KUKUA KWA KISWAHILI KIMATAIFA NA MAHITAJI YA UKALIMANI

By , in TAFSIRI/UKALIMANI on .

KUKUA KWA KISWAHILI KIMATAIFA NA MAHITAJI YA UKALIMANI

KISWAHILI ni lugha yenye asili ya Kibantu ambayo huzungumzwa zaidi na watu wa nchi za Afrika Mashariki na Kati hususani Tanzania, Kenya na Uganda. Pia, Kiswahili huzungumzwa Rwanda, Burundi, Somalia, Msumbiji, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Komoro na Malawi.

Hali kadhalika, Kiswahili huzungumzwa katika nchi za Uarabuni kama vile Dubai, Yemeni na kadhalika. KISWAHILI AFRIKA MASHARIKI Kiswahili kina nafasi kubwa na muhimu sana katika Afrika Mashariki hasa kwa sababu kimebeba majukumu makubwa katika nchi hizi na katika jumuiya inayaoundwa na nchi hizo. Nchini Tanzania, Kiswahili ni lugha ya Taifa na lugha rasmi. Lugha ambayo kutoka zama za kupigania uhuru iliweza kuwaunganisha Watanzania wote na kwa umoja wao kuweza kupata uhuru wao na dhima hiyo imedumu na kuendelea hadi leo.

Aidha, Kiswahili hutumika katika shughuli mbalimbali kama vile elimu, dini, siasa na katika mikusanyiko mingine inayokutanisha watu wa makabila zaidi ya moja. Kimsingi, Kiswahili kinazungumzwa na idadi kubwa kabisa ya Watanzania walio mijini na vijijini. Nchini Kenya Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi ambayo inatambuliwa katika Katiba ya mwaka 2000 ya nchi hiyo.

Kiswahili hufundishwa na kutahiniwa shuleni na vyuoni na pia hutumika katika shughuli za kisiasa ikiwa ni pamoja na kampeni za kisiasa za mijini na vijijini. Pia, Kiswahili ni lugha kuu ya mawasiliano pale wanapokutana watu wa makabila tofauti nchini humo. Halikadhalika, Kiswahili hutumika katika dini na katika programu kadhaa za vyombo vya habari kama vile redio, magazeti na televisheni.

Nchini Uganda Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi kuanzia mwaka 2005. Kiswahili kinafundishwa na kutahiniwa katika viwango vyote vya elimu. Aidha, Kiswahili kimekuwa ndiyo lugha ya mawasiliano ikitumiwa kufanya mawasiliano na wageni wanaotoka katika nchi jirani za Afrika Mashariki. Kiswahili ni lugha inayotumiwa zaidi na jeshi na polisi nchini Uganda, jambo ambalo huenda limekinza sana maendeleo ya lugha hii nchini humo kutokana na watu wengi kuihusisha na ukatili wa askari.

Kiswahili nchini Rwanda kinatumika sokoni na mijini lakini si kwa kiwango kikubwa. Pia lugha ya Kiswahili inafundishwa katika Chuo Kikuu cha Rwanda. Wapo baadhi ya wananchi wanajiandikisha kujifunza Kiswahili katika madarasa ya jioni. Rwanda imeingiza Kiswahili katika mtaala wa taifa na kuongezwa katika orodha ya lugha rasmi za nchi hiyo na kufanya idadi ya lugha rasmi kuwa nne nchini humo. Kiswahili kitaungana na lugha rasmi za Kinyarwanda, Kiingereza na Kifaransa.

Kwa sasa Kiswahili kitatumika katika shughuli za uongozi na kitaonekana kwenye baadhi ya nyaraka rasmi. Kuanzia mwaka 1961, Redio Rwanda imekuwa na programu za matangazo kwa Kiswahili kama vile taarifa ya habari, matangazo ya mpira, salamu za wasikilizaji. n.k. Kiswahili kinatumika sana Mashariki ya Burundi. Kiswahili kinafundishwa katika baadhi ya vyuo nchini humo m.f. Chuo cha Wanajeshi cha Bujumbura na katika Chuo Kikuu cha Bujumbura.

Aidha, Kiswahili pia hufundishwa katika taasisi za mabwana fedha na taasisi ya mawasiliano ya simu. Kiswahili hutumika pia katika baadhi ya programu za redio Burundi, Ibyizigiro, Isanganiro na katika televisheni kwa baadhi ya vipindi vyake kama vile habari, matangazo, vipindi vya utamaduni na mafunzo, matangazo ya mpira na maombi ya wasikilizaji. Kuwapo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kumefanya Kiswahili kiendelee kuwa na hadhi kubwa katika ukanda huu.

Kiswahili ndiyo lugha inayoweza kuwaunganisha watu wa ukanda huu na kitawezesha michakato ya mtangamano baina ya watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanikiwa. Hii ni kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha inayozungumzwa na watu wengi wa ukanda huu. Kifungu cha 5 cha mkataba wa uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kimeweka mihimili minne ya mtangamano, ambayo ni: Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Fedha ya Pamoja na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.

Mihimili hii ili iweze kutekelezwa kikamilifu kunahitajika kiungo kikuu miongoni mwa wanajumuiya na kwa uhakika hakuna ubishi kuwa lugha ya Kiswahili ndiyo inayokidhi. LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA Lugha ya Kiswahili hivi sasa imejitwalia umaarufu mkubwa duniani hususani baada ya kuanza kutumiwa katika mikutano mikubwa ndani na nje ya bara la Afrika. Kiswahili kimekuwa lugha ya kwanza miongoni mwa lugha za Kiafrika kutumika kama lugha rasmi na lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika (AU).

Azimio la kuteuliwa kwa Lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi na ya kazi lilifanyika huko Durban, Afrika Kusini tarehe 9 – 11 mwezi Julai mwaka 2002 na Julai 2004, aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Joachim Chissano alihutubia mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika kwa Kiswahili kwa mara ya kwanza alipokuwa akifunga mkutano huo na kumaliza muda wake wa kuwa mwenyekiti wa Umoja huo.

Baada ya hotuba ya Rais Chissano marais takribani kumi walianza hotuba zao kwa kutoa salamu kwa Kiswahili kama ishara ya kuunga mkono matumizi ya lugha ya Waafrika katika Umoja huo. Juhudi hizi ziliendelezwa na Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete alipohutubia umoja huo kwa lugha ya Kiswahili tarehe 23-24 mwezi Januari mwaka 2006 huko Sudan alipokuwa akifunga mkutano baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa umoja huo.

Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ulikiteua Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha za Kiafrika itakayotumika katika vikao vyake. Uteuzi wake ulitokana na kikao cha Mawaziri wa Utamaduni 1988. Mawaziri walitoa wazo la kuwa na lugha moja ya Kiafrika itakayotumika pamoja na lugha za kigeni kama vile Kiingereza, Kireno, Kifaransa na Kiarabu.

Pendekezo la Mawaziri wa Utamaduni la kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Kiafrika na ya tano katika vikao vya OAU ni uamuzi mzuri ambao umekipa Kiswahili hadhi kubwa kimataifa. Pendekezo hilo liliridhiwa na wakuu wa nchi katika mkutano wao huko Addis Ababa, Ethiopia. Aidha, Kiswahili kimekubaliwa kutumika katika mikutano ya UNESCO ili mradi tu kuwepo na mkalimani.

Kama wasemavyo Waswahili “Chechema utafika wendako” ndivyo ilivyokuwa kwa lugha ya Kiswahili kwamba sasa kimevuka mipaka yake na kufika katika anga za kimataifa. Hivi sasa kuna nchi mbalimbali duniani zimeanzisha programu ya somo la Kiswahili katika vyuo vyake vikuu au katika taasisi zake za lugha ya kigeni. Miongoni mwa nchi hizo ni pamoja na Marekani, Uchina, Urusi, Italia, Ujerumani, Japan, Korea Kusini, Ufaransa n.k.

Aidha, Kiswahili kinatumika katika idhaa mbalimbali za kimataifa kama vile Sauti ya Amerika (Marekani), BBC (Uingereza), Redio Deutche Welle (Ujerumani), Redio France International (Ufaransa), China Radio Inaternational (Uchina), Idhaa ya Kiswahili Redio Japan (Japan), Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran, Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa, Idhaa ya Kiswahili Iran, Redio Vatican, Redio India, Redio ya Korea Kusini, Redio Moscow International (Urusi) n.k.

NAFASI YA UKALIMANI Baada ya usuli huo unaotupatia picha ya jumla ya kuenea na kukubalika kwa lugha hii barani Afrika na kimataifa, hebu sasa tuone nafasi ya ukalimani wa lugha hii kimataifa. Kabla ya kulijua hili yafaa kujua tunapozungumzia ‘ukalimani’ maana yake ni nini hasa? Ukalimani ni taaluma ya kuhawilisha ujumbe, maana na mawazo yaliyo katika mazungumzo kutoka lugha moja (lugha chanzi) kwenda lugha nyingine (lugha lengwa).

Taaluma hii huwezesha mawasiliano ya lugha ya mdomo na alama kwa watumiaji wa lugha zaidi ya moja. Hii inamaanisha kwamba wakutanapo watu wa lugha zaidi ya moja ukalimani huhitajika ili kuwezesha mawasiliano yao. Aidha, ni vizuri pia tukajua dhana mbili muhimu ambazo haziepukiki katika kufafanua ukalimani. Dhana hizo ni “lugha chanzi” na “lugha lengwa”.

Lugha chanzi ni lugha ambayo inatumika kutolea ujumbe wa asili (lugha ya mtoa ujumbe wa awali). Lugha lengwa ni lugha inayotumika kuhawilisha ujumbe asili ili kuwafikia wahusika ambao hawajui ile lugha ya mtoa ujumbe (lugha anayotumia mkalimani). Imeandaliwa na Consolata P. Mushi, Msanifu Lugha Mkuu, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).

KWA HISANI YA >>>>>>

Recommended articles
error: Jisajili kupata uhuru zaidi !!