hakifai kutumiwa. Methali hii huasa watu kutofanya mambo ambayo hayana utu kwa walimwengu kwani hayo huwa ni ya kishetani.
 1. Kitumbua kimeingia mchanga.
 • Kitumbua ni aina ya kitafunwa kiachotokana na unga wa mchele, kitumbua kikiingia mchanga huwa hakiliki. Methali hii hutumiwa kuashiria jambo kuharibika mathalan mtu anapofukuzwa au kuachishwa kazi, husemwa kitumbua chake kimeingia mchanga.
 1. Kiwi cha yule ni chema cha; hata ulimwengu uwishe.
 • Kiwi hapa inamaanisha giza la machoni linalofanywa na kitu kinachong’aa sana. Methali hii hutumiwa kuwatambulisha watu ambao hawazingatii sana mvuto wa vitu kwa nje bali thamani ya kitu husika, huwa ni kama hawaoni vyenye mvuto wa nje wanapopata chenye thamani
 1. Konzi ya maji, haifumbatiki.
 • Konzi ni kiasi au kadiri inayoweza kushikwa kwa kufumbata vidole. Methali hii inaasa kuwa sio kila kitu kinafaa kushikiliwa katika maisha kwani vingine havishikiki.
 1. Kozi mwandada, kulala na njaa kupenda
 • Kozi ni ndege mkubwa kama mwewe anayekamata wanyama wadogowadogo. Ulaji wa ndege huyu hutegemea juhudi zake, akilala tu kwa uvivu wake atalala njaa. Methali hii huhimiza watu waache uvivu wajishughulishe na kuacha kukaa tu.
 1. Bwawa limeingia ruba.
 • Ruba ni mdudu anayefanana na nyungunyungu afyonzaye damu na huishi kwenye sehemu za majimaji na bwawa ni mkusanyiko mkubwa wa maji mengi ambao ni mdogo kuliko ziwa. Methali hii hutumiwa kuashiria kuwa uhuru uliozoeleka mahali sasa haupo tena kutokana na kuingia kwa mtu/kiongozi mwenye msimamo na kufuata taratibu na sheria.
 1. Chaka la samba, halilali nguruwe.
 • Chaka ni mwitu mkubwa. Sehemu ya mwitu anamokaa samba, nguruwe halali, au hakai kwa kituo, mahali hapo. Methali hii inatumiwa na mtu kwa maana ya kuwa hawezi kukaa mahali fulani kwa sababu ya maonevu ya aliyemzidi nguvu.
 1. Choko mchokoe pweza, binaadamu hutomuweza.
 • Pweza ni jamii ya samaki anayejificha mwambani ili kumpata lazima kumchokoa (kumchokoza) ilia toke alikojificha. Methali hii hutambiwa watu wanaopenda ugomvi ambao huchokoza wengine ili sababu ya kugombana ipatikane.
 1. Chombo cha kuzama hakina usukani.
 • Chombo kama jahazi au meli kikishajaaliwa kuzama kitazama tu, hakina nahodha wala baharia. Methali hii hutumiwa kuonesha kwamba jambo likipangwa kuharibika basi hakuna cha kuzuia
 1. Chovya – chovya yamaliza buyu la asali
 • Buyu la asali ni chombo cha asili kinachohifadhia asali, chovyachovya ni kule kulamba asali kwa kutumia kidole, kwa kufanya hivyo mtu hujikuta amemaliza buyu zima la asali bila kutarajia. Methali hii hutumika kuasa watu wasio na utaratibu mzuri katika matumizi hujikuta mtu amechukua pesa kidogo kidogo hata mwisho imekwisha na alichokifanya hakionekani.
 1. Chururu si ndo ndo ndo.
 • Chururu ni mlio wamaji yanapomiminika kwa wingi na ndo ndo ndo ni mlio wa matone ya maji yanapodondoka, hasa kwenye ndoo au debe, tone baada ya tone. Methali hii hutumika kwa maana ya kuwa bora mtu kupata kidogo kidogo kila siku kuliko wingi wa mara moja na kukosa. Kwa mfano afadhali mtu apate kitu cha matumizi japo ni kidogo cha kila siku kuliko kupata kingi cha mara moja kikiisha iwe basi
 1. Dalili ya mvua mawingu.
 • Dalili, yaani alama ya kuonesha kuwa itanyesha mvua ni kuyaona mawingu ya mvua angani. Dalili ya kupata ulilokusudia, kwanza ni kuiona ishara ya kukuonesha kuwa hicho kitu kipo tayari kukufika. Methali hii hutumiwa kwa maana ya kuwa jambo likitaka kuwa, huwepo ishara (dalili) kwanza inayoonesha kuwa jambo hilo litatokea. Watu husema methali hii wanapoiona dalili kama hiyo.
 1. Dau la mnyonge haliendi joshi, likienda joshi ni matakwa ya Mungu.
 • Dau ni Aina ya chombo cha majini. Joshi ni Chombo cha baharini kwenda kwa kasi/kina kirefu. Methali hii hutumika mtu anapoona jambo lake halinyooki au haliendi ipasavyo kwa sababu ya kukosa pesa au kwa kuwa hali yake ni duni.
 1. Donda ndugu halina dawa.
 • Donda ndugu ni donda la siku nyingi, lisilopona. Donda la siku nyingi hata ukilifanyia dawa namna gani huwa halisikii dawa, na kupoa huwa ni kwa bahati sana. Methali hii hutumiwa kwa mtu aliye na tabia mbaya na amezama kabisa katika tabia yake hiyo. Mtu huyo huwa ametolewa tamaa tena kuwa kuna dawa ya kumwachisha tabia yake mbovu.
 1. Fahari ya macho haifilisi duka.
 • Katika biashara wateja hurusiwa kutazama bidhaa ili kuona kama watavutiwa. Ili kuwahamasisha hasa iwapo wanaonekana kuogopa bei kutokana na uzuri wa bidhaa husika basi muuzaji huwatoa woga kwa kuwaambia fahari ya macho haifilisi duka. Yani hata kama hawakununua kutazama tu hakuwezi kumfilisi muuzaji.
 1. Farasi hamuwawezi, tembo mtawalishani?
 • Farasi ni mnyama anayekula kidogo kuliko tembo, methali hii huambiwa watu wanaotaka mambo makubwa hali madogo yenyewe hawayamudu.
 1. Funika kombe mwanakharamu apite.
 • Kufunika kombe ni kauli inayotumiwa kumwashiria mtu akubaliane tu ili yaishe yasifike kwa wakubwa na kuleta balaa zaidi, mwanaharamu ni mtu asistahili katikajambo au mazingira fulani. Iwapo tunakuwa na mambo yetu ya kuzungumza na ikatokea kubishana hata kutaka kuwanufaisha wasiohusika, methali hii ndipo hutumika kama namna ya kuwaasa wahusika kumaliza tofauti zao hata kama hawakuridhika.
 1. Ganda la mua la jana, chungu kaona kivuno.
 • Chungu ni aina ya wadudu wadogo wanaopenda sukari na aghalabu huwakuta wamejazana kwenye maganda ya muwa. Mtu anapofikia kutema ganda la muwa ni ishara kwamba hakuna kitu cha thamani amemaliza sukari yote hivyo halimfai, lakini pindi anapolitema tu hukuta chungu (wadudu) wamejaa tele wanafanya karamu. Hii ni kusema tusidharau visivyotufaa na kuvitupa kuna wanaovihitaji na kuvithamini. Mathalan mavazi yaliyochujuka kwako au kuwa madogo kuna watu wakiyapata hayo huwa ya kuzaa siku ya sikukuu.
 1. Gome la udi, si la mnuka uvundo.
 • Udi ni magome ya mti fulani yanayotoa harufu nzuri yanapoungua, agh. hutumika kufukizia. Uvundo ni harufu mbaya. Methali hii hutumiwa kuonesha kuwa kisicho chako hakiwezi kukusiri hivyo ni bora kukubaliana na hali yako kama ilivyo. Iwapo unanuka uvundo hata ukitumia udi kufukiza harufu ya uvundo itapotea tu kwa muda na harufu ya udi ukiisha unabaki na harufu yako ya asili, vivyo hivyo katika hali zetu tusiwe watu wa kuishi maisha ya kuigiza kwa vitu vya kuazima.
 1. Haba na haba, hujaza kibaba.
 • Haba katika methali hii inaukilia punje ya nafaka, kidogo na kibaba ni kipimo cha ujazo wa takriban gramu 700. Punje moja moja ukizikusanya mwishowe huwa nyingi za kuweza kujaza kibaba kizima. Methali hii inatufunza tusidharau kitu kidogo. Kwa mfano, pesa kidogo kidogo tukizikusanya mwishowe pesa hizo huwa nyingi.
 1. Hakuna masika yaso mbu
 • Masika ni Majira ya mvua nyingi. Masika kabisa hayakosi mbu (kwa sababu ya mvua na tope nyingi zinazokuwepo). Methali hii inatufahamisha kuwa kila wakati huja na taabu na shida zake, kama vile wakati wa masika unavyokuja na mbu.
 1. Hala hala mti na macho.
 • Methali hii hutahadharisha watu juu ya matendo yao kuwa huweza kuumiza wengine pasipo wao kujua au kukusudia. Ni sawa na mtu awapo na mti mkononi na akawa anaugeuzageuza bila kujali waliko pembeni mwake huweza kuwachoma machoni na ikaishia pole tu.
 1. Hamadi ni ilio kibindoni, na silaha ni iliyo mkononi. na mwisho.
 • Hamadi ni tamko la mtu anaposhtuka na kibindo ni mkunjo wa nguo unaofungwa kiunoni k.v. kwenye shuka au kikoi, unaotumiwa kama mfuko kuhifadhia pesa za mtu. Ukishtuliwa (na adui au mnyama mbaya) na kushituka, yataka silaha iweko kibindoni, haiko mbali. Methali nii inamfahamisha mtu kuwa wakati wa haja au dhiki kinachomfaa ni kile alichonacho mkononi, yaani karibu naye. Pia methali hii inamhimiza mtu aweke akiba, kwani ndiyo itakayomfaa akitokewa na haja ya ghafla.
 1. Akili ni nywele kila mtu ana zake.
 • Akili huchukuliwa sawa na nywele ambazo huwa kila mtu anazo na aghalabu hazifanani. Methali hii hutumiwa kuonesha tofauti baina ya watu katika kufanya maamuzi, jambo moja lile lile mmoja anaweza kuliamulia hivi na mwingine tofauti.
 1. Akili nyingi huondowa maarifa.
 • Kujitia akili nyingi au uwerevu mwingi wakati mwingine huondoa busara na hekima ya mtu, na baada ya mtu kufanya jambo likatengenea, huliharibu. Hutumiwa methali hii kwa mtu asiyesikia nasaha na mashauri ya wenziwe katika kufanya jambo; anahisi fikra zake tu ndizo sawa. Mwishowe mtu huyo anashtukia jambo lake limemharibikia.
 1. Moyo ukipenda chongo huita kengeza
 • Methali hii hutumiwa kuonesha nguvu ya mapenzi miongoni mwa wanadamu, kwamba mtu akipenda haoni dosari zilizopo na hata akiziona basi hutafuta namna ya kuzifanya zisionekane kubwa sana.
 1. Akupaye kisogo si mwenzio.
 • Kisogo ni sehemu ya nyuma ya kichwa. Anayekupa kisogo maana yake hataki mtazamane wala mfahamiane na hivyo hataki ukaribu na wewe. Methali hii huambiwa watu wasiopenda ushirikiano na wenzao.
 1. Aliye kupa wewe kiti (kibao) ndiye aliyenipa mimi kumbi.
 • Kumbi ni gamba la nje la nazi. Hutumiwa methali hii kumwambia mtu mwenye kujivuna na kumkandamiza mwenziwe aliyekuwa chini ambaye hana uwezo au madaraka kama yeye.
 1. Aliye kutwika, ndiye atakaye kutua.
 • Kutwika ni kubebesha hasa mzigo kichwani. Aliyekutweka mzigo huyo huyo ndiye atakayekutua mzigo wako. Methali hii hutumika kuambiwa mtu aliyejitakia taabu mfano binti kupata ujauzito.
 1. Aliyekupa mkeka ndiye aliyenipa kumbesa.
 • Mkeka ni zulia la ukili hutumiwa kukalia na kumbesa ni kumbi la nazi aghalabu mnapofika mahali ugenini mwenyeji wenu ndiye huwapa vya kukalia na hapana anayeamua akae wapi kati yenu zaidi ya mwenye wenu. Katika maisha inaaminika kila mmoja anapewa fungu lake na mtoaji ni mmoja tu Mungu. Hivyo hutumiwa methali hii kuwatia watu moyo wasijiumize kwa mafanikio ya wengine kwani kila mtu hupewa alichobarikiwa nacho.
 1. Amani haipatikani mpaka kwa ncha ya upanga.
 • Amani wakati mwingine haiji ila kwa kutumia nguvu. Methali hii inamnasihi mtu ambaye anaonewa na mwenziwe au wenziwe, kuwa apinge maonevu hayo – hapo ndio atapata suluhu na salama.
 1. Ana hasira za mkizi.
 • Mkizi ni samaki ambaye aghalabu huwa na tabia ya kujirusha juu na wakati mwingine huweza kujirusha na kuingia mwenyewe katika mtumbwi wa mvuvi akafurahia. Methali hii hutumiwa kwa watu ambao wakikasirika hufanya mambo yenye kuwanufaisha wengine.
 1. Anayekuja pasi na hodi, huondoka bila ya kuaga.
 • Kuja pasi na hodi ni kutokea bila taarifa na kuondoka bila ya kuaga ni kutoweka kimyakimya. Methali hii hutumiwa kuonesha hali ya kutokea kwa jambo lisilotarajiwa na kutoweka kwake, mathalan huweza kuzuka ugonjwa ukasumbua sana na kisha kutoweka bila ya watu kutegemea.
 1. Angurumapo simba, mcheza ni nani?
 • Simba ni mnyama mbabe na mkali ambaye akiunguruma sauti yake hutisha sana wanyama wengine. Methali hii hutumika kuonesha jinsi mtu fulani alivyombabe hasa katika mazingira ya ushindani kama mpira wa miguu timu moja inaposhinda huweza kuitambia timu pinzani kwa methali hiyo.
 1. Aninyimaye mbaazi kanipunguzia mashuzi
 • Mbaazi/kunde ni mazao jamii ya kunde yenye kusababisha matumbo kujaa gesi na kutoa harufu mbaya.Katika maisha hutokea mtu akakunyima baadhi ya vitu akidhani anakukomoa lakini kumbe amekuepusha na madhara mengine. Hutumiwa methali hii kwa watu wanaowanyima wengine mambo ambayo kimsingi hata wakiyakosa hawapati hasara.
 1. Atangaye na jua hujuwa.
 • Kutanga na jua ni kuhangaika katika kutafuta na kila anayejishughulisha huwa hakosi kupata japo taarifa itakayomwezesha kufahamu mafanikio yalipo. Kwa ujumla methali hii inahimiza watu kujituma na kujishughulisha.
 1. Atangazaye mirimo, si mwana wa ruwari (Liwali)
 • Mirimo ni siri, atoae habari za siri huwa si mhusika wa jambo lenyewe. Mara nyingi watu wasiohusika na jambo ndio hupenda kusema mambo yasiyowahusu.
 1. Avumaye baharini papa kumbe wengi wapo.
 • Katika mazingira ya bahari mnyama anayesifika sana ni papa licha ya kuwa hafui dafu kwa baadhi ya wanyama wakubwa kumzidi kama nyangumi. Methali hii inatoa hadhari juu ya kutolewa sifa na kujisahau hata ukajikuta unapata upinzani mkali kwa kutotambua kwamba kuna wenye uwezo kukuzidi.
 1. Bamba na waume ni bamba, hakuna bamba la mume.
 • Mume hakamiliki bila mke wala mke hakamiliki bila mume. Methali hii hutumika kuonesha hali ya kuhitajiana baina ya wake na waume.
 1. Bandu bandu huisha gogo.
 • Bandu bandu ni ile hali ya kuchonga sehemu ya gogo ili kupata vipande vya kuwashia moto, halii hii hufanywa taratibu na kwa muda mrefu na hatimaye hujikuta gogo limekwisha hata kama lilikuwa kubwa sana. Methali hii inataka watu kutoogopa mambo kwa kuyaona mazito bali kuyaingilia kidogokidogo na mwisho yatakamilika.

BOFYA HAPA CHINI KUSOMA ZAIDI>>>>>>>>>>>>>

MAELEZO YA METHALI ZA KISWAHILI