LEO KATIKA KAMUSI ‘Tofauti ya Kukubali na Kuafiki’

By , in Kamusi on . Tagged width:

Karibu katika KAMUSI.

JE, KUKUBALI NDIYO KUAFIKI?

Makala ya KAMUSI leo inaangazia tofauti ya maneno kukubali na kuafiki.

Watumiaji wa kawaida wa Lugha ya Kiswahili kama walivyo wazungumzaji wa lugha wengine husema lugha kwa mazoea na mara ya chache husema kwa mantiki.

Wakati mwingi hugha huwa na mazoea yasio ya kawaida. Yapo maneno mengine hayana mantiki kabisa. Kwa hiyo, wakati mwingine baadhi ya watu wajifunzao lugha hupata tabu sana pale wanapotafuta mantiki katika lugha wanazojifunza. ( Hoja hii itaelezwa wakati mwingine).

Turejeeni katika hoja ya leo. Katika Kiswahili yapo maneno kadhaa wa kadhaa ambayo maana zeke hushabihiana au kufanana au kukaribiana sana. Hata hivyo, kufanana au kukaribiana huko hakufanyi maneno ya namna hiyo yawe na maana moja.

Mathalani, wengi tunatumia maneno ‘ kukubali ‘ na ‘ kuafiki’ katika muktadha tofauti.

Ingawa maneno hayo huchukuliwa kama maneno yaliyo na maana sawa lakini kwa hakika maneno hayo yana maana na msisitizo uliyo tofauti kabisa.

Kwa mujibu wa kamusi kuu ya BAKITA ( 2016), uk. 534. Wanaeleza kuwa kukubali ni kuafiki.

Makala haya ya Kamusi ina maoni tofauti na maelezo hayo ya Kamusi kuu ya Kiswahili. ( BAKITA, 2016).

Ok wetu Makala ya KAMUSI tunaona kukubali si kuafiki. Hata hivyo, kukubali ni hatua ya awali ya kuafiki.

Mtu huanza kukubali kisha anafikia kilele cha kukubali huko ndiyo huitwa kuafiki.

Makala ya KAMUSI inayo mifano ya watu wanaokubali mambo bila kuafiki. Kukubali huko bila kuafiki Waswahili huita ‘ kubali yaishe’

Mtu anayekubali yaishe huwa hajaafiki. Mtu hukubali jambo ili kujiondosha ktk mtanziko wa hoja au mambo kwa matilaba ya kutaka mambo yaendelee.

Hata mke na mume wanapoingia katika majibizano makali aghalabu hutokea mke kukubali kukosea hata kama hajakosa. Kwa nadra sana wanaume pia hufanya hivyo.

Kukubali huko si kule kwa umuhimu wa hoja yenyewe bali ni kwa kujiepusha na mzozo hasa ikizingatiwa mfumo dume unaochagiza mwanamke kuwa chini daima dumu dawamu ndiyo humfunga mwanamke mdomo.

Kwa hiyo, makala haya ya KAMUSI inaona kuafiki huenda mbali zaidi ya kukubali. Kwa mintarafu hii, mtu hukubali lakini zaidi huwa na ridhaa juu ya jambo analolikubali.

Ridhaa ndiyo humfanya mtu kuafiki. Kuafiki maana yake ni kukubali kwa maneno, moyo, akili na matendo.

Kukubali kunaweza kuwa kwa kusema tu. Mtu anaweza kusema ndiyo hata kama moyo na akili yake haitaki au hata kama haamini jambo fulani.

Kwa mfano, Unaweza kukubali tu kuwa timu ya simba imekuwa bingwa wa kandanda Tanzania lakini si ajabu Mwinyi Zahera anaweza asiafiki jambo hilo.

Aidha, chama cha siasa kinaweza kumteua mgombea mmoja kati ya kumi na mmoja. Kwa muktadha huu wagombea wengine wanaweza kukubali lakini kwa kuwa baadhi yao huwa hawaafiki aghalabu huendeleza makundi, mizozo, fitna za chini kwa chini, nk. Kwa nini , ni kwa sababu hapakuwa na kuafikiana katika jambo hilo.

Itakumbukwa kuwa msanii wa Muziki wa Kikazi kipya Ngosha , amewahi kueleza kuwa ‘ Si kila ndiyo inamaanisha ndiyo kiundani, zipo ndiyo zimechanganyika na utani.

Je, BAKITA hamuoni kuwapo haja ya kutazama upya maana ya maneno haya katika kamusi yetu?

……………..Mwisho………….

Asante sana.

Kamusi imekujieni kwa hisani ya Utu- Tanzania, Culture Link Africa Ltd na KAMUSI Pevu ya Kiswahili.

Majid Mswahili
#BwanaKamusi
Mchambuzi wa Lugha, Fasihi na Fasaha ya Kiswahili
Tuandikie : majidkiswahili@gmail.com Au + 255 715 838480

error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!